Ezekieli. 19. “Wewe fanya maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli na useme: “ ‘Tazama jinsi gani mama yako alivyokuwa simba jike miongoni mwa simba! Alilala katikati ya wana simba na kulisha watoto wake. Alimlea mmoja wa watoto wake, naye akawa simba mwenye nguvu. Akajifunza kurarua mawindo naye akala watu. Mataifa wakasikia habari zake, naye akanaswa katika shimo lao. Wakamwongoza kwa ndoana mpaka nchi ya Misri. “ ‘Mama yake alipongoja na kuona tumaini lake halitimiziki, nayo matarajio yake yametoweka, akamchukua mwanawe mwingine na kumfanya simba mwenye nguvu. Alizungukazunguka miongoni mwa simba, kwa kuwa sasa alikuwa simba mwenye nguvu. Akajifunza kurarua mawindo naye akala watu. Akabomoa ngome zao na kuiharibu miji yao. Nchi na wote waliokuwa ndani yake wakatiwa hofu kwa kunguruma kwake. Kisha mataifa wakaja dhidi yake kutoka sehemu zilizomzunguka. Wakatanda nyavu zao kwa ajili yake, naye akanaswa katika shimo lao. Kwa kutumia ndoana wakamvutia kwenye tundu na kumleta mpaka kwa mfalme wa Babeli. Wakamtia gerezani, hivyo kunguruma kwake hakukusikika tena katika milima ya Israeli. “ ‘Mama yako alikuwa kama mzabibu katika shamba lako la mizabibu uliopandwa kando ya maji, ukiwa unazaa sana na wenye matawi mengi kwa sababu ya wingi wa maji. Matawi yake yalikuwa na nguvu, yaliyofaa kuwa fimbo ya enzi ya mtawala. Ulikuwa mrefu kupita miti mingine katikati ya matawi manene; ulionekana kwa urahisi kwa ajili ya urefu wake na wingi wa matawi yake. Lakini ulingʼolewa kwa hasira kali na kutupwa chini. Upepo wa mashariki uliufanya usinyae, matunda yake yakapukutika, matawi yake yenye nguvu yakanyauka na moto ukayateketeza. Sasa umepandwa jangwani katika nchi kame na ya kiu. Moto ulienea kuanzia katika mmojawapo ya matawi yake makubwa na kuteketeza matunda yake. Hakuna tawi lenye nguvu lililobaki juu yake lifaalo kuwa fimbo ya enzi ya mtawala.’ Hili ndilo ombolezo, na litumike kama ombolezo.”