Wimbo. 8. Laiti ungelikuwa kwangu kama ndugu wa kiume, ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu! Kisha, kama ningekukuta huko nje, ningelikubusu, wala hakuna mtu yeyote angelinidharau. Ningelikuongoza na kukuleta katika nyumba ya mama yangu, yeye ambaye amenifundisha. Ningelikupa divai iliyokolezwa unywe, asali ya maua ya mikomamanga yangu. Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia. Binti za Yerusalemu, ninawaagiza: msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe. Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani akimwegemea mpenzi wake? Mpendwa Nilikuamsha chini ya mtofaa, huko mama yako alipotunga mimba yako, huko yeye alipata utungu akakuzaa. Nitie kama muhuri moyoni mwako, kama muhuri kwenye mkono wako; kwa maana upendo una nguvu kama mauti, wivu wake ni mkatili kama kuzimu. Unachoma kama mwali wa moto, kama mwali mkubwa wa moto wa Bwana hasa. Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, mito haiwezi kuugharikisha. Kama mtu angelitoa mali yote ya nyumbani mwake kwa ajili ya upendo, angelidharauliwa kabisa. Tunaye dada mdogo, matiti yake hayajakua bado. Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu wakati atakapokuja kuposwa? Kama yeye ni ukuta, tutajenga minara ya fedha juu yake. Na kama yeye ni mlango, tutamzungushia mbao za mierezi. Mimi ni ukuta, nayo matiti yangu ni kama minara. Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake kama yule anayeleta utoshelevu. Solomoni alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni; alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji. Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake shekeli 1,000 za fedha. Lakini shamba langu la mizabibu ambalo ni langu mwenyewe ni langu kutoa; hizo shekeli 1,000 ni kwa ajili yako, ee Solomoni, na shekeli mia mbili ni kwa ajili ya wale wanaotunza matunda yake. Wewe ukaaye bustanini pamoja na marafiki mliohudhuria, hebu nisikie sauti yako! Njoo, mpenzi wangu, uwe kama swala au kama ayala kijana juu ya milima iliyojaa vikolezo.