Matendo Ya Mitume Kanisa La Kwanza (1:1–5:42) 1Matendo Ya MitumeAhadi Ya Roho Mtakatifu

1 1:1Katika kitabu changu cha kwanza nilikuandikia, mpendwa Theofilo, kuhusu mambo yote Yesu aliyofanya na kufundisha tangu mwanzo, 2 1:2hadi siku ile alipochukuliwa kwenda mbinguni, baada ya kuwapa maagizo kupitia kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. 3 1:3Baada ya mateso yake, alijionyesha kwao na kuwathibitishia kwa njia nyingi kwamba yeye yu hai. Katika muda wa siku arobaini baada ya kufufuka kwake aliwatokea na kunena kuhusu Ufalme wa Mungu. 4 1:4Wakati mmoja alipokuwa pamoja nao, aliwapa amri hii, “Msitoke Yerusalemu, bali ingojeni ahadi ya Baba, ambayo mmenisikia nikisema habari zake. 5 1:5 Yohana aliwabatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”

Yesu Apaa Mbinguni (Marko 16:19-20; Luka 24:50-53)

6 1:6Mitume walipokuwa wamekusanyika pamoja, wakamuuliza Yesu, “Bwana, je, huu ndio wakati wa kuwarudishia Israeli ufalme?”

7 1:7Yesu akawaambia, “Si juu yenu kujua nyakati na majira ambayo Baba ameyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. 8 1:8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, Uyahudi kote na Samaria, hadi miisho ya dunia.”

9 1:9Baada ya kusema mambo haya, walipokuwa wanatazama, akachukuliwa juu mbinguni mbele ya macho yao na wingu likampokea wasimwone tena.

10 1:10Walipokuwa bado wakikaza macho yao kuelekea juu alipokuwa akienda zake Mbinguni, tazama ghafula, wanaume wawili waliovaa mavazi meupe wakasimama karibu nao, 11 1:11wakasema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mnasimama mkitazama juu angani? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda Mbinguni, atarudi tena jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake Mbinguni.”

Mathiya Achaguliwa Badala Ya Yuda (Mathayo 27:3-10)

12 1:12Ndipo waliporudi Yerusalemu kutoka Mlima wa Mizeituni, uliokuwa karibu na Yerusalemu, umbali wa mwendo wa Sabato 1:12 Mwendo wa Sabato hapa ina maana umbali wa mita 1,100. kutoka mjini. 13 1:13Walipowasili mjini Yerusalemu, walikwenda ghorofani kwenye chumba walichokuwa wakiishi. Wale waliokuwepo walikuwa: Petro, Yohana, Yakobo, Andrea, Filipo, Tomaso, Bartholomayo, Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote 1:13 Zelote hapa ina maana alikuwa mwanachama wa Wazelote, kikundi cha Kiyahudi cha kupinga jeuri ya Warumi. na Yuda mwana wa Yakobo. 14 1:14Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Maria mama yake Yesu, pamoja na ndugu zake Yesu.

15 1:15Katika siku hizo Petro akasimama katikati ya waumini (jumla yao wote walikuwa watu wapatao 120), akasema, 16 1:16“Ndugu zangu, ilibidi Andiko litimie ambalo Roho Mtakatifu alitabiri kupitia kwa Daudi kumhusu Yuda aliyewaongoza wale waliomkamata Yesu. 17 1:17Yuda alikuwa mmoja wetu, kwa maana na yeye alichaguliwa ashiriki katika huduma hii.”

18 1:18(Basi Yuda alinunua shamba kwa zile fedha za uovu alizopata; akiwa huko shambani akaanguka, akapasuka na matumbo yote yakatoka nje. 19 1:19Kila mtu Yerusalemu akasikia habari hizi, kwa hiyo wakapaita mahali hapo kwa lugha yao, Akeldama, yaani Shamba la Damu).

20 1:20“Kama vile ilivyoandikwa katika kitabu cha Zaburi,

“ ‘Mahali pake na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi humo,’ na, “ ‘Mtu mwingine aichukue nafasi yake ya uongozi.’ 21 1:21Kwa hiyo inatubidi tumchague mtu mwingine miongoni mwa wale ambao wamekuwa pamoja nasi wakati wote Bwana Yesu alipoingia na kutoka katikati yenu, 22 1:22kuanzia ubatizo wa Yohana mpaka siku aliyochukuliwa kutoka kwetu kwenda Mbinguni. Kwa kuwa mmoja wao inabidi awe shahidi pamoja nasi wa ufufuo wake.”

23 1:23Wakapendekeza majina ya watu wawili: Yosefu, aitwaye Barsaba (ambaye pia alijulikana kama Yusto) na Mathiya. 24 1:24Kisha wakaomba, wakasema, “Bwana, wewe waujua moyo wa kila mtu. Tuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25 1:25ili achukue nafasi ya huduma ya utume ambayo Yuda aliiacha ili aende mahali pake mwenyewe.” 26 1:26Kisha wakawapigia kura, nayo kura ikamwangukia Mathiya, naye akaongezwa kwenye wale mitume kumi na mmoja.

2Kushuka Kwa Roho Mtakatifu

1 2:1Siku ya Pentekoste ilipowadia, waamini wote walikuwa mahali pamoja. 2 2:2Ghafula sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali uliotoka mbinguni ukaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. 3 2:3Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kukaa juu ya kila mmoja wao. 4 2:4Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.

5 2:5Basi walikuwepo Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. 6 2:6Waliposikia sauti hii, umati wa watu ulikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. 7 2:7Wakiwa wameshangaa na kustaajabu wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya? 8 2:8Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa? 9 2:9Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Uyahudi, Kapadokia, Ponto na Asia, 10 2:10Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libya karibu na Kirene na wageni kutoka Rumi, 11 2:11Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu, sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.” 12 2:12Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”

13 2:13Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa divai!”

Petro Ahutubia Umati

14 2:14Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akainua sauti yake na kuhutubia ule umati wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, jueni jambo hili mkanisikilize. 15 2:15Hakika watu hawa hawakulewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! 16 2:16La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:

17 2:17“ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zenu watatabiri, vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto. 18 2:18Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu, nao watatabiri. 19 2:19Nami nitaonyesha maajabu juu mbinguni, na ishara chini duniani: damu, moto, na mawimbi ya moshi. 20 2:20Jua litakuwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ile kuu ya Bwana iliyo tukufu. 21 2:21Na kila mtu atakayeliitia jina la Bwana, ataokolewa.’

22 2:22“Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Yesu wa Nazareti alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23 2:23Huyu mtu akiisha kutolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi, kwa mikono ya watu wabaya, mlimuua kwa kumgongomea msalabani. 24 2:24Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti. 25 2:25Kwa maana Daudi asema kumhusu yeye:

“ ‘Nalimwona Bwana mbele yangu daima. Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume, sitatikisika. 26 2:26Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia; mwili wangu nao utapumzika kwa tumaini. 27 2:27Kwa maana hutaniacha kaburini, wala hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu. 28 2:28Umenionyesha njia za uzima, utanijaza na furaha mbele zako.’

29 2:29“Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa mpaka leo. 30 2:30Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha enzi. 31 2:31Daudi, akiona mambo yaliyoko mbele, akanena juu ya kufufuka kwa Kristo, 2:31 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu. 32 2:32Mungu alimfufua huyu Yesu na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo. 33 2:33Basi ikiwa yeye ametukuzwa kwa mkono wa kuume wa Mungu, amepokea kutoka kwa Baba ahadi ya Roho Mtakatifu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia. 34 2:34Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema,

“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, 35 2:35hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’

36 2:36“Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Yesu, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Kristo.”

Waumini Waongezeka

37 2:37Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”

38 2:38Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. 39 2:39Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”

40 2:40Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 2:41Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa na siku ile waliongezeka watu wapatao 3,000.

Ushirika Wa Waumini

42 2:42Nao wakawa wanadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 2:43Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 2:44Walioamini wote walikuwa mahali pamoja, nao walikuwa na kila kitu shirika. 45 2:45Waliuza mali zao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 2:46Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa Hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 2:47wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kanisa wale waliokuwa wakiokolewa.

3Petro Amponya Mlemavu Kwa Jina La Yesu

1 3:1Siku moja Petro na Yohana walikuwa wanapanda kwenda Hekaluni kusali yapata saa tisa alasiri. 2 3:2Basi palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu kuzaliwa. Alichukuliwa na kuwekwa kwenye lango la Hekalu liitwalo Zuri, kila siku ili aombe msaada kwa watu wanaoingia Hekaluni. 3 3:3Huyu mtu alipowaona Petro na Yohana wakikaribia kuingia Hekaluni, akawaomba wampe sadaka. 4 3:4Wakamkazia macho, kisha Petro akamwambia, “Tutazame sisi.” 5 3:5Hivyo yule mtu akawatazama, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.

6 3:6Ndipo Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” 7 3:7Petro akamshika yule mtu kwa mkono wa kuume akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikapata nguvu. 8 3:8Akaruka juu na kusimama, akaanza kutembea. Kisha akaingia Hekaluni pamoja na Petro na Yohana, huku akitembea na kurukaruka na kumsifu Mungu. 9 3:9Watu wote walipomwona akitembea na kumsifu Mungu, 10 3:10wakamtambua kuwa ni yule mtu aliyekuwa akiketi nje ya Hekalu penye lango liitwalo Zuri akiomba msaada, nao wakajawa na mshangao, wakastaajabu juu ya yale yaliyomtukia.

Petro Anashuhudia Kuwa Yesu Anaponya

11 3:11Aliyeponywa alipokuwa akiambatana na Petro na Yohana, watu wote walishangaa mno, wakaja wakiwakimbilia pale ukumbi wa Solomoni. 12 3:12Petro alipoona watu wamekusanyika akawaambia, “Enyi Waisraeli, kwa nini mnastaajabu kuhusu jambo hili? Mbona mnatukazia macho kwa mshangao kana kwamba ni kwa uwezo wetu au utakatifu wetu tumemfanya mtu huyu kutembea? 13 3:13Mungu wa Abrahamu na Isaki na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Mwanawe Yesu, ambaye ninyi mlimtoa ahukumiwe kifo na mkamkana mbele ya Pilato, ingawa yeye alikuwa ameamua kumwachia aende zake. 14 3:14Ninyi mlimkataa huyo Mtakatifu na Mwenye Haki mkaomba mpewe yule muuaji. 15 3:15Hivyo mkamuua aliye chanzo cha uzima, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Sisi tu mashahidi wa mambo haya. 16 3:16Kwa imani katika jina la Yesu, huyu mtu mnayemwona na kumfahamu ametiwa nguvu. Ni kwa jina la Yesu na imani itokayo kwake ambayo imemponya kabisa huyu mtu, kama ninyi wote mnavyoona.

17 3:17“Sasa ndugu zangu, najua ya kuwa ninyi mlitenda bila kujua, kama walivyofanya viongozi wenu. 18 3:18Lakini kwa njia hii Mungu alitimiza kile ambacho alikuwa ametabiri kwa vinywa vya manabii wake wote, kwamba Kristo 3:18 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. atateswa. 19 3:19Tubuni basi mkamgeukie Mungu, dhambi zenu zifutwe, ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwepo kwake Bwana, 20 3:20naye apate kumtuma Kristo, ambaye ameteuliwa kwa ajili yenu, yaani Yesu. 21 3:21Ilimpasa mbingu zimpokee mpaka wakati wa kufanywa upya kila kitu, kama Mungu alivyoahidi zamani kupitia kwa vinywa vya manabii wake watakatifu. 22 3:22Kwa maana Mose alisema, ‘Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu. Itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia. 23 3:23Mtu yeyote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atatupiliwa mbali kabisa na watu wake.’

24 3:24“Naam, manabii wote tangu Samweli na waliokuja baada yake, wote walitabiri kuhusu siku hizi. 25 3:25Ninyi ndio wana wa manabii na wa Agano ambalo Mungu alifanya na baba zenu, akimwambia Abrahamu, ‘Kupitia kwa uzao wako, watu wote wa ulimwengu watabarikiwa.’ 26 3:26Mungu alipomfufua Yesu Mwanawe, alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kumgeuza kila mmoja wenu kutoka njia yake mbaya.”

4Petro Na Yohana Mbele Ya Baraza

1 4:1Wakati Petro na Yohana walipokuwa wakisema na watu, makuhani, mkuu wa walinzi wa Hekalu na Masadukayo wakawajia, 2 4:2huku wakiwa wamekasirika sana kwa sababu mitume walikuwa wanawafundisha watu na kuhubiri kwamba kuna ufufuo wa wafu ndani ya Yesu. 3 4:3Wakawakamata Petro na Yohana na kuwatia gerezani mpaka kesho yake kwa kuwa ilikuwa jioni. 4 4:4Lakini wengi waliosikia lile neno waliamini, idadi yao ilikuwa yapata wanaume 5,000.

5 4:5Kesho yake, viongozi wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria wakakusanyika Yerusalemu. 6 4:6Walikuwepo kuhani mkuu Anasi, Kayafa, Yohana, Iskanda, na wengi wa jamaa ya kuhani mkuu. 7 4:7Baada ya kuwasimamisha Petro na Yohana katikati yao, wakawauliza, “Ni kwa uwezo gani au kwa jina la nani mmefanya jambo hili?”

8 4:8Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akajibu, “Enyi watawala na wazee wa watu, 9 4:9kama leo tukihojiwa kwa habari ya mambo mema aliyotendewa yule kiwete na kuulizwa jinsi alivyoponywa, 10 4:10ijulikane kwenu nyote na kwa watu wote wa Israeli kwamba: Ni kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulubisha lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama mbele yenu akiwa mzima kabisa. 11 4:11Huyu ndiye

“ ‘jiwe ambalo ninyi wajenzi mlilikataa, ambalo limekuwa jiwe kuu la pembeni.’ 12 4:12Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Ujasiri Wa Petro Na Yohana Washangaza Watu

13 4:13Wale viongozi na wazee walipoona ujasiri wa Petro na Yohana na kujua ya kuwa walikuwa watu wa kawaida, wasio na elimu, walishangaa sana, wakatambua kwamba hawa watu walikuwa na Yesu. 14 4:14Lakini kwa kuwa walikuwa wanamwona yule kiwete aliyeponywa amesimama pale pamoja nao, hawakuweza kusema lolote kuwapinga. 15 4:15Wakawaamuru watoke nje ya Baraza la Wayahudi 4:15 Baraza la Wayahudi hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. wakati wakisemezana jambo hilo wao kwa wao. 16 4:16Wakaulizana, “Tuwafanyie nini watu hawa? Hatuwezi kukanusha muujiza huu mkubwa walioufanya ambao ni dhahiri kwa kila mtu Yerusalemu. 17 4:17Lakini ili kuzuia jambo hili lisiendelee kuenea zaidi kwa watu, ni lazima tuwaonye watu hawa ili wasiseme tena na mtu yeyote kwa jina la Yesu.” 18 4:18Kisha wakawaita tena ndani na kuwaamuru wasiseme wala kufundisha kamwe kwa hili jina la Yesu.

Imetupasa Kumtii Mungu Kuliko Wanadamu

19 4:19Lakini Petro na Yohana wakajibu, “Amueni ninyi wenyewe iwapo ni haki mbele za Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii Mungu. 20 4:20Lakini sisi hatuwezi kuacha kusema yale tuliyoyaona na kuyasikia.”

21 4:21Baada ya vitisho vingi, wakawaacha waende zao. Hawakuona njia yoyote ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu, kwa kuwa watu wote walikuwa wakimsifu Mungu kwa kile kilichokuwa kimetukia. 22 4:22Kwa kuwa umri wa yule mtu aliyekuwa ameponywa kwa muujiza ulikuwa zaidi ya miaka arobaini.

