Isaya

1Isaya1 1:1Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.

Taifa Asi 2 1:2Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia! Kwa maana Bwana amesema: “Nimewalisha watoto na kuwalea, lakini wameniasi mimi. 3 1:3Ngʼombe anamjua bwana wake, naye punda anajua hori la mmiliki wake, lakini Israeli hajui, watu wangu hawaelewi.” 4 1:4Lo! Taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, uzao wa watenda mabaya, watoto waliozoelea upotovu! Wamemwacha Bwana, Wamemkataa kwa dharau yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na kumgeuzia kisogo. 5 1:5Kwa nini mzidi kupigwa? Kwa nini kudumu katika uasi? Kichwa chako chote kimejeruhiwa, moyo wako wote ni mgonjwa. 6 1:6Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako hakuna uzima: ni majeraha matupu na makovu na vidonda vitokavyo damu, havikusafishwa au kufungwa wala kulainishwa kwa mafuta. 7 1:7Nchi yenu imekuwa ukiwa, miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu imeachwa tupu na wageni mbele ya macho yenu, imeharibiwa kama vile imepinduliwa na wageni. 8 1:8Binti Sayuni ameachwa kama kipenu katika shamba la mizabibu, kama kibanda katika shamba la matikitimaji, kama mji uliohusuriwa. 9 1:9Kama Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote 1:9 Bwana Mwenye Nguvu Zote hapa ni Yehova Sabaoth, yaani Bwana wa Majeshi; pia Warumi 9:29 na Yakobo 5:4. asingelituachia walionusurika, tungelikuwa kama Sodoma, tungelifanana na Gomora. 10 1:10Sikieni neno la Bwana, ninyi watawala wa Sodoma; sikilizeni sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora! 11 1:11 Bwana anasema, “Wingi wa sadaka zenu, ni kitu gani kwangu? Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi, za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona. Sipendezwi na damu za mafahali wala za wana-kondoo na mbuzi. 12 1:12Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu, ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo, huku kuzikanyaga nyua zangu? 13 1:13Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana! Uvumba wenu ni chukizo kwangu. Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada: siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu. 14 1:14Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa: moyo wangu unazichukia. Zimekuwa mzigo kwangu, nimechoka kuzivumilia. 15 1:15Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi, nitaficha macho yangu nisiwaone; hata mkiomba maombi mengi sitasikiliza. Mikono yenu imejaa damu; 16 1:16jiosheni na mkajitakase. Yaondoeni matendo yenu maovu mbele zangu! Acheni kutenda mabaya, 17 1:17jifunzeni kutenda mema! Tafuteni haki, watieni moyo walioonewa. Teteeni shauri la yatima, wateteeni wajane. 18 1:18“Njooni basi tuhojiane,” asema Bwana. “Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu, zitakuwa nyeupe kama theluji; ingawa ni nyekundu sana kama damu, zitakuwa nyeupe kama sufu. 19 1:19Kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi, 20 1:20lakini kama mkikataa na kuasi, mtaangamizwa kwa upanga.” Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena. 21 1:21Tazama jinsi mji uliokuwa mwaminifu umekuwa kahaba! Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu, haki ilikuwa inakaa ndani yake, lakini sasa ni wauaji! 22 1:22Fedha yenu imekuwa takataka, divai yenu nzuri imechanganywa na maji. 23 1:23Watawala wenu ni waasi, rafiki wa wevi, wote wanapenda rushwa na kukimbilia hongo. Hawatetei yatima, shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe. 24 1:24Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi: “Lo, nitapata faraja kutoka kwa adui zangu na kujilipizia kisasi juu ya watesi wangu. 25 1:25Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu, nitawasafisha takataka zenu zote na kuwaondolea unajisi wenu wote. 26 1:26Nitawarudishia waamuzi wenu kama ilivyokuwa siku za zamani, nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni. Baadaye utaitwa, Mji wa Haki, Mji Mwaminifu.” 27 1:27Sayuni itakombolewa kwa haki, wale waliomo ndani yake waliotubu kwa uaminifu. 28 1:28Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa, nao wanaomwacha Bwana wataangamia. 29 1:29“Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni ambayo mlifurahia, mtafadhaika kwa sababu ya bustani mlizozichagua. 30 1:30Mtakuwa kama mwaloni wenye majani yanayonyauka, kama bustani isiyokuwa na maji. 31 1:31Mtu mwenye nguvu atatoweka kama majani makavu yawakayo moto, na kazi yake kama cheche ya moto; vyote vitaungua pamoja, wala hakuna wa kuuzima huo moto.” 2Mlima Wa Bwana (Mika 4:1-3)

1 2:1Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu:

2 2:2Katika siku za mwisho

mlima wa Hekalu la Bwana utaimarishwa kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote, utainuliwa juu ya vilima, na mataifa yote yatamiminika huko.

3 2:3Mataifa mengi yatakuja na kusema,

“Njooni, twendeni mlimani mwa Bwana, kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo. Atatufundisha njia zake, ili tuweze kuenenda katika mapito yake.” Sheria itatoka Sayuni, neno la Bwana litatoka Yerusalemu. 4 2:4Atahukumu kati ya mataifa na ataamua migogoro ya mataifa mengi. Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine, wala hawatajifunza vita tena. 5 2:5Njooni, enyi nyumba ya Yakobo, tutembeeni katika nuru ya Bwana. Siku Ya Bwana 6 2:6Umewatelekeza watu wako, nyumba ya Yakobo. Wamejaa ushirikina utokao Mashariki, wanapiga ramli kama Wafilisti na wanashikana mikono na wapagani. 7 2:7Nchi yao imejaa fedha na dhahabu, hakuna mwisho wa hazina zao. Nchi yao imejaa farasi, hakuna mwisho wa magari yao. 8 2:8Nchi yao imejaa sanamu, wanasujudia kazi za mikono yao, vitu vile vidole vyao vimevitengeneza. 9 2:9Kwa hiyo mwanadamu atashushwa na binadamu atanyenyekezwa: usiwasamehe. 10 2:10Ingieni kwenye miamba, jificheni ardhini kutokana na utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake! 11 2:11Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa na kiburi cha wanadamu kitashushwa, Bwana peke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo. 12 2:12 Bwana Mwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi, kwa wote wanaojikweza (nao watanyenyekezwa), 13 2:13kwa mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu sana, na mialoni yote ya Bashani, 14 2:14kwa milima yote mirefu na vilima vyote vilivyoinuka, 15 2:15kwa kila mnara ulio mrefu sana na kila ukuta wenye ngome, 16 2:16kwa kila meli ya biashara, 2:16 Au: ya Tarshishi (ona pia 1Fal 10:22; 22:48; 2Nya 9:21; 20:36; Isa 60:9.) na kila chombo cha baharini cha fahari. 17 2:17Majivuno ya mwanadamu yatashushwa, na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa, Bwana peke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo, 18 2:18nazo sanamu zitatoweka kabisa. 19 2:19Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba, na kwenye mahandaki ardhini kutokana na utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia. 20 2:20Siku ile, watu watawatupia panya na popo sanamu zao za fedha na za dhahabu, walizozitengeneza ili waziabudu. 21 2:21Watakimbilia kwenye mapango miambani na kwenye nyufa za miamba kutokana na utisho wa Bwana na utukufu wa enzi yake, ainukapo kuitikisa dunia. 22 2:22Acheni kumtumainia mwanadamu, ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake. Yeye ana thamani gani? 3Hukumu Juu Ya Yerusalemu Na Yuda. 1 3:1Tazama sasa, Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda upatikanaji wa mahitaji na misaada, upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji, 2 3:2shujaa na mtu wa vita, mwamuzi na nabii, mwaguzi na mzee, 3 3:3jemadari wa kikosi cha watu hamsini na mtu mwenye cheo, mshauri, fundi stadi na mlozi mjanja. 4 3:4Nitawafanya wavulana wawe maafisa wao, watoto ndio watakaowatawala. 5 3:5Watu wataoneana wao kwa wao: mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake. Kijana atainuka dhidi ya mzee, mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima. 6 3:6Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake katika nyumba ya baba yake na kusema, “Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu, tawala lundo hili la magofu!” 7 3:7Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema, “Sina uponyaji. Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu, msinifanye niwe kiongozi wa watu.” 8 3:8Yerusalemu inapepesuka, Yuda inaanguka; maneno yao na matendo yao ni kinyume na Bwana, wakiudharau uwepo wake uliotukuka. 9 3:9Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao, hujivunia dhambi yao kama Sodoma, wala hawaifichi. Ole wao! Wamejiletea maafa juu yao wenyewe. 10 3:10Waambie wanyofu itakuwa heri kwao, kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao. 11 3:11Ole kwa watu waovu! Maafa yapo juu yao! Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda. 12 3:12Vijana wanawatesa watu wangu, wanawake wanawatawala. Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha, wanawapoteza njia. 13 3:13 Bwana anachukua nafasi yake mahakamani, anasimama kuhukumu watu. 14 3:14 Bwana anaingia katika hukumu dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake: “Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu, mali zilizonyangʼanywa maskini zimo nyumbani mwenu. 15 3:15Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu na kuzisaga nyuso za maskini?” asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote. 16 3:16 Bwana asema, “Wanawake wa Sayuni wana kiburi, wanatembea na shingo ndefu, wakikonyeza kwa macho yao, wanatembea kwa hatua za madaha, wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao. 17 3:17Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni; Bwana atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”

18 3:18Katika siku ile Bwana atawanyangʼanya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo, 19 3:19vipuli, vikuku, shela, 20 3:20vilemba, mikufu ya vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi, 21 3:21pete zenye muhuri, pete za puani, 22 3:22majoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha, 23 3:23vioo, mavazi ya kitani, taji na shali.

24 3:24Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo; badala ya mishipi, ni kamba; badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, ni upara; badala ya mavazi mazuri, ni nguo za magunia; badala ya uzuri, ni alama ya aibu kwa chuma cha moto. 25 3:25Wanaume wako watauawa kwa upanga, nao mashujaa wako watauawa vitani. 26 3:26Malango ya Sayuni yataomboleza na kulia, ataketi mavumbini akiwa fukara. 41 4:1Katika siku ile wanawake saba watamshika mwanaume mmoja wakisema, “Tutakula chakula chetu wenyewe na kuvaa nguo zetu wenyewe, ila wewe uturuhusu tu tuitwe kwa jina lako. Utuondolee aibu yetu!” Tawi La Bwana

2 4:2Katika siku ile Tawi la Bwana litakuwa zuri na lenye utukufu, nalo tunda la nchi litakuwa fahari na utukufu wa wale Waisraeli watakaonusurika. 3 4:3Wale watakaoachwa Sayuni, watakaobaki Yerusalemu, wataitwa watakatifu, wale wote ambao wameorodheshwa miongoni mwa walio hai huko Yerusalemu. 4 4:4Bwana atausafisha uchafu wa wanawake wa Sayuni, atatakasa madoa ya damu kutoka Yerusalemu kwa Roho ya hukumu na Roho ya moto. 5 4:5Kisha Bwana ataumba juu ya Mlima wote wa Sayuni, na juu ya wale wote wanaokusanyika hapo, wingu la moshi wakati wa mchana, na kungʼaa kwa miali ya moto wakati wa usiku, nako juu ya huo utukufu wote kutatanda kifuniko cha ulinzi. 6 4:6Utakuwa sitara na kivuli kutokana na joto la mchana, na kuwa mahali pa kujificha kutokana na dhoruba na mvua.

5Wimbo Wa Shamba La Mizabibu 1 5:1Nitaimba wimbo kwa ajili ya mmoja nimpendaye, kuhusu shamba lake la mizabibu: Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu kwenye kilima chenye rutuba. 2 5:2Alililima na kuondoa mawe na akaliotesha mizabibu bora sana. Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake, na kutengeneza shinikizo la kukamulia divai pia. Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri, lakini lilizaa matunda mabaya tu. 3 5:3“Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda, hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu. 4 5:4Ni nini zaidi ambacho kingeweza kufanyika kwa shamba langu la mizabibu kuliko yale niliyofanya? Nilipotazamia kupata zabibu nzuri, kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu? 5 5:5Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea shamba langu la mizabibu: Nitaondoa uzio wake, nalo litaharibiwa, nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa. 6 5:6Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu, halitakatiwa matawi wala kulimwa, nayo michongoma na miiba itamea huko, nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.” 7 5:7Shamba la mzabibu la Bwana Mwenye Nguvu Zote ni nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni bustani yake ya kumpendeza. Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu, alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu. Ole Na Hukumu 8 5:8Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi. 9 5:9 Bwana Mwenye Nguvu Zote amesema nikisikia: “Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa, nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa. 10 5:10Shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi 5:10 Bathi moja ni sawa na lita 22. moja ya divai, na homeri 5:10 Homeri moja ni sawa na lita 220. ya mbegu zilizopandwa itatoa efa 5:10 Efa moja ni sawa na lita 22. moja tu ya nafaka.” 11 5:11Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema wakikimbilia kunywa vileo, wale wakawiao sana mpaka usiku, mpaka wamewaka kwa mvinyo. 12 5:12Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao, matari, filimbi na mvinyo, lakini hawayajali matendo ya Bwana, wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake. 13 5:13Kwa hiyo watu wangu watakwenda uhamishoni kwa sababu ya kukosa ufahamu, watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa na watu wao wengi watakauka kwa kiu. 14 5:14Kwa hiyo kaburi 5:14 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol. limeongeza hamu yake na kupanua mdomo wake bila kikomo, ndani mwake watashuka wakuu wao na wingi wa watu, pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote. 15 5:15Hivyo mwanadamu atashushwa, na binadamu kunyenyekezwa, macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa. 16 5:16Lakini Bwana Mwenye Nguvu Zote atatukuzwa kwa ajili ya haki yake, naye Mungu Mtakatifu atajionyesha mwenyewe kuwa mtakatifu kwa haki yake. 17 5:17Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe, wana-kondoo watajilisha katika magofu ya matajiri. 18 5:18Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu na uovu kama kwa kamba za mkokoteni, 19 5:19kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka, aharakishe kazi yake ili tupate kuiona. Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike, tena udhihirike ili tupate kuujua.” 20 5:20Ole wao wanaoita ubaya ni wema, na wema ni ubaya, wawekao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza, wawekao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu. 21 5:21Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe, na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe. 22 5:22Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo, nao walio hodari katika kuchanganya vileo, 23 5:23wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo, lakini huwanyima haki wasio na hatia. 24 5:24Kwa hiyo, kama ndimi za moto zirambavyo nyasi, na kama vile majani makavu yazamavyo katika miali ya moto, ndivyo mizizi yao itakavyooza na maua yao yatakavyopeperushwa kama mavumbi; kwa kuwa wameikataa sheria ya Bwana Mwenye Nguvu Zote na kulisukumia mbali neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli. 25 5:25Kwa hiyo hasira ya Bwana inawaka dhidi ya watu wake, mkono wake umeinuliwa na anawapiga. Milima inatetemeka, maiti ni kama takataka kwenye barabara. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. 26 5:26Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali, anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia. Tazama wamekuja, kwa kasi na kwa haraka! 27 5:27Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa, hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala, hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni, hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika. 28 5:28Mishale yao ni mikali, pinde zao zote zimevutwa, kwato za farasi wao ziko kama jiwe la gumegume, magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli. 29 5:29Ngurumo yao ni kama ile ya simba, wananguruma kama wana simba, wanakoroma wanapokamata mawindo yao, na kuondoka nayo pasipo yeyote wa kuokoa. 30 5:30Katika siku ile watanguruma juu yake kama ngurumo za bahari. Kama mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki; hata nuru itatiwa giza kwa mawingu. 6Agizo Kwa Isaya

1 6:1Katika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu. 2 6:2Juu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka. 3 6:3Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake:

“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni Bwana Mwenye Nguvu Zote; dunia yote imejaa utukufu wake.” 4 6:4Kwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.

5 6:5Ndipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote.”

6 6:6Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni. 7 6:7Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”

8 6:8Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?”

Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”

9 6:9Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa:

“ ‘Mtaendelea daima kusikiliza, lakini kamwe hamtaelewa; mtaendelea daima kutazama, lakini kamwe hamtatambua.’ 10 6:10Fanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu, fanya masikio yao yasisikie, na upofushe macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, nao wakageuka, nikawaponywa.”

11 6:11Ndipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?”

Naye akanijibu:

“Hadi miji iwe imeachwa magofu na bila wakazi, hadi nyumba zitakapobaki bila watu, na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa, 12 6:12hadi Bwana atakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana, na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa. 13 6:13Hata kama sehemu ya kumi ya watu watabaki katika nchi, itaharibiwa tena. Lakini kama vile mvinje na mwaloni ibakizavyo visiki inapokatwa, ndivyo mbegu takatifu itakavyokuwa kisiki katika nchi.” 7Ishara Ya Imanueli

1 7:1Wakati Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramu, 7:1 Yaani Shamu. na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda.

2 7:2Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo mioyo ya Ahazi na watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo.

3 7:3Ndipo Bwana akamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubu, 7:3 Shear-Yashubu maana yake Mabaki Watarudi. mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi. 4 7:4Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia. 5 7:5Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga shauri baya ili wakuangamize, wakisema, 6 7:6“Tuishambulie Yuda, naam, tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu, na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.” 7 7:7Lakini Bwana Mwenyezi asema hivi:

“ ‘Jambo hili halitatendeka, halitatokea, 8 7:8kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski, na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake. Katika muda wa miaka sitini na mitano, Efraimu atakuwa ameharibiwa kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa. 9 7:9Kichwa cha Efraimu ni Samaria, na kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia peke yake. Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu, hamtaimarika kamwe.’ ”

10 7:10 Bwana akasema na Ahazi tena, 11 7:11“Mwombe Bwana Mungu wako ishara, iwe kwenye vina virefu sana, au kwenye vimo virefu sana.”

12 7:12Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribu Bwana.”

13 7:13Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia? 14 7:14Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli. 7:14 Imanueli maana yake Mungu yu pamoja nasi. 15 7:15Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema. 16 7:16Lakini kabla mtoto hajajua kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa. 17 7:17 Bwana ataleta juu yako, juu ya watu wako, na juu ya nyumba ya baba yako wakati ambao haujawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda: yeye atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”

18 7:18Katika siku ile Bwana atawapigia filimbi mainzi kutoka vijito vya mbali vya Misri, na nyuki kutoka nchi ya Ashuru. 19 7:19Wote watakuja na kukaa kwenye mabonde yenye miteremko, na kwenye nyufa za miamba, kwenye vichaka vyote vyenye miiba, na kwenye mashimo yote ya maji. 20 7:20Katika siku ile Bwana atatumia wembe ulioajiriwa kutoka ngʼambo ya Mto, 7:20 Yaani Frati. yaani mfalme wa Ashuru, kunyoa nywele za kichwa chako na malaika ya miguu yako, na kuziondoa ndevu zako pia. 21 7:21Katika siku ile, mtu atahifadhi hai ndama mmoja na kondoo wawili. 22 7:22Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali. 23 7:23Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli 1,000 7:23 Shekeli 1,000 ni kama kilo 11.5. za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu. 24 7:24Watu watakwenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba. 25 7:25Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtakwenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba. Patakuwa mahali ambapo ngʼombe wataachiwa huru, na kondoo kukimbia kimbia.

8Ashuru, Chombo Cha Bwana

1 8:1 Bwana akaniambia, “Chukua gombo kubwa, uandike juu yake kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi. 8:1 Maher-Shalal-Hash-Bazi maana yake ni Haraka kuteka nyara, Upesi kwenye hizo nyara. 2 8:2Nami nitawaita kuhani Uria, na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.”

3 8:3Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. Kisha Bwana akaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi. 4 8:4Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”

5 8:5 Bwana akasema nami tena:

6 8:6“Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yatiririkayo taratibu wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia, 7 8:7kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao mafuriko makubwa ya Mto: 8:7 Yaani Frati. yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote. Yatafurika juu ya mifereji yake yote, yatamwagikia juu ya kingo zake zote, 8 8:8na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake, yakipita katikati na yakifika hadi shingoni. Mabawa yake yaliyokunjuliwa yatafunika upana wa nchi yako, Ee Imanueli!” 8:8 Imanueli maana yake Mungu yu pamoja nasi. 9 8:9Inueni kilio cha vita, enyi mataifa, na mkavunjwevunjwe! Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali. Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe! Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe! 10 8:10Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa; fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa, kwa maana Mungu yu pamoja nasi. 8:10 Kiebrania ni Imanueli. Mwogope Mungu

11 8:11 Bwana alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:

12 8:12“Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina, usiogope kile wanachokiogopa, wala usikihofu. 13 8:13 Bwana Mwenye Nguvu Zote ndiye peke yake ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu, ndiye peke yake utakayemwogopa, ndiye peke yake utakayemhofu, 14 8:14naye atakuwa mahali patakatifu; lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa na mwamba wa kuwaangusha. Kwa watu wa Yerusalemu, atakuwa mtego na tanzi. 15 8:15Wengi wao watajikwaa; wataanguka na kuvunjika, watategwa na kunaswa.” 16 8:16Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria miongoni mwa wanafunzi wangu. 17 8:17Nitamngojea Bwana, ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake. Nitaliweka tumaini langu kwake.

18 8:18Niko hapa, pamoja na watoto ambao Bwana amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.

19 8:19Wakati watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunongʼona na kunungʼunika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai? 20 8:20Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko. 21 8:21Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao. 22 8:22Kisha wataangalia duniani na kuona tu dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.

9Kwa Ajili Yetu Mtoto Amezaliwa

1 9:1Hata hivyo, hapatakuwepo huzuni tena kwa wale waliokuwa katika dhiki. Wakati uliopita aliidhili nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, lakini katika siku zijazo ataiheshimu Galilaya ya Mataifa, karibu na njia ya bahari, kando ya Yordani:

2 9:2Watu wanaotembea katika giza wameona nuru kuu, wale wanaoishi katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewazukia. 3 9:3Umelikuza taifa, na kuzidisha furaha yao, wanafurahia mbele zako, kama watu wanavyofurahia wakati wa mavuno, kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. 4 9:4Kama vile siku ya kushindwa kwa Wamidiani, umevunja nira iliyowalemea, ile gongo mabegani mwao na fimbo yake yeye aliyewaonea. 5 9:5Kila kiatu cha askari kilichotumiwa vitani, na kila vazi lililovingirishwa katika damu vitawekwa kwa ajili ya kuchomwa, vitakuwa kuni za kuwasha moto. 6 9:6Kwa maana, kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanaume, nao utawala utakuwa mabegani mwake. Naye ataitwa Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani. 7 9:7Kuongezeka kwa utawala wake na amani hakutakuwa na mwisho. Atatawala katika kiti cha enzi cha Daudi na juu ya ufalme wake, akiuthibitisha na kuutegemeza kwa haki na kwa adili, tangu wakati huo na hata milele. Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote utatimiza haya. Hasira Ya Bwana Dhidi Ya Israeli 8 9:8Bwana ametuma ujumbe dhidi ya Yakobo, utamwangukia Israeli. 9 9:9Watu wote watajua hili: Efraimu na wakazi wa Samaria, wanaosema kwa kiburi na majivuno ya mioyo, 10 9:10“Matofali yameanguka chini, lakini tutajenga tena kwa mawe yaliyochongwa, mitini imeangushwa, lakini tutapanda mierezi badala yake.” 11 9:11Lakini Bwana amemtia nguvu adui wa Resini dhidi yao na kuchochea watesi wao. 12 9:12Waashuru kutoka upande wa mashariki na Wafilisti kutoka upande wa magharibi wameila Israeli kwa kinywa kilichopanuliwa. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. 13 9:13Lakini watu hawajamrudia yeye aliyewapiga, wala hawajamtafuta Bwana Mwenye Nguvu Zote. 14 9:14Kwa hiyo Bwana atakatilia mbali kutoka Israeli kichwa na mkia, tawi la mtende na tete katika siku moja. 15 9:15Wazee na watu mashuhuri ndio vichwa, nao manabii wanaofundisha uongo ndio mkia. 16 9:16Wale wanaowaongoza watu hawa wanawapotosha, nao wale wanaoongozwa wamepotoka. 17 9:17Kwa hiyo Bwana hatawafurahia vijana, wala hatawahurumia yatima na wajane, kwa kuwa kila mmoja wao hamchi Mungu, nao ni waovu, na kila kinywa kinanena upotovu. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. 18 9:18Hakika uovu huwaka kama moto; huteketeza michongoma na miiba, huwasha moto vichaka vya msituni, hujiviringisha kuelekea juu kama nguzo ya moshi. 19 9:19Kwa hasira ya Bwana Mwenye Nguvu Zote nchi itachomwa kwa moto, nao watu watakuwa kuni za kuchochea moto. Hakuna mtu atakayemhurumia ndugu yake. 20 9:20Upande wa kuume watakuwa wakitafuna, lakini bado wataona njaa; upande wa kushoto watakuwa wakila, lakini hawatashiba. Kila mmoja atajilisha kwa nyama ya mtoto wake mwenyewe: 21 9:21Manase atamla Efraimu, naye Efraimu atamla Manase; nao pamoja watakuwa kinyume na Yuda. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. 101 10:1Ole wao wawekao sheria zisizo za haki, kwa wale watoao amri za kuonea, 2 10:2kuwanyima maskini haki zao na kuzuilia haki za watu wangu walioonewa, kuwafanya wajane mawindo yao na kuwanyangʼanya yatima. 3 10:3Mtafanya nini siku ya kutoa hesabu, wakati maafa yatakapokuja kutoka mbali? Mtamkimbilia nani awape msaada? Mtaacha wapi mali zenu? 4 10:4Hakutasalia kitu chochote, isipokuwa kujikunyata miongoni mwa mateka, au kuanguka miongoni mwa waliouawa. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu. Hukumu Ya Mungu Juu Ya Ashuru 5 10:5“Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu, ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu! 6 10:6Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu, ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha, kukamata mateka na kunyakua nyara, pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani. 7 10:7Lakini hili silo analokusudia, hili silo alilo nalo akilini; kusudi lake ni kuangamiza, kuyakomesha mataifa mengi. 8 10:8Maana asema, ‘Je, wafalme wote si majemadari wangu? 9 10:9Je, Kalno hakutendwa kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi, nayo Samaria si kama Dameski? 10 10:10Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu, falme ambazo vinyago vyao vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria: 11 10:11je, nisiishughulikie Yerusalemu na sanamu zake kama nilivyoshughulikia Samaria na vinyago vyake?’ ”

12 10:12Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.” 13 10:13Kwa kuwa anasema:

“ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili, kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu. Niliondoa mipaka ya mataifa, niliteka nyara hazina zao, kama yeye aliye shujaa niliwatiisha wafalme wao. 14 10:14Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota, ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa; kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya nchi zote; wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ” 15 10:15Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu zaidi kuliko yule anayelitumia, au msumeno kujisifu dhidi ya yule anayeutumia? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye, au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia! 16 10:16Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa askari wake walio hodari, katika fahari yake moto utawaka kama mwali wa moto. 17 10:17Nuru ya Israeli itakuwa moto, Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto; katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba na michongoma yake. 18 10:18Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa, kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo. 19 10:19Nayo miti inayobaki katika misitu yake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo angeweza kuihesabu. Mabaki Ya Israeli 20 10:20Katika siku ile, mabaki ya Israeli, walionusurika wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, lakini watamtegemea kwa kweli Bwana Aliye Mtakatifu wa Israeli. 21 10:21Mabaki watarudi, 10:21 Kiebrania ni Shear-Yashubu, pia 22. mabaki wa Yakobo watamrudia Mungu Mwenye Nguvu. 22 10:22Ingawa watu wako, ee Israeli, ni wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki yao tu watakaorudi. Maangamizi yamekwisha amriwa, ni mengi tena ni haki. 23 10:23Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, atatekeleza maangamizi yaliyoamriwa juu ya nchi yote.

