Yoshua 1YoshuaBwana Anamwagiza Yoshua

1 1:1Baada ya kifo cha Mose mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Mose: 2 1:2“Mtumishi wangu Mose amekufa. Sasa basi, wewe pamoja na watu wote hawa, jiandaeni kuvuka huu Mto Yordani kuingia nchi ambayo karibu nitawapa wana wa Israeli. 3 1:3Kila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Mose. 4 1:4Nchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto mkubwa wa Frati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa 1:4 Yaani Bahari ya Mediterania. iliyoko upande wa magharibi. 5 1:5Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.

6 1:6“Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 1:7Uwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Mose mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 1:8Usiache Kitabu hiki cha Sheria kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 1:9Je, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

10 1:10Ndipo Yoshua akawaagiza maafisa wa watu akisema, 11 1:11“Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Wekeni tayari mahitaji yenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka hii Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa iwe yenu wenyewe.’ ”

12 1:12Lakini kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, Yoshua akasema, 13 1:13“Kumbukeni agizo lile Mose mtumishi wa Bwana alilowapa: ‘Bwana Mungu wenu anawapa ninyi raha, naye amewapa nchi hii.’ 14 1:14Wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu watakaa katika nchi ile Mose aliyowapa mashariki ya Yordani, lakini mashujaa wenu wote, wakiwa wamevikwa silaha kikamilifu lazima wavuke mbele ya ndugu zenu. Imewapasa kuwasaidia ndugu zenu hadi 15 1:15 Bwana awape nao raha, kama alivyokwisha kufanya kwa ajili yenu hadi wao pia watakapokuwa wamemiliki nchi ile Bwana Mungu wenu anayowapa. Baada ya hilo, mwaweza kurudi na kukalia nchi yenu wenyewe, ambayo Mose mtumishi wa Bwana aliwapa mashariki mwa Yordani kuelekea linakochomoza jua.”

16 1:16Ndipo wakamjibu Yoshua, “Chochote ambacho umetuagiza tutafanya na popote utakapotutuma tutakwenda. 17 1:17Kama vile tulivyomtii Mose kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. Bwana Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Mose. 18 1:18Yeyote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au chochote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”

2Rahabu Na Wapelelezi

1 2:1Kisha Yoshua mwana wa Nuni kwa siri akawatuma wapelelezi wawili kutoka Shitimu, akawaambia, “Nendeni mkaikague hiyo nchi, hasa Yeriko.” Kwa hiyo wakaenda na kuingia kwenye nyumba ya kahaba mmoja jina lake Rahabu na kukaa humo.

2 2:2Mfalme wa Yeriko akaambiwa, “Tazama! Baadhi ya Waisraeli wamekuja huku usiku huu kuipeleleza nchi.” 3 2:3Hivyo mfalme wa Yeriko akatuma huu ujumbe kwa Rahabu: “Watoe wale watu waliokujia na kuingia nyumbani mwako, kwa sababu wamekuja kuipeleleza nchi yote.”

4 2:4Lakini huyo mwanamke alikuwa amewachukua hao watu wawili na kuwaficha. Akasema, “Naam, watu hao walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka. 5 2:5Kulipoingia giza, wakati wa kufunga lango la mji, watu hao waliondoka. Sijui njia waliyoiendea. Wafuatilieni haraka. Huenda mkawapata.” 6 2:6(Lakini alikuwa amewapandisha darini akawafunika kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandika darini.) 7 2:7Basi hao watu wakaondoka kuwafuatilia hao wapelelezi katika njia ile inayoelekea vivuko vya Yordani, mara tu wafuatiliaji walipotoka nje, lango likafungwa.

8 2:8Kabla wale wapelelezi hawajalala, Rahabu akawaendea huko juu darini, 9 2:9akawaambia, “Ninajua kuwa Bwana amewapa nchi hii na hofu kuu imetuangukia kwa sababu yenu, kiasi kwamba wote waishio katika nchi hii wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yenu. 10 2:10Tumesikia jinsi Bwana alivyokausha maji ya Bahari ya Shamu kwa ajili yenu mlipotoka Misri, pia lile mlilowatendea Sihoni na Ogu, wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani, ambao mliwaangamiza kabisa. 11 2:11Tuliposikia juu ya hili, mioyo yetu iliyeyuka na kila mmoja alikosa ujasiri kwa sababu yenu, kwa maana Bwana Mungu wenu ni Mungu juu mbinguni na duniani chini. 12 2:12Sasa basi, tafadhali niapieni kwa Bwana, kwamba mtaitendea hisani jamaa ya baba yangu, kwa kuwa mimi nimewatendea hisani. Nipeni ishara ya uaminifu 13 2:13kwamba mtayahifadhi maisha ya baba yangu na mama yangu, ndugu zangu wa kiume na wa kike, pamoja na wale wote walio wa kwao na kwamba mtatuokoa na kifo.”

14 2:14Wale watu wakamhakikishia Rahabu, “Uhai wetu kwa uhai wenu! Ikiwa hutatoa habari ya nini tunachofanya, wakati Bwana atakapotupa nchi hii, tutawatendea kwa hisani na kwa uaminifu.”

15 2:15Kisha akawateremsha dirishani kwa kamba, kwa kuwa nyumba yake aliyokuwa anaishi ilikuwa sehemu ya ukuta wa mji. 16 2:16Alikuwa amewaambia, “Nendeni vilimani ili wale wafuatiliaji wasiwapate. Jificheni huko kwa siku tatu mpaka watakaporudi, hatimaye mwende zenu.”

