Zaburi Chapter 1(Zaburi 1–41) Zaburi 1 1 Heri mtu yule ambaye haendi katika shauri la watu waovu, wala hasimami katika njia ya wenye dhambi, au kuketi katika baraza la wenye mizaha. 2 Bali huifurahia sheria ya Bwana, naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana. 3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa kando ya vijito vya maji, ambao huzaa matunda kwa majira yake na majani yake hayanyauki. Lolote afanyalo hufanikiwa. 4 Sivyo walivyo waovu! Wao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. 5 Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu, wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki. 6 Kwa maana Bwana huziangalia njia za mwenye haki, bali njia ya waovu itaangamia. Chapter 2Zaburi 2 1 Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya, na kabila za watu kula njama bure? 2 Wafalme wa dunia wanajipanga na watawala wanajikusanya pamoja dhidi ya Bwana na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake. 3 Wanasema, “Tuvunje minyororo yao na kuvitupilia mbali vifungo vyao.” 4 Yeye atawalaye mbinguni hucheka, Bwana huwadharau. 5 Kisha huwakemea katika hasira yake na kuwaogopesha katika ghadhabu yake, akisema, 6 “Nimemtawaza Mfalme wangu juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.” 7 Nitatangaza amri ya Bwana: Yeye aliniambia, “Wewe ni Mwanangu, leo mimi nimekuzaa. 8 Niombe, nami nitayafanya mataifa kuwa urithi wako, miisho ya dunia kuwa milki yako. 9 Utawatawala kwa fimbo ya chuma na kuwavunjavunja kama chombo cha mfinyanzi.” 10 Kwa hiyo, ninyi wafalme, kuweni na hekima; mwonyeke, enyi watawala wa dunia. 11 Mtumikieni Bwana kwa hofu na mshangilie kwa kutetemeka. 12 Mbusu Mwana, asije akakasirika nawe ukaangamizwa katika njia yako, kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula. Heri wote wanaomkimbilia. Chapter 3Zaburi 3 1 Ee Bwana, tazama adui zangu walivyo wengi! Ni wengi kiasi gani wanaoinuka dhidi yangu! 2 Wengi wanasema juu yangu, “Mungu hatamwokoa.” 3 Lakini wewe, Ee Bwana, ni ngao pande zote; umeniwekea utukufu na kuinua kichwa changu. 4 Ninamlilia Bwana kwa sauti kuu, naye ananijibu kutoka mlima wake mtakatifu. 5 Ninajilaza na kupata usingizi; naamka tena, kwa maana Bwana hunitegemeza. 6 Sitaogopa makumi elfu ya adui, wanaojipanga dhidi yangu kila upande. 7 Ee Bwana, amka! Niokoe, Ee Mungu wangu! Wapige adui zangu wote kwenye taya, vunja meno ya waovu. 8 Kwa maana wokovu watoka kwa Bwana. Baraka yako na iwe juu ya watu wako. Chapter 4Zaburi 4 1 Nijibu nikuitapo, Ee Mungu wangu mwenye haki! Nipumzishe katika shida zangu; nirehemu, usikie ombi langu. 2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu kuwa aibu mpaka lini? Mtapenda udanganyifu na kufuata miungu ya uongo mpaka lini? 3 Fahamuni hakika kwamba Bwana amewatenga wale wamchao kwa ajili yake; Bwana atanisikia nimwitapo. 4 Katika hasira yako, usitende dhambi. Mkiwa vitandani mwenu, mtulie kimya mkiichunguza mioyo yenu. 5 Toeni dhabihu zilizo haki; mtegemeeni Bwana. 6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye kutuonyesha jema lolote?” Ee Bwana, tuangazie nuru ya uso wako. 7 Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi. 8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani, kwa kuwa wewe peke yako, Ee Bwana, waniwezesha kukaa kwa salama. Chapter 5Zaburi 5 1 Ee Bwana, tegea sikio maneno yangu, uangalie kupiga kite kwangu. 2 Sikiliza kilio changu ili unisaidie, Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa maana kwako ninaomba. 3 Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Bwana; asubuhi naleta haja zangu mbele zako, na kusubiri kwa matumaini. 4 Wewe si Mungu unayefurahia uovu, kwako mtu mwovu hataishi. 5 Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako, unawachukia wote watendao mabaya. 6 Unawaangamiza wasemao uongo. Bwana huwachukia wamwagao damu na wadanganyifu. 7 Lakini mimi, kwa rehema zako kuu, nitakuja katika nyumba yako, kwa unyenyekevu, nitasujudu kuelekea Hekalu lako takatifu. 8 Niongoze katika haki yako, Ee Bwana, kwa sababu ya adui zangu, nyoosha njia yako mbele yangu. 9 Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika, mioyo yao imejaa maangamizi. Koo lao ni kaburi lililo wazi, kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu. 10 Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu! Hila zao ziwe anguko lao wenyewe. Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi, kwa kuwa wamekuasi wewe. 11 Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi, waimbe kwa shangwe daima. Ueneze ulinzi wako juu yao, ili wale wapendao jina lako wapate kukushangilia. 12 Kwa hakika, Ee Bwana, unawabariki wenye haki, unawazunguka kwa wema wako kama ngao. Chapter 6Zaburi 6 1 Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako, wala usiniadhibu katika ghadhabu yako. 2 Unirehemu Bwana, kwa maana nimedhoofika; Ee Bwana, uniponye, kwa maana mifupa yangu ina maumivu makali. 3 Nafsi yangu ina uchungu mwingi. Mpaka lini, Ee Bwana, mpaka lini? 4 Geuka Ee Bwana, unikomboe, uniokoe kwa sababu ya fadhili zako. 5 Hakuna mtu anayekukumbuka akiwa amekufa. Ni nani awezaye kukusifu akiwa kuzimu? 6 Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni; usiku kucha nafurikisha kitanda changu kwa machozi; nimelowesha viti vyangu vya fahari kwa machozi. 7 Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika, yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote. 8 Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya, kwa maana Bwana amesikia kulia kwangu. 9 Bwana amesikia kilio changu kwa huruma, Bwana amekubali sala yangu. 10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula. Chapter 7Zaburi 7 1 Ee Bwana, Mungu wangu, ninakukimbilia wewe, uniokoe na kunikomboa na wote wanaonifuatia, 2 la sivyo watanirarua kama simba na kunichana vipande vipande, asiwepo wa kuniokoa. 3 Ee Bwana, Mungu wangu, kama nimetenda haya na kuna hatia mikononi mwangu, 4 au ikiwa nimemtenda uovu aliye na amani nami, au nimemnyangʼanya adui yangu pasipo sababu, 5 basi adui anifuatie na kunipata, auponde uhai wangu ardhini na kunilaza mavumbini. 6 Amka kwa hasira yako, Ee Bwana, inuka dhidi ya ghadhabu ya adui zangu. Amka, Mungu wangu, uamue haki. 7 Kusanyiko la watu na likuzunguke. Watawale kutoka juu. 8 Bwana na awahukumu kabila za watu. Nihukumu Ee Bwana, kwa kadiri ya haki yangu, kwa kadiri ya uadilifu wangu, Ewe Uliye Juu Sana. 9 Ee Mungu mwenye haki, uchunguzaye mawazo na mioyo, komesha ghasia za waovu na ufanye wenye haki waishi kwa amani. 10 Ngao langu ni Mungu Aliye Juu Sana, awaokoaye wanyofu wa moyo. 11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Mungu aghadhibikaye kila siku. 12 Kama hakutuhurumia, atanoa upanga wake, ataupinda na kuufunga uzi upinde wake. 13 Ameandaa silaha zake kali, ameweka tayari mishale yake ya moto. 14 Yeye aliye na mimba ya uovu na achukuaye mimba ya ghasia huzaa uongo. 15 Yeye achimbaye shimo na kulifukua hutumbukia katika shimo alilochimba mwenyewe. 16 Ghasia azianzishazo humrudia mwenyewe, ukatili wake humrudia kichwani. 17 Nitamshukuru Bwana kwa ajili ya haki yake, na nitaliimbia sifa jina la Bwana Aliye Juu Sana. Chapter 8Zaburi 8 1 Ee Bwana, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Umeuweka utukufu wako juu ya mbingu. 2 Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao umeamuru sifa, kwa sababu ya watesi wako, kumnyamazisha adui na mlipiza kisasi. 3 Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota, ulizoziratibisha, 4 mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria, binadamu ni nani hata unamjali? 5 Umemfanya chini kidogo kuliko viumbe wa mbinguni, ukamvika taji ya utukufu na heshima. 6 Umemfanya mtawala juu ya kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini ya miguu yake. 7 Mifugo na makundi yote pia, naam, na wanyama wa kondeni, 8 ndege wa angani na samaki wa baharini, naam, kila kiogeleacho katika njia za bahari. 9 Ee Bwana, Bwana wetu, tazama jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote! Chapter 9Zaburi 9 1 Ee Bwana, nitakutukuza kwa moyo wangu wote, nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. 2 Nitafurahi na kushangilia ndani yako. Nitaliimbia sifa jina lako, Ewe Uliye Juu Sana. 3 Adui zangu wamerudi nyuma, wamejikwaa na kuangamia mbele zako. 4 Kwa maana umetetea haki yangu na msimamo wangu; umeketi kwenye kiti chako cha enzi, ukihukumu kwa haki. 5 Umekemea mataifa na kuwaangamiza waovu; umeyafuta majina yao milele na milele. 6 Uharibifu usiokoma umempata adui, umeingʼoa miji yao; hata kumbukumbu lao limetoweka. 7 Bwana anatawala milele, ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu. 8 Mungu atahukumu ulimwengu kwa haki, atatawala mataifa kwa haki. 9 Bwana ni kimbilio la watu wanaoonewa, ni ngome imara wakati wa shida. 10 Wote wanaolijua jina lako watakutumaini wewe, kwa maana wewe Bwana, hujawaacha kamwe wakutafutao. 11 Mwimbieni Bwana sifa, amefanywa mtawala Sayuni, tangazeni miongoni mwa mataifa, yale aliyoyatenda. 12 Kwa maana yeye alipizaye kisasi cha damu hukumbuka, hapuuzi kilio cha wanaoonewa. 13 Ee Bwana, tazama jinsi walivyo wengi adui zangu wanaonitesa! Nihurumie, uniinue kutoka malango ya mauti, 14 ili niweze kutangaza sifa zako katika malango ya Binti Sayuni na huko niushangilie wokovu wako. 15 Mataifa wameanguka kwenye shimo walilolichimba, miguu yao imenaswa kwenye wavu waliouficha. 16 Bwana anajulikana kwa haki yake, waovu wamenaswa katika kazi za mikono yao. 17 Waovu wataishia kuzimu, naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu. 18 Lakini mhitaji hatasahaulika siku zote, wala matumaini ya walioonewa hayatapotea. 19 Ee Bwana, inuka, usimwache binadamu ashinde. Mataifa na yahukumiwe mbele zako. 20 Ee Bwana, wapige kwa hofu, mataifa na yajue kuwa wao ni watu tu. Chapter 10Zaburi 10 1 Kwa nini, Ee Bwana, unasimama mbali? Kwa nini unajificha wakati wa shida? 2 Katika kiburi chake, mwovu humtesa maskini, waovu na wanaswe katika hila wanazozitunga. 3 Hujivunia tamaa za moyo wake; humbariki mlafi na kumtukana Bwana. 4 Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu, katika mawazo yake yote hakuna nafasi ya Mungu. 5 Njia zake daima hufanikiwa; hujivuna na amri zako ziko mbali naye, huwacheka kwa dharau adui zake wote. 6 Anajisemea mwenyewe, “Hakuna kitakachonitikisa, daima nitakuwa na furaha, kamwe sitakuwa na shida.” 7 Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho; shida na ubaya viko chini ya ulimi wake. 8 Huvizia karibu na vijiji; kutoka mafichoni huwanasa wasio na hatia, akivizia wapitaji. 9 Huvizia kama simba aliye mawindoni; huvizia kumkamata mnyonge, huwakamata wanyonge na kuwaburuza katika wavu wake. 10 Mateka wake hupondwa, huzimia; wanaanguka katika nguvu zake. 11 Anajisemea mwenyewe, “Mungu amesahau, huficha uso wake na haoni kabisa.” 12 Inuka Bwana! Inua mkono wako, Ee Mungu. Usiwasahau wanyonge. 13 Kwa nini mtu mwovu anamtukana Mungu? Kwa nini anajiambia mwenyewe, “Hataniita nitoe hesabu?” 14 Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni, umekubali kuyapokea mkononi mwako. Mhanga anajisalimisha kwako, wewe ni msaada wa yatima. 15 Vunja mkono wa mtu mwovu na mbaya, mwite atoe hesabu ya maovu yake ambayo yasingejulikana. 16 Bwana ni Mfalme milele na milele, mataifa wataangamia watoke nchini mwake. 17 Unasikia, Ee Bwana, shauku ya wanaoonewa, wewe huwatia moyo, na kusikiliza kilio chao, 18 ukiwatetea yatima na walioonewa, ili mwanadamu, ambaye ni udongo, asiogopeshe tena. Chapter 11Zaburi 11 1 Kwa Bwana ninakimbilia, unawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege kwenye mlima wako. 2 Hebu tazama, waovu wanapinda pinde zao, huweka mishale kwenye uzi wake, wakiwa gizani ili kuwapiga wale wanyofu wa moyo. 3 Wakati misingi imeharibiwa, mwenye haki anaweza kufanya nini?” 4 Bwana yuko ndani ya Hekalu lake takatifu; Bwana yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni. Huwaangalia wana wa watu, macho yake yanawajaribu. 5 Bwana huwajaribu wenye haki, lakini waovu na wanaopenda jeuri, nafsi yake huwachukia. 6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali na kiberiti kinachowaka, upepo wenye joto kali ndio fungu lao. 7 Kwa kuwa Bwana ni mwenye haki, yeye hupenda haki. Wanyofu watauona uso wake. Chapter 12Zaburi 12 1 Bwana tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka; waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu. 2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo; midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu. 3 Bwana na akatilie mbali midomo yote ya hila na kila ulimi uliojaa majivuno, 4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda; midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?” 5 “Kwa sababu ya uonevu wa wanyonge na kulia kwa uchungu kwa wahitaji, nitainuka sasa,” asema Bwana. “Nitawalinda kutokana na wale wenye nia mbaya juu yao.” 6 Maneno ya Bwana ni safi, kama fedha iliyosafishwa katika tanuru, iliyosafishwa mara saba. 7 Ee Bwana, utatuweka salama na kutulinda na kizazi hiki milele. 8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali wakati ambapo yule aliye mbaya sana ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu. Chapter 13Zaburi 13 1 Mpaka lini, Ee Bwana? Je, utanisahau milele? Utanificha uso wako mpaka lini? 2 Nitapambana na mawazo yangu mpaka lini, na kila siku kuwa na majonzi moyoni mwangu? Adui zangu watanishinda mpaka lini? 3 Nitazame, unijibu, Ee Bwana Mungu wangu. Yatie nuru macho yangu, ama sivyo nitalala usingizi wa mauti. 4 Adui yangu atasema, “Nimemshinda,” nao adui zangu watashangilia nitakapoanguka. 5 Lakini ninategemea upendo wako usiokoma; moyo wangu unashangilia katika wokovu wako. 6 Nitamwimbia Bwana, kwa kuwa amekuwa mwema kwangu. Chapter 14Zaburi 14 1 Mpumbavu anasema moyoni mwake, “Hakuna Mungu.” Wameharibika, matendo yao ni maovu kabisa; hakuna hata mmoja atendaye mema. 2 Bwana anawachungulia wanadamu chini kutoka mbinguni aone kama wako wenye akili, wowote wanaomtafuta Mungu. 3 Wote wamepotoka, wameharibika wote pamoja, hakuna atendaye mema. Naam, hakuna hata mmoja! 4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza: wale ambao huwala watu wangu kama watu walavyo mkate, hao ambao hawamwiti Bwana? 5 Wako hapo, wameingiwa na hofu kuu, maana Mungu yupo pamoja na wenye haki. 6 Ninyi watenda mabaya mnakwamisha mipango ya maskini, bali Bwana ndiye kimbilio lao. 7 Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni! Wakati Bwana arejeshapo wafungwa wa watu wake, Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi! Chapter 15Zaburi 15 1 Bwana, ni nani awezaye kukaa katika Hekalu lako? Nani awezaye kuishi katika mlima wako mtakatifu? 2 Ni yule aendaye pasipo mawaa, atendaye yaliyo haki, asemaye kweli toka moyoni mwake, 3 na hana masingizio ulimini mwake, asiyemtenda jirani yake vibaya, na asiyemsingizia mwenzake, 4 ambaye humdharau mtu mbaya, lakini huwaheshimu wale wamwogopao Bwana, yule atunzaye kiapo chake hata kama anaumia. 5 Yeye akopeshaye fedha yake bila riba, na hapokei rushwa dhidi ya mtu asiye na hatia. Mtu afanyaye haya kamwe hatatikisika. Chapter 16Zaburi 16 1 Ee Mungu, uniweke salama, kwa maana kwako nimekimbilia. 2 Nilimwambia Bwana, “Wewe ndiwe Bwana wangu; pasipo wewe sina jambo jema.” 3 Kwa habari ya watakatifu walioko duniani, ndio walio wa fahari ambao ninapendezwa nao. 4 Huzuni itaongezeka kwa wale wanaokimbilia miungu mingine. Sitazimimina sadaka zao za damu au kutaja majina yao midomoni mwangu. 5 Bwana umeniwekea fungu langu na kikombe changu; umeyafanya mambo yangu yote yawe salama. 6 Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri, hakika nimepata urithi mzuri. 7 Nitamsifu Bwana ambaye hunishauri, hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha. 8 Nimemweka Bwana mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika. 9 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika salama, 10 kwa maana hutaniacha kaburini, wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu. 11 Umenijulisha njia ya uzima; utanijaza na furaha mbele zako, pamoja na furaha za milele katika mkono wako wa kuume. Chapter 17Zaburi 17 1 Sikia, Ee Bwana, kusihi kwangu kwa haki, sikiliza kilio changu. Tega sikio kwa ombi langu, halitoki kwenye midomo ya udanganyifu. 2 Hukumu yangu na itoke kwako, macho yako na yaone yale yaliyo haki. 3 Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku, ingawa umenijaribu, hutaona chochote. Nimeamua kwamba kinywa changu hakitatenda dhambi. 4 Kuhusu matendo ya wanadamu: kwa neno la midomo yako, nimejiepusha na njia za wenye jeuri. 5 Hatua zangu zimeshikamana na njia zako; nyayo zangu hazikuteleza. 6 Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu, nitegee sikio lako na usikie ombi langu. 7 Uonyeshe ajabu ya upendo wako mkuu, wewe uokoaye kwa mkono wako wa kuume wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao. 8 Nilinde kama mboni ya jicho lako, unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako 9 kutokana na waovu wanaonishambulia, kutokana na adui wauaji wanaonizunguka. 10 Huifunga mioyo yao iliyo migumu, vinywa vyao hunena kwa majivuno. 11 Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira, wakiwa macho, waniangushe chini. 12 Wamefanana na simba mwenye njaa awindaye, kama simba mkubwa anyemeleaye mafichoni. 13 Inuka, Ee Bwana, pambana nao, uwaangushe, niokoe kutokana na waovu kwa upanga wako. 14 Ee Bwana, mkono wako uniokoe na watu wa jinsi hii, kutokana na watu wa ulimwengu huu ambao fungu lao liko katika maisha haya. Na wapate adhabu ya kuwatosha. Watoto wao na wapate zaidi ya hayo, hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao. 15 Na mimi katika haki nitauona uso wako, niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako. Chapter 18Zaburi 18 1 Nakupenda wewe, Ee Bwana, nguvu yangu. 2 Bwana ni mwamba wangu, ngome yangu na mwokozi wangu, Mungu wangu ni mwamba, ambaye kwake ninakimbilia. Yeye ni ngao yangu na pembe ya wokovu wangu, ngome yangu. 3 Ninamwita Bwana anayestahili kusifiwa, nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu. 4 Kamba za mauti zilinizunguka, mafuriko ya maangamizi yalinilemea. 5 Kamba za kuzimu zilinizunguka, mitego ya mauti ilinikabili. 6 Katika shida yangu nalimwita Bwana, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika mbele zake, masikioni mwake. 7 Dunia ilitetemeka na kutikisika, misingi ya milima ikatikisika, vilitetemeka kwa sababu alikuwa amekasirika. 8 Moshi ukapanda kutoka puani mwake, moto uteketezao ukatoka kinywani mwake, makaa ya moto yawakayo yakatoka ndani mwake. 9 Akazipasua mbingu akashuka chini, mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake. 10 Alipanda juu ya kerubi akaruka, akapaa juu kwa mbawa za upepo. 11 Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika, hema lake kumzunguka, mawingu meusi ya mvua ya angani. 12 Kutokana na mwanga wa uwepo wake mawingu yalisogea, ikanyesha mvua ya mawe na umeme wa radi. 13 Bwana alinguruma kutoka mbinguni, sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika. 14 Aliipiga mishale yake na kutawanya adui, naam, umeme mwingi wa radi na kuwafukuza. 15 Mabonde ya bahari yalifunuliwa, na misingi ya dunia ikawa wazi kwa kukaripia kwako, Ee Bwana, kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwako. 16 Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika; alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu. 17 Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi, kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi. 18 Walinikabili siku ya msiba wangu, lakini Bwana alikuwa msaada wangu. 19 Alinileta nje mahali penye nafasi tele, akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami. 20 Bwana alinitendea sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa. 21 Kwa maana nimezishika njia za Bwana; sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu. 22 Sheria zake zote zi mbele yangu, wala sijayaacha maagizo yake. 23 Nimekuwa sina hatia mbele zake, nami nimejilinda nisitende dhambi. 24 Bwana amenilipa sawasawa na uadilifu wangu; sawasawa na usafi wa mikono yangu machoni pake. 25 Kwa yeye aliye mwaminifu, unajionyesha kuwa mwaminifu, kwa asiye na hatia, unajionyesha kutokuwa na hatia. 26 Kwa aliye mtakatifu, unajionyesha kuwa mtakatifu, lakini kwa aliyepotoka, unajionyesha kuwa mkaidi. 27 Wewe huwaokoa wanyenyekevu, lakini huwashusha wenye kiburi. 28 Wewe, Ee Bwana, unaifanya taa yangu iendelee kuwaka; Mungu wangu hulifanya giza langu kuwa mwanga. 29 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi, nikiwa pamoja na Mungu wangu nitaweza kuruka ukuta. 30 Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu, neno la Bwana halina dosari. Yeye ni ngao kwa wote wanaokimbilia kwake. 31 Kwa maana ni nani aliye Mungu zaidi ya Bwana? Ni nani aliye Mwamba isipokuwa Mungu wetu? 32 Mungu ndiye anivikaye nguvu na kufanya njia yangu kuwa kamilifu. 33 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu, huniwezesha kusimama mahali palipo juu. 34 Huifundisha mikono yangu kupigana vita; mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba. 35 Hunipa ngao yako ya ushindi, nao mkono wako wa kuume hunitegemeza, unajishusha chini ili kuniinua. 36 Huyapanua mapito yangu, ili miguu yangu isiteleze. 37 Niliwafuatia adui zangu na nikawapata, sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa. 38 Niliwaseta hata hawakuweza kuinuka tena; walianguka chini ya miguu yangu. 39 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita; uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu. 40 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia, nami nikawaangamiza adui zangu. 41 Walipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa; walimlilia Bwana, lakini hakuwajibu. 42 Niliwaponda kama mavumbi yanayopeperushwa na upepo; niliwamwaga nje kama tope barabarani. 43 Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu; umenifanya kuwa kiongozi wa mataifa, watu ambao sikuwajua wananitumikia. 44 Mara wanisikiapo hunitii, wageni hunyenyekea mbele yangu. 45 Wote wanalegea, wanatoka katika ngome zao wakitetemeka. 46 Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu! Atukuzwe Mungu Mwokozi wangu! 47 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi, awatiishaye mataifa chini yangu, 48 aniokoaye na adui zangu. Uliniinua juu ya adui zangu; uliniokoa toka kwa watu wajeuri. 49 Kwa hiyo nitakusifu katikati ya mataifa, Ee Bwana; nitaliimbia sifa jina lako. 50 Humpa mfalme wake ushindi mkuu, huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake, kwa Daudi na wazao wake milele. Chapter 19Zaburi 19 1 Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu, anga zahubiri kazi ya mikono yake. 2 Siku baada ya siku zinatoa habari, usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa. 3 Hakuna msemo wala lugha, ambapo sauti zao hazisikiki. 4 Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu. Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua, 5 linafanana na bwana arusi akitoka chumbani mwake, kama shujaa afurahiavyo kukamilisha kushindana kwake. 6 Huchomoza upande mmoja wa mbingu, na kufanya mzunguko wake hadi upande mwingine. Hakuna kilichojificha joto lake. 7 Sheria ya Bwana ni kamilifu, ikihuisha nafsi. Shuhuda za Bwana ni za kuaminika, zikimpa mjinga hekima. 8 Maagizo ya Bwana ni kamili, nayo hufurahisha moyo. Amri za Bwana huangaza, zatia nuru machoni. 9 Kumcha Bwana ni utakatifu, nako kwadumu milele. Amri za Bwana ni za hakika, nazo zina haki. 10 Ni za thamani kuliko dhahabu, kuliko dhahabu iliyo safi sana, ni tamu kuliko asali, kuliko asali kutoka kwenye sega. 11 Kwa hizo mtumishi wako anaonywa, katika kuzishika kuna thawabu kubwa. 12 Ni nani awezaye kutambua makosa yake? Nisamehe makosa yangu nisiyoyajua. 13 Mlinde mtumishi wako na dhambi za makusudi, nazo zisinitawale. Ndipo nitakapokuwa sina lawama, wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa. 14 Maneno ya kinywa changu na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu na Mkombozi wangu. Chapter 20Zaburi 20 1 Bwana na akujibu unapokuwa katika dhiki, jina la Mungu wa Yakobo na liwe kinga yako. 2 Na akutumie msaada kutoka patakatifu na akupatie msaada kutoka Sayuni. 3 Na azikumbuke dhabihu zako zote, na azikubali sadaka zako za kuteketezwa. 4 Na akujalie haja ya moyo wako, na aifanikishe mipango yako yote. 5 Tutashangilia kwa furaha utakaposhinda, tutainua bendera zetu kwa jina la Mungu wetu. Bwana na akupe haja zako zote. 6 Sasa nafahamu kuwa Bwana humwokoa mpakwa mafuta wake, humjibu kutoka mbingu yake takatifu kwa nguvu za wokovu wa mkono wake wa kuume. 7 Wengine wanatumaini magari ya vita, na wengine farasi, bali sisi tutalitumainia jina la Bwana, Mungu wetu. 8 Wao wameshushwa chini na kuanguka, bali sisi tunainuka na kusimama imara. 9 Ee Bwana, mwokoe mfalme! Tujibu tunapokuita! Chapter 21Zaburi 21 1 Ee Bwana, mfalme huzifurahia nguvu zako. Tazama jinsi ilivyo kuu furaha yake kwa ushindi unaompa! 2 Umempa haja ya moyo wake na hukumzuilia maombi ya midomo yake. 3 Ulimkaribisha kwa baraka tele na kumvika taji ya dhahabu safi kichwani pake. 4 Alikuomba maisha, nawe ukampa, wingi wa siku milele na milele. 5 Kutokana na ushindi uliompa, utukufu wake ni mkubwa, umeweka juu yake fahari na utukufu. 6 Hakika umempa baraka za milele, umemfanya awe na furaha kwa shangwe ya uwepo wako. 7 Kwa kuwa mfalme anamtumaini Bwana; kwa upendo usiokoma wa Aliye Juu Sana hatatikiswa. 8 Mkono wako utawashika adui zako wote, mkono wako wa kuume utawakamata adui zako. 9 Wakati utakapojitokeza utawafanya kama tanuru ya moto. Katika ghadhabu yake Bwana atawameza, moto wake utawateketeza. 10 Utawaangamiza wazao wao kutoka duniani, uzao wao kutoka wanadamu. 11 Ingawa watapanga mabaya dhidi yako na kutunga hila, hawawezi kufanikiwa, 12 kwa kuwa utawafanya wakimbie utakapowalenga usoni pao kwa mshale kutoka kwenye upinde wako. 13 Ee Bwana, utukuzwe katika nguvu zako, tutaimba na kusifu nguvu zako. Chapter 22Zaburi 22 1 Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Kwa nini uko mbali hivyo kuniokoa? Mbali hivyo na maneno ya kuugua kwangu? 2 Ee Mungu wangu, ninalia mchana, lakini hunijibu, hata usiku, sinyamazi. 3 Hata hivyo umesimikwa katika kiti cha enzi kama Uliye Mtakatifu; wewe ni sifa ya Israeli. 4 Kwako wewe baba zetu waliweka tumaini lao, walikutumaini nawe ukawaokoa. 5 Walikulilia wewe na ukawaokoa, walikutegemea wewe nao hawakuaibika. 6 Mimi ni mnyoo wala si mwanadamu, wanaume wamenibeza, na watu wamenidharau. 7 Wote wanionao hunidhihaki, hunivurumishia matusi, wakitikisa vichwa vyao: 8 Husema, “Anamtegemea Bwana, basi Bwana na amwokoe. Amkomboe basi, kwa maana anapendezwa naye.” 9 Hata hivyo ulinitoa tumboni, ukanifanya nikutegemee, hata nilipokuwa ninanyonya matiti ya mama yangu. 10 Nimekabidhiwa kwako tangu kuzaliwa, toka tumboni mwa mama yangu umekuwa Mungu wangu. 11 Usiwe mbali nami, kwa maana shida iko karibu na hakuna wa kunisaidia. 12 Mafahali wengi wamenizunguka, mafahali wa Bashani wenye nguvu wamenizingira. 13 Simba wangurumao wanaorarua mawindo yao hupanua vinywa vyao dhidi yangu. 14 Nimemiminwa kama maji, mifupa yangu yote imetoka katika viungo vyake. Moyo wangu umegeuka kuwa nta, umeyeyuka ndani yangu. 15 Nguvu zangu zimekauka kama kigae, ulimi wangu umegandamana na kaakaa la kinywa changu, kwa sababu umenilaza katika mavumbi ya kifo. 16 Mbwa wamenizunguka, kundi la watu waovu limenizingira, wametoboa mikono yangu na miguu yangu. 17 Naweza kuhesabu mifupa yangu yote, watu wananikodolea macho na kunisimanga. 18 Wanagawana nguo zangu wao kwa wao, na vazi langu wanalipigia kura. 19 Lakini wewe, Ee Bwana, usiwe mbali. Ee Nguvu yangu, uje haraka unisaidie. 20 Okoa maisha yangu na upanga, uhai wangu wa thamani kutoka nguvu za mbwa. 21 Niokoe kutoka kinywani mwa simba, niokoe kutoka pembe za mafahali mwitu. 22 Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu, katika kusanyiko nitakusifu wewe. 23 Ninyi ambao mnamcha Bwana, msifuni! Ninyi nyote wazao wote wa Yakobo, mheshimuni yeye! Mcheni yeye, ninyi wazao wote wa Israeli! 24 Kwa maana hakupuuza wala kudharau mateso ya aliyeonewa; hakumficha uso wake bali alisikiliza kilio chake ili amsaidie. 25 Kwako wewe hutoka kiini cha sifa zangu katika kusanyiko kubwa, nitatimiza nadhiri zangu mbele ya wale wakuchao wewe. 26 Maskini watakula na kushiba, wale wamtafutao Bwana watamsifu: mioyo yenu na iishi milele! 