Wagalatia 1WagalatiaSalamu

1 1:1Paulo mtume: si mtume wa wanadamu wala aliyetumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo na Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu; 2 1:2na ndugu wote walio pamoja nami:

Kwa makanisa ya Galatia:

3 1:3Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo, 4 1:4aliyejitoa kwa ajili ya dhambi zetu ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya, sawasawa na mapenzi yake yeye aliye Mungu na Baba yetu. 5 1:5Utukufu una yeye milele na milele. Amen.

Hakuna Injili Nyingine

6 1:6Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata Injili nyingine, 7 1:7ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo. 8 1:8Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele! 9 1:9Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!

10 1:10Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo.

Paulo Ameitwa Na Mungu

11 1:11Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu. 12 1:12Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo.

13 1:13Ninyi mmekwisha kusikia juu ya maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kwa nguvu na kujaribu kuliangamiza. 14 1:14Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika yangu maana nilijitahidi sana katika desturi za baba zangu. 15 1:15Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake, 16 1:16alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote, 17 1:17wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilikwenda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski.

18 1:18Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefa 1:18 Yaani Petro. na nilikaa naye siku kumi na tano. 19 1:19Lakini sikumwona mtume mwingine yeyote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana. 20 1:20Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo. 21 1:21Baadaye nilikwenda sehemu za Syria 1:21 Syria hapa ina maana ya Shamu. na Kilikia. 22 1:22Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makanisa ya huko Uyahudi yaliyo katika Kristo. 23 1:23Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo kwanza alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akijaribu kuiangamiza.” 24 1:24Nao wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.

2Paulo Akubaliwa Na Mitume

1 2:1Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nilipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito ili awe pamoja nami. 2 2:2Nilikwenda kwa sababu nilikuwa nimefunuliwa na Mungu, ili nikawaeleze kwa faragha wale walioonekana kuwa viongozi, ile Injili ninayoihubiri kwa watu wa Mataifa. Nilifanya hivyo kwa kuhofia kwamba nisije nikawa nilikuwa ninakimbia au nilikimbia bure. 3 2:3Lakini hata Tito ambaye alikuwa Myunani, hakulazimika kutahiriwa. 4 2:4Lakini kwa sababu ya ndugu wa uongo ambao walijiingiza kwa siri katikati yetu ili kupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, wapate kututia utumwani, 5 2:5hatukukubaliana nao hata dakika moja, ili kwamba ukweli wa Injili ubaki nanyi.

6 2:6Kwa habari ya wale waliokuwa wakubaliwe kuwa viongozi (kwangu mimi sikujali vyeo vyao, maana Mungu hana upendeleo), wale watu hawakuniongezea chochote. 7 2:7Badala yake walitambua kwamba nilikuwa nimekabidhiwa kazi ya kuhubiri Injili kwa watu wa Mataifa, kama vile Petro alivyokabidhiwa kuhubiri Injili kwa Wayahudi. 8 2:8Kwa maana, Mungu aliyekuwa akitenda kazi katika huduma ya Petro kama mtume kwa Wayahudi, ndiye pia aliyekuwa anatenda kazi katika huduma yangu kama mtume kwa watu wa Mataifa. 9 2:9Basi, Yakobo, Kefa 2:9 Yaani Petro, pia mstari 11, 14. na Yohana, walioonekana kama nguzo za kanisa, walitupa mkono wa shirika, mimi na Barnaba walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi twende kwa watu wa Mataifa na wao waende kwa Wayahudi. 10 2:10Walichotuomba ni kwamba tuendelee kuwakumbuka maskini, jambo ambalo ndilo nililokuwa na shauku ya kulifanya.

Paulo Ampinga Petro Huko Antiokia

11 2:11Lakini Petro alipofika Antiokia, mimi nilimpinga ana kwa ana kwa sababu alikuwa amekosea kwa wazi. 12 2:12Kabla baadhi ya watu waliotoka kwa Yakobo hawajafika, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa. Lakini hao watu walipofika alianza kujiondoa na kujitenga na watu wa Mataifa kwa sababu aliwaogopa wale wa kundi la tohara. 13 2:13Pia Wayahudi wengine waliungana naye katika unafiki huu, hata Barnaba naye akapotoshwa na unafiki wao.

