Yona
1
Yona Anamkimbia Bwana
Neno la Bwana lilimjia Yona mwana wa Amitai: “Nenda katika mji mkubwa wa Ninawi ukahubiri juu yake, kwa sababu uovu wake umekuja juu mbele zangu.”
Lakini Yona alimkimbia Bwana na kuelekea Tarshishi. Alishuka mpaka Yafa, ambapo alikuta meli iliyokuwa imepangwa kuelekea bandari ile. Baada ya kulipa nauli, akapanda melini na kuelekea Tarshishi ili kumkimbia Bwana. Ndipo Bwana akatuma upepo mkali baharini, nayo dhoruba kali sana ikavuma hata meli ikawa hatarini kuvunjika. Mabaharia wote waliogopa na kila mmoja akamlilia mungu wake mwenyewe. Nao wakatupa mizigo baharini ili meli ipungue uzito.
Lakini Yona alikuwa ameteremkia chumba cha ndani ya meli, mahali ambapo alilala na kupatwa na usingizi mzito. Nahodha akamwendea na kusema, “Wewe unawezaje kulala? Amka ukamwite mungu wako! Huenda akatuangalia, tusiangamie.”
Kisha mabaharia wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tupige kura tumtafute anayehusika na maafa haya.” Wakapiga kura, kura ikamwangukia Yona.
Kwa hiyo walimuuliza, “Tuambie, ni nani anayehusika kwa kutuletea tatizo hili lote? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? Nchi yako ni ipi? Wewe ni kutoka taifa lipi?”
Akajibu, “Mimi ni Mwebrania, nami namwabudu Bwana, Mungu wa Mbinguni, aliyeumba bahari na nchi kavu.”
10 Hili liliwaogopesha nao wakamuuliza,
“Umefanya nini?” (Walijua alikuwa anamkimbia Bwana, kwa sababu alishawaambia hivyo.)
11 Bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Kwa hiyo walimuuliza, “Tukutendee nini ili kufanya bahari itulie kwa ajili yetu?”
12 Akawajibu, “Niinueni mnitupe baharini, nayo itakuwa shwari. Ninajua mawimbi haya makubwa yamewatokea kwa ajili ya kosa langu.”
13 Badala yake, wale watu walijitahidi kupiga makasia wawezavyo ili wapate kurudi pwani. Lakini hawakuweza, kwa kuwa bahari ilizidi kuchafuka kuliko mwanzo. 14 Ndipo wakamlilia Bwana, “Ee Bwana, tafadhali usituue kwa kuondoa uhai wa mtu huyu. Usituhesabie hatia kwa kuutoa uhai wa mtu asiyekuwa na hatia, kwa kuwa wewe, Ee Bwana, umefanya kama ilivyokupendeza.” 15 Kisha walimchukua Yona, wakamtupa baharini nayo bahari iliyokuwa imechafuka ikatulia. 16 Katika jambo hili watu wakamwogopa Bwana sana, wakamtolea Bwana dhabihu na kumwekea nadhiri.
17 Lakini Bwana akamwandaa nyangumi* Yaani samaki mkubwa sana. kummeza Yona, naye Yona alikuwa ndani ya tumbo la nyangumi kwa siku tatu, usiku na mchana.

*1:17 Yaani samaki mkubwa sana.