Mika. 1. Neno la Bwana lilimjia Mika, Mmoreshethi, wakati wa utawala wa Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda; ufunuo aliouona kuhusu Samaria na Yerusalemu. Sikieni, enyi mataifa, enyi nyote, sikilizeni, ee dunia na wote mliomo ndani yake, ili Bwana Mwenyezi ashuhudie dhidi yenu, Bwana kutoka Hekalu lake takatifu. Tazama! Bwana anakuja kutoka mahali pake; anashuka na kukanyaga mahali palipoinuka juu pa dunia. Milima inayeyuka chini yake na mabonde yanagawanyika kama nta mbele ya moto, kama maji yatiririkayo kasi kwenye mteremko. Yote haya ni kwa sababu ya kosa la Yakobo, ni kwa sababu ya dhambi za nyumba ya Israeli. Kosa la Yakobo ni lipi? Je, sio Samaria? Je, mahali pa juu pa Yuda pa kuabudia miungu ni nini? Je, sio Yerusalemu? “Kwa hiyo nitaufanya Samaria kuwa lundo la kokoto, mahali pa kuotesha mizabibu. Nitayamwaga mawe yake katika bonde na kuacha wazi misingi yake. Sanamu zake zote zitavunjwa vipande vipande; zawadi zake zote za Hekalu zitachomwa kwa moto; nitaharibu vinyago vyake vyote. Kwa kuwa alikusanya zawadi zake kutokana na ujira wa kahaba, nazo zitatumika tena kulipa mishahara ya kahaba.” Kwa ajili ya hili nitalia na kuomboleza; nitatembea bila viatu na tena uchi. Nitabweka kama mbweha na kuomboleza kama bundi. Kwa sababu jeraha lake halitibiki; limekuja Yuda. Limefika hasa kwenye lango la watu wangu, hata Yerusalemu kwenyewe. Usiliseme hili huko Gathi; usilie hata kidogo. Huko Beth-le-Afra gaagaa mavumbini. Piteni mkiwa uchi na wenye aibu, ninyi mkaao Shafiri. Wale waishio Saanani hawatatoka nje. Beth-Eseli iko katika maombolezo; kinga yake imeondolewa kwako. Wale waishio Marothi wanagaagaa kwa maumivu wakingoja msaada, kwa sababu maangamizi yamekuja kutoka kwa Bwana, hata katika lango la Yerusalemu. Enyi mkaao Lakishi, fungeni farasi kwenye magari ya vita. Mlikuwa chanzo cha dhambi kwa Binti Sayuni, kwa kuwa makosa ya Israeli yalikutwa kwako. Kwa hiyo utaipa Moresheth-Gathi zawadi za kuagana. Mji wa Akzibu utaonyesha wazi udanganyifu kwa wafalme wa Israeli. Nitawaleteeni atakayewashinda ninyi mnaoishi Maresha. Yeye aliye utukufu wa Israeli atakuja Adulamu. Nyoeni nywele zenu katika kuomboleza kwa ajili ya watoto wenu mnaowafurahia; jifanyieni upara kama tai, kwa kuwa watawaacha na kwenda uhamishoni.