Maombi Ya Waumini

23 4:23Punde Petro na Yohana walipoachiliwa, walirudi kwa waumini wenzao wakawaeleza waliyoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee. 24 4:24Watu waliposikia hayo, wakainua sauti zao, wakamwomba Mungu kwa pamoja, wakisema, “Bwana Mwenyezi, uliyeziumba mbingu na nchi na bahari, na vitu vyote vilivyomo. 25 4:25Wewe ulisema kwa Roho Mtakatifu kupitia kwa kinywa cha baba yetu Daudi, mtumishi wako, ukasema:

“ ‘Mbona mataifa wanaghadhibika, na kabila za watu zinawaza ubatili? 26 4:26Wafalme wa dunia wamejipanga, na watawala wanakusanyika pamoja dhidi ya Bwana na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.’ 27 4:27Ni kweli Herode na Pontio Pilato pamoja na watu wa Mataifa na Waisraeli, walikusanyika katika mji huu dhidi ya mwanao mtakatifu Yesu uliyemtia mafuta. 28 4:28Wao wakafanya yale ambayo uweza wako na mapenzi yako yalikuwa yamekusudia yatokee tangu zamani. 29 4:29Sasa, Bwana angalia vitisho vyao na utuwezeshe sisi watumishi wako kulinena neno lako kwa ujasiri mkuu. 30 4:30Nyoosha mkono wako ili kuponya wagonjwa na kutenda ishara na miujiza kwa jina la Mwanao mtakatifu Yesu.”

31 4:31Walipokwisha kuomba, mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

Walioamini Washirikiana Mali Zao

32 4:32Wale walioamini wote walikuwa na moyo mmoja na nia moja. Wala hakuna hata mmoja aliyesema chochote alichokuwa nacho ni mali yake mwenyewe, lakini walishirikiana kila kitu walichokuwa nacho. 33 4:33Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwa Bwana Yesu kwa nguvu nyingi na neema ya Mungu ilikuwa juu yao wote. 34 4:34Wala hapakuwepo mtu yeyote miongoni mwao aliyekuwa mhitaji, kwa sababu mara kwa mara wale waliokuwa na mashamba na nyumba waliviuza, wakaleta thamani ya vitu vilivyouzwa, 35 4:35wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake.

36 4:36Yosefu, Mlawi kutoka Kipro, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake Mwana wa Faraja), 37 4:37aliuza shamba alilokuwa nalo, akaleta hizo fedha alizopata na kuziweka miguuni pa mitume.

5Anania Na Safira

1 5:1Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. 2 5:2Huku mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.

3 5:3Petro akamuuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4 5:4Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”

5 5:5Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. 6 5:6Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika.

7 5:7Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. 8 5:8Petro akamuuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”

9 5:9Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.”

10 5:10Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa. Nao wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. 11 5:11Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya.

Mitume Waponya Wengi

12 5:12Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Walioamini wote walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni. 13 5:13Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. 14 5:14Hata hivyo, waliomwamini Bwana wakazidi kuongezeka, wanaume na wanawake. 15 5:15Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. 16 5:16Pia watu wakakusanyika kutoka miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu. Hao wote wakaponywa.

Mitume Washtakiwa

17 5:17Kisha kuhani mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye, waliokuwa wa kundi la Masadukayo, wakajawa na wivu. 18 5:18Wakawakamata mitume na kuwatia gerezani. 19 5:19Lakini wakati wa usiku, malaika wa Bwana akaja, akafungua milango ya gereza na akawatoa nje. Akawaambia, 20 5:20“Nendeni, mkasimame Hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu mpya.”

21 5:21Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu.

Kuhani mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya baraza na wazee wote wa Israeli wakatuma wale mitume waletwe kutoka gerezani. 22 5:22Lakini wale walinzi wa Hekalu walipokwenda gerezani hawakuwakuta mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari. 23 5:23Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na askari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu yeyote ndani.” 24 5:24Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje.

25 5:25Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu mliowatia gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.” 26 5:26Ndipo yule mkuu wa walinzi wa Hekalu wakaenda pamoja na askari wakawaleta wale mitume, lakini bila ghasia kwa sababu waliogopa kupigwa mawe na watu.

27 5:27Wakiisha kuwaleta mitume wakawaamuru kusimama mbele ya baraza ili kuhani mkuu awahoji. 28 5:28“Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”

29 5:29Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30 5:30Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31 5:31Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32 5:32Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”

33 5:33Wale wajumbe wa baraza la wazee waliposikia haya, walijawa na ghadhabu, wakataka kuwaua mitume. 34 5:34Lakini Farisayo mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya baraza akaamuru mitume watolewe nje kwa muda. 35 5:35Ndipo alipowaambia wajumbe wa baraza, “Enyi watu wa Israeli, fikirini kwa uangalifu mnayotaka kuwatendea watu hawa. 36 5:36Kwa maana wakati uliopita, aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda, alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao 400 walioambatana naye. Lakini aliuawa, na wafuasi wake wote wakatawanyika, wakawa si kitu. 37 5:37Baada yake, alitokea Yuda Mgalilaya wakati wa kuorodhesha watu, naye akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye pia aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika. 38 5:38Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waacheni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu, haitafanikiwa. 39 5:39Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu, hamtaweza kuwazuia watu hawa. Badala yake mtajikuta mnapigana na Mungu.”

40 5:40Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Yesu, wakawaachia waende zao.

41 5:41Nao mitume wakatoka nje ya baraza, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Yesu. 42 5:42Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo. 5:42 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.

Mateso Na Kuenea Kwa Injili (6:1–9:31) 6Saba Wachaguliwa Kuhudumu

1 6:1Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manungʼuniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku. 2 6:2Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani. 3 6:3Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, 4 6:4nasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”

5 6:5Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia. 6 6:6Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono juu yao.

7 6:7Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu hata makuhani wengi wakaitii ile imani.

Kukamatwa Kwa Stefano

8 6:8Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu. 9 6:9Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano. 10 6:10Lakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake.

11 6:11Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Mose na dhidi ya Mungu.”

Stefano Afikishwa Mbele Ya Baraza

12 6:12Wakawachochea watu, wazee na walimu wa Sheria, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya baraza. 13 6:13Wakaweka mashahidi wa uongo ambao walishuhudia wakisema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Sheria. 14 6:14Kwa maana tumemsikia akisema kwamba Yesu wa Nazareti atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Mose.”

15 6:15Watu wote waliokuwa wameketi katika baraza wakimkazia macho Stefano, wakaona uso wake unangʼaa kama uso wa malaika.

7Hotuba Ya Stefano

1 7:1Ndipo kuhani mkuu akamuuliza Stefano, “Je, mashtaka haya ni ya kweli?”

2 7:2Stefano akajibu, “Ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni! Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Abrahamu, alipokuwa bado yuko Mesopotamia, kabla hajaishi Harani, 3 7:3akamwambia, ‘Ondoka kutoka nchi yako na kutoka kwa jamii yako, uende hadi nchi nitakayokuonyesha.’

4 7:4“Hivyo aliondoka katika nchi ya Wakaldayo akaenda kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu akamtoa huko akamleta katika nchi hii ambayo mnaishi sasa. 5 7:5Mungu hakumpa urithi wowote katika nchi hii, hakumpa hata mahali pa kuweka wayo mmoja. Bali Mungu alimwahidi kuwa yeye na uzao wake baada yake wangeirithi hii nchi, ingawa wakati huo Abrahamu hakuwa na mtoto. 6 7:6Mungu akasema naye hivi: ‘Wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne.’ 7 7:7Mungu akasema, ‘Lakini mimi nitaliadhibu taifa watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka katika nchi hiyo na wataniabudu mahali hapa.’ 8 7:8Ndipo akampa Abrahamu Agano la tohara. Naye Abrahamu akamzaa Isaki na kumtahiri siku ya nane. Baadaye Isaki akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa wale wazee wetu kumi na wawili.

9 7:9“Kwa sababu wazee wetu walimwonea wivu Yosefu ndugu yao, walimuuza kama mtumwa huko Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye. 10 7:10Akamwokoa kutoka mateso yote yaliyompata, tena akampa kibali na hekima aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri, ambaye alimweka kuwa mtawala juu ya Misri na juu ya jumba lote la kifalme.

11 7:11“Basi kukawa na njaa katika nchi yote ya Misri na Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa, nao baba zetu wakawa hawana chakula. 12 7:12Lakini Yakobo aliposikia kwamba kuna nafaka huko Misri, aliwatuma baba zetu, wakaenda huko kwa mara yao ya kwanza. 13 7:13Walipokwenda mara ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa ndugu zake, nao ndugu zake Yosefu wakajulishwa kwa Farao. 14 7:14Ndipo Yosefu akawatuma kumleta Yakobo baba yake pamoja na jamaa yake yote, jumla yao walikuwa watu sabini na watano. 15 7:15Hivyo Yakobo akaenda Misri ambako yeye na baba zetu walifia. 16 7:16Miili yao ilirudishwa Shekemu na kuzikwa katika kaburi ambalo Abrahamu alinunua kutoka kwa wana wa Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.

17 7:17“Lakini wakati ulipokuwa unakaribia wa kutimizwa kwa ile ahadi ambayo Mungu alikuwa amempa Abrahamu, watu wetu walizidi kuongezeka sana huko Misri. 18 7:18Ndipo mfalme mwingine ambaye hakujua lolote kuhusu Yosefu akatawala Misri. 19 7:19Huyu mfalme akawatendea watu wetu hila na kuwatesa baba zetu kwa kuwalazimisha wawatupe watoto wao wachanga ili wafe.

20 7:20“Wakati huo Mose alizaliwa, naye hakuwa mtoto wa kawaida. Akalelewa nyumbani kwa baba yake kwa muda wa miezi mitatu. 21 7:21Waliposhindwa kumficha zaidi, wakamweka nje mtoni na binti Farao akamchukua akamtunza kama mtoto wake mwenyewe. 22 7:22Mose akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa mtu hodari kwa maneno na matendo.

23 7:23“Mose alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kuwatembelea ndugu zake Waisraeli. 24 7:24Aliona mmoja wao akidhulumiwa na Mmisri, akamtetea yule aliyeonewa, akampiga yule Mmisri akamuua kulipiza kisasi. 25 7:25Mose alidhani kuwa ndugu zake wangetambua kwamba Mungu anamtumia ili kuwaokoa, lakini wao hawakuelewa. 26 7:26Siku iliyofuata Mose aliwakuta Waisraeli wawili wakigombana, akajaribu kuwapatanisha kwa kuwaambia, ‘Enyi watu, ninyi ni ndugu, mbona mnataka kudhulumiana?’

27 7:27“Lakini yule mtu aliyekuwa akimdhulumu mwenzake akamsukuma Mose kando, akamuuliza, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? 28 7:28Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?’ 29 7:29Mose aliposikia maneno haya, alikimbilia huko Midiani alikokaa kama mgeni, naye akapata watoto wawili wa kiume.

30 7:30“Basi baada ya miaka arobaini kupita, malaika wa Mungu akamtokea Mose jangwani karibu na Mlima Sinai katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto. 31 7:31Alipoona mambo haya, alishangaa yale maono. Aliposogea ili aangalie kwa karibu, akaisikia sauti ya Bwana, ikisema: 32 7:32‘Mimi ndimi Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Yakobo.’ Mose alitetemeka kwa hofu na hakuthubutu kutazama.

33 7:33“Ndipo Bwana akamwambia, ‘Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu. 34 7:34Hakika nimeona mateso ya watu wangu huko Misri. Nimesikia kilio chao cha uchungu, nami nimeshuka ili niwaokoe. Basi sasa njoo, nami nitakutuma Misri.’

35 7:35“Huyu ndiye Mose yule waliyemkataa wakisema, ‘Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu?’ Alikuwa ametumwa na Mungu mwenyewe kuwa mtawala na mkombozi wao, kwa njia ya yule malaika aliyemtokea katika kile kichaka. 36 7:36Aliwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri, baada ya kufanya ishara na maajabu mengi huko Misri, katika Bahari ya Shamu, 7:36 Yaani Bahari ya Mafunjo. na katika jangwa kwa muda wa miaka arobaini.

37 7:37“Huyu ndiye yule Mose aliyewaambia Waisraeli, ‘Mungu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe.’ 38 7:38Huyu ndiye yule Mose aliyekuwa katika kusanyiko huko jangwani, ambaye malaika alisema naye pamoja na baba zetu kwenye Mlima Sinai, naye akapokea maneno yaliyo hai ili atupatie.

39 7:39“Lakini baba zetu walikataa kumtii Mose, badala yake wakamkataa na kuielekeza mioyo yao Misri tena. 40 7:40Wakamwambia Aroni, ‘Tufanyie miungu watakaotuongoza, kwa maana mtu huyu Mose aliyetutoa nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.’ 41 7:41Huu ni ule wakati walitengeneza sanamu katika umbo la ndama, wakailetea sadaka kufanya maadhimisho kwa ajili ya kile kitu walichokitengeneza kwa mikono yao wenyewe. 42 7:42Ndipo Mungu akageuka, akawaacha waabudu jeshi lote la mbinguni, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Manabii:

“ ‘Je, mliniletea dhabihu na sadaka kwa miaka arobaini kule jangwani, ee nyumba ya Israeli? 43 7:43La, ninyi mliinua madhabahu ya Moleki, na nyota ya mungu wenu Refani, vinyago mlivyotengeneza ili kuviabudu. Kwa hiyo nitawapeleka mbali’ kuliko Babeli.

44 7:44“Baba zetu walikuwa na lile Hema la Ushuhuda huko jangwani. Lilikuwa limetengenezwa kama Mungu alivyokuwa amemwelekeza Mose, kulingana na kielelezo alichoona. 45 7:45Baba zetu wakiisha kulipokea hema kwa kupokezana wakiongozwa na Yoshua katika milki ya nchi kutoka kwa yale mataifa ambayo Mungu aliyafukuza mbele yao, nalo likadumu katika nchi mpaka wakati wa Daudi, 46 7:46ambaye alipata kibali kwa Mungu, naye akaomba kwamba ampatie Mungu wa Yakobo maskani. 47 7:47Lakini alikuwa Solomoni ndiye alimjengea Mungu nyumba.

48 7:48“Hata hivyo, Yeye Aliye Juu Sana hakai kwenye nyumba zilizojengwa kwa mikono ya wanadamu. Kama nabii alivyosema:

49 7:49“ ‘Mbingu ni kiti changu cha enzi, nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Mtanijengea nyumba ya namna gani? asema Bwana. Au mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi? 50 7:50Je, mkono wangu haukufanya vitu hivi vyote?’

51 7:51“Enyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zenu. 52 7:52Je, kuna nabii gani ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji. 53 7:53Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”

Stefano Apigwa Mawe

54 7:54Waliposikia haya wakaghadhibika, wakamsagia meno. 55 7:55Lakini yeye Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, na Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu. 56 7:56Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.”

57 7:57Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja. 58 7:58Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka mavazi yao miguuni mwa kijana mmoja ambaye jina lake aliitwa Sauli.

59 7:59Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 7:60Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.

81 8:1Naye Sauli alikuwepo pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano.

Kanisa Lateswa Na Kutawanyika

Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Uyahudi na Samaria. 2 8:2Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwombolezea sana. 3 8:3Lakini kwa habari ya Sauli alikuwa analiharibu kanisa, akiingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanawake na wanaume na kuwatupa gerezani.

Filipo Ahubiri Injili Samaria

4 8:4Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipokwenda. 5 8:5Filipo akateremkia mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo 8:5 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. 6 8:6Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema. 7 8:7Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. 8 8:8Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.

Simoni Mchawi

9 8:9Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu, 10 8:10nao watu wote wakubwa kwa wadogo wakamsikiliza na kumaka, wakisema “Mtu huyu ndiye uweza wa Mungu ujulikanao kama ‘Uweza Mkuu.’ ” 11 8:11Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake. 12 8:12Lakini watu walipomwamini Filipo alipohubiri habari njema za Ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa wanaume na wanawake. 13 8:13Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.

14 8:14Basi mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria wamelipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko. 15 8:15Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu, 16 8:16kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa bado hajawashukia hata mmoja ila wamebatizwa tu katika jina la Bwana Yesu. 17 8:17Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho Mtakatifu.

18 8:18Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho Mtakatifu mitume walipoweka mikono juu yao, akataka kuwapa fedha 19 8:19akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho Mtakatifu.”

20 8:20Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! 21 8:21Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. 22 8:22Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Bwana. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako. 23 8:23Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.”

24 8:24Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili hayo mliyosema lolote yasinitukie.”

25 8:25Nao walipokwisha kutoa ushuhuda na kuhubiri neno la Bwana, wakarudi Yerusalemu wakihubiri Injili katika vijiji vingi vya Samaria.