17 2:17Wale watu wakamwambia, “Hiki kiapo ulichotuapisha hakitatufunga, 18 2:18isipokuwa, hapo tutakapoingia katika nchi hii, utakuwa umefunga hii kamba nyekundu dirishani pale ulipotuteremshia na kama utakuwa umewaleta baba yako na mama yako, ndugu zako na jamaa yako yote ndani ya nyumba yako. 19 2:19Ikiwa mtu yeyote atatoka nje ya nyumba yako akaenda mtaani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, hatutawajibika. Lakini yule ambaye atakuwa ndani pamoja nawe, kama mkono wa mtu yeyote ukiwa juu yake damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu. 20 2:20Lakini ikiwa utatoa habari ya shughuli yetu tunayofanya, tutakuwa tumefunguliwa kutoka kwenye kiapo hiki ulichotufanya tuape.”

21 2:21Naye akajibu, “Nimekubali. Na iwe kama mnavyosema.” Kwa hiyo akaagana nao, nao wakaondoka. Yeye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.

22 2:22Walipoondoka, wakaelekea vilimani na kukaa huko siku tatu, hadi wale waliokuwa wakiwafuatilia wakawa wamewatafuta njia nzima na kurudi pasipo kuwapata. 23 2:23Ndipo wale watu wawili wakaanza kurudi. Wakashuka kutoka kule vilimani, wakavuka mto na kuja kwa Yoshua mwana wa Nuni, na kumweleza kila kitu kilichowapata. 24 2:24Wakamwambia Yoshua, “Hakika Bwana ametupa nchi yote mikononi mwetu; watu wote wanayeyuka kwa hofu kwa sababu yetu.”

3Kuvuka Yordani

1 3:1Yoshua na Waisraeli wote wakaondoka asubuhi na mapema kutoka Shitimu, wakaenda mpaka Mto Yordani, ambako walipiga kambi kabla ya kuvuka. 2 3:2Baada ya siku tatu maafisa wakapita katika kambi yote, 3 3:3wakitoa maagizo kwa watu, wakiwaambia: “Mtakapoona Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu, likichukuliwa na Walawi ambao ndio makuhani, mtaondoka hapo mlipo na kulifuata. 4 3:4Ndipo mtakapotambua njia mtakayoiendea, kwa kuwa hamjawahi kuipita kabla. Lakini msisogee karibu, bali kuwe na umbali wa dhiraa 2,000 3:4 Dhiraa 2,000 ni sawa na mita 900. kati yenu na Sanduku.”

5 3:5Ndipo Yoshua akawaambia hao watu, “Jitakaseni, kwa kuwa kesho Bwana atatenda mambo ya kushangaza katikati yenu.”

6 3:6Yoshua akawaambia makuhani, “Liinueni Sanduku la Agano mkatangulie mbele ya watu.” Hivyo wakaliinua na kutangulia mbele yao.

7 3:7Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Leo nitaanza kukutukuza machoni pa Israeli yote, ili wapate kujua kuwa niko pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. 8 3:8Uwaambie makuhani wanaochukua Sanduku la Agano, ‘Mnapofika kwenye ukingo wa maji ya Yordani, nendeni mkasimame ndani ya mto.’ ”

9 3:9Yoshua akawaambia Waisraeli, “Njooni hapa msikilize maneno ya Bwana Mungu wenu. 10 3:10Hivi ndivyo mtakavyojua ya kuwa Mungu aliye hai yupo katikati yenu, na kwamba kwa hakika atawafukuza mbele yenu hao Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi. 11 3:11Tazameni, Sanduku la Agano la Bwana wa dunia yote litaingia ndani ya Mto Yordani likiwa limewatangulia. 12 3:12Sasa basi, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, mtu mmoja kutoka kila kabila. 13 3:13Mara tu nyayo za makuhani walichukualo Sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakapokanyaga ndani ya Mto Yordani, maji hayo yatiririkayo kutoka juu yatatindika na kusimama kama chuguu.”

14 3:14Basi, watu walipovunja kambi ili kuvuka Yordani, makuhani wakiwa wamebeba Sanduku la Agano waliwatangulia. 15 3:15Wakati huu ulikuwa wakati wa mavuno, nao Mto Yordani ulikuwa umefurika hadi kwenye kingo zake. Ilikuwa kawaida ya Yordani kufurika nyakati zote za mavuno. Mara tu makuhani wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Agano walipofika mtoni na nyayo zao kuzama ndani ya yale maji, 16 3:16maji hayo yaliyotiririka kutoka upande wa juu yaliacha kutiririka yakasimama kama chuguu mbali kabisa nao, kwenye mji ulioitwa Adamu kwenye eneo la Sarethani, wakati yale maji yaliyokuwa yanatiririka kuingia kwenye Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi), yalitindika kabisa. Hivyo watu wakavuka kukabili Yeriko.

17 3:17Wale makuhani waliobeba Sanduku la Agano la Bwana, wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Mto Yordani, wakati Waisraeli wote wakiwa wanapita hadi taifa lote likaisha kuvuka mahali pakavu.

4Ukumbusho Wa Kuvuka Mto Yordani

1 4:1Wakati taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, Bwana akamwambia Yoshua, 2 4:2“Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja, 3 4:3nawe uwaambie wachukue mawe kumi na mawili katikati ya Mto Yordani, palepale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu wa leo.”

4 4:4Basi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua kutoka miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila, 5 4:5naye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la Bwana Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kufuatana na hesabu ya makabila ya Waisraeli, 6 4:6kuwa kama ishara katikati yenu. Siku zijazo, wakati watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’ 7 4:7waambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la Bwana. Wakati lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.”

8 4:8Hivyo Waisraeli wakafanya kama Yoshua alivyowaagiza. Wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya Mto Yordani, kulingana na hesabu ya kabila za Waisraeli kama Bwana alivyomwambia Yoshua, nao wakayabeba hadi kambini mwao, mahali walipoyatua chini. 9 4:9Yoshua akayasimamisha yale mawe kumi na mawili ambayo yalikuwa katikati ya Mto Yordani, mahali pale ambapo miguu ya makuhani waliobeba Sanduku la Agano iliposimama. Nayo yako huko mpaka leo.

