1 1 Neno la Bwana lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda:
2 Bwana asema,
“Nitafagia kila kitu
kutoka kwenye uso wa dunia.”
3 “Nitafagilia mbali watu na wanyama;
nitafagilia mbali ndege wa angani
na samaki wa baharini.
Wafanyao maovu watapata tu kokoto,
nami nitamkatilia mbali mwanadamu atoke katika dunia,”
asema Bwana.
4 “Nitaiadhibu Yuda
na wote wakaao Yerusalemu.
Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali
kila mabaki ya Baali,
majina ya wapagani na makuhani
waabuduo sanamu:
5 wale ambao husujudu juu ya mapaa
kuabudu jeshi la vitu vya angani,
wale ambao husujudu na kuapa kwa Bwana
na ambao pia huapa kwa Malkamu,
6 wale wanaoacha kumfuata Bwana,
wala hawamtafuti Bwana
wala kutaka shauri lake.
7 Nyamazeni mbele za Bwana Mwenyezi,
kwa maana siku ya Bwana iko karibu.
Bwana ameandaa dhabihu,
amewaweka wakfu wale aliowaalika.
8 Katika siku ya dhabihu ya Bwana
nitawaadhibu wakuu
na wana wa mfalme
na wale wote wanaovaa
nguo za kigeni.
9 Katika siku hiyo nitaadhibu wote ambao
hukwepa kukanyaga kizingiti,
ambao hujaza hekalu la miungu yao
kwa dhuluma na udanganyifu.”
10 Bwana asema, “Katika siku hiyo
kilio kitapanda juu kutoka lango la Samaki,
maombolezo kutoka mtaa wa pili,
na mshindo mkubwa kutoka vilimani.
11 Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni;
wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa,
wote ambao wanafanya biashara ya fedha
wataangamizwa.
12 Wakati huo nitasaka mji wa Yerusalemu kwa taa,
na kuwaadhibu wale ambao
wanakaa katika hali ya kuridhika,
ambao ni kama divai
iliyobaki kwenye machicha,
ambao hudhani, ‘Bwana hatafanya lolote,
jema au baya.’
13 Utajiri wao utatekwa nyara,
nyumba zao zitabomolewa.
Watajenga nyumba,
lakini hawataishi ndani yake;
watapanda mizabibu
lakini hawatakunywa divai yake.
14 “Siku kubwa ya Bwana iko karibu:
iko karibu na inakuja haraka.
Sikilizeni! Kilio katika siku ya Bwana
kitakuwa kichungu,
hata shujaa atapiga kelele.
15 Siku ile ni siku ya ghadhabu,
siku ya fadhaa na dhiki,
siku ya uharibifu na ukiwa,
siku ya giza na utusitusi,
siku ya mawingu na giza nene,
16 siku ya tarumbeta na mlio wa vita
dhidi ya miji yenye ngome
na dhidi ya minara mirefu.
17 Nitawaletea watu dhiki,
nao watatembea kama vipofu,
kwa sababu wametenda dhambi
dhidi ya Bwana.
Damu yao itamwagwa kama vumbi
na matumbo yao kama taka.
18 Fedha yao wala dhahabu yao
hazitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana.
Katika moto wa wivu wake
dunia yote itateketezwa,
kwa maana ataleta mwisho
wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.”
2 1 Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja,
enyi taifa lisilo na aibu,
2 kabla ya wakati ulioamriwa haujafika
na siku ile inayopeperusha kama makapi,
kabla hasira kali ya Bwana haijaja juu yenu,
kabla siku ya ghadhabu ya Bwana
haijaja juu yenu.
3 Mtafuteni Bwana, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi,
ninyi ambao hufanya lile analoamuru.
Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu;
labda mtahifadhiwa
siku ya hasira ya Bwana.
4 Gaza utaachwa
na Ashkeloni utaachwa magofu.
Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu
na Ekroni utangʼolewa.
5 Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari,
enyi Wakerethi;
neno la Bwana liko dhidi yenu,
ee Kanaani, nchi ya Wafilisti.
“Mimi nitawaangamiza,
na hakuna atakayebaki.”
6 Nchi kando ya bahari, mahali ambapo wanaishi Wakerethi,
patakuwa mahali pa wachungaji
na mazizi ya kondoo.
7 Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda,
hapo watapata malisho.
Wakati wa jioni watajilaza chini
katika nyumba za Ashkeloni.
Bwana Mungu wao atawatunza,
naye atawarudishia wafungwa wao.
8 “Nimeyasikia matukano ya Moabu
nazo dhihaka za Waamoni,
ambao waliwatukana watu wangu
na kutoa vitisho dhidi ya nchi yao.
9 Hakika, kama niishivyo,”
asema Bwana Mwenye Nguvu Zote,
Mungu wa Israeli,
“hakika Moabu itakuwa kama Sodoma,
Waamoni kama Gomora:
mahali pa magugu na mashimo ya chumvi,
nchi ya ukiwa milele.
Mabaki ya watu wangu watawateka nyara;
mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”
10 Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao,
kwa kutukana na kudhihaki
watu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote.