Filipo Na Towashi Wa Kushi

26 8:26Basi malaika wa Bwana akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara itokayo Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.” 27 8:27Hivyo akaondoka. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa amekwenda Yerusalemu ili kuabudu, 28 8:28naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi garini mwake akisoma kitabu cha nabii Isaya. 29 8:29Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.”

30 8:30Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamuuliza, “Je, unaelewa hayo usomayo?”

31 8:31Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye.

32 8:32Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la Maandiko:

“Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni, kama mwana-kondoo anyamazavyo mbele yake yule amkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake. 33 8:33Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake. Nani awezaye kueleza juu ya kizazi chake? Kwa maana maisha yake yaliondolewa kutoka duniani.”

34 8:34Yule towashi akamuuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?” 35 8:35Ndipo Filipo akaanza kutumia fungu lile la Maandiko, akamweleza habari njema za Yesu.

36 8:36Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamuuliza Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?” [ 37 8:37Filipo akamwambia, “Kama ukiamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Akajibu, “Naamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”] 38 8:38Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Wakateremka kwenye maji wote wawili, yule towashi na Filipo, naye Filipo akambatiza. 39 8:39Nao walipopanda kutoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi. 40 8:40Filipo akajikuta yuko Azoto, akasafiri akihubiri Injili katika miji yote mpaka alipofika Kaisaria.

9Kuokoka Kwa Sauli (Matendo 22:6-16; 26:12-18)

1 9:1Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani mkuu, 2 9:2naye akamwomba kuhani mkuu ampe barua za kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mtu yeyote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu. 3 9:3Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. 4 9:4Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”

5 9:5Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”

Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa. 6 9:6 Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”

7 9:7Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. 8 9:8Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. 9 9:9Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa chochote.

10 9:10Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!”

Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”

11 9:11Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, 12 9:12 katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”

13 9:13Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu. 14 9:14Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”

15 9:15Lakini Bwana akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo changu kiteule nilichokichagua, apate kulichukua Jina langu kwa watu wa Mataifa na wafalme wao na mbele ya watu wa Israeli. 16 9:16 Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”

17 9:17Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.” 18 9:18Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa. 19 9:19Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski.

Sauli Ahubiri Dameski

20 9:20Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba “Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu” 21 9:21Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu huko Yerusalemu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wafungwa mbele ya viongozi wa makuhani?” 22 9:22Sauli akazidi kuwa hodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo. 9:22 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.

23 9:23Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakafanya shauri kumuua Sauli. 24 9:24Lakini shauri lao likajulikana kwa Sauli. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, usiku na mchana ili wapate kumuua. 25 9:25Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani.

Sauli Huko Yerusalemu

26 9:26Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi. 27 9:27Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski. 28 9:28Kwa hiyo Sauli akakaa nao akitembea kwa uhuru kila mahali huko Yerusalemu, akihubiri kwa ujasiri katika jina la Bwana. 29 9:29Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani lakini wao walijaribu kumuua. 30 9:30Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso.

31 9:31Ndipo kanisa katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria likafurahia wakati wa amani. Likatiwa nguvu, na kwa faraja ya Roho Mtakatifu, idadi yake ikazidi kuongezeka, na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana.

Matendo Ya Petro (9:32–12:25) Kuponywa Kwa Ainea

32 9:32Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alikwenda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida. 33 9:33Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, ambaye alikuwa amepooza na kwa muda wa miaka minane alikuwa hajaondoka kitandani. 34 9:34Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka. 35 9:35Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana.

Petro Amfufua Dorkasi

36 9:36Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi 9:36 Tabitha kwa Kiaramu na Dorkasi kwa Kiaramu yote yamaanisha Paa.). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini. 37 9:37Wakati huo akaugua, akafa na wakiisha kuuosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani. 38 9:38Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”

39 9:39Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao, naye alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonyesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.

40 9:40Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. 41 9:41Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai. 42 9:42Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana. 43 9:43Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.

10Kornelio Amwita Petro

1 10:1Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu jina lake Kornelio, ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. 2 10:2Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima. 3 10:3Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”

4 10:4Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”

Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. 5 10:5Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro. 6 10:6Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”

7 10:7Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia. 8 10:8Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.

Maono Ya Petro

9 10:9Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. 10 10:10Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. 11 10:11Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. 12 10:12Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. 13 10:13Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”

14 10:14Petro akajibu, “La hasha Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”

15 10:15Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”

16 10:16Jambo hili lilitokea mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni.

17 10:17Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango. 18 10:18Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.

19 10:19Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta. 20 10:20Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”

21 10:21Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”

22 10:22Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” 23 10:23Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani, akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.

Petro Nyumbani Mwa Kornelio

24 10:24Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa yake na marafiki zake wa karibu. 25 10:25Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni pake kwa heshima. 26 10:26Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”

27 10:27Petro alipokuwa akizungumza naye akaingia ndani na kukuta watu wengi wamekusanyika. 28 10:28Akawaambia, “Mnajua kabisa kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi. 29 10:29Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”

30 10:30Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizongʼaa akasimama mbele yangu, 31 10:31akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako kwa maskini zimekumbukwa mbele za Mungu. 32 10:32Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’ 33 10:33Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”

Hotuba Ya Petro

34 10:34Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35 10:35Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye. 36 10:36Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote. 37 10:37Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji: 38 10:38Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.

39 10:39“Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani. 40 10:40Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41 10:41Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42 10:42Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alitiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. 43 10:43Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”

Watu Wa Mataifa Wapokea Roho Mtakatifu

44 10:44Wakati Petro alikuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45 10:45Wale wa tohara walioamini waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46 10:46Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.

Ndipo Petro akasema, 47 10:47“Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48 10:48Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.

11Petro Aeleza Alivyotumwa Kwa Watu Wa Mataifa

1 11:1Mitume na ndugu walioamini waliokuwa huko Uyahudi wakasikia kuwa watu wa Mataifa nao wamepokea neno la Mungu. 2 11:2Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, wale wa tohara waliokuwa wameamini wakamshutumu, 3 11:3wakisema, “Ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.”

4 11:4Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema, 5 11:5“Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia. 6 11:6Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne wa nchini, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani. 7 11:7Ndipo nikasikia sauti ikiniambia, ‘Petro, ondoka uchinje na ule.’

8 11:8“Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu chochote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’

9 11:9“Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.’ 10 11:10Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.

11 11:11“Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa. 12 11:12Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio. 13 11:13Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro. 14 11:14Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’

15 11:15“Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo. 16 11:16Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17 11:17Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”

18 11:18Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu wa Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”

Kanisa La Antiokia

19 11:19Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokana na kifo cha Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu yeyote isipokuwa Wayahudi. 20 11:20Lakini baadhi yao walikuwepo watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakiwahubiria habari njema za Bwana Yesu. 21 11:21Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana.

22 11:22Habari hizi zilipofika masikioni mwa kanisa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia. 23 11:23Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana kwa mioyo yao yote. 24 11:24Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu, mwenye imani, nayo idadi kubwa ya watu wakaongezeka kwa Bwana.

25 11:25Kisha Barnaba akaenda Tarso kumtafuta Sauli, 26 11:26naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na kanisa na kufundisha idadi kubwa ya watu. Ilikuwa ni katika kanisa la Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi waliitwa Wakristo.

27 11:27Wakati huo manabii walishuka toka Yerusalemu hadi Antiokia. 28 11:28Mmoja wao, jina lake Agabo, akasimama akatabiri kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itaenea ulimwengu mzima. Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio. 29 11:29Mitume wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo alio nao, atoe msaada kwa ajili ya ndugu wanaoishi Uyahudi. 30 11:30Wakafanya hivyo, misaada yao ikapelekwa kwa wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

12Yakobo Auawa, Petro Atiwa Gerezani

1 12:1Wakati huo huo Mfalme Herode Agripa aliwakamata baadhi ya watu wa kanisa. 2 12:2Akaamuru Yakobo, ndugu yake Yohana, auawe kwa upanga. 3 12:3Alipoona jambo hilo limewapendeza Wayahudi, akaendelea, akamkamata pia Petro. Hii ilitokea wakati wa Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. 4 12:4Baada ya kumkamata alimtia gerezani, chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari, vyenye askari wanne kila kimoja. Herode alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka mbele ya watu baada ya Pasaka.

5 12:5Kwa hiyo Petro akawekwa gerezani, lakini kanisa lilikuwa likimwombea kwa Mungu kwa bidii.

6 12:6Usiku ule kabla ya siku ambayo Herode Agripa alikuwa amekusudia kumtoa na kumfanyia mashtaka, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili, akiwa amefungwa kwa minyororo miwili. Nao walinzi wa zamu walikuwa wakilinda penye lango la gereza. 7 12:7Ghafula malaika wa Bwana akatokea na nuru ikamulika mle ndani ya gereza. Yule malaika akampiga Petro ubavuni na kumwamsha, akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo ikaanguka kutoka mikononi mwa Petro.

8 12:8Yule malaika akamwambia, “Vaa nguo zako na viatu vyako.” Petro akafanya hivyo. Kisha akamwambia, “Jifunge vazi lako na unifuate.” 9 12:9Petro akatoka mle gerezani akiwa amefuatana na yule malaika. Hakujua wakati huo kuwa yaliyokuwa yakitukia yalikuwa kweli. Alidhani kuwa anaona maono. 10 12:10Wakapita lindo la kwanza na la pili, ndipo wakafika kwenye lango la chuma linaloelekea mjini. Lango likawafungukia lenyewe, nao wakapita hapo wakatoka nje. Baada ya kutembea umbali wa mtaa mmoja, ghafula yule malaika akamwacha Petro.

11 12:11Ndipo Petro akarudiwa na fahamu, akasema, “Sasa ninajua bila shaka yoyote kuwa Bwana amemtuma malaika wake na kuniokoa kutoka makucha ya Herode Agripa na kutoka matazamio yote ya Wayahudi.”

12 12:12Mara Petro alipotambua hili alikwenda nyumbani kwa Maria, mama yake Yohana aliyeitwa pia Marko, ambako watu wengi walikuwa wamekutana kwa maombi. 13 12:13Petro alipobisha hodi kwenye lango la nje, mtumishi wa kike jina lake Roda, akaja kumfungulia. 14 12:14Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi mno akarudi bila kufungua na kuwaeleza kwamba, “Petro yuko langoni!”

15 12:15Wakamwambia yule mtumishi wa kike, “Umerukwa na akili.” Alipozidi kusisitiza kuwa ni kweli, wakasema, “Lazima awe ni malaika wake.”

16 12:16Lakini Petro aliendelea kugonga langoni, nao walipofungua lango na kumwona Petro, walistaajabu sana. 17 12:17Yeye akawaashiria kwa mkono wake wanyamaze kimya, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Naye akaongeza kusema, “Waelezeni Yakobo na ndugu wengine habari hizi.” Kisha akaondoka akaenda sehemu nyingine.

18 12:18Kulipokucha kukawa na fadhaa kubwa miongoni mwa wale askari kuhusu yaliyomtukia Petro. 19 12:19Baada ya Herode kuamuru atafutwe kila mahali na bila kumpata, aliwahoji wale askari walinzi kisha akatoa amri wauawe. Basi Herode Agripa akatoka Uyahudi akaenda Kaisaria, akakaa huko kwa muda.

Kifo Cha Herode Agripa

20 12:20Basi Herode Agripa alikuwa amekasirishwa sana na watu wa Tiro na Sidoni. Hivyo watu wa miji hiyo miwili wakaungana pamoja wakatafuta kukutana naye. Wakiisha kuungwa mkono na Blasto, mtumishi maalum wa Mfalme Herode Agripa aliyeaminika, wakaomba mapatano ya amani maana nchi zao zilitegemea nchi ya huyo mfalme kwa mahitaji yao ya chakula.

21 12:21Katika siku iliyochaguliwa Herode Agripa akavaa mavazi yake ya kifalme, akaketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu. 22 12:22Watu waliokuwa wamekusanyika wakapiga kelele, wakisema, “Hii si sauti ya mwanadamu, bali ni ya Mungu.” 23 12:23Ghafula, kwa kuwa Herode hakumpa Mungu utukufu, malaika wa Bwana akampiga, naye akaliwa na chango, akafa.

24 12:24Lakini neno la Mungu likaendelea mbele na kuenea, nao wengi wakaambatana nalo.

25 12:25Barnaba na Sauli walipomaliza ile huduma yao iliyowapeleka, wakarudi Yerusalemu wakiwa pamoja na Yohana aitwaye Marko.

Safari Ya Kwanza Ya Paulo Kueneza Injili (13:1–14:28) 13Barnaba Na Sauli Wanatumwa

1 13:1Katika kanisa huko Antiokia ya Shamu walikuwako manabii na walimu, yaani: Barnaba, Simeoni aitwaye Nigeri, Lukio Mkirene, Manaeni aliyekuwa amelelewa pamoja na Mfalme Herode Agripa, na Sauli. 2 13:2Walipokuwa wakimwabudu Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, “Nitengeeni Sauli na Barnaba kwa kazi ile maalum niliyowaitia.” 3 13:3Ndipo baada ya kufunga na kuomba, wakawawekea mikono yao na wakawatuma waende zao.

Barnaba Na Sauli Waenda Kipro

4 13:4Hivyo, wakiwa wametumwa na Roho Mtakatifu, wakashuka kwenda Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini mpaka kisiwa cha Kipro. 5 13:5Walipowasili katika mji wa Salami, wakahubiri neno la Mungu katika sinagogi la Wayahudi. Pia walikuwa na Yohana Marko kuwa msaidizi wao.

6 13:6Walipokwisha kupita katika nchi zote hizo wakafika Pafo, ambapo walikutana na Myahudi mmoja mchawi aliyekuwa nabii wa uongo, jina lake Bar-Yesu. 7 13:7Mtu huyu alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mtu mwenye hekima aliyekuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala wa kile kisiwa. Sergio Paulo akawaita Sauli na Barnaba akitaka kusikia neno la Mungu. 8 13:8Lakini Elima yule mchawi (hii ndiyo maana ya jina lake), aliwapinga Barnaba na Sauli na kujaribu kumpotosha yule mkuu wa kile kisiwa aiache imani. 9 13:9Ndipo Sauli, ambaye pia aliitwa Paulo, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akamkazia macho Elima huyo mchawi, 10 13:10akamwambia, “Ewe mwana wa ibilisi, wewe ni adui wa kila kilicho haki! Umejaa kila aina ya udanganyifu na ulaghai. Je, hutaacha kuzipotosha njia za Bwana zilizonyooka? 11 13:11Nawe sasa sikiliza, mkono wa Bwana u dhidi yako. Utakuwa kipofu, wala hutaona jua kwa muda.”

Mara ukungu na giza vikamfunika, naye akaenda huku na huko akitafuta mtu wa kumshika mkono ili amwonyeshe njia. 12 13:12Yule mkuu wa kile kisiwa alipoona yaliyotukia, akaamini kwa sababu alistaajabishwa na mafundisho kuhusu Bwana.

Paulo Na Barnaba Huko Antiokia Ya Pisidia

13 13:13Kisha Paulo na wenzake wakasafiri toka Pafo wakafika Perga huko Pamfilia. Lakini, Yohana Marko akawaacha huko, akarejea Yerusalemu. 14 13:14Kutoka Perga wakaendelea hadi Antiokia ya Pisidia. Siku ya Sabato wakaingia ndani ya sinagogi, wakaketi. 15 13:15Baada ya Sheria ya Mose na Kitabu cha Manabii kusomwa, viongozi wa sinagogi wakawatumia ujumbe wakisema, “Ndugu, kama mna neno la kuwafariji watu hawa, tafadhali lisemeni.”

16 13:16Paulo akasimama, akawapungia mkono na kusema: “Enyi wanaume wa Israeli na ninyi nyote mnaomcha Mungu. 17 13:17Mungu wa watu hawa wa Israeli aliwachagua baba zetu, akawafanya kustawi walipokuwa huko Misri, kwa uwezo mwingi akawaongoza na kuwatoa katika nchi ile. 18 13:18Kwa muda wa miaka arobaini alivumilia matendo yao walipokuwa jangwani. 19 13:19Naye baada ya kuyaangamiza mataifa saba waliokuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, akawapa Waisraeli nchi yao iwe urithi wao. 20 13:20Haya yote yalichukua kama muda wa miaka 450.