10 4:10Makuhani waliobeba lile Sanduku walibakia wakiwa wamesimama katikati ya Mto Yordani mpaka kila kitu Bwana alichomwamuru Yoshua kilipokuwa kimefanywa na watu, sawasawa na vile Mose alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Watu wakafanya haraka kuvuka, 11 4:11na mara tu watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Bwana na makuhani wakavuka watu wakiwa wanatazama. 12 4:12Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakavuka mbele ya Waisraeli, wakiwa wamevaa silaha, kama Mose alivyowaamuru. 13 4:13Kiasi cha watu 40,000 waliojiandaa kwa vita walivuka mbele za Bwana hadi nchi tambarare za Yeriko kwa ajili ya vita.

14 4:14Siku ile Bwana akamtukuza Yoshua mbele ya Israeli yote, nao wakamheshimu siku zote za maisha yake, kama vile walivyomheshimu Mose.

15 4:15Basi Bwana akamwambia Yoshua, 16 4:16“Waamuru hao makuhani wanaolibeba Sanduku la Ushuhuda, wapande kutoka ndani ya Mto Yordani.”

17 4:17Kwa hiyo Yoshua akawaamuru hao makuhani akisema, “Pandeni kutoka ndani ya Mto Yordani.”

18 4:18Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Bwana. Mara tu walipoiweka miguu yao penye kingo, nje ya mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.

19 4:19Siku ya kumi ya mwezi wa kwanza watu walipanda kutoka Yordani na kupiga kambi huko Gilgali, kwenye mpaka wa mashariki ya Yeriko. 20 4:20Naye Yoshua akayasimamisha huko Gilgali yale mawe kumi na mawili ambayo walikuwa wameyachukua katikati ya Mto Yordani. 21 4:21Akawaambia Waisraeli, “Wazao wenu watakapowauliza baba zao siku zijazo wakisema, ‘Mawe haya maana yake ni nini?’ 22 4:22Basi waambieni, ‘Israeli ilivukia mahali pakavu katika Mto Yordani.’ 23 4:23Kwa maana Bwana Mungu wenu alikausha maji ya Yordani mbele yenu, hadi mlipomaliza kuvuka. Bwana Mungu wenu alifanya haya kwa Mto Yordani sawasawa na kile alichoifanyia Bahari ya Shamu wakati alipoikausha mbele yetu hadi tulipomaliza kuvuka. 24 4:24Alifanya hivi ili kwamba mataifa yote ya dunia yapate kujua kuwa mkono wa Bwana ni wenye nguvu, na ili kwamba kila wakati mpate kumcha Bwana Mungu wenu.”

51 5:1Basi wafalme wote wa Waamori magharibi ya Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye pwani waliposikia jinsi Bwana alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri kuwakabili Waisraeli.

Tohara Huko Gilgali

2 5:2Wakati huo Bwana akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya mawe magumu sana na uwatahiri Waisraeli tena.” 3 5:3Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya mawe magumu sana na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi. 5:3 Gibeath-Haaralothi maana yake ni Kilima cha Magovi.

4 5:4Hii ndiyo sababu ya Yoshua kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani baada ya kuondoka Misri. 5 5:5Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini toka Misri walikuwa hawajatahiriwa. 6 5:6Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini mpaka wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati waliondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii Bwana. Kwa maana Bwana alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao katika kuapa kutupatia, nchi inayotiririka maziwa na asali. 7 5:7Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini. 8 5:8Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini mpaka walipokuwa wamepona.

9 5:9 Bwana akamwambia Yoshua, “Leo nimeiondoa aibu ya Wamisri kutoka kwenu.” Basi mahali pale pakaitwa Gilgali hadi leo.

10 5:10Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa kambini huko Gilgali katika tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka. 11 5:11Siku iliyofuata Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi, mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga. 12 5:12Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani.

Jemadari Wa Jeshi La Bwana

13 5:13Basi wakati Yoshua alipokuwa karibu na Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi uliofutwa kwenye ala. Yoshua akamwendea na kumuuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?”

14 5:14Akajibu, “La, siko upande wowote, lakini mimi nimekuja nikiwa jemadari wa jeshi la Bwana.” Yoshua akaanguka kifudifudi hadi chini, akasujudu, akamuuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?” 15 5:15Jemadari wa jeshi la Bwana akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali hapa unaposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.

6Yeriko Yatekwa Na Kuangamizwa

1 6:1Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa ajili ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia.

2 6:2Kisha Bwana akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na watu wake wa vita. 3 6:3Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita. 4 6:4Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. 5 6:5Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele.”

6 6:6Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, “Chukueni Sanduku la Agano la Bwana na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake.” 7 6:7Naye akawaagiza watu, “Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la Bwana.”

8 6:8Baada ya Yoshua kuzungumza na watu, wale makuhani saba wenye kuzibeba zile baragumu saba mbele za Bwana, wakatangulia mbele, wakipiga baragumu zao na Sanduku la Agano la Bwana likawafuata. 9 6:9Walinzi waliokuwa na silaha wakaenda mbele ya hao makuhani waliopiga hizo baragumu na hao walinzi wa nyuma wakafuata Sanduku. Wakati wote huu baragumu zilikuwa zikipigwa. 10 6:10Bali Yoshua alikuwa amewaagiza watu, “Msipige kelele ya vita, msipaze sauti zenu, wala kusema neno lolote mpaka siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!” 11 6:11Basi akalipeleka Sanduku la Bwana kuzungushwa huo mji, likizungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala.

12 6:12Yoshua akaamka mapema asubuhi iliyofuata nao makuhani wakalichukua Sanduku la Bwana. 13 6:13Wale Makuhani saba wakizibeba zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la Bwana wakizipiga. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao na walinzi wa nyuma wakalifuata Sanduku la Bwana, huku baragumu hizo zikiendelea kulia. 14 6:14Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita.

