Zaburi. 129. Wimbo wa kwenda juu. Wamenionea mno tangu ujana wangu; Israeli na aseme sasa: wamenionea mno tangu ujana wangu, lakini bado hawajanishinda. Wakulima wamelima mgongo wangu, na kufanya mifereji yao mirefu. Lakini Bwana ni mwenye haki; amenifungua toka kamba za waovu. Wale wote waichukiao Sayuni na warudishwe nyuma kwa aibu. Wawe kama majani juu ya paa, ambayo hunyauka kabla hayajakua; kwa hayo mvunaji hawezi kujaza vitanga vyake, wala akusanyaye kujaza mikono yake. Wale wapitao karibu na wasiseme, “Baraka ya Bwana iwe juu yako; tunakubariki katika jina la Bwana.”