Yohana
1
Neno Alifanyika Mwili
Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.
Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini. Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.
10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. 11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.
14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
15 Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ ” 16 Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. 17 Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Mose, lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo. 18 Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.
Ushuhuda Wa Yohana Mbatizaji
(Mathayo 3:1-12; Marko 1:1-8; Luka 3:1-18)
19 Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati Wayahudi walipowatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?” 20 Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha akasema, “Mimi si Kristo.”* Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
21 Wakamuuliza, “Wewe ni nani basi? Je, wewe ni Eliya?”
Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.”
“Je, wewe ni yule Nabii?”
Akajibu, “Hapana.”
22 Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”
23 Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Bwana.’ ”
24 Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo 25 wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?”
26 Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji, Hapa tafsiri zingine zinasema ndani ya maji. lakini katikati yenu yupo mtu msiyemjua. 27 Yeye ajaye baada yangu, sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”
28 Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ngʼambo ya Mto Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza.
Yesu Mwana-Kondoo Wa Mungu
29 Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu! 30 Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ 31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”
32 Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. 33 Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ 34 Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
Wanafunzi Wa Kwanza Wa Yesu
35 Siku iliyofuata, Yohana alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili. 36 Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”
37 Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yohana akisema haya, wakamfuata Yesu. 38 Yesu akageuka, akawaona wakimfuata akawauliza, “Mnataka nini?”
Wakamwambia, “Rabi,” (maana yake Mwalimu), “Unaishi wapi?”
39 Yesu akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!”
Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.
40 Andrea nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yohana aliyokuwa amesema, naye ndiye alimfuata Yesu. 41 Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masiya” (yaani, Kristo). 42 Naye akamleta kwa Yesu.
Yesu akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro Petro kwa Kiyunani au Kefa kwa Kiaramu; maana yake ni Kipande cha mwamba.).
Yesu Awaita Filipo Na Nathanaeli
43 Siku iliyofuata Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44 Basi Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji alikotoka Andrea na Petro. 45 Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Mose aliandika habari zake katika Sheria na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani, Yesu wa Nazareti, mwana wa Yosefu.”
46 Nathanaeli akauliza, “Nazareti! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47 Yesu alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.”
48 Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?”
Yesu akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”
49 Nathanaeli akamwambia, “Rabi, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
50 Yesu akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu zaidi kuliko hilo.” 51 Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

*1:20 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.

1:26 Hapa tafsiri zingine zinasema ndani ya maji.

1:42 Petro kwa Kiyunani au Kefa kwa Kiaramu; maana yake ni Kipande cha mwamba.