15 6:15Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba. 16 6:16Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipopiga baragumu kwa sauti kubwa, Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana Bwana amewapa mji huu! 17 6:17Mji huu pamoja na vyote vilivyomo ndani yake utawekwa wakfu kwa Bwana. Ila Rahabu tu, yule kahaba na wote ambao wako pamoja naye nyumbani mwake ndio watakaosalimishwa, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma. 18 6:18Lakini mjiepushe na vitu vilivyowekwa wakfu, msije mkachukua chochote katika hivyo, msije mkajiletea maangamizi katika maskani ya Israeli na kuiletea taabu. 19 6:19Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Bwana, lazima viletwe katika hazina yake.”

20 6:20Wakati baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele, na katika sauti ya baragumu, na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji. 21 6:21Wakauweka mji wakfu kwa Bwana, na kila chenye uhai ndani yake walikiangamiza kwa upanga, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee, ngʼombe, kondoo na punda.

22 6:22Yoshua akawaambia wale watu wawili waliokuwa wameipeleleza nchi, “Nendeni nyumbani kwa yule kahaba, mleteni pamoja na wote waliomo nyumbani mwake, kulingana na kiapo chenu kwake.” 23 6:23Basi wale vijana waliofanya upelelezi wakaenda kumleta Rahabu, baba yake na mama yake, na ndugu zake na watu wote waliokuwa pamoja naye. Wakaleta jamaa yake yote na kuwaweka mahali nje ya kambi ya Israeli.

24 6:24Kisha wakauchoma mji wote na kila kitu kilichokuwamo ndani yake. Lakini fedha, dhahabu, vyombo vya shaba na vya chuma wakaviweka katika hazina ya nyumba ya Bwana. 25 6:25Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu yule kahaba, jamaa yake yote na wote waliokuwa wa kwake, kwa sababu aliwaficha watu waliotumwa na Yoshua kuipeleleza Yeriko, naye anaishi miongoni mwa Waisraeli hata leo.

26 6:26Wakati ule Yoshua akatamka kiapo hiki akasema, “Aliyelaaniwa mbele za Bwana ni mtu atakayeinuka kuujenga tena mji huu wa Yeriko:

“Kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza wa kiume ataiweka misingi yake; kwa gharama ya mtoto wake wa mwisho atayaweka malango yake.”

27 6:27Hivyo Bwana alikuwa pamoja na Yoshua, na sifa zake zikaenea katika nchi yote.

7Dhambi Ya Akani

1 7:1Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyowekwa wakfu; Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alivichukua baadhi ya hivyo vitu. Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Israeli.

2 7:2Basi Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko waende Ai, karibu na Beth-Aveni mashariki ya Betheli, akawaambia, “Pandeni mkaipeleleze nchi.” Basi wale watu wakapanda wakaipeleleza Ai.

3 7:3Waliporudi kwa Yoshua, wakasema, “Si lazima watu wote waende kupigana na Ai. Watume watu elfu mbili au tatu wakauteke huo mji. Usiwachoshe watu wote, kwa sababu huko kuna watu wachache tu.” 4 7:4Basi wakapanda kama watu elfu tatu tu, lakini wakashambuliwa na watu wa Ai, 5 7:5ambao waliwaua watu kama thelathini na sita miongoni mwao. Wakawafukuza Waisraeli kutoka lango la mji hadi Shebarimu, nao wakawauwa huko kwenye materemko. Kutokana na hili mioyo ya watu ikayeyuka ikawa kama maji.

6 7:6Ndipo Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana, na akabakia hapo mpaka jioni. Wazee wa Israeli nao wakafanya vivyo hivyo wakatia mavumbi vichwani mwao. 7 7:7Yoshua akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, kwa nini umewavusha watu hawa ngʼambo ya Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Laiti tungeliridhika kukaa ngʼambo ile nyingine ya Yordani! 8 7:8Ee Bwana, niseme nini sasa, ikiwa sasa Israeli ameshafukuzwa na adui zake? 9 7:9Wakanaani na watu wengine wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka na kutufutilia jina letu duniani. Utafanya nini basi kwa ajili ya jina lako mwenyewe lililo kuu?”

10 7:10 Bwana akamwambia Yoshua, “Simama! Unafanya nini hapo chini kifudifudi? 11 7:11Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu, wameiba, wamesema uongo, wameviweka pamoja na mali zao. 12 7:12Ndiyo sababu Waisraeli hawawezi kusimama dhidi ya adui zao. Wanawapa visogo na kukimbia kwa kuwa wanastahili maangamizi. Sitakuwa pamoja nanyi tena mpaka mwangamize kila kitu miongoni mwenu kilichotengwa kwa maangamizi.

13 7:13“Nenda, ukawatakase watu. Waambie, ‘Jitakaseni mjiandae kwa kesho; kwa sababu hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Kitu kilichowekwa wakfu kipo katikati yenu, ee Israeli. Hamwezi kusimama dhidi ya adui zenu mpaka mtakapokiondoa.

14 7:14“ ‘Asubuhi, mjihudhurishe kabila kwa kabila. Itakuwa kabila lile atakalolitwaa Bwana litakuja mbele ukoo kwa ukoo, ukoo ule atakaoutwaa Bwana utakuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ile atakayoitwaa Bwana itakuja mbele mtu kwa mtu. 15 7:15Yule atakayekutwa na vitu vilivyowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, pamoja na vitu vyote alivyo navyo. Kwa kuwa amelivunja agano la Bwana na kufanya kitu cha aibu katika Israeli!’ ”

16 7:16Kesho yake asubuhi na mapema Yoshua akawaamuru Israeli kuja mbele kabila kwa kabila; na Yuda akatwaliwa. 17 7:17Koo za Yuda zikaja mbele, naye akawatwaa Wazera. Akaamuru ukoo wa Wazera kuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ya Zabdi ikatwaliwa. 18 7:18Yoshua akaamuru watu wa jamaa ya Zabdi kuja mbele mtu kwa mtu, naye Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, akatwaliwa.

19 7:19Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Bwana, Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.”

