Wimbo. 6. Mpenzi wako amekwenda wapi, ewe mzuri kupita wanawake wote? Mpenzi wako amegeukia njia ipi, tupate kumtafuta pamoja nawe? Mpenzi wangu amekwenda bustanini mwake, kwenye vitalu vya vikolezo, kujilisha bustanini na kukusanya yungiyungi. Mimi ni wake mpenzi wangu, na mpenzi wangu ni wangu; yeye hujilisha katikati ya yungiyungi. Wewe ni mzuri, mpenzi wangu, kama Tirsa, upendezaye kama Yerusalemu, umetukuka kama jeshi lenye bendera. Uyageuze macho yako mbali nami, yananigharikisha. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi wanaoteremka kutoka Gileadi. Meno yako ni kama kundi la kondoo watokao kuogeshwa. Kila mmoja ana pacha lake, hakuna hata mmoja aliye peke yake. Mashavu yako nyuma ya shela yako ni kama vipande viwili vya komamanga. Panaweza kuwepo malkia sitini, masuria themanini na mabikira wasiohesabika; lakini hua wangu, mkamilifu wangu, ni wa namna ya pekee, binti pekee kwa mama yake, kipenzi cha yeye aliyemzaa. Wanawali walimwona na kumwita aliyebarikiwa; malkia na masuria walimsifu. Ni nani huyu atokeaye kama mapambazuko, mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua, ametukuka kama nyota zifuatanazo? Niliteremka kwenye bustani ya miti ya milozi ili kutazama machipuko ya bondeni, kuona kama mizabibu imechipua au kama mikomamanga imechanua maua. Kabla sijangʼamua, shauku yangu iliniweka katikati ya magari ya kifalme ya kukokotwa na farasi ya watu wangu. Rudi, rudi, ee Mshulami; rudi, rudi ili tupate kukutazama! Mpenzi Kwa nini kumtazama Mshulami, kama kutazama ngoma ya Mahanaimu?