Hosea. 9. Usifurahie, ee Israeli; usishangilie kama mataifa mengine. Kwa kuwa hukuwa mwaminifu kwa Mungu wako; umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu ya kupuria nafaka. Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai havitalisha watu, divai mpya itawapungukia. Hawataishi katika nchi ya Bwana, Efraimu atarudi Misri na atakula chakula kilicho najisi huko Ashuru. Hawatammiminia Bwana sadaka ya divai wala dhabihu zao hazitampendeza. Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao kama mkate wa waombolezaji; nao wote wazilao watakuwa najisi. Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe; kisije katika Hekalu la Bwana. Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa, katika siku za sikukuu za Bwana? Hata ikiwa wataokoka maangamizi, Misri atawakusanya, nayo Memfisi itawazika. Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma, nayo miiba itafunika mahema yao. Siku za adhabu zinakuja, siku za malipo zimewadia. Israeli na afahamu hili. Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana na uadui wenu ni mkubwa sana, nabii anadhaniwa ni mpumbavu, mtu aliyeongozwa na Mungu anaonekana mwendawazimu. Nabii, pamoja na Mungu wangu, ndiye mlinzi juu ya Efraimu, hata hivyo mitego inamngojea katika mapito yake yote, na uadui katika nyumba ya Mungu wake. Wamezama sana katika rushwa, kama katika siku za Gibea. Mungu atakumbuka uovu wao na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao. “Nilipompata Israeli, ilikuwa kama kupata zabibu jangwani; nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona matunda ya kwanza katika mtini. Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu kwa ile sanamu ya aibu, nao wakawa najisi kama kitu kile walichokipenda. Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege: hakuna kuzaa, hakuna kuchukua mimba, hakuna kutunga mimba. Hata wakilea watoto, nitamuua kila mmoja. Ole wao nitakapowapiga kisogo! Nimemwona Efraimu, kama Tiro, aliyeoteshwa mahali pazuri. Lakini Efraimu wataleta watoto wao kwa mchinjaji.” Wape, Ee Bwana, je, utawapa nini? Wape matumbo ya kuharibu mimba na matiti yaliyokauka. “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali, niliwachukia huko. Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi, nitawafukuza katika nyumba yangu. Sitawapenda tena, viongozi wao wote ni waasi. Efraimu ameharibiwa, mzizi wao umenyauka, hawazai tunda. Hata kama watazaa watoto, nitawachinja watoto wao waliotunzwa vizuri.” Mungu wangu atawakataa kwa sababu hawakumtii; watakuwa watu wa kutangatanga miongoni mwa mataifa.