20 7:20Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya Bwana, Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya: 21 7:21Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili 7:21 Shekeli 200 za fedha ni sawa na kilo 2.3. za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, 7:21 Shekeli 50 ni sawa na gramu 600. nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.”

22 7:22Kwa hiyo Yoshua akatuma wajumbe, nao wakapiga mbio mpaka hemani, tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, pamoja na ile fedha chini yake. 23 7:23Wakavichukua vile vitu toka mle hemani, wakamletea Yoshua pamoja na Waisraeli wote, na wakavitandaza mbele za Bwana.

24 7:24Basi Yoshua, pamoja na Israeli yote, wakamchukua Akani mwana wa Zera, pamoja na ile fedha, lile joho, ile kabari ya dhahabu, wanawe na binti zake, ngʼombe, punda na kondoo wake, hema yake pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta katika Bonde la Akori. 25 7:25Yoshua akasema, “Kwa nini umeleta taabu hii juu yetu? Bwana ataleta taabu juu yako leo hii.”

Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto. 26 7:26Wakakusanya lundo la mawe juu ya Akani, ambalo lipo mpaka leo. Naye Bwana akageuka kutoka hasira yake kali. Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Bonde la Akori 7:26 Akori yamaanisha taabu. tangu siku hiyo.

8Mji Wa Ai Waangamizwa

1 8:1Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo. Chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. 2 8:2Utafanya Ai na mfalme wake kama ulivyofanya kwa mji wa Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kuchukua mateka wake na mifugo wake, kwa ajili yenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.”

3 8:3Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua watu mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku 4 8:4akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho. 5 8:5Mimi na watu walio pamoja nami, tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutawakimbia. 6 8:6Watatufuatilia mpaka tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia, 7 8:7ninyi inawapasa mwinuke mtoke huko mafichoni na kuuteka mji. Bwana Mungu wenu atautia mkononi mwenu. 8 8:8Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile Bwana alivyoamuru. Angalieni, nimewaagiza.”

9 8:9Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo.

10 8:10Asubuhi na mapema siku iliyofuatia, Yoshua akawakutanisha watu wake, na yeye na viongozi wa Israeli wakawa mbele ya watu kwenda Ai. 11 8:11Watu wote wa vita waliokuwa pamoja naye walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini mwa Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji. 12 8:12Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka katika uavizi kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji. 13 8:13Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wakivizia wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde.

14 8:14Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na watu wote wa mji wakatoka kwa haraka asubuhi na mapema, ili kukutana na Israeli katika vita mahali fulani panapotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji. 15 8:15Yoshua na Israeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, na kuelekea jangwani. 16 8:16Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji. 17 8:17Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.

18 8:18Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai. 19 8:19Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mavizioni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbilia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka.

20 8:20Watu wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wanawakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao. 21 8:21Basi Yoshua na Israeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kutoka kwenye mji, wakawageukia watu wa Ai na kuwashambulia. 22 8:22Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka. 23 8:23Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua.

24 8:24Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini. 25 8:25Watu kumi na mbili elfu, waume kwa wake, waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai. 26 8:26Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai. 27 8:27Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile Bwana alivyokuwa amemwagiza Yoshua.

28 8:28Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo. 29 8:29Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo mpaka jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe makubwa mengi juu yake, ambayo yamesalia mpaka leo.

Agano Linafanywa Upya Katika Mlima Ebali

30 8:30Kisha Yoshua akajenga madhabahu ya Bwana, Mungu wa Israeli, katika Mlima wa Ebali, 31 8:31kama Mose mtumishi wa Bwana alivyokuwa amewaamuru Waisraeli. Akaijenga sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Mose: madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo juu yake hakuna chombo cha chuma kilichotumika. Hapo juu yake wakamtolea Bwana sadaka za kuteketezwa na kutoa sadaka za amani. 8:31 Sadaka za ushirika. 32 8:32Pale, mbele ya Waisraeli Yoshua akanakili juu ya hayo mawe sheria ya Mose, aliyokuwa ameiandika. 33 8:33Israeli yote, wageni na wazawa sawasawa, wakiwa na wazee wao, maafisa na waamuzi, walikuwa wamesimama pande zote mbili za Sanduku la Agano la Bwana, wakiwaelekea wale waliokuwa wamelichukua, yaani makuhani, ambao ni Walawi. Nusu ya watu ilisimama mbele ya Mlima Gerizimu na nusu hiyo ingine ikasimama mbele ya Mlima Ebali, kama vile Mose mtumishi wa Bwana alivyokuwa ameamuru hapo mwanzo alipotoa maagizo ya kuwabariki watu wa Israeli.

34 8:34Hatimaye, Yoshua akasoma maneno yote ya sheria, yaani baraka na laana, kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria. 35 8:35Hakuna neno lolote katika yale yote ambayo Mose alikuwa ameamuru ambalo Yoshua hakulisomea kusanyiko lote la Israeli, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, na wageni walioishi miongoni mwao.

9Udanganyifu Wa Wagibeoni

1 9:1Basi ikawa wafalme wote waliokuwa magharibi mwa Yordani waliposikia juu ya haya yote, wale waliokuwa katika nchi ya vilima, upande wa magharibi mwa vilima na katika pwani yote ya hiyo Bahari Kuu, 9:1 Yaani Bahari ya Mediterania. hadi kufikia Lebanoni (wafalme wa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi), 2 9:2wakajiunga pamoja ili kupigana vita dhidi ya Yoshua na Israeli.

3 9:3Hata hivyo, watu wa Gibeoni waliposikia juu ya hayo yote Yoshua aliyowatendea watu wa Yeriko na Ai, 4 9:4nao wakaamua kufanya hila: Wakajifanya kama wajumbe wakiwa na punda waliobebeshwa mizigo wakiwa na magunia yaliyochakaa na viriba vya mvinyo vikuukuu vyenye nyufa zilizozibwa. 5 9:5Walivaa miguuni mwao viatu vilivyoraruka na kushonwa kisha wakavaa nguo kuukuu. Chakula chao kilikuwa mkate uliokauka na kuingia koga. 6 9:6Ndipo wakamwendea Yoshua kambini huko Gilgali wakamwambia yeye pamoja na watu wa Israeli, “Tumetoka katika nchi ya mbali, fanyeni mkataba nasi.”