14 2:14Nilipoona kwamba hawatendi sawasawa na kweli ya Injili, nilimwambia Petro mbele ya wote, “Wewe ni Myahudi, nawe unaishi kama mtu wa Mataifa na wala si kama Myahudi. Imekuwaje basi, mnawalazimisha watu wa Mataifa kufuata desturi za Kiyahudi?

Wayahudi Na Watu Wa Mataifa Wanaokolewa Kwa Imani

15 2:15“Sisi wenyewe ni Wayahudi kwa kuzaliwa na si watu wenye dhambi kama watu wa Mataifa, 16 2:16bado tunajua ya kwamba mtu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria bali kwa njia ya imani katika Yesu Kristo. Hivyo sisi pia, tumemwamini Kristo Yesu ili tupate kuhesabiwa haki kwa njia ya imani katika Kristo, wala si kwa matendo ya sheria, kwa sababu kwa kushika sheria hakuna hata mtu mmoja atakayehesabiwa haki.

17 2:17“Lakini tukitafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, inakuwa dhahiri kwamba sisi ni wenye dhambi. Je, ina maana kwamba Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? La hasha! 18 2:18Lakini ikiwa mimi ninajenga tena kile ambacho nimekwisha kukibomoa, basi ninaonyesha kwamba mimi ni mkosaji. 19 2:19Kwa maana mimi kwa njia ya sheria, nimeifia sheria ili nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. 20 2:20Nimesulubiwa pamoja na Kristo, wala si mimi tena ninayeishi, bali Kristo ndiye aishiye ndani yangu. Uhai nilio nao sasa katika mwili, ninaishi kwa imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda na kujitoa kwa ajili yangu. 21 2:21Siibatilishi neema ya Mungu, kwa maana kama haki ingeweza kupatikana kwa njia ya sheria, basi Kristo alikufa bure!”

3Imani Au Kushika Sheria?

1 3:1Ninyi Wagalatia wajinga! Ni nani aliyewaroga? Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele yenu kwamba amesulubiwa. 2 3:2Nataka nijifunze neno moja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa kushika sheria, au kwa kuyaamini yale mliyosikia? 3 3:3Je, ninyi ni wajinga kiasi hicho? Baada ya kuanza kwa Roho, je, sasa mwataka kumalizia katika mwili? 4 3:4Je, mlipata mateso kiasi hicho bure? Ni kama kweli yalikuwa bure! 5 3:5Je, Mungu huwapa Roho wake na kufanya miujiza katikati yenu kwa sababu mnatii sheria, au kwa sababu mnaamini kile mlichosikia?

6 3:6Kama vile “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.” 7 3:7Fahamuni basi kwamba wale walio na imani, hao ndio watoto wa Abrahamu. 8 3:8Maandiko yakitabiri kwamba Mungu angewahesabia haki watu wa Mataifa kwa imani, alitangulia kumtangazia Abrahamu Injili akisema kwamba, “Kwa kupitia kwako mataifa yote yatabarikiwa.” 9 3:9Kwa sababu hii, wale wote wanaoamini wanabarikiwa pamoja na Abrahamu, mtu wa imani.

Sheria Na Laana

10 3:10Kwa maana wote wanaotumainia matendo ya sheria wako chini ya laana, kwa kuwa imeandikwa, “Alaaniwe kila mtu asiyeshikilia kutii mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.” 11 3:11Basi ni dhahiri kwamba hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kushikilia sheria, kwa maana, “Mwenye haki ataishi kwa imani.” 12 3:12Lakini sheria haitegemei imani. Kinyume chake, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.” 13 3:13Kristo alitukomboa kutoka laana ya sheria kwa kufanyika laana kwa ajili yetu, kwa maana imeandikwa, “Amelaaniwa yeye aangikwaye juu ya mti.” 14 3:14Alitukomboa ili kwamba baraka aliyopewa Abrahamu ipate kuwafikia watu wa Mataifa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kwa imani tupate kupokea ile ahadi ya Roho.

