Isaya. 56. Hili ndilo asemalo Bwana: “Dumisheni haki na mkatende lile lililo sawa, kwa maana wokovu wangu u karibu na haki yangu itafunuliwa upesi. Amebarikiwa mtu yule atendaye hili, mtu yule alishikaye kwa uthabiti, yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.” Usimwache mgeni aambatanaye na Bwana aseme, “Hakika Bwana atanitenga na watu wake.” Usimwache towashi yeyote alalamike akisema, “Mimi ni mti mkavu tu.” Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana: “Kwa matowashi washikao Sabato zangu, ambao huchagua kile kinachonipendeza na kulishika sana agano langu: hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake kumbukumbu na jina bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike: nitawapa jina lidumulo milele, ambalo halitakatiliwa mbali. Wageni wanaoambatana na Bwana ili kumtumikia, kulipenda jina la Bwana, na kumwabudu yeye, wote washikao Sabato bila kuinajisi na ambao hushika sana agano langu: hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala. Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao zitakubalika juu ya madhabahu yangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.” Bwana Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye Waisraeli waliohamishwa: “Bado nitawakusanya wengine kwao zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.” Njooni, enyi wanyama wote wa kondeni, njooni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni! Walinzi wa Israeli ni vipofu, wote wamepungukiwa na maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kubweka; hulala na kuota ndoto, hupenda kulala. Ni mbwa wenye tamaa kubwa, kamwe hawatosheki. Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu; wote wamegeukia njia yao wenyewe, kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe. Kila mmoja hulia, “Njooni, tupate mvinyo! Tunywe kileo sana! Kesho itakuwa kama leo, au hata bora zaidi.”