Mithali. 31. Misemo ya Mfalme Lemueli, usia wa mama yake aliyomfundisha: “Ee mwanangu, ee mwana wa tumbo langu, ee mwana wa nadhiri zangu, Usitumie nguvu zako kwa wanawake, uhodari wako kwa wale wanaowaharibu wafalme. “Ee Lemueli, haifai wafalme, haifai wafalme kunywa mvinyo, haifai watawala kutamani sana kileo, wasije wakanywa na kusahau vile sheria inavyoamuru na kuwanyima haki zao wote walioonewa. Wape kileo wale wanaoangamia, mvinyo wale walio na uchungu, Wanywe na kusahau umaskini wao na wasikumbuke taabu yao tena. “Sema kwa ajili ya wale wasioweza kujisemea, kwa ajili ya haki za wote walioachwa ukiwa. Sema na uamue kwa haki, tetea haki za maskini na wahitaji.” Mke mwenye sifa nzuri, ni nani awezaye kumpata? Yeye ni wa thamani sana kuliko marijani. Mume wake anamwamini kikamilifu wala hakosi kitu chochote cha thamani. Humtendea mumewe mema, wala si mabaya, siku zote za maisha yake. Huchagua sufu na kitani naye hufanya kazi kwa mikono yenye bidii. Yeye ni kama meli za biashara akileta chakula chake kutoka mbali. Yeye huamka kungali bado giza huwapa jamaa yake chakula na mafungu kwa watumishi wake wa kike. Huangalia shamba na kulinunua, kutokana na mapato yake hupanda shamba la mizabibu. Hufanya kazi zake kwa nguvu, mikono yake ina nguvu kwa ajili ya kazi zake. Huona kwamba biashara yake ina faida, wala taa yake haizimiki usiku. Huweka mikono yake kwenye pia, navyo vidole vyake hushikilia kijiti chenye uzi. Huwanyooshea maskini mikono yake na kuwakunjulia wahitaji vitanga vyake. Theluji ishukapo, hana hofu kwa ajili ya watu wa nyumbani mwake, kwa maana wote wamevikwa nguo za kutia joto. Hutengeneza mazulia ya urembo ya kufunika kitanda chake, yeye huvaa kitani safi na urujuani. Mume wake anaheshimiwa kwenye lango la mji, aketipo miongoni mwa wazee wa nchi. Hutengeneza mavazi ya kitani na kuyauza, naye huwauzia wafanyabiashara mishipi. Amevikwa nguvu na heshima, anaweza kucheka bila kuwa na hofu kwa siku zijazo. Huzungumza kwa hekima na mafundisho ya kuaminika yapo ulimini mwake. Huangalia mambo ya nyumbani mwake wala hali chakula cha uvivu. Watoto wake huamka na kumwita aliyebarikiwa, mumewe pia humsifu, akisema: “Wanawake wengi hufanya vitu vyenye sifa nzuri, lakini wewe umewapita wote.” Kujipamba ili kuvutia ni udanganyifu na uzuri unapita upesi, bali mwanamke anayemcha Bwana atasifiwa. Mpe thawabu anayostahili, nazo kazi zake na zimletee sifa kwenye lango la mji.