Sheria Na Ahadi

15 3:15Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. 16 3:16Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo. 17 3:17Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. 18 3:18Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi.

Kusudi La Sheria

19 3:19Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. 20 3:20Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja.

21 3:21Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria. 22 3:22Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini.

23 3:23Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. 24 3:24Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. 25 3:25Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria.

Watoto Wa Mungu

26 3:26Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. 27 3:27Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. 28 3:28Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. 29 3:29Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

41 4:1Lile nisemalo ni kwamba wakati wote mrithi bado ni mtoto, hana tofauti na mtumwa, ingawa ndiye mmiliki wa mali yote. 2 4:2Yeye huwa yuko chini ya uangalizi wa walezi na wadhamini mpaka ufike wakati uliowekwa na baba yake. 3 4:3Vivyo hivyo na sisi, tulipokuwa bado watoto wadogo, tulikuwa utumwani chini ya taratibu za kawaida za ulimwengu. 4 4:4Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe, ambaye alizaliwa na mwanamke, akazaliwa chini ya sheria, 5 4:5kusudi awakomboe wale waliokuwa chini ya sheria, ili tupate kupokea zile haki kamili za kufanywa watoto wa Mungu. 6 4:6Kwa sababu ninyi ni watoto wa Mungu, Mungu amemtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, anayelia, “Abba, 4:6 Abba ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni Baba; lingeweza kutumiwa tu na mtoto wa kuzaa. Baba.” 7 4:7Kwa hiyo, wewe si mtumwa tena, bali ni mtoto, kwa kuwa wewe ni mtoto, Mungu amekufanya wewe pia kuwa mrithi kwa kupitia Kristo.

Paulo Awashawishi Wagalatia

8 4:8Zamani, mlipokuwa hammjui Mungu, mlikuwa watumwa wa viumbe ambavyo kwa asili si Mungu. 9 4:9Lakini sasa kwa kuwa mmemjua Mungu, au zaidi mmejulikana na Mungu, inakuwaje mnarejea tena katika zile kanuni za kwanza zenye udhaifu na upungufu? Mnataka ziwafanye tena watumwa? 10 4:10Mnaadhimisha siku maalum, miezi, nyakati na miaka! 11 4:11Nina hofu juu yenu, kwamba kazi niliyofanya kwa ajili yenu inaweza kuwa nimejitaabisha bure.

12 4:12Ndugu zangu, nawasihi mwe kama mimi, kwa sababu mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunitendea jambo lolote baya. 13 4:13Ninyi mwajua kwamba ni kwa ajili ya udhaifu wangu niliwahubiria Injili. 14 4:14Ingawa hali yangu iliwatia majaribuni, hamkunidharau wala kunidhihaki, bali mlinikaribisha kama malaika wa Mungu, kama vile Kristo Yesu. 15 4:15Ile hali ya furaha mliyokuwa nayo imekwenda wapi? Naweza kushuhudia kwamba, kama ingewezekana mngengʼoa macho yenu na kunipa mimi. 16 4:16Je, sasa nimekuwa adui yenu kwa kuwaambia kweli?

17 4:17Hao wana shauku ya kuwapata lakini si kwa kusudi zuri. Wanachotaka ni kuwatenga mbali nasi, ili ninyi mpate kuwaonea wao shauku. 18 4:18Ni vizuri wakati wote kuwa na shauku kwa ajili ya kusudi zuri, si wakati nikiwa pamoja nanyi tu. 19 4:19Watoto wangu wapendwa, ambao kwa mara nyingine ninawaonea utungu, ninatamani kwamba Kristo aumbike ndani yenu. 20 4:20Natamani kama ningekuwa pamoja nanyi sasa, pengine ningebadilisha sauti yangu. Kwa maana nina wasiwasi kwa ajili yenu.

