Zaburi. 25. Zaburi ya Daudi. Kwako wewe, Ee Bwana, nainua nafsi yangu, ni wewe ninayekutumainia, Ee Mungu wangu. Usiniache niaibike, wala usiache adui zangu wakanishinda. Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea atakayeaibishwa, bali wataaibishwa wafanyao hila bila sababu. Nionyeshe njia zako, Ee Bwana, nifundishe mapito yako, niongoze katika kweli yako na kunifundisha, kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu, nalo tumaini langu liko kwako wakati wote. Kumbuka, Ee Bwana, rehema zako kuu na upendo, kwa maana zimekuwepo tangu zamani. Usizikumbuke dhambi za ujana wangu wala njia zangu za uasi, sawasawa na upendo wako unikumbuke, kwa maana wewe ni mwema, Ee Bwana. Bwana ni mwema na mwenye adili, kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake. Huwaongoza wanyenyekevu katika haki, naye huwafundisha njia yake. Njia zote za Bwana ni za upendo na uaminifu kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake. Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, unisamehe uovu wangu, ijapokuwa ni mwingi. Ni nani basi, mtu yule anayemcha Bwana? Atamfundisha katika njia atakayoichagua kwa ajili yake. Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake, nao wazao wake watairithi nchi. Siri ya Bwana iko kwa wale wamchao, yeye huwajulisha agano lake. Macho yangu humwelekea Bwana daima, kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa miguu yangu kutoka mtego. Nigeukie na unihurumie, kwa maana mimi ni mpweke na mwenye kuteseka. Shida za moyo wangu zimeongezeka, niokoe katika dhiki yangu. Uangalie mateso na shida zangu na uniondolee dhambi zangu zote. Tazama adui zangu walivyo wengi, pia uone jinsi wanavyonichukia vikali! Uyalinde maisha yangu na uniokoe, usiniache niaibike, kwa maana nimekukimbilia wewe. Uadilifu na uaminifu vinilinde, kwa sababu tumaini langu ni kwako. Ee Mungu, wakomboe Israeli, katika shida zao zote!