Zaburi. 2. Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya, na kabila za watu kula njama bure? Wafalme wa dunia wanajipanga na watawala wanajikusanya pamoja dhidi ya Bwana na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake. Wanasema, “Tuvunje minyororo yao na kuvitupilia mbali vifungo vyao.” Yeye atawalaye mbinguni hucheka, Bwana huwadharau. Kisha huwakemea katika hasira yake na kuwaogopesha katika ghadhabu yake, akisema, “Nimemtawaza Mfalme wangu juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.” Nitatangaza amri ya Bwana: Yeye aliniambia, “Wewe ni Mwanangu, leo mimi nimekuzaa. Niombe, nami nitayafanya mataifa kuwa urithi wako, miisho ya dunia kuwa milki yako. Utawatawala kwa fimbo ya chuma na kuwavunjavunja kama chombo cha mfinyanzi.” Kwa hiyo, ninyi wafalme, kuweni na hekima; mwonyeke, enyi watawala wa dunia. Mtumikieni Bwana kwa hofu na mshangilie kwa kutetemeka. Mbusu Mwana, asije akakasirika nawe ukaangamizwa katika njia yako, kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula. Heri wote wanaomkimbilia.