7 9:7Basi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, “Lakini huenda mnakaa karibu nasi, twawezaje basi kufanya mapatano nanyi?”

8 9:8Wakamwambia Yoshua, “Sisi ni watumishi wako.”

Yoshua akawauliza, “Ninyi ni nani, nanyi mnatoka wapi?”

9 9:9Nao wakamjibu: “Watumishi wako wametoka nchi ya mbali sana kwa ajili ya umaarufu wa Bwana Mungu wenu. Kwa kuwa tumesikia taarifa zake: hayo yote aliyofanya huko Misri, 10 9:10pia yale yote aliyowatendea wafalme wawili wa Waamori mashariki ya Yordani; huyo Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani, aliyetawala huko Ashtarothi. 11 9:11Basi wazee wetu na wale wote wanaoishi katika nchi yetu walituambia, ‘Chukueni chakula cha safari; nendeni mkakutane na watu hao na kuwaambia, “Sisi tu watumishi wenu, fanyeni mapatano nasi.” ’ 12 9:12Mkate huu wetu ulikuwa wa moto tulipoufunga siku tulipoanza safari kuja kwenu, lakini sasa angalia jinsi ulivyokauka na kuota ukungu. 13 9:13Viriba hivi vya mvinyo vilikuwa vipya tulipovijaza, lakini ona jinsi vilivyo na nyufa. Nguo zetu na viatu vimechakaa kwa ajili ya safari ndefu.”

14 9:14Basi watu wa Israeli wakavikagua vyakula vyao bila kupata shauri kutoka kwa Bwana. 15 9:15Ndipo Yoshua akafanya mapatano ya amani pamoja nao kuwaacha waishi, nao viongozi wa kusanyiko wakathibitisha kwa kiapo.

16 9:16Siku ya tatu baada ya hao kufanya mapatano na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa hao watu ni jirani zao waliokuwa wanaishi karibu nao. 17 9:17Ndipo wana wa Israeli wakasafiri na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao ya Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu. 18 9:18Lakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli.

Kusanyiko lote likanungʼunika dhidi ya hao viongozi, 19 9:19lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa. 20 9:20Hivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.” 21 9:21Wakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo.

22 9:22Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ wakati ambapo ninyi mnaishi karibu nasi? 23 9:23Sasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”

24 9:24Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi Bwana Mungu wenu alivyomwamuru mtumishi wake Mose kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili. 25 9:25Sasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwako.”

26 9:26Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuuawa. 27 9:27Siku hiyo Yoshua akawafanya Wagibeoni wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya madhabahu ya Bwana mahali pale ambapo Bwana angepachagua. Hivyo ndivyo walivyo hadi hivi leo.

10Jua Linasimama

1 10:1Baada ya haya Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu alisikia kuwa Yoshua alikuwa ameteka mji wa Ai na kuuangamiza kabisa, tena alikuwa ameua mfalme wake, kama alivyofanya huko Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa watu wa Gibeoni walikuwa wamefanya mapatano ya amani na Waisraeli, na walikuwa wakiishi karibu yao. 2 10:2Yeye na watu wake wakataharuki mno kwa kuwa Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mmojawapo ya miji ya kifalme; ulikuwa mkubwa kuliko Ai, nao watu wake wote walikuwa mashujaa wa vita. 3 10:3Hivyo Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu akaomba msaada kwa Hohamu mfalme wa Hebroni, Piramu mfalme wa Yarmuthi, Yafia mfalme wa Lakishi, na Debiri mfalme wa Egloni. 4 10:4Akawaambia, “Njooni mnisaidie kuipiga Gibeoni, kwa sababu imefanya mapatano ya amani na Yoshua na Waisraeli.”

5 10:5Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, ambao ni wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni, wakaunganisha majeshi yao. Wakapanda na vikosi vyao vyote, nao wakajipanga dhidi ya Gibeoni na kuishambulia.

6 10:6Nao Wagibeoni wakatuma ujumbe kwa Yoshua kwenye kambi ya Gilgali na kumwambia, “Usiwatelekeze watumishi wako. Panda haraka uje kwetu kutuokoa! Tusaidie, kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao kwenye nchi ya vilima wameunganisha majeshi yao pamoja dhidi yetu.”

7 10:7Basi Yoshua akaondoka Gilgali pamoja na jeshi lake lote, wakiwepo watu wote mashujaa wa vita. 8 10:8 Bwana akamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna yeyote atakayeweza kushindana nawe.”

9 10:9Baada ya Yoshua kutembea usiku kucha kutoka Gilgali, akawashambulia ghafula. 10 10:10 Bwana akawafadhaisha mbele ya Waisraeli, nao wakawashinda kwa ushindi mkuu huko Gibeoni. Israeli wakawafukuza kuelekea njia iendayo Beth-Horoni wakiwaua mpaka kufikia njia iendayo Azeka na Makeda. 11 10:11Walipokuwa wakikimbia mbele ya Israeli kwenye barabara iteremkayo kutoka Beth-Horoni hadi Azeka, Bwana akawavumishia mawe makubwa ya mvua kutoka mbinguni, na wengi wao wakauawa na hayo mawe kuliko wale waliouawa kwa upanga wa Waisraeli.

12 10:12Katika siku ile ambayo Bwana aliwapeana Waamori kwa Israeli, Yoshua akanena na Bwana akiwa mbele ya Waisraeli akasema:

“Wewe jua, simama juu ya Gibeoni, wewe mwezi, tulia juu ya Bonde la Aiyaloni.” 13 10:13Hivyo jua likasimama, nao mwezi ukatulia, hadi taifa hilo lilipokwisha kujilipizia kisasi kwa adui wake, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari.

