Zaburi. 35. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, pingana na wale wanaopingana nami, upigane na hao wanaopigana nami. Chukua ngao na kigao. Inuka unisaidie. Inua mkuki wako na fumo lako dhidi ya hao wanaonifuatia. Iambie nafsi yangu, “Mimi ni wokovu wako.” Wafedheheshwe na waaibishwe wale wanaotafuta uhai wangu. Wanaofanya shauri kuniangamiza warudishwe nyuma kwa hofu. Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, malaika wa Bwana akiwafukuza. Njia yao na iwe giza na ya utelezi, malaika wa Bwana akiwafuatilia. Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu, na bila sababu wamenichimbia shimo, maafa na yawapate ghafula: wavu walionifichia na uwatege wenyewe, na waanguke katika shimo hilo, kwa maangamizo yao. Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Bwana na kuufurahia wokovu wake. Nitapaza sauti yangu nikisema, “Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana? Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao, maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!” Mashahidi wakatili wanainuka, wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa baya kwa jema na kuiacha nafsi yangu ukiwa. Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa nguo ya gunia na nikajinyenyekesha kwa kufunga. Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa, niliendelea kuomboleza kama vile wao ni rafiki au ndugu. Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni kama ninayemwombolezea mama yangu. Lakini nilipojikwaa, walikusanyika kwa shangwe; washambuliaji walijikusanya dhidi yangu bila mimi kujua. Walinisingizia pasipo kukoma. Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki, wamenisagia meno. Ee Bwana, utatazama mpaka lini? Niokoe maisha yangu na maangamizi yao, uhai wangu wa thamani kutokana na simba hawa. Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa, nitakusifu katikati ya watu wengi. Usiwaache wale wanaonisimanga, wale ambao ni adui zangu bila sababu; usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu wakonyeze jicho kwa hila. Hawazungumzi kwa amani, bali wanatunga mashtaka ya uongo dhidi ya wale wanaoishi kwa utulivu katika nchi. Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha! Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.” Ee Bwana, umeona hili, usiwe kimya. Usiwe mbali nami, Ee Bwana. Amka, inuka unitetee! Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu. Nihukumu kwa haki yako, Ee Bwana Mungu wangu, sawasawa na haki yako; usiwaache wakusimange. Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!” Au waseme, “Tumemmeza.” Wote wanaofurahia dhiki yangu waaibishwe na wachanganyikiwe; hao wanaojiinua dhidi yangu wavikwe aibu na dharau. Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki wapige kelele za shangwe na furaha; hebu waseme siku zote, “Bwana atukuzwe, ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.” Ulimi wangu utanena haki yako na sifa zako mchana kutwa.