“Baada ya haya, Mungu akawapa waamuzi mpaka wakati wa nabii Samweli. 21 13:21Ndipo watu wakaomba wapewe mfalme, naye Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini, aliyetawala kwa miaka arobaini. 22 13:22Baada ya kumwondoa Sauli katika ufalme, akawainulia Daudi kuwa mfalme wao. Mungu pia alimshuhudia, akisema, ‘Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayetimiza mapenzi yangu yote.’

23 13:23“Kutoka uzao wa mtu huyu, Mungu amewaletea Israeli Mwokozi Yesu, kama alivyoahidi. 24 13:24Kabla ya kuja kwa Yesu, Yohana alihubiri toba na ubatizo kwa watu wote wa Israeli. 25 13:25Yohana alipokuwa anakamilisha kazi yake, alisema: ‘Ninyi mnadhani mimi ni nani? Mimi si yeye. La hasha, lakini yeye yuaja baada yangu, ambaye mimi sistahili kufungua kamba za viatu vya miguu yake.’

26 13:26“Ndugu zangu, wana wa Abrahamu, nanyi watu wa Mataifa mnaomcha Mungu, ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu. 27 13:27Kwa sababu wakaao Yerusalemu na viongozi wao hawakumtambua wala kuelewa maneno ya manabii yasomwayo kila Sabato, bali waliyatimiza maneno hayo kwa kumhukumu yeye. 28 13:28Ijapokuwa hawakupata sababu yoyote ya kumhukumu kifo, walimwomba Pilato aamuru auawe. 29 13:29Walipokwisha kufanya yale yote yaliyoandikwa kumhusu, walimshusha kutoka msalabani na kumzika kaburini. 30 13:30Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. 31 13:31Naye kwa siku nyingi akawatokea wale waliokuwa pamoja naye kuanzia Galilaya hadi Yerusalemu. Nao sasa wamekuwa mashahidi wake kwa watu wetu.

32 13:32“Nasi tunawaletea habari njema, kwamba yale Mungu aliyowaahidi baba zetu 33 13:33sasa ameyatimiza kwetu sisi watoto wao, kwa kumfufua Yesu, kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili:

“ ‘Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuzaa.’ 34 13:34Kwa kuwa Mungu alimfufua kutoka kwa wafu asioze kamwe, alitamka maneno haya: “ ‘Nitakupa wewe baraka takatifu zilizo za hakika nilizomwahidi Daudi.’ 35 13:35Kama ilivyosemwa mahali pengine katika Zaburi, “ ‘Hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.’

36 13:36“Kwa maana Daudi akiisha kulitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake, alilala; akazikwa pamoja na baba zake na mwili wake ukaoza. 37 13:37Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu hakuona uharibifu.

38 13:38“Kwa hiyo ndugu zangu, nataka ninyi mjue kwamba kwa kupitia huyu Yesu msamaha wa dhambi unatangazwa kwenu. 39 13:39Kwa kupitia yeye, kila mtu amwaminiye anahesabiwa haki kwa kila kitu ambacho asingeweza kuhesabiwa haki kwa sheria ya Mose. 40 13:40Kwa hiyo jihadharini ili yale waliyosema manabii yasiwapate:

41 13:41“ ‘Angalieni, enyi wenye dhihaka, mkastaajabu, mkaangamie, kwa maana nitatenda jambo wakati wenu ambalo hamtasadiki, hata kama mtu akiwaambia.’ ”

42 13:42Paulo na Barnaba walipokuwa wakitoka nje ya sinagogi, watu wakawaomba wazungumze tena mambo hayo Sabato iliyofuata. 43 13:43Baada ya kusanyiko la Sinagogi kutawanyika, wengi wa Wayahudi na waongofu wa dini ya Kiyahudi wakawafuata Paulo na Barnaba, wakazungumza nao na kuwahimiza wadumu katika neema ya Mungu.

44 13:44Sabato iliyofuata, karibu watu wote wa mji walikuja kusikiliza neno la Bwana. 45 13:45Lakini Wayahudi walipoona ule umati mkubwa wa watu walijawa na wivu, wakayakanusha maneno Paulo aliyokuwa akisema.

46 13:46Ndipo Paulo na Barnaba wakawajibu kwa ujasiri, wakisema, “Ilitupasa kunena nanyi neno la Mungu kwanza. Lakini kwa kuwa mmelikataa, mkajihukumu wenyewe kuwa hamstahili uzima wa milele, sasa tunawageukia watu wa Mataifa. 47 13:47Kwa maana hili ndilo Bwana alilotuamuru:

“ ‘Nimewafanya ninyi kuwa nuru kwa watu wa Mataifa, ili mpate kuuleta wokovu hadi miisho ya dunia.’ ”

48 13:48Watu wa Mataifa waliposikia haya wakafurahi na kulitukuza neno la Bwana; nao wote waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

49 13:49Neno la Bwana likaenea katika eneo lile lote. 50 13:50Lakini Wayahudi wakawachochea wanawake wenye kumcha Mungu, wenye vyeo pamoja na watu maarufu katika mji, wakachochea mateso dhidi ya Paulo na Barnaba na kuwafukuza kutoka eneo hilo. 51 13:51Hivyo Paulo na Barnaba wakakungʼuta mavumbi ya miguu yao ili kuwapinga, nao wakaenda Ikonio. 52 13:52Wanafunzi wakajawa na furaha na Roho Mtakatifu.

14Paulo Na Barnaba Huko Ikonio

1 14:1Huko Ikonio Paulo na Barnaba waliingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi kama ilivyokuwa desturi yao. Huko wakahubiri kwa uwezo mkubwa kiasi kwamba Wayahudi pamoja na watu wa Mataifa wakaamini. 2 14:2Lakini wale Wayahudi waliokataa kuamini, wakawachochea watu wa Mataifa, wakatia chuki ndani ya mioyo yao dhidi ya wale walioamini. 3 14:3Hivyo Paulo na Barnaba wakakaa huko kwa muda wa kutosha wakihubiri kwa ujasiri juu ya Bwana, ambaye alithibitisha ujumbe wa neema yake kwa kuwawezesha kufanya ishara na miujiza. 4 14:4Lakini watu wa mji ule waligawanyika, wengine wakakubaliana na Wayahudi na wengine na mitume. 5 14:5Watu wa Mataifa na Wayahudi wakajiunga na baadhi ya viongozi, wakafanya mpango wa kuwatendea mitume mabaya na kuwapiga mawe. 6 14:6Lakini mitume walipopata habari hizi wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia na sehemu zilizopakana nayo. 7 14:7Huko wakaendelea kuhubiri habari njema.

Paulo Na Barnaba Huko Listra

8 14:8Katika mji wa Listra, alikuwako kiwete, ambaye alikuwa amelemaa tangu kuzaliwa na hakuwa ametembea kamwe. 9 14:9Alimsikiliza Paulo alipokuwa akihubiri. Paulo alipomtazama akaona ana imani ya kuponywa. 10 14:10Paulo akapaza sauti, “Simama kwa miguu yako!” Mara yule mtu akasimama upesi akaanza kutembea!

11 14:11Ule umati wa watu ulipoona yaliyokuwa yamefanywa na Paulo, wakapiga kelele kwa lugha yao ya Kilikaonia wakasema, “Miungu imetushukia katika umbo la binadamu!” 12 14:12Wakamwita Barnaba Zeu na Paulo wakamwita Herme kwa kuwa ndiye alikuwa msemaji mkuu. 13 14:13Kuhani wa Zeu, ambaye hekalu lake lilikuwa nje kidogo tu ya mji, akaleta mafahali na mashada ya maua penye lango la mji kwa sababu yeye na ule umati wa watu walitaka kuwatolea dhabihu.

14 14:14Lakini mitume Paulo na Barnaba waliposikia haya, wakararua nguo zao, wakawaendea wale watu kwa haraka, wakawapigia kelele, wakisema, 15 14:15“Enyi watu, kwa nini mnafanya mambo haya? Sisi ni wanadamu tu kama ninyi! Tunawaletea habari njema, tukiwaambia kwamba mgeuke mtoke katika mambo haya yasiyofaa, mmwelekee Mungu aliye hai, aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo. 16 14:16Zamani aliwaachia mataifa waishi walivyotaka. 17 14:17Lakini hakuacha kuwaonyesha watu uwepo wake: Ameonyesha wema kwa kuwanyeshea mvua toka mbinguni na kuwapa mazao kwa majira yake, naye amewapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu na furaha.” 18 14:18Hata kwa maneno haya yote, ilikuwa vigumu kuuzuia ule umati wa watu kuwatolea dhabihu.

19 14:19Ndipo wakaja baadhi ya Wayahudi kutoka Antiokia na Ikonio wakawashawishi wale watu, wakampiga Paulo kwa mawe, wakamburuta hadi nje ya mji, wakidhani amekufa. 20 14:20Lakini baada ya wanafunzi kukusanyika akainuka na kurudi mjini. Kesho yake yeye na Barnaba wakaondoka kwenda Derbe.

Paulo Na Barnaba Warudi Antiokia Huko Syria

21 14:21Wakahubiri habari njema katika mji huo na kupata wanafunzi wengi. Kisha wakarudi Listra, Ikonio na Antiokia, 22 14:22wakiwaimarisha wanafunzi na kuwatia moyo waendelee kudumu katika imani. Wakawaonya wakisema, “Imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa kupitia katika taabu nyingi.” 23 14:23Nao baada ya kuwateua wazee katika kila kanisa, kwa kufunga na kuomba wakawakabidhi kwa Bwana waliyemwamini. 24 14:24Kisha wakapitia Pisidia wakafika Pamfilia. 25 14:25Baada ya kuhubiri neno la Mungu huko Perga, wakateremkia Atalia.

26 14:26Kutoka Atalia wakasafiri baharini wakarudi Antiokia, ambako walikuwa wamesifiwa kwa ajili ya neema ya Mungu kutokana na ile huduma waliyokuwa wameikamilisha. 27 14:27Walipowasili Antiokia wakaliita kanisa pamoja na kutoa taarifa ya yale yote Mungu aliyokuwa ametenda kupitia kwao na jinsi alivyokuwa amefungua mlango wa imani kwa ajili ya watu wa Mataifa. 28 14:28Nao wakakaa huko pamoja na wanafunzi kwa muda mrefu.

15Baraza La Yerusalemu

1 15:1Baadhi ya watu wakashuka Antiokia kutoka Uyahudi, nao wakawa wanawafundisha wandugu: “Msipotahiriwa kufuatana na desturi aliyofundisha Mose, hamwezi kuokoka.” 2 15:2Baada ya Paulo na Barnaba kutokubaliana nao kukawa na mabishano makali, Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine miongoni mwao wakachaguliwa kwenda Yerusalemu ili kujadiliana jambo hili na mitume na wazee. 3 15:3Hivyo wakasafirishwa na kanisa, wakiwa njiani wakapitia nchi ya Foinike na Samaria, wakawaeleza jinsi watu wa Mataifa walivyookoka. Habari hizi zikaleta furaha kubwa kwa ndugu wote. 4 15:4Walipofika Yerusalemu, walipokelewa na kanisa na mitume pamoja na wazee, ndipo Paulo na Barnaba wakawaarifu kila kitu Mungu alichokuwa amefanya kupitia kwao.

5 15:5Ndipo baadhi ya walioamini wa madhehebu ya Mafarisayo wakasimama na kusema, “Hao watu wa Mataifa lazima watahiriwe na waagizwe kutii sheria ya Mose.”

6 15:6Mitume na wazee wakakutana pamoja ili kufikiri jambo hili. 7 15:7Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu wa Mataifa wapate kusikia ujumbe wa Injili na kuamini. 8 15:8Mungu, yeye ajuaye mioyo, alionyesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama vile alivyotupa sisi. 9 15:9Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani. 10 15:10Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka kongwa shingoni mwa wanafunzi ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulibeba? 11 15:11Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu Kristo, kama wao wanavyookolewa.”

12 15:12Kusanyiko lote likakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu wa Mataifa. 13 15:13Walipomaliza kunena, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni. 14 15:14Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonyesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka watu wa Mataifa kwa ajili ya Jina lake. 15 15:15Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa:

16 15:16“ ‘Baada ya mambo haya nitarudi, nami nitajenga upya nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena magofu yake na kuisimamisha, 17 15:17ili wanadamu wengine wote wapate kumtafuta Bwana, hata wale watu wa Mataifa wote ambao wanaitwa kwa Jina langu, asema Bwana, afanyaye mambo haya’ 18 15:18ambayo yamejulikana tangu zamani.

19 15:19“Kwa hivyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwataabishe watu wa Mataifa wanaomgeukia Mungu. 20 15:20Badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe na vyakula vilivyonajisiwa kwa kutolewa sanamu, wajiepushe na uasherati, au kula mnyama aliyenyongwa, na damu. 21 15:21Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Mose amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”

Barua Kwa Waumini Wa Mataifa

22 15:22Mitume na wazee pamoja na kanisa lote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu. 23 15:23Wakatumwa na barua ifuatayo:

Sisi mitume na wazee, ndugu zenu, Kwa ndugu Mataifa mlioamini mlioko Antiokia, Shamu na Kilikia: Salamu. 24 15:24Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiyataabisha mawazo yenu. 25 15:25Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, 26 15:26watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 27 15:27Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia. 28 15:28Kwa maana imempendeza Roho Mtakatifu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: 29 15:29Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema. Kwaherini.

30 15:30Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kanisa pamoja, wakawapa ile barua. 31 15:31Nao hao watu wakiisha kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo. 32 15:32Yuda na Sila, ambao wenyewe walikuwa manabii, wakanena maneno mengi ya kuwatia moyo na kuwajenga katika imani wale ndugu walioamini. 33 15:33Baada ya kukaa huko Antiokia kwa muda, wakaagwa kwa amani na wale ndugu ili waende kwa wale waliowatuma. [ 34 15:34Lakini Sila bado akaendelea kukaa huko.] 35 15:35Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi walifundisha na kuhubiri neno la Bwana.

Safari Ya Pili Ya Paulo Kueneza Injili (15:36–18:22) Paulo Na Barnaba Wagawanyika

36 15:36Baada ya muda, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote tuliyohubiri neno la Bwana tuone jinsi wanavyoendelea.” 37 15:37Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye. 38 15:38Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi naye. 39 15:39Pakatokea ubishi mkali kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro. 40 15:40Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana. 41 15:41Akapitia Shamu na Kilikia, akiimarisha makanisa ya huko.

16Timotheo Aungana Na Paulo Na Sila

1 16:1Paulo akafika Derbe na kisha Listra, ambako kulikuwa na mwanafunzi mmoja jina lake Timotheo, ambaye mama yake alikuwa Myahudi aliyeamini, lakini baba yake alikuwa Myunani. 2 16:2Alikuwa amesifiwa sana na wale ndugu waliokuwa wameamini huko Listra na Ikonio 3 16:3Paulo alitaka Timotheo afuatane naye, hivyo akamchukua na kumtahiri kwa sababu ya Wayahudi waliokuwa wanaishi eneo lile kwa maana wote walimjua baba yake ni Myunani. 4 16:4Walipokuwa wakienda mji kwa mji, wakawa wanawapa maamuzi yaliyotolewa na mitume na wazee huko Yerusalemu ili wayafuate. 5 16:5Hivyo makanisa yakawa imara katika imani na kuongezeka kiidadi kila siku.

6 16:6Paulo pamoja na wenzake wakasafiri sehemu za Frigia na Galatia, kwa kuwa Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kulihubiri neno huko Asia. 7 16:7Walipofika mpaka wa Misia, wakajaribu kuingia Bithinia lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu. 8 16:8Kwa hiyo wakapita Misia, wakafika Troa. 9 16:9Wakati wa usiku Paulo akaona maono, mtu wa Makedonia amesimama akimsihi, “Vuka uje huku Makedonia utusaidie.” 10 16:10Baada ya Paulo kuona maono haya, tulijiandaa kwa haraka kuondoka kwenda Makedonia tukiwa tumesadiki kuwa Mungu alikuwa ametuita kuhubiri habari njema huko.

Kuokoka Kwa Lidia

11 16:11Tukasafiri kwa njia ya bahari kutoka Troa na kwenda moja kwa moja hadi Samothrake, kesho yake tukafika Neapoli. 12 16:12Kutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa jimbo hilo la Makedonia, uliokuwa koloni ya Warumi. Nasi tukakaa huko siku kadhaa.