27 Miisho yote ya dunia itakumbuka na kumgeukia Bwana, nazo jamaa zote za mataifa watasujudu mbele zake, 28 kwa maana ufalme ni wa Bwana naye hutawala juu ya mataifa. 29 Matajiri wote wa dunia watasherehekea na kuabudu. Wote waendao mavumbini watapiga magoti mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao. 30 Wazao wa baadaye watamtumikia yeye; vizazi vijavyo vitajulishwa habari za Bwana. 31 Watatangaza haki yake kwa watu ambao hawajazaliwa bado, kwa maana yeye ametenda hili. Chapter 23Zaburi 23 1 Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. 2 Hunilaza katika malisho ya majani mabichi, kando ya maji matulivu huniongoza, 3 hunihuisha nafsi yangu. Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. 4 Hata kama nikipita katikati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami; fimbo yako na mkongojo wako vyanifariji. 5 Waandaa meza mbele yangu machoni pa adui zangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, kikombe changu kinafurika. 6 Hakika wema na upendo vitanifuata siku zote za maisha yangu, nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. Chapter 24Zaburi 24 1 Dunia ni mali ya Bwana, na vyote vilivyomo ndani yake, ulimwengu, na wote waishio ndani yake, 2 maana aliiwekea misingi yake baharini na kuifanya imara juu ya maji. 3 Nani awezaye kuupanda mlima wa Bwana? Ni nani awezaye kusimama patakatifu pake? 4 Ni yule mwenye mikono safi na moyo mweupe, yule ambaye hakuinulia sanamu nafsi yake au kuapa kwa kitu cha uongo. 5 Huyo atapokea baraka kutoka kwa Bwana, na hukumu ya haki kutoka kwa Mungu Mwokozi wake. 6 Hiki ndicho kizazi cha wale wamtafutao, wale wautafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. 7 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, inukeni enyi milango ya kale, ili mfalme wa utukufu apate kuingia. 8 Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Ni Bwana aliye na nguvu na uweza, ni Bwana aliye hodari katika vita. 9 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, viinueni juu enyi milango ya kale, ili Mfalme wa utukufu apate kuingia. 10 Ni nani yeye, huyu Mfalme wa utukufu? Ni Bwana Mwenye Nguvu Zote; yeye ndiye Mfalme wa utukufu. Chapter 25Zaburi 25 1 Kwako wewe, Ee Bwana, nainua nafsi yangu, 2 ni wewe ninayekutumainia, Ee Mungu wangu. Usiniache niaibike, wala usiache adui zangu wakanishinda. 3 Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea atakayeaibishwa, bali wataaibishwa wafanyao hila bila sababu. 4 Nionyeshe njia zako, Ee Bwana, nifundishe mapito yako, 5 niongoze katika kweli yako na kunifundisha, kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu, nalo tumaini langu liko kwako wakati wote. 6 Kumbuka, Ee Bwana, rehema zako kuu na upendo, kwa maana zimekuwepo tangu zamani. 7 Usizikumbuke dhambi za ujana wangu wala njia zangu za uasi, sawasawa na upendo wako unikumbuke, kwa maana wewe ni mwema, Ee Bwana. 8 Bwana ni mwema na mwenye adili, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake. 9 Huwaongoza wanyenyekevu katika haki, naye huwafundisha njia yake. 10 Njia zote za Bwana ni za upendo na uaminifu kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake. 11 Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, unisamehe uovu wangu, ijapokuwa ni mwingi. 12 Ni nani basi, mtu yule anayemcha Bwana? Atamfundisha katika njia atakayoichagua kwa ajili yake. 13 Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake, nao wazao wake watairithi nchi. 14 Siri ya Bwana iko kwa wale wamchao, yeye huwajulisha agano lake. 15 Macho yangu humwelekea Bwana daima, kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa miguu yangu kutoka mtego. 16 Nigeukie na unihurumie, kwa maana mimi ni mpweke na mwenye kuteseka. 17 Shida za moyo wangu zimeongezeka, niokoe katika dhiki yangu. 18 Uangalie mateso na shida zangu na uniondolee dhambi zangu zote. 19 Tazama adui zangu walivyo wengi, pia uone jinsi wanavyonichukia vikali! 20 Uyalinde maisha yangu na uniokoe, usiniache niaibike, kwa maana nimekukimbilia wewe. 21 Uadilifu na uaminifu vinilinde, kwa sababu tumaini langu ni kwako. 22 Ee Mungu, wakomboe Israeli, katika shida zao zote! Chapter 26Zaburi 26 1 Ee Bwana, nithibitishe katika haki, maana nimeishi maisha yasiyo na lawama; nimemtumainia Bwana bila kusitasita. 2 Ee Bwana, unijaribu, unipime, uuchunguze moyo wangu na mawazo yangu; 3 kwa maana upendo wako uko mbele yangu daima, nami natembea siku zote katika kweli yako. 4 Siketi pamoja na watu wadanganyifu, wala siandamani na wanafiki, 5 ninachukia kusanyiko la watenda mabaya na ninakataa kuketi pamoja na waovu. 6 Ninanawa mikono yangu kwa kuwa sina hatia, naikaribia madhabahu yako, Ee Bwana, 7 nikitangaza sifa yako kwa sauti kubwa, huku nikisimulia matendo yako ya ajabu. 8 Ee Bwana, naipenda nyumba yako mahali unakoishi, mahali ambapo utukufu wako hukaa. 9 Usiiondoe nafsi yangu pamoja na watenda dhambi, wala uhai wangu pamoja na wamwagao damu, 10 ambao mikononi mwao kuna mipango miovu, ambao mikono yao ya kuume imejaa rushwa. 11 Bali mimi ninaishi maisha yasiyo na lawama; nikomboe na unihurumie. 12 Miguu yangu imesimama katika uwanja tambarare; katika kusanyiko kuu nitamsifu Bwana. Chapter 27Zaburi 27 1 Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? 2 Waovu watakaposogea dhidi yangu ili wanile nyama yangu, adui zangu na watesi wangu watakaponishambulia, watajikwaa na kuanguka. 3 Hata jeshi linizunguke pande zote, moyo wangu hautaogopa; hata vita vitokee dhidi yangu, hata hapo nitakuwa na ujasiri. 4 Jambo moja ninamwomba Bwana, hili ndilo ninalolitafuta: niweze kukaa nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu, niutazame uzuri wa Bwana na kumtafuta hekaluni mwake. 5 Kwa kuwa siku ya shida, atanihifadhi salama katika maskani yake, atanificha uvulini mwa hema yake na kuniweka juu kwenye mwamba. 6 Kisha kichwa changu kitainuliwa juu ya adui zangu wanaonizunguka. Katika maskani yake nitatoa dhabihu kwa kelele za shangwe; nitamwimbia Bwana na kumsifu. 7 Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee Bwana, unihurumie na unijibu. 8 Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, Bwana “Nitautafuta.” 9 Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu. 10 Hata kama baba yangu na mama wakiniacha, Bwana atanipokea. 11 Nifundishe njia yako, Ee Bwana, niongoze katika njia iliyonyooka kwa sababu ya watesi wangu. 12 Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri. 13 Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai. 14 Mngojee Bwana, uwe hodari na mwenye moyo mkuu, nawe, umngojee Bwana. Chapter 28Zaburi 28 1 Ninakuita wewe, Ee Bwana, Mwamba wangu; usiwe kwangu kama kiziwi. Kwa sababu ukinyamaza nitafanana na walioshuka shimoni. 2 Sikia kilio changu unihurumie ninapokuita kwa ajili ya msaada, niinuapo mikono yangu kuelekea Patakatifu pa Patakatifu pako. 3 Usiniburute pamoja na waovu, pamoja na hao watendao mabaya, ambao huzungumza na jirani zao maneno mazuri, lakini mioyoni mwao wameficha chuki. 4 Walipe sawasawa na matendo yao, sawasawa na matendo yao maovu; walipe sawasawa na kazi za mikono yao, uwalipe wanavyostahili. 5 Kwa kuwa hawaheshimu kazi za Bwana, na yale ambayo mikono yake imetenda, atawabomoa na kamwe hatawajenga tena. 6 Bwana asifiwe, kwa maana amesikia kilio changu nikimwomba anihurumie. 7 Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu, moyo wangu umemtumaini yeye, nami nimesaidiwa. Moyo wangu unarukaruka kwa furaha nami nitamshukuru kwa wimbo. 8 Bwana ni nguvu ya watu wake, ngome ya wokovu kwa mpakwa mafuta wake. 9 Waokoe watu wako na uubariki urithi wako; uwe mchungaji wao na uwabebe milele. Chapter 29Zaburi 29 1 Mpeni Bwana, enyi mashujaa, mpeni Bwana utukufu na nguvu. 2 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake. 3 Sauti ya Bwana iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Bwana hupiga radi juu ya maji makuu. 4 Sauti ya Bwana ina nguvu; sauti ya Bwana ni tukufu. 5 Sauti ya Bwana huvunja mierezi; Bwana huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni. 6 Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati. 7 Sauti ya Bwana hupiga kwa miali ya umeme wa radi. 8 Sauti ya Bwana hutikisa jangwa; Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi. 9 Sauti ya Bwana huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!” 10 Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele. 11 Bwana huwapa watu wake nguvu; Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani. Chapter 30Zaburi 30 1 Nitakutukuza wewe, Ee Bwana, kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi, na hukuacha adui zangu washangilie juu yangu. 2 Ee Bwana, Mungu wangu, nilikuita unisaidie na wewe umeniponya. 3 Ee Bwana, umenitoa Kuzimu, umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti. 4 Mwimbieni Bwana, enyi watakatifu wake; lisifuni jina lake takatifu. 5 Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi, bali upendo wake hudumu siku zote. Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha, lakini asubuhi kukawa na furaha. 6 Nilipofanikiwa nilisema, “Sitatikiswa kamwe.” 7 Ee Bwana, uliponijalia, uliuimarisha mlima wangu, lakini ulipouficha uso wako nilifadhaika. 8 Kwako wewe, Ee Bwana, niliita, kwa Bwana niliomba rehema: 9 “Kuna faida gani katika kuangamia kwangu? Katika kushuka kwangu shimoni? Je, mavumbi yatakusifu? Je, yatatangaza uaminifu wako? 10 Ee Bwana, unisikie na kunihurumia, Ee Bwana, uwe msaada wangu.” 11 Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza, ulinivua nguo za gunia ukanivika shangwe, 12 ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya. Ee Bwana Mungu wangu, nitakushukuru milele. Chapter 31Zaburi 31 1 Ee Bwana, nimekukimbilia wewe, usiache nikaaibika kamwe, kwa haki yako uniokoe. 2 Nitegee sikio lako, uje uniokoe haraka; uwe kwangu mwamba wa kimbilio, ngome imara ya kuniokoa. 3 Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu, uniongoze na kunilinda kwa ajili ya jina lako. 4 Uniepushe na mtego niliotegewa, maana wewe ndiwe kimbilio langu. 5 Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako, unikomboe Ee Bwana, uliye Mungu wa kweli. 6 Ninawachukia wale wanaongʼangʼania sanamu batili; mimi ninamtumaini Bwana. 7 Nitafurahia na kushangilia upendo wako, kwa kuwa uliona mateso yangu na ulijua maumivu ya nafsi yangu. 8 Hukunikabidhi kwa adui yangu bali umeiweka miguu yangu mahali penye nafasi. 9 Ee Bwana unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida; macho yangu yanafifia kwa huzuni, nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko. 10 Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi, naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali; nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso, na mifupa yangu inachakaa. 11 Kwa sababu ya adui zangu wote, nimedharauliwa kabisa na jirani zangu, hata kwa rafiki zangu nimekuwa tisho, wale wanionao barabarani hunikimbia. 12 Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa, nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika. 13 Kwa maana nimesikia maneno niliyosingiziwa na wengi; vitisho viko pande zote; kwa kuwa wamefanya mashauri dhidi yangu, na kula njama kuniua. 14 Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee Bwana; nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.” 15 Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako, uniokoe mikononi mwa adui zangu na wale wanifuatiao. 16 Mwangazie mtumishi wako uso wako, uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma. 17 Usiniache niaibike, Ee Bwana, kwa maana nimekulilia wewe, bali waovu waaibishwe na kunyamazishwa Kuzimu. 18 Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe, kwa maana kwa kiburi na dharau wao husema kwa majivuno dhidi ya wenye haki. 19 Tazama jinsi ulivyo mkuu wema wako, uliowawekea akiba wakuchao, ambao huwapa wale wakukimbiliao machoni pa watu. 20 Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako kutokana na hila za wanadamu; katika makao yako huwaweka salama kutokana na ndimi za mashtaka. 21 Atukuzwe Bwana, kwa kuwa amenionyesha upendo wake wa ajabu nilipokuwa katika mji uliozingirwa. 22 Katika hofu yangu nilisema, “Nimekatiliwa mbali na macho yako!” Hata hivyo ulisikia kilio changu ukanihurumia nilipokuita unisaidie. 23 Mpendeni Bwana ninyi watakatifu wake wote! Bwana huwahifadhi waaminifu, lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu. 24 Kuweni hodari na mjipe moyo, ninyi nyote mnaomtumaini Bwana. Chapter 32Zaburi 32 1 Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake, ambaye dhambi zake zimefunikwa. 2 Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi, na ambaye rohoni mwake hamna udanganyifu. 3 Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa. 4 Usiku na mchana mkono wako ulinilemea, nguvu zangu zilinyonywa kama vile katika joto la kiangazi. 5 Kisha nilikujulisha dhambi yangu wala sikuficha uovu wangu. Nilisema, “Nitaungama makosa yangu kwa Bwana.” Ndipo uliponisamehe hatia ya dhambi yangu. 6 Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe wakati unapopatikana, hakika maji makuu yatakapofurika hayatamfikia yeye. 7 Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha, utaniepusha na taabu na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu. 8 Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; nitakushauri na kukuangalia. 9 Usiwe kama farasi au nyumbu wasio na akili, ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu la sivyo hawatakukaribia. 10 Mtu mwovu ana taabu nyingi, bali upendo usio na kikomo wa Bwana unamzunguka mtu anayemtumaini. 11 Shangilieni katika Bwana na mfurahi, enyi wenye haki! Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo! Chapter 33Zaburi 33 1 Mwimbieni Bwana kwa furaha, enyi wenye haki; kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. 2 Msifuni Bwana kwa kinubi, mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi. 3 Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe. 4 Maana neno la Bwana ni haki na kweli, ni mwaminifu kwa yote atendayo. 5 Bwana hupenda uadilifu na haki; dunia imejaa upendo wake usiokoma. 6 Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa, jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake. 7 Ameyakusanya maji ya bahari kama kwenye chungu; vilindi vya bahari ameviweka katika ghala. 8 Dunia yote na imwogope Bwana, watu wote wa dunia wamche. 9 Kwa maana Mungu alisema, na ikawa, aliamuru na ikasimama imara. 10 Bwana huzuia mipango ya mataifa, hupinga makusudi ya mataifa. 11 Lakini mipango ya Bwana inasimama imara milele, makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote. 12 Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake. 13 Kutoka mbinguni Bwana hutazama chini na kuwaona wanadamu wote; 14 kutoka maskani mwake huwaangalia wote wakaao duniani: 15 yeye ambaye huumba mioyo yao wote, ambaye huangalia kila kitu wanachokitenda. 16 Hakuna mfalme aokokaye kwa ukubwa wa jeshi lake; hakuna shujaa aokokaye kwa wingi wa nguvu zake. 17 Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu, licha ya nguvu zake nyingi, hawezi kuokoa. 18 Lakini macho ya Bwana yako kwa wale wamchao, kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo, 19 ili awaokoe na mauti, na kuwahifadhi wakati wa njaa. 20 Sisi tunamngojea Bwana kwa matumaini, yeye ni msaada wetu na ngao yetu. 21 Mioyo yetu humshangilia, kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu. 22 Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Bwana, tunapoliweka tumaini letu kwako. Chapter 34Zaburi 34 1 Nitamtukuza Bwana nyakati zote, sifa zake zitakuwa midomoni mwangu siku zote. 2 Nafsi yangu itajisifu katika Bwana, walioonewa watasikia na wafurahi. 3 Mtukuzeni Bwana pamoja nami, naam, na tulitukuze jina lake pamoja. 4 Nilimtafuta Bwana naye akanijibu, akaniokoa kwenye hofu zangu zote. 5 Wale wamtazamao hutiwa nuru, nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe. 6 Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia, akamwokoa katika taabu zake zote. 7 Malaika wa Bwana hufanya kituo akiwazunguka wale wamchao, naye huwaokoa. 8 Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema, heri mtu yule anayemkimbilia. 9 Mcheni Bwana enyi watakatifu wake, kwa maana wale wamchao hawapungukiwi na chochote. 10 Wana simba wenye nguvu hutindikiwa na kuona njaa, bali wale wamtafutao Bwana hawatakosa kitu chochote kilicho chema. 11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize, nitawafundisha kumcha Bwana. 12 Yeyote kati yenu anayependa uzima na kutamani kuziona siku nyingi njema, 13 basi auzuie ulimi wake na mabaya, na midomo yake kutokana na kusema uongo. 14 Aache uovu, atende mema, aitafute amani na kuifuatilia. 15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao. 16 Uso wa Bwana uko kinyume na watendao maovu, ili kufuta kumbukumbu lao duniani. 17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia, huwaokoa katika taabu zao zote. 18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo, na huwaokoa waliopondeka roho. 19 Mwenye haki ana mateso mengi, lakini Bwana humwokoa nayo yote, 20 huhifadhi mifupa yake yote, hata mmoja hautavunjika. 21 Ubaya utamuua mtu mwovu, nao adui za mwenye haki watahukumiwa. 22 Bwana huwakomboa watumishi wake, yeyote anayemkimbilia yeye hatahukumiwa kamwe. Chapter 35Zaburi 35 1 Ee Bwana, pingana na wale wanaopingana nami, upigane na hao wanaopigana nami. 2 Chukua ngao na kigao. Inuka unisaidie. 3 Inua mkuki wako na fumo lako dhidi ya hao wanaonifuatia. Iambie nafsi yangu, “Mimi ni wokovu wako.” 4 Wafedheheshwe na waaibishwe wale wanaotafuta uhai wangu. Wanaofanya shauri kuniangamiza warudishwe nyuma kwa hofu. 5 Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, malaika wa Bwana akiwafukuza. 6 Njia yao na iwe giza na ya utelezi, malaika wa Bwana akiwafuatilia. 7 Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu, na bila sababu wamenichimbia shimo, 8 maafa na yawapate ghafula: wavu walionifichia na uwatege wenyewe, na waanguke katika shimo hilo, kwa maangamizo yao. 9 Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Bwana na kuufurahia wokovu wake. 10 Nitapaza sauti yangu nikisema, “Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana? Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao, maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!” 11 Mashahidi wakatili wanainuka, wananiuliza mambo nisiyoyajua. 12 Wananilipa baya kwa jema na kuiacha nafsi yangu ukiwa. 13 Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa nguo ya gunia na nikajinyenyekesha kwa kufunga. Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa, 14 niliendelea kuomboleza kama vile wao ni rafiki au ndugu. Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni kama ninayemwombolezea mama yangu. 15 Lakini nilipojikwaa, walikusanyika kwa shangwe; washambuliaji walijikusanya dhidi yangu bila mimi kujua. Walinisingizia pasipo kukoma. 16 Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki, wamenisagia meno. 17 Ee Bwana, utatazama mpaka lini? Niokoe maisha yangu na maangamizi yao, uhai wangu wa thamani kutokana na simba hawa. 18 Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa, nitakusifu katikati ya watu wengi. 19 Usiwaache wale wanaonisimanga, wale ambao ni adui zangu bila sababu; usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu wakonyeze jicho kwa hila. 20 Hawazungumzi kwa amani, bali wanatunga mashtaka ya uongo dhidi ya wale wanaoishi kwa utulivu katika nchi. 21 Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha! Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.” 22 Ee Bwana, umeona hili, usiwe kimya. Usiwe mbali nami, Ee Bwana. 23 Amka, inuka unitetee! Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu. 24 Nihukumu kwa haki yako, Ee Bwana Mungu wangu, sawasawa na haki yako; usiwaache wakusimange. 25 Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!” Au waseme, “Tumemmeza.” 26 Wote wanaofurahia dhiki yangu waaibishwe na wachanganyikiwe; hao wanaojiinua dhidi yangu wavikwe aibu na dharau. 27 Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki wapige kelele za shangwe na furaha; hebu waseme siku zote, “Bwana atukuzwe, ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.” 28 Ulimi wangu utanena haki yako na sifa zako mchana kutwa. Chapter 36Zaburi 36 1 Kuna neno moyoni mwangu kuhusu hali ya dhambi ya mwovu. Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake. 2 Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake. 3 Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu, ameacha kuwa mwenye hekima na kutenda mema. 4 Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya, hujitia katika njia ya dhambi na hakatai lililo baya. 5 Upendo wako, Ee Bwana, unafika hadi mbinguni, uaminifu wako hadi kwenye anga. 6 Haki yako ni kama milima mikubwa, hukumu zako ni kama kilindi kikuu. Ee Bwana, wewe huwahifadhi mwanadamu na mnyama. 7 Upendo wako usiokoma ni wa thamani mno! Watu wakuu na wadogo hujificha uvulini wa mbawa zako. 8 Wanajifurahisha katika wingi nyumbani mwako, nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako. 9 Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima, katika nuru yako twaona nuru. 10 Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe, haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo. 11 Mguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu, wala mkono wa mwovu usinifukuze. 12 Angalia jinsi watenda mabaya walivyoanguka: wametupwa chini, hawawezi kuinuka! Chapter 37Zaburi 37 1 Usisumbuke kwa ajili ya watendao maovu, wala usiwaonee wivu watendao mabaya, 2 kwa maana kama majani watanyauka mara, kama mimea ya kijani watakufa mara. 3 Mtumaini Bwana na utende yaliyo mema; Kaa katika nchi ukafurahie malisho salama. 4 Jifurahishe katika Bwana naye atakupa haja za moyo wako. 5 Mkabidhi Bwana njia yako, mtumaini yeye, naye atatenda hili: 6 Yeye atafanya haki yako ingʼae kama mapambazuko, na hukumu ya shauri lako kama jua la adhuhuri. 7 Tulia mbele za Bwana na umngojee kwa uvumilivu; usisumbuke watu wanapofanikiwa katika njia zao, wanapotekeleza mipango yao miovu. 8 Epuka hasira na uache ghadhabu, usihangaike: itakuongoza tu kutenda uovu. 9 Kwa maana waovu watakatiliwa mbali, bali wale wanaomtumaini Bwana watairithi nchi. 10 Bado kitambo kidogo, nao waovu hawataonekana, ingawa utawatafuta, hawataonekana. 11 Bali wanyenyekevu watairithi nchi na wafurahie amani tele. 12 Waovu hula njama dhidi ya wenye haki na kuwasagia meno, 13 bali Bwana huwacheka waovu, kwa sababu anajua siku yao inakuja. 14 Waovu huchomoa upanga na kupinda upinde, ili wawaangushe maskini na wahitaji, kuwachinja wale ambao njia zao ni nyofu. 15 Lakini panga zao zitachoma mioyo yao wenyewe, na pinde zao zitavunjwa. 16 Bora kidogo walicho nacho wenye haki kuliko wingi wa mali wa waovu wengi; 17 kwa maana nguvu za waovu zitavunjwa, lakini Bwana humtegemeza mwenye haki. 18 Bwana anazifahamu siku za wanyofu, na urithi wao utadumu milele. 19 Siku za maafa hawatanyauka, siku za njaa watafurahia wingi wa vitu. 20 Lakini waovu wataangamia: Adui za Bwana watakuwa kama uzuri wa mashamba, watatoweka, watatoweka kama moshi. 21 Waovu hukopa na hawalipi, bali wenye haki hutoa kwa ukarimu. 22 Wale wanaobarikiwa na Bwana watairithi nchi, bali wale anaowalaani watakatiliwa mbali. 23 Kama Bwana akipendezwa na njia ya mtu, yeye huimarisha hatua zake, 24 ajapojikwaa, hataanguka, kwa maana Bwana humtegemeza kwa mkono wake. 25 Nilikuwa kijana na sasa ni mzee, lakini sijaona kamwe wenye haki wameachwa au watoto wao wakiombaomba chakula. 26 Wakati wote ni wakarimu na hukopesha bila masharti. Watoto wao watabarikiwa. 27 Acha ubaya na utende wema, nawe utaishi katika nchi milele. 28 Kwa kuwa Bwana huwapenda wenye haki naye hatawaacha waaminifu wake. Watalindwa milele, lakini uzao wa waovu utakatiliwa mbali. 29 Wenye haki watairithi nchi, na kuishi humo milele. 30 Kinywa cha mwenye haki hutamka hekima, nao ulimi wake huzungumza lililo haki. 31 Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake; nyayo zake hazitelezi. 32 Watu waovu huvizia wenye haki, wakitafuta kuwaua; 33 lakini Bwana hatawaacha mikononi mwao wala hatawaacha wahukumiwe kuwa wakosa wanaposhtakiwa. 34 Mngojee Bwana, na uishike njia yake. Naye atakutukuza uirithi nchi, waovu watakapokatiliwa mbali, utaliona hilo. 35 Nimemwona mtu mwovu na mkatili akistawi kama mwerezi wa Lebanoni, 36 lakini alitoweka mara na hakuonekana, ingawa nilimtafuta, hakupatikana. 37 Watafakari watu wasio na hatia, wachunguze watu wakamilifu, kuna mafanikio kwa mtu apendaye amani. 38 Lakini watenda dhambi wote wataangamizwa, mafanikio yao yatakatiliwa mbali. 39 Wokovu wa wenye haki hutoka kwa Bwana, yeye ni ngome yao wakati wa shida. 40 Bwana huwasaidia na kuwaokoa, huwaokoa kutoka kwa waovu na kuwahifadhi, kwa maana wanamkimbilia. Chapter 38Zaburi 38 1 Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako, wala kuniadhibu katika ghadhabu yako. 2 Kwa kuwa mishale yako imenichoma, na mkono wako umenishukia. 3 Hakuna afya mwilini mwangu kwa sababu ya ghadhabu yako, mifupa yangu haina uzima kwa sababu ya dhambi zangu. 4 Maovu yangu yamenifunika kama mzigo usiochukulika. 5 Majeraha yangu yameoza na yananuka, kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu. 6 Nimeinamishwa chini na kushushwa sana, mchana kutwa nazunguka nikiomboleza. 7 Viuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo, hakuna afya mwilini mwangu. 8 Nimedhoofika na kupondwa kabisa, nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni. 9 Ee Bwana, yote ninayoyaonea shauku yako wazi mbele zako, kutamani kwangu sana hakufichiki mbele zako. 10 Moyo wangu unapigapiga, nguvu zangu zimeniishia; hata macho yangu yametiwa giza. 11 Rafiki na wenzangu wananikwepa kwa sababu ya majeraha yangu; majirani zangu wanakaa mbali nami. 12 Wale wanaotafuta uhai wangu wanatega mitego yao, wale ambao wangetaka kunidhuru huongea juu ya maangamizi yangu; hufanya shauri la hila mchana kutwa. 13 Mimi ni kama mtu kiziwi, asiyeweza kusikia, ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake, 14 nimekuwa kama mtu asiyesikia, ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu. 15 Ee Bwana, ninakungojea wewe, Ee Bwana Mungu wangu, utajibu. 16 Kwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie, wala wasijitukuze juu yangu mguu wangu unapoteleza.” 17 Kwa maana ninakaribia kuanguka, na maumivu yangu yananiandama siku zote. 18 Naungama uovu wangu, ninataabishwa na dhambi yangu. 19 Wengi ni wale ambao ni adui zangu hodari, wale wanaonichukia bila sababu ni wengi. 20 Wanaolipa maovu kwa wema wangu hunisingizia ninapofuata lililo jema. 21 Ee Bwana, usiniache, usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu. 22 Ee Bwana Mwokozi wangu, uje upesi kunisaidia. Chapter 39Zaburi 39 1 Nilisema, “Nitaziangalia njia zangu na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi; nitaweka lijamu kinywani mwangu wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.” 2 Lakini niliponyamaza kimya na kutulia, hata pasipo kusema lolote jema, uchungu wangu uliongezeka. 3 Moyo wangu ulipata moto ndani yangu, nilipotafakari, moto uliwaka, ndipo nikasema kwa ulimi wangu: 4 “Ee Bwana, nijulishe mwisho wa maisha yangu na hesabu ya siku zangu; nijalie kujua jinsi maisha yangu yanavyopita upesi. 5 Umefanya maisha yangu mafupi kama pumzi; muda wangu wa kuishi ni kama hauna thamani kwako. Maisha ya kila mwanadamu ni kama pumzi. 6 Hakika kila binadamu ni kama njozi aendapo huku na huko: hujishughulisha na mengi lakini ni ubatili; anakusanya mali nyingi, wala hajui ni nani atakayeifaidi. 7 “Lakini sasa Bwana, nitafute nini? Tumaini langu ni kwako. 8 Niokoe kutoka kwenye makosa yangu yote, usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu. 9 Nilinyamaza kimya, sikufumbua kinywa changu, kwa sababu wewe ndiwe uliyetenda hili. 10 Niondolee mjeledi wako, nimeshindwa kwa mapigo ya mkono wako. 11 Unakemea na kuadhibu wanadamu kwa ajili ya dhambi zao; unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo: kila mwanadamu ni kama pumzi tu. 12 “Ee Bwana, usikie maombi yangu, usikie kilio changu unisaidie, usiwe kiziwi kwa kulia kwangu. Kwani mimi ninaishi na wewe kama mgeni, kama walivyokuwa baba zangu wote, 13 Tazama mbali nami, ili niweze kufurahi tena kabla sijaondoka na nisiwepo tena.” Chapter 40Zaburi 40 1 Nilimngoja Bwana kwa saburi, naye akaniinamia, akasikia kilio changu. 