Zaburi. 72. Zaburi ya Solomoni. Ee Mungu, mjalie mfalme aamue kwa haki yako, mwana wa mfalme kwa haki yako. Atawaamua watu wako kwa haki, watu wako walioonewa kwa haki. Milima italeta mafanikio kwa watu, vilima tunda la haki. Atawatetea walioonewa miongoni mwa watu na atawaokoa watoto wa wahitaji, ataponda mdhalimu. Atadumu kama jua lidumuvyo, kama mwezi, vizazi vyote. Atakuwa kama mvua inyeshayo juu ya shamba lililofyekwa, kama manyunyu yanyeshayo ardhi. Katika siku zake wenye haki watastawi; mafanikio yatakuwepo mpaka mwezi utakapokoma. Atatawala kutoka bahari hadi bahari na kutoka Mto mpaka miisho ya dunia. Makabila ya jangwani watamsujudia, na adui zake wataramba mavumbi. Wafalme wa Tarshishi na wa pwani za mbali watamletea kodi; wafalme wa Sheba na Seba watampa zawadi. Wafalme wote watamsujudia na mataifa yote yatamtumikia. Kwa maana atamwokoa mhitaji anayemlilia, aliyeonewa asiye na wa kumsaidia. Atawahurumia wanyonge na wahitaji na kuwaokoa wahitaji kutoka mauti. Atawaokoa kutoka uonevu na ukatili, kwani damu yao ni ya thamani machoni pake. Aishi maisha marefu! Na apewe dhahabu ya Sheba. Watu wamwombee daima na kumbariki mchana kutwa. Nafaka ijae tele katika nchi yote, juu ya vilele vya vilima na istawi. Tunda lake na listawi kama Lebanoni, listawi kama majani ya kondeni. Jina lake na lidumu milele, na lidumu kama jua. Mataifa yote yatabarikiwa kupitia kwake, nao watamwita aliyebarikiwa. Bwana Mungu, Mungu wa Israeli, apewe sifa, yeye ambaye peke yake hutenda mambo ya ajabu. Jina lake tukufu lisifiwe milele, ulimwengu wote ujae utukufu wake. Huu ndio mwisho wa maombi ya Daudi mwana wa Yese.