24 10:24Kwa hiyo, hili ndilo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:

“Enyi watu wangu mkaao Sayuni, msiwaogope Waashuru, wanaowapiga ninyi kwa fimbo na kuinua rungu dhidi yenu, kama Misri ilivyofanya. 25 10:25Bado kitambo kidogo sana hasira yangu dhidi yenu itakoma, na ghadhabu yangu itaelekezwa kwenye maangamizi yao.” 26 10:26 Bwana Mwenye Nguvu Zote atawachapa kwa mjeledi, kama alivyowapiga Wamidiani katika mwamba wa Orebu, naye atainua fimbo yake juu ya maji, kama alivyofanya huko Misri. 27 10:27Katika siku hiyo mzigo wao utainuliwa kutoka mabegani mwenu, na nira yao kutoka shingoni mwenu; nira itavunjwa kwa sababu ya kutiwa mafuta. 28 10:28Wanaingia Ayathi, wanapita katikati ya Migroni, wanahifadhi mahitaji huko Mikmashi. 29 10:29Wanavuka kivukoni, nao wanasema, “Tutapiga kambi huko Geba usiku kucha.” Rama inatetemeka; Gibea ya Sauli inakimbia. 30 10:30Piga kelele, ee Binti Galimu! Sikiliza, ee Laisha! Maskini Anathothi! 31 10:31Madmena inakimbia; watu wa Gebimu wanajificha. 32 10:32Siku hii ya leo watasimama Nobu; watatikisa ngumi zao kwa mlima wa Binti Sayuni, kwa kilima cha Yerusalemu. 33 10:33Tazama, Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, atayakata matawi kwa nguvu kuu. Miti mirefu sana itaangushwa, ile mirefu itashushwa chini. 34 10:34Atakata vichaka vya msitu kwa shoka; Lebanoni itaanguka mbele zake yeye Mwenye Nguvu. 11Tawi Kutoka Kwa Yese 1 11:1Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese, kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda. 2 11:2Roho wa Bwana atakaa juu yake, Roho wa hekima na wa ufahamu, Roho wa shauri na wa uweza, Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana 3 11:3naye atafurahia kumcha Bwana. Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake, wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake, 4 11:4bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji, kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia. Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu. 5 11:5Haki itakuwa mkanda wake na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake. 6 11:6Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo, naye chui atalala pamoja na mbuzi, ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja, naye mtoto mdogo atawaongoza. 7 11:7Ngʼombe na dubu watalisha pamoja, watoto wao watalala pamoja, na simba atakula majani makavu kama maksai. 8 11:8Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka, naye mtoto mdogo ataweka mkono wake kwenye kiota cha fira. 9 11:9Hawatadhuru wala kuharibu juu ya mlima wangu mtakatifu wote, kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Bwana kama maji yajazavyo bahari.

10 11:10Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu. 11 11:11Katika siku hiyo Bwana atanyoosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, 11:11 Pathrosi ina maana Misri ya Juu. Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi na kutoka visiwa vya baharini.

12 11:12Atainua bendera kwa mataifa na kuwakusanya Waisraeli walioko uhamishoni; atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika kutoka pembe nne za dunia. 13 11:13Wivu wa Efraimu utatoweka, na adui wa Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamwonea Yuda wivu, wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu. 14 11:14Watawashukia katika miteremko ya Wafilisti hadi upande wa magharibi, kwa pamoja watawateka watu nyara hadi upande wa mashariki. Watawapiga Edomu na Moabu, na Waamoni watatawaliwa nao. 15 11:15 Bwana atakausha ghuba ya bahari ya Misri; kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake juu ya Mto Frati. Ataugawanya katika vijito saba ili watu waweze kuuvuka wakiwa wamevaa viatu. 16 11:16Itakuwepo njia kuu kwa mabaki ya watu wake wale waliosalia kutoka Ashuru, kama ilivyokuwa kwa Israeli walipopanda kutoka Misri. 12Kushukuru Na Kusifu

1 12:1Katika siku ile utasema:

“Nitakusifu wewe, Ee Bwana. Ingawa ulinikasirikia, hasira yako imegeukia mbali nawe umenifariji. 2 12:2Hakika Mungu ni wokovu wangu; nitamtumaini wala sitaogopa. Bwana, Bwana, ni nguvu zangu na wimbo wangu; amekuwa wokovu wangu.” 3 12:3Kwa furaha mtachota maji kutoka visima vya wokovu.

4 12:4Katika siku hiyo mtasema:

“Mshukuruni Bwana, mliitie jina lake; julisheni miongoni mwa mataifa yale aliyoyafanya, tangazeni kuwa jina lake limetukuka. 5 12:5Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda mambo makuu, hili na lijulikane duniani kote. 6 12:6Pazeni sauti mwimbe kwa furaha, watu wa Sayuni, kwa maana mkuu ni yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli miongoni mwenu.” 13Unabii Dhidi Ya Babeli

1 13:1Neno kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona:

2 13:2Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu, wapazieni sauti, wapungieni mkono waingie katika malango ya wenye heshima. 3 13:3Nimewaamuru watakatifu wangu; nimewaita mashujaa wangu waitimize hasira yangu: wale wanaoshangilia ushindi wangu. 4 13:4Sikilizeni kelele juu ya milima, kama ile ya umati mkubwa wa watu! Sikilizeni, makelele katikati ya falme, kama mataifa yanayokusanyika pamoja! Bwana Mwenye Nguvu Zote anakusanya jeshi kwa ajili ya vita. 5 13:5Wanakuja kutoka nchi za mbali sana, kutoka miisho ya mbingu, Bwana na silaha za ghadhabu yake, kuangamiza nchi yote. 6 13:6Ombolezeni, kwa maana siku ya Bwana i karibu, itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi. 13:6 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania. 7 13:7Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea, moyo wa kila mtu utayeyuka. 8 13:8Hofu itawakamata, uchungu na maumivu makali yatawashika, watagaagaa kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa. Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake, nyuso zao zikiwaka kama moto. 9 13:9Tazameni, siku ya Bwana inakuja, siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali, kuifanya nchi kuwa ukiwa na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo ndani yake. 10 13:10Nyota za mbinguni na makundi ya nyota havitatoa mwanga wake. Jua linalochomoza litatiwa giza na mwezi hautatoa nuru yake. 11 13:11Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake, waovu kwa ajili ya dhambi zao. Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi, na nitakishusha kiburi cha watu wakatili. 12 13:12Nitawafanya wanadamu kuwa adimu kuliko dhahabu safi, watakuwa wachache sana kuliko dhahabu ya Ofiri. 13 13:13Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke, nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake katika ghadhabu ya Bwana Mwenye Nguvu Zote, katika siku ya hasira yake iwakayo. 14 13:14Kama swala awindwaye, kama kondoo wasio na mchungaji, kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe, kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa. 15 13:15Yeyote atakayetekwa atapasuliwa tumbo, wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga. 16 13:16Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande mbele ya macho yao; nyumba zao zitatekwa na wake zao watatendwa jeuri. 17 13:17Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao, ambao hawajali fedha wala hawafurahii dhahabu. 18 13:18Mishale yao itawaangusha vijana, hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga wala hawataangalia watoto kwa huruma. 19 13:19Babeli, johari ya falme, utukufu wa kiburi cha Wababeli, 13:19 Wababeli hapa maana yake ni Wakaldayo. itaangushwa na Mungu kama Sodoma na Gomora. 20 13:20Hautakaliwa na watu kamwe wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote. Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko, hakuna mchungaji atakayepumzisha makundi yake huko. 21 13:21Lakini viumbe wa jangwani watalala huko, mbweha watajaza nyumba zake, bundi wataishi humo nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo. 22 13:22Fisi watalia ndani ya ngome zake, mbweha ndani ya majumba yake ya kifahari. Wakati wake umewadia, na siku zake hazitaongezwa. 14Yuda Kufanywa Upya 1 14:1 Bwana atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, na kuwakalisha katika nchi yao wenyewe. Wageni wataungana nao na kujiunga na nyumba ya Yakobo. 2 14:2Mataifa watawachukua na kuwaleta mahali pao wenyewe. Nayo nyumba ya Israeli itamiliki mataifa kama watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana. Watawafanya watekaji wao kuwa mateka, na kutawala juu ya wale waliowaonea.

3 14:3Katika siku Bwana atakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili, 4 14:4utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli:

Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho! Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma! 5 14:5 Bwana amevunja fimbo ya mwovu, fimbo ya utawala ya watawala, 6 14:6ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa kwa mapigo yasiyo na kikomo, nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa kwa jeuri pasipo huruma. 7 14:7Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani, wanabubujika kwa kuimba. 8 14:8Hata misunobari na mierezi ya Lebanoni inashangilia mbele yako na kusema, “Basi kwa sababu umeangushwa chini, hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.” 9 14:9Kuzimu kote kumetaharuki kukulaki unapokuja, kunaamsha roho za waliokufa ili kukupokea, wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu, kunawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme: wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa. 10 14:10Wote wataitikia, watakuambia, “Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo; wewe umekuwa kama sisi.” 11 14:11Majivuno yako yote yameshushwa mpaka kuzimu, pamoja na kelele ya vinubi vyako, mafunza yametanda chini yako, na minyoo imekufunika. 12 14:12Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya asubuhi, mwana wa mapambazuko! Umetupwa chini duniani, wewe uliyepata kuangusha mataifa! 13 14:13Ulisema moyoni mwako, “Nitapanda juu hadi mbinguni, nitakiinua kiti changu cha enzi juu ya nyota za Mungu, nitaketi nimetawazwa juu ya mlima wa kusanyiko, kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu. 14 14:14Nitapaa juu kupita mawingu, nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.” 15 14:15Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu, hadi kwenye vina vya shimo. 16 14:16Wale wanaokuona wanakukazia macho, wanatafakari hatima yako: “Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia na kufanya falme zitetemeke, 17 14:17yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa, aliyeipindua miji yake, na ambaye hakuwaachia mateka wake waende nyumbani?” 18 14:18Wafalme wote wa mataifa wamelala kwa heshima kila mmoja katika kaburi lake. 19 14:19Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako kama tawi lililokataliwa, umefunikwa na waliouawa pamoja na wale waliochomwa kwa upanga, wale washukao mpaka kwenye mawe ya shimo. Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo, 20 14:20Hutajumuika nao kwenye mazishi, kwa kuwa umeharibu nchi yako na kuwaua watu wako. Mzao wa mwovu hatatajwa tena kamwe. 21 14:21Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe kwa ajili ya dhambi za baba zao, wasije wakainuka ili kuirithi nchi na kuijaza dunia kwa miji yao. 22 14:22 Bwana Mwenye Nguvu Zote asema, “Nitainuka dhidi yao, nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli pamoja na watu wake walionusurika, watoto wake na wazao wake,” asema Bwana. 23 14:23“Nitaifanya kuwa mahali pa bundi, na kuwa nchi ya matope; nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. Unabii Dhidi Ya Ashuru

24 14:24 Bwana Mwenye Nguvu Zote ameapa,

“Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa, nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama. 25 14:25Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu, juu ya milima yangu nitawakanyagia chini. Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu, nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.” 26 14:26Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote, huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote. 27 14:27Kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amekusudia, ni nani awezaye kumzuia? Mkono wake umenyooshwa, ni nani awezaye kuurudisha? Unabii Dhidi Ya Wafilisti

28 14:28Neno hili lilikuja mwaka ule Mfalme Ahazi alipofariki:

29 14:29Msifurahi, enyi Wafilisti wote, kwamba fimbo iliyowapiga imevunjika; kutoka mzizi wa huyo nyoka atachipuka nyoka mwenye sumu kali, uzao wake utakuwa joka lirukalo, lenye sumu kali. 30 14:30Maskini kuliko maskini wote watapata malisho, nao wahitaji watalala salama. Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa, nayo njaa itawaua walionusurika. 31 14:31Piga yowe, ee lango! Bweka, ee mji! Yeyukeni, enyi Wafilisti wote! Wingu la moshi linakuja toka kaskazini, wala hakuna atakayechelewa katika safu zake. 32 14:32Ni jibu gani litakalotolewa kwa wajumbe wa taifa hilo? Bwana ameifanya imara Sayuni, nako ndani yake watu wake walioonewa watapata kimbilio.” 15Unabii Dhidi Ya Moabu

1 15:1Neno kuhusu Moabu:

Ari iliyo Moabu imeangamizwa: imeharibiwa kwa usiku mmoja! Kiri iliyo Moabu imeangamizwa, imeharibiwa kwa usiku mmoja! 2 15:2Diboni anakwea hadi kwenye hekalu lake, mpaka mahali pake pa juu ili walie, Moabu anaombolezea Nebo na Medeba. Kila kichwa kimenyolewa na kila ndevu limeondolewa. 3 15:3Wamevaa nguo za magunia barabarani, juu ya mapaa na kwenye viwanja wote wanaomboleza, wamelala kifudifudi kwa kulia. 4 15:4Heshboni na Eleale wanalia, sauti zao zinasikika hadi Yahazi. Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu wanapiga kelele, nayo mioyo yao imezimia. 5 15:5Moyo wangu unamlilia Moabu; wakimbizi wake wanakimbilia Soari, hadi Eglath-Shelishiya. Wanapanda njia ya kwenda Luhithi, wanakwenda huku wanalia; barabarani iendayo Horonaimu wanaombolezea maangamizi yao. 6 15:6Maji ya Nimrimu yamekauka na majani yamenyauka; mimea imekauka wala hakuna kitu chochote kibichi kilichobaki. 7 15:7Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi. 8 15:8Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu, kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu, maombolezo yao hadi Beer-Elimu. 9 15:9Maji ya Dimoni yamejaa damu, lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni: simba juu ya wakimbizi wa Moabu na juu ya wale wanaobaki katika nchi. 16Hali Ya Kukata Tamaa Ya Moabu 1 16:1Pelekeni wana-kondoo kama ushuru kwa mtawala wa nchi, Kutoka Sela, kupitia jangwani, hadi mlima wa Binti Sayuni. 2 16:2Kama ndege wanaopapatika waliofukuzwa kutoka kwenye kiota, ndivyo walivyo wanawake wa Moabu kwenye vivuko vya Arnoni. 3 16:3“Tupeni shauri, toeni uamuzi. Wakati wa adhuhuri, fanyeni kivuli chenu kama usiku. Waficheni watoro, msisaliti wakimbizi. 4 16:4Waacheni watoro wa Moabu wakae pamoja nanyi; kuweni mahali pao pa salama ili kuepuka mharabu.” Mtesi atafikia mwisho na maangamizi yatakoma, aletaye vita atatoweka kutoka nchi. 5 16:5Kwa upendo kiti cha enzi kitaimarishwa, kwa uaminifu mtu ataketi juu yake, yeye atokaye nyumba ya Daudi: yeye ambaye katika kuhukumu hutafuta haki, na huhimiza njia ya haki. 6 16:6Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu: kiburi chake cha kujivuna na udanganyifu, kiburi chake na ufidhuli wake, lakini majivuno yake si kitu. 7 16:7Kwa hiyo Wamoabu wanaomboleza, wanaiombolezea Moabu kwa pamoja. Wanaomboleza na kuhuzunika kwa ajili ya watu wa Kir-Haresethi. 8 16:8Mashamba ya Heshboni yananyauka, pia na mizabibu ya Sibma. Watawala wa mataifa wamekanyaga mizabibu iliyo mizuri sana, ambayo ilipata kufika Yazeri na kuenea kuelekea jangwani. Machipukizi yake yalienea yakafika hadi baharini. 9 16:9Hivyo ninalia kama Yazeri aliavyo, kwa ajili ya mizabibu ya Sibma. Ee Heshboni, ee Eleale, ninakulowesha kwa machozi! Kelele za furaha kwa ajili ya tunda lako lililoiva na kwa ajili ya mavuno zimekomeshwa. 10 16:10Furaha na shangwe zimeondolewa kutoka mashamba ya matunda; hakuna yeyote aimbaye wala apazaye sauti katika mashamba ya mizabibu; hakuna yeyote akanyagaye zabibu shinikizoni, kwa kuwa nimekomesha makelele. 11 16:11Moyo wangu unaomboleza kwa ajili ya Moabu kama kinubi, nafsi yangu yote kwa ajili ya Kir-Haresethi. 12 16:12Wakati Moabu anapojitokeza mahali pake pa juu, anajichosha mwenyewe tu; anapokwenda mahali pake pa kuabudia miungu ili kuomba, haitamfaidi lolote.

13 16:13Hili ndilo neno ambalo Bwana ameshasema kuhusu Moabu. 14 16:14Lakini sasa Bwana anasema: “Katika miaka mitatu, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, fahari ya Moabu na watu wake wengi watadharauliwa, nao walionusurika watakuwa wachache sana, tena wanyonge.”

17Neno Dhidi Ya Dameski

1 17:1Neno kuhusu Dameski:

“Tazama, Dameski haitakuwa tena mji bali itakuwa lundo la magofu. 2 17:2Miji ya Aroeri itaachwa na itaachiwa mifugo ambayo italala huko, bila yeyote wa kuyaogopesha. 3 17:3Mji wenye ngome utatoweka kutoka Efraimu, nao uweza wa ufalme kutoka Dameski; mabaki ya Aramu yatakuwa kama utukufu wa Waisraeli,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote. 4 17:4“Katika siku ile utukufu wa Yakobo utafifia, unono wa mwili wake utadhoofika. 5 17:5Itakuwa kama mvunaji akusanyavyo nafaka na kuvuna nafaka kwa mikono yake, kama wakati mtu aokotapo masazo ya masuke katika Bonde la Warefai. 6 17:6Hata hivyo baadhi ya masazo yatabaki, kama vile mti wa mzeituni unavyopigwa, kukiachwa zeituni mbili au tatu juu ya matawi kileleni, nne au tano katika matawi yazaayo sana,” asema Bwana, Mungu wa Israeli. 7 17:7Katika siku ile watu watamwangalia Muumba wao, na kuelekeza macho yao kwa yule Aliye Mtakatifu wa Israeli. 8 17:8Hawataziangalia tena madhabahu, kazi za mikono yao, nao hawataheshimu nguzo za Ashera, 17:8 Ashera hapa maana yake ni mungu mke aliyekuwa akiabudiwa pamoja na Baali. na madhabahu za kufukizia uvumba zilizofanywa kwa mikono yao.

9 17:9Katika siku ile miji yao iliyo imara, ambayo waliihama kwa sababu ya Waisraeli, itakuwa kama mahali palipoachwa pa vichaka na magugu. Nayo yote itakuwa ukiwa.

10 17:10Mmemsahau Mungu Mwokozi wenu, hamkumkumbuka Mwamba aliye ngome yenu. Kwa hiyo, hata ingawa mlipandikiza mimea iliyo mizuri sana na kuotesha mizabibu ya kigeni, 11 17:11hata kama siku ile unapoipandikiza, unaifanya iote na asubuhi ile ile unayoipanda, unaifanya ichipue, hata hivyo mavuno yatakuwa kama si kitu katika siku ile ya ugonjwa na maumivu yasiyoponyeka. 12 17:12Lo! Ghadhabu ya mataifa mengi, wanaghadhibika kama bahari iliyochafuka! Lo! Makelele ya mataifa wanavuma kama ngurumo za maji mengi! 13 17:13Ingawa mataifa yanavuma kama ngurumo za maji yanayofanya mawimbi, wakati anapoyakemea yanakimbia mbali, yanafukuzwa mbele ya upepo kama makapi juu ya milima, kama jani livingirishwapo na dhoruba. 14 17:14Wakati wa jioni, hofu ya ghafula! Kabla ya asubuhi, wametoweka! Hili ndilo fungu la wale wanaotupora, fungu la wale wanaotunyangʼanya mali zetu. 18Unabii Dhidi Ya Kushi 1 18:1Ole kwa nchi ya mvumo wa mabawa, 18:1 Au: wa nzige. kando ya mito ya Kushi, 2 18:2iwapelekayo wajumbe wake kwa njia ya bahari kwa mashua za mafunjo juu ya maji. Nendeni, wajumbe wepesi, kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito. 3 18:3Enyi mataifa yote ya ulimwengu, ninyi mnaoishi duniani wakati bendera itakapoinuliwa milimani, mtaiona, nayo tarumbeta itakapolia, mtaisikia. 4 18:4Hili ndilo Bwana aliloniambia: “Nitatulia kimya na kutazama kutoka maskani yangu, kama joto linalometameta katika mwanga wa jua, kama wingu la umande katika joto la wakati wa mavuno.” 5 18:5Kwa maana, kabla ya mavuno, wakati wa kuchanua ukishapita na maua yakawa zabibu zinazoiva, atayakata machipukizi kwa mundu wa kupogolea matawi, naye atakata na kuyaondoa matawi yaliyopanuka. 6 18:6Yote yataachwa kwa ajili ya ndege wawindao wa mlimani na wanyama pori, ndege watajilisha juu yake wakati wote wa kiangazi, nao wanyama pori wakati wote wa masika.

7 18:7Wakati huo matoleo yataletwa kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote

kutoka kwa taifa la watu warefu wenye ngozi nyororo, kutoka kwa taifa linaloogopwa mbali na karibu, kutoka taifa gomvi lenye lugha ngeni, ambalo nchi yao imegawanywa kwa mito, matoleo yataletwa katika Mlima Sayuni, mahali pa Jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote. 19Unabii Kuhusu Misri

1 19:1Neno kuhusu Misri:

Tazama, Bwana amepanda juu ya wingu liendalo kwa haraka naye anakuja Misri. Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake, nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao. 2 19:2“Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri, ndugu atapigana dhidi ya ndugu, jirani dhidi ya jirani, mji dhidi ya mji, ufalme dhidi ya ufalme. 3 19:3Wamisri watakufa moyo, na nitaibatilisha mipango yao. Watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa, kwa waaguzi na kwa wale waongeao na mizimu. 4 19:4Nitawatia Wamisri mikononi mwa bwana mkatili na mfalme mkali atatawala juu yao,” asema Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote. 5 19:5Maji ya mito yatakauka, chini ya mto kutakauka kwa jua. 6 19:6Mifereji itanuka; vijito vya Misri vitapungua na kukauka. Mafunjo na nyasi vitanyauka, 7 19:7pia mimea iliyoko kando ya Mto Naili, pale mto unapomwaga maji baharini. Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Naili litakauka, litapeperushwa na kutoweka kabisa. 8 19:8Wavuvi watalia na kuomboleza, wale wote watupao ndoano katika Mto Naili, watadhoofika kwa majonzi. 9 19:9Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa, wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo. 10 19:10Wafanyao kazi ya kufuma nguo watahuzunishwa, nao vibarua wataugua moyoni. 11 19:11Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa, washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga. Unawezaje kumwambia Farao, “Mimi ni mmojawapo wa watu wenye hekima, mwanafunzi wa wafalme wa zamani”? 12 19:12Wako wapi sasa watu wako wenye hekima? Wao wakuonyeshe na kukufahamisha ni nini Bwana Mwenye Nguvu Zote amepanga dhidi ya Misri. 13 19:13Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu, viongozi wa Memfisi 19:13 Memfisi kwa Kiebrania ni Nofu. wamedanganyika, walio mawe ya pembe ya taifa lake wameipotosha Misri. 14 19:14 Bwana amewamwagia roho ya kizunguzungu; wanaifanya Misri iyumbayumbe katika yale yote inayoyafanya, kama vile mlevi ayumbayumbavyo katika kutapika kwake. 15 19:15Misri haiwezi kufanya kitu chochote, cha kichwa wala cha mkia, cha tawi la mtende wala cha tete.

16 19:16Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono wa Bwana Mwenye Nguvu Zote anaoinua dhidi yao. 17 19:17Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambacho Bwana Mwenye Nguvu Zote anapanga dhidi yao.

18 19:18Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtii Bwana Mwenye Nguvu Zote. Mji mmojawapo utaitwa Mji wa Uharibifu. 19:18 Yaani Heliopoli (Mji wa Jua).

19 19:19Katika siku hiyo patakuwepo madhabahu ya Bwana katikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwa Bwana kwenye mpaka wa Misri. 20 19:20Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili ya Bwana Mwenye Nguvu Zote katika nchi ya Misri. Watakapomlilia Bwana kwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa. 21 19:21Hivyo Bwana atajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubali Bwana. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekea Bwana nadhiri na kuzitimiza. 22 19:22 Bwana ataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. Watamgeukia Bwana, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya.

23 19:23Katika siku hiyo kutakuwepo na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru watakwenda Misri, na Wamisri watakwenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja. 24 19:24Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia. 25 19:25 Bwana Mwenye Nguvu Zote atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu, na kwa Israeli urithi wangu.”

20Unabii Dhidi Ya Misri Na Kushi

1 20:1Katika mwaka ule ambao jemadari mkuu alitumwa na Mfalme Sargoni wa Ashuru, naye akaja mpaka Ashdodi, akaushambulia na kuuteka, 2 20:2wakati ule Bwana alisema kwa kinywa cha Isaya mwana wa Amozi. Akamwambia, “Vua nguo ya gunia kutoka mwilini mwako na viatu kutoka miguuni mwako.” Naye akafanya hivyo, akatembea huku na huko uchi, bila viatu.

3 20:3Kisha Bwana akasema, “Kama vile mtumishi wangu Isaya alivyotembea uchi na bila viatu kwa miaka mitatu, kama ishara na dalili mbaya dhidi ya nchi ya Misri na Kushi, 4 20:4vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawaongoza mateka wa Wamisri, na watu wa uhamisho wa Kushi, uchi na bila viatu, vijana hata wazee, wakiwa matako wazi, kwa aibu ya Wamisri. 5 20:5Wale waliotegemea Kushi na kujivunia Misri wataogopa na kuaibika. 6 20:6Katika siku ile watu wanaoishi katika pwani hii watasema, ‘Tazama lililowapata wale tuliowategemea, wale tuliowakimbilia kwa msaada na wokovu kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru! Tutawezaje basi kupona?’ ”

21Unabii Dhidi Ya Babeli 1 21:1Neno kuhusu Jangwa kando ya Bahari: Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini, mshambuliaji anakuja kutoka jangwani, kutoka nchi inayotisha. 2 21:2Nimeonyeshwa maono ya kutisha: Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara. Elamu, shambulia! Umedi, izunguke kwa jeshi! Nitakomesha huzuni zote alizosababisha. 3 21:3Katika hili mwili wangu umeteswa na maumivu, maumivu makali ya ghafula yamenishika, kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa. Nimeduwazwa na lile ninalolisikia, nimeshangazwa na lile ninaloliona. 4 21:4Moyo wangu unababaika, woga unanifanya nitetemeke, gizagiza la jioni nililolitamani sana, limekuwa hofu kuu kwangu. 5 21:5Wanaandaa meza, wanatandaza mazulia, wanakula, wanakunywa! Amkeni, enyi maafisa, zitieni ngao mafuta!

