Zaburi. 137. Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza tulipokumbuka Sayuni. Kwenye miti ya huko tulitundika vinubi vyetu, kwa maana huko hao waliotuteka walitaka tuwaimbie nyimbo, watesi wetu walidai nyimbo za furaha; walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja kati ya nyimbo za Sayuni!” Tutaimbaje nyimbo za Bwana, tukiwa nchi ya kigeni? Nikikusahau wewe, ee Yerusalemu, basi mkono wangu wa kuume na usahau ujuzi wake. Ulimi wangu ushikamane na kaakaa la kinywa changu kama sitakukumbuka wewe, kama nisipokufikiri Yerusalemu kuwa furaha yangu kubwa. Kumbuka, Ee Bwana, walichokifanya Waedomu, siku ile Yerusalemu ilipoanguka. Walisema, “Bomoa, Bomoa mpaka kwenye misingi yake!” Ee binti Babeli, uliyehukumiwa kuangamizwa, heri yeye atakayekulipiza wewe kwa yale uliyotutenda sisi: yeye ambaye atawakamata watoto wako wachanga na kuwaponda juu ya miamba.