11 Bwana atakuwa wa kuhofisha kwao
atakapoangamiza miungu yote ya nchi.
Mataifa katika kila pwani yatamwabudu,
kila moja katika nchi yake.
12 “Ninyi pia, ee Wakushi,
mtauawa kwa upanga wangu.”
13 Mungu atanyoosha mkono wake dhidi ya kaskazini
na kuangamiza Waashuru,
akiiacha Ninawi ukiwa
na pakame kama jangwa.
14 Makundi ya kondoo na ngʼombe yatajilaza pale,
viumbe vya kila aina.
Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba
wataishi juu ya nguzo zake.
Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani,
kifusi kitakuwa milangoni,
boriti za mierezi zitaachwa wazi.
15 Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha
wakijisikia salama.
Ulisema moyoni mwako,
“Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.”
Jinsi gani umekuwa gofu,
mahali pa kulala wanyama pori!
Wote wanaopita kando yake wanauzomea
na kutikisa mkono kwa dharau.
3 1 Ole mji wa wadhalimu,
waasi na waliotiwa unajisi!
2 Hautii mtu yeyote,
haukubali maonyo.
Haumtumaini Bwana,
haukaribii karibu na Mungu wake.
3 Maafisa wake ni simba wangurumao,
watawala wake ni mbwa mwitu wa jioni,
ambao hawabakizi chochote
kwa ajili ya asubuhi.
4 Manabii wake ni wenye kiburi,
ni wadanganyifu.
Makuhani wake hunajisi patakatifu
na kuihalifu sheria.
5 Bwana aliye ndani yake ni mwenye haki,
hafanyi kosa.
Asubuhi kwa asubuhi hutoa haki yake,
kila kukipambazuka huitimiza,
bali mtu dhalimu hana aibu.
6 “Nimeyafutilia mbali mataifa,
ngome zao zimebomolewa.
Nimeziacha barabara ukiwa,
hakuna anayepita humo.
Miji yao imeharibiwa;
hakuna mmoja atakayeachwa:
hakuna hata mmoja.
7 Niliuambia huo mji,
‘Hakika utaniogopa na kukubali maonyo!’
Ndipo makao yake hayatafutiliwa mbali,
wala adhabu zangu zote hazitakuja juu yake.
Lakini walikuwa bado na shauku
kutenda kwa upotovu katika yote waliyofanya.”
8 Bwana anasema,
“Kwa hiyo ningojee mimi,
siku nitakayosimama kuteka nyara.
Nimeamua kukusanya mataifa,
kukusanya falme
na kumimina ghadhabu yangu juu yao,
hasira yangu kali yote.
Dunia yote itateketezwa
kwa moto wa wivu wa hasira yangu.
9 “Ndipo nitatakasa midomo ya mataifa,
kwamba wote waweze kuliitia jina la Bwana
na kumtumikia kwa pamoja.
10 Kutoka ngʼambo ya mito ya Kushi
watu wangu wanaoniabudu,
watu wangu waliotawanyika,
wataniletea sadaka.
11 Siku hiyo hutaaibishwa
kwa ajili ya makosa yote ulionitendea,
kwa sababu nitawaondoa kutoka mji huu
wale wote wanaoshangilia
katika kiburi chao.
Kamwe hutajivuna tena
katika kilima changu kitakatifu.
12 Lakini nitakuachia ndani yako
wapole na wanyenyekevu,
ambao wanatumaini jina la Bwana.
13 Mabaki ya Israeli hayatafanya kosa;
hawatasema uongo,
wala udanganyifu hautakuwa
katika vinywa vyao.
Watakula na kulala
wala hakuna yeyote
atakayewaogopesha.”
14 Imba, ee Binti Sayuni;
paza sauti, ee Israeli!
Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote,
ee Binti Yerusalemu!
15 Bwana amekuondolea adhabu yako,
amewarudisha nyuma adui zako.
Bwana, Mfalme wa Israeli, yu pamoja nawe;
kamwe hutaogopa tena madhara yoyote.
16 Katika siku hiyo watauambia Yerusalemu,
“Usiogope, ee Sayuni;
usiiache mikono yako ilegee.
17 Bwana Mungu wako yu pamoja nawe,
yeye ni mwenye nguvu kuokoa.
Atakufurahia kwa furaha kubwa,
atakutuliza kwa pendo lake,
atakufurahia kwa kuimba.”
18 “Huzuni katika sikukuu zilizoamriwa
nitaziondoa kwenu;
hizo ni mzigo na fedheha kwenu.
19 Wakati huo nitawashughulikia
wote waliokudhulumu;
nitaokoa vilema na kukusanya
wale ambao wametawanywa.
Nitawapa sifa na heshima
katika kila nchi ambayo waliaibishwa.
20 Wakati huo nitawakusanya;
wakati huo nitawaleta nyumbani.
Nitawapa sifa na heshima
miongoni mwa mataifa yote ya dunia
wakati nitakapowarudishia mateka yenu
mbele ya macho yenu hasa,”
asema Bwana.