6 21:6Hili ndilo Bwana analoniambia:

“Nenda, weka mlinzi, na atoe taarifa ya kile anachokiona. 7 21:7Anapoona magari ya vita pamoja na kundi la farasi, wapanda punda au wapanda ngamia, na awe macho, awe macho kikamilifu.”

8 21:8Naye mlinzi alipaza sauti,

“Mchana baada ya mchana, bwana wangu, ninasimama katika mnara wa ulinzi, kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa. 9 21:9Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita pamoja na kundi la farasi. Naye anajibu: ‘Babeli umeanguka, umeanguka! Vinyago vyote vya miungu yake vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ” 10 21:10Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria, ninawaambia kile nilichokisikia kutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote, kutoka kwa Mungu wa Israeli. Unabii Dhidi Ya Edomu

11 21:11Neno kuhusu Duma:

Mtu fulani ananiita kutoka Seiri, “Mlinzi, usiku utaisha lini? Mlinzi, usiku utaisha lini?” 12 21:12Mlinzi anajibu, “Asubuhi inakuja, lakini pia usiku. Kama ungeliuliza, basi uliza; bado na urudi tena.” Unabii Dhidi Ya Arabia

13 21:13Neno kuhusu Arabia:

Enyi misafara ya Wadedani, mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia, 14 21:14leteni maji kwa wenye kiu, ninyi mnaoishi Tema, leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi. 15 21:15Wanaukimbia upanga, kutoka upanga uliochomolewa alani, kutoka upinde uliopindwa, na kutoka kwenye joto la vita.

16 21:16Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho. 17 21:17Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.” Bwana, Mungu wa Israeli, amesema.

22Unabii Kuhusu Yerusalemu

1 22:1Neno kuhusu Bonde la Maono:

Nini kinachokutaabisha sasa, kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa? 2 22:2Ewe mji uliojaa ghasia, ewe mji wa makelele na sherehe! Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga, wala hawakufa vitani. 3 22:3Viongozi wako wote wamekimbia pamoja, wamekamatwa bila kutumia upinde. Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja, mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali. 4 22:4Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami, niache nilie kwa uchungu. Usijaribu kunifariji juu ya maangamizi ya watu wangu.” 5 22:5Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, anayo siku ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya katika Bonde la Maono, siku ya kuangusha kuta na ya kupiga kelele mpaka milimani. 6 22:6Elamu analichukua podo, pamoja na waendesha magari ya vita na farasi. Kiri anaifungua ngao. 7 22:7Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita, nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji; 8 22:8ulinzi wa Yuda umeondolewa. Nawe ulitazama siku ile silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni, 9 22:9mkaona kuwa Mji wa Daudi una matundu mengi katika ulinzi wake, mkaweka akiba ya maji kwenye Bwawa la Chini. 10 22:10Mlihesabu majengo katika Yerusalemu nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta. 11 22:11Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani, lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza, au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale. 12 22:12Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, aliwaita siku ile ili kulia na kuomboleza, kungʼoa nywele zenu na kuvaa nguo ya gunia. 13 22:13Lakini tazama, kuna furaha na sherehe, kuchinja ngʼombe na kuchinja kondoo, kula nyama na kunywa mvinyo! Mnasema, “Tuleni na kunywa, kwa kuwa kesho tutakufa!”

14 22:14 Bwana Mwenye Nguvu Zote amelifunua hili nikiwa ninasikia: Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, asema: “Mpaka siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”

15 22:15Hili ndilo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, asemalo:

“Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna, ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme: 16 22:16Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa kujikatia kaburi lako mwenyewe, ukichonga kaburi lako mahali palipo juu, na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba? 17 22:17“Jihadhari, Bwana yu karibu kukukamata thabiti, na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu. 18 22:18Atakuvingirisha uwe kama mpira na kukutupa katika nchi kubwa. Huko ndiko utakakofia, na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia, wewe unayeifedhehesha nyumba ya bwana wako! 19 22:19Nitakuondoa kutoka kazi yako, nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako.

20 22:20“Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia. 21 22:21Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda. 22 22:22Nitaweka mabegani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua. 23 22:23Nitamgongomea kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha enzi cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake. 24 22:24Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Watoto wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”

25 22:25 Bwana Mwenye Nguvu Zote asema, “Katika siku ile, kigingi kilichogongomewa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioningʼinia juu yake utaanguka chini.” Bwana amesema.

23Unabii Kuhusu Tiro

1 23:1Neno kuhusu Tiro:

Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi! Kwa kuwa Tiro imeangamizwa, imeachwa bila nyumba wala bandari. Kuanzia nchi ya Kitimu 23:1 Kitimu hapa ni Kipro, kisiwa katika Bahari ya Mediterania. neno limewajia. 2 23:2Nyamazeni kimya, enyi watu wa kisiwani, pia ninyi wafanyabiashara wa Sidoni, ambao mabaharia wamewatajirisha. 3 23:3Kwenye maji makuu nafaka za Shihori zilikuja; mavuno ya Naili yalikuwa mapato ya Tiro, naye akawa soko la mataifa. 4 23:4Uaibishwe ee Sidoni, nawe ee ngome la bahari, kwa kuwa bahari imesema: “Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa wala sijapata kuzaa, wala sijapata kulea wana wala kutunza mabinti.” 5 23:5Habari ifikapo Misri, watakuwa katika maumivu makuu kwa ajili ya taarifa kutoka Tiro. 6 23:6Vukeni mpaka Tarshishi, ombolezeni, enyi watu wa kisiwani. 7 23:7Je, huu ndio mji wenu uliojaa sherehe, mji wa zamani, zamani kabisa ambao miguu yake imeuchukua kufanya makao nchi za mbali sana? 8 23:8Ni nani amepanga hili dhidi ya Tiro, mji utoao mataji, ambao wafanyabiashara wake ni wana wa mfalme na wachuuzi wake ni watu mashuhuri wa dunia? 9 23:9 Bwana Mwenye Nguvu Zote ndiye alipanga jambo hili, ili kukishusha kiburi cha utukufu wote na kuwanyenyekesha wale wote ambao ni mashuhuri duniani. 10 23:10Ee Binti Tarshishi, pita katika nchi yako kama vile Mto Naili kwa kuwa huna tena bandari. 11 23:11 Bwana amenyoosha mkono wake juu ya bahari na kuzifanya falme zake zitetemeke. Ametoa amri kuhusu Kanaani kwamba ngome zake ziangamizwe. 12 23:12Alisema, “Usizidi kufurahi, ee Bikira Binti Sidoni, sasa umepondwa! “Simama, vuka uende Kitimu; hata huko hutapata pumziko.” 13 23:13Tazama katika nchi ya Wakaldayo, watu hawa ambao sasa hawaonekani kama wapo! Waashuru wameifanya nchi hiyo kuwa mahali pa viumbe wa jangwani. Wamesimamisha minara yao ya vita kuuzunguka, wameziteka ngome zake na kuziacha tupu na kuufanya kuwa magofu. 14 23:14Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi; ngome yenu imeangamizwa!

15 23:15Wakati huo Tiro utasahauliwa kwa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Lakini mwisho wa miaka hiyo sabini, itakuwa kwa Tiro kama ilivyo katika wimbo wa kahaba:

16 23:16“Twaa kinubi, tembea mjini kote, ewe kahaba uliyesahauliwa; piga kinubi vizuri, imba nyimbo nyingi, ili upate kukumbukwa.”

17 23:17Mwishoni mwa miaka sabini, Bwana atashughulika na Tiro. Naye atarudia ajira yake ya ukahaba, na atafanya biashara yake na falme zote juu ya uso wa dunia. 18 23:18Lakini faida na mapato yake yatawekwa wakfu kwa Bwana; hayatahifadhiwa wala kufichwa. Faida zake zitakwenda kwa wale wakaao mbele za Bwana kwa ajili ya chakula tele na mavazi mazuri.

24Dunia Kuharibiwa Upesi 1 24:1Tazama, Bwana ataifanya dunia kuwa ukiwa na kuiharibu, naye atauharibu uso wake na kutawanya wakaao ndani yake: 2 24:2ndivyo itakavyokuwa kwa makuhani na kwa watu, kwa bwana na kwa mtumishi, kwa bibi na kwa mtumishi wake wa kike, kwa muuzaji na kwa mnunuzi, kwa mkopaji na kwa mkopeshaji, kwa mdaiwa na kwa mdai. 3 24:3Dunia itaharibiwa kabisa na kutekwa nyara kabisa. Bwana amesema neno hili. 4 24:4Dunia inakauka na kunyauka, dunia inanyongʼonyea na kunyauka, waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea. 5 24:5Dunia imetiwa unajisi na watu wake; wameacha kutii sheria, wamevunja amri na kuvunja agano la milele. 6 24:6Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia, watu wake lazima waichukue hatia yao. Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa, nao waliosalia ni wachache sana. 7 24:7Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka, watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni. 8 24:8Furaha ya matoazi imekoma, kelele za wenye furaha zimekoma, shangwe za kinubi zimenyamaza. 9 24:9Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo, kileo ni kichungu kwa wanywaji wake. 10 24:10Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa, mlango wa kila nyumba umefungwa. 11 24:11Barabarani wanalilia kupata mvinyo, furaha yote imegeuka kuwa majonzi, furaha yote imefukuziwa mbali na dunia. 12 24:12Mji umeachwa katika uharibifu, lango lake limevunjwa vipande. 13 24:13Ndivyo itakavyokuwa duniani na miongoni mwa mataifa, kama vile wakati mzeituni upigwavyo, au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa. 14 24:14Wanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha, kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Bwana. 15 24:15Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni Bwana utukufu, liadhimisheni jina la Bwana, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari. 16 24:16Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji: “Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.” Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika! Ole wangu! Watenda hila wanasaliti! Kwa hila watenda hila wanasaliti!” 17 24:17Hofu, shimo na mtego vinakungojea, ewe mtu ukaaye duniani. 18 24:18Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu atatumbukia shimoni, naye yeyote apandaye kutoka shimoni, atanaswa kwenye mtego. Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika. 19 24:19Dunia imepasuka, dunia imechanika, dunia imetikiswa kabisa. 20 24:20Dunia inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo; imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake na ikianguka kamwe haitainuka tena. 21 24:21Katika siku ile Bwana ataadhibu nguvu zilizoko mbinguni juu, na wafalme walioko duniani chini. 22 24:22Watakusanywa pamoja kama wafungwa waliofungwa gerezani, watafungiwa gerezani na kuadhibiwa baada ya siku nyingi. 23 24:23Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa; kwa maana Bwana Mwenye Nguvu Zote atawala juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu, tena mbele ya wazee wake kwa utukufu. 25Msifuni Bwana 1 25:1Ee Bwana, wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza na kulisifu jina lako, kwa maana katika ukamilifu wa uaminifu umetenda mambo ya ajabu, mambo yaliyokusudiwa tangu zamani. 2 25:2Umeufanya mji kuwa lundo la kifusi, mji wenye ngome kuwa magofu, ngome imara ya wageni kuwa si mji tena, wala hautajengwa tena kamwe. 3 25:3Kwa hiyo mataifa yenye nguvu yatakuheshimu, miji ya mataifa katili itakuheshimu wewe. 4 25:4Umekuwa kimbilio la watu maskini, kimbilio la mhitaji katika taabu yake, hifadhi wakati wa dhoruba na kivuli wakati wa hari. Kwa maana pumzi ya wakatili ni kama dhoruba ipigayo ukuta 5 25:5na kama joto la jangwani. Wewe wanyamazisha makelele ya wageni; kama vile hari ipunguzwavyo na kivuli cha wingu, ndivyo wimbo wa wakatili unyamazishwavyo. 6 25:6Juu ya mlima huu Bwana Mwenye Nguvu Zote ataandaa karamu ya vinono kwa mataifa yote, karamu ya mvinyo wa zamani, nyama nzuri sana na divai zilizo bora sana. 7 25:7Juu ya mlima huu ataharibu sitara ihifadhiyo mataifa yote, kile kifuniko kifunikacho mataifa yote, 8 25:8yeye atameza mauti milele. Bwana Mwenyezi atafuta machozi katika nyuso zote; ataondoa aibu ya watu wake duniani kote. Bwana amesema hili. 9 25:9Katika siku ile watasema, “Hakika huyu ndiye Mungu wetu; tulimtumaini, naye akatuokoa. Huyu ndiye Bwana, tuliyemtumaini; sisi tushangilie na kufurahia katika wokovu wake.” 10 25:10Mkono wa Bwana utatulia juu ya mlima huu, bali Moabu atakanyagwa chini kama majani makavu yakanyagwavyo kwenye shimo la mbolea. 11 25:11Watakunjua mikono yao katikati yake, kama vile mwogeleaji akunjuavyo mikono yake ili aogelee. Mungu atashusha kiburi chao licha ya ujanja wa mikono yao. 12 25:12Atabomoa kuta ndefu za maboma yako na kuziangusha chini, atazishusha chini ardhini, mpaka mavumbini kabisa. 26Wimbo Wa Ushindi

1 26:1Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda:

Tuna mji ulio na nguvu, Mungu huufanya wokovu kuwa kuta zake na maboma yake. 2 26:2Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia, taifa lile lidumishalo imani. 3 26:3Utamlinda katika amani kamilifu yeye ambaye moyo wake ni thabiti kwa sababu anakutumaini wewe. 4 26:4Mtumaini Bwana milele, kwa kuwa Bwana, Bwana, ni Mwamba wa milele. 5 26:5Huwashusha wale wajikwezao, huushusha chini mji wenye kiburi, huushusha hadi ardhini na kuutupa chini mavumbini. 6 26:6Miguu huukanyaga chini, miguu ya hao walioonewa, hatua za hao maskini. 7 26:7Mapito ya wenye haki yamenyooka. Ewe uliye Mwenye Haki, waisawazisha njia ya mtu mnyofu. 8 26:8Naam, Bwana, tukienenda katika sheria zako, twakungojea wewe, jina lako na sifa zako ndizo shauku za mioyo yetu. 9 26:9Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku, wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku. Wakati hukumu zako zinapokuja juu ya dunia, watu wa ulimwengu hujifunza haki. 10 26:10Ingawa neema yaonyeshwa kwa waovu, hawajifunzi haki, hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya wala hawazingatii utukufu wa Bwana. 11 26:11Ee Bwana, mkono wako umeinuliwa juu, lakini hawauoni. Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe, moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze. 12 26:12 Bwana, unaamuru amani kwa ajili yetu, yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu. 13 26:13Ee Bwana, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala, lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu. 14 26:14Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai, roho za waliokufa hazitarudi tena. Uliwaadhibu na kuwaangamiza, umefuta kumbukumbu lao lote. 15 26:15Umeliongeza hilo taifa, Ee Bwana, umeliongeza hilo taifa. Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe, umepanua mipaka yote ya nchi. 16 26:16 Bwana, walikujia katika taabu yao, wewe ulipowarudi, waliweza kuomba kwa kunongʼona tu. 17 26:17Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa mbele zako, Ee Bwana. 18 26:18Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu, lakini tulizaa upepo. Hatukuleta wokovu duniani, hatujazaa watu katika ulimwengu huu. 19 26:19Lakini wafu wenu wataishi, nayo miili yao itafufuka. Ninyi mnaokaa katika mavumbi, amkeni mkapige kelele kwa furaha. Umande wenu ni kama umande wa asubuhi, dunia itawazaa wafu wake. 20 26:20Nendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu na mfunge milango nyuma yenu, jificheni kwa kitambo kidogo mpaka ghadhabu yake ipite. 21 26:21Tazama, Bwana anakuja kutoka makao yake ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao. Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake, wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa. 27Wokovu Kwa Ajili Ya Israeli

1 27:1Katika siku ile,

Bwana ataadhibu kwa upanga wake, upanga wake mkali, mkubwa na wenye nguvu, ataadhibu Lewiathani 27:1 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa. yule nyoka apitaye kwa mwendo laini, Lewiathani yule nyoka mwenye kujipinda; atamuua joka huyo mkubwa sana wa baharini.

2 27:2Katika siku ile:

“Imbeni kuhusu shamba la mizabibu lililozaa: 3 27:3Mimi, Bwana, ninalitunza, nalinyweshea maji mfululizo. Ninalichunga usiku na mchana ili mtu yeyote asije akalidhuru. 4 27:4Mimi sijakasirika. Licha pangekuwepo michongoma na miiba kunikabili! Ningepambana dhidi yake katika vita, ningeliichoma moto yote. 5 27:5Au niwaache waje kwangu kwa ajili ya kupata kimbilio, wao na wafanye amani nami, naam, wafanye amani nami.” 6 27:6Katika siku zijazo, Yakobo atatia mizizi, Israeli atatoa chipukizi na kuchanua maua, naye atajaza ulimwengu wote kwa matunda. 7 27:7Je, Bwana amempiga vile alivyowapiga wale waliompiga? Je, yeye ameuawa vile walivyouawa wale waliomuua yeye? 8 27:8Kwa vita na kwa kumfukuza unapingana naye: kwa mshindo wake mkali anamfukuza, kama siku ile uvumapo upepo wa mashariki. 9 27:9Kwa hili, basi, hatia ya Yakobo itafanyiwa upatanisho, nalo hili litakuwa matunda ya utimilizo wa kuondolewa kwa dhambi yake: Wakati atakapoyafanya mawe yote ya madhabahu kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa vipande vipande, hakuna nguzo za Ashera au madhabahu za kufukizia uvumba zitakazobaki zimesimama. 10 27:10Mji ulio na boma umebaki ukiwa, makao yaliyotelekezwa, yaliyoachwa kama jangwa. Huko ndama hulisha, huko hujilaza, wanakwanyua matawi yake. 11 27:11Wakati vijiti vyake vimekauka, huvunjwa nao wanawake huja na kuwasha navyo moto. Kwa kuwa hili ni taifa lisilo na ufahamu, kwa hiyo yeye aliyewafanya hana huruma juu yao, Muumba wao hawaonyeshi fadhili.

12 27:12Katika siku ile Bwana atapura kutoka matiririko ya Mto Frati hadi Kijito cha Misri, nanyi ee Waisraeli, mtakusanywa mmoja mmoja. 13 27:13Katika siku ile tarumbeta kubwa italia. Wale waliokuwa wakiangamia katika nchi ya Ashuru, nao wale waliokuwa uhamishoni katika nchi ya Misri watakuja na kumwabudu Bwana katika mlima mtakatifu huko Yerusalemu.

28Ole Wa Efraimu 1 28:1Ole kwa lile taji la maua, kiburi cha walevi wa Efraimu, kwa ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba: kwa ule mji, kiburi cha wale walioshushwa na mvinyo! 2 28:2Tazama, Bwana anaye mmoja aliye na uwezo na nguvu. Kama dhoruba ya mvua ya mawe na upepo uharibuo, kama mvua inyeshayo kwa nguvu na mafuriko yashukayo, atakiangusha chini kwa nguvu. 3 28:3Lile taji la maua, kiburi cha walevi cha Efraimu, kitakanyagwa chini ya nyayo. 4 28:4Lile ua linalosinyaa, uzuri wa utukufu wake, uliowekwa kwenye kichwa cha bonde lenye rutuba, litakuwa kama tini iliyoiva kabla ya mavuno: mara mtu aionapo, huichuma na kuila. 5 28:5Katika siku ile, Bwana Mwenye Nguvu Zote atakuwa taji la utukufu, taji zuri la maua kwa mabaki ya watu wake. 6 28:6Atakuwa roho ya haki kwa yeye aketiye katika kiti cha hukumu, chanzo cha nguvu kwa wale wazuiao vita langoni. 7 28:7Hawa pia wanapepesuka kwa sababu ya mvinyo, wanayumbayumba kwa sababu ya kileo: Makuhani na manabii wanapepesuka kwa sababu ya kileo, wanachanganyikiwa kwa sababu ya mvinyo; wanapepesuka wanapoona maono, wanajikwaa wanapotoa maamuzi. 8 28:8Meza zote zimejawa na matapishi wala hakuna sehemu hata ndogo isiyokuwa na uchafu. 9 28:9“Yeye anajaribu kumfundisha nani? Yeye anamwelezea nani ujumbe wake? Je, ni kwa watoto walioachishwa kunyonya? Je, ni wale ambao ndipo tu wametolewa matitini? 10 28:10Kwa maana ni: Amri juu ya amri, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni; hapa kidogo, kule kidogo.” 11 28:11Sawa kabisa, kwa midomo migeni na kwa lugha ngeni, Mungu atasema na watu hawa, 12 28:12wale ambao aliwaambia, “Hapa ni mahali pa kupumzika, waliochoka na wapumzike,” na, “Hapa ni mahali pa mapumziko,” lakini hawakutaka kusikiliza. 13 28:13Hivyo basi, neno la Bwana kwao litakuwa: Amri juu ya amri, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, kanuni juu ya kanuni, hapa kidogo, kule kidogo: ili waende na kuanguka chali, wakijeruhiwa, wakinaswa na kukamatwa. 14 28:14Kwa hiyo sikieni neno la Bwana, enyi watu wenye dharau mnaotawala watu hawa wa Yerusalemu. 15 28:15Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti, tumefanya mapatano na kuzimu. Wakati pigo lifurikalo litakapopita, haliwezi kutugusa sisi, kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio letu na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.”

16 28:16Kwa hiyo hivi ndivyo Bwana Mwenyezi asemavyo:

“Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni la thamani kwa ajili ya msingi thabiti. Yeye atumainiye kamwe hatatiwa hofu. 17 28:17Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia na uadilifu kuwa timazi; mvua ya mawe itafagia kimbilio lenu, huo uongo, nayo maji yatafurikia mahali penu pa kujificha. 18 28:18Agano lenu na kifo litabatilishwa, patano lenu na kuzimu halitasimama. Wakati pigo lifurikalo litakapowakumba, litawaangusha chini. 19 28:19Kila mara lijapo litawachukua, asubuhi baada ya asubuhi, wakati wa mchana na wakati wa usiku, litawakumba tangu mwanzo hadi mwisho.” Kuuelewa ujumbe huu utaleta hofu tupu. 20 28:20Kitanda ni kifupi mno kujinyoosha juu yake, nguo ya kujifunikia ni nyembamba mno mtu hawezi kujifunikia. 21 28:21 Bwana atainuka kama alivyofanya kwenye Mlima Perasimu, ataghadhibika kama alivyofanya katika Bonde la Gibeoni: ili kufanya kazi yake, kazi yake ya ajabu, ili kutimiza kazi yake, kazi yake ngeni. 22 28:22Sasa acheni dharau zenu, la sivyo minyororo yenu itakuwa mizito zaidi. Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, ameniambia habari za maangamizi yaliyoamriwa dhidi ya nchi yote. 23 28:23Sikilizeni msikie sauti yangu, tegeni masikio na msikie niyasemayo. 24 28:24Wakati mkulima alimapo ili apande, je, hulima siku zote? Je, huendelea kubomoa ardhi na kusawazisha udongo? 25 28:25Akiisha kusawazisha shamba, je, hatapanyi mbegu za bizari na kutawanya jira? Je, hapandi ngano katika sehemu yake, shayiri katika eneo lake, na nafaka nyingine katika shamba lake? 26 28:26Mungu wake humwelekeza na kumfundisha njia iliyo sahihi. 27 28:27Iliki haipurwi kwa nyundo, wala gurudumu la gari halivingirishwi juu ya jira; iliki hupurwa kwa fimbo, na jira kwa ufito. 28 28:28Nafaka lazima isagwe ili kutengeneza mkate, kwa hiyo mtu haendelei kuipura daima. Ingawa huendesha magurudumu ya gari lake la kupuria juu yake, farasi wake hawasagi. 29 28:29Haya yote pia hutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote, mwenye mashauri ya ajabu, na anayepita wote kwa hekima. 29Ole Wa Mji Wa Daudi 1 29:1Ole wako, wewe Arieli, Arieli, mji alimokaa Daudi! Ongezeni mwaka kwa mwaka, na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee. 2 29:2Hata hivyo nitauzunguka Arieli kwa jeshi, utalia na kuomboleza, utakuwa kwangu kama mahali pa kuwashia moto madhabahuni. 3 29:3Nitapiga kambi pande zote dhidi yako, nitakuzunguka kwa minara na kupanga mazingirwa yangu dhidi yako. 4 29:4Utakaposhushwa, utanena kutoka ardhini, utamumunya maneno yako kutoka mavumbini. Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu, utanongʼona maneno yako toka mavumbini. 5 29:5Lakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini, kundi la wakatili watakuwa kama makapi yapeperushwayo. Naam, ghafula, mara moja, 6 29:6 Bwana Mwenye Nguvu Zote atakuja na ngurumo, tetemeko la ardhi, na kwa sauti kuu, atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo. 7 29:7Kisha makundi ya mataifa yote yale yapiganayo dhidi ya Arieli, yale yanayomshambulia yeye na ngome zake, na kumzunguka kwa jeshi, watakuwa kama ilivyo ndoto, kama maono wakati wa usiku: 8 29:8kama vile mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula, lakini huamka, bado njaa yake ingalipo, kama vile mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji, lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu. Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni. 9 29:9Duwaeni na kushangaa, jifanyeni vipofu wenyewe na msione, leweni, lakini si kwa mvinyo, pepesukeni lakini si kwa kileo. 10 29:10 Bwana amewaleteeni usingizi mzito: Ameziba macho yenu (ninyi manabii); amefunika vichwa vyenu (ninyi waonaji).

11 29:11Kwa maana kwenu ninyi, maono haya yote si kitu ila maneno yaliyotiwa lakiri katika kitabu. Kama mkimpa mtu yeyote awezaye kusoma kitabu hiki, nanyi mkamwambia, “Tafadhali kisome,” yeye atajibu, “Mimi siwezi, kwa kuwa kimetiwa lakiri.” 12 29:12Au kama mkimpa mtu yeyote kitabu hiki asiyeweza kusoma na kumwambia, “Tafadhali kisome,” atajibu, “Mimi sijui kusoma.”

13 29:13Bwana anasema:

“Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao na kuniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. Ibada yao kwangu inatokana na maagizo waliyofundishwa na wanadamu. 14 29:14Kwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa, kwa ajabu juu ya ajabu. Hekima ya wenye hekima itapotea, nayo akili ya wenye akili itatoweka.” 15 29:15Ole kwa wale wanaokwenda kwenye vilindi virefu kumficha Bwana mipango yao, wafanyao kazi zao gizani na kufikiri, “Ni nani anayetuona? Ni nani atakayejua?” 16 29:16Mnapindua mambo juu chini, kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi! Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga, “Wewe hukunifinyanga mimi?” Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi, “Wewe hujui chochote?” 17 29:17Kwa muda mfupi sana, je, Lebanoni haitageuzwa kuwa shamba lenye rutuba, na shamba lenye rutuba liwe kama msitu? 18 29:18Katika siku ile viziwi watasikia maneno ya kitabu, na katika utusitusi na giza macho ya kipofu yataona. 19 29:19Mara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katika Bwana, wahitaji watafurahi katika yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. 20 29:20Wakatili watatoweka na wenye kudhihaki watatokomea, nao wote wenye jicho la uovu watakatiliwa mbali, 21 29:21wale ambao kwa neno humfanya mtu kuwa mwenye hatia, wamtegeao mtego mtetezi katika mahakama, na kwa ushuhuda wa uongo humnyima haki yeye asiye na hatia.

