Hesabu
1
Watu Wahesabiwa Kwa Mara Ya Kwanza
Bwana alisema na Mose katika Jangwa la Sinai, katika Hema la Kukutania, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, katika mwaka wa pili baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri. Akamwambia, “Hesabu watu wa jumuiya yote ya Waisraeli kwa kufuata koo zao na jamaa zao, ukiorodhesha kila mwanaume kwa jina lake, mmoja mmoja. Wewe na Aroni mtawahesabu kwa migawanyo yao wanaume wote katika Israeli wenye miaka ishirini na kuendelea ambao wanaweza kutumika katika jeshi. Mwanaume mmoja kutoka kila kabila, kila aliye kiongozi wa jamaa yake, atawasaidia. Haya ndiyo majina ya wanaume watakaowasaidia:
 
“kutoka Reubeni, ni Elisuri mwana wa Shedeuri;
kutoka Simeoni, ni Shelumieli mwana wa Surishadai;
kutoka Yuda, ni Nashoni mwana wa Aminadabu;
kutoka Isakari, ni Nethaneli mwana wa Suari;
kutoka Zabuloni, ni Eliabu mwana wa Heloni;
10 kutoka wana wa Yosefu:
kutoka Efraimu, ni Elishama mwana wa Amihudi;
kutoka Manase, ni Gamalieli mwana wa Pedasuri;
11 kutoka Benyamini, ni Abidani mwana wa Gideoni;
12 kutoka Dani, ni Ahiezeri mwana wa Amishadai;
13 kutoka Asheri, ni Pagieli mwana wa Okrani;
14 kutoka Gadi, ni Eliasafu mwana wa Deueli;
15 kutoka Naftali, ni Ahira mwana wa Enani.”
 
16 Hawa walikuwa wanaume walioteuliwa kutoka jumuiya, viongozi wa makabila ya baba zao. Walikuwa wakuu wa koo za Israeli.
17 Mose na Aroni wakawachukua wanaume hao waliokuwa wamepewa majina yao, 18 wakaita jumuiya yote pamoja katika siku ya kwanza ya mwezi wa pili. Watu wakaonyesha nasaba zao kwa koo zao na jamaa zao, nao wanaume waliokuwa na miaka ishirini au zaidi waliorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja, 19 kama Bwana alivyomwagiza Mose. Hivyo aliwahesabu katika Jangwa la Sinai:
 
20 Kutoka wazao wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa kiume wa Israeli:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 21 Idadi kutoka kabila la Reubeni ilikuwa watu 46,500.
 
22 Kutoka wazao wa Simeoni:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi walihesabiwa na kuorodheshwa kwa majina, mmoja mmoja, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 23 Idadi kutoka kabila la Simeoni walikuwa watu 59,300.
 
24 Kutoka wazao wa Gadi:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 25 Idadi kutoka kabila la Gadi walikuwa watu 45,650.
 
26 Kutoka wazao wa Yuda:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 27 Idadi kutoka kabila la Yuda walikuwa watu 74,600.
 
28 Kutoka wazao wa Isakari:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 29 Idadi kutoka kabila la Isakari walikuwa watu 54,400.
 
30 Kutoka wazao wa Zabuloni:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 31 Idadi kutoka kabila la Zabuloni walikuwa watu 57,400.
 
32 Kutoka wana wa Yosefu:
Kutoka wazao wa Efraimu:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 33 Idadi kutoka kabila la Efraimu walikuwa watu 40,500.
34 Kutoka wazao wa Manase:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 35 Idadi kutoka kabila la Manase walikuwa watu 32,200.
 
36 Kutoka wazao wa Benyamini:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 37 Idadi kutoka kabila la Benyamini walikuwa watu 35,400.
 
38 Kutoka wazao wa Dani:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 39 Idadi kutoka kabila la Dani walikuwa watu 62,700.
 
40 Kutoka wazao wa Asheri:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 41 Idadi kutoka kabila la Asheri walikuwa watu 41,500.
 
42 Kutoka wazao wa Naftali:
Wanaume wote waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi waliorodheshwa kwa majina, kufuatana na kumbukumbu za koo zao na jamaa zao. 43 Idadi kutoka kabila la Naftali walikuwa watu 53,400.
 
44 Hawa walikuwa wanaume waliohesabiwa na Mose, Aroni na viongozi kumi na wawili wa Israeli, kila mmoja akiwakilisha jamaa yake. 45 Wanaume wote Waisraeli waliokuwa na miaka ishirini au zaidi ambao waliweza kutumika katika jeshi la Israeli walihesabiwa kufuatana na jamaa zao. 46 Jumla ya hesabu yao ilikuwa watu 603,550.
47 Hata hivyo, jamaa ya kabila la Lawi hawakuhesabiwa pamoja na wengine. 48  Bwana alikuwa amemwambia Mose: 49 “Kamwe usihesabu kabila la Lawi wala kuwaweka pamoja katika hesabu ya Waisraeli wengine. 50 Badala yake, waweke Walawi kuwa viongozi wa Maskani ya Ushuhuda, juu ya samani zake na kila kitu kilichomo ndani yake. Wao watabeba Maskani na samani zake zote; wataitunza na kupiga kambi kuizunguka. 51 Wakati wowote Maskani inapohamishwa, Walawi wataifungua, na wakati wowote maskani inapotakiwa kusimamishwa, Walawi watafanya kazi hiyo. Mtu yeyote mwingine ambaye atasogea karibu nayo atauawa. 52 Waisraeli watapiga mahema yao kwa makundi makundi, kila mwanaume katika kambi yake mwenyewe chini ya bendera yake. 53 Hata hivyo, Walawi watapiga mahema yao kuzunguka Maskani ya Ushuhuda ili ghadhabu isiipate jumuiya ya Waisraeli. Walawi watawajibika kwa utunzaji wa Maskani ya Ushuhuda.”
54 Waisraeli walifanya yote haya sawasawa kama Bwana alivyomwamuru Mose.