13 16:13Siku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, mahali ambapo tulitarajia tungepata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko. 14 16:14Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo. 15 16:15Basi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumba yake, alitukaribisha nyumbani kwake akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.

Paulo Na Sila Watiwa Gerezani

16 16:16Siku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mtumwa mmoja wa kike ambaye alikuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri. 17 16:17Huyu msichana alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipiga kelele, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.” 18 16:18Akaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Yesu Kristo, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka saa ile ile.

19 16:19Basi mabwana wa yule mtumwa wa kike walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta mpaka sokoni mbele ya viongozi wa mji. 20 16:20Baada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, “Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi. 21 16:21Wanafundisha desturi ambazo sisi raiya wa Kirumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza.”

22 16:22Umati wa watu waliokuwepo wakajiunga katika kuwashambulia Paulo na Sila na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wachapwe viboko. 23 16:23Baada ya kuwachapa sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu. 24 16:24Kufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.

25 16:25Ilipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 16:26Ghafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. 27 16:27Yule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. 28 16:28Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”

29 16:29Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. 30 16:30Kisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”

31 16:31Wakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.” 32 16:32Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake. 33 16:33Wakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. 34 16:34Akawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.

35 16:35Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, “Wafungue wale watu, waache waende zao.” 36 16:36Mkuu wa gereza akamwambia Paulo “Mahakimu wameagiza niwaache huru, kwa hiyo tokeni na mwende zenu kwa amani.”

37 16:37Lakini Paulo akawaambia wale maafisa, “Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raiya wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani.”

38 16:38Wale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raiya wa Rumi. 39 16:39Kwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji. 40 16:40Baada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walikwenda nyumbani kwa Lidia, ambapo walikutana na wale ndugu walioamini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.

17Ghasia Huko Thesalonike

1 17:1Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi. 2 17:2Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko, 3 17:3akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristo 17:3 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.” 4 17:4Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.

5 17:5Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani kwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye ule umati wa watu. 6 17:6Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipiga kelele: “Watu hawa ni wale walioupindua ulimwengu wamekuja huku, 7 17:7naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Yesu.” 8 17:8Waliposikia haya, ule umati wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia. 9 17:9Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaacha waende zao.

Paulo Na Sila Huko Beroya

10 17:10Usiku ule ule, wale ndugu walioamini wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi. 11 17:11Hawa Waberoya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli. 12 17:12Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume wa Kiyunani wa tabaka la juu.

13 17:13Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko ili kuwashawishi watu na kuwachochea. 14 17:14Mara hiyo, wale ndugu wakamsafirisha Paulo hadi pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya. 15 17:15Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye mpaka Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo.

Paulo Huko Athene

16 17:16Paulo alipokuwa akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona vile mji huo ulivyojaa sanamu. 17 17:17Hivyo akahojiana kwenye sinagogi na Wayahudi pamoja na Wayunani waliomcha Mungu, na pia sokoni kila siku na watu aliopatana nao huko. 18 17:18Kisha baadhi ya Waepikureo na Wastoiko wenye falsafa wakakutana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri habari njema kuhusu Yesu na ufufuo wa wafu. 19 17:19Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini? 20 17:20Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.” 21 17:21(Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya chochote kingine isipokuwa kueleza au kusikia mambo mapya).

22 17:22Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana. 23 17:23Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.

24 17:24“Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu. 25 17:25Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote. 26 17:26Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi. 27 17:27Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu. 28 17:28‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’

29 17:29“Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu. 30 17:30Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu. 31 17:31Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”

32 17:32Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.” 33 17:33Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao. 34 17:34Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao alikuwepo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari na wengine wengi.

18Paulo Huko Korintho

1 18:1Baada ya haya, Paulo akaondoka Athene akaenda Korintho. 2 18:2Huko akakutana na Myahudi mmoja jina lake Akila, mwenyeji wa Ponto, ambaye alikuwa amewasili karibuni kutoka Italia pamoja na mkewe Prisila, kwa sababu Klaudio alikuwa ameamuru Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo akaenda kuwaona, 3 18:3naye kwa kuwa alikuwa mtengeneza mahema kama wao, akakaa na kufanya kazi pamoja nao. 4 18:4Kila Sabato Paulo alikuwa akihojiana nao katika sinagogi, akijitahidi kuwashawishi Wayahudi na Wayunani.

5 18:5Sila na Timotheo walipowasili kutoka Makedonia, walimkuta Paulo akiwa amejitolea muda wake wote katika kuhubiri, akiwashuhudia Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo 18:5 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. 6 18:6Wayahudi walipompinga Paulo na kukufuru, yeye aliyakungʼuta mavazi yake, akawaambia, “Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu! Mimi sina hatia, nimetimiza wajibu wangu. Kuanzia sasa nitawaendea watu wa Mataifa.”

7 18:7Kisha akaondoka mle kwenye sinagogi, akaenda nyumbani kwa mtu mmoja jina lake Tito Yusto, aliyekuwa mcha Mungu. Nyumba yake ilikuwa karibu na sinagogi. 8 18:8Kiongozi wa hilo sinagogi, aliyeitwa Krispo, akamwamini Bwana, yeye pamoja na watu wote wa nyumbani mwake. Nao Wakorintho wengi waliomsikia Paulo pia wakaamini na kubatizwa.

9 18:9Usiku mmoja Bwana akamwambia Paulo katika maono, “Usiogope, lakini endelea kusema wala usinyamaze, 10 18:10 kwa maana mimi niko pamoja nawe, wala hakuna mtu atakayeweza kukushambulia ili kukudhuru, kwa kuwa ninao watu wengi katika mji huu ambao ni watu wangu.” 11 18:11Hivyo Paulo akakaa huko kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, akiwafundisha neno la Mungu.

12 18:12Lakini wakati Galio alipokuwa msaidizi wa mwakilishi wa mtawala huko Akaya, Wayahudi waliungana kumshambulia Paulo, wakamkamata na kumpeleka mahakamani. 13 18:13Wakamshtaki wakisema, “Mtu huyu anawashawishi watu wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.”

14 18:14Paulo alipotaka kujitetea, Galio akawaambia Wayahudi, “Kama ninyi Wayahudi mlikuwa mkilalamika kuhusu makosa makubwa ya uhalifu ingekuwa haki kwangu kuwasikiliza. 15 18:15Lakini kwa kuwa linahusu maneno, majina na sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitakuwa mwamuzi wa mambo haya.” 16 18:16Akawafukuza kutoka mahakamani. 17 18:17Ndipo wote wakamkamata Sosthene kiongozi wa sinagogi, wakampiga mbele ya mahakama, lakini Galio hakujali kitendo chao hata kidogo.

Paulo Arudi Antiokia

18 18:18Baada ya kukaa Korintho kwa muda, Paulo akaagana na wale ndugu walioamini, akasafiri kwa njia ya bahari kwenda Shamu akiwa amefuatana na Prisila na Akila. Walipofika Kenkrea, Paulo alinyoa nywele zake kwa kuwa alikuwa ameweka nadhiri. 19 18:19Walipofika Efeso, Paulo aliwaacha Prisila na Akila huko, lakini yeye akaingia kwenye sinagogi akawa anajadiliana na Wayahudi. 20 18:20Walipomwomba akae nao kwa muda mrefu zaidi hakukubali. 21 18:21Lakini alipokuwa akiondoka, akaahidi, “Nitarudi kama Mungu akipenda.” Kisha akasafiri kwa njia ya bahari kutoka Efeso. 22 18:22Alitia nanga Kaisaria, akaenda Yerusalemu na kulisalimu kanisa, kisha akaenda Antiokia.

Safari Ya Tatu Ya Paulo Kueneza Injili (18:23–21:16)

23 18:23Baada ya kukaa huko kwa muda, akaondoka na kwenda sehemu moja hadi nyingine huko Galatia na Frigia, akiwaimarisha wanafunzi wote.

Huduma Ya Apolo Huko Efeso Na Korintho

24 18:24Basi akaja Efeso Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mwenyeji wa Iskanderia. Yeye alikuwa na elimu kubwa, pia alikuwa hodari katika Maandiko. 25 18:25Alikuwa amefundishwa katika njia ya Bwana, naye alikuwa na bidii katika roho, akafundisha kwa usahihi juu ya Yesu, ingawa alijua tu ubatizo wa Yohana. 26 18:26Apolo alianza kunena kwa ujasiri mkubwa katika sinagogi. Lakini Prisila na Akila walipomsikia, walimchukua kando na kumweleza njia ya Mungu kwa ufasaha zaidi.

27 18:27Naye Apolo alipotaka kwenda Akaya, ndugu wa Efeso walimtia moyo, wakawaandikia wanafunzi huko ili wamkaribishe. Alipofika huko, aliwasaidia sana wale ambao, kwa neema ya Mungu, walikuwa wameamini. 28 18:28Kwa uwezo mkubwa aliwakanusha hadharani Wayahudi waliokuwa wakipinga, akionyesha kwa njia ya Maandiko kwamba Yesu ndiye Kristo.

19Paulo Huko Efeso

1 19:1Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa, 2 19:2akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?”

Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.” 3 19:3Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.”

4 19:4Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani, Yesu.” 5 19:5Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu. 6 19:6Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri. 7 19:7Walikuwa kama wanaume kumi na wawili.

8 19:8Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya Ufalme wa Mungu. 9 19:9Lakini baadhi yao walikaidi. Walikataa kuamini, na wakakashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu. Basi Paulo aliachana nao. Akawachukua wanafunzi naye, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano. 10 19:10Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko Asia wakawa wamesikia neno la Bwana.

Wana Wa Skewa Wajaribu Kutoa Pepo Mchafu

11 19:11Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo, 12 19:12hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.

13 19:13Basi baadhi ya Wayahudi wenye kutangatanga huku na huko wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Yesu wale wenye pepo wakisema, “Kwa jina la Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.” 14 19:14Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo. 15 19:15Lakini pepo mchafu akawajibu, “Yesu namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?” 16 19:16Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.

17 19:17Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Yesu likaheshimiwa sana. 18 19:18Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu. 19 19:19Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma 50,000 19:19 Drakma ilikuwa ni sarafu ya fedha, thamani yake ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja. za fedha. 20 19:20Hivyo neno la Bwana likaenea sana na kuwa na nguvu.

21 19:21Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.” 22 19:22Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko Asia.

Ghasia Huko Efeso

23 19:23Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia ile ya Bwana. 24 19:24Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa, 25 19:25aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii! 26 19:26Pia ninyi mmeona na kusikia jinsi ambavyo si huku Efeso peke yake lakini ni karibu Asia yote, huyu Paulo amewashawishi na kuvuta idadi kubwa ya watu kwa kusema kuwa miungu iliyotengenezwa na watu si miungu. 27 19:27Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu mke Artemi, aliye mkuu, anayeabudiwa Asia yote na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”

28 19:28Waliposikia maneno haya, wakaghadhibika, wakaanza kupiga kelele, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!” 29 19:29Mara mji wote ukajaa ghasia. Wakawakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliokuwa wakisafiri pamoja na Paulo, na watu wakakimbilia katika ukumbi wa michezo kama mtu mmoja. 30 19:30Paulo akataka kuingia katikati ya umati huo, lakini wanafunzi hawakumruhusu. 31 19:31Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi.

32 19:32Ule umati ulikuwa na taharuki. Wengine walikuwa wakipiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko. 33 19:33Wayahudi wakamsukumia Aleksanda mbele na baadhi ya watu kwenye ule umati wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu. 34 19:34Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”

35 19:35Baadaye karani wa mji akaunyamazisha ule umati wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni? 36 19:36Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayakanushiki, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lolote kwa haraka. 37 19:37Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike. 38 19:38Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana jambo zito dhidi ya mtu yeyote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka. 39 19:39Lakini kama kuna jambo jingine lolote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali. 40 19:40Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.” 41 19:41Baada ya kusema haya akavunja mkutano.

20Paulo Apita Makedonia Na Uyunani

1 20:1Baada ya zile ghasia kumalizika, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia. 2 20:2Alipita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo. Ndipo hatimaye akawasili Uyunani, 3 20:3ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Alipokuwa anakaribia kuanza safari kwa njia ya bahari kwenda Shamu, kwa sababu Wayahudi walikuwa wamefanya shauri baya dhidi yake, aliamua kurudi kupitia njia ya Makedonia. 4 20:4Paulo alikuwa amefuatana na Sopatro mwana wa Piro, Mberoya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike na Gayo, mtu wa Derbe, Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka sehemu ya Asia. 5 20:5Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa. 6 20:6Lakini sisi tukasafiri kwa njia ya bahari kwa siku tano kutoka Filipi baada ya siku za Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, nasi tukaungana na wengine huko Troa, ambako tulikaa kwa siku saba.

Eutiko Afufuliwa Huko Troa

7 20:7Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea mpaka usiku wa manane. 8 20:8Kwenye chumba cha ghorofani walimokuwa wamekutania kulikuwa na taa nyingi. 9 20:9Kijana mmoja jina lake Eutiko, alikuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akihubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamwinua akiwa amekufa. 10 20:10Paulo akashuka chini, akajitupa juu yake na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, uzima wake bado umo ndani yake.” 11 20:11Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea mpaka mapambazuko, akaondoka. 12 20:12Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana.

Paulo Awaaga Wazee Wa Efeso

13 20:13Tukatangulia melini tukasafiri mpaka Aso ambako tungempakia Paulo. Alikuwa amepanga hivyo kwa maana alitaka kufika kwa miguu. 14 20:14Alipotukuta huko Aso, tulimpakia melini, tukasafiri wote mpaka Mitilene. 15 20:15Kutoka huko tuliendelea kwa njia ya bahari, na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo, na kesho yake tukawasili Mileto. 16 20:16Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko sehemu za Asia, kwa sababu alikuwa anatamani kama ikiwezekana kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste.

17 20:17Paulo akiwa Mileto, alituma mjumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa waje wakutane naye. 18 20:18Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi katikati yenu muda wote tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia. 19 20:19Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. 20 20:20Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. 21 20:21Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

22 20:22“Nami sasa nimesukumwa na Roho, ninakwenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko. 23 20:23Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja. 24 20:24Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Yesu aliyonipa, yaani, kazi ya kuishuhudia Injili ya neema ya Mungu.

25 20:25“Nami sasa najua ya kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu ambaye nimemhubiria Ufalme wa Mungu katika kwenda kwangu huku na huko, atakayeniona uso tena. 26 20:26Kwa hiyo nawatangazia leo, sina hatia ya damu ya mtu awaye yote. 27 20:27Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu. 28 20:28Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. 29 20:29Najua kwamba baada yangu kuondoka, mbwa mwitu wakali watakuja katikati yenu ambao hawatalihurumia kundi. 30 20:30Hata kutoka miongoni mwenu watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. 31 20:31Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.

32 20:32“Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa. 33 20:33Sikutamani fedha wala dhahabu wala vazi la mtu yeyote. 34 20:34Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. 35 20:35Katika kila jambo nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”

36 20:36Paulo alipomaliza kusema haya akapiga magoti pamoja nao wote akaomba. 37 20:37Wote wakalia, wakamkumbatia Paulo na kumbusu, 38 20:38Kilichowahuzunisha zaidi ni kwa sababu ya yale maneno aliyosema kwamba kamwe hawatauona uso wake tena. Wakaenda naye mpaka kwenye meli.

21Paulo Aenda Yerusalemu

1 21:1Tulipokwisha kujitenga nao, tukaanza safari kwa njia ya bahari moja kwa moja mpaka Kosi. Siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukaenda Patara. 2 21:2Hapo tukapata meli iliyokuwa inavuka kwenda Foinike tukapanda tukasafiri nayo. 3 21:3Tulipokiona kisiwa cha Kipro, tukakizunguka tukakiacha upande wetu wa kushoto, tukasafiri mpaka Shamu, tukatia nanga katika bandari ya Tiro ambapo meli yetu ilikuwa ipakue shehena yake. 4 21:4Baada ya kuwatafuta wanafunzi wa huko, tukakaa nao kwa siku saba. Wale wanafunzi wakiongozwa na Roho wakamwambia Paulo asiende Yerusalemu. 5 21:5Lakini muda wetu ulipokwisha, tukaondoka tukaendelea na safari yetu. Wale wanafunzi pamoja na wake zao na watoto wakatusindikiza hadi nje ya mji. Wote tukapiga magoti pale pwani tukaomba. 6 21:6Baada ya kuagana, tukapanda melini, nao wakarudi majumbani mwao.