22 29:22Kwa hiyo hili ndilo Bwana, aliyemkomboa Abrahamu, analosema kwa nyumba ya Yakobo:

“Yakobo hataaibishwa tena, wala nyuso zao hazitabadilika sura tena. 23 29:23Wakati watakapoona watoto wao miongoni mwao, kazi ya mikono yangu, watalitakasa Jina langu takatifu; wataukubali utakatifu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli. 24 29:24Wale wanaopotoka rohoni watapata ufahamu, nao wale wanaolalamika watayakubali mafundisho.” 30Ole Wa Taifa Kaidi 1 30:1 Bwana asema, “Ole kwa watoto wakaidi, kwa wale wanaotimiza mipango ambayo si yangu, wakifanya makubaliano, lakini si kwa Roho wangu, wakilundika dhambi juu ya dhambi, 2 30:2wale washukao kwenda Misri bila kutaka shauri langu, wanaotafuta msaada wa ulinzi wa Farao, watafutao kivuli cha Misri kwa ajili ya kimbilio. 3 30:3Lakini ulinzi wa Farao utakuwa kwa aibu yenu, kivuli cha Misri kitawaletea fedheha. 4 30:4Ingawa wana maafisa katika Soani na wajumbe wamewasili katika Hanesi, 5 30:5kila mmoja ataaibishwa kwa sababu ya taifa lisilowafaa kitu, ambalo haliwaletei msaada wala faida, bali aibu tu na fedheha.”

6 30:6Neno kuhusu wanyama wa Negebu:

Katika nchi ya taabu na shida, ya simba za dume na jike, ya nyoka mwenye sumu kali na nyoka warukao, wajumbe huchukua utajiri wao juu ya migongo ya punda, hazina zao juu ya nundu za ngamia, kwa lile taifa lisilokuwa na faida, 7 30:7kuvipeleka Misri, ambaye msaada wake haufai kabisa. Kwa hiyo nimemwita “Rahabu Asiyefanya Chochote.” 8 30:8Nenda sasa, liandike neno hili juu ya kibao kwa ajili yao, liandike kwenye kitabu, ili liweze kuwa shahidi milele kwa ajili ya siku zijazo. 9 30:9Hawa ni watu waasi, watoto wadanganyifu, watoto ambao hawataki kusikiliza mafundisho ya Bwana. 10 30:10Wanawaambia waonaji, “Msione maono tena!” Nako kwa manabii wanasema, “Msiendelee kutupatia maono ambayo ni ya kweli! Tuambieni mambo ya kupendeza, tabirini mambo ya uongo. 11 30:11Acheni njia hii, ondokeni katika mapito haya, nanyi acheni kutukabili pamoja na yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli!”

12 30:12Kwa hiyo, hili ndilo asemalo yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli:

“Kwa sababu mmekataa ujumbe huu, mkategemea uonevu na kutumainia udanganyifu, 13 30:13dhambi hii itakuwa kwenu kama ukuta mrefu, wenye ufa na wenye kubetuka, ambao unaanguka ghafula, mara moja. 14 30:14Utavunjika vipande vipande kama chombo cha udongo ukipasuka pasipo huruma ambapo katika vipande vyake hakuna kipande kitakachopatikana kwa kuukulia makaa kutoka jikoni au kuchotea maji kisimani.”

15 30:15Hili ndilo Bwana Mwenyezi, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, asemalo:

“Katika kutubu na kupumzika ndio wokovu wenu, katika kutulia na kutumaini ndizo nguvu zenu, lakini hamkutaka. 16 30:16Mlisema, ‘Hapana, tutakimbia kwa farasi.’ Kwa hiyo mtakimbia! Mlisema, ‘Tutakimbia kwa farasi waendao kasi.’ Kwa hiyo wanaowafukuza watakwenda kasi! 17 30:17Watu 1,000 watakimbia kwa ajili ya kitisho cha mtu mmoja, kwa vitishio vya watu watano wote mtakimbia, hadi mtakapoachwa kama mlingoti wa bendera juu ya kilele cha mlima, kama bendera juu ya kilima.” 18 30:18Hata hivyo Bwana anatamani kutupatia neema, anainuka ili kuwaonyesha huruma. Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa haki. Wamebarikiwa wote wanaomngojea yeye!

19 30:19Enyi watu wa Sayuni, mnaoishi Yerusalemu, hamtalia tena. Tazameni jinsi atakavyokuwa na huruma mtakapolia kwa kumwomba msaada! Mara asikiapo, atawajibu. 20 30:20Ingawa Bwana huwapa chakula cha shida na maji ya taabu, walimu wenu hawatafichwa tena, kwa macho yenu wenyewe mtawaona. 21 30:21Mkigeuka kuume au kushoto, masikio yenu yatasikia sauti nyuma yenu ikisema, “Hii ndiyo njia, ifuateni.” 22 30:22Kisha mtanajisi sanamu zenu zilizofunikwa kwa fedha, na vinyago vyenu vilivyofunikwa kwa dhahabu. Mtazitupilia mbali kama vitambaa vya wakati wa hedhi na kuziambia, “Haya, tokeni hapa!”

23 30:23Pia atawapa mvua kwa ajili ya mbegu mnazootesha ardhini, chakula kinachotoka ardhini kitakuwa kizuri sana, tena tele. Katika siku ile, ngʼombe wenu watalisha katika shamba pana la majani. 24 30:24Maksai na punda walimao watakula majani makavu na vyakula vilivyotengenezwa, vinavyotandazwa kwa uma na sepeto. 25 30:25Katika siku ile ya mauaji makuu, wakati minara itakapoanguka, vijito vya maji vitatiririka juu ya kila mlima mrefu na kila kilima kilichoinuka sana. 26 30:26Mwezi utaangaza kama jua, nao mwanga wa jua utangʼaa mara saba zaidi, kama nuru ya siku saba, wakati Bwana atakapoyafunga majeraha ya watu wake na kuwaponya vidonda alivyowatia.

27 30:27Tazama, Jina la Bwana linakuja kutoka mbali, likiwa na hasira kali inayowaka pamoja na wingu zito la moshi, midomo yake imejaa ghadhabu na ulimi wake ni moto ulao. 28 30:28Pumzi yake ni kama mkondo wa maji yaendayo kasi, yakipanda hadi shingoni. Hutikisa mataifa katika chekecheke ya uharibifu, huweka lijamu katika mataya ya mataifa ambayo huwaongoza upotevuni. 29 30:29Nanyi mtaimba kama usiku ule mnaadhimisha sikukuu takatifu. Mioyo yenu itashangilia kama vile watu wanapokwea na filimbi kwenye mlima wa Bwana, kwa Mwamba wa Israeli. 30 30:30 Bwana atawasababisha watu waisikie sauti yake ya utukufu, naye atawafanya wauone mkono wake ukishuka pamoja na hasira yake kali na moto ulao, kukiwa na tufani ya mvua, ngurumo za radi na mvua ya mawe. 31 30:31Sauti ya Bwana itaivunjavunja Ashuru, kwa fimbo yake ya utawala atawapiga. 32 30:32Kila pigo Bwana atakaloliweka juu yao kwa fimbo yake ya kuadhibu, litakuwa kwa wimbo wa matari na vinubi, anapopigana nao katika vita kwa mapigo ya mkono wake. 33 30:33Tofethi imeandaliwa toka zamani, imewekwa tayari kwa ajili ya mfalme. Shimo lake la moto limetengenezwa kwa kina kirefu na kwa upana mkubwa, likiwa na moto na kuni tele; pumzi ya Bwana, kama kijito cha kiberiti, huuwasha moto. 31Ole Wa Wale Wanaotegemea Misri 1 31:1Ole wao wale washukao Misri kwa ajili ya msaada, wale wategemeao farasi, wanaoweka tumaini katika wingi wa magari yao ya vita, na katika nguvu nyingi za wapanda farasi, lakini hawamwangalii yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, wala hawatafuti msaada kwa Bwana. 2 31:2Hata hivyo yeye pia ana hekima na anaweza kuleta maafa, wala hayatangui maneno yake. Yeye atainuka dhidi ya nyumba ya mwovu, dhidi ya wale ambao huwasaidia watenda mabaya. 3 31:3Lakini Wamisri ni wanadamu, wala si Mungu, farasi wao ni nyama, wala si roho. Wakati Bwana atakaponyoosha Mkono wake, yeye anayesaidia atajikwaa, naye anayesaidiwa ataanguka, wote wawili wataangamia pamoja.

4 31:4Hili ndilo Bwana analoniambia:

“Kama vile simba angurumavyo, simba mkubwa juu ya mawindo yake: hata ingawa kundi lote la wachunga mifugo huitwa pamoja dhidi yake, hatiwi hofu na kelele zao wala kusumbuliwa na ghasia zao; ndivyo Bwana Mwenye Nguvu Zote atakavyoshuka kufanya vita juu ya Mlima Sayuni na juu ya vilele vyake. 5 31:5Kama ndege warukao, Bwana Mwenye Nguvu Zote ataukinga Yerusalemu; ataukinga na kuuokoa, atapita juu yake na kuufanya salama.”

6 31:6Mrudieni yeye ambaye nyumba ya Israeli imemwasi sana. 7 31:7Kwa kuwa katika siku ile kila mmoja wenu atazikataa sanamu za fedha na za dhahabu zilizotengenezwa kwa mikono yenu yenye dhambi.

8 31:8“Ashuru itaanguka kwa upanga ambao si wa mwanadamu; upanga usio wa kibinadamu utawaangamiza. Watakimbia mbele ya upanga na vijana wao wa kiume watafanyizwa kazi kwa lazima. 9 31:9Ngome zao zitaanguka kwa sababu ya hofu; kwa kuona bendera ya vita, majemadari wao watashikwa na hofu ya ghafula,” asema Bwana, ambaye moto wake uko Sayuni, nayo tanuru yake iko Yerusalemu. 32Ufalme Wa Haki 1 32:1Tazama, mfalme atatawala kwa uadilifu na watawala watatawala kwa haki. 2 32:2Kila mtu atakuwa kama kivuli cha kujificha kutokana na upepo na kimbilio kutokana na dhoruba, kama vijito vya maji jangwani na kivuli cha mwamba mkubwa katika ardhi yenye kiu. 3 32:3Ndipo macho ya wale wanaoona hayatafumbwa tena, nayo masikio ya wale wanaosikia yatasikiliza. 4 32:4Moyo wa mtu mwenye hamaki utafahamu na kuelewa, nao ulimi wenye kigugumizi utanena kwa ufasaha. 5 32:5Mpumbavu hataitwa tena muungwana, wala mtu mbaya kabisa kupewa heshima ya juu. 6 32:6Kwa kuwa mpumbavu hunena upumbavu, moyo wake hushughulika na uovu: Hutenda mambo yasiyo ya kumcha Mungu, na hueneza habari za makosa kuhusu Bwana; yeye huwaacha wenye njaa bila kitu, na wenye kiu huwanyima maji. 7 32:7Taratibu za mtu mbaya kabisa ni ovu, hufanya mipango miovu ili kumwangamiza maskini kwa uongo, hata wakati ambapo hoja za mhitaji ni za haki. 8 32:8Lakini mtu muungwana hufanya mipango ya kiungwana, na kwa matendo ya kiungwana yeye hufanikiwa. Wanawake Wa Yerusalemu 9 32:9Enyi wanawake wenye kuridhika sana, amkeni na mnisikilize. Enyi binti mnaojisikia kuwa salama, sikieni lile ninalotaka kuwaambia! 10 32:10Muda zaidi kidogo ya mwaka mmoja, ninyi mnaojisikia salama mtatetemeka, mavuno ya zabibu yatakoma na mavuno ya matunda hayatakuwepo. 11 32:11Tetemekeni, enyi wanawake wenye kuridhika, tetemekeni kwa hofu, enyi binti mnaojisikia salama! Vueni nguo zenu, vaeni nguo ya gunia viunoni mwenu. 12 32:12Pigeni matiti yenu kwa ajili ya mashamba mazuri, kwa ajili ya mizabibu iliyozaa vizuri 13 32:13na kwa ajili ya nchi ya watu wangu, nchi ambayo miiba na michongoma imemea: naam, ombolezeni kwa ajili ya nyumba zote za furaha na kwa ajili ya mji huu wenye kufanya sherehe. 14 32:14Ngome itaachwa, mji wenye kelele nyingi utahamwa, ngome ndani ya mji na mnara wa ulinzi vitakuwa ukiwa milele, mahali pazuri pa punda na malisho ya makundi ya kondoo, 15 32:15mpaka Roho amwagwe juu yetu kutoka juu, nalo jangwa kuwa shamba lenye rutuba, na shamba lenye rutuba kuwa kama msitu. 16 32:16Haki itakaa katika jangwa, na uadilifu utakaa katika shamba lenye rutuba. 17 32:17Matunda ya haki yatakuwa amani, matokeo ya haki yatakuwa utulivu na matumaini milele. 18 32:18Watu wangu wataishi katika makao ya mahali pa amani, katika nyumba zilizo salama, katika mahali pa kupumzika pasipo na usumbufu. 19 32:19Hata kama mvua ya mawe iangushe msitu na mji ubomolewe kabisa, 20 32:20tazama jinsi utakavyobarikiwa, ukipanda mbegu yako katika kila kijito, na kuwaacha ngʼombe wako na punda wajilishe kwa uhuru. 33Taabu Na Msaada 1 33:1Ole wako wewe, ee mharabu, wewe ambaye hukuharibiwa! Ole wako, ee msaliti, wewe ambaye hukusalitiwa! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa; utakapokwisha kusaliti, utasalitiwa. 2 33:2Ee Bwana, uturehemu, tunakutamani. Uwe nguvu yetu kila asubuhi na wokovu wetu wakati wa taabu. 3 33:3Kwa ngurumo ya sauti yako, mataifa yanakimbia; unapoinuka, mataifa hutawanyika. 4 33:4Mateka yenu, enyi mataifa, yamevunwa kama vile wafanyavyo madumadu, kama kundi la nzige watu huvamia juu yake. 5 33:5 Bwana ametukuka, kwa kuwa anakaa mahali palipoinuka, ataijaza Sayuni kwa haki na uadilifu. 6 33:6Atakuwa msingi ulio imara kwa wakati wenu, ghala za wokovu tele, hekima na maarifa; kumcha Bwana ni ufunguo wa hazina hii. 7 33:7Angalia, watu wake mashujaa wanapiga kelele kwa nguvu barabarani, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu. 8 33:8Njia kuu zimeachwa, hakuna wasafiri barabarani. Mkataba umevunjika, mashahidi wake wamedharauliwa, 33:8 Au: miji yake imedharauliwa. hakuna yeyote anayeheshimiwa. 9 33:9Ardhi inaomboleza 33:9 Au: Ardhi inakauka. na kuchakaa, Lebanoni imeaibika na kunyauka, Sharoni ni kama Araba, nayo Bashani na Karmeli wanapukutisha majani yao. 10 33:10“Sasa nitainuka,” asema Bwana. “Sasa nitatukuzwa; sasa nitainuliwa juu. 11 33:11Mlichukua mimba ya makapi, mkazaa mabua, pumzi yenu ni moto uwateketezao. 12 33:12Mataifa yatachomwa kama ichomwavyo chokaa, kama vichaka vya miiba vilivyokatwa ndivyo watakavyochomwa.” 13 33:13Ninyi mlio mbali sana, sikieni lile nililofanya; ninyi mlio karibu, tambueni uweza wangu! 14 33:14Wenye dhambi katika Sayuni wametiwa hofu, kutetemeka kumewakumba wasiomcha Mungu: “Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto ulao? Ni nani miongoni mwetu awezaye kuishi na moto unaowaka milele?” 15 33:15Yeye aendaye kwa uadilifu na kusema lililo haki, yeye anayekataa faida ipatikanayo kwa dhuluma na kuizuia mikono yake isipokee rushwa, yeye azuiaye masikio yake dhidi ya mashauri ya mauaji, na yeye afumbaye macho yake yasitazame sana uovu: 16 33:16huyu ndiye mtu atakayeishi mahali pa juu, ambaye kimbilio lake litakuwa ngome ya mlimani. Atapewa mkate wake, na maji yake hayatakoma. 17 33:17Macho yenu yatamwona mfalme katika uzuri wake na kuiona nchi inayoenea mbali. 18 33:18Katika mawazo yenu mtaifikiria hofu iliyopita: “Yuko wapi yule afisa mkuu? Yuko wapi yule aliyechukua ushuru? Yuko wapi afisa msimamizi wa minara?” 19 33:19Hutawaona tena wale watu wenye kiburi, wale watu wenye usemi wa mafumbo, wenye lugha ngeni, isiyoeleweka. 20 33:20Mtazame Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yenu yatauona Yerusalemu, mahali pa amani pa kuishi, hema ambalo halitaondolewa, nguzo zake hazitangʼolewa kamwe, wala hakuna kamba yake yoyote itakayokatika. 21 33:21Huko Bwana atakuwa Mwenye Nguvu wetu. Patakuwa kama mahali pa mito mipana na vijito. Hakuna jahazi lenye makasia litakalopita huko, wala hakuna meli yenye nguvu itakayopita huko. 22 33:22Kwa kuwa Bwana ni mwamuzi wetu, Bwana ndiye mtoa sheria wetu, Bwana ni mfalme wetu, yeye ndiye atakayetuokoa. 23 33:23Kamba zenu za merikebu zimelegea: Mlingoti haukusimama imara, nalo tanga halikukunjuliwa. Wingi wa mateka yatagawanywa, hata yeye aliye mlemavu atachukua nyara. 24 33:24Hakuna yeyote aishiye Sayuni atakayesema, “Mimi ni mgonjwa”; nazo dhambi za wale waishio humo zitasamehewa. 34Hukumu Dhidi Ya Mataifa 1 34:1Njooni karibu, enyi mataifa, nanyi msikilize; sikilizeni kwa makini, enyi kabila za watu! Dunia na isikie, navyo vyote vilivyo ndani yake, ulimwengu na vyote vitokavyo ndani yake! 2 34:2 Bwana ameyakasirikia mataifa yote; ghadhabu yake ni juu ya majeshi yao yote. Atawaangamiza kabisa, atawatia mikononi mwa wachinjaji. 3 34:3Waliouawa watatupwa nje, maiti zao zitatoa uvundo, milima itatota kwa damu zao. 4 34:4Nyota zote za mbinguni zitayeyuka na anga litasokotwa kama kitabu, jeshi lote la angani litaanguka kama majani yaliyonyauka kutoka kwenye mzabibu, kama tini iliyonyauka kutoka kwenye mtini. 5 34:5Upanga wangu umekunywa na kushiba huko mbinguni, tazama, unashuka katika hukumu juu ya Edomu, wale watu ambao nimeshawahukumu, kuwaangamiza kabisa. 6 34:6Upanga wa Bwana umeoga katika damu, umefunikwa na mafuta ya nyama: damu ya kondoo na mbuzi, mafuta kutoka figo za kondoo dume. Kwa maana Bwana ana dhabihu huko Bosra, na machinjo makuu huko Edomu. 7 34:7Nyati wataanguka pamoja nao, ndama waume na mafahali wakubwa. Nchi yao italowana kwa damu, nayo mavumbi yataloa mafuta ya nyama. 8 34:8Kwa sababu Bwana anayo siku ya kulipiza kisasi, mwaka wa malipo, siku ya kushindania shauri la Sayuni. 9 34:9Vijito vya Edomu vitageuka kuwa lami, mavumbi yake yatakuwa kiberiti kiunguzacho, nchi yake itakuwa lami iwakayo! 10 34:10Haitazimishwa usiku wala mchana, moshi wake utapaa juu milele. Kutoka kizazi hadi kizazi itakuwa ukiwa, hakuna mtu yeyote atakayepita huko tena. 11 34:11Bundi wa jangwani na bundi mwenye sauti nyembamba wataimiliki, bundi wakubwa na kunguru wataweka viota humo. Mungu atanyoosha juu ya Edomu kamba ya kupimia ya machafuko matupu, na timazi ya ukiwa. 12 34:12Watu wake wa kuheshimiwa hawatakuwa na chochote kitakachoitwa ufalme huko, nao wakuu wao wote watatoweka. 13 34:13Miiba itaenea katika ngome za ndani, viwawi na michongoma itaota kwenye ngome zake. Itakuwa maskani ya mbweha, makao ya bundi. 14 34:14Viumbe vya jangwani vitakutana na fisi, nao mbuzi-mwitu watalia wakiitana; huko viumbe vya usiku vitastarehe pia na kujitafutia mahali pa kupumzika. 15 34:15Bundi wataweka viota huko na kutaga mayai, atayaangua na kutunza makinda yake chini ya uvuli wa mabawa yake; pia huko vipanga watakusanyika, kila mmoja na mwenzi wake.

16 34:16Angalieni katika gombo la Bwana na msome:

Hakuna hata mmoja katika hawa atakayekosekana, hakuna hata mmoja atakayemkosa mwenzi wake. Kwa kuwa ni kinywa chake Mungu kimeagiza, na Roho wake atawakusanya pamoja. 17 34:17Huwagawia sehemu zao, mkono wake huwagawanyia kwa kipimo. Wataimiliki hata milele na kuishi humo kutoka kizazi hadi kizazi. 35Furaha Ya Waliokombolewa 1 35:1Jangwa na nchi kame vitafurahi; nyika itashangilia na kuchanua maua. Kama waridi, 2 35:2litachanua maua, litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha. Litapewa utukufu wa Lebanoni, fahari ya Karmeli na Sharoni; wataona utukufu wa Bwana, fahari ya Mungu wetu. 3 35:3Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea, 4 35:4waambieni wale wenye mioyo ya hofu, “Kuweni hodari, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja, pamoja na malipo ya Mungu, atakuja na kuwaokoa ninyi.” 5 35:5Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa. 6 35:6Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu, nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe. Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika, na vijito katika jangwa. 7 35:7Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji, ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi. Maskani ya mbweha walikolala hapo awali patamea majani, matete na mafunjo. 8 35:8Nako kutakuwa na njia kuu, nayo itaitwa Njia ya Utakatifu. Wasio safi hawatapita juu yake; itakuwa ya wale watembeao katika Njia ile; yeye asafiriye juu yake, ajapokuwa mjinga, hatapotea. 9 35:9Huko hakutakuwepo na simba, wala mnyama mkali hatapita njia hiyo, wala hawatapatikana humo. Ila waliokombolewa tu ndio watakaopita huko, 10 35:10waliokombolewa na Bwana watarudi. Wataingia Sayuni wakiimba; furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao. Watapata furaha na shangwe; huzuni na majonzi vitakimbia. 36Senakeribu Atishia Yerusalemu (2 Wafalme 18:13-27; 2 Nyakati 32:1-19)

1 36:1Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka. 2 36:2Kisha mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wa jeshi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Jemadari wa jeshi akasimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi. 3 36:3Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakamwendea.

4 36:4Jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia,

“ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako? 5 36:5Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi? 6 36:6Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea. 7 36:7Nawe kama ukiniambia, “Tunamtumainia Bwana Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia miungu na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya”? 8 36:8“ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao! 9 36:9Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi? 10 36:10Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza nchi hii bila Bwana? Bwana mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”

11 36:11Ndipo Eliakimu, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walioko juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”

12 36:12Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mikojo yao wenyewe?”

13 36:13Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! 14 36:14Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa! 15 36:15Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini Bwana kwa kuwaambia, ‘Hakika Bwana atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’

16 36:16“Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe, 17 36:17mpaka nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na ya mashamba ya mizabibu.

18 36:18“Msikubali Hezekia awapotoshe asemapo, ‘Bwana atatuokoa.’ Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru? 19 36:19Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu? 20 36:20Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Bwana aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”

21 36:21Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.”

22 36:22Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia yale jemadari wa jeshi aliyoyasema.

37Kuokolewa Kwa Yerusalemu Kunatabiriwa (2 Wafalme 19:1-7)

1 37:1Mfalme Hezekia aliposikia haya, akararua nguo zake na kuvaa nguo ya gunia, naye akaenda katika Hekalu la Bwana. 2 37:2Akawatuma Eliakimu msimamizi wa nyumba ya mfalme, Shebna mwandishi, na viongozi wa makuhani, wote wakiwa wamevaa nguo za magunia, waende kwa nabii Isaya mwana wa Amozi. 3 37:3Wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Hezekia: Siku hii ni siku ya dhiki, ya kukaripiwa na ya aibu, kama wakati watoto wanapofikia karibu kuzaliwa na kumbe hakuna nguvu ya kuwazaa. 4 37:4Yamkini Bwana, Mungu wako atayasikia maneno ya jemadari wa jeshi, ambaye bwana wake, mfalme wa Ashuru, amemtuma kumdhihaki Mungu aliye hai, tena kwamba atamkemea kwa maneno ambayo Bwana, Mungu wako ameyasikia. Kwa hiyo omba kwa ajili ya mabaki ambao bado wako.”

5 37:5Maafisa wa Mfalme Hezekia walipofika kwa Isaya, 6 37:6Isaya akawaambia, “Mwambieni bwana wenu, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Usiogope kwa hayo uliyoyasikia, yale maneno ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana nayo. 7 37:7Sikiliza! Nitatia roho fulani ndani yake ili kwamba atakaposikia taarifa fulani, atarudi nchi yake mwenyewe, nami huko nitafanya auawe kwa upanga.’ ”

8 37:8Jemadari wa jeshi aliposikia kwamba mfalme wa Ashuru ameondoka Lakishi, alirudi, akamkuta mfalme akipigana na Libna.

9 37:9Basi Senakeribu akapata taarifa kwamba Tirhaka, Mkushi mfalme wa Misri, alikuwa anaenda kupigana naye. Aliposikia jambo hili akatuma wajumbe kwa Hezekia na neno hili: 10 37:10“Mwambieni Hezekia mfalme wa Yuda: Usikubali huyo Mungu unayemtumainia akudanganye wakati anaposema, ‘Yerusalemu haitatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’ 11 37:11Hakika umesikia yale ambayo wafalme wa Ashuru wametenda kwa nchi zote, wakiwaangamiza kabisa. Je, wewe utaokolewa? 12 37:12Je, miungu ya mataifa ambayo yaliangamizwa na baba zangu iliweza kuwaokoa? Yaani miungu ya Gozani, Harani, Resefu, na ya watu wa Edeni waliokuwa Telasari? 13 37:13Yuko wapi mfalme wa Hamathi, mfalme wa Arpadi, mfalme wa mji wa Sefarvaimu, au wa Hena au wa Iva?”

Maombi Ya Hezekia

14 37:14Hezekia akapokea barua kutoka kwa wale wajumbe naye akaisoma. Kisha akapanda katika Hekalu la Bwana, akaikunjua mbele za Bwana. 15 37:15Naye Hezekia akamwomba Bwana akisema: 16 37:16“Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, uketiye juu ya kiti cha enzi kati ya makerubi, wewe peke yako ndiwe Mungu juu ya falme zote za dunia. Wewe umeumba mbingu na nchi. 17 37:17Tega sikio, Ee Bwana, usikie; fungua macho yako, Ee Bwana, uone; sikiliza maneno yote ambayo Senakeribu ametuma kumtukana Mungu aliye hai.

