Zaburi. 80. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Yungiyungi za Agano.” Zaburi ya Asafu. Ee Mchungaji wa Israeli tusikie, wewe umwongozaye Yosefu kama kundi; wewe uketiye katika kiti cha enzi katikati ya makerubi, angaza mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase. Uamshe nguvu zako, uje utuokoe. Ee Mungu, uturejeshe, utuangazie uso wako, ili tuweze kuokolewa. Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, hata lini hasira yako itawaka na kufoka moshi dhidi ya maombi ya watu wako? Umewalisha kwa mkate wa machozi, umewafanya wanywe machozi bakuli tele. Tumekuwa chanzo cha ugomvi kwa jirani zetu, na adui zetu wanatudhihaki. Ee Mungu Mwenye Nguvu Zote, uturejeshe; utuangazie uso wako, nasi tuweze kuokolewa. Ulileta mzabibu kutoka Misri, ukawafukuza mataifa, ukaupanda. Uliandaa shamba kwa ajili yake, mizizi ikawa imara, ukajaza nchi. Milima ilifunikwa kwa kivuli chake, matawi yake yakafunika mierezi mikubwa. Matawi yake yalienea mpaka Baharini, machipukizi yake mpaka kwenye Mto. Mbona umebomoa kuta zake ili wote wapitao karibu wazichume zabibu zake? Nguruwe mwitu wanauharibu na wanyama wa kondeni hujilisha humo. Turudie, Ee Mungu Mwenye Nguvu Zote! Tazama chini kutoka mbinguni na uone! Linda mzabibu huu, mche ulioupanda kwa mkono wako wa kuume, mwana uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe. Mzabibu wako umekatwa, umechomwa moto, unapowakemea, watu wako huangamia. Mkono wako na utulie juu ya mtu aliyeko mkono wako wa kuume, mwana wa mtu uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe. Ndipo hatutakuacha tena, utuhuishe, nasi tutaliitia jina lako. Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, uturejeshe; utuangazie uso wako, ili tuweze kuokolewa.