2 Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu, kutoka matope na utelezi; akaiweka miguu yangu juu ya mwamba na kunipa mahali imara pa kusimama. 3 Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa na kuweka tumaini lao kwa Bwana. 4 Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake, asiyewategemea wenye kiburi, wale wenye kugeukia miungu ya uongo. 5 Ee Bwana Mungu wangu, umefanya mambo mengi ya ajabu. Mambo uliyopanga kwa ajili yetu hakuna awezaye kukuhesabia; kama ningesema na kuyaelezea, yangekuwa mengi mno kuyaelezea. 6 Dhabihu na sadaka hukuvitaka, lakini umefungua masikio yangu; sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukuzihitaji. 7 Ndipo niliposema, “Mimi hapa, nimekuja: imeandikwa kunihusu katika kitabu. 8 Ee Mungu wangu, natamani kuyafanya mapenzi yako; sheria yako iko ndani ya moyo wangu.” 9 Nimehubiri haki katika kusanyiko kubwa, sikufunga mdomo wangu, Ee Bwana, kama ujuavyo. 10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu; ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha upendo wako na kweli yako mbele ya kusanyiko kubwa. 11 Ee Bwana, usizuilie huruma zako, upendo wako na kweli yako daima vinilinde. 12 Kwa maana taabu zisizo na hesabu zimenizunguka, dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona. Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu, nao moyo unazimia ndani yangu. 13 Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa; Ee Bwana, njoo hima unisaidie. 14 Wote wanaotafuta kuuondoa uhai wangu, waaibishwe na kufadhaishwa; wote wanaotamani kuangamizwa kwangu, warudishwe nyuma kwa aibu. 15 Wale waniambiao, “Aha! Aha!” wafadhaishwe na iwe aibu yao. 16 Lakini wote wakutafutao washangilie na kukufurahia, wale wapendao wokovu wako siku zote waseme, “Bwana atukuzwe!” 17 Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji; Bwana na anifikirie. Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu; Ee Mungu wangu, usikawie. Chapter 41Zaburi 41 1 Heri mtu yule anayemjali mnyonge, Bwana atamwokoa wakati wa shida. 2 Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake, atambariki katika nchi na hatamwacha katika tamaa ya adui zake. 3 Bwana atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani, atamwinua kutoka kitandani mwake. 4 Nilisema, “Ee Bwana nihurumie, niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.” 5 Adui zangu wanasema kwa hila, “Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.” 6 Kila anapokuja mtu kunitazama, huzungumza uongo, huku moyo wake hukusanya masingizio; kisha huondoka na kuyasambaza huku na huko. 7 Adui zangu wote hunongʼonezana dhidi yangu, hao huniwazia mabaya sana, wakisema, 8 “Ugonjwa mbaya sana umempata, kamwe hatainuka tena kitandani mwake.” 9 Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini, yule aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino chake. 10 Lakini wewe, Ee Bwana, nihurumie, ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi. 11 Najua kwamba wapendezwa nami, kwa kuwa adui yangu hanishindi. 12 Katika uadilifu wangu unanitegemeza na kuniweka kwenye uwepo wako milele. 13 Msifuni Bwana, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Amen na Amen. Chapter 42(Zaburi 42–72) Zaburi 42 1 Kama vile ayala aoneavyo shauku vijito vya maji, ndivyo nafsi yangu ikuoneavyo shauku, Ee Mungu. 2 Nafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai. Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu? 3 Machozi yangu yamekuwa chakula changu usiku na mchana, huku watu wakiniambia mchana kutwa, “Yuko wapi Mungu wako?” 4 Mambo haya nayakumbuka ninapoimimina nafsi yangu: Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu, nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu, kwa kelele za shangwe na za shukrani katikati ya umati uliosherehekea. 5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa sababu bado nitamsifu, Mwokozi wangu na 6 Mungu wangu. Nafsi yangu inasononeka ndani yangu; kwa hiyo nitakukumbuka kutoka nchi ya Yordani, katika vilele vya Hermoni, kutoka Mlima Mizari. 7 Kilindi huita kilindi, katika ngurumo za maporomoko ya maji yako; mawimbi yako yote pamoja na viwimbi vimepita juu yangu. 8 Mchana Bwana huelekeza upendo wake, usiku wimbo wake uko nami: maombi kwa Mungu wa uzima wangu. 9 Ninamwambia Mungu Mwamba wangu, “Kwa nini umenisahau? Kwa nini niendelee kuomboleza, nikiwa nimeonewa na adui?” 10 Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali adui zangu wanaponidhihaki, wakiniambia mchana kutwa, “Yuko wapi Mungu wako?” 11 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa sababu bado nitamsifu, Mwokozi wangu na Mungu wangu. Chapter 43Zaburi 43 1 Ee Mungu unihukumu, nitetee dhidi ya taifa lisilomcha Mungu, niokoe na watu wadanganyifu na waovu. 2 Wewe ni Mungu ngome yangu. Kwa nini umenikataa? Kwa nini niendelee kuomboleza, nikiwa nimeonewa na adui? 3 Tuma hima nuru yako na kweli yako na viniongoze; vinilete mpaka mlima wako mtakatifu, mpaka mahali unapoishi. 4 Ndipo nitakwenda madhabahuni pa Mungu, kwa Mungu, furaha yangu na shangwe yangu. Nitakusifu kwa kinubi, Ee Mungu, Mungu wangu. 5 Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa sababu bado nitamsifu Mwokozi wangu na Mungu wangu. Chapter 44Zaburi 44 1 Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu, baba zetu wametueleza yale uliyotenda katika siku zao, siku za kale. 2 Kwa mkono wako uliwafukuza mataifa na ukawapanda baba zetu, uliangamiza mataifa na kuwastawisha baba zetu. 3 Sio kwa upanga wao waliipata nchi, wala si mkono wao uliwapatia ushindi; ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume, na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwapenda. 4 Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu, unayeamuru ushindi kwa Yakobo. 5 Kwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu; kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu. 6 Siutumaini upinde wangu, upanga wangu hauniletei ushindi; 7 bali wewe unatupa ushindi juu ya adui zetu, unawaaibisha watesi wetu. 8 Katika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa, nasi tutalisifu jina lako milele. 9 Lakini sasa umetukataa na kutudhili, wala huendi tena na jeshi letu. 10 Umetufanya turudi nyuma mbele ya adui, nao watesi wetu wametuteka nyara. 11 Umetuacha tutafunwe kama kondoo na umetutawanya katika mataifa. 12 Umewauza watu wako kwa fedha kidogo, wala hukupata faida yoyote kwa mauzo yao. 13 Umetufanya lawama kwa jirani zetu, dharau na dhihaka kwa wale wanaotuzunguka. 14 Umetufanya kuwa mithali miongoni mwa mataifa, mataifa hutikisa vichwa vyao. 15 Fedheha yangu iko mbele yangu mchana kutwa, na uso wangu umejaa aibu tele, 16 kwa ajili ya dhihaka ya wale wanaonilaumu na kunitukana, kwa sababu ya adui, ambaye anatamani kulipiza kisasi. 17 Hayo yote yametutokea, ingawa tulikuwa hatujakusahau wala hatujaenda kinyume na agano lako. 18 Mioyo yetu ilikuwa haijarudi nyuma; nyayo zetu zilikuwa hazijaiacha njia yako. 19 Lakini ulituponda na kutufanya makao ya mbweha, na ukatufunika kwa giza nene. 20 Kama tungalikuwa tumelisahau jina la Mungu wetu au kunyooshea mikono yetu kwa mungu mgeni, 21 je, Mungu hangaligundua hili, kwa kuwa anazijua siri za moyo? 22 Hata hivyo kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa. 23 Amka, Ee Bwana! Kwa nini unalala? Zinduka! Usitukatae milele. 24 Kwa nini unauficha uso wako na kusahau taabu na mateso yetu? 25 Tumeshushwa hadi mavumbini, miili yetu imegandamana na ardhi. 26 Inuka na utusaidie, utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho. Chapter 45Zaburi 45 1 Moyo wangu umesisimuliwa na jambo jema ninapomsimulia mfalme mabeti yangu; ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi. 2 Wewe ni bora kuliko watu wengine wote na midomo yako imepakwa neema, kwa kuwa Mungu amekubariki milele. 3 Jifunge upanga wako pajani mwako, ee mwenye nguvu, jivike fahari na utukufu. 4 Katika fahari yako, songa mbele kwa ushindi, kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki, mkono wako wa kuume na uonyeshe matendo ya kutisha. 5 Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme, mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako. 6 Ee Mungu, kiti chako cha enzi kitadumu milele na milele, fimbo ya utawala wa haki itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako. 7 Unaipenda haki na kuchukia uovu; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekuweka juu ya wenzako, kwa kukupaka mafuta ya furaha. 8 Mavazi yako yote yana harufu nzuri ya manemane, udi na mdalasini; kutoka kwenye majumba ya kifalme yaliyopambwa kwa pembe za ndovu, sauti za vinanda vya nyuzi zinakufanya ufurahi. 9 Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa; kuume kwako yupo bibi arusi malkia aliyevaa dhahabu ya Ofiri. 10 Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio: Sahau watu wako na nyumba ya baba yako. 11 Mfalme ameshangazwa na uzuri wako; mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako. 12 Binti wa Tiro atakuletea zawadi, watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako. 13 Utukufu wote una binti mfalme katika chumba chake; vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu. 14 Anaongozwa kwa mfalme, akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa, mabikira wenzake wanamfuata na wanaletwa kwako. 15 Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha, na kuingia katika jumba la mfalme. 16 Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu, mtawafanya wakuu katika nchi yote. 17 Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote, kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele. Chapter 46Zaburi 46 1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. 2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari. 3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka, milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake. 4 Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu, mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi. 5 Mungu yuko katikati yake, hautaanguka, Mungu atausaidia asubuhi na mapema. 6 Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka, Yeye huinua sauti yake, dunia ikayeyuka. 7 Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. 8 Njooni mkaone kazi za Bwana jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi. 9 Anakomesha vita hata miisho ya dunia, anakata upinde na kuvunjavunja mkuki, anateketeza ngao kwa moto. 10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu; nitatukuzwa katikati ya mataifa, nitatukuzwa katika dunia.” 11 Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi; Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. Chapter 47Zaburi 47 1 Pigeni makofi, enyi mataifa yote, mpigieni Mungu kelele za shangwe! 2 Jinsi gani alivyo wa kutisha, Bwana Aliye Juu Sana, Mfalme mkuu juu ya dunia yote! 3 Ametiisha mataifa chini yetu watu wengi chini ya miguu yetu. 4 Alituchagulia urithi wetu, fahari ya Yakobo, aliyempenda. 5 Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti za tarumbeta. 6 Mwimbieni Mungu sifa, imbeni sifa, mwimbieni sifa Mfalme wetu, imbeni sifa. 7 Kwa kuwa Mungu ni mfalme wa dunia yote, mwimbieni zaburi za sifa. 8 Mungu anatawala juu ya mataifa, Mungu ameketi juu ya kiti chake cha enzi kitakatifu. 9 Wakuu wa mataifa wanakusanyika kama watu wa Mungu wa Abrahamu, kwa kuwa wafalme wa dunia ni mali ya Mungu; yeye ametukuka sana. Chapter 48Zaburi 48 1 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana, katika mji wa Mungu wetu, mlima wake mtakatifu. 2 Ni mzuri katika kuinuka kwake juu sana, furaha ya dunia yote. Kama vilele vya juu sana vya Safoni ni Mlima Sayuni, mji wa Mfalme Mkuu. 3 Mungu yuko katika ngome zake; amejionyesha mwenyewe kuwa ngome yake. 4 Wakati wafalme walipounganisha nguvu, waliposonga mbele pamoja, 5 walimwona nao wakashangaa, wakakimbia kwa hofu. 6 Kutetemeka kuliwashika huko, maumivu kama ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa. 7 Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi zilizovunjwa na upepo wa mashariki. 8 Kama tulivyokuwa tumesikia, ndivyo tulivyoona katika mji wa Bwana Mwenye Nguvu Zote, katika mji wa Mungu wetu: Mungu ataufanya uwe salama milele. 9 Ee Mungu, hekaluni mwako tunatafakari upendo wako usiokoma. 10 Ee Mungu, kama jina lako lilivyo, sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia, mkono wako wa kuume umejazwa na haki. 11 Mlima Sayuni unashangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako. 12 Tembeeni katika Sayuni, uzungukeni mji, hesabuni minara yake; 13 yatafakarini vyema maboma yake, angalieni ngome zake, ili mpate kusimulia habari zake kwa kizazi kijacho. 14 Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele; atakuwa kiongozi wetu hata mwisho. Chapter 49Zaburi 49 1 Sikieni haya, enyi mataifa yote, sikilizeni, ninyi wote mkaao dunia hii. 2 Wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini pamoja: 3 Kinywa changu kitasema maneno ya hekima, usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu. 4 Nitatega sikio langu nisikilize mithali, nitafafanua kitendawili kwa zeze: 5 Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja, wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka, 6 wale wanaotegemea mali zao na kujivunia utajiri wao mwingi? 7 Hakuna mwanadamu awaye yote awezaye kuukomboa uhai wa mwingine, au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake. 8 Fidia ya uhai ni gharama kubwa, hakuna malipo yoyote yanayotosha, 9 ili kwamba aishi milele na asione uharibifu. 10 Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa; wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia na kuwaachia wengine mali zao. 11 Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele, makao yao vizazi vyote; ingawa walikuwa na mashamba na kuyaita kwa majina yao. 12 Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu; anafanana na mnyama aangamiaye. 13 Hii ndiyo hatima ya wale wanaojitumainia wenyewe, pia ya wafuasi wao, waliothibitisha misemo yao. 14 Kama kondoo, wamewekewa kwenda kaburini, nacho kifo kitawala. Wanyofu watawatawala asubuhi, maumbile yao yataozea kaburini, mbali na majumba yao makubwa ya fahari. 15 Lakini Mungu atakomboa uhai wangu na kaburi, hakika atanichukua kwake. 16 Usitishwe mtu anapotajirika, fahari ya nyumba yake inapoongezeka, 17 kwa maana hatachukua chochote atakapokufa, fahari yake haitashuka pamoja naye. 18 Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri, na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa, 19 atajiunga na kizazi cha baba zake, ambao hawataona kamwe nuru ya uzima. 20 Mwanadamu mwenye utajiri bila ufahamu ni kama wanyama waangamiao. Chapter 50Zaburi 50 1 Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana, asema na kuiita dunia, tangu mawio ya jua hadi mahali pake liendapo kutua. 2 Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu, Mungu anaangaza. 3 Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya, moto uteketezao unamtangulia, akiwa amezungukwa na tufani kali. 4 Anaziita mbingu zilizo juu, na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake: 5 “Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu, waliofanya agano nami kwa dhabihu.” 6 Nazo mbingu zinatangaza haki yake, kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu. 7 “Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema, ee Israeli, nami nitashuhudia dhidi yenu: Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu. 8 Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako, au sadaka zako za kuteketezwa, ambazo daima ziko mbele zangu. 9 Sina haja ya fahali wa banda lako, au mbuzi wa zizi lako. 10 Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu, na pia makundi ya mifugo juu ya vilima elfu. 11 Ninamjua kila ndege mlimani, nao viumbe wa kondeni ni wangu. 12 Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi, kwa maana ulimwengu ni wangu, pamoja na vyote vilivyomo ndani yake. 13 Je, mimi hula nyama ya mafahali au kunywa damu ya mbuzi? 14 Toa sadaka za shukrani kwa Mungu, timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana, 15 na uniite siku ya taabu; nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.” 16 Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema: “Una haki gani kunena sheria zangu au kuchukua agano langu midomoni mwako? 17 Unachukia mafundisho yangu na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. 18 Unapomwona mwizi, unaungana naye, unapiga kura yako pamoja na wazinzi. 19 Unakitumia kinywa chako kwa mabaya na kuuongoza ulimi wako kwa hila. 20 Wanena daima dhidi ya ndugu yako na kumsingizia mwana wa mama yako. 21 Mambo haya unayafanya, nami nimekaa kimya, ukafikiri Mimi nami ni kama wewe. Lakini nitakukemea na kuweka mashtaka mbele yako. 22 “Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu, ama sivyo nitawararua vipande vipande, wala hapatakuwepo na yeyote wa kuwaokoa: 23 Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi, naye aiandaa njia yake ili nimwonyeshe wokovu wa Mungu.” Chapter 51Zaburi 51 1 Ee Mungu, unihurumie, kwa kadiri ya upendo wako usiokoma, kwa kadiri ya huruma yako kuu, uyafute makosa yangu. 2 Unioshe na uovu wangu wote na unitakase dhambi yangu. 3 Kwa maana ninajua makosa yangu, na dhambi yangu iko mbele yangu daima. 4 Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi na kufanya yaliyo mabaya machoni pako, ili uthibitike kuwa wa kweli unenapo, na kuwa na haki utoapo hukumu. 5 Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi, mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba kwa mama yangu. 6 Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni, ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima. 7 Nioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi, unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. 8 Unipe kusikia furaha na shangwe, mifupa uliyoiponda na ifurahi. 9 Ufiche uso wako usizitazame dhambi zangu, na uufute uovu wangu wote. 10 Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu. 11 Usinitupe kutoka mbele zako wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu. 12 Unirudishie tena furaha ya wokovu wako, unipe roho ya utii, ili initegemeze. 13 Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watakugeukia wewe. 14 Ee Mungu, Mungu uniokoaye, niokoe na hatia ya kumwaga damu, nao ulimi wangu utaimba juu ya haki yako. 15 Ee Bwana, fungua midomo yangu, na kinywa changu kitatangaza sifa zako. 16 Wewe hupendezwi na dhabihu, au ningaliileta, hufurahii sadaka za kuteketezwa. 17 Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika, moyo uliovunjika wenye toba, Ee Mungu, hutaudharau. 18 Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi, ukazijenge upya kuta za Yerusalemu. 19 Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki, sadaka nzima za kuteketezwa za kukupendeza sana, pia mafahali watatolewa madhabahuni mwako. Chapter 52Zaburi 52 1 Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya? Kwa nini unajivuna mchana kutwa, wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu? 2 Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi. Ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila. 3 Unapenda mabaya kuliko mema, uongo kuliko kusema kweli. 4 Unapenda kila neno lenye kudhuru, ewe ulimi wenye hila! 5 Hakika Mungu atakushusha chini kwa maangamizi ya milele: atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu kutoka hema yako, atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai. 6 Wenye haki wataona na kuogopa, watamcheka, wakisema, 7 “Huyu ni yule mtu ambaye hakumfanya Mungu kuwa ngome yake, bali alitumainia wingi wa utajiri wake, na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!” 8 Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni unaostawi katika nyumba ya Mungu, nautegemea upendo wa Mungu usiokoma milele na milele. 9 Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda, nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema. Nitakusifu mbele ya watakatifu wako. Chapter 53Zaburi 53 1 Mpumbavu anasema moyoni mwake, “Hakuna Mungu.” Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa, hakuna hata mmoja atendaye mema. 2 Mungu anawachungulia wanadamu chini kutoka mbinguni aone kama wako wenye akili, wowote wanaomtafuta Mungu. 3 Kila mmoja amegeukia mbali, wameharibika wote pamoja, hakuna atendaye mema. Naam, hakuna hata mmoja! 4 Je, watendao mabaya kamwe hawatajifunza: wale ambao huwala watu wangu kama watu walavyo mkate, hao ambao hawamwiti Mungu? 5 Hapo waliingiwa na hofu kuu, ambapo hapakuwa cha kutetemesha. Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia; uliwaaibisha, kwa sababu Mungu aliwadharau. 6 Laiti wokovu wa Israeli ungalikuja kutoka Sayuni! Wakati Mungu arejeshapo wafungwa wa watu wake, Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi! Chapter 54Zaburi 54 1 Ee Mungu uniokoe kwa jina lako, unifanyie hukumu kwa uwezo wako. 2 Ee Mungu, sikia maombi yangu, usikilize maneno ya kinywa changu. 3 Wageni wananishambulia, watu wakatili wanayatafuta maisha yangu, watu wasiomjali Mungu. 4 Hakika Mungu ni msaada wangu, Bwana ndiye anayenitegemeza. 5 Mabaya na yawarudie wale wanaonisingizia, kwa uaminifu wako uwaangamize. 6 Nitakutolea dhabihu za hiari; Ee Bwana, nitalisifu jina lako kwa kuwa ni vyema. 7 Kwa maana ameniokoa katika shida zangu zote, na macho yangu yamewatazama adui zangu kwa ushindi. Chapter 55Zaburi 55 1 Ee Mungu, sikiliza maombi yangu, wala usidharau hoja yangu. 2 Nisikie na unijibu. Mawazo yangu yananisumbua na nimehangaishwa 3 kwa sauti ya adui, kwa kukaziwa macho na waovu, kwa sababu wananiletea mateso juu yangu na kunitukana kwa hasira zao. 4 Moyo wangu umejaa uchungu, hofu ya kifo imenishambulia. 5 Woga na kutetemeka vimenizunguka, hofu kuu imenigharikisha. 6 Nilisema, “Laiti ningekuwa na mbawa za njiwa! Ningeruka niende mbali kupumzika. 7 Ningalitorokea mbali sana na kukaa jangwani, 8 ningaliharakisha kwenda mahali pa salama, mbali na tufani kali na dhoruba.” 9 Ee Bwana, uwatahayarishe waovu na uwachanganyishie semi zao, maana nimeona jeuri na ugomvi mjini. 10 Usiku na mchana wanazunguka juu ya kuta zake, uovu na dhuluma vimo ndani yake. 11 Nguvu za uharibifu zinatenda kazi mjini, vitisho na uongo haviondoki mitaani mwake. 12 Kama aliyenitukana ni adui yangu, ningevumilia, kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu, ningejificha asinione. 13 Kumbe ni wewe, mwenzangu, mshiriki na rafiki yangu wa karibu, 14 ambaye awali tulifurahia ushirika mzuri, tulipokuwa tukienda na umati hekaluni mwa Mungu. 15 Kifo na kiwajie adui zangu ghafula, na washuke kuzimu wangali hai, kwa maana uovu upo ndani yao. 16 Lakini ninamwita Mungu, naye Bwana huniokoa. 17 Jioni, asubuhi na adhuhuri ninalia kwa huzuni, naye husikia sauti yangu. 18 Huniokoa nikawa salama katika vita vilivyopangwa dhidi yangu, ingawa watu wengi hunipinga. 19 Mungu anayemiliki milele, atawasikia na kuwaadhibu, watu ambao hawabadilishi njia zao, wala hawana hofu ya Mungu. 20 Mwenzangu hushambulia rafiki zake, naye huvunja agano lake. 21 Mazungumzo yake ni laini kama siagi, hata hivyo vita vimo moyoni mwake. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa. 22 Mtwike Bwana fadhaa zako, naye atakutegemeza, hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke. 23 Lakini wewe, Ee Mungu, utawashusha waovu katika shimo la uharibifu. Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila, hawataishi nusu ya siku zao. Lakini mimi ninakutumaini wewe. Chapter 56Zaburi 56 1 Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali; mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao. 2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa, wengi wananishambulia kwa kiburi chao. 3 Wakati ninapoogopa, nitakutumaini wewe. 4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu, katika Mungu ninatumaini; sitaogopa. Mwanadamu apatikanaye na kufa, atanitenda nini? 5 Mchana kutwa wanayageuza maneno yangu, siku zote wanapanga shauri la kunidhuru. 6 Wananifanyia hila, wanajificha, wanatazama hatua zangu, wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu. 7 Wasiepuke kwa vyovyote, Ee Mungu, katika hasira yako yaangushe mataifa. 8 Andika maombolezo yangu, orodhesha machozi yangu katika gombo lako: je, haya hayapo katika kumbukumbu zako? 9 Ndipo adui zangu watarudi nyuma ninapoita msaada. Kwa hili nitajua kwamba Mungu yuko upande wangu. 10 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu, katika Bwana, ambaye neno lake ninalisifu, 11 katika Mungu ninatumaini, sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini? 12 Ee Mungu, nina nadhiri kwako, nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani. 13 Kwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti na miguu yangu kwenye kujikwaa, ili niweze kuenenda mbele za Mungu katika nuru ya uzima. Chapter 57Zaburi 57 1 Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie, kwa maana nafsi yangu inakukimbilia. Chini ya uvuli wa mbawa zako nitakimbilia mpaka maafa yapite. 2 Namlilia Mungu Aliye Juu Sana, Mungu atimizaye makusudi yake kwangu. 3 Hutumana kutoka mbinguni na kuniokoa, akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali; Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake. 4 Niko katikati ya simba, nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kuu: watu ambao meno yao ni mikuki na mishale, ambao ndimi zao ni panga kali. 5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, utukufu wako na uenee duniani kote. 6 Waliitegea miguu yangu nyavu, nikainamishwa chini na dhiki. Wamechimba shimo katika njia yangu, lakini wametumbukia humo wao wenyewe. 7 Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti; nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote. 8 Amka, nafsi yangu! Amka, kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko. 9 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa; nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu. 10 Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni, uaminifu wako unazifikia anga. 11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni, utukufu wako na uwe duniani pote. Chapter 58Zaburi 58 1 Enyi watawala, je, kweli mwanena kwa haki? Je, mnahukumu kwa unyofu miongoni mwa watu? 2 La, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu, na mikono yenu hupima jeuri duniani. 3 Waovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao, toka tumboni mwa mama zao ni wakaidi na husema uongo. 4 Sumu yao ni kama sumu ya nyoka, kama ile ya fira ambaye ameziba masikio yake, 5 ambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi, hata kama mganga angecheza kwa ustadi kiasi gani. 6 Ee Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao; Ee Bwana, vunja meno makali ya hao simba! 7 Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi, wavutapo pinde zao, mishale yao na iwe butu. 8 Kama konokono ayeyukavyo akitembea, kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu, wasilione jua. 9 Kabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba, zikiwa mbichi au kavu, waovu watakuwa wamefagiliwa mbali. 10 Wenye haki watafurahi waonapo wakilipizwa kisasi, watakapochovya nyayo zao katika damu ya waovu. 11 Ndipo wanadamu watasema, “Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu, hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.” Chapter 59Zaburi 59 1 Ee Mungu, uniokoe na adui zangu, unilinde kutokana na hao wanaoinuka dhidi yangu. 2 Uniponye na watu watendao mabaya, uniokoe kutokana na wamwagao damu. 3 Tazama wanavyonivizia! Watu wakali wananifanyia hila, ingawa Ee Bwana, mimi sijakosea wala kutenda dhambi. 4 Sijatenda kosa; hata hivyo wako tayari kunishambulia. Inuka unisaidie, uone hali yangu mbaya! 5 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli! Zinduka uyaadhibu mataifa yote, usionyeshe huruma kwa wasaliti. 6 Hurudi wakati wa jioni, wakibweka kama mbwa, wakiuzurura mji. 7 Tazama yale wanayotema kutoka vinywa vyao, hutema upanga kutoka midomo yao, nao husema, “Ni nani atakayetusikia?” 