Zaburi. 87. Zaburi ya wana wa Kora. Wimbo. Ameuweka msingi wake katika mlima mtakatifu; Bwana anayapenda malango ya Sayuni kuliko makao yote ya Yakobo. Mambo matukufu yanasemwa juu yako, ee mji wa Mungu: “Nitaweka kumbukumbu ya Rahabu na Babeli miongoni mwa wale wanaonikubali mimi: Ufilisti pia na Tiro, pamoja na Kushi, nami nitasema, ‘Huyu alizaliwa Sayuni.’ ” Kuhusu Sayuni itasemwa hivi, “Huyu na yule walizaliwa humo, naye Aliye Juu Sana mwenyewe atamwimarisha.” Bwana ataandika katika orodha ya mataifa: “Huyu alizaliwa Sayuni.” Watakapokuwa wanapiga vinanda wataimba, “Chemchemi zangu zote ziko kwako.”