18 37:18“Ni kweli, Ee Bwana, kwamba wafalme wa Ashuru wameyaangamiza mataifa haya yote pamoja na nchi zao. 19 37:19Wameitupa miungu yao kwenye moto na kuiangamiza, kwa kuwa haikuwa miungu, bali miti na mawe tu, iliyotengenezwa kwa mikono ya wanadamu. 20 37:20Sasa basi, Ee Bwana Mungu wetu, tuokoe kutoka mkononi mwake, ili kwamba falme zote duniani zipate kujua kwamba wewe peke yako, Ee Bwana, ndiwe Mungu.”

Kuanguka Kwa Senakeribu (2 Wafalme 19:20-37)

21 37:21Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Kwa sababu umeniomba kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru, 22 37:22hili ndilo neno ambalo Bwana amelisema dhidi yake:

“Bikira binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki. Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia. 23 37:23Ni nani uliyemtukana na kumkufuru? Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake, na kumwinulia macho yako kwa kiburi? Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli! 24 37:24Kupitia kwa wajumbe wako umelundika matukano juu ya Bwana. Nawe umesema, ‘Kwa magari yangu mengi ya vita, nimepanda juu ya vilele vya milima, vilele vya juu sana katika Lebanoni. Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu, misunobari yake iliyo bora sana. Nimefikia sehemu zake zilizoinuka juu sana, misitu yake iliyo mizuri sana. 25 37:25Nimechimba visima katika nchi za kigeni na kunywa maji yake. Kwa nyayo za miguu yangu nimekausha vijito vyote vya Misri.’ 26 37:26“Je, hujasikia? Zamani sana niliamuru hili. Siku za kale nilipanga hili; sasa nimelifanya litokee, kwamba umegeuza miji yenye ngome kuwa malundo ya mawe. 27 37:27Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu, wanavunjika mioyo na kuaibishwa. Wao ni kama mimea katika shamba, kama machipukizi mororo ya kijani, kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba, ambayo hukauka kabla ya kukua. 28 37:28“Lakini ninajua mahali ukaapo, kutoka kwako na kuingia kwako, na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu. 29 37:29Kwa sababu unaghadhibika na ufidhuli dhidi yangu, na kwa sababu ufidhuli wako umefika masikioni mwangu, nitaweka ndoana yangu puani mwako na hatamu yangu kinywani mwako, nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.

30 37:30“Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia:

“Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe, na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake. Lakini katika mwaka wa tatu panda na uvune, panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake. 31 37:31Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu. 32 37:32Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki, na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika. Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote, ndio utatimiza jambo hili.

33 37:33“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu mfalme wa Ashuru:

“Hataingia katika mji huu wala hatapiga mshale hapa. Hatakuja mbele yake na ngao wala kupanga majeshi kuuzingira. 34 37:34Kwa njia ile aliyoijia ndiyo atakayorudi; hataingia katika mji huu,” asema Bwana. 35 37:35“Nitaulinda mji huu na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu!”

36 37:36Ndipo malaika wa Bwana akaenda, akawaua wanajeshi 185,000 katika kambi ya Waashuru. Wenzao walipoamka asubuhi yake, walikuta maiti kila mahali! 37 37:37Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akavunja kambi na kuondoka. Akarudi Ninawi na kukaa huko.

38 37:38Siku moja, alipokuwa akiabudu katika hekalu la mungu wake Nisroki, wanawe Adrameleki na Shareza wakamuua kwa upanga, nao wakakimbilia nchi ya Ararati. Naye Esar-Hadoni mwanawe akawa mfalme badala yake.

38Kuugua Kwa Mfalme Hezekia (2 Wafalme 20:1-11; 2 Nyakati 32:24-26)

1 38:1Katika siku hizo Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”

2 38:2Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana: 3 38:3“Ee Bwana, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.

4 38:4Ndipo neno la Bwana likamjia Isaya, kusema: 5 38:5“Nenda ukamwambie Hezekia, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako. Nitakuongezea miaka kumi na mitano katika maisha yako. 6 38:6Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu.

7 38:7“ ‘Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako ya kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi: 8 38:8Nitafanya kivuli cha jua kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi kirudi nyuma madaraja kumi.’ ” Hivyo jua likarudi nyuma madaraja kumi ambayo lilikuwa limeshuka.

9 38:9Maandiko ya Hezekia mfalme wa Yuda baada ya kuugua kwake na kupona:

10 38:10Nilisema, “Katika ustawi wa maisha yangu, je, ni lazima nipite katika malango ya mauti, 38:10 Mauti hapa maana yake ni Kuzimu. na kupokonywa miaka yangu iliyobaki?” 11 38:11Nilisema, “Sitamwona tena Bwana, Bwana katika nchi ya walio hai, wala sitamtazama tena mwanadamu, wala kuwa na wale ambao sasa wanakaa katika ulimwengu huu. 12 38:12Kama hema la mchunga mifugo, nyumba yangu imebomolewa na kutwaliwa kutoka kwangu. Kama mfumaji nimevingirisha maisha yangu, naye amenikatilia mbali kutoka kitanda cha mfumi. Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu. 13 38:13Nilingoja kwa uvumilivu hadi mapambazuko, lakini alivunja mifupa yangu yote kama simba. Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu. 14 38:14Nililia kama mbayuwayu au korongo, niliomboleza kama hua aombolezaye. Macho yangu yalififia nilipotazama mbinguni. Ee Bwana, ninataabika, njoo unisaidie!” 15 38:15Lakini niseme nini? Amesema nami, naye yeye mwenyewe amelitenda hili. Nitatembea kwa unyenyekevu katika miaka yangu yote kwa sababu ya haya maumivu makali ya nafsi yangu. 16 38:16Bwana, kwa mambo kama haya watu huishi, nayo roho yangu hupata uzima katika hayo pia. Uliniponya na kuniacha niishi. 17 38:17Hakika ilikuwa ya faida yangu ndiyo maana nikapata maumivu makali. Katika upendo wako ukaniokoa kutoka shimo la uharibifu; umeziweka dhambi zangu zote nyuma yako. 18 38:18Kwa maana kaburi 38:18 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol. haliwezi kukusifu, mauti haiwezi kuimba sifa zako; wale washukao chini shimoni hawawezi kuutarajia uaminifu wako. 19 38:19Walio hai, walio hai: hao wanakusifu, kama ninavyofanya leo. Baba huwaambia watoto wao habari za uaminifu wako. 20 38:20 Bwana ataniokoa, nasi tutaimba kwa vyombo vya nyuzi siku zote za maisha yetu katika Hekalu la Bwana.

21 38:21Isaya alikuwa amesema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini, mweke juu ya jipu, naye atapona.”

22 38:22Hezekia alikuwa ameuliza, “Kutakuwa na ishara gani kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Bwana?”

39Wajumbe Kutoka Babeli (2 Wafalme 20:12-19)

1 39:1Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua na kupona kwake. 2 39:2Hezekia akawapokea wale wajumbe kwa furaha na kuwaonyesha vitu vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha lote, na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu chochote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.

3 39:3Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”

Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kwangu kutoka Babeli.”

4 39:4Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”

Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu chochote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”

5 39:5Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote: 6 39:6Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana. 7 39:7Nao baadhi ya wazao wako, nyama yako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”

8 39:8Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Patakuwepo amani na usalama wakati wa uhai wangu.”

40Faraja Kwa Watu Wa Mungu 1 40:1Wafarijini, wafarijini watu wangu, asema Mungu wenu. 2 40:2Sema na Yerusalemu kwa upole, umtangazie kwamba kazi yake ngumu imekamilika, kwamba dhambi yake imefanyiwa fidia, kwamba amepokea kutoka mkononi mwa Bwana maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote. 3 40:3Sauti ya mtu aliaye: “Itengenezeni jangwani njia ya Bwana, nyoosheni njia kuu nyikani kwa ajili ya Mungu wetu. 4 40:4Kila bonde litainuliwa, kila mlima na kilima kitashushwa; penye mabonde patanyooshwa, napo palipoparuza patasawazishwa. 5 40:5Utukufu wa Bwana utafunuliwa, nao wanadamu wote watauona pamoja. Kwa maana kinywa cha Bwana kimenena.” 6 40:6Sauti husema, “Piga kelele.” Nami nikasema, “Nipige kelele gani?” “Wanadamu wote ni kama majani, nao utukufu wao wote ni kama maua ya kondeni. 7 40:7Majani hunyauka na maua huanguka, kwa sababu pumzi ya Bwana huyapuliza. Hakika wanadamu ni majani. 8 40:8Majani hunyauka na maua huanguka, lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.” 9 40:9Wewe uletaye habari njema Sayuni, panda juu ya mlima mrefu. Wewe uletaye habari njema Yerusalemu, inua sauti yako kwa kupiga kelele, inua sauti, usiogope; iambie miji ya Yuda, “Yuko hapa Mungu wenu!” 10 40:10Tazameni, Bwana Mwenyezi anakuja na nguvu, nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake. Tazameni, ujira wake u pamoja naye, nayo malipo yake yanafuatana naye. 11 40:11Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo: Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake na kuwachukua karibu na moyo wake, huwaongoza taratibu wale wanyonyeshao. 12 40:12Ni nani aliyepima maji ya bahari kwenye konzi ya mkono wake, au kuzipima mbingu kwa shibiri 40:12 Shibiri ni sawa na sentimita 20 au inchi 8. yake? Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu, au kupima milima kwenye kipimio na vilima kwenye mizani? 13 40:13Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana, au kumfundisha akiwa kama mshauri wake? 14 40:14Ni nani ambaye Bwana ametaka shauri kwake ili kumwelimisha, naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa? Ni nani aliyemfundisha maarifa au kumwonyesha mapito ya ufahamu? 15 40:15Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo, ni kama vumbi jembamba juu ya mizani, huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini. 16 40:16Lebanoni hautoshi kwa moto wa madhabahuni, wala wanyama wake hawatoshi kwa sadaka za kuteketezwa. 17 40:17Mbele yake mataifa yote ni kama si kitu, yanaonekana yasio na thamani na zaidi ya bure kabisa. 18 40:18Basi, utamlinganisha Mungu na nani? Utamlinganisha na kitu gani? 19 40:19Kwa habari ya sanamu, fundi huisubu, naye mfua dhahabu huifunika kwa dhahabu na kuitengenezea mikufu ya fedha. 20 40:20Mtu aliye maskini sana asiyeweza kuleta sadaka kama hii huuchagua mti usiooza. Humtafuta fundi stadi wa kusimamisha sanamu ambayo haitatikisika. 21 40:21Je, hujui? Je, hujasikia? Je, hujaambiwa tangu mwanzo? Je, hujafahamu tangu kuumbwa kwa dunia? 22 40:22Anakaa kwenye kiti cha enzi juu ya duara ya dunia, nao watu wakaao ndani yake ni kama panzi. Huzitandaza mbingu kama chandarua, na kuzitandaza kama hema la kuishi. 23 40:23Huwafanya wakuu kuwa si kitu, na kuwashusha watawala wa dunia hii kuwa kitu bure. 24 40:24Mara baada ya kupandwa, mara baada ya kutiwa ardhini, mara baada ya kutoa mizizi yao ardhini, ndipo huwapulizia nao wakanyauka, nao upepo wa kisulisuli huwapeperusha kama makapi. 25 40:25“Utanilinganisha mimi na nani? Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu. 26 40:26Inueni macho yenu mtazame mbinguni: Ni nani aliyeumba hivi vyote? Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine na kuziita kila moja kwa jina lake. Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu, hakuna hata mojawapo inayokosekana. 27 40:27Kwa nini unasema, ee Yakobo, nanyi ee Israeli, kulalamika, “Njia yangu imefichwa Bwana asiione, Mungu wangu hajali shauri langu?” 28 40:28Je wewe, hufahamu? Je wewe, hujasikia? Bwana ni Mungu wa milele, Muumba wa miisho ya dunia. Hatachoka wala kulegea, wala hakuna hata mmoja awezaye kuupima ufahamu wake. 29 40:29Huwapa nguvu waliolegea na huongeza nguvu za wadhaifu. 30 40:30Hata vijana huchoka na kulegea, nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka, 31 40:31bali wale wamtumainio Bwana atafanya upya nguvu zao. Watapaa juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio wala hawatachoka, watatembea kwa miguu wala hawatazimia. 41Msaidizi Wa Israeli 1 41:1“Nyamazeni kimya mbele zangu, enyi visiwa! Mataifa na wafanye upya nguvu zao! Wao na wajitokeze, kisha waseme, tukutane pamoja mahali pa hukumu. 2 41:2“Ni nani aliyemchochea mmoja kutoka mashariki, akimwita katika haki kwa utumishi wake? Huyatia mataifa mikononi mwake, na kuwatiisha wafalme mbele zake. Huwafanya kuwa mavumbi kwa upanga wake, huwafanya makapi yapeperushwayo na upepo kwa upinde wake. 3 41:3Huwafuatia na kuendelea salama, katika njia ambayo miguu yake haijawahi kupita. 4 41:4Ni nani aliyefanya jambo hili na kulitimiliza, akiita vizazi tangu mwanzo? Mimi, Bwana, ni wa kwanza nami nitakuwa pamoja na wa mwisho: mimi Bwana ndiye.” 5 41:5Visiwa vimeliona na kuogopa, miisho ya dunia inatetemeka. Wanakaribia na kuja mbele, 6 41:6kila mmoja humsaidia mwingine na kusema kwa ndugu yake, “Uwe hodari!” 7 41:7Fundi humtia moyo sonara, yeye alainishaye kwa nyundo humhimiza yeye agongeaye kwenye fuawe, Humwambia yeye aunganishaye, “Ni kazi njema.” Naye huikaza sanamu kwa misumari ili isitikisike. 8 41:8“Lakini wewe, ee Israeli, mtumishi wangu, Yakobo, niliyemchagua, ninyi wazao wa Abrahamu rafiki yangu, 9 41:9nilikuchukua toka miisho ya dunia, nilikuita kutoka pembe zake za mbali. Nilisema, ‘Wewe ni mtumishi wangu’; nimekuchagua, wala sikukukataa. 10 41:10Hivyo usiogope, kwa maana niko pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu na kukusaidia; nitakutegemeza kwa mkono wa kuume wa haki yangu. 11 41:11“Wote walioona hasira dhidi yako hakika wataaibika na kutahayarika, wale wakupingao watakuwa kama vile si kitu, na kuangamia. 12 41:12Ingawa utawatafuta adui zako, hutawaona. Wale wanaopigana vita dhidi yako watakuwa kama vile si kitu kabisa. 13 41:13Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, nikushikaye mkono wako wa kuume na kukuambia, Usiwe na hofu, nitakusaidia. 14 41:14Usiogope, ee Yakobo uliye mdudu, ee Israeli uliye mdogo, kwa kuwa Mimi mwenyewe nitakusaidia,” asema Bwana, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. 15 41:15“Tazama, nitakufanya chombo cha kupuria, kipya na chenye makali, chenye meno mengi. Utaipura milima na kuiponda na kuvifanya vilima kuwa kama makapi. 16 41:16Utaipepeta, nao upepo utaichukua, dhoruba itaipeperushia mbali. Bali wewe utajifurahisha katika Bwana na katika utukufu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. 17 41:17“Maskini na wahitaji wanatafuta maji, lakini hayapo, ndimi zao zimekauka kwa kiu. Lakini Mimi Bwana nitawajibu, Mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. 18 41:18Nitaifanya mito itiririke juu ya vilima vilivyo kame, nazo chemchemi ndani ya mabonde. Nitaligeuza jangwa liwe mabwawa ya maji, nayo ardhi iliyokauka kuwa chemchemi za maji. 19 41:19Katika jangwa nitaotesha mwerezi, mshita, mhadasi na mzeituni. Nitaweka misunobari, mivinje na misanduku pamoja huko nyikani, 20 41:20ili kwamba watu wapate kuona na kujua, wapate kufikiri na kuelewa, kwamba mkono wa Bwana umetenda hili, kwamba yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ndiye alilifanya.” 21 41:21 Bwana asema, “Leta shauri lako. Toa hoja yako,” asema Mfalme wa Yakobo. 22 41:22“Leteni sanamu zenu zituambie ni nini kitakachotokea. Tuambieni mambo ya zamani yalikuwa nini, ili tupate kuyatafakari na kujua matokeo yake ya mwisho. Au tutangazieni mambo yatakayokuja, 23 41:23tuambieni ni nini kitakachotokea baadaye, ili tupate kujua kuwa ninyi ni miungu. Fanyeni jambo lolote zuri au baya, ili tupate kutishika na kujazwa na hofu. 24 41:24Lakini ninyi ni zaidi ya bure kabisa, na kazi zenu hazifai kitu kabisa; yeye awachaguaye ni chukizo sana. 25 41:25“Nimemchochea mtu mmoja kutoka kaskazini, naye yuaja, mmoja toka mawio ya jua aliitaye Jina langu. Huwakanyaga watawala kana kwamba ni matope, kama mfinyanzi akanyagavyo udongo wa kufinyangia. 26 41:26Ni nani aliyenena hili tokea mwanzoni, ili tupate kujua, au kabla, ili tuweze kusema, ‘Alikuwa sawa’? Hakuna aliyenena hili, hakuna aliyetangulia kusema hili, hakuna yeyote aliyesikia maneno kutoka kwenu. 27 41:27Nilikuwa wa kwanza kumwambia Sayuni, ‘Tazama, wako hapa!’ Nilimpa Yerusalemu mjumbe wa habari njema. 28 41:28Ninatazama, lakini hakuna yeyote: hakuna yeyote miongoni mwao awezaye kutoa shauri, hakuna yeyote wa kutoa jibu wakati ninapowauliza. 29 41:29Tazama, wote ni ubatili! Matendo yao ni bure; vinyago vyao ni upepo mtupu na machafuko. 42Mtumishi Wa Bwana 1 42:1“Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza, mteule wangu, ambaye ninapendezwa naye; nitaweka Roho yangu juu yake, naye ataleta haki kwa mataifa. 2 42:2Hatapaza sauti wala kupiga kelele, wala hataiinua sauti yake barabarani. 3 42:3Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima. Kwa uaminifu ataleta haki, 4 42:4hatazimia roho wala kukata tamaa, mpaka atakaposimamisha haki juu ya dunia. Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.” 5 42:5Hili ndilo asemalo Mungu, Bwana, yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda, aliyeitandaza dunia na vyote vitokavyo humo, awapaye watu wake pumzi, na uzima kwa wale waendao humo: 6 42:6“Mimi, Bwana, nimekuita katika haki; nitakushika mkono wako. Nitakulinda na kukufanya kuwa Agano kwa ajili ya watu na nuru kwa Mataifa, 7 42:7kuwafungua macho wale wasioona, kuwaacha huru kutoka kifungoni waliofungwa jela, na kuwafungua kutoka gerezani wale wanaokaa gizani. 8 42:8“Mimi ndimi Bwana; hilo ndilo Jina langu! Sitampa mwingine utukufu wangu wala sanamu sifa zangu. 9 42:9Tazama, mambo ya kwanza yametokea, nami natangaza mambo mapya; kabla hayajatokea nawatangazia habari zake.” Wimbo Wa Kumsifu Bwana 10 42:10Mwimbieni Bwana wimbo mpya, sifa zake toka miisho ya dunia, ninyi mshukao chini baharini, na vyote vilivyomo ndani yake, enyi visiwa na wote wakaao ndani yake. 11 42:11Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao; makao anamoishi Kedari na yashangilie. Watu wa Sela waimbe kwa furaha, na wapige kelele kutoka vilele vya milima. 12 42:12Wampe Bwana utukufu, na kutangaza sifa zake katika visiwa. 13 42:13 Bwana ataenda kama mtu mwenye nguvu, kama shujaa atachochea shauku yake, kwa kelele ataamsha kilio cha vita, naye atashinda adui zake. 14 42:14“Kwa muda mrefu nimenyamaza kimya, nimekaa kimya na kujizuia. Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua, ninapiga kelele, ninatweta na kushusha pumzi. 15 42:15Nitaharibu milima na vilima na kukausha mimea yako yote; nitafanya mito kuwa visiwa na kukausha mabwawa. 16 42:16Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua, kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao, na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini. Haya ndiyo mambo nitakayofanya; mimi sitawaacha. 17 42:17Lakini wale wanaotumaini sanamu, wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’ watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa. Israeli Kipofu Na Kiziwi 18 42:18“Sikieni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona! 19 42:19Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu, na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma? Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu, aliye kipofu kama mtumishi wa Bwana? 20 42:20Mmeona vitu vingi, lakini hamkuzingatia; masikio yenu yako wazi, lakini hamsikii chochote.” 21 42:21Ilimpendeza Bwana kwa ajili ya haki yake kufanya sheria yake kuwa kuu na tukufu. 22 42:22Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara, wote wamenaswa katika mashimo, au wamefichwa katika magereza. Wamekuwa nyara, wala hapana yeyote awaokoaye. Wamefanywa mateka, wala hapana yeyote asemaye, “Warudishe.” 23 42:23Ni nani miongoni mwenu atakayesikiliza hili, au atakayezingatia kwa makini katika wakati ujao? 24 42:24Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka, na Israeli kwa wateka nyara? Je, hakuwa yeye, Bwana, ambaye tumetenda dhambi dhidi yake? Kwa kuwa hawakufuata njia zake, hawakutii sheria zake. 25 42:25Hivyo akawamwagia hasira yake inayowaka, ukali wa vita. Iliwazunguka kwa miali ya moto, lakini hata hivyo hawakuelewa; iliwateketeza, lakini hawakuyatia moyoni. 43Mwokozi Pekee Wa Israeli 1 43:1Lakini sasa hili ndilo asemalo Bwana, yeye aliyekuumba, ee Yakobo, yeye aliyekuhuluku, ee Israeli: “Usiogope kwa maana nimekukomboa, nimekuita wewe kwa jina lako, wewe u wangu. 2 43:2Unapopita kwenye maji makuu, nitakuwa pamoja nawe, unapopita katika mito ya maji, hayatakugharikisha. Utakapopita katika moto, hutaungua, miali ya moto haitakuunguza. 3 43:3Kwa kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako. Ninaitoa Misri kuwa fidia yako, Kushi na Seba badala yako. 4 43:4Kwa kuwa wewe ni wa thamani na wa kuheshimiwa machoni pangu, nami kwa kuwa ninakupenda, nitatoa watu badala yako na mataifa badala ya maisha yako. 5 43:5Usiogope, kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe, nitawaleta watoto wako kutoka mashariki, na kukukusanya kutoka magharibi. 6 43:6Nitaiambia kaskazini, ‘Watoe!’ nayo kusini, ‘Usiwazuie.’ Walete wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia: 7 43:7kila mmoja ambaye ameitwa kwa Jina langu, niliyemuumba kwa utukufu wangu, niliyemhuluku na kumfanya.” 8 43:8Uwaongoze wale wenye macho lakini hawaoni, wenye masikio lakini hawasikii. 9 43:9Mataifa yote yanakutanika pamoja, na makabila yanakusanyika. Ni nani miongoni mwao aliyetangulia kutuambia haya, na kututangazia mambo yaliyopita? Walete mashahidi wao ili kuwathibitisha kuwa walikuwa sahihi, ili wengine waweze kusikia, waseme, “Ni kweli.” 10 43:10“Ninyi ni mashahidi wangu,” asema Bwana, “na mtumishi wangu niliyemchagua, ili mpate kunijua na kuniamini, na kutambua kwamba Mimi ndiye. Kabla yangu hakuna mungu aliyefanyizwa, wala hatakuwepo mwingine baada yangu. 11 43:11Mimi, naam mimi, ndimi Bwana, zaidi yangu hakuna mwokozi. 12 43:12Nimedhihirisha, kuokoa na kutangaza: Mimi, wala si mungu mgeni katikati yenu. Ninyi ni mashahidi wangu,” asema Bwana, “kwamba Mimi ndimi Mungu. 13 43:13Naam, tangu siku za kale, Mimi ndiye. Hakuna hata mmoja awezaye kuokoa kutoka mkononi wangu. Mimi ninapotenda, ni nani awezaye kutangua?” Huruma Za Mungu, Na Kukosa Uaminifu Kwa Israeli 14 43:14Hili ndilo Bwana asemalo, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Kwa ajili yenu nitatumana Babeli na kuwaleta Wakaldayo wote kama wakimbizi, katika meli walizozionea fahari. 15 43:15Mimi ndimi Bwana, yeye Aliye Mtakatifu wako, Muumba wa Israeli, Mfalme wako.” 16 43:16Hili ndilo asemalo Bwana, yeye aliyefanya njia baharini, mahali pa kupita kwenye maji mengi, 17 43:17aliyeyakokota magari ya vita na farasi, jeshi pamoja na askari wa msaada, nao wakalala huko, wala hawatainuka tena kamwe, wakakomeshwa, na wakazimika kama utambi: 18 43:18“Msiyakumbuke mambo yaliyopita, wala msiyatafakari mambo ya zamani. 19 43:19Tazama, nitafanya jambo jipya! Sasa litachipuka, je, hamtalitambua? Nitafanya njia jangwani na vijito vya maji katika nchi kame. 20 43:20Wanyama wa mwituni wataniheshimu, mbweha na bundi, kwa sababu ninawapatia maji jangwani, na vijito katika nchi kame, ili kuwapa watu wangu maji, wale niliowachagua, 21 43:21watu wale niliowaumba kwa ajili yangu, ili wapate kutangaza sifa zangu. 22 43:22“Hata hivyo hukuniita mimi, ee Yakobo, hujajitaabisha kwa ajili yangu, ee Israeli. 23 43:23Hujaniletea kondoo kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukulemea kwa sadaka za nafaka wala kukuchosha kwa kuhitaji uvumba. 24 43:24Hukuninunulia uvumba wowote wenye manukato, wala hukunipa kwa ukarimu mafuta ya wanyama wa dhabihu zako. Lakini umenilemea kwa dhambi zako, na kunitaabisha kwa makosa yako. 25 43:25“Mimi, naam mimi, ndimi nizifutaye dhambi zako, kwa ajili yangu mwenyewe, wala sizikumbuki dhambi zako tena. 26 43:26Tafakari mambo yaliyopita, njoo na tuhojiane, leta shauri lako uweze kupewa haki yako. 27 43:27Baba yako wa kwanza alitenda dhambi, wasemaji wako wameasi dhidi yangu. 28 43:28Kwa hiyo nitawaaibisha wakuu wa Hekalu lako, nami nitamtoa Yakobo aangamizwe, na Israeli adhihakiwe. 44Israeli Aliyechaguliwa 1 44:1“Lakini sasa sikiliza, ee Yakobo, mtumishi wangu, Israeli, niliyemchagua. 2 44:2Hili ndilo asemalo Bwana, yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni, yeye atakayekusaidia: Usiogope, ee Yakobo, mtumishi wangu, Yeshuruni, 44:2 Yeshuruni hapa maana yake ni Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli (ona pia Kum 32:15). niliyekuchagua. 3 44:3Kwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu, na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka; nitamimina Roho wangu juu ya watoto wako, nayo baraka yangu juu ya wazao wako. 4 44:4Nao watachipua kama manyasi katika shamba la majani, kama mierezi kando ya vijito vya maji yatiririkayo. 5 44:5Mmoja atasema, ‘Mimi ni wa Bwana’; mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; vilevile mwingine ataandika juu ya mkono wake, ‘Wa Bwana,’ na kujiita kwa jina la Israeli. Ni Bwana, Siyo Sanamu 6 44:6“Hili ndilo asemalo Bwana, Mfalme wa Israeli na Mkombozi, Bwana Mwenye Nguvu Zote: Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho; zaidi yangu hakuna Mungu. 7 44:7Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze. Yeye atangaze na kuweka mbele yangu ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale, tena ni nini kitakachotokea: naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja. 8 44:8Msitetemeke, msiogope. Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani? Ninyi ni mashahidi wangu. Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hasha, hakuna Mwamba mwingine; mimi simjui mwingine.” 9 44:9Wote wachongao sanamu ni ubatili, navyo vitu wanavyovithamini havifai kitu. Wale ambao wanazitetea ni vipofu, ni wajinga, nao waaibika. 10 44:10Ni nani atengenezaye mungu na kusubu sanamu, ambayo haiwezi kumfaidia kitu chochote? 11 44:11Yeye pamoja na wenziwe wa aina yake wataaibishwa, mafundi wao si kitu ila ni wanadamu tu. Wote wakusanyike pamoja na kuwa na msimamo wao, watashushwa chini kwa hofu na kwa fedheha. 12 44:12Muhunzi huchukua kifaa na kukifanyia kazi kwenye makaa ya moto, hutengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake. Huona njaa na kupoteza nguvu zake, asipokunywa maji huzimia. 13 44:13Seremala hupima kwa kutumia kamba na huuchora mstari kwa kalamu; huchonga kwa patasi na kutia alama kwa bikari. Huifanyiza katika umbo la binadamu, la mwanadamu katika utukufu wake wote, ili iweze kukaa katika sehemu yake ya ibada ya miungu. 14 44:14Hukata miti ya mierezi, huchukua mtiriza au mwaloni. Huuacha ukue miongoni mwa miti ya msituni, au hupanda msunobari, nayo mvua huufanya ukue. 15 44:15Ni kuni ya binadamu: yeye huchukua baadhi yake na kuota moto, huwasha moto na kuoka mkate. Lakini pia huutumia kumtengeneza mungu na akamwabudu, huitengeneza sanamu na kuisujudia. 16 44:16Sehemu ya kuni huziweka motoni, akapikia chakula chake, hubanika nyama na kula hadi ashibe. Huota moto na kusema, “Aha! Ninahisi joto, ninaona moto.” 17 44:17Mabaki yake hutengeneza mungu, sanamu yake; yeye huisujudia na kuiabudu. Huiomba na kusema, “Niokoe; wewe ni mungu wangu.” 18 44:18Hawajui chochote, hawaelewi chochote, macho yao yamefungwa hata hawawezi kuona, akili zao zimefungwa hata hawawezi kufahamu. 19 44:19Hakuna anayefikiri, hakuna mwenye maarifa wala ufahamu wa kusema, “Sehemu yake nilitumia kwa kuni; hata pia nilioka mkate juu ya makaa yake, nikabanika nyama na kuila. Je, nifanye machukizo kwa kile kilichobaki? Je, nisujudie gogo la mti?” 20 44:20Hujilisha kwa majivu, moyo uliodanganyika humpotosha; hawezi kujiokoa mwenyewe, au kusema, “Je, kitu hiki kilichoko katika mkono wangu wa kuume si ni uongo?” 21 44:21“Ee Yakobo, kumbuka mambo haya, ee Israeli, kwa kuwa wewe ni mtumishi wangu. Nimekuumba wewe, wewe ni mtumishi wangu. Ee Israeli, sitakusahau. 22 44:22Nimeyafuta makosa yako kama wingu, dhambi zako kama ukungu wa asubuhi. Nirudie mimi, kwa kuwa nimekukomboa wewe.” 23 44:23Enyi mbingu, imbeni kwa furaha, kwa maana Bwana amefanya jambo hili. Ee vilindi vya dunia, piga kelele. Enyi milima, pazeni sauti kwa nyimbo, enyi misitu na miti yenu yote, kwa maana Bwana amemkomboa Yakobo, ameuonyesha utukufu wake katika Israeli. Yerusalemu Kukaliwa 24 44:24“Hili ndilo asemalo Bwana, Mkombozi wako, aliyekuumba tumboni: “Mimi ni Bwana, niliyeumba vitu vyote, niliyezitanda mbingu peke yangu, niliyeitandaza nchi mwenyewe, 25 44:25“mimi huzipinga ishara za manabii wa uongo, na kuwatia upumbavu waaguzi, niyapinduaye maarifa ya wenye hekima, na kuyafanya kuwa upuzi, 26 44:26niyathibitishaye maneno ya watumishi wake, na kutimiza utabiri wa wajumbe wake, “niambiaye Yerusalemu, ‘Itakaliwa na watu,’ niambiaye miji ya Yuda kuwa, ‘Itajengwa,’ na kuhusu magofu yake, ‘Mimi nitayatengeneza,’ 27 44:27niambiaye kilindi cha maji, ‘Kauka, nami nitakausha vijito vyako,’ 28 44:28nisemaye kuhusu Koreshi, ‘Yeye ni mchungaji wangu, naye atatimiza yote yanipendezayo; atauambia Yerusalemu, “Ukajengwe tena,” na kuhusu Hekalu, “Misingi yake na iwekwe.” ’ 45Koreshi Chombo Cha Mungu 1 45:1“Hili ndilo asemalo Bwana kwa mpakwa mafuta wake, Koreshi, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume kutiisha mataifa mbele yake na kuwavua wafalme silaha zao, kufungua milango mbele yake ili malango yasije yakafungwa: 2 45:2Nitakwenda mbele yako na kusawazisha milima; nitavunjavunja malango ya shaba na kukatakata mapingo ya chuma. 3 45:3Nitakupa hazina za gizani, mali zilizofichwa mahali pa siri, ili upate kujua ya kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wa Israeli, akuitaye kwa jina lako. 4 45:4Kwa ajili ya Yakobo mtumishi wangu, Israeli niliyemchagua, nimekuita wewe kwa jina lako, na kukupa jina la heshima, ingawa wewe hunitambui. 5 45:5Mimi ndimi Bwana, wala hakuna mwingine, zaidi yangu hakuna Mungu. Nitakutia nguvu, ingawa wewe hujanitambua, 6 45:6ili kutoka mawio ya jua mpaka machweo yake, watu wapate kujua kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mimi. Mimi ndimi Bwana wala hakuna mwingine. 7 45:7Mimi ninaumba nuru na kuhuluku giza, ninaleta mafanikio na kusababisha maafa. Mimi, Bwana, huyatenda haya yote. 8 45:8“Enyi mbingu juu, nyesheni haki, mawingu na yaidondoshe. Dunia na ifunguke sana, wokovu na uchipuke, haki na ikue pamoja nao. Mimi, Bwana, ndiye niliyeiumba. 9 45:9“Ole wake yeye ashindanaye na Muumba wake, yeye ambaye ni kigae tu kati ya vigae juu ya ardhi. Je, udongo wa kufinyangia humwambia mfinyanzi, ‘Unatengeneza nini wewe?’ Je, kazi yako husema, ‘Hana mikono’? 10 45:10Ole wake amwambiaye baba yake, ‘Umezaa nini?’ Au kumwambia mama yake, ‘Umezaa kitu gani?’ 11 45:11“Hili ndilo asemalo Bwana, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na Muumba wake: Kuhusu mambo yatakayokuja, je, unaniuliza habari za watoto wangu, au kunipa amri kuhusu kazi za mikono yangu? 12 45:12Mimi ndiye niliyeumba dunia na kumuumba mwanadamu juu yake. Mikono yangu mwenyewe ndiyo iliyozitanda mbingu, nikayapanga majeshi yake yote ya angani. 13 45:13Mimi nitamwinua Koreshi katika haki yangu: nitazinyoosha njia zake zote. Yeye atajenga mji wangu upya, na kuwaweka huru watu wangu walio uhamishoni, lakini si kwa kulipiwa fedha wala kupewa zawadi, asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.”