Jua likasimama kimya katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku moja nzima. 14 10:14Haijakuwepo siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo Bwana alimsikiliza mwanadamu. Hakika Bwana alikuwa akiwapigania Israeli.

15 10:15Ndipo Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Israeli yote.

Wafalme Watano Wa Waamori Wauawa

16 10:16Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda. 17 10:17Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda, 18 10:18akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mdomo wa hilo pango, tena wekeni walinzi wa kulilinda. 19 10:19Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni kutoka nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu amewatia mkononi mwenu.”

20 10:20Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza kabisa karibu wote, lakini wachache waliosalia walifika kwenye miji yao yenye maboma. 21 10:21Basi jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda, na hakuna yeyote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli.

22 10:22Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.” 23 10:23Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni. 24 10:24Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita watu wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita waliokwenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni.

25 10:25Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo Bwana atakalowatendea adui zenu wote mnaokwenda kupigana nao.” 26 10:26Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wakiningʼinia juu ya ile miti hadi jioni.

27 10:27Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru, nao wakawashusha kutoka kwenye ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Kwenye mdomo wa lile pango wakaweka mawe makubwa, ambayo yapo hadi leo.

28 10:28Siku ile Yoshua akateka Makeda. Akamuua kila mmoja katika ule mji, pamoja na mfalme wake kwa upanga. Hakubakiza mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Makeda kama vile alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.

Israeli Yaangamiza Miji Ya Kusini

29 10:29Ndipo Yoshua akaondoka Makeda akiwa pamoja na Israeli yote mpaka mji wa Libna na kuushambulia. 30 10:30 Bwana pia akautia huo mji wa Libna pamoja na mfalme wake mikononi mwa Israeli. Yoshua akaangamiza ule mji na kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza huko mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Libna kama alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko.

31 10:31Kisha Yoshua akaondoka Libna kwenda Lakishi akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia. 32 10:32 Bwana akautia Lakishi mikononi mwa Israeli, Yoshua akauteka siku ya pili. Yoshua akauangamiza mji na kila kilichokuwa ndani yake kwa upanga, kama tu vile alivyokuwa ameufanyia mji wa Libna. 33 10:33Wakati huo huo, Horamu mfalme wa Gezeri alikuwa amepanda ili kusaidia Lakishi, lakini Yoshua akamshinda pamoja na jeshi lake, hadi hapakubakia mtu yeyote.

34 10:34Ndipo Yoshua akaondoka Lakishi kwenda Egloni akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia. 35 10:35Wakauteka mji huo siku ile ile, wakaupiga kwa upanga na kumwangamiza kila mmoja aliyekuwa ndani yake, kama vile walivyokuwa wameufanyia Lakishi.

36 10:36Kisha Yoshua akapanda kutoka Egloni kwenda Hebroni akiwa pamoja na Israeli yote na kuushambulia. 37 10:37Wakauteka mji na kuupiga kwa upanga, pamoja na mfalme wake, vijiji vyake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Hawakubakiza mtu yeyote. Kama vile huko Egloni, waliuangamiza kabisa pamoja na kila mmoja aliyekuwa ndani yake.

38 10:38Ndipo Yoshua na Israeli wote wakageuka na kuushambulia Debiri. 39 10:39Wakauteka mji, mfalme wake na vijiji vyake, na kuupiga kwa upanga. Kila mmoja aliyekuwa ndani yake wakamwangamiza kabisa. Hawakubakiza mtu yeyote. Wakaufanyia Debiri na mfalme wake kama vile walivyokuwa wameifanyia miji ya Libna na Hebroni na wafalme wao.

40 10:40Hivyo Yoshua akalishinda eneo hilo lote, ikiwa ni pamoja na nchi ya vilima, na Negebu, na sehemu ya magharibi chini ya vilima, materemko ya milima, pamoja na wafalme wake wote. Hakubakiza mtu yeyote. Akaangamiza kabisa kila kitu chenye pumzi, kama vile Bwana, Mungu wa Israeli, alivyokuwa ameamuru. 41 10:41Yoshua akawashinda kuanzia Kadesh-Barnea hadi Gaza na kutoka eneo lote la Gosheni hadi Gibeoni. 42 10:42Wafalme hawa wote pamoja na nchi zao Yoshua aliwashinda kwa wakati mmoja, kwa sababu Bwana, Mungu wa Israeli, aliwapigania Israeli.

43 10:43Ndipo Yoshua akarudi pamoja na Israeli yote kwenye kambi huko Gilgali.

11Wafalme Wa Kaskazini Washindwa

1 11:1Ikawa Yabini mfalme wa Hazori aliposikia habari za mambo haya, akatuma ujumbe kwa Yobabu mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na kwa mfalme wa Akishafu, 2 11:2na pia kwa wafalme wa upande wa kaskazini wale waliokuwa milimani, katika Araba upande wa kusini mwa Kinerethi, kwenye shefela, upande wa magharibi na katika miinuko ya Nafoth-Dori upande wa magharibi; 3 11:3kwa Wakanaani upande wa mashariki na magharibi; kwa Waamori, Wahiti, Waperizi na Wayebusi katika nchi ya vilima; na kwa Wahivi chini ya Hermoni katika eneo ya Mispa. 4 11:4Wakaja na vikosi vyao vyote na hesabu kubwa ya farasi na magari ya kuvutwa na farasi, jeshi kubwa, kama wingi wa mchanga ulio pwani ya bahari. 5 11:5Wafalme hawa wote wakaunganisha majeshi yao na kupiga kambi pamoja kwenye Maji ya Meromu, ili kupigana dhidi ya Israeli.

6 11:6 Bwana akamwambia Yoshua, “Usiwaogope, kwa sababu kesho saa kama hii nitawatia wote mikononi mwa Israeli, wakiwa wameuawa. Utakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuyachoma moto magari yao ya vita.”