Mfano Wa Hagari Na Sara

21 4:21Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je, hamjui sheria inavyosema? 22 4:22Kwa maana imeandikwa kwamba Abrahamu alikuwa na wana wawili, mmoja wa mwanamke mtumwa na wa pili wa mwanamke huru. 23 4:23Lakini, mtoto wa mwanamke mtumwa alizaliwa kwa mapenzi ya mwili, na yule mwingine wa mwanamke huru alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu.

24 4:24Mambo haya yanaweza kuchukuliwa kama mfano. Kwa maana hao wanawake wawili ni mfano wa maagano mawili: Agano la kwanza, ni lile lililofanyika katika Mlima Sinai, lizaalo watoto wa utumwa. Hili ndilo huyo Hagari. 25 4:25Basi Hagari anawakilisha Mlima Sinai ulioko Arabuni, na unafanana na Yerusalemu ya sasa ambayo iko utumwani pamoja na watoto wake. 26 4:26Lakini Yerusalemu wa juu ni huru, nayo ndiye mama yetu. 27 4:27Kwa maana imeandikwa:

“Furahi, ewe mwanamke tasa, wewe usiyezaa; paza sauti, na kuimba kwa furaha, wewe usiyepatwa na utungu wa kuzaa; kwa maana watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi kuliko wa mwanamke mwenye mume.”

28 4:28Basi, sisi ndugu zangu, ni kama Isaki, tu watoto wa ahadi. 29 4:29Lakini, kama vile ilivyokuwa siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomchokoza yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo hata sasa. 30 4:30Lakini Maandiko yasemaje? “Mwondoe mwanamke mtumwa pamoja na mwanawe, kwa sababu mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwana wa aliye huru.” 31 4:31Kwa hiyo ndugu zangu, sisi si watoto wa mwanamke mtumwa, bali wa yule aliye huru.

5Uhuru Ndani Ya Kristo

1 5:1Kristo alitupa uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na kongwa la utumwa.

2 5:2Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba kama mkikubali kutahiriwa, basi Kristo hatawafaidia chochote. 3 5:3Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika sheria yote. 4 5:4Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kwa njia ya sheria mmetengwa na Kristo, mko mbali na neema ya Mungu. 5 5:5Kwa maana, kwa njia ya Roho kwa imani, tunangojea kwa shauku tumaini la haki. 6 5:6Kwa maana ndani ya Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kwa njia ya upendo.

7 5:7Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? 8 5:8Ushawishi wa namna hiyo haukutokana na yule anayewaita. 9 5:9“Chachu kidogo huchachua donge zima.” 10 5:10Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. 11 5:11Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. 12 5:12Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!

13 5:13Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 5:14Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 5:15Kama mkiumana na kutafunana, angalieni, msije mkaangamizana.

Maisha Ya Kiroho

16 5:16Kwa hiyo nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 5:17Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 5:18Lakini kama mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria.

19 5:19Basi matendo ya mwili ni dhahiri nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 5:20kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 5:21husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi Ufalme wa Mungu.

22 5:22Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 5:23upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 5:24Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 5:25Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. 26 5:26Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.

6Chukulianeni Mizigo

1 6:1Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejesheni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. 2 6:2Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. 3 6:3Kama mtu yeyote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. 4 6:4Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. 5 6:5Kwa maana, kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe. 6 6:6Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

7 6:7Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. 8 6:8Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. 9 6:9Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 6:10Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

Si Kutahiriwa Bali Kuwa Kiumbe Kipya

11 6:11Angalieni herufi kubwa nitumiazo ninapowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!

12 6:12Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanataka wawalazimishe kutahiriwa. Sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo. 13 6:13Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu. 14 6:14Mungu apishie mbali nisije nikajivunia kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye ulimwengu umesulubiwa kwangu, nami nimesulubiwa kwa ulimwengu. 15 6:15Kwa maana katika Kristo Yesu, kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! 16 6:16Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii, na juu ya Israeli wa Mungu.

17 6:17Hatimaye, tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu.

18 6:18Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.