14 45:14Hili ndilo asemalo Bwana:

“Mazao ya Misri na bidhaa za Kushi, nao wale Waseba warefu, watakujia na kuwa wako, watakujia wakijikokota nyuma yako, watakujia wamefungwa minyororo. Watasujudu mbele yako wakikusihi na kusema, ‘Hakika Mungu yu pamoja nawe, wala hakuna mwingine; hakuna Mungu mwingine.’ ” 15 45:15Hakika wewe u Mungu unayejificha, Ee Mungu na Mwokozi wa Israeli. 16 45:16Wote watengenezao sanamu wataaibika na kutahayarika; wataenda kutahayarika pamoja. 17 45:17Lakini Israeli ataokolewa na Bwana kwa wokovu wa milele; kamwe hutaaibika wala kutatahayarika, milele yote. 18 45:18Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana, yeye aliyeumba mbingu, ndiye Mungu; yeye aliyeifanya dunia na kuiumba, yeye ndiye aliiwekea misingi imara, hakuiumba ili iwe tupu, bali aliiumba ikaliwe na viumbe vyake. Anasema: “Mimi ndimi Bwana, wala hakuna mwingine. 19 45:19Sijasema sirini, kutoka mahali fulani katika nchi ya giza; sijawaambia wazao wa Yakobo, ‘Nitafuteni bure.’ Mimi, Bwana, nasema kweli; ninatangaza lililo sahihi. 20 45:20“Kusanyikeni pamoja mje, enyi wakimbizi kutoka mataifa. Wale wabebao sanamu za mti ni watu wasio na akili, wale waombao miungu isiyoweza kuokoa. 21 45:21Tangazeni litakalokuwepo, lisemeni hilo, wao na wafanye shauri pamoja. Ni nani aliyetangulia kusema hili tangu zamani, aliyetangaza tangu zamani za kale? Je, haikuwa Mimi, Bwana? Wala hapana Mungu mwingine zaidi yangu mimi, Mungu mwenye haki na Mwokozi; hapana mwingine ila mimi. 22 45:22“Nigeukieni mimi, nanyi mkaokolewe, enyi miisho yote ya dunia; kwa maana mimi ndimi Mungu, wala hapana mwingine. 23 45:23Nimeapa kwa nafsi yangu, kinywa changu kimenena katika uadilifu wote neno ambalo halitatanguka: Kila goti litapigwa mbele zangu, kwangu mimi kila ulimi utaapa. 24 45:24Watasema kuhusu mimi, ‘Katika Bwana peke yake ndiko kuna haki na nguvu.’ ” Wote ambao wamemkasirikia Mungu watamjia yeye, nao watatahayarika. 25 45:25Lakini katika Bwana wazao wote wa Israeli wataonekana wenye haki na watashangilia. 46Miungu Ya Babeli 1 46:1Beli anasujudu hadi nchi, Nebo anainama; sanamu zao zabebwa na wanyama wa mizigo. Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea, mzigo kwa waliochoka. 2 46:2Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini; hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu, wote wanakwenda utumwani pamoja. 3 46:3“Nisikilizeni mimi, ee nyumba ya Yakobo, ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli, ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba, nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu. 4 46:4Hata mpaka wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye, Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi. Nimewahuluku, nami nitawabeba, nitawasaidia ninyi na kuwaokoa. 5 46:5“Mtanilinganisha na nani, au mtanihesabu kuwa sawa na nani? Ni nani mtakayenifananisha naye ili tuweze kulinganishwa? 6 46:6Wengine humwaga dhahabu kutoka kwenye mifuko yao, na kupima fedha kwenye mizani; huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu, kisha huisujudia na kuiabudu. 7 46:7Huiinua mabegani na kuichukua; huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo. Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale. Ingawa mtu huililia, haimjibu; haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake. 8 46:8“Kumbukeni hili, litieni akilini, liwekeni moyoni, enyi waasi. 9 46:9Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale; mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine; mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine aliye kama mimi. 10 46:10Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo, naam, tangu zamani za kale, mambo ambayo hayajatendeka. Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote. 11 46:11Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye; kutoka nchi ya mbali, mtu atakayetimiza kusudi langu. Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza; lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda. 12 46:12Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu, ninyi mlio mbali na haki. 13 46:13Ninaleta haki yangu karibu, haiko mbali; wala wokovu wangu hautachelewa. Nitawapa Sayuni wokovu, Israeli utukufu wangu. 47Anguko La Babeli 1 47:1“Shuka uketi mavumbini, ee Bikira Binti Babeli; keti chini pasipo na kiti cha enzi, ee binti wa Wakaldayo. Hutaitwa tena mwororo wala wa kupendeza. 2 47:2Chukua mawe ya kusagia, usage unga, vua shela yako. Pandisha mavazi yako, ondoa viatu vyako, vuka vijito kwa shida. 3 47:3Uchi wako utafunuliwa na aibu yako itaonekana. Nitalipa kisasi; sitamhurumia hata mmoja.” 4 47:4Mkombozi wetu: Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake; ndiye yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli. 5 47:5“Keti kimya, ingia gizani, Binti wa Wakaldayo, hutaitwa tena malkia wa falme. 6 47:6Niliwakasirikia watu wangu na kuaibisha urithi wangu; niliwatia mikononi mwako, nawe hukuwaonea huruma. Hata juu ya wazee uliweka nira nzito sana. 7 47:7Ukasema, ‘Nitaendelea kuwa malkia milele!’ Lakini hukutafakari mambo haya wala hukuwaza juu ya kile kingeweza kutokea. 8 47:8“Sasa basi, sikiliza, ewe kiumbe mpenda anasa, ukaaye mahali pako pa salama, na kujiambia mwenyewe, ‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu. Kamwe sitakuwa mjane, wala sitafiwa na watoto.’ 9 47:9Haya mawili yatakupata, kufumba na kufumbua, katika siku moja: kufiwa na watoto, na ujane. Yote yatakupata kwa kipimo kikamilifu, ijapokuwa uchawi wako ni mwingi, na uaguzi wako ni mwingi. 10 47:10Umeutegemea uovu wako, nawe umesema, ‘Hakuna yeyote anionaye.’ Hekima yako na maarifa yako vinakupoteza unapojiambia mwenyewe, ‘Mimi ndiye, wala hakuna mwingine zaidi yangu.’ 11 47:11Maafa yatakujia, nawe hutaweza kuyaondoa kwa uaguzi. Janga litakuangukia, wala hutaweza kulikinga kwa fidia; msiba mkuu usioweza kuutabiri utakujia ghafula. 12 47:12“Endelea basi na uaguzi wako, na wingi wa uchawi wako, ambao umeutumikia tangu utoto wako. Labda utafanikiwa, labda unaweza ukasababisha hofu kuu. 13 47:13Ushauri wote uliopokea umekuchosha bure! Wanajimu wako na waje mbele, wale watazama nyota watabiriao mwezi baada ya mwezi, wao na wawaokoe na lile linalokuja juu yenu. 14 47:14Hakika wako kama mabua makavu; moto utawateketeza. Hawawezi hata kujiokoa wao wenyewe kutokana na nguvu za mwali wa moto. Hapa hakuna makaa ya kumtia mtu yeyote joto; hapa hakuna moto wa kuota. 15 47:15Hayo ndiyo yote wanayoweza kuwatendea ninyi, hawa ambao umetaabika nao na kufanya nao biashara tangu utoto. Kila mmoja atatoroka; hakuna yeyote awezaye kukuokoa. 48Israeli Mkaidi 1 48:1“Sikilizeni hili, ee nyumba ya Yakobo, ninyi mnaoitwa kwa jina la Israeli, na mnaotoka katika ukoo wa Yuda, ninyi mnaoapa kwa jina la Bwana, mnaomwomba Mungu wa Israeli, lakini si katika kweli au kwa haki; 2 48:2ninyi mnaojiita raiya wa mji mtakatifu, na kumtegemea Mungu wa Israeli, Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake: 3 48:3Nilitoa unabii mambo ya kwanza tangu zamani, kinywa changu kiliyatangaza na kuyafanya yajulikane; kisha ghafula nikayatenda, nayo yakatokea. 4 48:4Kwa kuwa nalijua jinsi ulivyokuwa mkaidi; mishipa ya shingo yako ilikuwa chuma, kipaji chako cha uso kilikuwa shaba. 5 48:5Kwa hiyo nilikuambia mambo haya tangu zamani, kabla hayajatokea nilikutangazia ili usije ukasema, ‘Sanamu zangu zilifanya hayo; kinyago changu cha mti na mungu wangu wa chuma aliyaamuru.’ 6 48:6Umesikia mambo haya; yaangalie hayo yote. Je, hutayakubali? “Kuanzia sasa na kuendelea nitakueleza mambo mapya, juu ya mambo yaliyofichika usiyoyajua. 7 48:7Yameumbwa sasa, wala si tangu zamani; hukupata kuyasikia kabla ya siku ya leo. Hivyo huwezi kusema, ‘Naam, niliyajua hayo.’ 8 48:8Hujayasikia wala kuyaelewa, tangu zamani sikio lako halikufunguka. Ninafahamu vyema jinsi ulivyo mdanganyifu, uliitwa mwasi tangu kuzaliwa kwako. 9 48:9Kwa ajili ya Jina langu mwenyewe ninaichelewesha ghadhabu yangu, kwa ajili ya sifa zangu nimeizuia isikupate, ili nisije nikakukatilia mbali. 10 48:10Tazama, nimekusafisha, ingawa si kama fedha, nimekujaribu katika tanuru ya mateso. 11 48:11Kwa ajili yangu mwenyewe, kwa ajili yangu mwenyewe, nafanya hili. Jinsi gani niliache Jina langu lichafuliwe? Sitautoa utukufu wangu kwa mwingine. Israeli Anawekwa Huru 12 48:12“Ee Yakobo, nisikilize mimi, Israeli, ambaye nimekuita: Mimi ndiye; mimi ndimi mwanzo na mwisho. 13 48:13Mkono wangu mwenyewe uliweka misingi ya dunia, nao mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo, zote husimama pamoja. 14 48:14“Kusanyikeni, ninyi nyote, msikilize: Ni ipi miongoni mwa hizo sanamu ambayo imetabiri vitu hivi? Watu wa Bwana waliochaguliwa na kuungana watatimiza kusudi lake dhidi ya Babeli; mkono wa Mungu utakuwa dhidi ya Wakaldayo. 15 48:15Mimi, naam, Mimi, nimenena; naam, nimemwita yeye. Nitamleta, naye atafanikiwa katika lile nililomtuma.

16 48:16“Nikaribieni na msikilize hili:

“Tangu tangazo la kwanza sikusema kwa siri; wakati litokeapo, nitakuwako hapo.” Sasa Bwana Mwenyezi amenituma, kwa Roho wake. 17 48:17Hili ndilo asemalo Bwana, Mkombozi wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli: “Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye katika njia ikupasayo kuiendea. 18 48:18Laiti ungesikiliza kwa makini maagizo yangu, amani yako ingekuwa kama mto, haki yako kama mawimbi ya bahari. 19 48:19Wazao wako wangekuwa kama mchanga, watoto wako kama chembe zake zisizohesabika; kamwe jina lao lisingefutiliwa mbali, wala kuangamizwa kutoka mbele zangu.” 20 48:20Tokeni huko Babeli, kimbieni kutoka kwa Wakaldayo! Tangazeni hili kwa kelele za shangwe na kulihubiri. Lipelekeni mpaka miisho ya dunia; semeni, “Bwana amemkomboa mtumishi wake Yakobo.” 21 48:21Hawakuona kiu alipowaongoza kupita jangwani; alifanya maji yatiririke kutoka kwenye mwamba kwa ajili yao; akapasua mwamba na maji yakatoka kwa nguvu. 22 48:22“Hakuna amani kwa waovu,” asema Bwana. 49Mtumishi Wa Bwana 1 49:1Nisikilizeni, enyi visiwa, sikieni hili, ninyi mataifa mlio mbali: Kabla sijazaliwa, Bwana aliniita, tangu kuzaliwa kwangu, amelitaja jina langu. 2 49:2Akafanya kinywa changu kuwa kama upanga ulionolewa, katika uvuli wa mkono wake akanificha; akanifanya kuwa mshale uliosuguliwa, na kunificha katika podo lake. 3 49:3Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika yeye nitaonyesha utukufu wangu.” 4 49:4Lakini nilisema, “Nimetumika bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida. Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwa Bwana, nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.” 5 49:5Sasa Bwana asema: yeye aliyeniumba tumboni kuwa mtumishi wake, kumrudisha tena Yakobo kwake na kumkusanyia Israeli, kwa maana nimepata heshima machoni pa Bwana, naye Mungu wangu amekuwa nguvu yangu; 6 49:6yeye asema: “Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kurejeza makabila ya Yakobo, na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi? Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa, ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.” 7 49:7Hili ndilo asemalo Bwana, yeye Mkombozi na Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwake yeye aliyedharauliwa na kuchukiwa na taifa, kwa mtumishi wa watawala: “Wafalme watakuona na kusimama, wakuu wataona na kuanguka kifudifudi, kwa sababu ya Bwana, aliye mwaminifu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, aliyekuchagua wewe.” Kurejezwa Kwa Israeli

8 49:8Hili ndilo asemalo Bwana:

“Wakati wangu uliokubalika nitakujibu, nami katika siku ya wokovu nitakusaidia; nitakuhifadhi, nami nitakufanya kuwa agano kwa ajili ya watu, ili kurudisha nchi na kugawanyia urithi tena wale waliokuwa ukiwa, 9 49:9kuwaambia mateka, ‘Tokeni nje,’ nao wale walio gizani, ‘Kuweni huru!’ “Watajilisha kando ya barabara na kupata malisho yao juu ya kila kilima kilicho kitupu. 10 49:10Hawataona njaa wala kuona kiu, wala hari ya jangwani au jua halitawapiga. Yeye mwenye huruma juu yao atawaonyesha njia, na kuwaongoza kando ya chemchemi za maji. 11 49:11Nitaifanya milima yangu yote kuwa barabara, na njia kuu zangu zitainuliwa. 12 49:12Tazama, watakuja kutoka mbali: wengine kutoka kaskazini, wengine kutoka magharibi, wengine kutoka nchi ya Sinimu.” 49:12 Sinimu hapa ina maana ya Aswani. 13 49:13Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu; furahi, ee dunia; pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima! Kwa maana Bwana anawafariji watu wake, naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa. 14 49:14Lakini Sayuni alisema, “Bwana ameniacha, Bwana amenisahau.” 15 49:15“Je, mama aweza kumsahau mtoto aliyeko matitini mwake akinyonya, wala asiwe na huruma juu ya mtoto aliyemzaa? Ingawa anaweza kusahau, mimi sitakusahau wewe! 16 49:16Tazama, nimekuchora kama muhuri katika vitanga vya mikono yangu, kuta zako zi mbele yangu daima. 17 49:17Wana wako wanaharakisha kurudi, nao wale waliokuteka wanaondoka kwako. 18 49:18Inua macho yako ukatazame pande zote: wana wako wote wanakusanyika na kukujia. Kwa hakika kama vile niishivyo, utawavaa wote kama mapambo, na kujifunga nao kama bibi arusi,” asema Bwana. 19 49:19“Ingawa uliangamizwa na kufanywa ukiwa, na nchi yako ikaharibiwa, sasa nafasi itakuwa finyu kwa ajili ya watu wako, nao wale waliokuangamiza watakuwa mbali sana. 20 49:20Watoto waliozaliwa wakati wa msiba wako bado watakuambia, ‘Mahali hapa ni finyu sana kwetu, tupe eneo kubwa zaidi la kuishi.’ 21 49:21Ndipo utasema moyoni mwako, ‘Ni nani aliyenizalia hawa? Nilikuwa nimefiwa, tena tasa; nilikuwa nimehamishwa na kukataliwa. Ni nani aliyewalea hawa? Niliachwa peke yangu, lakini hawa wametoka wapi?’ ”

22 49:22Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Tazama, nitawaashiria watu wa Mataifa, nitainua bendera yangu kwa mataifa; watawaleta wana wako mikononi yao, na kuwabeba binti zenu juu ya mabega yao. 23 49:23Wafalme watakuwa baba zenu wa kuwalea, na malkia wao watakuwa mama zenu wa kuwalea. Watasujudu mbele yako nyuso zao zikigusa ardhi; wataramba mavumbi yaliyo miguuni mwako. Ndipo utajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana; wale wanaonitumaini mimi hawataaibika.” 24 49:24Je, nyara zaweza kuchukuliwa kutoka kwa mashujaa wa vita, au mateka kuokolewa kutoka kwa watu wakali?