8 Lakini wewe, Bwana, uwacheke; unayadharau mataifa hayo yote. 9 Ee nguvu yangu, ninakutazama wewe, wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu, 10 Mungu wangu unipendaye. Mungu atanitangulia, naye atanifanya niwachekelee wale wanaonisingizia. 11 Lakini usiwaue, Ee Bwana, ngao yetu, au sivyo watu wangu watasahau. Katika uwezo wako wafanye watangetange na uwashushe chini. 12 Kwa ajili ya dhambi za vinywa vyao, kwa ajili ya maneno ya midomo yao, waache wanaswe katika kiburi chao. Kwa ajili ya laana na uongo wanaotamka, 13 wateketeze katika ghadhabu, wateketeze hadi wasiwepo tena. Ndipo itakapofahamika katika miisho ya dunia kwamba Mungu anatawala juu ya Yakobo. 14 Hurudi jioni, wakibweka kama mbwa, wakiuzurura mji. 15 Wanatangatanga wakitafuta chakula, wasipotosheka hubweka kama mbwa. 16 Lakini mimi nitaziimba nguvu zako, asubuhi nitaimba juu ya upendo wako; kwa maana wewe ndiwe ngome yangu na kimbilio langu wakati wa shida. 17 Ee uliye Nguvu zangu, ninakuimbia sifa. Wewe, Ee Mungu, ndiwe ngome yangu, Mungu unipendaye. Chapter 60Zaburi 60 1 Ee Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu, umekasirika: sasa turejeshe upya! 2 Umetetemesha nchi na kuipasua; uiponye mavunjiko yake, kwa maana inatetemeka. 3 Umewaonyesha watu wako nyakati za kukata tamaa; umetunywesha mvinyo unaotuyumbisha. 4 Kwa wale wanaokucha wewe, umewainulia bendera, ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde. 5 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume, ili wale uwapendao wapate kuokolewa. 6 Mungu amenena kutoka patakatifu pake: “Nitaigawa Shekemu kwa ushindi na kulipima Bonde la Sukothi. 7 Gileadi ni yangu na Manase ni yangu; Efraimu ni kofia yangu ya chuma, nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala. 8 Moabu ni sinia langu la kunawia, juu ya Edomu natupa kiatu changu; nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.” 9 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome? Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu? 10 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi, na hutoki tena na majeshi yetu? 11 Tuletee msaada dhidi ya adui, kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu. 12 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi, naye atawaponda adui zetu. Chapter 61Zaburi 61 1 Ee Mungu, sikia kilio changu, usikilize maombi yangu. 2 Kutoka miisho ya dunia ninakuita, ninaita huku moyo wangu unadhoofika; uniongoze kwenye mwamba ule ulio juu kuliko mimi. 3 Kwa kuwa umekuwa kimbilio langu, ngome imara dhidi ya adui. 4 Natamani kukaa hemani mwako milele, na kukimbilia chini ya uvuli wa mbawa zako. 5 Ee Mungu, kwa kuwa umesikia nadhiri zangu, umenipa urithi wa wale wanaoliogopa jina lako. 6 Mwongezee mfalme siku za maisha yake, miaka yake kwa vizazi vingi. 7 Yeye na atawazwe kwenye kiti cha enzi mbele za Mungu milele; amuru upendo wako na uaminifu wako vimlinde. 8 Ndipo daima nitaliimbia sifa jina lako na kuzitimiza nadhiri zangu siku baada ya siku. Chapter 62Zaburi 62 1 Kwa Mungu peke yake nafsi yangu inapata pumziko; wokovu wangu watoka kwake. 2 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; yeye ni ngome yangu, sitatikisika kamwe. 3 Mtamshambulia mtu hata lini? Je, ninyi nyote mtamtupa chini, ukuta huu ulioinama na uzio huu unaotikisika? 4 Walikusudia kikamilifu kumwangusha toka mahali pake pa fahari; wanafurahia uongo. Kwa vinywa vyao hubariki, lakini ndani ya mioyo yao hulaani. 5 Ee nafsi yangu, upumzike, kwa Mungu peke yake, tumaini langu latoka kwake. 6 Yeye peke yake ndiye mwamba wangu na wokovu wangu; ndiye ngome yangu, sitatikisika. 7 Wokovu wangu na heshima yangu viko kwa Mungu, ndiye mwamba wangu wenye nguvu na kimbilio langu. 8 Enyi watu, mtumainini yeye wakati wote, miminieni mioyo yenu kwake, kwa kuwa Mungu ni kimbilio letu. 9 Binadamu wa ngazi ya chini ni pumzi tu, nao wa ngazi ya juu ni uongo tu; wakipimwa kwenye mizani, si chochote; wote kwa pamoja ni pumzi tu. 10 Usitumainie vya udhalimu wala usijivune kwa vitu vya wizi; ingawa utajiri wako utaongezeka, usiviwekee moyo wako. 11 Jambo moja Mungu amelisema, mambo mawili nimeyasikia: kwamba, Ee Mungu, wewe una nguvu, 12 na kwamba, Ee Bwana, wewe ni mwenye upendo. Hakika utampa kila mtu thawabu kwa kadiri ya alivyotenda. Chapter 63Zaburi 63 1 Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo wote; nafsi yangu inakuonea kiu, mwili wangu unakuonea wewe shauku, katika nchi kame na iliyochoka mahali ambapo hapana maji. 2 Nimekuona katika mahali patakatifu na kuuona uwezo wako na utukufu wako. 3 Kwa sababu upendo wako ni bora kuliko uhai, midomo yangu itakuadhimisha. 4 Nitakusifu siku zote za maisha yangu, na kwa jina lako nitainua mikono yangu. 5 Nafsi yangu itatoshelezwa kama kwa wingi wa vyakula; kwa midomo iimbayo kinywa changu kitakusifu wewe. 6 Kitandani mwangu ninakukumbuka wewe, ninawaza juu yako makesha yote ya usiku. 7 Kwa sababu wewe ndiwe msaada wangu, chini ya uvuli wa mbawa zako naimba. 8 Nafsi yangu inaambatana nawe, mkono wako wa kuume hunishika. 9 Wale wanaotafuta uhai wangu wataharibiwa, watakwenda chini kwenye vilindi vya dunia. 10 Watatolewa wafe kwa upanga, nao watakuwa chakula cha mbweha. 11 Bali mfalme atafurahi katika Mungu, wale wote waapao kwa jina la Mungu watamsifu, bali vinywa vya waongo vitanyamazishwa. Chapter 64Zaburi 64 1 Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu, uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui. 2 Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu, kutokana na zile kelele za kundi la watenda mabaya. 3 Wananoa ndimi zao kama panga na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha. 4 Hurusha mishale kutoka kwenye mavizio kwa mtu asiye na hatia, humrushia ghafula bila woga. 5 Kila mmoja humtia moyo mwenzake katika mipango mibaya; huzungumza juu ya kuficha mitego yao, nao husema, “Ni nani ataiona?” 6 Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema, “Tumebuni mpango mkamilifu!” Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila. 7 Bali Mungu atawapiga kwa mishale, nao ghafula wataangushwa. 8 Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao na kuwaleta kwenye maangamizi; wote wawaonao watatikisa vichwa vyao kwa dharau. 9 Wanadamu wote wataogopa, watatangaza kazi za Mungu na kutafakari yale aliyoyatenda. 10 Wenye haki na wafurahi katika Bwana, na wakimbilie kwake; wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye! Chapter 65Zaburi 65 1 Ee Mungu, sifa zakungojea katika Sayuni; kwako wewe nadhiri zetu zitatimizwa. 2 Ewe usikiaye maombi, kwako wewe watu wote watakuja. 3 Tulipokuwa tumefunikwa kabisa na dhambi, wewe ulisamehe makosa yetu. 4 Heri wale uliowachagua na kuwaleta karibu ili waishi katika nyua zako! Tunashibishwa kwa mema ya nyumba yako, mema ya Hekalu lako takatifu. 5 Unatujibu kwa matendo ya kushangaza ya haki, Ee Mungu Mwokozi wetu, tumaini la miisho yote ya duniani na la bahari zilizo mbali sana, 6 uliyeumba milima kwa uwezo wako, ukiwa umejivika nguvu, 7 uliyenyamazisha dhoruba za bahari, ngurumo za mawimbi yake, na ghasia za mataifa. 8 Wale wanaoishi mbali sana wanaogopa maajabu yako, kule asubuhi ipambazukiapo na kule jioni inakofifilia umeziita nyimbo za furaha. 9 Waitunza nchi na kuinyeshea, waitajirisha kwa wingi. Vijito vya Mungu vimejaa maji ili kuwapa watu nafaka, kwa maana wewe umeviamuru. 10 Umeilowesha mifereji yake na kusawazisha kingo zake; umeilainisha kwa manyunyu na kuibariki mimea yake. 11 Umeuvika mwaka taji ya baraka, magari yako yanafurika kwa wingi. 12 Mbuga za majani za jangwani umezineemesha; vilima vimevikwa furaha. 13 Penye nyanda za malisho pamejaa makundi ya wanyama, na mabonde yamepambwa kwa mavuno; vyote vinashangilia kwa furaha na kuimba. Chapter 66Zaburi 66 1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote! 2 Imbeni utukufu wa jina lake; mpeni sifa zake kwa utukufu! 3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako! Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba adui wananyenyekea mbele zako. 4 Dunia yote yakusujudia, wanakuimbia wewe sifa, wanaliimbia sifa jina lako.” 5 Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda, mambo ya kutisha aliyoyatenda miongoni mwa wanadamu! 6 Alifanya bahari kuwa nchi kavu, wakapita kati ya maji kwa miguu, njooni, tumshangilie. 7 Yeye hutawala kwa uwezo wake milele, macho yake huangalia mataifa yote: waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake. 8 Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu, sauti ya sifa yake isikike, 9 ameyahifadhi maisha yetu na kuizuia miguu yetu kuteleza. 10 Ee Mungu, wewe ulitujaribu, ukatusafisha kama fedha. 11 Umetuingiza kwenye nyavu na umetubebesha mizigo mizito migongoni mwetu. 12 Uliwaruhusu watu watukalie vichwani, tulipita kwenye moto na kwenye maji, lakini ulituleta kwenye nchi iliyojaa utajiri tele. 13 Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa na kukutimizia nadhiri zangu: 14 nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi na nilizotamka kwa kinywa changu nilipokuwa katika shida. 15 Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono na sadaka za kondoo dume, nitakutolea mafahali na mbuzi. 16 Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu, nami niwaambie aliyonitendea. 17 Nilimlilia kwa kinywa changu, sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu. 18 Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu, Bwana asingekuwa amenisikiliza; 19 lakini hakika Mungu amenisikiliza na amesikia sauti yangu katika maombi. 20 Sifa apewe Mungu, ambaye hakulikataa ombi langu wala kunizuilia upendo wake! Chapter 67Zaburi 67 1 Mungu aturehemu na kutubariki, na kutuangazia nuru za uso wake, 2 ili njia zako zijulikane duniani, wokovu wako katikati ya mataifa yote. 3 Ee Mungu, mataifa na wakusifu, mataifa yote na wakusifu. 4 Mataifa yote wafurahi na kuimba kwa shangwe, kwa kuwa unatawala watu kwa haki na kuongoza mataifa ya dunia. 5 Ee Mungu, mataifa na wakusifu, mataifa yote na wakusifu. 6 Ndipo nchi itatoa mazao yake, naye Mungu, Mungu wetu, atatubariki. 7 Mungu atatubariki na miisho yote ya dunia itamcha yeye. Chapter 68Zaburi 68 1 Mungu na ainuke, watesi wake watawanyike, adui zake na wakimbie mbele zake. 2 Kama vile moshi upeperushwavyo na upepo, vivyo hivyo uwapeperushe mbali, kama vile nta iyeyukavyo kwenye moto, vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu. 3 Bali wenye haki na wafurahi, washangilie mbele za Mungu, wafurahi na kushangilia. 4 Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake, mtukuzeni yeye aendeshwaye juu ya mawingu: jina lake ni Bwana, furahini mbele zake. 5 Baba wa yatima, mtetezi wa wajane, ni Mungu katika makao yake matakatifu. 6 Mungu huwaweka wapweke katika jamaa, huwaongoza wafungwa wakiimba, bali waasi huishi katika nchi kame. 7 Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako, ulipopita nyikani, 8 dunia ilitikisika, mbingu zikanyesha mvua, mbele za Mungu, Yule wa Sinai, mbele za Mungu, Mungu wa Israeli. 9 Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka. 10 Ee Mungu, watu wako waliishi huko, nawe kwa wingi wa utajiri wako uliwapa maskini mahitaji yao. 11 Bwana alitangaza neno, waliolitangaza neno hilo walikuwa kundi kubwa: 12 “Wafalme na majeshi walikimbia upesi, watu waliobaki kambini waligawana nyara. 13 Hata ulalapo katikati ya mioto ya kambini, mabawa ya njiwa wangu yamefunikwa kwa fedha, manyoya yake kwa dhahabu ingʼaayo.” 14 Wakati Mwenyezi alipowatawanya wafalme katika nchi, ilikuwa kama theluji iliyoanguka juu ya Salmoni. 15 Milima ya Bashani ni milima iliyotukuka, milima ya Bashani ina vilele vilivyochongoka. 16 Enyi milima yenye vilele vilivyochongoka, kwa nini mnakazia macho kwa wivu, katika mlima Mungu anaochagua kutawala, ambako Bwana mwenyewe ataishi milele? 17 Magari ya Mungu ni makumi ya maelfu, na maelfu ya maelfu; Bwana amekuja kutoka Sinai hadi katika patakatifu pake. 18 Ulipopanda juu, uliteka mateka, ukapokea vipawa kutoka kwa wanadamu, hata kutoka kwa wale walioasi, ili wewe, Ee Bwana Mungu, upate kuishi huko. 19 Sifa apewe Bwana, Mungu Mwokozi wetu, ambaye siku kwa siku hutuchukulia mizigo yetu. 20 Mungu wetu ni Mungu aokoaye, Bwana Mwenyezi hutuokoa na kifo. 21 Hakika Mungu ataponda vichwa vya adui zake, vichwa vya hao waendao katika njia za dhambi. 22 Bwana alisema, “Nitawarudisha kutoka Bashani; nitawarudisha kutoka vilindi vya bahari, 23 ili uweze kuchovya miguu yako katika damu ya adui zako, huku ndimi za mbwa wako zikiwa na fungu lake.” 24 Ee Mungu, maandamano yako yameonekana, maandamano ya Mungu wangu, Mfalme wangu, yakielekea patakatifu pake. 25 Mbele wako waimbaji, baada yao wapiga vinanda, pamoja nao wako wanawali wakipiga matari. 26 Msifuni Mungu katika kusanyiko kubwa, msifuni Bwana katika kusanyiko la Israeli. 27 Liko kabila dogo la Benyamini likiwaongoza, wakifuatwa na kundi kubwa la watawala wa Yuda, hatimaye watawala wa Zabuloni na Naftali. 28 Ee Mungu, amuru uwezo wako, Ee Mungu tuonyeshe nguvu zako, kama ulivyofanya hapo awali. 29 Kwa sababu ya Hekalu lako Yerusalemu wafalme watakuletea zawadi. 30 Mkemee mnyama aliyeko kwenye manyasi, kundi la mafahali katikati ya ndama za mataifa. Na walete minara ya madini ya fedha wakinyenyekea. Tawanya mataifa yapendayo vita. 31 Wajumbe watakuja kutoka Misri, Kushi atajisalimisha kwa Mungu. 32 Mwimbieni Mungu, enyi falme za dunia, mwimbieni Bwana sifa, 33 mwimbieni sifa yeye apandaye mbingu za kale zilizo juu, yeye angurumaye kwa sauti kuu. 34 Tangazeni uwezo wa Mungu, ambaye fahari yake iko juu ya Israeli, ambaye uwezo wake uko katika anga. 35 Ee Mungu, wewe unatisha katika mahali patakatifu pako, Mungu wa Israeli huwapa watu wake uwezo na nguvu. Mungu Asifiwe! Chapter 69Zaburi 69 1 Ee Mungu, niokoe, kwa maana maji yamenifika shingoni. 2 Ninazama kwenye vilindi vya matope, pasipo mahali pa kukanyaga, Nimefika kwenye maji makuu, mafuriko yamenigharikisha. 3 Nimechoka kwa kuomba msaada, koo langu limekauka. Macho yangu yanafifia, nikimtafuta Mungu wangu. 4 Wale wanaonichukia bila sababu ni wengi kuliko nywele za kichwa changu; wengi ni adui kwangu bila sababu, wale wanaotafuta kuniangamiza. Ninalazimishwa kurudisha kitu ambacho sikuiba. 5 Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu, wala hatia yangu haikufichika kwako. 6 Ee Bwana, ewe Bwana Mwenye Nguvu Zote, wakutumainio wasiaibishwe kwa ajili yangu; wakutafutao wasifedheheshwe kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli. 7 Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako, aibu imefunika uso wangu. 8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe. 9 Kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila, matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia. 10 Ninapolia na kufunga, lazima nivumilie matusi. 11 Ninapovaa nguo ya gunia, watu hunidharau. 12 Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga, nimekuwa wimbo wa walevi. 13 Lakini Ee Bwana, ninakuomba, kwa wakati ukupendezao; katika upendo wako mkuu, Ee Mungu, unijibu kwa wokovu wako wa hakika. 14 Uniokoe katika matope, usiniache nizame; niokoe na hao wanichukiao, kutoka kwenye vilindi vya maji. 15 Usiache mafuriko yanigharikishe au vilindi vinimeze, au shimo lifumbe kinywa chake juu yangu. 16 Ee Bwana, unijibu, kwa wema wa upendo wako; kwa huruma zako nyingi unigeukie. 17 Usimfiche mtumishi wako uso wako, uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida. 18 Njoo karibu uniokoe, nikomboe kwa sababu ya adui zangu. 19 Unajua jinsi ninavyodharauliwa, kufedheheshwa na kuaibishwa, adui zangu wote unawajua. 20 Dharau zimenivunja moyo na nimekata tamaa, nimetafuta wa kunihurumia, lakini sikumpata, wa kunituliza, lakini sikumpata. 21 Waliweka nyongo katika chakula changu na walinipa siki nilipokuwa na kiu. 22 Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego, nayo iwe upatilizo na tanzi. 23 Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona, nayo migongo yao iinamishwe daima. 24 Uwamwagie ghadhabu yako, hasira yako kali na iwapate. 25 Mahali pao na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi katika mahema yao. 26 Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi, na kuzungumza juu ya maumivu ya wale uliowaumiza. 27 Walipize uovu juu ya uovu, usiwaache washiriki katika wokovu wako. 28 Wafutwe kutoka kitabu cha uzima na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki. 29 Mimi niko katika maumivu na dhiki; Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi. 30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani. 31 Hili litampendeza Bwana kuliko ngʼombe dume, zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake. 32 Maskini wataona na kufurahi: ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi! 33 Bwana huwasikia wahitaji wala hadharau watu wake waliotekwa. 34 Mbingu na dunia zimsifu, bahari na vyote viendavyo ndani yake, 35 kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni na kuijenga tena miji ya Yuda. Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki, 36 watoto wa watumishi wake watairithi na wale wote walipendao jina lake wataishi humo. Chapter 70Zaburi 70 1 Ee Mungu, ufanye haraka kuniokoa; Ee Bwana, njoo hima unisaidie. 2 Wale wanaotafuta kuuondoa uhai wangu, waaibishwe na kufadhaishwa; wote wanaotamani kuangamizwa kwangu, warudishwe nyuma kwa aibu. 3 Wale waniambiao, “Aha! Aha!” warudi nyuma kwa sababu ya aibu yao. 4 Lakini wote wakutafutao washangilie na kukufurahia, wale wapendao wokovu wako siku zote waseme, “Mungu na atukuzwe!” 5 Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji; Ee Mungu, unijie haraka. Wewe ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; Ee Bwana, usikawie. Chapter 71Zaburi 71 1 Ee Bwana, nimekukimbilia wewe, usiache nikaaibika kamwe. 2 Kwa haki yako uniponye na kuniokoa, unitegee sikio lako uniokoe. 3 Uwe kwangu mwamba wa kimbilio, mahali nitakapokimbilia kila wakati; toa amri ya kuniokoa, kwa kuwa wewe ni mwamba wangu na ngome yangu. 4 Ee Mungu wangu uniokoe kutoka kwenye mkono wa mwovu, kutoka kwenye makucha ya watu wabaya na wakatili. 5 Kwa kuwa umekuwa tumaini langu, Ee Bwana Mwenyezi, tegemeo langu tangu ujana wangu. 6 Tangu kuzaliwa nimekutegemea wewe, ulinitoa tumboni mwa mama yangu. Nitakusifu wewe daima. 7 Nimekuwa kama kioja kwa wengi, lakini wewe ni kimbilio langu imara. 8 Kinywa changu kimejazwa sifa zako, nikitangaza utukufu wako mchana kutwa. 9 Usinitupe wakati wa uzee, wala usiniache nguvu zangu zinapopungua. 10 Kwa maana adui zangu wananisengenya, wale wanaonivizia kuniua wafanya hila. 11 Wanasema, “Mungu amemwacha, mkimbilieni mkamkamate, kwani hakuna wa kumwokoa.” 12 Ee Mungu, usiwe mbali nami, njoo haraka kunisaidia, Ee Mungu wangu. 13 Washtaki wangu na waangamie kwa aibu, wale wanaotaka kunidhuru na wafunikwe kwa dharau na fedheha. 14 Lakini mimi, nitatumaini siku zote, nitakusifu zaidi na zaidi. 15 Kinywa changu kitasimulia haki yako, wokovu wako mchana kutwa, ingawa sifahamu kipimo chake. 16 Ee Bwana Mwenyezi, nitakuja na kutangaza matendo yako makuu, nitatangaza haki yako, yako peke yako. 17 Ee Mungu, umenifundisha tangu ujana wangu, hadi leo ninatangaza matendo yako ya ajabu. 18 Ee Mungu, usiniache, hata niwapo mzee wa mvi, mpaka nitangaze uwezo wako kwa kizazi kijacho, nguvu zako kwa wote watakaokuja baadaye. 19 Ee Mungu, haki yako imefika juu katika mbingu, wewe ambaye umefanya mambo makuu. Ee Mungu, ni nani aliye kama wewe? 20 Ingawa umenifanya nipate taabu, nyingi na chungu, utanihuisha tena, kutoka vilindi vya dunia utaniinua tena. 21 Utaongeza heshima yangu na kunifariji tena. 22 Ee Mungu wangu, nitakusifu kwa kinubi kwa ajili ya uaminifu wako; Ee Uliye Mtakatifu wa Israeli, nitakuimbia sifa kwa zeze. 23 Midomo yangu itapaza sauti kwa furaha ninapokuimbia sifa, mimi, ambaye umenikomboa. 24 Ulimi wangu utasimulia matendo yako ya haki mchana kutwa, kwa maana wale waliotaka kunidhuru, wameaibishwa na kufadhaishwa. Chapter 72Zaburi 72 1 Ee Mungu, mjalie mfalme aamue kwa haki yako, mwana wa mfalme kwa haki yako. 2 Atawaamua watu wako kwa haki, watu wako walioonewa kwa haki. 3 Milima italeta mafanikio kwa watu, vilima tunda la haki. 4 Atawatetea walioonewa miongoni mwa watu na atawaokoa watoto wa wahitaji, ataponda mdhalimu. 5 Atadumu kama jua lidumuvyo, kama mwezi, vizazi vyote. 6 Atakuwa kama mvua inyeshayo juu ya shamba lililofyekwa, kama manyunyu yanyeshayo ardhi. 7 Katika siku zake wenye haki watastawi; mafanikio yatakuwepo mpaka mwezi utakapokoma. 8 Atatawala kutoka bahari hadi bahari na kutoka Mto mpaka miisho ya dunia. 9 Makabila ya jangwani watamsujudia, na adui zake wataramba mavumbi. 10 Wafalme wa Tarshishi na wa pwani za mbali watamletea kodi; wafalme wa Sheba na Seba watampa zawadi. 11 Wafalme wote watamsujudia na mataifa yote yatamtumikia. 12 Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia, aliyeonewa asiye na wa kumsaidia. 13 Atawahurumia wanyonge na wahitaji na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti. 14 Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili, kwani damu yao ni ya thamani machoni pake. 15 Aishi maisha marefu! Na apewe dhahabu ya Sheba. Watu wamwombee daima na kumbariki mchana kutwa. 16 Nafaka ijae tele katika nchi yote, juu ya vilele vya vilima na istawi. Tunda lake na listawi kama Lebanoni, listawi kama majani ya kondeni. 17 Jina lake na lidumu milele, na lidumu kama jua. Mataifa yote yatabarikiwa kupitia kwake, nao watamwita aliyebarikiwa. 18 Bwana Mungu, Mungu wa Israeli, apewe sifa, yeye ambaye peke yake hutenda mambo ya ajabu. 19 Jina lake tukufu lisifiwe milele, ulimwengu wote ujae utukufu wake. Amen na Amen. 20 Huu ndio mwisho wa maombi ya Daudi mwana wa Yese. Chapter 73(Zaburi 73–89) Zaburi 73 1 Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, kwa wale ambao mioyo yao ni safi. 2 Bali kwangu mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza; nilikuwa karibu mguu wangu kuachia uliposimama. 3 Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna nilipoona kufanikiwa kwa waovu. 4 Wao hawana taabu, miili yao ina afya na nguvu. 5 Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine, wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine. 6 Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao, wamejivika jeuri. 7 Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi, majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo. 8 Hudhihaki na kusema kwa ukorofi, katika majivuno yao wanatishia kutesa. 9 Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu, nazo ndimi zao humiliki duniani. 10 Kwa hiyo watu wao huwageukia na kunywa maji tele. 11 Wanasema, “Mungu awezaje kujua? Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?” 12 Hivi ndivyo walivyo waovu: siku zote hawajali, wanaongezeka katika utajiri. 13 Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure, ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia. 14 Mchana kutwa nimetaabika, nimeadhibiwa kila asubuhi. 15 Kama ningesema, “Nitasema hivi,” ningelikuwa nimewasaliti watoto wako. 16 Nilipojaribu kuelewa haya yote, yalikuwa magumu kwangu kuelewa. 17 Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu, ndipo nilipotambua mwisho wao. 18 Hakika unawaweka mahali pa utelezi, unawaangusha chini kwa uharibifu. 19 Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula, wanatoweshwa kabisa na vitisho! 20 Kama ndoto mtu aamkapo, hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana, utawatowesha kama ndoto. 21 Wakati moyo wangu ulipohuzunishwa, na roho yangu ilipotiwa uchungu, 22 nilikuwa mpumbavu na mjinga, nilikuwa mnyama mkatili mbele yako. 23 Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote, umenishika mkono wangu wa kuume. 24 Unaniongoza kwa shauri lako, hatimaye utaniingiza katika utukufu. 25 Nani niliye naye mbinguni ila wewe? Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe. 26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa, bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu na fungu langu milele. 27 Wale walio mbali nawe wataangamia, unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako. 28 Lakini kwangu mimi, ni vyema kuwa karibu na Mungu. Nimemfanya Bwana Mwenyezi kimbilio langu; nami nitayasimulia matendo yako yote. Chapter 74Zaburi 74 1 Ee Mungu, mbona umetukataa milele? Mbona hasira yako inatoka moshi juu ya kondoo wa malisho yako? 2 Kumbuka watu uliowanunua zamani, kabila la urithi wako, ambao uliwakomboa: Mlima Sayuni, ambamo uliishi. 3 Geuza hatua zako kuelekea magofu haya ya kudumu, uharibifu wote huu ambao adui ameuleta pale patakatifu. 4 Adui zako wamenguruma pale ulipokutana nasi, wanaweka bendera zao kama alama. 5 Walifanya kama watu wanaotumia mashoka kukata kichaka cha miti. 6 Walivunjavunja milango yote iliyonakshiwa kwa mashoka na vishoka vyao. 7 Waliteketeza kabisa mahali pako patakatifu, wakayanajisi makao ya Jina lako. 8 Walisema mioyoni mwao, “Tutawaponda kabisa!” Walichoma kila mahali ambapo Mungu aliabudiwa katika nchi. 9 Hatukupewa ishara za miujiza; hakuna manabii waliobaki, hakuna yeyote kati yetu ajuaye hali hii itachukua muda gani. 10 Ee Mungu, mtesi atakudhihaki mpaka lini? Je, adui watalitukana jina lako milele? 11 Kwa nini unazuia mkono wako, mkono wako wa kuume? Uutoe kutoka makunjo ya vazi lako na uwaangamize! 12 Lakini wewe, Ee Mungu, ni mfalme wangu tangu zamani, unaleta wokovu duniani. 13 Ni wewe uliyeigawanya bahari kwa uweza wako; ulivunja vichwa vya wanyama wakubwa wa kutisha katika maji. 14 Ni wewe uliyeponda vichwa vya Lewiathani nawe ukamtoa kama chakula kwa viumbe vya jangwani. 15 Ni wewe uliyefungua chemchemi na vijito, ulikausha mito ambayo ilikuwa ikitiririka daima. 16 Mchana ni wako, nao usiku ni wako pia, uliziweka jua na mwezi. 17 Ni wewe uliyeiweka mipaka yote ya dunia, ulifanya kiangazi na masika. 18 Ee Bwana, kumbuka jinsi mtesi alivyokudhihaki, jinsi watu wapumbavu walivyolitukana jina lako. 19 Usiukabidhi uhai wa njiwa wako kwa wanyama wakali wa mwitu; usisahau kabisa uhai wa watu wako wanaoteseka milele. 20 Likumbuke agano lako, maana mara kwa mara mambo ya jeuri yamejaa katika sehemu za giza nchini. 21 Usiruhusu walioonewa warudi nyuma kwa aibu; maskini na wahitaji hebu walisifu jina lako. 22 Inuka, Ee Mungu, ujitetee; kumbuka jinsi wapumbavu wanavyokudhihaki mchana kutwa. 23 Usipuuze makelele ya watesi wako, ghasia za adui zako, zinazoinuka mfululizo. Chapter 75Zaburi 75 1 Ee Mungu, tunakushukuru, tunakushukuru wewe, kwa kuwa jina lako li karibu; watu husimulia matendo yako ya ajabu. 2 Unasema, “Ninachagua wakati maalum; ni mimi nihukumuye kwa haki. 3 Wakati dunia na watu wake wote inapotetemeka, ni mimi ninayezishikilia nguzo zake imara. 4 Kwa wale wenye majivuno ninasema, ‘Msijisifu tena,’ kwa wale waovu, ‘Msiinue pembe zenu. 5 Msiinue pembe zenu dhidi ya mbingu; msiseme kwa shingo zilizonyooshwa.’ ” 6 Hakuna yeyote atokaye mashariki wala magharibi au kutoka jangwani awezaye kumkweza mwanadamu. 7 Bali Mungu ndiye ahukumuye: Humshusha huyu na kumkweza mwingine. 8 Mkononi mwa Bwana kuna kikombe kilichojaa mvinyo unaotoka povu uliochanganywa na vikolezo; huumimina, nao waovu wote wa dunia hunywa mpaka tone la mwisho. 9 Bali mimi, nitatangaza hili milele; nitaimba sifa kwa Mungu wa Yakobo. 10 Nitazikatilia mbali pembe za waovu wote, bali pembe za wenye haki zitainuliwa juu. Chapter 76Zaburi 76 1 Katika Yuda, Mungu anajulikana, jina lake ni kuu katika Israeli. 2 Hema lake liko Salemu, makao yake katika Sayuni. 3 Huko alivunja mishale imetametayo, ngao na panga, silaha za vita. 4 Wewe unangʼaa kwa mwanga, mwenye fahari zaidi ya milima yenye utajiri wa wanyama pori. 5 Mashujaa hulala wametekwa nyara, hulala usingizi wao wa mwisho; hakuna hata mmoja wa watu wa vita anayeweza kuinua mikono yake. 6 Kwa kukemea kwako, Ee Mungu wa Yakobo, farasi na gari la vita vilikaa kimya. 7 Wewe peke yako ndiye wa kuogopwa. Ni nani awezaye kusimama mbele yako unapokasirika? 8 Kutoka mbinguni ulitamka hukumu, nayo nchi ikaogopa, ikawa kimya: 9 wakati wewe, Ee Mungu, ulipoinuka kuhukumu, kuwaokoa wote walioonewa katika nchi. 10 Hakika ghadhabu yako dhidi ya wanadamu inakuletea sifa, na masalia ya ghadhabu yako unajifunga mshipi. 11 Wekeni nadhiri kwa Bwana Mungu wenu na kuzitimiza; nchi zote za jirani na walete zawadi kwa Yule astahiliye kuogopwa. 