Yoeli. 2. Pigeni tarumbeta katika Sayuni; pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu. Wote waishio katika nchi na watetemeke, kwa kuwa siku ya Bwana inakuja. Iko karibu, siku ya giza na huzuni, siku ya mawingu na utusitusi. Kama mapambazuko yasambaavyo toka upande huu wa milima hata upande mwingine jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja. Jambo kama hili halijakuwepo tangu zamani wala halitakuwepo tena kamwe kwa vizazi vijavyo. Mbele yao moto unateketeza, nyuma yao miali ya moto inawaka kwa nguvu. Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni, nyuma yao ni jangwa lisilofaa: hakuna kitu kinachowaepuka. Wanaonekana kama farasi; wanakwenda mbio kama askari wapanda farasi. Wanatoa sauti kama magari ya vita, wanaporukaruka juu ya vilele vya milima, kama mlio wa miali ya moto ilayo mabua, kama jeshi kubwa lililojipanga kwa ajili ya vita. Wanapoonekana, mataifa yanakuwa katika maumivu makuu; kila uso unabadilika rangi. Wanashambulia kama wapiganaji wa vita; wanapanda kuta kama askari. Wote wanatembea katika safu, hawapotoshi safu zao. Hakuna anayemsukuma mwenzake; kila mmoja anakwenda mbele moja kwa moja. Wanapita katika vizuizi bila kuharibu safu zao. Wanaenda kasi kuingia mjini; wanakimbia ukutani. Wanaingia ndani ya nyumba; kwa kuingilia madirishani kama wevi. Mbele yao dunia inatikisika, anga linatetemeka, jua na mwezi vinatiwa giza, na nyota hazitoi mwanga wake tena. Bwana anatoa mshindo wa ngurumo mbele ya jeshi lake; majeshi yake hayana idadi, ni wenye nguvu nyingi wale ambao hutii agizo lake. Siku ya Bwana ni kuu, ni ya kutisha. Ni nani anayeweza kuistahimili? “Hata sasa,” asema Bwana, “nirudieni kwa mioyo yenu yote, kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.” Rarueni mioyo yenu na siyo mavazi yenu. Mrudieni Bwana, Mungu wenu, kwa maana yeye ndiye mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo, huona huruma, hujizuia kuleta maafa. Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma na kuacha baraka nyuma yake: sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji kwa ajili ya Bwana Mungu wenu. Pigeni tarumbeta katika Sayuni, tangazeni saumu takatifu, liiteni kusanyiko takatifu. Wakusanyeni watu, wekeni wakfu kusanyiko; waleteni pamoja wazee, wakusanyeni watoto, wale wanyonyao maziwa. Bwana arusi na atoke chumbani mwake na bibi arusi naye atoke katika chumba chake. Makuhani, ambao wanahudumu mbele za Bwana, na walie katikati ya ukumbi wa Hekalu na madhabahu. Waseme, “Wahurumie watu wako, Ee Bwana. Usifanye urithi wako kitu cha kudharauliwa, neno la dhihaka kati ya mataifa. Kwa nini wasemezane miongoni mwao, ‘Yuko wapi Mungu wao?’ ” Kisha Bwana atakuwa na wivu kwa ajili ya nchi yake na kuwa na huruma juu ya watu wake. Bwana atawajibu: “Ninawapelekea nafaka, mvinyo mpya na mafuta, vya kuwatosha ninyi hadi mridhike kabisa; kamwe sitawafanya tena kitu cha kudharauliwa na mataifa. “Nitafukuza jeshi la kaskazini likae mbali nanyi, nikilisukuma ndani ya jangwa, askari wa safu za mbele wakienda ndani ya bahari ya mashariki na wale wa safu za nyuma katika bahari ya magharibi. Uvundo wake utapaa juu; harufu yake itapanda juu.” Hakika ametenda mambo makubwa. Usiogope, ee nchi; furahi na kushangilia. Hakika Bwana ametenda mambo makubwa. Msiogope, enyi wanyama pori, kwa kuwa mbuga za malisho yenu zinarudia ubichi. Miti nayo inazaa matunda, mtini na mzabibu inatoa utajiri wake. Furahini, enyi watu wa Sayuni, shangilieni katika Bwana Mungu wenu, kwa kuwa amewapa mvua za vuli kwa kipimo cha haki. Anawapelekea mvua nyingi, mvua ya vuli na ya masika, kama mwanzoni. Sakafu za kupuria zitajaa nafaka, mapipa yatafurika mvinyo mpya na mafuta. “Nitawalipa kwa ajili ya miaka ile iliyoliwa na nzige: parare, madumadu na tunutu, jeshi langu kubwa ambalo nililituma katikati yenu. Mtakuwa na wingi wa vyakula mpaka mshibe, na mtalisifu jina la Bwana Mungu wenu, ambaye amefanya maajabu kwa ajili yenu; kamwe watu wangu hawataaibishwa tena. Ndipo mtakapojua kwamba mimi niko katika Israeli kwamba mimi ndimi Bwana Mungu wenu, na kwamba hakuna mwingine; kamwe watu wangu hawataaibika tena. “Hata itakuwa, baada ya hayo, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zenu watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono. Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu. Nami nitaonyesha maajabu katika mbingu na duniani: damu, moto na mawimbi ya moshi. Jua litageuzwa kuwa giza na mwezi kuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ya Bwana ile kuu na ya kutisha. Na kila mtu atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa. Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu kutakuwepo wokovu, kama Bwana alivyosema, miongoni mwa walionusurika ambao Bwana awaita.