Amosi. 5. Sikia neno hili, ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi: “Bikira Israeli ameanguka, kamwe hatainuka tena, ameachwa pweke katika nchi yake, hakuna yeyote wa kumwinua.” Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “Wakati mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani kwa ajili ya Israeli, mia moja tu watarudi; wakati mji utakapopeleka mia moja, kumi tu ndio watarudi hai.” Hili ndilo Bwana asemalo kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni mpate kuishi; msitafute Betheli, msiende Gilgali, msisafiri kwenda Beer-Sheba. Kwa maana kwa hakika Gilgali itakwenda uhamishoni, na Betheli itafanywa kuwa si kitu.” Mtafuteni Bwana mpate kuishi, au atafagia nyumba ya Yosefu kama moto; utawateketeza, nayo Betheli haitakuwa na yeyote wa kuuzima. Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu na kuiangusha haki chini (yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni, ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko na mchana kuwa usiku, ambaye huyaita maji ya bahari na kuyamwaga juu ya uso wa nchi: Bwana ndilo jina lake; yeye hufanya maangamizo kwenye ngome na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa), mnamchukia yule akemeaye mahakamani, na kumdharau yule ambaye husema kweli. Mnamgandamiza maskini na kumlazimisha awape nafaka. Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari, hamtaishi ndani yake; ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, hamtakunywa divai yake. Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu na ukubwa wa dhambi zenu. Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa na kuzuia haki ya maskini mahakamani. Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza kimya nyakati kama hizo, kwa kuwa nyakati ni mbaya. Tafuteni mema, wala si mabaya, ili mpate kuishi. Ndipo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo yupo nanyi. Yachukieni maovu, yapendeni mema; dumisheni haki mahakamani. Yamkini Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote atawahurumia mabaki ya Yosefu. Kwa hiyo hili ndilo Bwana, Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, asemalo: “Kutakuwepo maombolezo katika barabara zote na vilio vya uchungu katika njia kuu zote. Wakulima wataitwa kuja kulia, na waombolezaji waje kuomboleza. Kutakuwepo kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu, kwa kuwa nitapita katikati yenu,” asema Bwana. Ole wenu ninyi mnaoitamani siku ya Bwana! Kwa nini mnaitamani siku ya Bwana? Siku hiyo itakuwa giza, si nuru. Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba kumbe akakutana na dubu, kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta, kumbe akaumwa na nyoka. Je, siku ya Bwana haitakuwa giza, na si nuru: giza nene, bila mwonzi wa mwanga? “Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini; siwezi kuvumilia makusanyiko yenu. Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka za nafaka, sitazikubali. Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani, sitazitambua. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu! Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu. Lakini acheni haki itiririke kama mto, na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka! “Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli? Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu, Sikuthi mungu wenu mtawala, na Kiuni mungu wenu wa nyota, ambao mliwatengeneza wenyewe. Kwa sababu hiyo nitawapeleka uhamishoni mbali kupita Dameski,” asema Bwana, ambaye jina lake ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.