Zaburi. 42. Kwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora. Kama vile ayala aoneavyo shauku vijito vya maji, ndivyo nafsi yangu ikuoneavyo shauku, Ee Mungu. Nafsi yangu inamwonea Mungu kiu, Mungu aliye hai. Ni lini nitaweza kwenda kukutana na Mungu? Machozi yangu yamekuwa chakula changu usiku na mchana, huku watu wakiniambia mchana kutwa, “Yuko wapi Mungu wako?” Mambo haya nayakumbuka ninapoimimina nafsi yangu: Jinsi nilivyokuwa nikienda na umati wa watu, nikiongoza maandamano kuelekea kwenye nyumba ya Mungu, kwa kelele za shangwe na za shukrani katikati ya umati uliosherehekea. Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa sababu bado nitamsifu, Mwokozi wangu na Mungu wangu. Nafsi yangu inasononeka ndani yangu; kwa hiyo nitakukumbuka kutoka nchi ya Yordani, katika vilele vya Hermoni, kutoka Mlima Mizari. Kilindi huita kilindi, katika ngurumo za maporomoko ya maji yako; mawimbi yako yote pamoja na viwimbi vimepita juu yangu. Mchana Bwana huelekeza upendo wake, usiku wimbo wake uko nami: maombi kwa Mungu wa uzima wangu. Ninamwambia Mungu Mwamba wangu, “Kwa nini umenisahau? Kwa nini niendelee kuomboleza, nikiwa nimeonewa na adui?” Mifupa yangu inateseka kwa maumivu makali adui zangu wanaponidhihaki, wakiniambia mchana kutwa, “Yuko wapi Mungu wako?” Ee nafsi yangu, kwa nini unasononeka? Kwa nini unafadhaika hivyo ndani yangu? Weka tumaini lako kwa Mungu, kwa sababu bado nitamsifu, Mwokozi wangu na Mungu wangu.