7 21:7Tukaendelea na safari yetu toka Tiro tukafika Tolemai, tukawasalimu ndugu wa huko, tukakaa nao kwa siku moja. 8 21:8Siku iliyofuata tukaondoka, tukafika Kaisaria. Huko tukaenda nyumbani kwa mwinjilisti mmoja jina lake Filipo, aliyekuwa mmoja wa wale Saba, tukakaa kwake. 9 21:9Filipo alikuwa na binti wanne mabikira waliokuwa wanatoa unabii.

10 21:10Baada ya kukaa kwa siku kadhaa, akateremka nabii mmoja kutoka Uyahudi jina lake Agabo. 11 21:11Alipotufikia akachukua mshipi wa Paulo akajifunga, akautumia kufunga mikono na miguu yake mwenyewe akasema, “Roho Mtakatifu anasema: ‘Hivi ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mwenye mshipi huu na kumkabidhi kwa watu wa Mataifa.’ ”

12 21:12Tuliposikia maneno haya sisi na ndugu wengine tukamsihi Paulo asiende Yerusalemu. 13 21:13Lakini Paulo akajibu, “Kwa nini mnalia na kunivunja moyo? Mimi niko tayari si kufungwa tu, bali hata kufa huko Yerusalemu kwa ajili ya jina la Bwana Yesu.” 14 21:14Alipokuwa hashawishiki, tukaacha kumsihi, tukasema, “Mapenzi ya Bwana na yatendeke.”

15 21:15Baada ya haya, tukajiandaa, tukaondoka kwenda Yerusalemu. 16 21:16Baadhi ya wanafunzi kutoka Kaisaria wakafuatana nasi na kutupeleka nyumbani kwa Mnasoni, ambaye tungekaa kwake. Yeye alikuwa mtu wa Kipro, mmoja wa wanafunzi wa zamani.

Kukamatwa Kwa Paulo, Na Safari Yake Kwenda Rumi (21:17–28:31) Paulo Awasili Yerusalemu

17 21:17Tulipofika Yerusalemu ndugu wakatukaribisha kwa furaha. 18 21:18Kesho yake Paulo pamoja na wengine wetu tulikwenda kumwona Yakobo, na wazee wote walikuwepo. 19 21:19Baada ya kuwasalimu, Paulo akatoa taarifa kamili ya mambo yote ambayo Mungu alikuwa amefanya miongoni mwa watu wa Mataifa kupitia huduma yake.

20 21:20Baada ya kusikia mambo haya wakamwadhimisha Mungu. Ndipo wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaona kulivyo na maelfu ya Wayahudi walioamini, nao wote wana juhudi kwa ajili ya sheria. 21 21:21Lakini wameambiwa habari zako kwamba unafundisha Wayahudi wote waishio miongoni mwa watu wa Mataifa kumkataa Mose, na kwamba unawaambia wasiwatahiri watoto wao wala kufuata desturi zetu. 22 21:22Sasa tufanyeje? Bila shaka watasikia kwamba umekuja Yerusalemu. 23 21:23Kwa hiyo fanya lile tunalokuambia. Tunao watu wanne hapa ambao wameweka nadhiri. 24 21:24Jiunge na watu hawa, mfanye utaratibu wa ibada ya kujitakasa pamoja nao, na ulipe gharama ili wanyoe nywele zao. Kwa njia hii kila mtu atafahamu ya kuwa mambo waliyosikia si ya kweli na kwamba wewe unaishika sheria. 25 21:25Lakini kuhusu wale watu wa Mataifa walioamini, tumewaandikia uamuzi wetu: kwamba wajitenge na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na wajiepushe na uasherati.”

26 21:26Ndipo kesho yake Paulo akawachukua wale watu na akajitakasa pamoja nao. Akaingia ndani ya hekalu ili atoe taarifa ya tarehe ambayo siku zao za utakaso zingemalizika na sadaka ingetolewa kwa ajili ya kila mmoja wao.

Paulo Akamatwa

27 21:27Zile siku saba zilipokaribia kumalizika, baadhi ya Wayahudi kutoka sehemu za Asia waliokuwa wamemwona Paulo ndani ya Hekalu, wakachochea umati wote wa watu, nao wakamkamata. 28 21:28Wakapiga kelele wakisema, “Waisraeli wenzetu, tusaidieni! Huyu ndiye yule mtu anayefundisha kila mtu na kila mahali, kinyume na watu wetu, sheria zetu na hata Hekalu hili. Zaidi ya hayo amewaleta Wayunani ndani ya Hekalu na kupanajisi mahali hapa patakatifu.” 29 21:29(Walikuwa wamemwona Trofimo, mwenyeji wa Efeso, akiwa mjini pamoja na Paulo wakadhani kuwa Paulo alikuwa amemwingiza Hekaluni.)

30 21:30Mji wote ukataharuki, watu wakaja wakikimbia kutoka pande zote wakamkamata Paulo, wakamburuta kutoka Hekaluni. Milango ya Hekalu ikafungwa. 31 21:31Walipokuwa wakitaka kumuua, habari zikamfikia jemadari wa jeshi la askari wa Kirumi kwamba mji wa Yerusalemu wote ulikuwa katika machafuko. 32 21:32Mara yule jemadari akachukua maafisa wengine wa jeshi pamoja na askari wakakimbilia kwenye ile ghasia, wale watu waliokuwa wakifanya ghasia walipomwona yule jemadari na askari wakija, wakaacha kumpiga Paulo.

33 21:33Yule jemadari akaja, akamkamata Paulo akaamuru afungwe kwa minyororo miwili. Akauliza yeye ni nani, na alikuwa amefanya nini. 34 21:34Baadhi ya watu katika ule umati wakapiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Yule jemadari alipoona kuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akaamuru Paulo apelekwe katika ngome ya jeshi. 35 21:35Paulo alipofika penye ngazi, ilibidi askari wambebe juu juu kwa sababu fujo za ule umati wa watu zilikuwa kubwa. 36 21:36Umati wa watu ulikuwa ukifuata ukiendelea kupiga kelele ukisema, “Mwondoe huyu!”

Paulo Anajitetea

37 21:37Mara tu Paulo alipokaribia kuingizwa kwenye ngome ya jeshi, akamwambia yule jemadari, “Je, naweza kukuambia jambo moja?”

Yule jemadari akamjibu, “Je, unajua Kiyunani? 38 21:38Je, wewe si yule Mmisri ambaye siku hizi za karibuni alianzisha uasi akaongoza kundi la magaidi 4,000 wenye silaha jangwani?”

39 21:39Paulo akajibu, “Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso, huko Kilikia, raiya wa mji maarufu. Tafadhali niruhusu nizungumze na hawa watu.”

40 21:40Akiisha kupata ruhusa ya yule jemadari, Paulo akasimama penye ngazi akawapungia watu mkono ili wanyamaze. Wote waliponyamaza kimya, Paulo akazungumza nao kwa lugha ya Kiebrania, akasema:

22Ushuhuda Wa Paulo Kwa Wayahudi Wa Yerusalemu

1 22:1“Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni utetezi wangu.”

2 22:2Waliposikia akisema kwa lugha ya Kiebrania, wakanyamaza kimya kabisa.

Ndipo Paulo akasema, 3 22:3“Mimi ni Myahudi, niliyezaliwa Tarso huko Kilikia, lakini nimelelewa katika mji huu. Miguuni mwa Gamalieli, nilifundishwa kikamilifu katika sheria ya baba zetu, na nikawa mwenye juhudi kwa ajili ya Mungu kama kila mmoja wenu alivyo leo. 4 22:4Niliwatesa watu wa Njia hii hadi kufa, nikiwakamata waume kwa wake na kuwatupa gerezani, 5 22:5kama kuhani mkuu na baraza zima la wazee wanavyoweza kushuhudia kunihusu. Hata nilipokea barua kutoka kwao kwenda kwa ndugu wale wa Dameski, nami nikaenda huko ili kuwaleta watu hawa Yerusalemu kama wafungwa ili waadhibiwe.

Paulo Aeleza Juu Ya Kuokoka Kwake (Matendo 9:1-19; 26:12-18)

6 22:6“Nilipokuwa njiani kuelekea Dameski, yapata saa sita mchana, ghafula nuru kubwa kutoka mbinguni ikanimulika kotekote. 7 22:7Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, ‘Sauli, Sauli! Mbona unanitesa?’

8 22:8“Nikajibu, ‘Wewe ni nani Bwana?’

“Naye akaniambia, ‘Mimi ni Yesu wa Nazareti unayemtesa.’ 9 22:9Basi wale watu waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia sauti ya yule aliyekuwa akisema nami.

10 22:10“Nikauliza, ‘Nifanye nini Bwana?’

“Naye Bwana akaniambia, ‘Inuka uingie Dameski, huko utaambiwa yote yakupasayo kufanya.’ 11 22:11Kwa kuwa nilikuwa siwezi kuona kwa ajili ya mngʼao wa ile nuru, wenzangu wakanishika mkono wakaniongoza kuingia Dameski.

12 22:12“Mtu mmoja mcha Mungu, jina lake Anania, alikuja kuniona. Alizishika sana sheria zetu, na aliheshimiwa sana na Wayahudi waliokuwa wakiishi huko Dameski. 13 22:13Akasimama karibu nami, akasema, ‘Ndugu Sauli, pata kuona tena!’ Saa ile ile nikapata kuona tena, nami nikaweza kumwona.

14 22:14“Akasema, ‘Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe ili ujue mapenzi yake, umwone yeye Aliye Mwenye Haki na upate kusikia maneno kutoka kinywani mwake. 15 22:15Kwa kuwa utakuwa shahidi wake kwa watu kuhusu kile ulichokiona na kukisikia. 16 22:16Sasa basi, mbona unakawia? Inuka, ukabatizwe na dhambi zako zikasafishwe, ukiliita Jina lake.’

Paulo Atumwa Kwa Watu Wa Mataifa

17 22:17“Baada ya kurudi Yerusalemu, nilipokuwa ninaomba Hekaluni, nilipitiwa na usingizi wa ghafula 18 22:18nikamwona Bwana akiniambia, ‘Harakisha utoke Yerusalemu upesi, maana hawataukubali ushuhuda wako kunihusu mimi.’

19 22:19“Nami nikasema, ‘Bwana, wao wenyewe wanajua jinsi nilivyokwenda kwenye kila sinagogi ili kuwatupa gerezani na kuwapiga wale waliokuamini. 20 22:20Wakati damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama kando, nikikubaliana na kitendo hicho na kutunza mavazi ya wale waliomuua.’

21 22:21“Ndipo Bwana akaniambia, ‘Nenda, kwa maana nitakutuma mbali, kwa watu wa Mataifa.’ ”

Paulo Na Jemadari Wa Kirumi

22 22:22Ule umati wa watu wakamsikiliza Paulo mpaka aliposema neno hilo, ndipo wakapaza sauti zao na kupiga kelele wakisema, “Mwondoeni duniani, hafai kuishi!”

23 22:23Walipokuwa wakipiga kelele na kutoa mavazi yao huku wakirusha mavumbi juu hewani, 24 22:24yule jemadari akaamuru Paulo aingizwe kwenye ngome. Akaelekeza kwamba achapwe viboko na aulizwe ili kujua kwa nini watu walikuwa wanampigia kelele namna hiyo. 25 22:25Lakini walipokwisha kumfunga kwa kamba za ngozi ili wamchape viboko, Paulo akamwambia kiongozi wa askari aliyekuwa amesimama pale karibu naye, “Je, ni halali kwenu kwa mujibu wa sheria kumchapa mtu ambaye ni raiya wa Rumi hata kabla hajapatikana na hatia?”

26 22:26Yule kiongozi aliposikia maneno haya, alimwendea yule jemadari na kumwambia, “Unataka kufanya nini? Kwa maana huyu mtu ni raiya wa Rumi.”

27 22:27Yule jemadari akaja akamuuliza Paulo, “Niambie, wewe ni raiya wa Rumi?”

Paulo akajibu, “Naam, hakika ndiyo.”

28 22:28Ndipo yule jemadari akasema, “Mimi ilinigharimu kiasi kikubwa cha fedha kupata uraia wangu.”

Paulo akasema “Lakini mimi ni raiya wa Rumi kwa kuzaliwa.”

29 22:29Mara wale waliokuwa wanataka kumhoji wakajiondoa haraka, naye yule jemadari akaingiwa na hofu alipotambua ya kuwa amemfunga Paulo, ambaye ni raia wa Rumi, kwa minyororo.

Paulo Apelekwa Mbele Ya Baraza

30 22:30Kesho yake, kwa kuwa yule jemadari alitaka kujua hakika kwa nini Paulo alikuwa anashutumiwa na Wayahudi, alimfungua, na akawaagiza viongozi wa makuhani na baraza lote likutane. Kisha akamleta Paulo, akamsimamisha mbele yao.

231 23:1Paulo akawakazia macho wale wajumbe wa baraza, akasema, “Ndugu zangu, nimetimiza wajibu wangu kwa Mungu kwa dhamiri safi kabisa hadi leo.” 2 23:2Kwa ajili ya jambo hili kuhani mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi kinywani. 3 23:3Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa! Wewe umeketi hapo ili kunihukumu kwa mujibu wa sheria, lakini wewe mwenyewe unakiuka sheria kwa kuamuru kwamba nipigwe kinyume cha sheria!”

4 23:4Wale watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Je, wewe wathubutu kumtukana kuhani mkuu wa Mungu?”

5 23:5Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye alikuwa kuhani mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usimnenee mabaya kiongozi wa watu wako.’ ”

6 23:6Paulo alipotambua ya kuwa baadhi yao walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo, akapaza sauti kwenye baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana Farisayo. Hapa nimeshtakiwa kuhusu tumaini langu katika ufufuo wa wafu.” 7 23:7Aliposema haya, farakano likaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo na baraza lote likagawanyika. 8 23:8(Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.)

9 23:9Kukawa na ghasia kubwa, nao baadhi ya walimu wa sheria ambao ni Mafarisayo, wakasimama wakapinga kwa nguvu wakisema, “Hatuoni kosa lolote la mtu huyu! Huenda ikawa roho au malaika amezungumza naye” 10 23:10Ugomvi ukawa mkubwa kiasi kwamba yule jemadari akahofu kuwa wangemrarua Paulo vipande vipande, akaamuru vikosi vya askari vishuke na kumwondoa Paulo katikati yao kwa nguvu na kumleta ndani ya ngome ya jeshi.

11 23:11Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”

Hila Za Kumuua Paulo

12 23:12Kulipopambazuka Wayahudi wakafanya shauri pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wawe wamemuua Paulo. 13 23:13Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini. 14 23:14Wakawaendea viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejifunga pamoja kwa kiapo kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tuwe tumemuua Paulo. 15 23:15Hivyo basi, wewe pamoja na baraza, inawapasa mkamjulishe jemadari ili amteremshe Paulo kwenu, mjifanye kama mnataka kufanya uchunguzi wa kina zaidi wa shauri lake. Nasi tuko tayari kumuua kabla hajafika hapa.”

16 23:16Lakini mtoto wa dada yake Paulo aliposikia juu ya shauri hilo baya, alikwenda kule kwenye ngome ya askari na kumweleza Paulo.

17 23:17Ndipo Paulo akamwita mmoja wa viongozi wa askari, akamwambia, “Mpeleke huyu kijana kwa jemadari, analo jambo la kumweleza.” 18 23:18Hivyo yule kiongozi wa askari akampeleka yule kijana kwa jemadari, akamwambia, “Paulo yule mfungwa aliniita na kuniomba nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukueleza.”

19 23:19Yule jemadari akamshika yule kijana mkono, akampeleka kando na kumuuliza, “Unataka kuniambia nini?”

20 23:20Yule kijana akasema, “Wayahudi wamekubaliana wakuombe umpeleke Paulo kwenye baraza lao kesho kwa kisingizio kwamba wanataka kufanya uchunguzi wa kina wa shauri lake. 21 23:21Lakini usishawishiwe nao kwa maana zaidi ya watu arobaini wanamvizia. Wamejifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wawe wamemuua Paulo. Sasa wako tayari, wanangoja idhini yako kwa ajili ya ombi lao.”

