Mithali. 5. Mwanangu, sikiliza kwa makini hekima yangu, sikiliza vizuri maneno yangu ya busara, ili uweze kutunza busara na midomo yako ihifadhi maarifa. Kwa maana midomo ya mwanamke kahaba hudondoza asali, na maneno ya kinywa chake ni laini kuliko mafuta; lakini mwisho wake ni mchungu kama nyongo, mkali kama upanga ukatao kuwili. Miguu yake hushuka kuelekea kwenye kifo; hatua zake huelekea moja kwa moja kaburini. Yeye hafikiri juu ya njia ya uzima; njia zake zimepotoka, lakini yeye hajui. Sasa basi wanangu, nisikilizeni; msiache ninalowaambia. Njia zenu ziwe mbali naye, msiende karibu na mlango wa nyumba yake, usije ukatoa nguvu zako nzuri kwa wengine na miaka yako kwa aliye mkatili, wageni wasije wakasherehekea utajiri wako na jitihada yako ikatajirisha nyumba ya mwanaume mwingine. Mwishoni mwa maisha yako utalia kwa uchungu, wakati nyama na mwili wako vimechakaa. Utasema, “Tazama jinsi gani nilivyochukia adhabu! Tazama jinsi moyo wangu ulivyodharau maonyo! Sikuwatii walimu wangu wala kuwasikiliza wakufunzi wangu. Nimefika ukingoni mwa maangamizi kabisa katikati ya kusanyiko lote.” Kunywa maji kutoka kwenye kisima chako mwenyewe, maji yanayotiririka kutoka kwenye kisima chako mwenyewe. Je, chemchemi zako zifurike katika barabara za mji na vijito vyako vya maji viwanjani? Na viwe vyako mwenyewe, kamwe visishirikishwe wageni. Chemchemi yako na ibarikiwe na umfurahie mke wa ujana wako. Kulungu jike apendaye, kulungu mzuri: matiti yake na yakutosheleze siku zote, nawe utekwe daima na upendo wake. Kwa nini mwanangu, utekwe na mwanamke kahaba? Kwa nini ukumbatie kifua cha mke wa mwanaume mwingine? Kwa maana njia za mtu ni wazi kabisa mbele za Bwana, naye huyapima mapito yake yote. Matendo mabaya ya mtu mwovu humnasa yeye mwenyewe; kamba za dhambi yake humkamata kwa nguvu. Atakufa kwa kukosa nidhamu, akipotoshwa kwa upumbavu wake mwenyewe.