12 Huvunja roho za watawala; anaogopwa na wafalme wa dunia. Chapter 77Zaburi 77 1 Nilimlilia Mungu ili anisaidie, nilimlilia Mungu ili anisikie. 2 Nilipokuwa katika taabu, nilimtafuta Bwana, usiku nilinyoosha mikono bila kuchoka na nafsi yangu ilikataa kufarijika. 3 Ee Mungu, nilikukumbuka wewe, nikalia kwa huzuni; nikatafakari, roho yangu ikadhoofika. 4 Ulizuia macho yangu kufumba; nilikuwa nasumbuka, nikashindwa kusema. 5 Nilitafakari juu ya siku zilizopita, miaka mingi iliyopita, 6 nilikumbuka nilivyoimba nyimbo usiku. Moyo wangu ulitafakari na roho yangu ikauliza: 7 “Je, Bwana atakataa milele? Je, hatatenda mema tena? 8 Je, upendo wake usio na mwisho umetoweka milele? Je, ahadi yake imekoma nyakati zote? 9 Je, Mungu amesahau kuwa na huruma? Je, katika hasira amezuia huruma yake?” 10 Ndipo nikawaza, “Huu ndio udhaifu wangu: lakini nitakumbuka miaka ya mkono wa kuume wa Aliye Juu Sana.” 11 Nitayakumbuka matendo ya Bwana; naam, nitaikumbuka miujiza yako ya zamani. 12 Nitazitafakari kazi zako zote na kuyawaza matendo yako makuu. 13 Ee Mungu, njia zako ni takatifu. Ni mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu? 14 Wewe ndiwe Mungu utendaye miujiza, umeonyesha uwezo wako katikati ya mataifa. 15 Kwa mkono wako wenye nguvu umewakomboa watu wako, uzao wa Yakobo na Yosefu. 16 Maji yalikuona, Ee Mungu, maji yalikuona yakakimbia, vilindi vilitetemeka. 17 Mawingu yalimwaga maji, mbingu zikatoa ngurumo kwa radi, mishale yako ikametameta huku na huko. 18 Ngurumo yako ilisikika katika upepo wa kisulisuli, umeme wako wa radi ukaangaza dunia, nchi ikatetemeka na kutikisika. 19 Njia yako ilipita baharini, mapito yako kwenye maji makuu, ingawa nyayo zako hazikuonekana. 20 Uliongoza watu wako kama kundi kwa mkono wa Mose na Aroni. Chapter 78Zaburi 78 1 Enyi watu wangu, sikieni mafundisho yangu, sikilizeni maneno ya kinywa changu. 2 Nitafungua kinywa changu kwa mafumbo, nitazungumza mambo yaliyofichika, mambo ya kale: 3 yale ambayo tuliyasikia na kuyajua, yale ambayo baba zetu walituambia. 4 Hatutayaficha kwa watoto wao; tutakiambia kizazi kijacho matendo yastahiliyo sifa ya Bwana, uweza wake, na maajabu aliyoyafanya. 5 Aliagiza amri kwa Yakobo na akaweka sheria katika Israeli, ambazo aliwaamuru baba zetu wawafundishe watoto wao, 6 ili kizazi kijacho kizijue, pamoja na watoto ambao watazaliwa, nao pia wapate kuwaeleza watoto wao. 7 Ndipo wangeweka tumaini lao kwa Mungu, nao wasingesahau matendo yake, bali wangalizishika amri zake. 8 Ili wasifanane na baba zao, waliokuwa kizazi cha ukaidi na uasi, ambao roho zao hazikuwa na uaminifu kwake, ambao roho zao hazikumwamini. 9 Watu wa Efraimu, ingawa walijifunga pinde, walikimbia siku ya vita. 10 Hawakulishika agano la Mungu na walikataa kuishi kwa sheria yake. 11 Walisahau aliyokuwa ameyatenda, maajabu aliyokuwa amewaonyesha. 12 Alitenda miujiza machoni mwa baba zao, huko Soani, katika nchi ya Misri. 13 Aliigawanya bahari akawapitisha, alifanya maji yasimame imara kama ukuta. 14 Aliwaongoza kwa wingu mchana na kwa nuru kutoka kwenye moto usiku kucha. 15 Alipasua miamba jangwani na akawapa maji tele kama bahari, 16 alitoa vijito kutoka kwenye jabali lililochongoka, akayafanya maji yatiririke kama mito. 17 Lakini waliendelea kutenda dhambi dhidi yake, wakiasi jangwani dhidi ya Aliye Juu Sana. 18 Kwa makusudi walimjaribu Mungu, wakidai vyakula walivyovitamani. 19 Walinena dhidi ya Mungu, wakisema, “Je, Mungu aweza kuandaa meza jangwani? 20 Alipopiga mwamba, maji yalitoka kwa nguvu, vijito vikatiririka maji mengi. Lakini je, aweza kutupa chakula pia? Je, anaweza kuwapa watu wake nyama?” 21 Bwana alipowasikia, alikasirika sana, moto wake ukawa dhidi ya Yakobo, na ghadhabu yake ikawaka dhidi ya Israeli, 22 kwa kuwa hawakumwamini Mungu, wala kuutumainia ukombozi wake. 23 Hata hivyo alitoa amri kwa anga zilizo juu na kufungua milango ya mbingu, 24 akawanyeshea mana ili watu wale; aliwapa nafaka ya mbinguni. 25 Watu walikula mkate wa malaika, akawatumia chakula chote ambacho wangeliweza kula. 26 Aliachia upepo wa mashariki kutoka kwenye mbingu na kuuongoza upepo wa kusini kwa uwezo wake. 27 Aliwanyeshea nyama kama mavumbi, ndege warukao kama mchanga wa pwani. 28 Aliwafanya washuke ndani ya kambi yao, kuzunguka mahema yao yote. 29 Walikula na kusaza, kwa maana alikuwa amewapa kile walichotamani. 30 Kabla hawajamaliza kula walichokitamani, hata kilipokuwa kingali bado vinywani mwao, 31 hasira ya Mungu ikawaka juu yao, akawaua wale waliokuwa na nguvu zaidi miongoni mwao, akiwaangusha vijana wa Israeli. 32 Licha ya haya yote, waliendelea kutenda dhambi, licha ya maajabu yake, hawakuamini. 33 Kwa hiyo akamaliza siku zao katika ubatili na miaka yao katika vitisho. 34 Kila mara Mungu alipowaua baadhi yao, waliosalia walimtafuta, walimgeukia tena kwa shauku. 35 Walikumbuka kwamba Mungu alikuwa Mwamba wao, kwamba Mungu Aliye Juu Sana alikuwa Mkombozi wao. 36 Lakini walimdanganya kwa vinywa vyao, wakisema uongo kwa ndimi zao, 37 mioyo yao haikuwa thabiti kwake, wala hawakuwa waaminifu katika agano lake. 38 Hata hivyo alikuwa na huruma, alisamehe maovu yao na hakuwaangamiza. Mara kwa mara alizuia hasira yake, wala hakuchochea ghadhabu yake yote. 39 Alikumbuka kwamba wao walikuwa nyama tu, upepo upitao ambao haurudi. 40 Mara ngapi walimwasi jangwani na kumhuzunisha nyikani! 41 Walimjaribu Mungu mara kwa mara, wakamkasirisha yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. 42 Hawakukumbuka uwezo wake, siku aliyowakomboa kutoka kwa mtesi, 43 siku aliyoonyesha ishara zake za ajabu huko Misri, maajabu yake huko Soani. 44 Aligeuza mito yao kuwa damu, hawakuweza kunywa maji kutoka vijito vyao. 45 Aliwapelekea makundi ya mainzi yakawala, na vyura wakawaharibu. 46 Aliruhusu tunutu kuharibu mimea yao, mazao yao kwa nzige. 47 Aliharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe na mikuyu yao kwa mvua iliyochangamana na theluji. 48 Aliwaachia mifugo yao mvua ya mawe, akayapiga makundi ya wanyama wao kwa radi. 49 Aliwafungulia hasira yake kali, ghadhabu yake, hasira na uadui, na kundi la malaika wa kuharibu. 50 Aliitengenezea njia hasira yake, hakuwaepusha na kifo, bali aliwaachia tauni. 51 Aliwapiga wazaliwa wote wa kwanza wa Misri, matunda ya kwanza ya ujana katika mahema ya Hamu. 52 Lakini aliwatoa watu wake kama kundi, akawaongoza kama kondoo kupitia jangwani. 53 Aliwaongoza salama, wala hawakuogopa, bali bahari iliwameza adui zao. 54 Hivyo akawaleta hadi kwenye mpaka wa nchi yake takatifu, hadi nchi ya vilima ambayo mkono wake wa kuume ulikuwa umeitwaa. 55 Aliyafukuza mataifa mbele yao, na kuwagawia nchi zao kama urithi, aliwakalisha makabila ya Israeli katika makao yao. 56 Lakini wao walimjaribu Mungu, na kuasi dhidi ya Yeye Aliye Juu Sana, wala hawakuzishika sheria zake. 57 Kama baba zao, hawakuwa thabiti wala waaminifu, wakawa wasioweza kutegemewa kama upinde wenye kasoro. 58 Wakamkasirisha Mungu kwa mahali pao pa juu pa kuabudia miungu, wakachochea wivu wake kwa sanamu zao. 59 Wakati Mungu alipowasikia, alikasirika sana, akamkataa Israeli kabisa. 60 Akaiacha hema ya Shilo, hema aliyokuwa ameiweka katikati ya wanadamu. 61 Akalipeleka Sanduku la nguvu zake utumwani, utukufu wake mikononi mwa adui. 62 Aliachia watu wake wauawe kwa upanga, akaukasirikia sana urithi wake. 63 Moto uliwaangamiza vijana wao, na wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi, 64 makuhani wao waliuawa kwa upanga, wala wajane wao hawakuweza kulia. 65 Ndipo Bwana alipoamka kama vile kuamka usingizini, kama vile mtu aamkavyo kutoka kwenye bumbuazi la mvinyo. 66 Aliwapiga na kuwashinda adui zake, akawatia katika aibu ya milele. 67 Ndipo alipozikataa hema za Yosefu, hakulichagua kabila la Efraimu, 68 lakini alilichagua kabila la Yuda, Mlima Sayuni, ambao aliupenda. 69 Alijenga patakatifu pake kama vilele, kama dunia ambayo aliimarisha milele. 70 Akamchagua Daudi mtumishi wake na kumtoa kwenye mazizi ya kondoo. 71 Kutoka kuchunga kondoo alimleta kuwa mchungaji wa watu wake Yakobo, wa Israeli urithi wake. 72 Naye Daudi aliwachunga kwa uadilifu wa moyo, kwa mikono ya ustadi aliwaongoza. Chapter 79Zaburi 79 1 Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako, wamelinajisi Hekalu lako takatifu, wameifanya Yerusalemu kuwa magofu. 2 Wametoa maiti za watumishi kuwa chakula cha ndege wa angani na nyama ya watakatifu wako kwa wanyama wa nchi. 3 Wamemwaga damu kama maji kuzunguka Yerusalemu yote, wala hakuna yeyote wa kuwazika. 4 Tumekuwa kitu cha aibu kwa jirani zetu, cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka. 5 Hata lini, Ee Bwana? Je, wewe utakasirika milele? Wivu wako utawaka kama moto hadi lini? 6 Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali, juu ya falme za hao wasioliitia jina lako, 7 kwa maana wamemrarua Yakobo na kuharibu nchi ya makao yake. 8 Usituhesabie dhambi za baba zetu, huruma yako na itujie hima, kwa maana tu wahitaji mno. 9 Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; tuokoe na kutusamehe dhambi zetu kwa ajili ya jina lako. 10 Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wenu?” Mbele ya macho yetu, dhihirisha kati ya mataifa kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa ya watumishi wako. 11 Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako; kwa nguvu za mkono wako hifadhi wale waliohukumiwa kufa. 12 Walipize jirani zetu mara saba vifuani mwao aibu walizovurumisha juu yako, Ee Bwana. 13 Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako, tutakusifu milele; toka kizazi hadi kizazi tutasimulia sifa zako. Chapter 80Zaburi 80 1 Ee Mchungaji wa Israeli tusikie, wewe umwongozaye Yosefu kama kundi; wewe uketiye katika kiti cha enzi katikati ya makerubi, angaza 2 mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase. Uamshe nguvu zako, uje utuokoe. 3 Ee Mungu, uturejeshe, utuangazie uso wako, ili tuweze kuokolewa. 4 Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, hata lini hasira yako itawaka na kufoka moshi dhidi ya maombi ya watu wako? 5 Umewalisha kwa mkate wa machozi, umewafanya wanywe machozi bakuli tele. 6 Tumekuwa chanzo cha ugomvi kwa jirani zetu, na adui zetu wanatudhihaki. 7 Ee Mungu Mwenye Nguvu Zote, uturejeshe; utuangazie uso wako, nasi tuweze kuokolewa. 8 Ulileta mzabibu kutoka Misri, ukawafukuza mataifa, ukaupanda. 9 Uliandaa shamba kwa ajili yake, mizizi ikawa imara, ukajaza nchi. 10 Milima ilifunikwa kwa kivuli chake, matawi yake yakafunika mierezi mikubwa. 11 Matawi yake yalienea mpaka Baharini, machipukizi yake mpaka kwenye Mto. 12 Mbona umebomoa kuta zake ili wote wapitao karibu wazichume zabibu zake? 13 Nguruwe mwitu wanauharibu na wanyama wa kondeni hujilisha humo. 14 Turudie, Ee Mungu Mwenye Nguvu Zote! Tazama chini kutoka mbinguni na uone! Linda mzabibu huu, 15 mche ulioupanda kwa mkono wako wa kuume, mwana uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe. 16 Mzabibu wako umekatwa, umechomwa moto, unapowakemea, watu wako huangamia. 17 Mkono wako na utulie juu ya mtu aliyeko mkono wako wa kuume, mwana wa mtu uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe. 18 Ndipo hatutakuacha tena, utuhuishe, nasi tutaliitia jina lako. 19 Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, uturejeshe; utuangazie uso wako, ili tuweze kuokolewa. Chapter 81Zaburi 81 1 Mwimbieni kwa furaha, Mungu aliye nguvu yetu; mpigieni kelele za shangwe Mungu wa Yakobo! 2 Anzeni wimbo, pigeni matari, pigeni kinubi na zeze kwa sauti nzuri. 3 Pigeni baragumu za pembe za kondoo dume wakati wa Mwandamo wa Mwezi, na wakati wa mwezi mpevu, katika siku ya Sikukuu yetu; 4 hii ni amri kwa Israeli, agizo la Mungu wa Yakobo. 5 Aliiweka iwe kama sheria kwa Yosefu alipotoka dhidi ya Misri, huko tulikosikia lugha ambayo hatukuielewa. 6 Asema, “Nimeondoa mzigo mabegani mwao; mikono yao iliwekwa huru kutoka kwenye kikapu. 7 Katika shida yako uliniita nami nikakuokoa, nilikujibu katika mawingu yenye ngurumo; nilikujaribu katika maji ya Meriba. 8 “Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya: laiti kama mngenisikiliza, ee Israeli! 9 Hamtakuwa na mungu mgeni miongoni mwenu; msimsujudie mungu wa kigeni. 10 Mimi ni Bwana Mungu wako, niliyekutoa nchi ya Misri. Panua sana kinywa chako nami nitakijaza. 11 “Lakini watu wangu hawakutaka kunisikiliza; Israeli hakutaka kunitii. 12 Basi niliwaacha katika ukaidi wa mioyo yao wafuate mashauri yao wenyewe. 13 “Laiti kama watu wangu wangalinisikiliza, kama Israeli wangalifuata njia zangu, 14 ningaliwatiisha adui zao kwa haraka, na kuugeuza mkono wangu dhidi ya watesi wao! 15 Wale wanaomchukia Bwana wangalinyenyekea mbele zake, na adhabu yao ingedumu milele. 16 Bali ninyi mngalilishwa ngano iliyo bora, na kuwatosheleza kwa asali itokayo kwenye mwamba.” Chapter 82Zaburi 82 1 Mungu anaongoza kusanyiko kuu, anatoa hukumu miongoni mwa “miungu”: 2 “Hata lini utaendelea kuwatetea wasio haki na kuonyesha upendeleo kwa waovu? 3 Teteeni wanyonge na yatima, tunzeni haki za maskini na walioonewa. 4 Mwokoeni mnyonge na mhitaji, wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu. 5 “Hawajui lolote, hawaelewi lolote. Wanatembea gizani; misingi yote ya dunia imetikisika. 6 “Nilisema, ‘Ninyi ni “miungu”; ninyi nyote ni wana wa Aliye Juu Sana.’ 7 Lakini mtakufa kama wanadamu wa kawaida; mtaanguka kama mtawala mwingine yeyote.” 8 Ee Mungu, inuka uihukumu nchi, kwa kuwa mataifa yote ni urithi wako. Chapter 83Zaburi 83 1 Ee Mungu, usinyamaze kimya, usinyamaze, Ee Mungu, usitulie. 2 Tazama watesi wako wanafanya fujo, jinsi adui zako wanavyoinua vichwa vyao. 3 Kwa hila, wanafanya shauri dhidi ya watu wako, wanafanya shauri baya dhidi ya wale unaowapenda. 4 Wanasema, “Njooni, tuwaangamize kama taifa, ili jina la Israeli lisikumbukwe tena.” 5 Kwa nia moja wanapanga mashauri mabaya pamoja, wanafanya muungano dhidi yako, 6 mahema ya Edomu na Waishmaeli, ya Wamoabu na Wahagari, 7 Gebali, Amoni na Amaleki, Ufilisti, pamoja na watu wa Tiro. 8 Hata Ashuru wameungana nao kuwapa nguvu wazao wa Loti. 9 Uwatendee kama vile ulivyowatendea Midiani, na kama vile ulivyowatendea Sisera na Yabini hapo kijito cha Kishoni, 10 ambao waliangamia huko Endori na wakawa kama takataka juu ya nchi. 11 Wafanye wakuu wao kama Orebu na Zeebu, watawala wao kama Zeba na Salmuna, 12 ambao walisema, “Na tumiliki nchi ya malisho ya Mungu.” 13 Ee Mungu wangu, wapeperushe kama mavumbi ya kisulisuli, kama makapi yapeperushwayo na upepo. 14 Kama vile moto uteketezavyo msitu au mwali wa moto unavyounguza milima, 15 wafuatilie kwa tufani yako na kuwafadhaisha kwa dhoruba yako. 16 Funika nyuso zao kwa aibu ili watu walitafute jina lako, Ee Bwana. 17 Wao na waaibishwe na kufadhaishwa milele, na waangamie kwa aibu. 18 Hebu wajue kwamba wewe, ambaye jina lako ni Bwana, kwamba wewe peke yako ndiwe Uliye Juu Sana ya dunia yote. Chapter 84Zaburi 84 1 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, makao yako yapendeza kama nini! 2 Nafsi yangu inatamani sana, naam, hata kuona shauku, kwa ajili ya nyua za Bwana; moyo wangu na mwili wangu vinamlilia Mungu Aliye Hai. 3 Hata shomoro amejipatia makao, mbayuwayu amejipatia kiota mahali awezapo kuweka makinda yake: mahali karibu na madhabahu yako, Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mfalme wangu na Mungu wangu. 4 Heri wale wanaokaa nyumbani mwako, wanaokusifu wewe daima. 5 Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako, na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao. 6 Wanapopita katika Bonde la Baka, hulifanya mahali pa chemchemi, pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi. 7 Huendelea toka nguvu hadi nguvu, hadi kila mmoja afikapo mbele za Mungu huko Sayuni. 8 Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, sikia maombi yangu; nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo. 9 Ee Mungu, uitazame ngao yetu, mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako. 10 Siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu kuliko kukaa katika mahema ya waovu. 11 Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao, Bwana hutoa wema na heshima; hakuna kitu chema anachowanyima wale ambao hawana hatia. 12 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, heri ni mtu yule anayekutumaini wewe. Chapter 85Zaburi 85 1 Ee Bwana, ulionyesha wema kwa nchi yako. Ulimrejeshea Yakobo baraka zake. 2 Ulisamehe uovu wa watu wako, na kufunika dhambi zao zote. 3 Uliweka kando ghadhabu yako yote na umegeuka na kuiacha hasira yako kali. 4 Ee Mungu Mwokozi wetu, uturejeshe tena, nawe uiondoe chuki yako juu yetu. 5 Je, utatukasirikia milele? Utaendeleza hasira yako kwa vizazi vyote? 6 Je, hutatuhuisha tena, ili watu wako wakufurahie? 7 Utuonyeshe upendo wako usiokoma, Ee Bwana, utupe wokovu wako. 8 Nitasikiliza lile atakalosema Mungu aliye Bwana; anaahidi amani kwa watu wake, watakatifu wake: lakini nao wasirudie upumbavu. 9 Hakika wokovu wake uko karibu na wale wamchao, ili utukufu wake udumu katika nchi yetu. 10 Upendo na uaminifu hukutana pamoja, haki na amani hubusiana. 11 Uaminifu huchipua kutoka nchi, haki hutazama chini kutoka mbinguni. 12 Naam, hakika Bwana atatoa kilicho chema, nayo nchi yetu itazaa mavuno yake. 13 Haki itatangulia mbele yake na kutengeneza njia kwa ajili ya hatua zake. Chapter 86Zaburi 86 1 Ee Bwana, sikia na unijibu, kwa maana mimi ni maskini na mhitaji. 2 Linda maisha yangu, kwa maana nimejiweka kwako, wewe ni Mungu wangu, mwokoe mtumishi wako anayekutumaini. 3 Ee Bwana, nihurumie mimi, kwa maana ninakuita mchana kutwa. 4 Mpe mtumishi wako furaha, kwa kuwa kwako wewe, Ee Bwana, ninainua nafsi yangu. 5 Ee Bwana, wewe ni mwema na mwenye kusamehe, umejaa upendo kwa wote wakuitao. 6 Ee Bwana, sikia maombi yangu, sikiliza kilio changu unihurumie. 7 Katika siku ya shida yangu nitakuita, kwa maana wewe utanijibu. 8 Ee Bwana, katikati ya miungu hakuna kama wewe, hakuna matendo ya kulinganishwa na yako. 9 Ee Bwana, mataifa yote uliyoyafanya yatakuja na kuabudu mbele zako; wataliletea utukufu jina lako. 10 Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu; wewe peke yako ndiwe Mungu. 11 Ee Bwana, nifundishe njia yako, nami nitakwenda katika kweli yako; nipe moyo usiositasita, ili niweze kulicha jina lako. 12 Ee Bwana wangu, nitakusifu kwa moyo wote; nitaliadhimisha jina lako milele. 13 Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu; umeniokoa kutoka kwenye vilindi vya kaburi. 14 Ee Mungu, wenye majivuno wananishambulia; kundi la watu wakatili linatafuta uhai wangu: watu wasiokuheshimu wewe. 15 Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu. 16 Nigeukie na unihurumie; mpe mtumishi wako nguvu zako, mwokoe mwana wa mtumishi wako wa kike. 17 Nipe ishara ya wema wako, ili adui zangu waione nao waaibishwe, kwa kuwa wewe, Ee Bwana, umenisaidia na kunifariji. Chapter 87Zaburi 87 1 Ameuweka msingi wake katika mlima mtakatifu; 2 Bwana anayapenda malango ya Sayuni kuliko makao yote ya Yakobo. 3 Mambo matukufu yanasemwa juu yako, ee mji wa Mungu: 4 “Nitaweka kumbukumbu ya Rahabu na Babeli miongoni mwa wale wanaonikubali mimi: Ufilisti pia na Tiro, pamoja na Kushi, nami nitasema, ‘Huyu alizaliwa Sayuni.’ ” 5 Kuhusu Sayuni itasemwa hivi, “Huyu na yule walizaliwa humo, naye Aliye Juu Sana mwenyewe atamwimarisha.” 6 Bwana ataandika katika orodha ya mataifa: “Huyu alizaliwa Sayuni.” 7 Watakapokuwa wanapiga vinanda wataimba, “Chemchemi zangu zote ziko kwako.” Chapter 88Zaburi 88 1 Ee Bwana, Mungu uniokoaye, nimelia mbele zako usiku na mchana. 2 Maombi yangu yafike mbele zako, utegee kilio changu sikio lako. 3 Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu, na maisha yangu yanakaribia kaburi. 4 Nimehesabiwa miongoni mwa wale waendao shimoni, niko kama mtu asiye na nguvu. 5 Nimetengwa pamoja na wafu, kama waliochinjwa walalao kaburini, ambao huwakumbuki tena, ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako. 6 Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana, katika vina vya giza nene. 7 Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu, umenigharikisha kwa mawimbi yako yote. 8 Umenitenga na rafiki zangu wa karibu na kunifanya chukizo kwao. Nimezuiliwa, wala siwezi kutoroka; 9 nuru ya macho yangu imefifia kwa ajili ya huzuni. Ee Bwana, ninakuita kila siku, ninakunyooshea wewe mikono yangu. 10 Je, wewe huwaonyesha wafu maajabu yako? Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu? 11 Je, upendo wako hutangazwa kaburini, uaminifu wako katika Uharibifu? 12 Je, maajabu yako hujulikana mahali pa giza, au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu? 13 Lakini ninakulilia wewe, Ee Bwana, unisaidie; asubuhi maombi yangu huja mbele zako. 14 Ee Bwana, kwa nini unanikataa na kunificha uso wako? 15 Tangu ujana wangu nimeteseka, nikakaribia kifo; nimepatwa na hofu zako, nami nimekata tamaa. 16 Ghadhabu yako imepita juu yangu; hofu zako zimeniangamiza. 17 Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko; zimenimeza kabisa. 18 Umeniondolea marafiki na wapendwa wangu; giza limekuwa ndilo rafiki yangu wa karibu kuliko wote. Chapter 89Zaburi 89 1 Nitaimba juu ya upendo mkuu wa Bwana milele; kwa kinywa changu nitajulisha uaminifu wako ujulikane kwa vizazi vyote. 2 Nitatangaza kuwa upendo wako unasimama imara milele na uaminifu wako umeuthibitisha mbinguni. 3 Ulisema, “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi, 4 ‘Nitaimarisha uzao wako milele na kudumisha ufalme wako kwa vizazi vyote.’ ” 5 Ee Bwana, mbingu zinayasifu maajabu yako, uaminifu wako pia katika kusanyiko la watakatifu. 6 Kwa kuwa ni nani katika mbingu anayeweza kulinganishwa na Bwana? Ni nani miongoni mwa viumbe vya mbinguni aliye kama Bwana? 7 Katika kusanyiko la watakatifu, Mungu huogopwa sana, anahofiwa kuliko wote wanaomzunguka. 8 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, ni nani aliye kama wewe? Ee Bwana, wewe ni mwenye nguvu, na uaminifu wako unakuzunguka. 9 Wewe unatawala bahari yenye msukosuko; wakati mawimbi yake yanapoinuka, wewe unayatuliza. 10 Wewe ulimponda Rahabu kama mmojawapo wa waliochinjwa; kwa mkono wako wenye nguvu, uliwatawanya adui zako. 11 Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako, uliuwekea ulimwengu msingi pamoja na vyote vilivyomo. 12 Uliumba kaskazini na kusini; Tabori na Hermoni wanaliimbia jina lako kwa furaha. 13 Mkono wako umejaa uwezo; mkono wako una nguvu, mkono wako wa kuume umetukuzwa. 14 Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako cha enzi; upendo na uaminifu vinakutangulia. 15 Heri ni wale ambao wamejifunza kukusifu kwa shangwe, wanaotembea katika mwanga wa uwepo wako, Ee Bwana. 16 Wanashangilia katika jina lako mchana kutwa, wanafurahi katika haki yako. 17 Kwa kuwa wewe ni utukufu na nguvu yao, kwa wema wako unatukuza pembe yetu. 18 Naam, ngao yetu ni mali ya Bwana, na mfalme wetu mali ya Aliye Mtakatifu wa Israeli. 19 Ulizungumza wakati fulani katika maono, kwa watu wako waaminifu, ukasema: “Nimeweka nguvu kwa shujaa, nimemwinua kijana miongoni mwa watu. 20 Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, na nimemtia mafuta yangu matakatifu. 21 Kitanga changu kitamtegemeza, hakika mkono wangu utamtia nguvu. 22 Hakuna adui atakayemtoza ushuru, hakuna mtu mwovu atakayemwonea. 23 Nitawaponda adui zake mbele zake na kuwaangamiza watesi wake. 24 Upendo wangu mkamilifu utakuwa pamoja naye, kwa Jina langu pembe yake itatukuzwa. 25 Nitauweka mkono wake juu ya bahari, mkono wake wa kuume juu ya mito. 26 Naye ataniita kwa sauti, ‘Wewe ni Baba yangu, Mungu wangu, Mwamba na Mwokozi wangu.’ 27 Nitamteua pia awe mzaliwa wangu wa kwanza, aliyetukuka kuliko wafalme wote wa dunia. 28 Nitadumisha upendo wangu kwake milele, na agano langu naye litakuwa imara. 29 Nitaudumisha uzao wake milele, kiti chake cha enzi kama mbingu zinavyodumu. 30 “Kama wanae wataacha amri yangu na wasifuate sheria zangu, 31 kama wakihalifu maagizo yangu na kutoshika amri zangu, 32 nitaadhibu dhambi yao kwa fimbo, uovu wao kwa kuwapiga, 33 lakini sitauondoa upendo wangu kwake, wala sitausaliti uaminifu wangu kamwe. 34 Mimi sitavunja agano langu wala sitabadili lile ambalo midomo yangu imelitamka. 35 Mara moja na kwa milele, nimeapa kwa utakatifu wangu, nami sitamdanganya Daudi: 36 kwamba uzao wake utaendelea milele, na kiti chake cha enzi kitadumu mbele zangu kama jua; 37 kitaimarishwa milele kama mwezi, shahidi mwaminifu angani.” 38 Lakini wewe umemkataa, umemdharau, umemkasirikia sana mpakwa mafuta wako. 39 Umelikana agano lako na mtumishi wako, na umeinajisi taji yake mavumbini. 40 Umebomoa kuta zake zote, na ngome zake zote umezifanya kuwa magofu. 41 Wote wapitao karibu wamemnyangʼanya mali zake; amekuwa dharau kwa jirani zake. 42 Umeutukuza mkono wa kuume wa adui zake, umewafanya watesi wake wote washangilie. 43 Umegeuza makali ya upanga wake, na hukumpa msaada katika vita. 44 Umeikomesha fahari yake, na kukiangusha kiti chake cha enzi. 45 Umezifupisha siku za ujana wake, umemfunika kwa vazi la aibu. 46 Hata lini, Ee Bwana? Utajificha milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto hata lini? 47 Kumbuka jinsi maisha yangu yanavyopita haraka. Ni kwa ubatili kiasi gani umemuumba mwanadamu! 48 Ni mtu gani awezaye kuishi na asione kifo, au kujiokoa mwenyewe kutoka nguvu za kaburi? 49 Ee Bwana, uko wapi upendo wako mkuu wa mwanzoni, ambao katika uaminifu wako ulimwapia Daudi? 50 Bwana kumbuka jinsi mtumishi wako amesimangwa, jinsi ninavyovumilia moyoni mwangu dhihaka za mataifa yote, 51 dhihaka ambazo kwazo adui zako wamenisimanga, Ee Bwana, ambazo kwazo wamesimanga kila hatua ya mpakwa mafuta wako. 52 Msifuni Bwana milele! Amen na Amen. Chapter 90(Zaburi 90–106) Zaburi 90 1 Bwana, wewe umekuwa makao yetu katika vizazi vyote. 2 Kabla ya kuzaliwa milima au hujaumba dunia na ulimwengu, wewe ni Mungu tangu milele hata milele. 3 Huwarudisha watu mavumbini, ukisema, “Rudini mavumbini, enyi wanadamu.” 4 Kwa maana kwako miaka elfu ni kama siku moja iliyokwisha pita, au kama kesha la usiku. 5 Unawatowesha wanadamu katika usingizi wa kifo, nao ni kama majani machanga ya asubuhi: 6 ingawa asubuhi yanachipua, ifikapo jioni huwa yamenyauka na kukauka. 7 Tumeangamizwa kwa hasira yako na tumetishwa kwa ghadhabu yako. 8 Umeyaweka maovu yetu mbele yako, dhambi zetu za siri katika nuru ya uwepo wako. 9 Tumeishi siku zetu zote chini ya ghadhabu yako, tunamaliza miaka yetu kwa kuomboleza. 10 Siku zetu za kuishi ni miaka sabini, au miaka themanini ikiwa tuna nguvu, lakini yote ni ya shida na taabu, nazo zapita haraka, nasi twatoweka. 11 Ni nani ajuaye nguvu za hasira yako? Kwa maana ghadhabu yako ni kubwa kama hofu tunayopaswa kuwa nayo kwako. 12 Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri, ili tujipatie moyo wa hekima. 13 Ee Bwana, uwe na huruma! Utakawia hata lini? Wahurumie watumishi wako. 14 Tushibishe asubuhi kwa upendo wako usiokoma, ili tuweze kuimba kwa shangwe na kufurahi siku zetu zote. 15 Utufurahishe kulingana na siku ulizotuadhibu, kulingana na miaka tuliyotaabika. 16 Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, utukufu wako kwa watoto wao. 17 Wema wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu; uzithibitishe kazi za mikono yetu: naam, uzithibitishe kazi za mikono yetu. Chapter 91Zaburi 91 1 Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana, atadumu katika uvuli wake Mwenyezi. 2 Nitasema kumhusu Bwana, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu, ambaye ninamtumaini.” 3 Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji, na maradhi ya kuambukiza ya kuua. 4 Atakufunika kwa manyoya yake, chini ya mbawa zake utapata kimbilio, uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako. 5 Hutaogopa vitisho vya usiku, wala mshale urukao mchana, 6 wala maradhi ya kuambukiza yanayonyemelea gizani, wala tauni iharibuyo adhuhuri. 7 Ijapo watu elfu wataangukia kando yako, kumi elfu mkono wako wa kuume, lakini haitakukaribia wewe. 8 Utatazama tu kwa macho yako na kuona adhabu ya waovu. 