22 23:22Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende na akamwonya, akisema, “Usimwambie mtu yeyote kwamba umenieleza habari hizi.”

Paulo Ahamishiwa Kaisaria

23 23:23Kisha yule jemadari akawaita viongozi wake wawili wa askari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari 200, wapanda farasi sabini na watu 200 wenye mikuki. 24 23:24Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mkampeleke salama kwa mtawala Feliksi.”

25 23:25Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo:

26 23:26Klaudio Lisia, Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi: Salamu. 27 23:27Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumuua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya askari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raiya wa Rumi. 28 23:28Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya baraza lao. 29 23:29Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lolote linalostahili kifo au kifungo. 30 23:30Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na shauri baya dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara moja. Niliwaagiza washtaki wake pia waeleze mashtaka yao dhidi yake mbele yako.

31 23:31Hivyo askari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta mpaka Antipatri. 32 23:32Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wao wakarudi kwenye ngome ya askari. 33 23:33Askari walipofika Kaisaria, walimpa mtawala ile barua, na kumkabidhi Paulo kwake. 34 23:34Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimuuliza Paulo alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia, 35 23:35alisema, “Nitasikiliza shauri lako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.

24Mbele Ya Feliksi Huko Kaisaria

1 24:1Baada ya siku tano, kuhani mkuu Anania akashuka akiwa amefuatana na baadhi ya wazee pamoja na mwanasheria mmoja aitwaye Tertulo, nao wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala. 2 24:2Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na matengenezo mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele. 3 24:3Wakati wote na kila mahali, kwa namna yoyote, mtukufu sana Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi. 4 24:4Lakini nisije nikakuchosha zaidi, ningekuomba kwa hisani yako utusikilize kwa kifupi.

5 24:5“Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanazarayo, 6 24:6na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata; [tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu. 7 24:7Lakini jemadari Lisia alitujia na nguvu nyingi, akamwondoa mikononi mwetu, 8 24:8akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako: ili] kwa kumchunguza wewe mwenyewe unaweza kujua kutoka kwake mambo yote tunayomshtaki kwayo.”

9 24:9Pia wale Wayahudi wakaunga mkono wakithibitisha kuwa mashtaka yote haya ni kweli.

Paulo Ajitetea Mbele Ya Feliksi

10 24:10Mtawala Feliksi alipompungia Paulo mkono ili ajitetee, yeye akajibu, “Najua kwamba wewe umekuwa hakimu katika taifa hili kwa miaka mingi, hivyo natoa utetezi wangu kwa furaha. 11 24:11Unaweza kuhakikisha kwa urahisi kuwa hazijapita zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu kuabudu. 12 24:12Hawa wanaonishtaki hawakunikuta nikibishana na mtu yeyote Hekaluni au kuchochea umati wa watu katika sinagogi au mahali pengine popote mjini. 13 24:13Wala hawawezi kabisa kukuthibitishia mashtaka haya wanayonishtaki kwayo. 14 24:14Lakini, ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu, mfuasi wa Njia, ile ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Sheria na kile kilichoandikwa katika Manabii, 15 24:15nami ninalo tumaini kwa Mungu, ambalo hata wao wenyewe wanalikubali kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, kwa wenye haki na wasio na haki. 16 24:16Kwa hiyo ninajitahidi siku zote kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu na mbele za wanadamu.

17 24:17“Basi, baada ya kutokuwepo kwa miaka mingi nilikuja Yerusalemu ili kuwaletea watu wangu msaada kwa ajili ya maskini na kutoa dhabihu. 18 24:18Nilikuwa nimeshatakaswa kwa taratibu za kiibada waliponikuta Hekaluni nikifanya mambo haya. Hapakuwa na umati wa watu, pamoja nami wala aliyehusika kwenye fujo yoyote. 19 24:19Lakini kulikuwa na baadhi ya Wayahudi kutoka Asia, ambao wangelazimika wawepo hapa mbele yako ili watoe mashtaka kama wanalo jambo lolote dhidi yangu. 20 24:20Au, watu hawa walioko hapa waseme ni uhalifu gani walioniona nao waliponisimamisha mbele ya baraza, 21 24:21isipokuwa ni kuhusu jambo hili moja nililopiga kelele mbele yao kwamba, ‘Mimi nashtakiwa mbele yenu leo kwa sababu ya ufufuo wa wafu.’ ”

22 24:22Basi Feliksi ambaye alikuwa anafahamu vizuri habari za Njia ile, akaahirisha shauri lile kwa maelezo yake akisema, “Wakati jemadari Lisia atakapoteremka huku, nitaamua shauri lako.” 23 24:23Ndipo akaamuru kiongozi wa askari amweke chini ya ulinzi lakini ampe uhuru na kuwaruhusu rafiki zake wamhudumie.

24 24:24Baada ya siku kadhaa, Feliksi alikuja pamoja na Drusila mkewe, ambaye alikuwa Myahudi. Alituma aitiwe Paulo, naye akamsikiliza alipokuwa akinena juu ya imani katika Kristo Yesu. 25 24:25Naye Paulo alipokuwa akinena juu ya haki, kuwa na kiasi na juu ya hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu na kusema, “Hiyo yatosha sasa! Waweza kuondoka. Nitakapokuwa na wasaa nitakuita.” 26 24:26Wakati huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempa rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye.

27 24:27Baada ya miaka miwili kupita, Porkio Festo akaingia kwenye utawala mahali pa Feliksi, lakini kwa kuwa Feliksi alitaka kuwapendeza Wayahudi, akamwacha Paulo gerezani.

25Paulo Mbele Ya Festo

1 25:1Siku tatu baada ya Festo kuwasili Kaisaria kuchukua wajibu wake mpya, alipanda kwenda Yerusalemu, 2 25:2ambako viongozi wa makuhani na viongozi wa Wayahudi walikuja mbele yake na kuleta mashtaka yao dhidi ya Paulo. 3 25:3Wakamsihi sana Festo, kama upendeleo kwao, aamuru Paulo ahamishiwe Yerusalemu, kwa kuwa walikuwa wanaandaa kumvizia ili wamuue akiwa njiani. 4 25:4Festo akawajibu, “Paulo amezuiliwa huko Kaisaria, nami mwenyewe ninakwenda huko hivi karibuni. 5 25:5Baadhi ya viongozi wenu wafuatane nami na kutoa mashtaka dhidi ya mtu huyo huko, kama amekosa jambo lolote.”

6 25:6Baada ya Festo kukaa miongoni mwao kwa karibu siku nane au kumi, akashuka kwenda Kaisaria na siku iliyofuata akaitisha mahakama, akaketi penye kiti chake cha hukumu, akaamuru Paulo aletwe mbele yake. 7 25:7Paulo alipotokea, wale Wayahudi waliokuwa wameteremka toka Yerusalemu wakasimama wakiwa wamemzunguka, wakileta mashtaka mengi mazito dhidi yake ambayo hawakuweza kuyathibitisha.

8 25:8Ndipo Paulo akajitetea, akasema, “Mimi sikufanya jambo lolote kinyume cha sheria ya Wayahudi au dhidi ya Hekalu au kinyume cha Kaisari.”

9 25:9Festo, akitaka kuwapendeza Wayahudi, akamuuliza Paulo, “Je, ungependa kwenda Yerusalemu na kukabili mashtaka mbele yangu huko?”

10 25:10Paulo akasema, “Mimi sasa nimesimama mbele ya mahakama ya Kaisari, ambako ndiko ninakostahili kushtakiwa. Kama vile wewe mwenyewe ujuavyo vyema kabisa sijawatendea Wayahudi kosa lolote. 11 25:11Basi kama mimi nina hatia ya kutenda kosa lolote linalostahili kifo, sikatai kufa. Lakini kama mashtaka yaliyoletwa dhidi yangu na hawa Wayahudi si kweli, hakuna yeyote aliye na haki ya kunikabidhi mikononi mwao. Naomba rufaa kwa Kaisari!”

12 25:12Baada ya Festo kufanya shauri pamoja na baraza lake, akatangaza, “Wewe umeomba rufaa kwa Kaisari, nako kwa Kaisari utakwenda!”

Festo Aomba Ushauri Kwa Agripa

13 25:13Baada ya siku kadhaa Mfalme Agripa na Bernike wakapanda kuja Kaisaria kumsalimu Festo. 14 25:14Kwa kuwa walikuwa wakae huko Kaisaria kwa siku nyingi, Festo alijadili shauri la Paulo na mfalme, akisema, “Kuna mtu mmoja hapa ambaye Feliksi alimwacha gerezani. 15 25:15Nilipokuwa huko Yerusalemu, viongozi wa makuhani na wazee wa Wayahudi walinijulisha habari zake na wakaomba hukumu dhidi yake.

16 25:16“Lakini mimi nikawaambia kwamba si desturi ya Kirumi kumtoa mtu yeyote auawe kabla mshtakiwa kuonana uso kwa uso na washtaki wake, naye awe amepewa nafasi ya kujitetea kuhusu mashtaka anayoshutumiwa. 17 25:17Hivyo walipokutana hapa, sikukawia, kesho yake niliitisha baraza, nikaketi penye kiti changu cha hukumu, nikaagiza huyo mtu aletwe. 18 25:18Washtaki wake waliposimama, hawakushtaki kwa uhalifu wowote niliokuwa ninatarajia. 19 25:19Badala yake walikuwa na vipengele fulani vya kutokukubaliana naye kuhusu dini yao na juu ya mtu mmoja aitwaye Yesu, ambaye alikufa, lakini yeye Paulo alidai kwamba yu hai. 20 25:20Kwa kuwa sikujua jinsi ya kupeleleza jambo hili, nilimuuliza kama angependa kwenda Yerusalemu na kuhojiwa huko kuhusu mashtaka haya. 21 25:21Lakini Paulo alipoomba afadhiliwe ili rufaa yake isikilizwe na Mfalme Agusto, nilimwamuru alindwe mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari.”

22 25:22Ndipo Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyo mimi mwenyewe.”

Yeye akajibu, “Kesho utamsikia.”

Paulo Aletwa Mbele Ya Agripa

23 25:23Siku iliyofuata Agripa na Bernike walifika kwa fahari kubwa wakaingia katika ukumbi wa mahakama, pamoja na majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa mji. Ndipo kwa amri ya Festo, Paulo akaletwa ndani. 24 25:24Festo akasema, “Mfalme Agripa, nanyi nyote mlio hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu! Jumuiya yote ya Kiyahudi wamenilalamikia kuhusu mtu huyu huko Yerusalemu na hapa Kaisaria, wakipiga kelele kwamba haimpasi kuendelea kuishi. 25 25:25Sikuona kwamba ametenda jambo lolote linalostahili kifo, ila kwa kuwa alikuwa ameomba rufaa yake kwa mfalme, niliamua kumpeleka Rumi. 26 25:26Lakini mimi sina kitu maalum cha kumwandikia Bwana Mtukufu kumhusu mtu huyu. Kwa hiyo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa mbele yako, Mfalme Agripa, ili kutokana na matokeo ya uchunguzi huu, niweze kupata kitu cha kuandika. 27 25:27Kwa kuwa naona hakuna sababu ya kumpeleka mfungwa bila kuainisha mashtaka dhidi yake.”

26Paulo Ajitetea Mbele Ya Agripa

1 26:1Ndipo Agripa akamwambia Paulo, “Unayo ruhusa kujitetea.”

Hivyo Paulo akawaashiria kwa mkono wake, akaanza kujitetea, akasema: 2 26:2“Mfalme Agripa, najiona kuwa na heri kusimama mbele yako leo ninapojitetea kuhusu mashtaka yote ya Wayahudi, 3 26:3hasa kwa sababu unajua vyema desturi zote za Kiyahudi na ya kuwa wewe unajua kwa undani mila na masuala ya mabishano. Kwa hiyo, nakusihi unisikilize kwa uvumilivu.

4 26:4“Wayahudi wote wanajua jinsi nilivyoishi tangu nilipokuwa mtoto, kuanzia mwanzo wa maisha yangu katika nchi yangu na pia huko Yerusalemu. 5 26:5Wao wamefahamu kwa muda mrefu na wanaweza kushuhudia kama wakipenda, ya kwamba kutokana na misimamo mikali sana ya dhehebu letu kwenye dini yetu, niliishi nikiwa Farisayo. 6 26:6Nami sasa ni kwa sababu ya tumaini langu katika kile ambacho Mungu aliwaahidi baba zetu, ninashtakiwa leo. 7 26:7Hii ndiyo ahadi ambayo makabila yetu kumi na mawili yanatarajia kuiona ikitimizwa wanapomtumikia Mungu kwa bidii usiku na mchana. Ee mfalme, ninashtakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hili. 8 26:8Kwa nini yeyote miongoni mwenu afikiri kwamba ni jambo lisilosadikika Mungu kufufua wafu?

9 26:9“Mimi pia nilikuwa nimeshawishika kwamba imenipasa kufanya yote yale yaliyowezekana kupinga Jina la Yesu wa Nazareti. 10 26:10Nami hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Kwa mamlaka ya viongozi wa makuhani, niliwatia wengi wa watakatifu gerezani na walipokuwa wakiuawa, nilipiga kura yangu kuunga mkono. 11 26:11Mara nyingi nilikwenda kutoka sinagogi moja hadi ingine nikiamuru waadhibiwe, nami nilijaribu kuwalazimisha wakufuru. Katika shauku yangu dhidi yao, hata nilikwenda miji ya kigeni ili kuwatesa.

Paulo Aeleza Kuhusu Kuokoka Kwake (Matendo 9:1-19; 22:6-16)

12 26:12“Siku moja nilipokuwa katika mojawapo ya safari hizi nikiwa ninakwenda Dameski, nilikuwa na mamlaka na agizo kutoka kwa kiongozi wa makuhani. 13 26:13Ilikuwa yapata adhuhuri, ee mfalme, nilipokuwa njiani, niliona nuru kutoka mbinguni kali kuliko jua, ikingʼaa kunizunguka pande zote mimi na wale niliokuwa pamoja nao. 14 26:14Wote tulipokuwa tumeanguka chini, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, ‘Sauli, Sauli, mbona unanitesa? Ni vigumu kwako kuupiga teke mchokoo.’

15 26:15“Nikauliza, ‘Ni nani wewe, Bwana?’

“Naye Bwana akajibu, ‘Ni Mimi Yesu unayemtesa. 16 26:16 Sasa inuka usimame kwa miguu yako. Nimekutokea ili nikuteue uwe mtumishi na shahidi wa mambo ambayo umeyaona, na yale nitakayokuonyesha. 17 26:17 Nitakuokoa kutoka kwa watu wako na watu wa Mataifa ambao ninakutuma kwao, 18 26:18 uyafumbue macho yao ili wageuke kutoka gizani waingie nuruni, na kutoka kwenye nguvu za Shetani wamgeukie Mungu, ili wapate msamaha wa dhambi na sehemu miongoni mwa wale waliotakaswa kwa kuniamini mimi.’

19 26:19“Hivyo basi, Mfalme Agripa, sikuacha kuyatii yale maono yaliyotoka mbinguni, 20 26:20bali niliyatangaza kwanza kwa wale wa Dameski, kisha Yerusalemu na katika vijiji vyote vya Uyahudi na pia kwa watu wa Mataifa, kwamba inawapasa kutubu na kumgeukia Mungu na kuthibitisha toba yao kwa matendo yao. 21 26:21Ni kwa sababu hii Wayahudi walinikamata nilipokuwa Hekaluni, wakataka kuniua. 22 26:22Hadi leo nimepata msaada kutoka kwa Mungu, na hivyo nasimama hapa nikishuhudia kwa wakubwa na wadogo. Sisemi chochote zaidi ya yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia: 23 26:23kwamba Kristo 26:23 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. atateswa, na kwamba yeye atakuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu, na atatangaza nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.”

Paulo Aeleza Juu Ya Kuhubiri Kwake

24 26:24Paulo alipokuwa akifanya utetezi huu, Festo akasema kwa sauti kubwa, “Paulo, wewe umerukwa na akili! Kusoma kwingi kunakufanya uwe kichaa!”