25 49:25Lakini hili ndilo asemalo Bwana:

“Naam, mateka watachukuliwa kutoka kwa mashujaa, na nyara zitapokonywa kutoka kwa watu wakali. Nitashindana na wale wanaoshindana nawe, nami nitawaokoa watoto wako. 26 49:26Nitawafanya wale wanaokuonea kula nyama yao wenyewe, watalewa kwa damu yao wenyewe, kama vile kwa mvinyo. Ndipo wanadamu wote watajua ya kuwa Mimi, Bwana, ni Mwokozi wako, Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo.” 50Dhambi Ya Israeli Na Utii Wa Mtumishi

1 50:1Hili ndilo asemalo Bwana:

“Iko wapi hati ya talaka ya mama yako ambayo kwayo niliachana naye? Au nimewauza ninyi kwa nani miongoni mwa watu wanaonidai? Kwa ajili ya dhambi zenu mliuzwa, kwa sababu ya makosa, mama yenu aliachwa. 2 50:2Nilipokuja, kwa nini hakuwepo hata mmoja? Nilipoita, kwa nini hakuwepo hata mmoja wa kujibu? Je, mkono wangu ni mfupi mno hata nisiweze kuwakomboa? Je, mimi sina nguvu za kukuokoa? Kwa kukemea tu naikausha bahari, naigeuza mito ya maji kuwa jangwa; samaki wake wanaoza kwa kukosa maji na kufa kwa ajili ya kiu. 3 50:3Ninalivika anga weusi na kufanya nguo ya gunia kuwa kifuniko chake.” 4 50:4 Bwana Mwenyezi amenipa ulimi uliofundishwa, ili kujua neno limtegemezalo aliyechoka. Huniamsha asubuhi kwa asubuhi, huamsha sikio langu lisikie kama mtu afundishwaye. 5 50:5 Bwana Mwenyezi amezibua masikio yangu, nami sikuwa mwasi, wala sikurudi nyuma. 6 50:6Niliwapa mgongo wangu wale wanipigao, mashavu yangu wale wangʼoao ndevu zangu; sikuuficha uso wangu kutokana na fedheha na kutemewa mate. 7 50:7Kwa sababu Bwana Mwenyezi ananisaidia, sitatahayarika. Kwa hiyo nimekaza uso wangu kama jiwe la gumegume, nami ninajua sitaaibika. 8 50:8Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu. Ni nani basi atakayeleta mashtaka dhidi yangu? Tukabiliane uso kwa uso! Mshtaki wangu ni nani? Ni nani aliye mshtaki wangu? 9 50:9Ni Bwana Mwenyezi anisaidiaye mimi. Ni nani huyo atakayenihukumu? Wote watachakaa kama vazi, nondo watawala wawamalize. 10 50:10Ni nani miongoni mwenu amchaye Bwana, na kulitii neno la mtumishi wake? Yeye atembeaye gizani, yeye asiye na nuru, na alitumainie jina la Bwana, na amtegemee Mungu wake. 11 50:11Lakini sasa, ninyi nyote mnaowasha mioto, na kupeana mienge iwakayo ninyi kwa ninyi, nendeni, tembeeni katika nuru ya moto wenu na ya mienge mliyoiwasha. Hili ndilo mtakalolipokea kutoka mkononi mwangu: Mtalala chini kwa mateso makali. 51Wokovu Wa Milele Kwa Sayuni 1 51:1“Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki na mnaomtafuta Bwana: Tazameni mwamba ambako mlichongwa, na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa; 2 51:2mwangalieni Abrahamu, baba yenu, na Sara, ambaye aliwazaa. Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu, nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi. 3 51:3Hakika Bwana ataifariji Sayuni, naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote; atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni, nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani ya Bwana. Shangwe na furaha zitakuwako ndani yake, shukrani na sauti za kuimba. 4 51:4“Nisikilizeni, watu wangu; nisikieni, taifa langu: Sheria itatoka kwangu; haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa. 5 51:5Haki yangu inakaribia mbio, wokovu wangu unakuja, nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa. Visiwa vitanitegemea na kungojea mkono wangu kwa matumaini. 6 51:6Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame dunia chini; mbingu zitatoweka kama moshi, dunia itachakaa kama vazi, na wakazi wake kufa kama mainzi. Bali wokovu wangu utadumu milele, haki yangu haitakoma kamwe. 7 51:7“Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa, ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu: Msiogope mashutumu ya wanadamu wala msitiwe hofu na matukano yao. 8 51:8Kwa maana nondo atawala kama vazi, nao funza atawatafuna kama sufu. Lakini haki yangu itadumu milele, wokovu wangu kwa vizazi vyote.” 9 51:9Amka, Amka! Jivike nguvu, ewe mkono wa Bwana, Amka, kama siku zilizopita, kama vile vizazi vya zamani. Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande, uliyemchoma yule joka? 10 51:10Si ni wewe uliyekausha bahari, maji ya kilindi kikuu, uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari ili waliokombolewa wapate kuvuka? 11 51:11Wale waliolipiwa fidia na Bwana watarudi. Wataingia Sayuni wakiimba; furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao. Furaha na shangwe zitawapata, huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka. 12 51:12“Mimi, naam mimi, ndimi niwafarijie ninyi. Ninyi ni nani hata kuwaogopa wanadamu wanaokufa, wanadamu ambao ni majani tu, 13 51:13kwamba mnamsahau Bwana Muumba wenu, aliyezitanda mbingu na kuiweka misingi ya dunia, kwamba mnaishi katika hofu siku zote kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu, ambaye nia yake ni kuangamiza? Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu? 14 51:14Wafungwa waliojikunyata kwa hofu watawekwa huru karibuni; hawatafia kwenye gereza lao, wala hawatakosa chakula. 15 51:15Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume: Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake. 16 51:16Nimeweka maneno yangu kinywani mwako na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu: Mimi niliyeweka mbingu mahali pake, niliyeweka misingi ya dunia, niwaambiaye Sayuni, ‘Ninyi ni watu wangu.’ ” Kikombe Cha Ghadhabu Ya Bwana 17 51:17Amka, amka! Simama, ee Yerusalemu, wewe uliyekunywa kutoka mkono wa Bwana kikombe cha ghadhabu yake, wewe uliyekunywa mpaka kufikia machujo yake, kikombe kile cha kunywea kiwafanyacho watu kuyumbayumba. 18 51:18Kati ya wana wote aliowazaa hakuwepo hata mmoja wa kumwongoza, kati ya wana wote aliowalea hakuwepo hata mmoja wa kumshika mkono. 19 51:19Majanga haya mawili yamekuja juu yako: ni nani awezaye kukufariji? Maangamizi, uharibifu, njaa na upanga: ni nani awezaye kukutuliza? 20 51:20Wana wako wamezimia, wamelala kwenye mwanzo wa kila barabara, kama swala aliyenaswa kwenye wavu. Wamejazwa na ghadhabu ya Bwana na makaripio ya Mungu wako. 21 51:21Kwa hiyo sikiliza hili, wewe uliyeteswa, uliyelewa, lakini si kwa mvinyo. 22 51:22Hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi wako, Mungu wako, yeye ambaye huwatetea watu wake: “Tazama, nimeondoa mkononi mwako kikombe kilichokufanya uyumbayumbe; kutoka kikombe hicho, kikombe cha kunywa cha ghadhabu yangu, kamwe hutakunywa tena. 23 51:23Nitakiweka mikononi mwa watesi wako, wale waliokuambia, ‘Anguka kifudifudi ili tuweze kutembea juu yako.’ Ukaufanya mgongo wako kama ardhi, kama njia yao ya kupita.” 521 52:1Amka, amka, ee Sayuni, jivike nguvu. Vaa mavazi yako ya fahari, ee Yerusalemu, mji mtakatifu. Asiyetahiriwa na aliye najisi hataingia kwako tena. 2 52:2Jikungʼute mavumbi yako, inuka, uketi kwenye kiti cha enzi, ee Yerusalemu. Jifungue minyororo iliyo shingoni mwako, ee Binti Sayuni uliye mateka.

3 52:3Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:

“Mliuzwa pasipo malipo, nanyi mtakombolewa bila fedha.”

4 52:4Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Hapo kwanza watu wangu walishuka Misri kuishi, hatimaye, Ashuru wakawaonea.

5 52:5“Basi sasa nina nini hapa?” asema Bwana.

“Kwa kuwa watu wangu wamechukuliwa pasipo malipo, nao wale wanaowatawala wanawadhihaki,” asema Bwana. “Mchana kutwa jina langu limetukanwa bila kikomo. 6 52:6Kwa hiyo watu wangu watalijua Jina langu; kwa hiyo katika siku ile watajua kwamba ndimi niliyetangulia kulisema. Naam, ni mimi.” 7 52:7Tazama jinsi miguu ya wale waletao habari njema ilivyo mizuri juu ya milima, wale wanaotangaza amani, wanaoleta habari njema, wanaotangaza wokovu, wauambiao Sayuni, “Mungu wako anatawala!” 8 52:8Sikiliza! Walinzi wako wanapaza sauti zao, pamoja wanapaza sauti zao kwa furaha. Wakati Bwana atakaporejea Sayuni, wataliona kwa macho yao wenyewe. 9 52:9Pazeni sauti ya nyimbo za furaha pamoja, enyi magofu ya Yerusalemu, kwa maana Bwana amewafariji watu wake, ameikomboa Yerusalemu. 10 52:10Mkono mtakatifu wa Bwana umefunuliwa machoni pa mataifa yote, nayo miisho yote ya dunia itaona wokovu wa Mungu wetu. 11 52:11Ondokeni, ondokeni, tokeni huko! Msiguse kitu chochote kilicho najisi! Tokeni kati yake mwe safi, ninyi mchukuao vyombo vya Bwana. 12 52:12Lakini hamtaondoka kwa haraka, wala hamtakwenda kwa kukimbia; kwa maana Bwana atatangulia mbele yenu, Mungu wa Israeli atakuwa mlinzi nyuma yenu. Mateso Na Utukufu Wa Mtumishi 13 52:13Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa hekima; atatukuzwa, na kuinuliwa juu, na kukwezwa sana. 14 52:14Kama walivyokuwa wengi walioshangazwa naye, kwani uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu yeyote na umbo lake kuharibiwa zaidi ya mfano wa mwanadamu: 15 52:15hivyo atayashangaza mataifa mengi, nao wafalme watafunga vinywa vyao kwa sababu yake. Kwa kuwa yale ambayo hawakuambiwa, watayaona, nayo yale wasiyoyasikia, watayafahamu. 531 53:1Ni nani aliyeamini ujumbe wetu, na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani? 2 53:2Alikua mbele yake kama mche mwororo na kama mzizi katika nchi kavu. Hakuwa na uzuri wala utukufu wa kutuvutia kwake, hakuwa na chochote katika sura yake cha kutufanya tumtamani. 3 53:3Alidharauliwa na kukataliwa na wanadamu, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye mateso. Kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa, wala hatukumhesabu kuwa kitu. 4 53:4Hakika alichukua udhaifu wetu na akajitwika huzuni zetu, hata hivyo tulidhania kuwa amepigwa na Mungu, akapigwa sana naye, na kuteswa. 5 53:5Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu, alichubuliwa kwa ajili ya maovu yetu; adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake, na kwa majeraha yake sisi tumepona. 6 53:6Sisi sote, kama kondoo, tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe, naye Bwana aliweka juu yake maovu yetu sisi sote. 7 53:7Alionewa na kuteswa, hata hivyo hakufungua kinywa chake; aliongozwa kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya wao wamkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake. 8 53:8Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa. Nani awezaye kueleza kuhusu kizazi chake? Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai, alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu. 9 53:9Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu, pamoja na matajiri katika kifo chake, ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake. 10 53:10Lakini yalikuwa ni mapenzi ya Bwana kumchubua na kumsababisha ateseke. Ingawa Bwana amefanya maisha yake kuwa sadaka ya hatia, ataona uzao wake na kuishi siku nyingi, nayo mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake. 11 53:11Baada ya maumivu ya nafsi yake, ataona nuru ya uzima na kuridhika; kwa maarifa yake, mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki, naye atayachukua maovu yao. 12 53:12Kwa hiyo nitamgawia sehemu miongoni mwa wakuu, naye atagawana nyara pamoja na wenye nguvu, kwa sababu aliyamimina maisha yake hadi mauti, naye alihesabiwa pamoja na wakosaji. Kwa kuwa alichukua dhambi za wengi, na kuwaombea wakosaji. 54Utukufu Wa Baadaye Wa Sayuni 1 54:1“Imba, ewe mwanamke tasa, wewe ambaye kamwe hukuzaa mtoto; paza sauti kwa kuimba, piga kelele kwa furaha, wewe ambaye kamwe hukupata utungu; kwa sababu watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi kuliko wa mwanamke mwenye mume,” asema Bwana. 2 54:2“Panua mahali pa hema lako, tandaza mapazia ya hema lako uyaeneze mbali, wala usiyazuie; ongeza urefu wa kamba zako, imarisha vigingi vyako. 3 54:3Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; wazao wako watayamiliki mataifa na kukaa katika miji yao iliyoachwa ukiwa. 4 54:4“Usiogope, wewe hutaaibika. Usiogope aibu, wewe hutaaibishwa. Wewe utasahau aibu ya ujana wako, wala hutakumbuka tena mashutumu ya ujane wako. 5 54:5Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako, Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako, yeye anaitwa Mungu wa dunia yote. 6 54:6 Bwana atakuita urudi kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni; kama mke aliyeolewa bado angali kijana na kukataliwa,” asema Mungu wako. 7 54:7“Kwa kitambo kidogo nilikuacha, lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha. 8 54:8Katika ukali wa hasira nilikuficha uso wangu kwa kitambo, lakini kwa fadhili za milele nitakuwa na huruma juu yako,” asema Bwana Mkombozi wako. 9 54:9“Kwangu mimi jambo hili ni kama siku za Noa, nilipoapa kuwa maji ya Noa kamwe hayatafunika tena dunia. Hivyo sasa nimeapa sitawakasirikia ninyi, kamwe sitawakemea tena. 10 54:10Ijapotikisika milima, na vilima viondolewe, hata hivyo upendo wangu usiokoma kwenu hautatikisika, wala agano langu la amani halitaondolewa,” asema Bwana, mwenye huruma juu yenu. 11 54:11“Ewe mji uliyeteswa, uliyepigwa kwa dhoruba na usiyetulizwa, nitakujenga kwa almasi, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi. 12 54:12Nitafanya minara yako ya akiki, malango yako kwa vito vingʼaavyo, nazo kuta zako zote za vito vya thamani. 13 54:13Watoto wako wote watafundishwa na Bwana, nayo amani ya watoto wako itakuwa kuu. 14 54:14Kwa haki utathibitika: Kuonewa kutakuwa mbali nawe; hutaogopa chochote. Hofu itakuwa mbali nawe; haitakukaribia wewe. 15 54:15Kama mtu yeyote akikushambulia, haitakuwa kwa ruhusa yangu; yeyote akushambuliaye atajisalimisha kwako. 16 54:16“Tazama, ni mimi niliyemuumba mhunzi, yeye afukutaye makaa kuwa moto, na kutengeneza silaha inayofaa kwa kazi yake. Tena ni mimi niliyemwambia mharabu kufanya uharibifu mwingi. 17 54:17Hakuna silaha itakayofanyizwa dhidi yako itakayofanikiwa, nawe utauthibitisha kuwa mwongo kila ulimi utakaokushtaki. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana na hii ndiyo haki yao itokayo kwangu,” asema Bwana. 55Mwaliko Kwa Wenye Kiu 1 55:1“Njooni, ninyi nyote wenye kiu, njooni kwenye maji; nanyi ambao hamna fedha, njooni, nunueni na mle! Njooni, nunueni divai na maziwa bila fedha na bila gharama. 2 55:2Kwa nini kutumia fedha kwa kitu ambacho si chakula, na kutaabikia kitu kisichoshibisha? Sikilizeni, nisikilizeni mimi na mle kilicho kizuri, nazo nafsi zenu zitafurahia utajiri wa unono. 3 55:3Tegeni sikio mje kwangu, nisikieni mimi, ili nafsi zenu zipate kuishi. Nitafanya agano la milele nanyi, pendo la uaminifu nililomwahidi Daudi. 4 55:4Tazama, nimemfanya kuwa shahidi wa mataifa, kiongozi na jemadari wa mataifa. 5 55:5Hakika utaita mataifa usiyoyajua, nayo mataifa yale yasiyokujua yataharakisha kukujia, kwa sababu ya Bwana Mungu wako, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwa maana amekutukuza.” 6 55:6Mtafuteni Bwana maadamu anapatikana; mwiteni maadamu yu karibu. 7 55:7Mtu mwovu na aiache njia yake, na mtu mbaya na ayaache mawazo yake. Yeye na amrudie Bwana, naye atamrehemu, arudi kwa Mungu wetu, kwa kuwa atamsamehe bure kabisa. 8 55:8“Kwa kuwa mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu,” asema Bwana. 9 55:9“Kama vile mbingu zilivyo juu kuliko dunia, ndivyo njia zangu zilivyo juu kuliko njia zenu na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. 10 55:10Kama vile mvua na theluji ishukavyo kutoka mbinguni, nayo hairudi tena huko bila kunywesha dunia na kuichipusha na kuistawisha, hivyo hutoa mbegu kwa mpanzi na mkate kwa mlaji, 11 55:11ndivyo lilivyo neno langu lile litokalo kinywani mwangu: Halitanirudia tupu, bali litatimiliza lile nililokusudia na litafanikiwa katika kusudi lile nililolituma. 12 55:12Mtatoka nje kwa furaha na kuongozwa kwa amani; milima na vilima vitapaza sauti kwa nyimbo mbele yenu, nayo miti yote ya shambani itapiga makofi. 13 55:13Badala ya kichaka cha miiba itaota miti ya misunobari, na badala ya michongoma utaota mhadasi. 55:13 Mhadasi ni aina ya mti ambao huota milimani karibu na Yerusalemu, hutoa harufu nzuri itumikayo kutengeneza manukato; kwa Kiebrania ni “hadas”, na ilikuwa inatumika kujenga vibanda wakati wa Sikukuu ya Vibanda (ona pia Neh 8:15). Hili litakuwa jambo la kumpatia Bwana jina, kwa ajili ya ishara ya milele, ambayo haitaharibiwa.” 56Wokovu Kwa Ajili Ya Wengine

1 56:1Hili ndilo asemalo Bwana:

“Dumisheni haki na mkatende lile lililo sawa, kwa maana wokovu wangu u karibu na haki yangu itafunuliwa upesi. 2 56:2Amebarikiwa mtu yule atendaye hili, mtu yule alishikaye kwa uthabiti, yeye ashikaye Sabato bila kuinajisi, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wowote.” 3 56:3Usimwache mgeni aambatanaye na Bwana aseme, “Hakika Bwana atanitenga na watu wake.” Usimwache towashi yeyote alalamike akisema, “Mimi ni mti mkavu tu.”

4 56:4Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:

“Kwa matowashi washikao Sabato zangu, ambao huchagua kile kinachonipendeza na kulishika sana agano langu: 5 56:5hao nitawapa ndani ya Hekalu langu na kuta zake kumbukumbu na jina bora kuliko kuwa na watoto wa kiume na wa kike: nitawapa jina lidumulo milele, ambalo halitakatiliwa mbali. 6 56:6Wageni wanaoambatana na Bwana ili kumtumikia, kulipenda jina la Bwana, na kumwabudu yeye, wote washikao Sabato bila kuinajisi na ambao hushika sana agano langu: 7 56:7hawa nitawaleta kwenye mlima wangu mtakatifu na kuwapa furaha ndani ya nyumba yangu ya sala. Sadaka zao za kuteketeza na dhabihu zao zitakubalika juu ya madhabahu yangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.” 8 56:8 Bwana Mwenyezi asema, yeye awakusanyaye Waisraeli waliohamishwa: “Bado nitawakusanya wengine kwao zaidi ya hao ambao wamekusanywa tayari.” Mashtaka Ya Mungu Dhidi Ya Waovu 9 56:9Njooni, enyi wanyama wote wa kondeni, njooni mle, ninyi wanyama wote wa mwituni! 10 56:10Walinzi wa Israeli ni vipofu, wote wamepungukiwa na maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kubweka; hulala na kuota ndoto, hupenda kulala. 11 56:11Ni mbwa wenye tamaa kubwa, kamwe hawatosheki. Wao ni wachungaji waliopungukiwa na ufahamu; wote wamegeukia njia yao wenyewe, kila mmoja hutafuta faida yake mwenyewe. 12 56:12Kila mmoja hulia, “Njooni, tupate mvinyo! Tunywe kileo sana! Kesho itakuwa kama leo, au hata bora zaidi.” 57Ibada Ya Sanamu Ya Israeli Iliyo Batili 1 57:1Mwenye haki hupotea, wala hakuna hata mmoja awazaye hilo moyoni mwake; watu wanaomcha Mungu huondolewa, wala hakuna hata mmoja anayeelewa kuwa wenye haki wameondolewa ili wasipatikane na maovu. 2 57:2Wale waendao kwa unyofu huwa na amani; hupata pumziko walalapo mautini. 3 57:3“Lakini ninyi: Njooni hapa, ninyi wana wa wachawi, ninyi wazao wa wazinzi na makahaba! 4 57:4Mnamdhihaki nani? Ni nani mnayemcheka kwa dharau, na kumtolea ndimi zenu? Je, ninyi si watoto wa waasi, uzao wa waongo? 5 57:5Mnawaka tamaa katikati ya mialoni na chini ya kila mti uliotanda matawi; mnawatoa kafara watoto wenu kwenye mabonde na chini ya majabali yenye mianya. 6 57:6“Sanamu zilizo katikati ya mawe laini ya mabondeni ndizo fungu lenu; hizo ndizo sehemu yenu. Naam, kwa hizo mmemimina sadaka za vinywaji, na kutoa sadaka za nafaka. Katika haya yote, niendelee kuona huruma? 7 57:7Umeweka kitanda chako juu kwenye kilima kirefu kilichoinuka, huko ulikwenda kutoa dhabihu zako. 8 57:8Nyuma ya milango yako na miimo yako umeweka alama zako za kipagani. Kwa kuniacha mimi, ulifunua kitanda chako, umepanda juu yake na kukipanua sana; ulifanya patano na wale ambao unapenda vitanda vyao, nawe uliangalia uchi wao. 9 57:9Ulikwenda kwa Moleki 57:9 Moleki alikuwa mungu aliyekuwa anaabudiwa na Waamoni; pia alijulikana kama Malkomu, Maloki au Kemoshi wa Moabu. ukiwa na mafuta ya zeituni, na ukaongeza manukato yako. Ukawatuma wajumbe wako mbali sana, ukashuka kwenye kaburi 57:9 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol. lenyewe! 10 57:10Ulikuwa umechoshwa na njia zako zote, lakini hukusema, ‘Hakuna tumaini.’ Ulipata uhuisho wa nguvu zako, kwa sababu hiyo hukuzimia. 11 57:11“Ni nani uliyemhofu hivyo na kumwogopa hata ukawa mwongo kwangu, wala hukunikumbuka au kutafakari hili moyoni mwako? Si ni kwa sababu nimekuwa kimya muda mrefu hata huniogopi? 12 57:12Nitaifunua haki yako na matendo yako, nayo hayatakufaidi. 13 57:13Utakapolia kwa kuhitaji msaada, sanamu zako ulizojikusanyia na zikuokoe! Upepo utazipeperusha zote, pumzi peke yake itazipeperusha, Lakini mtu atakayenifanya kimbilio lake, atairithi nchi na kuumiliki mlima wangu mtakatifu.” Faraja Kwa Wenye Majuto

14 57:14Tena itasemwa:

“Jengeni, jengeni, itengenezeni njia! Ondoeni vikwazo katika njia ya watu wangu.” 15 57:15Kwa maana hili ndilo asemalo Aliye juu, yeye aliyeinuliwa sana, yeye aishiye milele, ambaye jina lake ni Mtakatifu: “Ninaishi mimi mahali palipoinuka na patakatifu, lakini pia pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na mwenye roho ya unyenyekevu, ili kuzihuisha roho za wanyenyekevu na kuihuisha mioyo yao waliotubu. 16 57:16Sitaendelea kulaumu milele, wala sitakasirika siku zote, kwa kuwa roho ya mwanadamu ingezimia mbele zangu: yaani pumzi ya mwanadamu niliyemuumba. 17 57:17Nilighadhibika na tamaa yake ya dhambi; nilimwadhibu, nikauficha uso wangu kwa hasira, na bado aliendelea katika njia zake za tamaa. 18 57:18Nimeziona njia zake, lakini nitamponya, nitamwongoza na kumrudishia upya faraja, 19 57:19nikiumba sifa midomoni ya waombolezaji katika Israeli. Amani, amani, kwa wale walio mbali na kwa wale walio karibu,” asema Bwana. “Nami nitawaponya.” 20 57:20Bali waovu ni kama bahari ichafukayo, ambayo haiwezi kutulia, mawimbi yake hutupa takataka na matope. 21 57:21Mungu wangu asema, “Hakuna amani kwa waovu.” 58Mfungo Wa Kweli 1 58:1“Piga kelele, usizuie. Paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazieni watu wangu uasi wao, na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao. 2 58:2Kwa maana kila siku hunitafuta, wanaonekana kutaka kujua njia zangu, kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa, na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake. Hutaka kwangu maamuzi ya haki, nao hutamani Mungu awakaribie. 3 58:3Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona? Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’ “Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote. 4 58:4Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano, na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu. Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu. 5 58:5Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua, siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza? Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete, na kwa kujilaza juu ya nguo ya gunia na majivu? Je, huo ndio mnaouita mfungo, siku iliyokubalika kwa Bwana? 6 58:6“Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua: kufungua minyororo ya udhalimu, na kufungua kamba za nira, kuwaweka huru walioonewa, na kuvunja kila nira? 7 58:7Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi, unapomwona aliye uchi, umvike, wala si kumkimbia mtu wa nyama na damu yako mwenyewe? 8 58:8Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko na uponyaji wako utatokea upesi; ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako, na utukufu wa Bwana utakuwa mlinzi nyuma yako. 9 58:9Ndipo utaita, naye Bwana atajibu, utalia kuomba msaada, naye atasema: Mimi hapa. “Kama ukiiondoa nira ya udhalimu, na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu, 10 58:10nanyi kama mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu na kutosheleza mahitaji ya walioonewa, ndipo nuru yenu itakapongʼaa gizani, nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri. 11 58:11 Bwana atakuongoza siku zote, atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame, naye ataitia nguvu mifupa yako. Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri, kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe. 12 58:12Watu wako watajenga tena magofu ya zamani na kuinua misingi ya kale; utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka, Mwenye Kurejeza Barabara za Makao. 13 58:13“Kama ukitunza miguu yako isivunje Sabato, na kutokufanya kama vile upendavyo katika siku yangu takatifu, kama ukiita Sabato siku ya furaha na siku takatifu ya Bwana ya kuheshimiwa, kama utaiheshimu kwa kutoenenda katika njia zako mwenyewe, na kutokufanya yakupendezayo au kusema maneno ya upuzi, 14 58:14ndipo utakapojipatia furaha yako katika Bwana, nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.” Kinywa cha Bwana kimenena haya. 59Dhambi, Toba Na Ukombozi 1 59:1Hakika mkono wa Bwana si mfupi hata usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito hata lisiweze kusikia. 2 59:2Lakini maovu yenu yamewatenga ninyi na Mungu wenu, dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake, ili asisikie. 3 59:3Kwa maana mikono yenu imetiwa mawaa kwa damu na vidole vyenu kwa hatia. Midomo yenu imenena uongo, nazo ndimi zenu zimenongʼona mambo maovu. 4 59:4Hakuna hata mmoja anayedai kwa haki; hakuna hata mmoja anayetetea shauri lake kwa haki. Wanategemea mabishano matupu na kusema uongo, huchukua mimba ya magomvi na kuzaa uovu. 5 59:5Huangua mayai ya nyoka wenye sumu kali na kutanda wavu wa buibui. Yeyote alaye mayai yao atakufa, na wakati moja lianguliwapo, nyoka hutoka humo. 6 59:6Utando wao wa buibui haufai kwa nguo; hawawezi kujifunika kwa kile walichokitengeneza. Matendo yao ni matendo maovu, vitendo vya jeuri vipo mikononi mwao. 7 59:7Miguu yao hukimbilia kwenye dhambi, ni myepesi kumwaga damu isiyo na hatia. Mawazo yao ni mawazo maovu; uharibifu na maangamizi huonekana katika njia zao. 8 59:8Hawajui njia ya amani, hakuna haki katika mapito yao. Wameyageuza kuwa njia za upotovu, hakuna apitaye njia hizo atakayeifahamu amani. 9 59:9Hivyo uadilifu uko mbali nasi, nayo haki haitufikii. Tunatazamia nuru, kumbe! Yote ni giza, tunatazamia mwanga, lakini tunatembea katika giza kuu. 10 59:10Tunapapasa ukuta kama kipofu, tunapapasa katika njia zetu kama watu wasio na macho. Adhuhuri tunajikwaa kama wakati wa gizagiza; katikati ya wenye nguvu, tuko kama wafu. 11 59:11Wote tunanguruma kama dubu; tunalia kwa maombolezo kama hua. Tunatafuta haki, kumbe hakuna kabisa; tunatafuta wokovu, lakini uko mbali. 12 59:12Kwa sababu makosa yetu ni mengi machoni pako, na dhambi zetu zinashuhudia dhidi yetu. Makosa yetu yako pamoja nasi daima, nasi tunayatambua maovu yetu: 13 59:13Uasi na udanganyifu dhidi ya Bwana, kumgeuzia Mungu wetu kisogo, tukichochea udhalimu na maasi, tukinena uongo ambao mioyo yetu imeuhifadhi. 14 59:14Hivyo uadilifu umerudishwa nyuma, nayo haki inasimama mbali, kweli imejikwaa njiani, uaminifu hauwezi kuingia. 15 59:15Kweli haipatikani popote, na yeyote aepukaye uovu huwa mawindo. Bwana alitazama naye akachukizwa kwamba hapakuwepo haki. 16 59:16Aliona kuwa hakuwepo hata mtu mmoja, akashangaa kwamba hakuwepo hata mmoja wa kuingilia kati; hivyo mkono wake mwenyewe ndio uliomfanyia wokovu, nayo haki yake mwenyewe ndiyo iliyomtegemeza. 17 59:17Alivaa haki kama dirii kifuani mwake, na chapeo ya wokovu kichwani mwake, alivaa mavazi ya kisasi naye akajifunga wivu kama joho. 18 59:18Kulingana na kile walichokuwa wametenda, ndivyo atakavyolipa ghadhabu kwa watesi wake na kisasi kwa adui zake, atavilipa visiwa sawa na wanavyostahili. 19 59:19Kuanzia magharibi, watu wataliogopa jina la Bwana na kuanzia mawio ya jua, watauheshimu utukufu wake. Wakati adui atakapokuja kama mafuriko, Roho wa Bwana atainua kiwango dhidi yake na kumshinda. 20 59:20“Mkombozi atakuja Sayuni, kwa wale wa Yakobo wanaozitubu dhambi zao,” asema Bwana.