9 Kama ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako: naam, Bwana ambaye ni kimbilio langu, 10 basi hakuna madhara yatakayokupata wewe, hakuna maafa yataikaribia hema yako. 11 Kwa kuwa atawaagiza malaika zake kwa ajili yako, wakulinde katika njia zako zote. 12 Mikononi mwao watakuinua, ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe. 13 Utawakanyaga simba na nyoka wakali, simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu. 14 Bwana asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa; nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu. 15 Ataniita, nami nitamjibu; nitakuwa pamoja naye katika taabu, nitamwokoa na kumheshimu. 16 Kwa siku nyingi nitamshibisha na kumwonyesha wokovu wangu.” Chapter 92Zaburi 92 1 Ni vyema kumshukuru Bwana na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana, 2 kuutangaza upendo wako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku, 3 kwa zeze yenye nyuzi kumi na kwa sauti ya kinubi. 4 Ee Bwana, kwa kuwa matendo yako yamenifurahisha, nitaziimba kwa shangwe kazi za mikono yako. 5 Ee Bwana, tazama jinsi yalivyo makuu matendo yako, tazama jinsi yalivyo ya kina mawazo yako! 6 Mjinga hafahamu, mpumbavu haelewi, 7 ingawa waovu huchipua kama majani na wote watendao mabaya wanastawi, wataangamizwa milele. 8 Bali wewe, Ee Bwana, utatukuzwa milele. 9 Ee Bwana, hakika adui zako, hakika adui zako wataangamia. Wote watendao mabaya watatawanyika. 10 Umeitukuza pembe yangu kama ile ya nyati dume, mafuta mazuri yamemiminwa juu yangu. 11 Macho yangu yamewaona adui zangu wakishindwa, masikio yangu yamesikia maangamizi ya adui zangu waovu. 12 Wenye haki watastawi kama mtende, watakuwa kama mwerezi wa Lebanoni, 13 waliopandwa katika nyumba ya Bwana, watastawi katika nyua za Mungu wetu. 14 Wakati wa uzee watakuwa bado wanazaa matunda, watakuwa wabichi tena wamejaa nguvu, 15 wakitangaza, “Bwana ni mkamilifu; yeye ni Mwamba wangu, na ndani yake hamna uovu.” Chapter 93Zaburi 93 1 Bwana anatawala, amejivika utukufu; Bwana amejivika utukufu tena amejivika nguvu. Dunia imewekwa imara, haitaondoshwa. 2 Kiti chako cha enzi kimekuwa thabiti tangu zamani; wewe umekuwako tangu milele. 3 Bahari zimeinua, Ee Bwana, bahari zimeinua sauti zake; bahari zimeinua sauti za mawimbi yake. 4 Yeye ni mkuu kuliko ngurumo ya maji makuu, ni mkuu kuliko mawimbi ya bahari: Bwana aishiye juu sana ni mkuu. 5 Ee Bwana, sheria zako ni imara; utakatifu umepamba nyumba yako pasipo mwisho. Chapter 94Zaburi 94 1 Ee Bwana, ulipizaye kisasi, Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa. 2 Ee Mhukumu wa dunia, inuka, uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili. 3 Hata lini, waovu, Ee Bwana, hata lini waovu watashangilia? 4 Wanamimina maneno ya kiburi, watenda mabaya wote wamejaa majivuno. 5 Ee Bwana, wanawaponda watu wako, wanawaonea urithi wako. 6 Wanamchinja mjane na mgeni, na kuwaua yatima. 7 Nao husema, “Bwana haoni, Mungu wa Yakobo hafahamu.” 8 Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu; enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima? 9 Je, aliyeweka sikio asisikie? Aliyeumba jicho asione? 10 Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu? Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa? 11 Bwana anajua mawazo ya mwanadamu; anajua kwamba ni ubatili. 12 Ee Bwana, heri mtu anayeadhibishwa na wewe, mtu unayemfundisha kwa sheria yako, 13 unampa utulivu siku za shida, mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa kwa ajili ya mwovu. 14 Kwa kuwa Bwana hatawakataa watu wake, hatauacha urithi wake. 15 Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki, wote walio na mioyo minyofu wataifuata. 16 Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu? Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu? 17 Kama Bwana asingelinisaidia upesi, ningelikuwa ninaishi katika ukimya wa kifo. 18 Niliposema, “Mguu wangu unateleza,” Ee Bwana, upendo wako ulinishikilia. 19 Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu, faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu. 20 Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe, ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake? 21 Huungana kuwashambulia wenye haki, kuwahukumu kufa wasio na hatia. 22 Lakini Bwana amekuwa ngome yangu, na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia. 23 Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao; Bwana Mungu wetu atawaangamiza. Chapter 95Zaburi 95 1 Njooni, tumwimbie Bwana kwa furaha; tumfanyie kelele za shangwe Mwamba wa wokovu wetu. 2 Tuje mbele zake kwa shukrani, tumtukuze kwa vinanda na nyimbo. 3 Kwa kuwa Bwana ni Mungu mkuu, mfalme mkuu juu ya miungu yote. 4 Mkononi mwake mna vilindi vya dunia, na vilele vya milima ni mali yake. 5 Bahari ni yake, kwani ndiye aliifanya, na mikono yake iliumba nchi kavu. 6 Njooni, tusujudu, tumwabudu, tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu, 7 kwa maana yeye ndiye Mungu wetu, na sisi ni watu wa malisho yake, kondoo chini ya utunzaji wake. Kama mkiisikia sauti yake leo, 8 msiifanye mioyo yenu migumu kama mlivyofanya kule Meriba, kama mlivyofanya siku ile kule Masa jangwani, 9 ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima, ingawa walikuwa wameyaona matendo yangu. 10 Kwa miaka arobaini nilikasirikia kizazi kile, nikasema, “Hawa ni taifa ambalo mioyo yao imepotoka, nao hawajazijua njia zangu.” 11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.” Chapter 96Zaburi 96 1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya; mwimbieni Bwana dunia yote. 2 Mwimbieni Bwana, lisifuni jina lake; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku. 3 Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote. 4 Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. 5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini Bwana aliziumba mbingu. 6 Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake. 7 Mpeni Bwana, enyi jamaa za mataifa, mpeni Bwana utukufu na nguvu. 8 Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; leteni sadaka na mje katika nyua zake. 9 Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake; dunia yote na itetemeke mbele zake. 10 Katikati ya mataifa semeni, “Bwana anatawala.” Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa; atawahukumu watu kwa uadilifu. 11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; bahari na ivume, na vyote vilivyomo ndani yake; 12 mashamba na yashangilie, pamoja na vyote vilivyomo ndani yake. Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha; 13 itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja, anakuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa katika kweli yake. Chapter 97Zaburi 97 1 Bwana anatawala, nchi na ifurahi, visiwa vyote vishangilie. 2 Mawingu na giza nene vinamzunguka, haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake cha enzi. 3 Moto hutangulia mbele zake na huteketeza adui zake pande zote. 4 Umeme wake wa radi humulika dunia, nchi huona na kutetemeka. 5 Milima huyeyuka kama nta mbele za Bwana, mbele za Bwana wa dunia yote. 6 Mbingu zinatangaza haki yake, na mataifa yote huona utukufu wake. 7 Wote waabuduo sanamu waaibishwa, wale wajisifiao sanamu: mwabuduni yeye, enyi miungu yote! 8 Sayuni husikia na kushangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako, Ee Bwana. 9 Kwa kuwa wewe, Ee Bwana, ndiwe Uliye Juu Sana kuliko dunia yote; umetukuka sana juu ya miungu yote. 10 Wale wanaompenda Bwana na wauchukie uovu, kwa maana yeye hulinda maisha ya waaminifu wake na kuwaokoa kutoka mkononi mwa mwovu. 11 Nuru huangaza wenye haki na furaha kwa watu wanyofu wa moyo. 12 Furahini katika Bwana, ninyi mlio wenye haki, lisifuni jina lake takatifu. Chapter 98Zaburi 98 1 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu umemfanyia wokovu. 2 Bwana ameufanya wokovu wake ujulikane na amedhihirisha haki yake kwa mataifa. 3 Ameukumbuka upendo wake na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli; miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu. 4 Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote, ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda; 5 mwimbieni Bwana kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za kuimba, 6 kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume: shangilieni kwa furaha mbele za Bwana, aliye Mfalme. 7 Bahari na ivume na kila kiliomo ndani yake, dunia na wote wakaao ndani yake. 8 Mito na ipige makofi, milima na iimbe pamoja kwa furaha, 9 vyote na viimbe mbele za Bwana, kwa maana yuaja kuhukumu dunia. Atahukumu dunia kwa haki na mataifa kwa haki. Chapter 99Zaburi 99 1 Bwana anatawala, mataifa na yatetemeke; anakalia kiti cha enzi katikati ya makerubi, dunia na itikisike. 2 Bwana ni mkuu katika Sayuni; ametukuzwa juu ya mataifa yote. 3 Wanalisifu jina lako ambalo ni kuu na la kuogopwa: yeye ni mtakatifu! 4 Mfalme ni mwenye nguvu na hupenda haki, wewe umethibitisha adili; katika Yakobo umefanya yaliyo haki na sawa. 5 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake; yeye ni mtakatifu. 6 Mose na Aroni walikuwa miongoni mwa makuhani wake, Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake; walimwita Bwana, naye aliwajibu. 7 Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu; walizishika sheria zake na amri alizowapa. 8 Ee Bwana, wetu, ndiwe uliyewajibu, kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe, ingawa uliadhibu matendo yao mabaya. 9 Mtukuzeni Bwana Mungu wetu, mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu, kwa maana Bwana Mungu wetu ni mtakatifu. Chapter 100Zaburi 100 1 Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote. 2 Mwabuduni Bwana kwa furaha; njooni mbele zake kwa nyimbo za shangwe. 3 Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu. Yeye ndiye alituumba, sisi tu mali yake; sisi tu watu wake, kondoo wa malisho yake. 4 Ingieni malangoni mwake kwa shukrani na katika nyua zake kwa kusifu, mshukuruni yeye na kulisifu jina lake. 5 Kwa maana Bwana ni mwema na upendo wake wadumu milele; uaminifu wake unadumu kwa vizazi vyote. Chapter 101Zaburi 101 1 Nitaimba juu ya upendo wako na haki yako; kwako wewe, Ee Bwana, nitaimba sifa. 2 Nitazingatia kuishi maisha yasiyo na lawama: utakuja kwangu lini? Nitatembea nyumbani mwangu kwa moyo usio na lawama. 3 Sitaweka mbele ya macho yangu kitu kiovu. Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani; hawatashikamana nami. 4 Moyo wa ukaidi utakuwa mbali nami; nitajitenga na kila ubaya. 5 Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri, huyo nitamnyamazisha; mwenye macho ya dharau na moyo wa kiburi huyo sitamvumilia. 6 Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, ili waweze kuishi pamoja nami; yeye ambaye moyo wake hauna lawama atanitumikia. 7 Mdanganyifu hatakaa nyumbani mwangu, yeye asemaye kwa uongo hatasimama mbele yangu. 8 Kila asubuhi nitawanyamazisha waovu wote katika nchi; nitamkatilia mbali kila mtenda mabaya kutoka mji wa Bwana. Chapter 102Zaburi 102 1 Ee Bwana, usikie maombi yangu, kilio changu cha kuomba msaada kikufikie. 2 Usinifiche uso wako ninapokuwa katika shida. Unitegee sikio lako, ninapoita, unijibu kwa upesi. 3 Kwa kuwa siku zangu zinatoweka kama moshi, mifupa yangu inaungua kama kaa la moto. 4 Moyo wangu umefifia na kunyauka kama jani, ninasahau kula chakula changu. 5 Kwa sababu ya kusononeka kwangu kwa uchungu, nimebakia ngozi na mifupa. 6 Nimekuwa kama bundi wa jangwani, kama bundi kwenye magofu. 7 Nilalapo sipati usingizi, nimekuwa kama ndege mpweke kwenye paa la nyumba. 8 Mchana kutwa adui zangu hunidhihaki, wale wanaonizunguka hutumia jina langu kama laana. 9 Ninakula majivu kama chakula changu na nimechanganya kinywaji changu na machozi 10 kwa sababu ya ghadhabu yako kuu, kwa maana umeniinua na kunitupa kando. 11 Siku zangu ni kama kivuli cha jioni, ninanyauka kama jani. 12 Lakini wewe, Ee Bwana, umeketi katika kiti chako cha enzi milele, sifa zako za ukuu zaendelea vizazi vyote. 13 Utainuka na kuihurumia Sayuni, kwa maana ni wakati wa kumwonyesha wema; wakati uliokubalika umewadia. 14 Kwa maana mawe yake ni ya thamani kwa watumishi wako, vumbi lake lenyewe hulionea huruma. 15 Mataifa wataogopa jina la Bwana, wafalme wote wa dunia watauheshimu utukufu wako. 16 Kwa maana Bwana ataijenga tena Sayuni na kutokea katika utukufu wake. 17 Ataitikia maombi ya mtu mkiwa, wala hatadharau hoja yao. 18 Hili na liandikwe kwa ajili ya kizazi kijacho, ili taifa litakaloumbwa baadaye waweze kumsifu Bwana: 19 “Bwana alitazama chini kutoka patakatifu pake palipo juu, kutoka mbinguni alitazama dunia, 20 kusikiliza vilio vya uchungu vya wafungwa na kuwaweka huru wale waliohukumiwa kufa.” 21 Kwa hiyo jina la Bwana latangazwa huko Sayuni na sifa zake katika Yerusalemu, 22 wakati mataifa na falme zitakapokusanyika ili kumwabudu Bwana. 23 Katika kuishi kwangu alivunja nguvu zangu, akafupisha siku zangu. 24 Ndipo niliposema: “Ee Mungu wangu, usinichukue katikati ya siku zangu; miaka yako inaendelea vizazi vyote. 25 Hapo mwanzo uliweka misingi ya dunia, nazo mbingu ni kazi ya mikono yako. 26 Hizi zitatoweka, lakini wewe utadumu, zote zitachakaa kama vazi. Utazibadilisha kama nguo nazo zitaondoshwa. 27 Lakini wewe, U yeye yule, nayo miaka yako haikomi kamwe. 28 Watoto wa watumishi wako wataishi mbele zako; wazao wao wataimarishwa mbele zako.” Chapter 103Zaburi 103 1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Vyote vilivyomo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu. 2 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usisahau wema wake wote, 3 akusamehe dhambi zako zote, akuponya magonjwa yako yote, 4 aukomboa uhai wako na kaburi, akuvika taji ya upendo na huruma, 5 atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema, ili ujana wako uhuishwe kama wa tai. 6 Bwana hutenda haki, naye huwapa hukumu ya haki wote wanaoonewa. 7 Alijulisha Mose njia zake, na wana wa Israeli matendo yake. 8 Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema; si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo. 9 Yeye hatalaumu siku zote, wala haweki hasira yake milele, 10 yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu. 11 Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha; 12 kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi. 13 Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha; 14 kwa kuwa anajua tulivyoumbwa, anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi. 15 Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani, anachanua kama ua la shambani; 16 upepo huvuma juu yake nalo hutoweka, mahali pake hapalikumbuki tena. 17 Lakini kutoka milele hata milele upendo wa Bwana uko kwa wale wamchao, nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao: 18 kwa wale walishikao agano lake na kukumbuka kuyatii mausia yake. 19 Bwana ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni, ufalme wake unatawala juu ya vyote. 20 Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake, ninyi mnaotii neno lake. 21 Mhimidini Bwana, ninyi jeshi lake lote la mbinguni, ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake. 22 Mhimidini Bwana, kazi zake zote kila mahali katika milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Chapter 104Zaburi 104 1 Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Ee Bwana Mungu wangu, wewe ni mkuu sana, umejivika utukufu na enzi. 2 Amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi, amezitandaza mbingu kama hema 3 na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji. Huyafanya mawingu kuwa gari lake, na hupanda kwenye mbawa za upepo. 4 Huzifanya pepo kuwa wajumbe wake, miali ya moto watumishi wake. 5 Ameiweka dunia kwenye misingi yake, haiwezi kamwe kuondoshwa. 6 Uliifunika kwa kilindi kama kwa vazi, maji yalisimama juu ya milima. 7 Lakini kwa kukemea kwako maji yalikimbia, kwa sauti ya radi yako yakatoroka, 8 yakapanda milima, yakateremka mabondeni, hadi mahali pale ulipoyakusudia. 9 Uliyawekea mpaka ambao hayawezi kuuvuka, kamwe hayataifunika dunia tena. 10 Huzifanya chemchemi zimwage maji mabondeni, hutiririka kati ya milima. 11 Huwapa maji wanyama wote wa kondeni, punda-mwitu huzima kiu yao. 12 Ndege wa angani hufanya viota kando ya maji, huimba katikati ya matawi. 13 Huinyeshea milima kutoka orofa zake, dunia inatoshelezwa kwa matunda ya kazi yake. 14 Huyafanya majani ya mifugo yaote, na mimea kwa watu kulima, wajipatie chakula kutoka ardhini: 15 divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu, mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake, na mkate wa kutia mwili nguvu. 16 Miti ya Bwana inanyeshewa vizuri, mierezi ya Lebanoni aliyoipanda. 17 Humo ndege hufanya viota vyao, korongo ana nyumba yake kwenye msunobari. 18 Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu, majabali ni kimbilio la pelele. 19 Mwezi hugawanya majira, na jua hutambua wakati wake wa kutua. 20 Unaleta giza, kunakuwa usiku, wanyama wote wa mwituni huzurura. 21 Simba hunguruma kwa mawindo yao, na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu. 22 Jua huchomoza, nao huondoka, hurudi na kulala katika mapango yao. 23 Kisha mwanadamu huenda kazini mwake, katika kazi yake mpaka jioni. 24 Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi! Kwa hekima ulizifanya zote, dunia imejaa viumbe vyako. 25 Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele, imejaa viumbe visivyo na idadi, vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo. 26 Huko meli huenda na kurudi, pia Lewiathani, uliyemuumba acheze ndani yake. 27 Hawa wote wanakutazamia wewe, uwape chakula chao kwa wakati wake. 28 Wakati unapowapa, wanakikusanya, unapofumbua mkono wako, wao wanashibishwa mema. 29 Unapoficha uso wako, wanapata hofu, unapoondoa pumzi yao, wanakufa na kurudi mavumbini. 30 Unapopeleka Roho wako, wanaumbwa, nawe huufanya upya uso wa dunia. 31 Utukufu wa Bwana na udumu milele, Bwana na azifurahie kazi zake: 32 yeye aitazamaye dunia, nayo ikatetemeka, aigusaye milima, nayo ikatoa moshi. 33 Nitamwimbia Bwana maisha yangu yote; nitaimba sifa kwa Mungu wangu muda wote ninaoishi. 34 Kutafakari kwangu na kumpendeze yeye, ninapofurahi katika Bwana. 35 Lakini wenye dhambi na watoweke katika dunia na waovu wasiwepo tena. Ee nafsi yangu, msifu Bwana. Msifuni Bwana. Chapter 105Zaburi 105 1 Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake, wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda. 2 Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa, waambieni matendo yake yote ya ajabu. 3 Lishangilieni jina lake takatifu, mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi. 4 Mtafuteni Bwana na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote. 5 Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka, 6 enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake. 7 Yeye ndiye Bwana Mungu wetu, hukumu zake zimo duniani pote. 8 Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu, 9 agano alilolifanya na Abrahamu, kiapo alichomwapia Isaki. 10 Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele: 11 “Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.” 12 Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake, 13 walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine. 14 Hakuruhusu mtu yeyote awaonee; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema: 15 “Msiwaguse niliowatia mafuta; msiwadhuru manabii wangu.” 16 Akaiita njaa juu ya nchi na kuharibu chakula chao chote, 17 naye akatuma mtu mbele yao, Yosefu, aliyeuzwa kama mtumwa. 18 Walichubua miguu yake kwa minyororo, shingo yake ilifungwa kwa chuma, 19 hadi yale aliyotangulia kusema yalipotimia, hadi neno la Bwana lilipomthibitisha. 20 Mfalme alituma watu wakamfungua, mtawala wa watu alimwachia huru. 21 Alimfanya mkuu wa nyumba yake, mtawala juu ya vyote alivyokuwa navyo, 22 kuwaelekeza wakuu wa mfalme apendavyo na kuwafundisha wazee wake hekima. 23 Kisha Israeli akaingia Misri, Yakobo akaishi kama mgeni katika nchi ya Hamu. 24 Bwana aliwafanya watu wake kuzaana sana, akawafanya kuwa wengi sana kuliko adui zao, 25 ndiye aliigeuza mioyo yao iwachukie watu wake, wakatenda hila dhidi ya watumishi wake. 26 Akamtuma Mose mtumishi wake, pamoja na Aroni, aliyemchagua. 27 Walifanya ishara zake za ajabu miongoni mwao, miujiza yake katika nchi ya Hamu. 28 Alituma giza na nchi ikajaa giza, kwani si walikuwa wameyaasi maneno yake? 29 Aligeuza maji yao kuwa damu, ikasababisha samaki wao kufa. 30 Nchi yao ilijaa vyura tele, ambao waliingia hadi kwenye vyumba vya kulala vya watawala wao. 31 Alisema, yakaja makundi ya mainzi, na viroboto katika nchi yao yote. 32 Alibadilisha mvua yao ikawa mvua ya mawe, yenye umeme wa radi nchini yao yote, 33 akaharibu mizabibu yao na miti ya tini, na akaangamiza miti ya nchi yao. 34 Alisema, nzige wakaja, tunutu wasio na idadi, 35 wakala kila jani katika nchi yao, wakala mazao ya ardhi yao. 36 Kisha akawaua wazaliwa wote wa kwanza katika nchi yao, matunda ya kwanza ya ujana wao wote. 37 Akawatoa Israeli katika nchi wakiwa na fedha na dhahabu nyingi, wala hakuna hata mmoja kutoka kabila zao aliyejikwaa. 38 Misri ilifurahi walipoondoka, kwa sababu hofu ya Israeli ilikuwa imewaangukia. 39 Alitandaza wingu kama kifuniko, na moto kuwamulikia usiku. 40 Waliomba, naye akawaletea kware, akawashibisha kwa mkate wa mbinguni. 41 Alipasua mwamba, maji yakabubujika, yakatiririka jangwani kama mto. 42 Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu, aliyompa Abrahamu mtumishi wake. 43 Aliwatoa watu wake kwa furaha, wateule wake kwa kelele za shangwe, 44 akawapa nchi za mataifa, wakawa warithi wa mali wengine walikuwa wameitaabikia: 45 alifanya haya ili wayashike mausia yake na kuzitii sheria zake. Msifuni Bwana. Chapter 106Zaburi 106 1 Msifuni Bwana. Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele. 2 Ni nani awezaye kusimulia matendo makuu ya Bwana au kutangaza kikamilifu sifa zake? 3 Heri wale wanaodumisha haki, ambao daima wanafanya yaliyo mema. 4 Ee Bwana, unikumbuke unapowatendea mema watu wako, uwe msaada wangu unapowaokoa, 5 ili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako, niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako, na kuungana na urithi wako katika kukusifu. 6 Tumetenda dhambi, kama vile baba zetu walivyotenda, tumekosa na tumetenda uovu. 7 Wakati baba zetu walipokuwa Misri, hawakuzingatia maajabu yako, wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako, bali waliasi kando ya bahari, Bahari ya Shamu. 8 Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake, ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu. 9 Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka, akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani. 10 Aliwaokoa mikononi mwa adui; kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa. 11 Maji yaliwafunika adui zao, hakunusurika hata mmoja. 12 Ndipo walipoamini ahadi zake, nao wakaimba sifa zake. 13 Lakini mara walisahau aliyowatendea, wala hawakungojea shauri lake. 14 Jangwani walitawaliwa na tamaa zao, walimjaribu Mungu nyikani. 15 Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba, lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha. 16 Kambini walimwonea wivu Mose, na pia Aroni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa Bwana. 17 Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani, ikawazika Abiramu na kundi lake. 18 Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao, mwali wa moto uliwateketeza waovu. 19 Huko Horebu walitengeneza ndama, na kuabudu sanamu ya kusubu kwa chuma. 20 Waliubadilisha Utukufu wao kwa sanamu ya fahali, ambaye hula majani. 21 Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyekuwa ametenda mambo makuu huko Misri, 22 miujiza katika nchi ya Hamu na mambo ya kutisha huko Bahari ya Shamu. 23 Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza: kama Mose mteule wake, asingesimama kati yao na Mungu kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza. 24 Kisha waliidharau ile nchi nzuri, hawakuiamini ahadi yake. 25 Walinungʼunika ndani ya mahema yao, wala hawakumtii Bwana. 26 Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba atawafanya waanguke jangwani, 27 kuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa, na kuwatawanya katika nchi zote. 28 Walijifunga nira na Baali wa Peori, wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai. 29 Waliichochea hasira ya Bwana, wakamkasirisha kwa matendo yao maovu, nayo tauni ikazuka katikati yao. 30 Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati, nayo tauni ikazuiliwa. 31 Hili likahesabiwa kwake haki, kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo. 32 Kwenye maji ya Meriba, walimkasirisha Bwana, janga likampata Mose kwa sababu yao; 33 kwa maana walimwasi Roho wa Mungu, na maneno yasiyofaa yakatoka midomoni kwa Mose. 34 Hawakuyaangamiza yale mataifa kama Bwana alivyowaagiza, 35 bali walijichanganya na mataifa na wakazikubali desturi zao. 36 Waliabudu sanamu zao, zikawa mtego kwao. 37 Wakawatoa wana wao na binti zao dhabihu kwa mashetani. 38 Walimwaga damu isiyo na hatia, damu za wana wao na binti zao, ambao waliwatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani, nayo nchi ikanajisika kwa damu zao. 39 Wakajinajisi wenyewe kwa yale waliyotenda; kwa matendo yao wenyewe wakajifanyia ukahaba. 40 Kwa hiyo Bwana akawakasirikia watu wake na akauchukia sana urithi wake. 41 Akawakabidhi kwa mataifa na adui zao wakawatawala. 42 Adui zao wakawaonea na kuwatia chini ya mamlaka yao. 43 Mara nyingi aliwaokoa lakini walikuwa wamezama kwenye uasi, nao wakajiharibu katika dhambi zao. 44 Lakini akaangalia mateso yao wakati aliposikia kilio chao; 45 kwa ajili yao akakumbuka agano lake, na kutokana na upendo wake mkuu akapooza hasira yake. 46 Akawafanya wahurumiwe na wote waliowashikilia mateka. 47 Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe. Tukusanye tena kutoka kwa mataifa, ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu, na kushangilia katika sifa zako. 48 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele. Watu wote na waseme, “Amen!” Msifuni Bwana. Chapter 107(Zaburi 107–150) Zaburi 107 1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa yeye ni mwema, upendo wake wadumu milele. 2 Waliokombolewa wa Bwana na waseme hivi, wale aliowaokoa kutoka mkono wa adui, 3 wale aliowakusanya kutoka nchi mbalimbali, kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. 4 Baadhi yao walitangatanga jangwani, hawakuona njia ya kuwafikisha mji ambao wangeweza kuishi. 5 Walikuwa na njaa na kiu, nafsi zao zikadhoofika. 6 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. 7 Akawaongoza kwa njia iliyo sawa hadi mji ambao wangeweza kuishi. 8 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, 9 kwa maana yeye humtosheleza mwenye kiu, na kumshibisha mwenye njaa kwa vitu vyema. 10 Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu, wafungwa wakiteseka katika minyororo, 11 kwa sababu walikuwa wameasi dhidi ya maneno ya Mungu na kudharau shauri la Aliye Juu Sana. 12 Aliwatumikisha kwa kazi ngumu; walijikwaa na hapakuwepo yeyote wa kuwasaidia. 13 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. 14 Akawatoa katika giza na huzuni kuu na akavunja minyororo yao. 15 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, 16 kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma. 17 Wengine wakawa wapumbavu kutokana na uasi wao, wakapata mateso kwa sababu ya uovu wao. 18 Wakachukia kabisa vyakula vyote, wakakaribia malango ya mauti. 19 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. 20 Akalituma neno lake na kuwaponya, akawaokoa kutoka maangamizo yao. 21 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu. 22 Na watoe dhabihu za kushukuru, na wasimulie matendo yake kwa nyimbo za furaha. 23 Wengine walisafiri baharini kwa meli, walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu. 24 Waliziona kazi za Bwana, matendo yake ya ajabu kilindini. 25 Kwa maana alisema na kuamsha tufani iliyoinua mawimbi juu. 26 Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini, katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka. 27 Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi, ujanja wao ukafikia ukomo. 28 Ndipo walipomlilia Bwana katika shida yao, naye akawatoa kwenye taabu yao. 29 Akatuliza dhoruba kwa mnongʼono, mawimbi ya bahari yakatulia. 30 Walifurahi ilipokuwa shwari, naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani. 31 Basi na wamshukuru Bwana kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu. 32 Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu, na wamsifu katika baraza la wazee. 