25 26:25Lakini Paulo akajibu, “Mimi sijarukwa na akili, mtukufu sana Festo, bali nanena kweli nikiwa na akili zangu timamu. 26 26:26Naam, Mfalme anajua kuhusu mambo haya yote, nami nasema naye kwa uhuru. Kwa sababu nina hakika kwamba hakuna hata mojawapo ya mambo haya asilolijua, kwa kuwa hayakufanyika mafichoni. 27 26:27Mfalme Agripa, je, unaamini manabii? Najua kuwa unaamini.”

28 26:28Agripa akamwambia Paulo, “Je, unanishawishi kwa haraka namna hii niwe Mkristo?”

29 26:29Paulo akasema, “Ikiwa ni kwa haraka au la, namwomba Mungu, si wewe peke yako bali pia wale wote wanaonisikiliza leo, wawe kama mimi nilivyo, kasoro minyororo hii.”

30 26:30Baada ya kusema hayo, mfalme akainuka pamoja na mtawala na Bernike na wale waliokuwa wameketi pamoja nao. 31 26:31Walipokuwa wakiondoka, wakaambiana, “Mtu huyu hafanyi jambo lolote linalostahili kufa au kufungwa.”

32 26:32Agripa akamwambia Festo, “Mtu huyu angeachwa huru kama hangekuwa amekata rufaa kwa Kaisari.”

27Paulo Asafiri Kwenda Rumi

1 27:1Ilipoamuliwa kwamba tungesafiri kwa njia ya bahari kwenda Italia, Paulo na wafungwa wengine wakakabidhiwa kwa kiongozi mmoja wa askari aliyeitwa Juliasi, aliyekuwa wa Kikosi cha Walinzi wa Kaisari. 2 27:2Tulipanda meli iliyotoka Adramitio, iliyokuwa inakaribia kusafiri kwenda kwenye bandari zilizopo pwani ya Asia, tukaanza safari yetu tukiwa pamoja na Aristarko, Mmakedonia kutoka Thesalonike.

3 27:3Kesho yake tukatia nanga Sidoni, naye Juliasi akamfanyia wema Paulo, akamruhusu aende kwa rafiki zake ili wamtimizie mahitaji yake. 4 27:4Kutoka huko tukaingia baharini tena na tukapita upande wa chini wa kisiwa cha Kipro kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. 5 27:5Baada ya sisi kuvuka bahari iliyoko upande wa Kilikia na Pamfilia, tukafika Mira huko Likia. 6 27:6Huko yule kiongozi wa askari akapata meli ya Iskanderia ikielekea Italia, akatupandisha humo. 7 27:7Tukasafiri polepole kwa siku nyingi na kwa shida, hatimaye tukafika karibu na Nido. Kwa kuwa upepo wa mbisho ulituzuia tusiweze kushika mwelekeo tuliokusudia, tukapita chini ya Krete mkabala na Salmone. 8 27:8Tukaambaa na pwani kwa shida, tukafika sehemu iitwayo Bandari Nzuri, karibu na mji wa Lasea.

9 27:9Muda mwingi ulikuwa umepotea na kusafiri baharini kulikuwa hatari kwa sababu wakati huu ulikuwa baada ya siku za kufunga. Hivyo Paulo akawaonya akasema, 10 27:10“Mabwana, naona kuwa hii safari ni yenye maafa na ya kuleta hasara kubwa kwa meli na shehena, pia kwa maisha yetu.” 11 27:11Lakini badala ya yule kiongozi wa askari kusikiliza yale Paulo aliyosema, akafuata zaidi ushauri wa nahodha na mwenye meli. 12 27:12Kwa kuwa ile bandari ilikuwa haifai kukaa wakati wa majira ya baridi, wengi wakashauri kwamba tuendelee na safari wakitarajia kufika Foinike na kukaa huko kwa majira ya baridi. Hii ilikuwa bandari iliyoko katika kisiwa cha Krete ikikabili upande wa kusini-magharibi na kaskazini-magharibi.

Dhoruba Baharini

13 27:13Upepo mtulivu ulipoanza kuvuma toka kusini, wakadhani kuwa wangeweza kufikia lengo lao, hivyo wakangʼoa nanga na kusafiri wakipita kandokando ya pwani ya kisiwa cha Krete. 14 27:14Lakini baada ya muda mfupi ikavuma tufani kubwa iitwayo “Eurakilo” toka kisiwa cha Krete. 15 27:15Meli ikapigwa na dhoruba na haikuweza kushindana na ule upepo, tukarudishwa baharini upepo ulikokuwa unaelekea. 16 27:16Hatimaye tukisafiri kupita chini ya kisiwa kidogo kiitwacho Kauda, ambapo kwa kuwa tulikuwa tumekingiwa upepo na hicho kisiwa, tuliweza kwa shida kuifunga mashua ya kuokolea watu. 17 27:17Watu walipokwisha kuivuta mashua hiyo na kuiingiza katika meli, waliifunga kwa kamba chini ya meli yenyewe ili kuzishikanisha pamoja. Wakiogopa kupelekwa kwenye mchanga karibu na pwani ya Sirti, wakashusha matanga wakaiacha meli isukumwe na huo upepo. 18 27:18Tulikuwa tunapigwa na dhoruba kwa nguvu, kiasi kwamba kesho yake walianza kutupa shehena toka melini. 19 27:19Siku ya tatu, wakatupa vyombo vya meli baharini kwa mikono yao wenyewe. 20 27:20Kulipokuwa hakuna kuonekana kwa jua wala nyota kwa siku nyingi, nayo dhoruba ikiwa inaendelea kuwa kali, hatimaye tulikata kabisa tamaa ya kuokoka.

21 27:21Baada ya watu kukaa siku nyingi bila kula chakula, Paulo akasimama katikati yao akasema, “Enyi watu, iliwapasa kunisikiliza na kuacha kusafiri baharini kutoka Krete, ndipo ninyi mngekuwa mmejinusuru na uharibifu huu na hasara hii. 22 27:22Sasa ninawasihi sana, jipeni moyo mkuu kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha yake, ila meli itaangamia. 23 27:23Jana usiku, malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake na ambaye ninamwabudu alisimama karibu nami, 24 27:24naye akasema, ‘Paulo usiogope, kwa kuwa ni lazima usimame mbele ya Kaisari, naye Mungu amekupa kwa neema uhai wa wote wanaosafiri pamoja nawe. 25 27:25Hivyo jipeni moyo, enyi watu, kwa kuwa ninamwamini Mungu kwamba yatakuwa kama vile alivyoniambia.’ 26 27:26Lakini hata hivyo meli yetu itakwama kwenye kisiwa fulani.”

Maangamizi Ya Meli

27 27:27Usiku wa kumi na nne ulipofika, tulikuwa bado tunasukumwa na upepo katika Bahari ya Adria. Ilipokuwa yapata usiku wa manane, mabaharia wakahisi kwamba walikuwa wanakaribia nchi kavu. 28 27:28Kwa hiyo wakapima kina cha maji na kukuta kilikuwa pima ishirini, 27:28 Pima 20 ni kama mita 40. baada ya kuendelea mbele kidogo wakapima tena wakapata kina cha pima kumi na tano. 27:28 Pima 15 ni kama mita 30. 29 27:29Wakiogopa kwamba meli yetu ingegonga kwenye miamba, wakashusha nanga nne za nyuma ya meli, wakawa wanaomba kupambazuke. 30 27:30Katika jaribio la kutoroka kutoka kwenye meli, mabaharia wakashusha mashua ya kuokolea watu baharini, wakijifanya kwamba wanakwenda kushusha nanga za omo. 27:30 Omo hapa maana yake ni sehemu ya mbele ya meli, yaani gubeti. 31 27:31Ndipo Paulo akamwambia yule jemadari na askari, “Hawa watu wasipobaki katika meli, hamtaweza kuokoka.” 32 27:32Hivyo basi wale askari wakakata kamba zilizoshikilia ile mashua ya kuokolea watu kwenye meli, wakaiacha ianguke humo baharini.

33 27:33Kabla ya mapambazuko, Paulo akawasihi watu wote wale chakula akisema, “Leo ni siku ya kumi na nne mmekuwa katika wasiwasi mkiwa mmefunga na bila kula chochote. 34 27:34Kwa hiyo nawasihi mle chakula, kwa maana itawasaidia ili mweze kuishi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza unywele hata mmoja kutoka kichwani mwake.” 35 27:35Baada ya kusema maneno haya, Paulo akachukua mkate, akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega akaanza kula. 36 27:36Ndipo wote wakatiwa moyo, wakaanza kula chakula. 37 27:37Ndani ya meli tulikuwa jumla ya watu 276. 38 27:38Baada ya watu wote kula chakula cha kutosha, wakapunguza uzito wa meli kwa kutupa ngano baharini.

39 27:39Kulipopambazuka, mabaharia hawakuitambua ile nchi, lakini waliona ghuba yenye ufuko wa mchanga, ambako waliamua kuipweleza meli kama ingewezekana. 40 27:40Kwa hiyo wakatupa nanga zote na kuziacha baharini, na wakati huo huo wakalegeza kamba zilizokuwa zikishikilia usukani wa meli. Kisha wakatweka tanga la mbele lishike upepo na kuisukuma meli kuelekea pwani. 41 27:41Lakini wakafika mahali ambapo bahari mbili zinakutana, wakaipweleza meli ufuoni, omo ikakwama sana, ikawa haiwezi kuondolewa, lakini sehemu ya shetri 27:41 Shetri ni sehemu ya nyuma ya meli ambayo pia huitwa tezi. ikavunjika vipande vipande kwa kule kupiga kwa mawimbi yenye nguvu.

42 27:42Wale askari wakapanga kuwaua wale wafungwa ili kuzuia hata mmoja wao asiogelee na kutoroka. 43 27:43Lakini yule jemadari alitaka kuokoa maisha ya Paulo, basi akawazuia askari wasitekeleze mpango wao. Akaamuru wale wanaoweza kuogelea wajitupe baharini kwanza, waogelee mpaka nchi kavu. 44 27:44Waliosalia wangefika nchi kavu kwa kutumia mbao au vipande vya meli iliyovunjika, hivyo ikatimia kwamba wote wakaokoka na kufika nchi kavu salama.

28Paulo Kisiwani Malta

1 28:1Baada ya kufika nchi kavu salama, ndipo tukafahamu kwamba jina la kile kisiwa ni Malta. 2 28:2Wenyeji wa kile kisiwa wakatufanyia ukarimu usio wa kawaida. Waliwasha moto na kutukaribisha sisi sote kwa sababu mvua ilikuwa inanyesha na kulikuwa na baridi. 3 28:3Paulo alikuwa amekusanya mzigo wa kuni na alipokuwa anaweka kwenye moto kwa ajili ya joto, nyoka mwenye sumu akatoka humo na kujisokotea mkononi mwake. 4 28:4Wale wenyeji wa kile kisiwa walipomwona yule nyoka akiningʼinia mkononi mwa Paulo, wakaambiana, “Huyu mtu lazima awe ni muuaji, ingawa ameokoka kutoka baharini, haki haijamwacha aishi.” 5 28:5Lakini Paulo akamkungʼutia yule nyoka ndani ya moto wala yeye hakupata madhara yoyote. 6 28:6Watu walikuwa wanangoja avimbe au aanguke ghafula na kufa. Lakini baada ya kungoja kwa muda mrefu na kuona kwamba hakuna chochote kisicho cha kawaida kilichomtokea, wakabadili mawazo yao na kuanza kusema kwamba yeye ni mungu.

7 28:7Basi karibu na sehemu ile, palikuwa na shamba kubwa la mtu mmoja kiongozi wa kile kisiwa, aliyeitwa Publio. Alitupokea na akatuhudumia kwa ukarimu mkubwa kwa muda wa siku tatu. 8 28:8Baba yake Publio alikuwa mgonjwa kitandani, akiwa anaumwa homa na kuhara damu. Paulo akaingia ndani ili kumwona na baada ya maombi, akaweka mikono juu yake na kumponya. 9 28:9Jambo hili lilipotukia, watu wote wa kisiwa kile waliokuwa wagonjwa wakaja, nao wakaponywa. 10 28:10Wakatupa heshima nyingi, nasi tulipokuwa tayari kusafiri kwa njia ya bahari, wakapakia melini vitu vyote tulivyokuwa tunavihitaji.

Paulo Awasili Rumi

11 28:11Miezi mitatu baadaye tukaanza safari kwa meli iliyokuwa imetia nanga kwenye kisiwa hicho kwa ajili ya majira ya baridi. Hii ilikuwa meli ya Iskanderia yenye alama ya miungu pacha waitwao Kasta na Poluksi. 12 28:12Kituo chetu cha kwanza kilikuwa Sirakusa na tukakaa huko siku tatu. 13 28:13Kisha tukangʼoa nanga, tukafika Regio. Siku iliyofuata, upepo mkali wa kusi ukavuma, na siku ya pili yake tukafika Puteoli. 14 28:14Huko tukawakuta ndugu, nasi tukakaribishwa tukae nao kwa siku saba. Hivyo tukaendelea na safari mpaka Rumi. 15 28:15Ndugu wa huko Rumi waliposikia habari zetu, walikuja mpaka Soko la Apio na mahali paitwapo Mikahawa Mitatu kutulaki. Paulo alipowaona, alimshukuru Mungu akatiwa moyo. 16 28:16Tulipofika Rumi, Paulo aliruhusiwa kuishi peke yake akiwa na askari wa kumlinda.

Paulo Ahubiri Rumi Chini Ya Ulinzi

17 28:17Siku tatu baadaye Paulo akawaita pamoja viongozi wa Kiyahudi. Walipokwisha kukusanyika akawaambia, “Ndugu zangu, ingawa sikufanya jambo lolote dhidi ya watu wetu au dhidi ya desturi za baba zetu, lakini nilikamatwa huko Yerusalemu nikakabidhiwa kwa Warumi. 18 28:18Wao walipokwisha kunihoji, wakataka kuniachia huru kwa sababu hawakuona kosa lolote nililolifanya linalostahili adhabu ya kifo. 19 28:19Lakini Wayahudi walipopinga uamuzi huo, nililazimika kukata rufaa kwa Kaisari, ingawa sikuwa na lalamiko lolote juu ya taifa langu. 20 28:20Basi hii ndiyo sababu nimewatumania, ili niseme nanyi. Kwa kuwa ni kwa ajili ya tumaini la Israeli nimefungwa kwa minyororo.”

21 28:21Wakamjibu, “Hatujapokea barua zozote kutoka Uyahudi zinazokuhusu, wala hapana ndugu yeyote aliyekuja hapa ambaye ametoa taarifa au kuzungumza jambo lolote baya juu yako. 22 28:22Lakini tungependa kusikia kutoka kwako unalofikiri kwa sababu tunajua kwamba kila mahali watu wanazungumza mabaya kuhusu jamii hii.”

23 28:23Baada ya kupanga siku ya kuonana naye, watu wengi wakaja kuanzia asubuhi hadi jioni akawaeleza na kutangaza kuhusu Ufalme wa Mungu akijaribu kuwahadithia juu ya Yesu kutoka Sheria ya Mose na kutoka Manabii. 24 28:24Baadhi wakasadiki yale aliyosema, lakini wengine hawakuamini. 25 28:25Hivyo hawakukubaliana, nao walipokuwa wanaondoka, Paulo akatoa kauli moja zaidi: “Roho Mtakatifu alinena kweli na baba zenu aliposema mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:

26 28:26“ ‘Nenda kwa watu hawa na useme, “Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama, lakini hamtaona.” 27 28:27Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’

28 28:28“Basi na ijulikane kwenu kwamba, huu wokovu wa Mungu umepelekwa kwa watu wa Mataifa, nao watasikiliza.” [ 29 28:29Naye akiisha kusema maneno haya, Wayahudi wakaondoka wakiwa na hoja nyingi miongoni mwao.]

30 28:30Kwa miaka miwili mizima Paulo alikaa huko kwa nyumba aliyokuwa amepanga. Akawakaribisha wote waliokwenda kumwona. 31 28:31Akahubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha mambo yale yaliyomhusu Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri wote na bila kizuizi chochote.