Zaburi. 138. Zaburi ya Daudi. Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako. Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa kuwa umelikuza jina lako na neno lako juu ya vitu vyote. Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari. Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Bwana, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako. Wao na waimbe kuhusu njia za Bwana, kwa maana utukufu wa Bwana ni mkuu. Ingawa Bwana yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali. Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa. Bwana atatimiza kusudi lake kwangu, Ee Bwana, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako.