Mika. 6. Sikiliza asemalo Bwana: “Simama, tetea shauri lako mbele ya milima; vilima na visikie lile unalotaka kusema. Sikilizeni, ee milima, mashtaka ya Bwana, sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia. Kwa kuwa Bwana ana shauri dhidi ya watu wake; anatoa mashtaka dhidi ya Israeli. “Watu wangu, nimewatendea nini? Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu. Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa. Nilimtuma Mose awaongoze, pia Aroni na Miriamu. Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu alivyofanya shauri na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu. Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu mpaka Gilgali, ili mfahamu matendo ya haki ya Bwana.” Nimjie Bwana na kitu gani na kusujudu mbele za Mungu aliyetukuka? Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa, nije na ndama za mwaka mmoja? Je, Bwana atafurahishwa na kondoo dume elfu, au mito elfu kumi ya mafuta? Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu, mtoto wangu mwenyewe kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu? Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu. Bwana anataka nini kwako? Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako. Sikiliza! Bwana anauita mji: kulicha jina lako ni hekima: “Tii hiyo fimbo na yeye aliyeiamuru. Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu, hazina yako uliyopata kwa udanganyifu na vipimo vilivyopunguka, ambavyo vimelaaniwa? Je, naweza kuhukumu kuwa mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia, aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo? Matajiri wake ni wajeuri; watu wake ni waongo na ndimi zao zinazungumza kwa udanganyifu. Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu, kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu. Mtakula lakini hamtashiba; matumbo yenu bado yatakuwa matupu. Mtaweka akiba lakini hamtaokoa chochote, kwa sababu mtakachoweka akiba nitatoa kwa upanga. Mtapanda lakini hamtavuna; mtakamua zeituni lakini hamtatumia mafuta yake. Mtakamua zabibu lakini hamtakunywa hiyo divai. Mmezishika sheria za Omri na matendo yote ya nyumba ya Ahabu, tena umefuata desturi zao. Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi na watu wako kuwa dhihaka; mtachukua dharau za mataifa.”