Yona. 2. Akiwa ndani ya tumbo la nyangumi, Yona alimwomba Bwana Mungu wake. Akasema: “Katika shida yangu nalimwita Bwana, naye akanijibu. Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada, nawe ukasikiliza kilio changu. Ulinitupa kwenye kilindi, ndani kabisa ya moyo wa bahari, mikondo ya maji ilinizunguka, mawimbi yako yote na viwimbi vilipita juu yangu. Nikasema, ‘Nimefukuziwa mbali na uso wako, hata hivyo nitatazama tena kuelekea Hekalu lako takatifu.’ Maji yaliyonimeza yalinitisha, kilindi kilinizunguka; mwani ulijisokota kichwani pangu. Nilizama chini sana mpaka pande za mwisho za milima, makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele. Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni, Ee Bwana Mungu wangu. “Wakati uhai wangu ulipokuwa unatoka, nilikukumbuka wewe, Bwana, nayo maombi yangu yalikufikia wewe, katika Hekalu lako takatifu. “Wale watu wanaongʼangʼana na sanamu zisizofaa hupoteza neema ile ambayo ingekuwa yao. Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani, nitakutolea dhabihu. Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza. Wokovu watoka kwa Bwana.” Basi Bwana akamwamuru yule nyangumi, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.