; TITLE: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version ; ABBREVIATION: KCV ; HAS ITALICS ; HAS FOOTNOTES ; HAS REDLETTER $$ TI2 1:1 ¶ Paulo mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima uliomo ndani ya Kristo Yesu. $$ TI2 1:2 ¶ Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa: Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba, na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. $$ TI2 1:3 ¶ Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi, kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. $$ TI2 1:4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha. $$ TI2 1:5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike na ambayo mimi ninasadiki sasa wewe pia unayo. $$ TI2 1:6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu, iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. $$ TI2 1:7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi. $$ TI2 1:8 ¶ Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, $$ TI2 1:9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele. $$ TI2 1:10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili. $$ TI2 1:11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. $$ TI2 1:12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile. $$ TI2 1:13 ¶ Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima yale uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Kristo Yesu. $$ TI2 1:14 Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu. $$ TI2 1:15 ¶ Unajua ya kuwa watu wote katika Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene. $$ TI2 1:16 ¶ Bwana akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara wala hakuionea aibu minyororo yangu. $$ TI2 1:17 Badala yake, alipokuwa Rumi, alinitafuta kwa bidii mpaka akanipata. $$ TI2 1:18 Bwana na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso. $$ TI2 2:1 ¶ Basi, wewe mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Kristo Yesu. $$ TI2 2:2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile. $$ TI2 2:3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu. $$ TI2 2:4 Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari. $$ TI2 2:5 Vivyo hivyo, yeye ashindanaye katika michezo hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano. $$ TI2 2:6 Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno. $$ TI2 2:7 Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Bwana atakupa ufahamu katika mambo hayo yote. $$ TI2 2:8 ¶ Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, $$ TI2 2:9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. $$ TI2 2:10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. $$ TI2 2:11 ¶ Hili ni neno la kuaminiwa: Kwa maana kama tumekufa pamoja naye, tutaishi pia pamoja naye. $$ TI2 2:12 Kama tukistahimili, pia tutatawala pamoja naye. Kama tukimkana yeye, naye atatukana sisi. $$ TI2 2:13 Kama tusipoamini, yeye hudumu kuwa mwaminifu, kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. $$ TI2 2:14 ¶ Endelea kuwakumbusha mambo haya ukiwaonya mbele za Bwana waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia. $$ TI2 2:15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. $$ TI2 2:16 Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu. $$ TI2 2:17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto $$ TI2 2:18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako, nao huharibu imani ya baadhi ya watu. $$ TI2 2:19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Bwana, na auache uovu.” $$ TI2 2:20 ¶ Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo; vingine kwa matumizi maalum, na vingine kwa matumizi ya kawaida. $$ TI2 2:21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema. $$ TI2 2:22 ¶ Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. $$ TI2 2:23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. $$ TI2 2:24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. $$ TI2 2:25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, $$ TI2 2:26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake. $$ TI2 3:1 ¶ Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. $$ TI2 3:2 Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, $$ TI2 3:3 wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, $$ TI2 3:4 wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu: $$ TI2 3:5 wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo. $$ TI2 3:6 ¶ Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. $$ TI2 3:7 Wakijifunza siku zote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli. $$ TI2 3:8 Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Mose, vivyo hivyo watu hawa hupingana na ile kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani. $$ TI2 3:9 Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama ulivyokuwa dhahiri upumbavu wa hao watu wawili. $$ TI2 3:10 ¶ Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu, $$ TI2 3:11 mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana aliniokoa katika hayo yote. $$ TI2 3:12 Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa. $$ TI2 3:13 Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. $$ TI2 3:14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, $$ TI2 3:15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. $$ TI2 3:16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, $$ TI2 3:17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema. $$ TI2 4:1 ¶ Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: $$ TI2 4:2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. $$ TI2 4:3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia. $$ TI2 4:4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo. $$ TI2 4:5 Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako. $$ TI2 4:6 ¶ Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia. $$ TI2 4:7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda. $$ TI2 4:8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake. $$ TI2 4:9 ¶ Jitahidi kuja kwangu upesi $$ TI2 4:10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na amekwenda Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia na Tito amekwenda Dalmatia. $$ TI2 4:11 Ni Luka peke yake aliye hapa pamoja nami. Mtafute Marko uje naye kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu. $$ TI2 4:12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso. $$ TI2 4:13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi. $$ TI2 4:14 ¶ Aleksanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda. $$ TI2 4:15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu. $$ TI2 4:16 ¶ Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. $$ TI2 4:17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba. $$ TI2 4:18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen. $$ TI2 4:19 ¶ Wasalimu Prisila na Akila, na wote wa nyumbani kwa Onesiforo. $$ TI2 4:20 Erasto alibaki Korintho. Nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa. $$ TI2 4:21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi. Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote. $$ TI2 4:22 ¶ Bwana awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi. Amen.