Sefania. 1. Neno la Bwana lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda: Bwana asema, “Nitafagia kila kitu kutoka kwenye uso wa dunia.” “Nitafagilia mbali watu na wanyama; nitafagilia mbali ndege wa angani na samaki wa baharini. Wafanyao maovu watapata tu kokoto, nami nitamkatilia mbali mwanadamu atoke katika dunia,” asema Bwana. “Nitaiadhibu Yuda na wote wakaao Yerusalemu. Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali kila mabaki ya Baali, majina ya wapagani na makuhani waabuduo sanamu: wale ambao husujudu juu ya mapaa kuabudu jeshi la vitu vya angani, wale ambao husujudu na kuapa kwa Bwana na ambao pia huapa kwa Malkamu, wale wanaoacha kumfuata Bwana, wala hawamtafuti Bwana wala kutaka shauri lake. Nyamazeni mbele za Bwana Mwenyezi, kwa maana siku ya Bwana iko karibu. Bwana ameandaa dhabihu, amewaweka wakfu wale aliowaalika. Katika siku ya dhabihu ya Bwana nitawaadhibu wakuu na wana wa mfalme na wale wote wanaovaa nguo za kigeni. Katika siku hiyo nitaadhibu wote ambao hukwepa kukanyaga kizingiti, ambao hujaza hekalu la miungu yao kwa dhuluma na udanganyifu.” Bwana asema, “Katika siku hiyo kilio kitapanda juu kutoka lango la Samaki, maombolezo kutoka mtaa wa pili, na mshindo mkubwa kutoka vilimani. Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni; wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa, wote ambao wanafanya biashara ya fedha wataangamizwa. Wakati huo nitasaka mji wa Yerusalemu kwa taa, na kuwaadhibu wale ambao wanakaa katika hali ya kuridhika, ambao ni kama divai iliyobaki kwenye machicha, ambao hudhani, ‘Bwana hatafanya lolote, jema au baya.’ Utajiri wao utatekwa nyara, nyumba zao zitabomolewa. Watajenga nyumba, lakini hawataishi ndani yake; watapanda mizabibu lakini hawatakunywa divai yake. “Siku kubwa ya Bwana iko karibu: iko karibu na inakuja haraka. Sikilizeni! Kilio katika siku ya Bwana kitakuwa kichungu, hata shujaa atapiga kelele. Siku ile ni siku ya ghadhabu, siku ya fadhaa na dhiki, siku ya uharibifu na ukiwa, siku ya giza na utusitusi, siku ya mawingu na giza nene, siku ya tarumbeta na mlio wa vita dhidi ya miji yenye ngome na dhidi ya minara mirefu. Nitawaletea watu dhiki, nao watatembea kama vipofu, kwa sababu wametenda dhambi dhidi ya Bwana. Damu yao itamwagwa kama vumbi na matumbo yao kama taka. Fedha yao wala dhahabu yao hazitaweza kuwaokoa katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana. Katika moto wa wivu wake dunia yote itateketezwa, kwa maana ataleta mwisho wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.”