Mika. 3. Kisha nikasema, “Sikilizeni enyi viongozi wa Yakobo, enyi watawala wa nyumba ya Israeli. Je, hampaswi kujua hukumu, ninyi mnaochukia mema na kupenda maovu; ninyi mnaowachuna watu wangu ngozi na kuondoa nyama kwenye mifupa yao; ninyi mnaokula nyama ya watu wangu, mnaowachuna ngozi na kuvunja mifupa yao vipande vipande; mnaowakatakata kama nyama ya kuwekwa kwenye sufuria na kama nyama ya kuwekwa kwenye chungu?” Kisha watamlilia Bwana, lakini hatawajibu. Wakati huo atawaficha uso wake kwa sababu ya uovu waliotenda. Hili ndilo asemalo Bwana: “Kuhusu manabii wanaowapotosha watu wangu, mtu akiwalisha, wanatangaza ‘amani’; kama hakufanya hivyo, wanaandaa kupigana vita dhidi yake. Kwa hiyo usiku utawajieni, msiweze kuwa na maono, na giza, msiweze kubashiri. Jua litawachwea manabii hao, nao mchana utakuwa giza kwao. Waonaji wataaibika na waaguzi watafedheheka. Wote watafunika nyuso zao kwa sababu hakuna jibu litokalo kwa Mungu.” Lakini kuhusu mimi, nimejazwa nguvu, nimejazwa Roho wa Bwana, haki na uweza, kumtangazia Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake. Sikieni hili, enyi viongozi wa nyumba ya Yakobo, enyi watawala wa nyumba ya Israeli, mnaodharau haki na kupotosha kila lililo sawa; mnaojenga Sayuni kwa kumwaga damu na Yerusalemu kwa uovu. Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa, na makuhani wake wanafundisha kwa malipo, nao manabii wake wanatabiri kwa fedha. Hata hivyo wanamwegemea Bwana na kusema, “Je, Bwana si yumo miongoni mwetu? Hakuna maafa yatakayotupata.” Kwa hiyo kwa sababu yenu, Sayuni italimwa kama shamba, Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto, na kilima cha Hekalu kitakuwa kichuguu kilichofunikwa na vichaka.