Zaburi. 79. Zaburi ya Asafu. Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako, wamelinajisi Hekalu lako takatifu, wameifanya Yerusalemu kuwa magofu. Wametoa maiti za watumishi kuwa chakula cha ndege wa angani na nyama ya watakatifu wako kwa wanyama wa nchi. Wamemwaga damu kama maji kuzunguka Yerusalemu yote, wala hakuna yeyote wa kuwazika. Tumekuwa kitu cha aibu kwa jirani zetu, cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka. Hata lini, Ee Bwana? Je, wewe utakasirika milele? Wivu wako utawaka kama moto hadi lini? Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali, juu ya falme za hao wasioliitia jina lako, kwa maana wamemrarua Yakobo na kuharibu nchi ya makao yake. Usituhesabie dhambi za baba zetu, huruma yako na itujie hima, kwa maana tu wahitaji mno. Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie, kwa ajili ya utukufu wa jina lako; tuokoe na kutusamehe dhambi zetu kwa ajili ya jina lako. Kwa nini mataifa waseme, “Yuko wapi Mungu wenu?” Mbele ya macho yetu, dhihirisha kati ya mataifa kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa ya watumishi wako. Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako; kwa nguvu za mkono wako hifadhi wale waliohukumiwa kufa. Walipize jirani zetu mara saba vifuani mwao aibu walizovurumisha juu yako, Ee Bwana. Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako, tutakusifu milele; toka kizazi hadi kizazi tutasimulia sifa zako.