; TITLE: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version ; ABBREVIATION: KCV ; HAS ITALICS ; HAS FOOTNOTES ; HAS REDLETTER $$ OBA 1:1 ¶ Maono ya Obadia. Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi kuhusu Edomu: Tumesikia ujumbe kutoka kwa Bwana: Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema, “Inukeni, twendeni tukapigane vita dhidi yake.” $$ OBA 1:2 ¶ “Angalieni, nitawafanya wadogo miongoni mwa mataifa, mtadharauliwa kabisa. $$ OBA 1:3 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, wewe unayeishi katika majabali ya miamba na kufanya makao yako juu, wewe unayejiambia mwenyewe, ‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’ $$ OBA 1:4 Ingawa unapaa juu kama tai na kufanya kiota chako kati ya nyota, nitakushusha chini kutoka huko,” asema Bwana. $$ OBA 1:5 “Ikiwa wevi wangekuja kwako, ikiwa wanyangʼanyi wangekujia usiku: Lo! Tazama ni maafa kiasi gani yangekuwa yanakungojea: je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji? Kama wachuma zabibu wangekuja kwako, je, wasingebakiza zabibu chache? $$ OBA 1:6 Lakini tazama jinsi Esau atakavyotekwa, jinsi hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara! $$ OBA 1:7 Wote ulioungana nao watakufukuza hadi mpakani, rafiki zako watakudanganya na kukushinda, wale wanaokula mkate wako watakutegea mtego, lakini hutaweza kuugundua. $$ OBA 1:8 “Katika siku hiyo,” asema Bwana, “je, sitaangamiza watu wenye hekima wa Edomu, watu wenye ufahamu katika milima ya Esau? $$ OBA 1:9 Ee Temani, mashujaa wako watatiwa hofu, kila mmoja katika milima ya Esau ataangushwa chini kwa kuchinjwa. $$ OBA 1:10 Kwa sababu ya jeuri uliyofanya dhidi ya ndugu yako Yakobo, aibu itakufunika; utaangamizwa milele. $$ OBA 1:11 Siku ile ulisimama mbali ukiangalia wakati wageni walipojichukulia utajiri wake na watu wa nchi nyingine walipoingia malango yake wakipiga kura kwa ajili ya Yerusalemu, ulikuwa kama mmoja wao. $$ OBA 1:12 Usingemdharau ndugu yako katika siku ya msiba wake, wala kufurahia juu ya watu wa Yuda katika siku ya maangamizi yao, wala kujigamba sana katika siku ya taabu yao. $$ OBA 1:13 Usingeingia katika malango ya watu wangu katika siku ya maafa yao, wala kuwadharau katika janga lao katika siku ya maafa yao, wala kunyangʼanya mali zao katika siku ya maafa yao. $$ OBA 1:14 Usingengoja kwenye njia panda na kuwaua wakimbizi wao, wala kuwatoa watu wake waliosalia katika siku ya shida yao. $$ OBA 1:15 “Siku ya Bwana iko karibu kwa mataifa yote. Kama ulivyofanya, nawe utafanyiwa vivyo hivyo, matendo yako yatakurudia juu ya kichwa chako. $$ OBA 1:16 Kama vile ulivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu, vivyo hivyo mataifa yote watakunywa mfululizo, watakunywa na kunywa, nao watatoweka kana kwamba hawajawahi kuwepo. $$ OBA 1:17 Lakini katika Mlima Sayuni kutakuwepo na wale watakaookoka; nao utakuwa mtakatifu, nayo nyumba ya Yakobo itamiliki urithi wake. $$ OBA 1:18 Nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yosefu itakuwa mwali wa moto; nayo nyumba ya Esau itakuwa bua kavu, nao wataiwasha moto na kuiteketeza. Hakutakuwa na watakaosalimika kutoka nyumba ya Esau.” Bwana amesema. $$ OBA 1:19 Watu kutoka nchi ya Negebu wataikalia milima ya Esau, na watu kutoka miteremko ya vilima watamiliki nchi ya Wafilisti. Watayakalia mashamba ya Efraimu na Samaria, naye Benyamini atamiliki Gileadi. $$ OBA 1:20 Kundi la Waisraeli walioko uhamishoni Kanaani watarudi na kumiliki nchi mpaka Sarepta. Walioko uhamishoni Sefaradi kutoka Yerusalemu watamiliki miji ya Negebu. $$ OBA 1:21 Waokoaji watakwea juu ya Mlima Sayuni kutawala milima ya Esau. Nao ufalme utakuwa wa Bwana.