21 59:21“Kwa habari yangu mimi, hili ndilo agano langu nao,” asema Bwana. “Roho wangu, aliye juu yenu, na maneno yangu ambayo nimeyaweka katika vinywa vyenu, havitaondoka vinywani mwenu, wala kutoka vinywani mwa watoto wenu, wala kutoka vinywani mwa wazao wao, kuanzia sasa na hata milele,” asema Bwana.

60Utukufu Wa Sayuni 1 60:1“Ondoka, angaza, kwa kuwa nuru yako imekuja na utukufu wa Bwana umezuka juu yako. 2 60:2Tazama, giza litaifunika dunia na giza kuu litayafunika mataifa, lakini Bwana atazuka juu yako na utukufu wake utaonekana juu yako. 3 60:3Mataifa watakuja kwenye nuru yako na wafalme kwa mwanga wa mapambazuko yako. 4 60:4“Inua macho yako na utazame pande zote: Wote wanakusanyika na kukujia, wana wako wanakuja toka mbali, nao binti zako wanabebwa mikononi. 5 60:5Ndipo utatazama na kutiwa nuru, moyo wako utasisimka na kujaa furaha, mali zilizo baharini zitaletwa kwako, utajiri wa mataifa utakujilia. 6 60:6Makundi ya ngamia yatajaa katika nchi yako, ngamia vijana wa Midiani na Efa. Nao wote watokao Sheba watakuja, wakichukua dhahabu na uvumba na kutangaza sifa za Bwana. 7 60:7Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako, kondoo dume wa Nebayothi watakutumikia, watakubalika kama sadaka juu ya madhabahu yangu, nami nitalipamba Hekalu langu tukufu. 8 60:8“Ni nani hawa warukao kama mawingu, kama hua kuelekea kwenye viota vyao? 9 60:9Hakika visiwa vinanitazama, merikebu za Tarshishi 60:9 Au: za biashara (ona pia 1Fal 10:22; 22:48; 2Nya 9:21; 20:36; Isa 2:16). ndizo zinazotangulia, zikiwaleta wana wenu kutoka mbali, wakiwa na fedha na dhahabu zao, kwa heshima ya Bwana, Mungu wenu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwa maana amekujalia utukufu. 10 60:10“Wageni watazijenga upya kuta zako, na wafalme wao watakutumikia. Ingawa katika hasira nilikupiga, lakini katika upendeleo wangu nitakuonyesha huruma. 11 60:11Malango yako yatakuwa wazi siku zote, kamwe hayatafungwa, mchana wala usiku, ili watu wapate kukuletea utajiri wa mataifa: wafalme wao wakiongoza maandamano ya ushindi. 12 60:12Kwa maana taifa au ufalme ule ambao hautakutumikia utaangamia; utaharibiwa kabisa. 13 60:13“Utukufu wa Lebanoni utakujilia, msunobari, mvinje pamoja na mteashuri, ili kupapamba mahali pangu patakatifu, nami nitapatukuza mahali pa miguu yangu. 14 60:14Wana wa wale waliokuonea watakuja wakisujudu mbele yako, wote wanaokudharau watasujudu kwenye miguu yako, nao watakuita Mji wa Bwana, Sayuni ya Aliye Mtakatifu wa Israeli. 15 60:15“Ingawa umeachwa na kuchukiwa, bila yeyote anayesafiri ndani yako, nitakufanya kuwa fahari ya milele, na furaha ya vizazi vyote. 16 60:16Utanyonya maziwa ya mataifa, na kunyonyeshwa matiti ya wafalme. Ndipo utakapojua kwamba Mimi, Bwana, ni Mwokozi wako, Mkombozi wako, niliye Mwenye Nguvu wa Yakobo. 17 60:17Badala ya shaba nitakuletea dhahabu, na fedha badala ya chuma. Badala ya mti nitakuletea shaba, na chuma badala ya mawe. Nitafanya amani kuwa mtawala wako, na haki kuwa mfalme wako. 18 60:18Jeuri hazitasikika tena katika nchi yako, wala maangamizi au uharibifu ndani ya mipaka yako, lakini utaita kuta zako Wokovu, na malango yako Sifa. 19 60:19Jua halitakuwa tena nuru yako mchana, wala mwangaza wa mwezi hautakuangazia, kwa maana Bwana atakuwa nuru yako ya milele, naye Mungu wako atakuwa utukufu wako. 20 60:20Jua lako halitazama tena, nao mwezi wako hautafifia tena; Bwana atakuwa nuru yako milele, nazo siku zako za huzuni zitakoma. 21 60:21Ndipo watu wako wote watakuwa waadilifu, nao wataimiliki nchi milele. Wao ni chipukizi nililolipanda, kazi ya mikono yangu, ili kuonyesha utukufu wangu. 22 60:22Aliye mdogo kwenu atakuwa elfu, mdogo kuliko wote atakuwa taifa lenye nguvu. Mimi ndimi Bwana; katika wakati wake nitayatimiza haya upesi.” 61Mwaka Wa Upendeleo Wa Bwana 1 61:1Roho wa Bwana Mwenyezi yu juu yangu, kwa sababu Bwana amenitia mafuta kuwahubiria maskini habari njema. Amenituma kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao; 2 61:2kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi ya Mungu wetu, kuwafariji wote waombolezao, 3 61:3na kuwapa mahitaji wale wanaohuzunika katika Sayuni, ili kuwapa taji ya uzuri badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho ya kukata tamaa. Nao wataitwa mialoni ya haki, pando la Bwana, ili kuonyesha utukufu wake. 4 61:4Watajenga upya magofu ya zamani na kupatengeneza mahali palipoachwa ukiwa zamani; watafanya upya miji iliyoharibiwa, iliyoachwa ukiwa kwa vizazi vingi. 5 61:5Wageni watayachunga makundi yenu, wageni watafanya kazi katika mashamba yenu, na kutunza mashamba yenu ya mizabibu. 6 61:6Nanyi mtaitwa makuhani wa Bwana, mtaitwa watumishi wa Mungu wetu. Mtakula utajiri wa mataifa, nanyi katika utajiri wao mtajisifu. 7 61:7Badala ya aibu yao watu wangu watapokea sehemu maradufu, na badala ya fedheha watafurahia katika urithi wao; hivyo watarithi sehemu maradufu katika nchi yao, nayo furaha ya milele itakuwa yao. 8 61:8“Kwa maana Mimi, Bwana, napenda haki, na ninachukia unyangʼanyi na uovu. Katika uaminifu wangu nitawapa malipo yao na kufanya agano la milele nao. 9 61:9Wazao wao watajulikana miongoni mwa mataifa, na uzao wao miongoni mwa kabila za watu. Wale wote watakaowaona watatambua kuwa ni taifa ambalo Bwana amelibariki.” 10 61:10Ninafurahia sana katika Bwana, nafsi yangu inashangilia katika Mungu wangu. Kwa maana amenivika mavazi ya wokovu, na kunipamba kwa joho la haki, kama vile bwana arusi apambavyo kichwa chake kama kuhani, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vito vyake vya thamani. 11 61:11Kwa maana kama vile ardhi ifanyavyo chipukizi kuota, na bustani isababishavyo mbegu kuota, ndivyo Bwana Mwenyezi atafanya haki na sifa zichipuke mbele ya mataifa yote. 62Jina Jipya La Sayuni 1 62:1Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, mpaka haki yake itakapoangaza kama mapambazuko, wokovu wake kama mwanga wa moto. 2 62:2Mataifa wataona haki yako, nao wafalme wote wataona utukufu wako; wewe utaitwa kwa jina jipya lile ambalo kinywa cha Bwana kitatamka. 3 62:3Utakuwa taji ya fahari mkononi mwa Bwana, taji ya kifalme mkononi mwa Mungu wako. 4 62:4Hawatakuita tena Aliyeachwa, wala nchi yako kuiita Ukiwa. Bali utaitwa Hefsiba, 62:4 Hefsiba maana yake Yeye ninayemfurahia. nayo nchi yako itaitwa Beula, 62:4 Beula maana yake Aliyeolewa. kwa maana Bwana atakufurahia, nayo nchi yako itaolewa. 5 62:5Kama vile kijana aoavyo mwanamwali, ndivyo wanao 62:5 Au: wajenzi wako. watakavyokuoa wewe; kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe. 6 62:6Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, ee Yerusalemu, hawatanyamaza mchana wala usiku. Ninyi wenye kumwita Bwana, msitulie, 7 62:7msimwache apumzike hadi atakapoufanya imara Yerusalemu na kuufanya uwe sifa ya dunia. 8 62:8 Bwana ameapa kwa mkono wake wa kuume na kwa mkono wake wenye nguvu: “Kamwe sitawapa tena adui zenu nafaka zenu kama chakula chao; kamwe wageni hawatakunywa tena divai mpya ambayo mmeitaabikia, 9 62:9lakini wale waivunao nafaka wataila na kumsifu Bwana, nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake katika nyua za patakatifu pangu.” 10 62:10Piteni, piteni katika malango! Tengenezeni njia kwa ajili ya watu. Jengeni, jengeni njia kuu! Ondoeni mawe. Inueni bendera kwa ajili ya mataifa. 11 62:11 Bwana ametoa tangazo mpaka miisho ya dunia: “Mwambie Binti Sayuni, ‘Tazama, mwokozi wako anakuja! Tazama ujira wake uko pamoja naye, na malipo yake yanafuatana naye!’ ” 12 62:12Wataitwa Watu Watakatifu, Waliokombolewa na Bwana; nawe utaitwa Aliyetafutwa, Mji Usioachwa Tena. 63Siku Ya Mungu Ya Kisasi Na Ukombozi 1 63:1Ni nani huyu anayekuja kutoka Edomu, kutoka Bosra, mwenye mavazi yaliyotiwa madoa mekundu? Ni nani huyu, aliyevikwa joho la kifahari, anayetembea kwa ukuu wa nguvu zake? “Mimi ndimi, nisemaye katika haki, mwenye nguvu wa kuokoa.” 2 63:2Kwa nini mavazi yako ni mekundu, kama ya yule akanyagaye shinikizo la zabibu? 3 63:3“Nimekanyaga shinikizo la zabibu peke yangu; kutoka mataifa hakuna mtu aliyekuwa pamoja nami. Nimewaponda kwa miguu katika hasira yangu na kuwakanyaga chini katika ghadhabu yangu; damu yao ilitia matone kwenye mavazi yangu, na kutia madoa nguo zangu zote. 4 63:4Kwa kuwa siku ya kisasi ilikuwa moyoni mwangu, mwaka wa ukombozi wangu umefika. 5 63:5Nilitazama, lakini hakuwepo yeyote wa kunisaidia, nilishangaa kwa kuwa hakuwepo yeyote aliyetoa msaada; hivyo mkono wangu wenyewe ndio ulionifanyia wokovu, na ghadhabu yangu mwenyewe ndiyo iliyonitegemeza. 6 63:6Nilikanyaga mataifa kwa miguu katika hasira yangu, katika ghadhabu yangu niliwalewesha, na kumwaga damu yao juu ya ardhi.” Kusifu Na Kuomba 7 63:7Nitasimulia juu ya wema wa Bwana, kwa matendo ambayo apaswa kusifiwa, sawasawa na yote ambayo Bwana ametenda kwa ajili yetu: naam, mambo mengi mema aliyoyatenda kwa ajili ya nyumba ya Israeli, sawasawa na huruma zake na wema wake mwingi. 8 63:8Alisema, “Hakika wao ni watu wangu, wana ambao hawatanidanganya”; hivyo akawa Mwokozi wao. 9 63:9Katika taabu zao zote naye alitaabika, na malaika wa uso wake akawaokoa. Katika upendo wake na rehema zake aliwakomboa, akawainua na kuwachukua siku zote zilizopita. 10 63:10Lakini waliasi, na kumhuzunisha Roho Mtakatifu wake. Hivyo aligeuka na kuwa adui yao, na yeye mwenyewe akapigana dhidi yao. 11 63:11Ndipo watu wake wakazikumbuka siku zilizopita, siku za Mose na watu wake: yuko wapi yeye aliyewaleta kupitia katikati ya bahari, pamoja na wachungaji wa kundi lake? Yuko wapi yule aliyeweka Roho wake Mtakatifu katikati yao, 12 63:12aliyetuma mkono wake uliotukuka wenye nguvu kuwa katika mkono wa kuume wa Mose, aliyegawa maji ya bahari mbele yao, ili kujipatia jina milele, 13 63:13aliyewaongoza kupitia kwenye vilindi? Kama farasi katika nchi iliyo wazi, wao hawakujikwaa, 14 63:14kama ngʼombe washukao bondeni kwenye malisho, walipewa pumziko na Roho wa Bwana. Hivi ndivyo ulivyowaongoza watu wako ili kujipatia mwenyewe jina tukufu. 15 63:15Tazama chini kutoka mbinguni ukaone kutoka kiti chako cha enzi kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu. Uko wapi wivu wako na uweza wako? Umetuzuilia wema wako na huruma zako. 16 63:16Lakini wewe ni Baba yetu, ingawa Abrahamu hatufahamu sisi wala Israeli hatutambui; wewe, Ee Bwana, ndiwe Baba yetu, Mkombozi wetu tangu zamani za kale ndilo jina lako. 17 63:17Ee Bwana, kwa nini unatuacha twende mbali na njia zako, na kuifanya mioyo yetu migumu hata hatukukuheshimu? Rudi kwa ajili ya watumishi wako, yale makabila ambayo ni urithi wako. 18 63:18Kwa maana kwa muda mfupi watu wako walimiliki mahali pako patakatifu, lakini sasa adui zetu wamepakanyaga mahali patakatifu pako. 19 63:19Sisi tumekuwa kama wale ambao hujawatawala kamwe, kama wale ambao hawajaitwa kwa jina lako. 641 64:1Laiti ungelipasua mbingu na kushuka chini, ili milima ingelitetemeka mbele zako! 2 64:2Kama vile moto uteketezavyo vijiti na kusababisha maji kuchemka, shuka ukafanye jina lako lijulikane kwa adui zako, na kusababisha mataifa yatetemeke mbele zako! 3 64:3Kwa maana ulipofanya mambo ya kutisha ambayo hatukuyatazamia, ulishuka, nayo milima ikatetemeka mbele zako. 4 64:4Tangu nyakati za zamani hakuna yeyote aliyesikia, hakuna sikio lililotambua, hakuna jicho lililomwona Mungu mwingine ila wewe, anayetenda mambo kwa ajili ya wale wamngojeao. 5 64:5Uliwasaidia watu wale watendao yaliyo haki kwa furaha, wale wazikumbukao njia zako. Lakini wakati tulipoendelea kutenda dhambi kinyume na njia zako, ulikasirika. Tutawezaje basi kuokolewa? 6 64:6Sisi sote tumekuwa kama mtu aliye najisi, nayo matendo yetu yote ya uadilifu ni kama matambaa machafu; sisi sote tunasinyaa kama jani, na kama upepo maovu yetu hutupeperusha. 7 64:7Hakuna yeyote anayeliitia jina lako wala anayejitahidi kukushika, kwa kuwa umetuficha uso wako na kutuacha tudhoofike kwa sababu ya dhambi zetu. 8 64:8Lakini, Ee Bwana, wewe ndiwe Baba yetu. Sisi ni udongo, wewe ndiye mfinyanzi; sisi sote tu kazi ya mkono wako. 9 64:9Ee Bwana, usikasirike kupita kiasi, usizikumbuke dhambi zetu milele. Ee Bwana, utuangalie, twakuomba, kwa kuwa sisi sote tu watu wako. 10 64:10Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa; hata Sayuni ni jangwa, Yerusalemu ni ukiwa. 11 64:11Hekalu letu takatifu na tukufu, mahali ambapo baba zetu walikusifu wewe, limechomwa kwa moto, navyo vitu vyote tulivyovithamini vimeharibika. 12 64:12Ee Bwana, baada ya haya yote, utajizuia? Je, utanyamaza kimya na kutuadhibu kupita kiasi? 65Hukumu Na Wokovu 1 65:1“Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia. Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu, nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’ 2 65:2Mchana kutwa nimeinyoosha mikono yangu kwa watu wakaidi, wanaokwenda katika njia ambazo si nzuri, wafuatao mawazo yao wenyewe: 3 65:3taifa ambalo daima hunikasirisha machoni pangu, wakitoa dhabihu katika bustani na kufukiza uvumba juu ya madhabahu za matofali; 4 65:4watu waketio katikati ya makaburi na kukesha mahali pa siri, walao nyama za nguruwe, nazo sufuria zao zina mchuzi wa nyama zilizo najisi, 5 65:5wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie, kwa maana mimi ni mtakatifu mno kwako!’ Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu, ni moto uwakao mchana kutwa. 6 65:6“Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu: sitanyamaza, bali nitalipiza kwa ukamilifu; nitalipiza mapajani mwao: 7 65:7dhambi zenu na dhambi za baba zenu,” asema Bwana. “Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima na kunichokoza mimi juu ya vilima, nitawapimia mapajani mwao malipo makamilifu kwa matendo yao ya zamani.”

8 65:8Hili ndilo asemalo Bwana:

“Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana katika kishada cha zabibu, nao watu husema, ‘Usikiharibu, kwa kuwa bado kuna kitu kizuri ndani yake,’ hivyo ndivyo nitakavyofanya kwa ajili ya watumishi wangu; sitawaangamiza wote. 9 65:9Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo, na kutoka kwa Yuda wale watakaomiliki milima yangu, nao watu wangu wateule watairithi, nako huko wataishi watumishi wangu. 10 65:10Sharoni itakuwa malisho kwa ajili ya makundi ya kondoo, na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia kwa makundi ya ngʼombe, kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta. 11 65:11“Bali kwenu ninyi mnaomwacha Bwana na kuusahau mlima wangu mtakatifu, ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati, 65:11 Bahati alikuwa mungu wa Wakaldayo ambaye pia alijulikana kama Gadi. na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa kwa ajili ya Ajali, 65:11 Ajali au Meni alikuwa mungu wa majaliwa. 12 65:12nitawaagiza mfe kwa upanga, nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa; kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika, nilisema lakini hamkusikiliza. Mlitenda maovu machoni pangu, nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”

13 65:13Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi:

“Watumishi wangu watakula, lakini ninyi mtaona njaa; watumishi wangu watakunywa lakini ninyi mtaona kiu; watumishi wangu watafurahi, lakini ninyi mtaona haya. 14 65:14Watumishi wangu wataimba kwa furaha ya mioyo yao, lakini ninyi mtalia kutokana na uchungu wa moyoni, na kupiga yowe kwa sababu ya uchungu wa roho zenu. 15 65:15Mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa watu wangu waliochaguliwa; Bwana Mwenyezi atawaua ninyi, lakini watumishi wake atawapa jina jingine. 16 65:16Yeye aombaye baraka katika nchi atafanya hivyo kwa Mungu wa kweli; yeye aapaye katika nchi ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za zamani zitasahaulika na kufichwa kutoka machoni pangu. Mbingu Mpya Na Dunia Mpya 17 65:17“Tazama, nitaumba mbingu mpya na dunia mpya. Mambo ya zamani hayatakumbukwa, wala hayatakuja akilini. 18 65:18Lakini furahini na kushangilia daima katika hivi nitakavyoumba, kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza, nao watu wake wawe furaha. 19 65:19Nami nitaifurahia Yerusalemu na kuwafurahia watu wangu; sauti ya maombolezo na ya kilio haitasikika humo tena. 20 65:20“Kamwe hatakuwepo tena ndani yake mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu, au mzee ambaye hataishi akatimiza miaka yake. Yeye atakayekufa akiwa na umri wa miaka mia moja atahesabiwa kwamba ni kijana tu, yeye ambaye hatafika miaka mia moja, atahesabiwa kuwa amelaaniwa. 21 65:21Watajenga nyumba na kuishi ndani yake; watapanda mashamba ya mizabibu na kula matunda yake. 22 65:22Hawatajenga nyumba, nao watu wengine waishi ndani yake, au kupanda mazao na wengine wale. Kwa kuwa kama zilivyo siku za mti, ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, wateule wangu watafurahia kwa siku nyingi kazi za mikono yao. 23 65:23Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa watoto ili wapatwe na majanga, kwa kuwa watakuwa taifa lililobarikiwa na Bwana, wao na wazao wao pamoja nao. 24 65:24Kabla hawajaita, nitajibu, nao wakiwa katika kunena, nitasikia. 25 65:25Mbwa mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, naye simba atakula nyasi kama maksai, lakini mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote,” asema Bwana. 66Hukumu Na Matumaini

1 66:1Hili ndilo asemalo Bwana,

“Mbingu ni kiti changu cha enzi, nayo dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu. Iko wapi nyumba mtakayoijenga kwa ajili yangu? Mahali pangu pa kupumzikia patakuwa wapi? 2 66:2Je, mkono wangu haukufanya vitu hivi vyote, hivyo vikapata kuwepo?” asema Bwana. “Mtu huyu ndiye ninayemthamini: yeye ambaye ni mnyenyekevu na mwenye roho yenye toba, atetemekaye asikiapo neno langu. 3 66:3Lakini yeyote atoaye dhabihu ya fahali ni kama yeye auaye mtu, na yeyote atoaye sadaka ya mwana-kondoo, ni kama yule avunjaye shingo ya mbwa. Yeyote atoaye sadaka ya nafaka, ni kama yule aletaye damu ya nguruwe, na yeyote afukizaye uvumba wa kumbukumbu, ni kama yule aabuduye sanamu. Wamejichagulia njia zao wenyewe, nazo nafsi zao zinafurahia machukizo yao. 4 66:4Hivyo, mimi pia nitawachagulia mapigo makali, nami nitaleta juu yao kile wanachokiogopa. Kwa maana nilipoita, hakuna yeyote aliyejibu, niliposema, hakuna yeyote aliyesikiliza. Walifanya maovu machoni pangu na kuchagua lile linalonichukiza.” 5 66:5Sikieni neno la Bwana, ninyi mtetemekao kwa neno lake: “Ndugu zenu wanaowachukia ninyi na kuwatenga ninyi kwa sababu ya Jina langu, wamesema, Bwana na atukuzwe, ili tupate kuona furaha yenu!’ Hata sasa wataaibika. 6 66:6Sikieni hizo ghasia kutoka mjini, sikieni hizo kelele kutoka hekaluni! Ni sauti ya Bwana ikiwalipa adui zake yote wanayostahili. 7 66:7“Kabla hajasikia utungu, alizaa; kabla hajapata maumivu, alizaa mtoto mwanaume. 8 66:8Ni nani amepata kusikia jambo kama hili? Ni nani amepata kuona mambo kama haya? Je, nchi yaweza kuzaliwa kwa siku moja, au taifa laweza kutokea mara? Mara Sayuni alipoona utungu, alizaa watoto wake. 9 66:9Je, nilete mwana hadi wakati wa kuzaliwa na nisizalishe?” asema Bwana. “Je, nifunge tumbo la uzazi wakati mimi ndiye nizalishaye?” asema Mungu wako. 10 66:10“Shangilieni pamoja na Yerusalemu na mfurahi kwa ajili yake, ninyi nyote mnaompenda, shangilieni kwa nguvu pamoja naye, ninyi nyote mnaoomboleza juu yake. 11 66:11Kwa kuwa mtanyonya na kutosheka katika faraja ya matiti yake; mtakunywa sana, na kuufurahia wingi wa mafuriko ya ustawi wake.”

12 66:12Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:

“Nitamwongezea amani kama mto, nao utajiri wa mataifa kama kijito kifurikacho; utanyonya na kuchukuliwa mikononi mwake na kubembelezwa magotini pake. 13 66:13Kama mama anavyomfariji mtoto wake, ndivyo nitakavyokufariji wewe, nawe utafarijiwa huko Yerusalemu.” 14 66:14Wakati mtakapoona jambo hili, mioyo yenu itashangilia, nanyi mtastawi kama majani; mkono wa Bwana utajulikana kwa watumishi wake, bali ghadhabu yake kali itaonyeshwa kwa adui zake. 15 66:15Tazama, Bwana anakuja na moto, magari yake ya vita ni kama upepo wa kisulisuli, atateremsha hasira yake kwa ghadhabu kali, na karipio lake pamoja na miali ya moto. 16 66:16Kwa maana kwa moto na kwa upanga wake Bwana atatekeleza hukumu juu ya watu wote, nao wengi watakuwa ni wale waliouawa na Bwana.

17 66:17“Watu wote wanaojiweka wakfu na kujitakasa wenyewe ili kwenda bustanini, wakimfuata aliye katikati ya wale ambao hula nyama za nguruwe na panya pamoja na vitu vingine vilivyo machukizo, watafikia mwisho wao pamoja,” asema Bwana.

18 66:18“Nami, kwa sababu ya matendo yao na mawazo yao, niko karibu kuja na kukusanya mataifa yote na lugha zote, nao watakuja na kuuona utukufu wangu.

19 66:19“Nitaweka ishara katikati yao, nami nitapeleka baadhi ya hao walionusurika kwa mataifa, hadi Tarshishi, kwa Puli 66:19 Puli hapa inamaanisha Libya. na Waludi (wanaojulikana kama wapiga upinde), kwa Tubali na Uyunani, hadi visiwa vya mbali ambavyo havijasikia juu ya sifa zangu au kuuona utukufu wangu. Watatangaza utukufu wangu miongoni mwa mataifa. 20 66:20Nao watawaleta ndugu zenu wote, kutoka mataifa yote, mpaka kwenye mlima wangu mtakatifu katika Yerusalemu kama sadaka kwa Bwana, juu ya farasi, katika magari ya vita na magari makubwa, juu ya nyumbu na ngamia,” asema Bwana. “Watawaleta, kama Waisraeli waletavyo sadaka zao za nafaka, katika Hekalu la Bwana, katika vyombo safi kwa kufuata desturi za ibada. 21 66:21Nami nitachagua baadhi yao pia wawe makuhani na Walawi,” asema Bwana.

22 66:22“Kama vile mbingu mpya na nchi mpya ninazozifanya zitakavyodumu mbele zangu,” asema Bwana, “ndivyo jina lenu na wazao wenu watakavyodumu. 23 66:23Kutoka Mwezi Mpya hata mwingine, na kutoka Sabato hadi nyingine, wanadamu wote watakuja na kusujudu mbele zangu,” asema Bwana. 24 66:24“Nao watatoka nje na kuona maiti za wale walioniasi mimi. Funza wao hawatakufa, wala moto wao hautazimika, nao watakuwa kitu cha kuchukiza sana kwa wanadamu wote.”