33 Yeye aligeuza mito kuwa jangwa, chemchemi za maji zitiririkazo kuwa ardhi yenye kiu, 34 nchi izaayo ikawa ya chumvi isiyofaa, kwa sababu ya uovu wa wale walioishi humo. 35 Aligeuza jangwa likawa madimbwi ya maji, nayo ardhi kame kuwa chemchemi za maji zitiririkazo; 36 aliwaleta wenye njaa wakaishi humo, nao wakajenga mji wangeweza kuishi. 37 Walilima mashamba na kupanda mizabibu, nayo ikazaa matunda mengi, 38 Mungu aliwabariki, hesabu yao ikaongezeka sana, wala hakuruhusu mifugo yao kupungua. 39 Kisha hesabu yao ilipungua, na walinyenyekeshwa kwa kuonewa, maafa na huzuni. 40 Yeye ambaye huwamwagia dharau wakuu, aliwafanya watangetange nyikani isiyo na njia. 41 Lakini yeye aliwainua wahitaji katika taabu zao, na kuongeza jamaa zao kama makundi ya kondoo. 42 Wanyofu wataona na kufurahi, lakini waovu wote watafunga vinywa vyao. 43 Yeyote aliye na hekima, ayasikie mambo haya, na atafakari upendo mkuu wa Bwana. Chapter 108Zaburi 108 1 Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti; nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote. 2 Amka, kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko. 3 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa; nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu. 4 Kwa maana upendo wako ni mkuu, ni juu kuliko mbingu; uaminifu wako unazifikia anga. 5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, utukufu wako na uenee duniani kote. 6 Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume, ili wale uwapendao wapate kuokolewa. 7 Mungu amenena kutoka patakatifu pake: “Nitaigawa Shekemu kwa ushindi na kulipima Bonde la Sukothi. 8 Gileadi ni yangu, Manase ni yangu, Efraimu ni kofia yangu ya chuma, nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala. 9 Moabu ni sinia langu la kunawia, juu ya Edomu natupa kiatu changu; nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.” 10 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome? Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu? 11 Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi, na hutoki tena na majeshi yetu? 12 Tuletee msaada dhidi ya adui, kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu. 13 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi, naye atawaponda adui zetu. Chapter 109Zaburi 109 1 Ee Mungu, ambaye ninakusifu, usiwe kimya, 2 kwa maana watu waovu na wadanganyifu wamefungua vinywa vyao dhidi yangu; wasema dhidi yangu kwa ndimi za udanganyifu. 3 Wamenizunguka kwa maneno ya chuki, wananishambulia bila sababu. 4 Wanachonilipa badala ya urafiki wangu ni kunishtaki, lakini mimi ninawaombea. 5 Wananilipiza mabaya kwa mema, chuki badala ya urafiki wangu. 6 Agiza mtu mwovu ampinge, mshtaki asimame mkono wake wa kuume. 7 Anapohukumiwa, apatikane na hatia, nayo maombi yake yamhukumu. 8 Siku zake za kuishi na ziwe chache, nafasi yake ya uongozi ichukuliwe na mtu mwingine. 9 Watoto wake na waachwe yatima, mke wake na awe mjane. 10 Watoto wake na watangetange wakiomba, na wafukuzwe kwenye magofu ya nyumba zao. 11 Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo, matunda ya kazi yake yatekwe nyara na wageni. 12 Asiwepo mtu yeyote wa kumtendea mema wala wa kuwahurumia yatima wake. 13 Uzao wake na ukatiliwe mbali, majina yao yafutike katika kizazi kifuatacho. 14 Maovu ya baba zake na yakumbukwe mbele za Bwana, dhambi ya mama yake isifutwe kamwe. 15 Dhambi zao na zibaki daima mbele za Bwana, ili apate kukatilia mbali kumbukumbu lao duniani. 16 Kwa maana kamwe hakuweza kutenda wema, bali alimfukuza mnyonge na mhitaji, aliwafanyia jeuri wahitaji na waliovunjika moyo. 17 Alipenda kulaani, nayo laana ikampata; hakupenda kubariki, kwa hiyo baraka na ikae mbali naye. 18 Alivaa kulaani kama vazi lake, nayo laana ikamwingia mwilini mwake kama maji, kwenye mifupa yake kama mafuta. 19 Na iwe kama joho alilozungushiwa, kama mshipi aliofungiwa daima. 20 Haya na yawe malipo ya Bwana kwa washtaki wangu, kwa wale wanaoninenea mabaya. 21 Lakini wewe, Ee Bwana Mwenyezi, unitendee wema kwa ajili ya jina lako, uniokoe kwa wema wa pendo lako. 22 Maana mimi ni maskini na mhitaji, moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu. 23 Ninafifia kama kivuli cha jioni, nimerushwa-rushwa kama nzige. 24 Magoti yangu yamelegea kwa kufunga, mwili wangu umedhoofika na kukonda. 25 Nimekuwa kitu cha kudharauliwa kwa washtaki wangu, wanionapo, hutikisa vichwa vyao. 26 Ee Bwana, Mungu wangu nisaidie, niokoe sawasawa na upendo wako. 27 Watu na wafahamu kuwa ni mkono wako, kwamba wewe, Ee Bwana, umetenda hili. 28 Wanaweza kulaani, lakini wewe utabariki, watakaposhambulia wataaibishwa, lakini mtumishi wako atashangilia. 29 Washtaki wangu watavikwa fedheha, na kufunikwa na aibu kama joho. 30 Kwa kinywa changu nitamtukuza sana Bwana, katika umati mkubwa nitamsifu. 31 Kwa maana husimama mkono wa kuume wa mhitaji, kuokoa maisha yake kutoka kwa wale wanaomhukumu. Chapter 110Zaburi 110 1 Bwana amwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, mpaka nitakapowafanya adui zako kuwa mahali pa kuweka miguu yako.” 2 Bwana ataeneza fimbo yako ya utawala yenye nguvu kutoka Sayuni; utatawala katikati ya adui zako. 3 Askari wako watajitolea kwa hiari katika siku yako ya vita. Ukiwa umevikwa fahari takatifu, kutoka tumbo la mapambazuko utapokea umande wa ujana wako. 4 Bwana ameapa, naye hatabadilisha mawazo yake: “Wewe ni kuhani milele, kwa mfano wa Melkizedeki.” 5 Bwana yuko mkono wako wa kuume, atawaponda wafalme siku ya ghadhabu yake. 6 Atawahukumu mataifa, akilundika mizoga na kuwaponda watawala wa dunia nzima. 7 Atakunywa maji katika kijito kando ya njia, kwa hiyo atainua kichwa chake juu. Chapter 111Zaburi 111 1 Msifuni Bwana. Nitamtukuza Bwana kwa moyo wangu wote, katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko. 2 Kazi za Bwana ni kuu, wote wanaopendezwa nazo huzitafakari. 3 Kazi zake zimejaa fahari na utukufu, haki yake hudumu daima. 4 Amefanya maajabu yake yakumbukwe, Bwana ni mwenye neema na huruma. 5 Huwapa chakula wale wanaomcha, hulikumbuka agano lake milele. 6 Amewaonyesha watu wake uwezo wa kazi zake, akiwapa nchi za mataifa mengine. 7 Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki, mausia yake yote ni ya kuaminika. 8 Zinadumu milele na milele, zikifanyika kwa uaminifu na unyofu. 9 Aliwapa watu wake ukombozi, aliamuru agano lake milele: jina lake ni takatifu na la kuogopwa. 10 Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima, wote wanaozifuata amri zake wana busara. Sifa zake zadumu milele. Chapter 112Zaburi 112 1 Msifuni Bwana. Heri mtu yule amchaye Bwana, mtu yule apendezwaye sana na amri zake. 2 Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi, kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa. 3 Nyumbani mwake kuna mali na utajiri, haki yake hudumu milele. 4 Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu, yule mwenye rehema, huruma na haki. 5 Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba, anayefanya mambo yake kwa haki. 6 Hakika hatatikisika kamwe, mtu mwenye haki atakumbukwa milele. 7 Hataogopa habari mbaya, moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Bwana. 8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu, mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake. 9 Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini; haki yake hudumu milele; pembe yake itatukuzwa kwa heshima. 10 Mtu mwovu ataona na kuchukizwa, atasaga meno yake na kutoweka, kutamani kwa mtu mwovu kutaishia patupu. Chapter 113Zaburi 113 1 Msifuni Bwana. Enyi watumishi wa Bwana msifuni, lisifuni jina la Bwana. 2 Jina la Bwana na lisifiwe, sasa na hata milele. 3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake, jina la Bwana linapaswa kusifiwa. 4 Bwana ametukuka juu ya mataifa yote, utukufu wake juu ya mbingu. 5 Ni nani aliye kama Bwana Mungu wetu, Yeye ambaye ameketi juu kwenye kiti cha enzi, 6 ambaye huinama atazame chini aone mbingu na nchi? 7 Huwainua maskini kutoka mavumbini, na kuwanyanyua wahitaji kutoka kwenye jalala, 8 huwaketisha pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake. 9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake, akiwa mama watoto mwenye furaha. Msifuni Bwana. Chapter 114Zaburi 114 1 Wakati Israeli walipotoka Misri, nyumba ya Yakobo kutoka kwa watu wa lugha ngeni, 2 Yuda alifanywa makao matakatifu ya Mungu, Israeli akawa milki yake. 3 Bahari ilitazama ikakimbia, Yordani ulirudi nyuma, 4 milima ilirukaruka kama kondoo dume, vilima kama wana-kondoo. 5 Ee bahari, ni nini kilichokufanya ukakimbia, nawe, ee Yordani, ukarudi nyuma, 6 enyi milima mkarukaruka kama kondoo dume, enyi vilima, kama wana-kondoo? 7 Ee dunia, tetemeka mbele za Bwana, mbele za Mungu wa Yakobo, 8 aliyegeuza mwamba kuwa dimbwi la maji, mwamba mgumu kuwa chemchemi za maji. Chapter 115Zaburi 115 1 Sio kwetu sisi, Ee Bwana, sio kwetu sisi, bali utukufu ni kwa jina lako, kwa sababu ya upendo na uaminifu wako. 2 Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wao?” 3 Mungu wetu yuko mbinguni, naye hufanya lolote limpendezalo. 4 Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 5 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema, zina macho, lakini haziwezi kuona; 6 zina masikio, lakini haziwezi kusikia, zina pua, lakini haziwezi kunusa; 7 zina mikono, lakini haziwezi kupapasa, zina miguu, lakini haziwezi kutembea; wala koo zao haziwezi kutoa sauti. 8 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo, vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia. 9 Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Bwana, yeye ni msaada na ngao yao. 10 Ee nyumba ya Aroni, mtumainini Bwana, yeye ni msaada na ngao yao. 11 Ninyi mnaomcha, mtumainini Bwana, yeye ni msaada na ngao yao. 12 Bwana anatukumbuka na atatubariki: ataibariki nyumba ya Israeli, ataibariki nyumba ya Aroni, 13 atawabariki wale wanaomcha Bwana, wadogo kwa wakubwa. 14 Bwana na awawezeshe kuongezeka, ninyi na watoto wenu. 15 Mbarikiwe na Bwana Muumba wa mbingu na dunia. 16 Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Bwana, lakini dunia amempa mwanadamu. 17 Sio wafu wanaomsifu Bwana, wale washukao mahali pa kimya, 18 bali ni sisi tunaomtukuza Bwana, sasa na hata milele. Msifuni Bwana. Chapter 116Zaburi 116 1 Ninampenda Bwana kwa maana amesikia sauti yangu; amesikia kilio changu ili anihurumie. 2 Kwa sababu amenitegea sikio lake, nitamwita siku zote za maisha yangu. 3 Kamba za mauti zilinizunguka, maumivu makuu ya kuzimu yalinipata, nikalemewa na taabu na huzuni. 4 Ndipo nikaliitia jina la Bwana: “Ee Bwana, niokoe!” 5 Bwana ni mwenye neema na haki, Mungu wetu ni mwingi wa huruma. 6 Bwana huwalinda wanyenyekevu, nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa. 7 Ee nafsi yangu, tulia tena, kwa kuwa Bwana amekuwa mwema kwako. 8 Kwa kuwa wewe, Ee Bwana, umeniokoa nafsi yangu na mauti, macho yangu kutokana na machozi, miguu yangu kutokana na kujikwaa, 9 ili niweze kutembea mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai. 10 Niliamini, kwa hiyo nilisema, “Mimi nimeteseka sana.” 11 Katika taabu yangu nilisema, “Wanadamu wote ni waongo.” 12 Nimrudishie Bwana nini kwa wema wake wote alionitendea? 13 Nitakiinua kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la Bwana. 14 Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Bwana mbele za watu wake wote. 15 Kifo cha watakatifu kina thamani machoni pa Bwana. 16 Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako, mimi ni mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako; umeniweka huru toka katika minyororo yangu. 17 Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru na kuliita jina la Bwana. 18 Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Bwana mbele za watu wake wote, 19 katika nyua za nyumba ya Bwana, katikati yako, ee Yerusalemu. Msifuni Bwana. Chapter 117Zaburi 117 1 Msifuni Bwana, enyi mataifa yote; mtukuzeni yeye, enyi watu wote. 2 Kwa kuwa upendo wake kwetu ni mkuu, uaminifu wa Bwana unadumu milele. Msifuni Bwana. Chapter 118Zaburi 118 1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele. 2 Israeli na aseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.” 3 Nyumba ya Aroni na iseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.” 4 Wote wamchao Bwana na waseme sasa: “Upendo wake wadumu milele.” 5 Wakati wa maumivu yangu makuu nilimlilia Bwana, naye akanijibu kwa kuniweka huru. 6 Bwana yuko pamoja nami, sitaogopa. Mwanadamu anaweza kunitenda nini? 7 Bwana yuko pamoja nami, yeye ni msaidizi wangu. Nitawatazama adui zangu wakiwa wameshindwa. 8 Ni bora kumkimbilia Bwana kuliko kumtumainia mwanadamu. 9 Ni bora kumkimbilia Bwana kuliko kuwatumainia wakuu. 10 Mataifa yote yalinizunguka, lakini kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. 11 Walinizunguka pande zote, lakini kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. 12 Walinizunguka kama kundi la nyuki, lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo; kwa jina la Bwana naliwakatilia mbali. 13 Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka, lakini Bwana alinisaidia. 14 Bwana ni nguvu yangu na wimbo wangu, yeye amefanyika wokovu wangu. 15 Sauti za shangwe na ushindi zinavuma hemani mwa wenye haki: “Mkono wa kuume wa Bwana umetenda mambo makuu! 16 Mkono wa kuume wa Bwana umeinuliwa juu, mkono wa kuume wa Bwana umetenda mambo makuu!” 17 Sitakufa, bali nitaishi, nami nitatangaza yale Bwana aliyoyatenda. 18 Bwana ameniadhibu vikali, lakini hakuniacha nife. 19 Nifungulie malango ya haki, nami nitaingia na kumshukuru Bwana. 20 Hili ni lango la Bwana ambalo wenye haki wanaweza kuliingia. 21 Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu, umekuwa wokovu wangu. 22 Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni. 23 Bwana ametenda hili, nalo ni la kushangaza machoni petu. 24 Hii ndiyo siku Bwana aliyoifanya, tushangilie na kufurahi ndani yake. 25 Ee Bwana, tuokoe, Ee Bwana, utujalie mafanikio. 26 Heri yule ajaye kwa jina la Bwana. Kutoka nyumba ya Bwana tunakubariki. 27 Bwana ndiye Mungu, naye ametuangazia nuru yake. Mkiwa na matawi mkononi, unganeni kwenye maandamano ya sikukuu hadi kwenye pembe za madhabahu. 28 Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru, wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza. 29 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; upendo wake wadumu milele. Chapter 119Zaburi 119 1 Heri wale walio waadilifu katika njia zao, wanaoenenda katika sheria ya Bwana. 2 Heri wale wanaozishika shuhuda zake, wamtafutao kwa moyo wao wote. 3 Wasiofanya lolote lililo baya, wanaoenenda katika njia zake. 4 Umetoa maagizo yako ili tuyatii kwa ukamilifu. 5 Laiti mwenendo wangu ungekuwa imara katika kuyatii maagizo yako! 6 Hivyo mimi sitaaibishwa ninapozingatia amri zako zote. 7 Nitakusifu kwa moyo mnyofu ninapojifunza sheria zako za haki. 8 Nitayatii maagizo yako; usiniache kabisa. 9 Kijana aifanye njia yake kuwa safi jinsi gani? Ni kwa kutii, akilifuata neno lako. 10 Ninakutafuta kwa moyo wangu wote, usiniache niende mbali na amri zako. 11 Nimelificha neno lako moyoni mwangu ili nisikutende dhambi. 12 Sifa ni zako, Ee Bwana, nifundishe maagizo yako. 13 Kwa midomo yangu nitasimulia sheria zote zinazotoka katika kinywa chako. 14 Ninafurahia kufuata sheria zako kama mtu afurahiaye mali nyingi. 15 Ninatafakari maagizo yako na kuziangalia njia zako. 16 Ninafurahia maagizo yako, wala sitalipuuza neno lako. 17 Mtendee mema mtumishi wako, nami nitaishi; nitalitii neno lako. 18 Yafungue macho yangu nipate kuona mambo ya ajabu katika sheria yako. 19 Mimi ni mgeni duniani, usinifiche amri zako. 20 Nafsi yangu inataabika kwa shauku kubwa juu ya sheria zako wakati wote. 21 Unawakemea wenye majivuno, waliolaaniwa waendao mbali na amri zako. 22 Niondolee dharau na dhihaka, kwa kuwa ninazishika sheria zako. 23 Ingawa watawala huketi pamoja na kunisingizia, mtumishi wako atatafakari juu ya maagizo yako. 24 Sheria zako ni furaha yangu, nazo ni washauri wangu. 25 Nimelazwa chini mavumbini, yahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. 26 Nilikueleza njia zangu ukanijibu, nifundishe sheria zako. 27 Nijulishe mafundisho ya mausia yako, nami nitatafakari maajabu yako. 28 Nafsi yangu imechakazwa kwa huzuni, uniimarishe sawasawa na neno lako. 29 Niepushe na njia za udanganyifu, kwa neema unifundishe sheria zako. 30 Nimechagua njia ya kweli, nimekaza moyo wangu katika sheria zako. 31 Nimengʼangʼania sheria zako, Ee Bwana, usiniache niaibishwe. 32 Nakimbilia katika njia ya maagizo yako, kwa kuwa umeuweka moyo wangu huru. 33 Ee Bwana, nifundishe kuyafuata maagizo yako, nami nitayashika mpaka mwisho. 34 Nipe ufahamu, nami nitaishika sheria yako na kuitii kwa moyo wangu wote. 35 Niongoze kwenye njia ya amri zako, kwa kuwa huko napata furaha. 36 Ugeuze moyo wangu kuelekea sheria zako, na siyo kwenye mambo ya ubinafsi. 37 Geuza macho yangu kutoka kwenye mambo yasiyofaa, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na neno lako. 38 Mtimizie mtumishi wako ahadi yako, ili upate kuogopwa. 39 Niondolee aibu ninayoiogopa, kwa kuwa sheria zako ni njema. 40 Tazama jinsi ninavyoonea shauku mausia yako! Hifadhi maisha yangu katika haki yako. 41 Ee Bwana, upendo wako usiokoma unijie, wokovu wako sawasawa na ahadi yako, 42 ndipo nitakapomjibu anayenidhihaki, kwa kuwa ninalitumainia neno lako. 43 Usilinyakue neno la kweli kutoka kinywani mwangu, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika amri zako. 44 Nitaitii amri yako daima, naam, milele na milele. 45 Nitatembea nikiwa huru, kwa kuwa nimejifunza mausia yako. 46 Nitasema sheria zako mbele za wafalme wala sitaaibishwa, 47 kwa kuwa ninazifurahia amri zako kwa sababu ninazipenda. 48 Ninaziinulia amri zako ambazo ninazipenda mikono yangu, nami ninatafakari juu ya maagizo yako. 49 Kumbuka neno lako kwa mtumishi wako, kwa sababu umenipa tumaini. 50 Faraja yangu katika mateso yangu ni hii: Ahadi yako inahifadhi maisha yangu. 51 Wenye majivuno wamenisimanga bila kuchoka, hata hivyo sitaiacha sheria yako. 52 Ee Bwana, ninazikumbuka sheria zako za zamani, nazo zinanifariji. 53 Nimeshikwa sana na ghadhabu kwa ajili ya waovu, ambao wameacha sheria yako. 54 Maagizo yako ni kiini cha nyimbo zangu popote ninapoishi. 55 Ee Bwana, wakati wa usiku ninalikumbuka jina lako, nami nitatii sheria yako. 56 Hili limekuwa zoezi langu: nami ninayatii mausia yako. 57 Ee Bwana, wewe ni fungu langu, nimeahidi kuyatii maneno yako. 58 Nimetafuta uso wako kwa moyo wangu wote, nihurumie sawasawa na ahadi yako. 59 Nimezifikiri njia zangu na nimeelekeza hatua zangu katika mausia yako. 60 Nitafanya haraka bila kuchelewa kuzitii amri zako. 61 Hata waovu wanifunge kwa kamba, sitasahau sheria yako. 62 Usiku wa manane ninaamka kukushukuru kwa sababu ya sheria zako za haki. 63 Mimi ni rafiki kwa wale wote wakuchao, kwa wote wanaofuata mausia yako. 64 Ee Bwana, dunia imejaa upendo wako, nifundishe maagizo yako. 65 Mtendee wema mtumishi wako Ee Bwana, sawasawa na neno lako. 66 Nifundishe maarifa na uamuzi mzuri, kwa kuwa ninaamini amri zako. 67 Kabla sijapata shida nilipotea njia, lakini sasa ninalitii neno lako. 68 Wewe ni mwema, unalotenda ni jema, nifundishe maagizo yako. 69 Ingawa wenye majivuno wamenisingizia uongo, nitafuata mausia yako kwa moyo wangu wote. 70 Mioyo yao ni katili na migumu, bali mimi napendezwa na sheria yako. 71 Ilikuwa vyema mimi kupata shida ili nipate kujifunza maagizo yako. 72 Sheria inayotoka kinywani mwako ina thamani kubwa kwangu kuliko maelfu ya vipande vya fedha na dhahabu. 73 Mikono yako ilinifanya na kuniumba, nipe ufahamu niweze kujifunza amri zako. 74 Wakuchao wafurahie wanaponiona, kwa kuwa nimeweka tumaini langu katika neno lako. 75 Ee Bwana, ninajua kwamba sheria zako ni za haki, katika uaminifu wako umeniadhibu. 76 Upendo wako usiokoma uwe faraja yangu, sawasawa na ahadi yako kwa mtumishi wako. 77 Huruma yako na inijie ili nipate kuishi, kwa kuwa naifurahia sheria yako. 78 Wenye majivuno na waaibishwe kwa kunikosea mimi bila sababu, lakini mimi nitatafakari juu ya mausia yako. 79 Wale wakuchao na wanigeukie mimi, hao ambao wanazielewa sheria zako. 80 Moyo wangu usiwe na lawama katika kutii maagizo yako, ili nisiaibishwe. 81 Nafsi yangu inazimia kwa kutamani wokovu wako, lakini nimeweka tumaini langu katika neno lako. 82 Macho yangu yamefifia, nikingoja ahadi yako; ninasema, “Utanifajiri lini?” 83 Ingawa nimekuwa kama kiriba kwenye moshi, bado sijasahau maagizo yako. 84 Mtumishi wako itampasa angoje mpaka lini? Ni lini utawaadhibu washtaki wangu? 85 Wenye majivuno wananichimbia mashimo, kinyume na sheria yako. 86 Amri zako zote ni za kuaminika; unisaidie, kwa sababu watu wananishtaki bila sababu. 87 Walikaribia kabisa kunifuta kutoka uso wa dunia, lakini sijaacha mausia yako. 88 Yahifadhi maisha yangu sawasawa na upendo wako, nami nitatii sheria za kinywa chako. 89 Ee Bwana, neno lako ni la milele, linasimama imara mbinguni. 90 Uaminifu wako unaendelea kwa vizazi vyote, umeiumba dunia, nayo inadumu. 91 Sheria zako zinadumu hadi leo, kwa kuwa vitu vyote vinakutumikia. 92 Kama nisingefurahia sheria yako, ningeangamia katika taabu zangu. 93 Sitasahau mausia yako kamwe, kwa maana kwayo umehifadhi maisha yangu. 94 Uniokoe, kwa maana mimi ni wako, kwa kuwa nimetafuta mausia yako. 95 Waovu wanangojea kuniangamiza, bali mimi ninatafakari sheria zako. 96 Katika ukamilifu wote ninaona mna kikomo, lakini amri zako hazina mpaka. 97 Aha! Tazama, sheria yako naipenda mno ajabu. Ninaitafakari mchana kutwa. 98 Amri zako zimenipa hekima zaidi kuliko adui zangu, kwa kuwa nimezishika daima. 99 Nina akili zaidi kuliko walimu wangu wote, kwa kuwa ninatafakari juu ya sheria zako. 100 Nina ufahamu zaidi kuliko wazee, kwa kuwa ninayatii mausia yako. 101 Nimezuia miguu yangu isiende kwenye kila njia mbaya, ili niweze kutii neno lako. 102 Sijaziacha sheria zako, kwa kuwa umenifundisha wewe mwenyewe. 103 Tazama jinsi maneno yako yalivyo matamu kwangu, matamu kuliko asali katika kinywa changu! 104 Ninapata ufahamu kutoka mausia yako, kwa hiyo ninachukia kila njia ya upotovu. 105 Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga katika njia yangu. 106 Nimeapa na nimethibitisha, kwamba nitafuata sheria zako za haki. 107 Nimeteseka sana, uhifadhi maisha yangu, Ee Bwana, sawasawa na neno lako. 108 Ee Bwana, pokea sifa za hiari za kinywa changu, nifundishe sheria zako. 109 Ingawa maisha yangu yako hatarini siku zote, sitasahau sheria yako. 110 Waovu wamenitegea mtego, lakini sijayakiuka maagizo yako. 111 Sheria zako ni urithi wangu milele, naam ni furaha ya moyo wangu. 112 Nimekusudia moyoni mwangu kuyafuata maagizo yako mpaka mwisho. 113 Ninachukia watu wa nia mbili, lakini ninapenda sheria yako. 114 Wewe ni kimbilio langu na ngao yangu, nimeweka tumaini langu katika neno lako. 115 Ondokeni kwangu, ninyi mtendao mabaya, ili niweze kushika amri za Mungu wangu! 116 Nihifadhi sawasawa na ahadi yako, nami nitaishi; usiache matumaini yangu yakavunjwa. 117 Nitegemeze, nami nitaokolewa, nami daima nitayaheshimu maagizo yako. 118 Unawakataa wote wanaoyaasi maagizo yako, kwa maana udanganyifu wao ni bure. 119 Waovu wa nchi unawatupa kama takataka, kwa hivyo nazipenda sheria zako. 120 Mwili wangu unatetemeka kwa kukuogopa wewe, ninaziogopa sheria zako. 121 Nimetenda yaliyo haki na sawa, usiniache mikononi mwa watesi wangu. 122 Mhakikishie mtumishi wako usalama, usiache wenye kiburi wanionee. 123 Macho yangu yamefifia, yakitazamia wokovu wako, na kuitazamia ahadi yako ya kweli. 124 Mfanyie mtumishi wako kulingana na upendo wako na unifundishe maagizo yako. 125 Mimi ni mtumishi wako; nipe ufahamu ili niweze kuelewa sheria zako. 126 Ee Bwana, wakati wako wa kutenda umewadia, kwa kuwa sheria yako inavunjwa. 127 Kwa sababu nazipenda amri zako zaidi ya dhahabu, naam, zaidi ya dhahabu safi, 128 na kwa sababu naona maagizo yako yote ni adili, nachukia kila njia potovu. 129 Sheria zako ni za ajabu, hivyo ninazitii. 130 Kuingia kwa maneno yako kunaleta nuru, kunampa mjinga ufahamu. 131 Nimefungua kinywa changu na kuhema, nikitamani amri zako. 132 Nigeukie na unihurumie, kama uwafanyiavyo siku zote wale wanaolipenda jina lako. 133 Ongoza hatua zangu kulingana na neno lako, usiache dhambi yoyote initawale. 134 Niokoe na uonevu wa wanadamu, ili niweze kutii mausia yako. 135 Mwangazie mtumishi wako uso wako na unifundishe amri zako. 136 Chemchemi za machozi zinatiririka kutoka machoni yangu, kwa kuwa sheria yako haifuatwi. 137 Ee Bwana, wewe ni mwenye haki, sheria zako ni sahihi. 138 Sheria ulizoziweka ni za haki, ni za kuaminika kikamilifu. 139 Jitihada yangu imenidhoofisha, kwa kuwa adui zangu wanayapuuza maneno yako. 140 Ahadi zako zimejaribiwa kikamilifu, mtumishi wako anazipenda. 141 Ingawa ni mdogo na ninadharauliwa, sisahau mausia yako. 142 Haki yako ni ya milele, na sheria yako ni kweli. 143 Shida na dhiki zimenipata, lakini amri zako ni furaha yangu. 144 Sheria zako ni sahihi milele, hunipa ufahamu ili nipate kuishi. 145 Ee Bwana, ninakuita kwa moyo wangu wote, nami nitayatii maagizo yako. 146 Ninakuita; niokoe nami nitazishika sheria zako. 147 Ninaamka asubuhi na mapema na kukuomba msaada; nimeweka tumaini langu katika neno lako. 148 Sikufumba macho yangu usiku kucha, ili niweze kutafakari juu ya ahadi zako. 149 Usikie sauti yangu sawasawa na upendo wako, Ee Bwana, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na sheria zako. 150 Wale wanaopanga mipango miovu wako karibu nami, lakini wako mbali na sheria yako. 151 Ee Bwana, hata hivyo wewe u karibu, na amri zako zote ni za kweli. 152 Tangu zamani nimejifunza kutoka shuhuda zako kwamba umezithibitisha ili zidumu milele. 153 Yaangalie mateso yangu, uniokoe, kwa kuwa sijasahau sheria yako. 154 Nitetee katika hali hii yangu na unikomboe, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na ahadi yako. 155 Wokovu uko mbali na waovu, kwa kuwa hawatafuti maagizo yako. 156 Ee Bwana, huruma zako ni kuu, uyahifadhi maisha yangu sawasawa na sheria zako. 157 Adui wanaonitesa ni wengi, lakini mimi sitaziacha sheria zako. 158 Ninawatazama wasioamini kwa chuki, kwa kuwa hawalitii neno lako. 159 Tazama jinsi ninavyopenda mausia yako; Ee Bwana, uyahifadhi maisha yangu, sawasawa na upendo wako. 160 Maneno yako yote ni kweli, sheria zako zote za haki ni za milele. 161 Watawala wamenitesa bila sababu, lakini moyo wangu unatetemeka kwa neno lako. 162 Nafurahia ahadi zako kama mtu aliyepata mateka mengi. 163 Ninachukia na kuchukizwa sana na uongo, lakini napenda sheria yako. 164 Ninakusifu mara saba kwa siku, kwa ajili ya sheria zako za haki. 165 Wanaopenda sheria yako wana amani tele, wala hakuna kitu kinachoweza kuwakwaza. 166 Ee Bwana, ninangojea wokovu wako, nami ninafuata amri zako, 167 Ninazitii sheria zako, kwa sababu ninazipenda mno. 168 Nimetii mausia yako na sheria zako, kwa kuwa njia zangu zote zinajulikana kwako. 169 Ee Bwana, kilio changu na kifike mbele zako, nipe ufahamu sawasawa na neno lako. 170 Maombi yangu na yafike mbele zako, niokoe sawasawa na ahadi yako. 171 Midomo yangu na ibubujike sifa, kwa kuwa unanifundisha maagizo yako. 172 Ulimi wangu na uimbe kuhusu neno lako, kwa kuwa amri zako zote ni za haki. 173 Mkono wako uwe tayari kunisaidia, kwa kuwa nimechagua mausia yako. 174 Ee Bwana, ninatamani wokovu wako, na sheria yako ni furaha yangu. 175 Nijalie kuishi ili nipate kukusifu, na sheria zako zinitegemeze. 176 Nimetangatanga kama kondoo aliyepotea. Mtafute mtumishi wako, kwa kuwa sijasahau amri zako. Chapter 120Zaburi 120 1 Katika dhiki yangu namwita Bwana, naye hunijibu. 2 Ee Bwana, uniokoe kutoka midomo ya uongo na ndimi za udanganyifu. 3 Atakufanyia nini, au akufanyie nini zaidi, ewe ulimi mdanganyifu? 4 Atakuadhibu kwa mishale mikali ya shujaa, kwa makaa yanayowaka ya mti wa mretemu. 5 Ole wangu kwa kuwa naishi Mesheki, kwamba naishi katikati ya hema za Kedari! 6 Nimeishi muda mrefu mno miongoni mwa wale wanaochukia amani. 7 Mimi ni mtu wa amani; lakini ninaposema, wao wanataka vita. Chapter 121Zaburi 121 1 Nayainua macho yangu nitazame vilima, msaada wangu utatoka wapi? 2 Msaada wangu hutoka kwa Bwana, Muumba wa mbingu na dunia. 3 Hatauacha mguu wako uteleze, yeye akulindaye hatasinzia, 4 hakika, yeye alindaye Israeli hatasinzia wala hatalala usingizi. 5 Bwana anakulinda, Bwana ni uvuli wako mkono wako wa kuume, 6 jua halitakudhuru mchana, wala mwezi wakati wa usiku. 7 Bwana atakukinga na madhara yote, atayalinda maisha yako, 8 Bwana atakulinda unapoingia na unapotoka, tangu sasa na hata milele. Chapter 122Zaburi 122 1 Nilishangilia pamoja na wale walioniambia, “Twende nyumbani ya Bwana.” 2 Ee Yerusalemu, miguu yetu imesimama malangoni mwako. 3 Yerusalemu imejengwa vyema kama mji ambao umeshikamanishwa pamoja. 4 Huko ndiko makabila hukwea, makabila ya Bwana, kulisifu jina la Bwana kulingana na maagizo waliopewa Israeli. 5 Huko viti vya enzi vya hukumu hukaa, viti vya enzi vya nyumba ya Daudi. 6 Omba kwa ajili ya amani ya Yerusalemu: “Wote wakupendao na wawe salama. 7 Amani na iwepo ndani ya kuta zako na usalama ndani ya ngome zako.” 8 Kwa ajili ya ndugu zangu na marafiki, nitasema, “Amani iwe ndani yako.” 9 Kwa ajili ya nyumba ya Bwana Mungu wetu, nitatafuta mafanikio yako. Chapter 123Zaburi 123 1 Ninayainua macho yangu kwako, kwako wewe ambaye kiti chako cha enzi kiko mbinguni. 2 Kama vile macho ya watumwa yatazamavyo mkono wa bwana wao, kama vile macho ya mtumishi wa kike yatazamavyo mkono wa bibi yake, ndivyo macho yetu yamtazamavyo Bwana Mungu wetu, mpaka atakapotuhurumia. 3 Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu, kwa maana tumevumilia dharau nyingi. 4 Tumevumilia dhihaka nyingi kutoka kwa wenye kiburi, dharau nyingi kutoka kwa wenye majivuno. Chapter 124Zaburi 124 1 Kama Bwana asingalikuwa upande wetu; Israeli na aseme sasa: 2 kama Bwana asingalikuwa upande wetu, wakati watu walipotushambulia, 3 wakati hasira yao ilipowaka dhidi yetu, wangalitumeza tungali hai, 4 mafuriko yangalitugharikisha, maji mengi yangalitufunika, 5 maji yaendayo kasi yangalituchukua. 6 Bwana asifiwe, yeye ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao. 7 Tumeponyoka kama ndege kutoka mtego wa mwindaji; mtego umevunjika, nasi tukaokoka. 8 Msaada wetu ni katika jina la Bwana, Muumba wa mbingu na dunia. Chapter 125Zaburi 125 1 Wale wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, ambao hauwezi kutikisika, bali wadumu milele. 2 Kama milima inavyozunguka Yerusalemu, ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake sasa na hata milele. 3 Fimbo ya waovu haitadumu juu ya nchi waliopewa wenye haki, ili wenye haki wasije wakatumia mikono yao kutenda ubaya. 4 Ee Bwana, watendee mema walio wema, wale walio wanyofu wa moyo. 5 Bali wale wanaogeukia njia zilizopotoka, Bwana atawafukuza pamoja na watenda mabaya. Amani iwe juu ya Israeli. Chapter 126Zaburi 126 1 Bwana alipowarejeza mateka Sayuni, tulikuwa kama watu walioota ndoto. 2 Vinywa vyetu vilijaa kicheko, ndimi zetu zilijaa nyimbo za shangwe. Ndipo iliposemwa miongoni mwa mataifa, “Bwana amewatendea mambo makuu.” 3 Bwana ametutendea mambo makuu, nasi tumejaa furaha. 4 Ee Bwana, turejeshee watu wetu waliotekwa, kama vijito katika Negebu. 5 Wapandao kwa machozi watavuna kwa nyimbo za shangwe. 6 Yeye azichukuaye mbegu zake kwenda kupanda, huku akilia, atarudi kwa nyimbo za shangwe, akichukua miganda ya mavuno yake. Chapter 127Zaburi 127 1 Bwana asipoijenga nyumba, wajengao hufanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji, walinzi wakesha bure. 2 Mnajisumbua bure kuamka mapema na kuchelewa kulala, mkitaabikia chakula: kwa maana yeye huwapa usingizi wapenzi wake. 3 Wana ni urithi utokao kwa Bwana, watoto ni zawadi kutoka kwake. 4 Kama mishale mikononi mwa shujaa ndivyo walivyo wana awazaao mtu katika ujana wake. 5 Heri mtu ambaye podo lake limejazwa nao. Hawataaibishwa wanaposhindana na adui zao langoni. Chapter 128Zaburi 128 1 Heri ni wale wote wamchao Bwana, waendao katika njia zake. 2 Utakula matunda ya kazi yako; baraka na mafanikio vitakuwa vyako. 3 Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao ndani ya nyumba yako; wana wako watakuwa kama machipukizi ya mizeituni kuizunguka meza yako. 4 Hivyo ndivyo atakavyobarikiwa mtu amchaye Bwana. 5 Bwana na akubariki kutoka Sayuni siku zote za maisha yako, na uone mafanikio ya Yerusalemu, 6 nawe ujaliwe kuishi uone watoto wa watoto wako. Amani iwe juu ya Israeli. Chapter 129Zaburi 129 1 Wamenionea mno tangu ujana wangu; Israeli na aseme sasa: 2 wamenionea mno tangu ujana wangu, lakini bado hawajanishinda. 3 Wakulima wamelima mgongo wangu, na kufanya mifereji yao mirefu. 4 Lakini Bwana ni mwenye haki; amenifungua toka kamba za waovu. 5 Wale wote waichukiao Sayuni na warudishwe nyuma kwa aibu. 6 Wawe kama majani juu ya paa, ambayo hunyauka kabla hayajakua; 7 kwa hayo mvunaji hawezi kujaza vitanga vyake, wala akusanyaye kujaza mikono yake. 8 Wale wapitao karibu na wasiseme, “Baraka ya Bwana iwe juu yako; tunakubariki katika jina la Bwana.” Chapter 130Zaburi 130 1 Kutoka vilindini ninakulilia, Ee Bwana. 2 Ee Bwana, sikia sauti yangu. Masikio yako na yawe masikivu kwa kilio changu unihurumie. 3 Kama wewe, Ee Bwana, ungeweka kumbukumbu ya dhambi, Ee Bwana, ni nani angeliweza kusimama? 4 Lakini kwako kuna msamaha, kwa hiyo wewe unaogopwa. 5 Namngojea Bwana, nafsi yangu inangojea, katika neno lake naweka tumaini langu. 6 Nafsi yangu inamngojea Bwana kuliko walinzi waingojeavyo asubuhi, naam, kuliko walinzi waingojeavyo asubuhi. 7 Ee Israeli, mtumaini Bwana, maana kwa Bwana kuna upendo usiokoma, na kwake kuna ukombozi kamili. 8 Yeye mwenyewe ataikomboa Israeli kutoka dhambi zao zote. Chapter 131Zaburi 131 1 Moyo wangu hauna kiburi, Ee Bwana, macho yangu hayajivuni; sijishughulishi na mambo makuu kunizidi wala mambo ya ajabu mno kwangu. 2 Lakini nimetuliza na kunyamazisha nafsi yangu; kama mtoto aliyeachishwa kunyonya na mama yake, kama mtoto aliyeachishwa kunyonya ndivyo ilivyo nafsi iliyoko ndani yangu. 3 Ee Israeli, mtumaini Bwana tangu sasa na hata milele. Chapter 132Zaburi 132 1 Ee Bwana, mkumbuke Daudi na taabu zote alizozistahimili. 2 Aliapa kiapo kwa Bwana na akaweka nadhiri kwa Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo: 3 “Sitaingia nyumbani mwangu au kwenda kitandani mwangu: 4 sitaruhusu usingizi katika macho yangu, wala kope zangu kusinzia, 5 mpaka nitakapompatia Bwana mahali, makao kwa ajili ya Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo.” 6 Tulisikia habari hii huko Efrathi, tulikutana nayo katika mashamba ya Yaara: 7 “Twendeni kwenye makao yake, na tuabudu kwenye kiti cha kuwekea miguu yake; 8 inuka, Ee Bwana, uje mahali pako pa kupumzikia, wewe na Sanduku la nguvu zako. 9 Makuhani wako na wavikwe haki, watakatifu wako na waimbe kwa furaha.” 10 Kwa ajili ya Daudi mtumishi wako, usimkatae mpakwa mafuta wako. 11 Bwana alimwapia Daudi kiapo, kiapo cha uhakika ambacho hatakitangua: “Nitamweka mmoja wa wazao wako mwenyewe katika kiti chako cha enzi, 12 kama wanao watashika Agano langu na sheria ninazowafundisha, ndipo wana wao watarithi kiti chako cha enzi milele na milele.” 13 Kwa maana Bwana ameichagua Sayuni, amepaonea shauku pawe maskani yake: 14 “Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele na milele; hapa ndipo nitakapoketi nikitawala, kwa sababu nimepaonea shauku: 15 Nitambariki kwa kumpa mahitaji tele: nitashibisha maskini wake kwa chakula. 16 Nitawavika makuhani wake wokovu, nao watakatifu wake watadumu wakiimba kwa furaha. 17 “Hapa nitamchipushia Daudi pembe, na kuweka taa kwa ajili ya masiya wangu. 18 Adui zake nitawavika aibu, bali taji kichwani pake itangʼaa sana.” Chapter 133Zaburi 133 1 Tazama jinsi ilivyo vyema na kupendeza wakati ndugu wanapoishi pamoja katika umoja! 2 Ni kama mafuta ya thamani yaliyomiminwa kichwani, yakitiririka kwenye ndevu, yakitiririka kwenye ndevu za Aroni, mpaka kwenye upindo wa mavazi yake. 3 Ni kama vile umande wa Hermoni unavyoanguka juu ya Mlima Sayuni. Kwa maana huko ndiko Bwana alikoamuru baraka yake, naam, hata uzima milele. Chapter 134Zaburi 134 1 Msifuni Bwana, ninyi nyote watumishi wa Bwana, ninyi mnaotumika usiku ndani ya nyumba ya Bwana. 2 Inueni mikono yenu katika pale patakatifu na kumsifu Bwana. 3 Naye Bwana, Muumba wa mbingu na dunia, awabariki kutoka Sayuni. Chapter 135Zaburi 135 1 Msifuni Bwana. Lisifuni jina la Bwana, msifuni, enyi watumishi wa Bwana, 2 ninyi ambao mnatumika ndani ya nyumba ya Bwana, katika nyua za nyumba ya Mungu wetu. 3 Msifuni Bwana, kwa kuwa Bwana ni mwema, liimbieni sifa jina lake, kwa maana hilo lapendeza. 4 Kwa maana Bwana amemchagua Yakobo kuwa wake mwenyewe, Israeli kuwa mali yake ya thamani. 5 Ninajua ya kuwa Bwana ni mkuu, kwamba Bwana wetu ni mkuu kuliko miungu yote. 6 Bwana hufanya lolote apendalo, mbinguni na duniani, katika bahari na vilindi vyake vyote. 7 Hufanya mawingu kupanda kutoka miisho ya dunia; hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua na huleta upepo kutoka ghala zake. 8 Alimuua mzaliwa wa kwanza wa Misri, mzaliwa wa kwanza wa wanadamu na wanyama. 9 Alipeleka ishara zake na maajabu katikati yako, ee Misri, dhidi ya Farao na watumishi wake wote. 10 Aliyapiga mataifa mengi, na akaua wafalme wenye nguvu: 11 Mfalme Sihoni na Waamori, Ogu mfalme wa Bashani na wafalme wote wa Kanaani: 12 akatoa nchi yao kuwa urithi, urithi kwa watu wake Israeli. 13 Ee Bwana, jina lako ladumu milele, kumbukumbu za fahari zako, Ee Bwana, kwa vizazi vyote. 14 Maana Bwana atawathibitisha watu wake, na kuwahurumia watumishi wake. 15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 16 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema, zina macho, lakini haziwezi kuona; 17 zina masikio, lakini haziwezi kusikia, wala hakuna pumzi katika vinywa vyao. 18 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo, vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia. 19 Ee nyumba ya Israeli, msifuni Bwana; ee nyumba ya Aroni, msifuni Bwana; 20 ee nyumba ya Lawi, msifuni Bwana; ninyi mnaomcha, msifuni Bwana. 21 Msifuni Bwana kutoka Sayuni, msifuni yeye aishiye Yerusalemu. Msifuni Bwana. Chapter 136Zaburi 136 1 Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema. Fadhili zake zadumu milele. 2 Mshukuruni Mungu wa miungu. Fadhili zake zadumu milele. 3 Mshukuruni Bwana wa mabwana: Fadhili zake zadumu milele. 4 Kwake yeye pekee atendaye maajabu makuu, Fadhili zake zadumu milele. 5 Ambaye kwa ufahamu wake aliziumba mbingu, Fadhili zake zadumu milele. 6 Ambaye aliitandaza dunia juu ya maji, Fadhili zake zadumu milele. 7 Ambaye aliumba mianga mikubwa, Fadhili zake zadumu milele. 8 Jua litawale mchana, Fadhili zake zadumu milele. 9 Mwezi na nyota vitawale usiku, Fadhili zake zadumu milele. 10 Kwake yeye aliyemuua mzaliwa wa kwanza wa Misri, Fadhili zake zadumu milele. 11 Na kuwatoa Israeli katikati yao, Fadhili zake zadumu milele. 12 Kwa mkono wenye nguvu ulionyooshwa, Fadhili zake zadumu milele. 13 Kwake yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu, Fadhili zake zadumu milele. 14 Na kuwapitisha Israeli katikati yake, Fadhili zake zadumu milele. 15 Lakini alimfagia Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu, Fadhili zake zadumu milele. 16 Kwake yeye aliyewaongoza watu wake katika jangwa, Fadhili zake zadumu milele. 17 Ambaye aliwapiga wafalme wenye nguvu, Fadhili zake zadumu milele. 18 Naye aliwaua wafalme wenye nguvu, Fadhili zake zadumu milele. 19 Sihoni mfalme wa Waamori, Fadhili zake zadumu milele. 20 Ogu mfalme wa Bashani, Fadhili zake zadumu milele. 21 Akatoa nchi yao kuwa urithi, Fadhili zake zadumu milele. 22 Urithi kwa Israeli mtumishi wake, Fadhili zake zadumu milele. 23 Aliyetukumbuka katika unyonge wetu, Fadhili zake zadumu milele. 24 Alituweka huru toka adui zetu, Fadhili zake zadumu milele. 25 Ambaye humpa chakula kila kiumbe. Fadhili zake zadumu milele. 26 Mshukuruni Mungu wa mbinguni, Fadhili zake zadumu milele. Chapter 137Zaburi 137 1 Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza tulipokumbuka Sayuni. 2 Kwenye miti ya huko tulitundika vinubi vyetu, 3 kwa maana huko hao waliotuteka walitaka tuwaimbie nyimbo, watesi wetu walidai nyimbo za furaha; walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja kati ya nyimbo za Sayuni!” 4 Tutaimbaje nyimbo za Bwana, tukiwa nchi ya kigeni? 5 Nikikusahau wewe, ee Yerusalemu, basi mkono wangu wa kuume na usahau ujuzi wake. 6 Ulimi wangu ushikamane na kaakaa la kinywa changu kama sitakukumbuka wewe, kama nisipokufikiri Yerusalemu kuwa furaha yangu kubwa. 7 Kumbuka, Ee Bwana, walichokifanya Waedomu, siku ile Yerusalemu ilipoanguka. Walisema, “Bomoa, Bomoa mpaka kwenye misingi yake!” 8 Ee binti Babeli, uliyehukumiwa kuangamizwa, heri yeye atakayekulipiza wewe kwa yale uliyotutenda sisi: 9 yeye ambaye atawakamata watoto wako wachanga na kuwaponda juu ya miamba. Chapter 138Zaburi 138 1 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako. 2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako juu ya vitu vyote. 3 Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari. 4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako. 5 Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana, kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. 6 Ingawa Bwana yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali. 7 Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa. 8 Bwana atatimiza kusudi lake kwangu, Ee Bwana, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako. Chapter 139Zaburi 139 1 Ee Bwana, umenichunguza na kunijua. 2 Unajua ninapoketi na ninapoinuka; unatambua mawazo yangu tokea mbali. 3 Unafahamu kutoka kwangu na kulala kwangu; unaelewa njia zangu zote. 4 Kabla neno halijafika katika ulimi wangu, wewe walijua kikamilifu, Ee Bwana. 5 Umenizunguka nyuma na mbele; umeweka mkono wako juu yangu. 6 Maarifa haya ni ya ajabu mno kwangu, ni ya juu sana kwangu kuyafikia. 7 Niende wapi nijiepushe na Roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? 8 Kama nikienda juu mbinguni, wewe uko huko; nikifanya vilindi kuwa kitanda changu, wewe uko huko. 9 Kama nikipanda juu ya mbawa za mapambazuko, kama nikikaa pande za mbali za bahari, 10 hata huko mkono wako utaniongoza, mkono wako wa kuume utanishika kwa uthabiti. 11 Kama nikisema, “Hakika giza litanificha na nuru inayonizunguka iwe usiku,” 12 hata giza halitakuwa giza kwako, usiku utangʼaa kama mchana, kwa kuwa giza ni kama nuru kwako. 13 Kwa maana wewe ndiwe uliyeumba utu wangu wa ndani; uliniunga pamoja tumboni mwa mama yangu. 14 Ninakusifu kwa sababu nimeumbwa kwa namna ya ajabu na ya kutisha; kazi zako ni za ajabu, ninajua hayo kikamilifu. 15 Umbile langu halikufichika kwako, nilipoumbwa mahali pa siri. Nilipoungwa pamoja kwa ustadi katika vilindi vya nchi, 16 macho yako yaliniona kabla mwili wangu haujakamilika. Siku zangu zote ulizonipangia ziliandikwa katika kitabu chako kabla haijakuwepo hata moja. 17 Tazama jinsi yalivyo ya thamani mawazo yako kwangu, Ee Mungu! Jinsi jumla yake ilivyo kubwa! 18 Kama ningezihesabu, zingekuwa nyingi kuliko mchanga. Niamkapo, bado niko pamoja nawe. 19 Laiti ungewachinja waovu, Ee Mungu! Ondokeni kwangu, ninyi wamwaga damu! 20 Wanazungumza juu yako wakiwa na kusudi baya, adui zako wanatumia vibaya jina lako. 21 Ee Bwana, je, nisiwachukie wanaokuchukia? Nisiwachukie sana wanaoinuka dhidi yako? 22 Sina kitu zaidi ya chuki dhidi yao, ninawahesabu ni adui zangu. 23 Ee Mungu, nichunguze, uujue moyo wangu, nijaribu na ujue mawazo yangu. 24 Uone kama kuna njia iletayo machukizo ndani yangu, uniongoze katika njia ya milele. Chapter 140Zaburi 140 1 Ee Bwana, niokoe, kutoka kwa watu waovu; nilinde na watu wenye jeuri, 2 ambao hupanga mipango mibaya mioyoni mwao, na kuchochea vita siku zote. 3 Wao hufanya ndimi zao kali kama za nyoka, sumu ya nyoka iko midomoni mwao. 4 Ee Bwana, niepushe na mikono ya waovu; nilinde na watu wenye jeuri wanaopanga kunikwaza miguu yangu. 5 Wenye kiburi wameficha mtego wa kuninasa, wametandaza kamba za wavu wao, wametega mitego kwenye njia yangu. 6 Ee Bwana, ninakuambia, “Wewe ni Mungu wangu.” Ee Bwana, usikie kilio changu na kunihurumia. 7 Ee Bwana Mwenyezi, Mwokozi wangu mwenye nguvu, unikingaye kichwa changu siku ya vita: 8 Ee Bwana, usiwape waovu matakwa yao, usiache mipango yao ikafanikiwa, wasije wakajisifu. 9 Vichwa vya wanaonizunguka vifunikwe na shida zinazosababishwa na midomo yao. 10 Makaa ya mawe ya moto na yawaangukie! Na watupwe motoni, katika mashimo ya matope, wasiinuke tena kamwe. 11 Wasingiziaji wasifanikiwe katika nchi; maafa na yawawinde watu wenye jeuri. 12 Najua kwamba Bwana huwapatia maskini haki, na kuitegemeza njia ya mhitaji. 13 Hakika wenye haki watalisifu jina lako, na waadilifu wataishi mbele zako. Chapter 141Zaburi 141 1 Ee Bwana, ninakuita wewe, uje kwangu hima. Sikia sauti yangu ninapokuita. 2 Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba; kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni. 3 Ee Bwana, weka mlinzi kinywani mwangu, weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu. 4 Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya, nisije nikashiriki katika matendo maovu pamoja na watu watendao mabaya, wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa. 5 Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma; na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu. Kichwa changu hakitalikataa. Hata hivyo, maombi yangu daima ni kinyume cha watenda mabaya, 6 watawala wao watatupwa chini kutoka kwenye majabali, waovu watajifunza kwamba maneno yangu yalikuwa kweli. 7 Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi, ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.” 8 Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mwenyezi, ndani yako nimekimbilia, usiniache nife. 9 Niepushe na mitego waliyonitegea, kutokana na mitego iliyotegwa na watenda mabaya. 10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe, wakati mimi ninapita salama. Chapter 142Zaburi 142 1 Namlilia Bwana kwa sauti, nainua sauti yangu kwa Bwana anihurumie. 2 Namimina malalamiko yangu mbele zake, mbele zake naeleza shida zangu. 3 Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu, wewe ndiwe unajua njia zangu. Katika njia ninayopita watu wameniwekea mtego. 4 Tazama kuume kwangu na uone, hakuna hata mmoja anayejihusisha nami. Sina kimbilio, hakuna anayejali maisha yangu. 5 Ee Bwana, nakulilia wewe, nasema, “Wewe ni kimbilio langu, fungu langu katika nchi ya walio hai.” 6 Sikiliza kilio changu, kwa sababu mimi ni mhitaji sana; niokoe na wale wanaonifuatilia, kwa kuwa wamenizidi nguvu. 7 Nifungue kutoka kifungo changu, ili niweze kulisifu jina lako. Ndipo wenye haki watanizunguka, kwa sababu ya wema wako kwangu. Chapter 143Zaburi 143 1 Ee Bwana, sikia sala yangu, sikiliza kilio changu unihurumie; katika uaminifu na haki yako njoo unisaidie. 2 Usimhukumu mtumishi wako, kwa kuwa hakuna mtu anayeishi aliye mwenye haki mbele zako. 3 Adui hunifuatilia, hunipondaponda chini; hunifanya niishi gizani kama wale waliokufa zamani. 4 Kwa hiyo roho yangu inazimia ndani yangu, moyo wangu ndani yangu unakata tamaa. 5 Nakumbuka siku za zamani; natafakari juu ya kazi zako zote, naangalia juu ya kazi ambazo mikono yako imezifanya. 6 Nanyoosha mikono yangu kwako, nafsi yangu inakuonea kiu kama ardhi kame. 7 Ee Bwana, unijibu haraka, roho yangu inazimia. Usinifiche uso wako, ama sivyo nitafanana na wale washukao shimoni. 8 Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma, kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako. Nionyeshe njia nitakayoiendea, kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu. 9 Ee Bwana, uniokoe na adui zangu, kwa kuwa nimejificha kwako. 10 Nifundishe kufanya mapenzi yako, kwa maana wewe ndiwe Mungu wangu, Roho wako mwema na aniongoze katika nchi tambarare. 11 Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, hifadhi maisha yangu, kwa haki yako nitoe katika taabu. 12 Kwa upendo wako usiokoma, nyamazisha adui zangu; waangamize watesi wangu wote, kwa kuwa mimi ni mtumishi wako. Chapter 144Zaburi 144 1 Sifa ni kwa Bwana Mwamba wangu, aifundishaye mikono yangu vita, na vidole vyangu kupigana. 2 Yeye ni Mungu wangu wa upendo na boma langu, ngome yangu na mwokozi wangu, ngao yangu ninayemkimbilia, ambaye huwatiisha mataifa chini yangu. 3 Ee Bwana, mwanadamu ni nini hata umjali, Binadamu ni nini hata umfikirie? 4 Mwanadamu ni kama pumzi, siku zake ni kama kivuli kinachopita. 5 Ee Bwana, pasua mbingu zako, ushuke, gusa milima ili itoe moshi. 6 Peleka umeme uwatawanye adui, lenga mishale yako uwashinde. 7 Nyoosha mkono wako kutoka juu, nikomboe na kuniokoa kutoka maji makuu, kutoka mikononi mwa wageni 8 ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu. 9 Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya, kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia, 10 kwa Yule awapaye wafalme ushindi, ambaye humwokoa Daudi, mtumishi wake kutokana na upanga hatari. 11 Nikomboe na uniokoe kutoka mikononi mwa wageni ambao vinywa vyao vimejaa uongo, na mikono yao ya kuume ni midanganyifu. 12 Kisha wana wetu wakati wa ujana wao watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri, binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa kurembesha jumba la kifalme. 13 Ghala zetu zitajazwa aina zote za mahitaji. Kondoo zetu watazaa kwa maelfu, kwa makumi ya maelfu katika mashamba yetu; 14 maksai wetu watakokota mizigo mizito. Hakutakuwa na kubomoka kuta, hakuna kuchukuliwa mateka, wala kilio cha taabu katika barabara zetu. 15 Heri watu ambao hili ni kweli; heri wale ambao Bwana ni Mungu wao. Chapter 145Zaburi 145 1 Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme, nitalisifu jina lako milele na milele. 2 Kila siku nitakusifu na kulitukuza jina lako milele na milele. 3 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana, ukuu wake haupimiki. 4 Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine, watasimulia matendo yako makuu. 5 Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako, nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu. 6 Watasimulia uwezo wa kazi zako za kutisha, nami nitatangaza matendo yako makuu. 7 Wataadhimisha wema wako mwingi, na wataimba kwa shangwe juu ya haki yako. 8 Bwana ni mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo. 9 Bwana ni mwema kwa wote, ana huruma kwa vyote alivyovifanya. 10 Ee Bwana, vyote ulivyovifanya vitakusifu, watakatifu wako watakutukuza. 11 Watasimulia utukufu wa ufalme wako na kusema juu ya ukuu wako, 12 ili watu wote wajue matendo yako makuu na utukufu wa fahari ya ufalme wako. 13 Ufalme wako ni ufalme wa milele, mamlaka yako hudumu vizazi vyote. Bwana ni mwaminifu kwa ahadi zake zote na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya. 14 Bwana huwategemeza wote waangukao, na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao. 15 Macho yao wote yanakutazama wewe, nawe huwapa chakula chao wakati wake. 16 Waufumbua mkono wako, watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai. 17 Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya. 18 Bwana yu karibu na wote wamwitao, karibu na wote wamwitao kwa uaminifu. 19 Huwatimizia wamchao matakwa yao, husikia kilio chao na kuwaokoa. 20 Bwana huwalinda wote wampendao, bali waovu wote atawaangamiza. 21 Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana. Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu milele na milele. Chapter 146Zaburi 146 1 Msifuni Bwana! Ee nafsi yangu, umsifu Bwana, 2 Nitamsifu Bwana maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu sifa wakati wote niishipo. 3 Usiweke tumaini lako kwa wakuu, kwa wanadamu ambao hufa, ambao hawawezi kuokoa. 4 Roho yao itokapo hurudi mavumbini, siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma. 5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, ambaye tumaini lake ni katika Bwana, Mungu wake, 6 Muumba wa mbingu na nchi, na bahari na vyote vilivyomo ndani yake: Bwana anayedumu kuwa mwaminifu milele na milele. 7 Naye huwapatia haki walioonewa na kuwapa wenye njaa chakula. Bwana huwaweka wafungwa huru, 8 Bwana huwafumbua vipofu macho, Bwana huwainua waliolemewa na mizigo yao, Bwana huwapenda wenye haki. 9 Bwana huwalinda wageni na kuwategemeza yatima na wajane, lakini hupinga njia za waovu. 10 Bwana atamiliki milele, Mungu wako, ee Sayuni, kwa vizazi vyote. Msifuni Bwana. Chapter 147Zaburi 147 1 Msifuni Bwana. Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa, jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye! 2 Bwana hujenga Yerusalemu, huwakusanya Israeli walio uhamishoni. 3 Anawaponya waliovunjika mioyo na kuvifunga vidonda vyao. 4 Huzihesabu nyota na huipa kila moja jina lake. 5 Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi, ufahamu wake hauna kikomo. 6 Bwana huwahifadhi wanyenyekevu lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini. 7 Mwimbieni Bwana kwa shukrani, mpigieni Mungu wetu kinubi. 8 Yeye huzifunika anga kwa mawingu, huinyeshea ardhi mvua, na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima. 9 Huwapa chakula mifugo na pia makinda ya kunguru yanapolia. 10 Furaha yake haipo katika nguvu za farasi, wala furaha yake kwenye miguu ya mwanadamu. 11 Bwana hupendezwa na wale wamchao, wale wanaoweka tumaini lao katika upendo wake usiokoma. 12 Mtukuze Bwana, ee Yerusalemu, msifu Mungu wako, ee Sayuni, 13 kwa maana huimarisha makomeo ya malango yako na huwabariki watu wako walio ndani yako. 14 Huwapa amani mipakani mwenu na kukushibisha kwa ngano safi kabisa. 15 Hutuma amri yake duniani, neno lake hukimbia kasi. 16 Anatandaza theluji kama sufu na kutawanya umande kama majivu. 17 Huvurumisha mvua yake ya mawe kama changarawe. Ni nani awezaye kustahimili ukali wa baridi yake? 18 Hutuma neno lake na kuviyeyusha, huvumisha upepo wake, nayo maji hutiririka. 19 Amemfunulia Yakobo neno lake, sheria zake na maagizo yake kwa Israeli. 20 Hajafanya hivyo kwa taifa lingine lolote, hawazijui sheria zake. Msifuni Bwana. Chapter 148Zaburi 148 1 Msifuni Bwana. Msifuni Bwana kutoka mbinguni, msifuni juu vileleni. 2 Msifuni, enyi malaika wake wote, msifuni yeye, enyi jeshi lake lote la mbinguni. 3 Msifuni yeye, enyi jua na mwezi, msifuni yeye, enyi nyota zote zingʼaazo. 4 Msifuni yeye, enyi mbingu zilizo juu sana, na ninyi maji juu ya anga. 5 Vilisifu jina la Bwana kwa maana aliamuru navyo vikaumbwa. 6 Aliviweka mahali pake milele na milele, alitoa amri ambayo haibadiliki milele. 7 Mtukuzeni Bwana kutoka duniani, ninyi viumbe vikubwa vya baharini na vilindi vyote vya bahari, 8 umeme wa radi na mvua ya mawe, theluji na mawingu, pepo za dhoruba zinazofanya amri zake, 9 ninyi milima na vilima vyote, miti ya matunda na mierezi yote, 10 wanyama wa mwituni na mifugo yote, viumbe vidogo na ndege warukao, 11 wafalme wa dunia na mataifa yote, ninyi wakuu na watawala wote wa dunia, 12 wanaume vijana na wanawali, wazee na watoto. 13 Wote na walisifu jina la Bwana, kwa maana jina lake pekee limetukuka, utukufu wake uko juu ya nchi na mbingu. 14 Amewainulia watu wake pembe, sifa ya watakatifu wake wote, ya Israeli, watu walio karibu na moyo wake. Msifuni Bwana. Chapter 149Zaburi 149 1 Msifuni Bwana. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, sifa zake katika kusanyiko la watakatifu. 2 Israeli na washangilie katika Muumba wao, watu wa Sayuni na wafurahi katika Mfalme wao. 3 Na walisifu jina lake kwa kucheza na wampigie muziki kwa matari na kinubi. 4 Kwa maana Bwana anapendezwa na watu wake, anawavika wanyenyekevu taji ya wokovu. 5 Watakatifu washangilie katika heshima hii, na waimbe kwa shangwe vitandani mwao. 6 Sifa za Mungu na ziwe vinywani mwao na upanga ukatao kuwili mikononi mwao, 7 ili walipize mataifa kisasi na adhabu juu ya mataifa, 8 wawafunge wafalme wao kwa minyororo, wakuu wao kwa pingu za chuma, 9 ili kuwafanyia hukumu iliyoandikwa dhidi yao. Huu ndio utukufu wa watakatifu wake wote. Msifuni Bwana. Chapter 150Zaburi 150 1 Msifuni Bwana. Msifuni Mungu katika patakatifu pake, msifuni katika mbingu zake kuu. 2 Msifuni kwa matendo yake makuu, msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake. 3 Msifuni kwa mvumo wa tarumbeta, msifuni kwa kinubi na zeze, 4 msifuni kwa matari na kucheza, msifuni kwa kinanda cha nyuzi na filimbi, 5 msifuni kwa matoazi yaliayo, msifuni kwa matoazi yavumayo sana. 6 Kila chenye pumzi na kimsifu Bwana. Msifuni Bwana!