7 11:7Hivyo Yoshua pamoja na jeshi lake lote wakaja dhidi yao ghafula kwenye Maji ya Meromu kuwashambulia, 8 11:8naye Bwana akawatia mikononi mwa Israeli. Wakawashinda na kuwafukuza hadi Sidoni Kuu na kuwafikisha Misrefoth-Maimu, hadi Bonde la Mispa upande wa mashariki, hadi pakawa hakuna yeyote aliyebaki. 9 11:9Yoshua akawatendea kama Bwana alivyoamuru. Akakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuchoma moto magari yao ya vita.

10 11:10Wakati huo Yoshua akarudi na kuuteka mji wa Hazori na kumuua mfalme wake kwa upanga. (Hazori ulikuwa mji mkuu wa falme hizo zote.) 11 11:11Kila aliyekuwa ndani yake wakamuua kwa upanga. Wakawaangamiza kabisa, wala hawakusaza chochote chenye pumzi na akauchoma Hazori kwenyewe kwa moto.

12 11:12Yoshua akaiteka hii miji yote ya kifalme pamoja na wafalme wake na kuwapiga kwa upanga. Akawaangamiza kabisa wote, jinsi Mose mtumishi wa Bwana alivyowaagiza. 13 11:13Lakini Israeli hawakuichoma moto hata mojawapo ya miji iliyojengwa katika vilima vyao vidogo isipokuwa mji wa Hazori ambao Yoshua aliuchoma moto. 14 11:14Waisraeli wakajichukulia nyara zote na mifugo yote ya miji hii, bali waliwaua watu wote kwa upanga hadi walipowaangamiza kabisa, pasipo kumbakiza yeyote mwenye pumzi. 15 11:15Kama vile Bwana alivyomwagiza Mose mtumishi wake, vivyo hivyo Mose alimwagiza Yoshua, naye Yoshua akafanya kama vivyo, hakukosa kufanya lolote katika yale yote Bwana aliyomwagiza Mose.

16 11:16Yoshua akaiteka nchi hii yote: nchi ya vilima, Negebu yote, eneo yote ya Gosheni, shefela ya upande wa magharibi, Araba na milima ya Israeli pamoja na shefela zao, 17 11:17kuanzia Mlima Halaki ambao umeinuka kuelekea Seiri hadi Baal-Gadi katika Bonde la Lebanoni chini ya Mlima Hermoni. Akawateka wafalme wake wote, akawapiga na kuwaua. 18 11:18Yoshua akapigana vita dhidi ya wafalme hawa wote kwa muda mrefu. 19 11:19Hakuna mji wowote katika eneo hili uliofanya mkataba wa amani na Israeli, isipokuwa hao Wahivi wa Gibeoni. Wengine wote walishindwa katika vita. 20 11:20Kwa maana Bwana mwenyewe ndiye aliifanya mioyo yao iwe migumu, ili kupigana vita dhidi ya Israeli ili apate kuwafutilia mbali pasipo huruma, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

21 11:21Wakati huo Yoshua akaenda kuwaangamiza Waanaki kutoka nchi ya vilima: kuanzia Hebroni, Debiri na Anabu, na kutoka nchi yote ya vilima ya Yuda na kutoka nchi yote ya vilima ya Israeli. Yoshua akawaangamiza kabisa pamoja na miji yao. 22 11:22Hawakubaki Waanaki wowote katika nchi ya Israeli, ila tu katika nchi ya Gaza, Gathi na Ashdodi. 23 11:23Hivyo Yoshua akaiteka nchi hiyo yote kama vile Bwana alivyokuwa amemwagiza Mose, naye Yoshua akawapa Israeli kuwa urithi wao, kulingana na walivyogawanyika katika kabila zao.

Ndipo nchi ikawa na amani bila vita.

12Orodha Ya Wafalme Walioshindwa

1 12:1Hawa ndio wafalme wa nchi ambao Waisraeli waliwashinda na kuitwaa nchi yao upande wa mashariki mwa Yordani, kuanzia Bonde la Arnoni mpaka Mlima Hermoni, pamoja na eneo lote la upande wa mashariki ya Araba:

2 12:2Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni. Alitawala kuanzia Aroeri kwenye ukingo wa Bonde la Arnoni, kuanzia katikati ya bonde, hadi kwenye Mto Yaboki, ambao ni mpaka wa Waamoni. Hii ilijumlisha nusu ya Gileadi. 3 12:3Pia alitawala Araba ya mashariki kuanzia Bahari ya Kinerethi 12:3 Yaani Bahari ya Galilaya. hadi Bahari ya Araba (yaani Bahari ya Chumvi 12:3 Yaani Bahari Mfu.), hadi Beth-Yeshimothi, kisha kuelekea kusini chini ya materemko ya Pisga. 4 12:4Nayo nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa mmoja wa mabaki ya Warefai, aliyetawala Ashtarothi na Edrei. 5 12:5Naye alitawala katika Mlima Hermoni, Saleka, Bashani yote hadi mpaka wa watu wa Geshuri, na watu wa Maaka na nusu ya Gileadi, hadi kwenye mpaka wa Sihoni mfalme wa Heshboni.

6 12:6Mose, mtumishi wa Bwana, na Waisraeli wakawashinda. Naye Mose mtumishi wa Bwana akawapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase nchi ya hao wafalme ili iwe milki yao.

7 12:7Hawa ndio wafalme wa nchi ambao Yoshua na Waisraeli waliwashinda upande wa magharibi mwa Yordani, kuanzia Baal-Gadi katika Bonde la Lebanoni hadi kufikia Mlima Halaki, unaoinuka ukielekea Seiri. (Yoshua alitoa nchi zao kwa makabila ya Israeli iwe urithi wao sawasawa na mgawanyiko wa makabila yao: 8 12:8nchi ya vilima, shefela, upande wa magharibi, Araba, materemko ya milima, jangwa, na Negebu; nchi za Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi):

9 12:9mfalme wa Yeriko mmoja mfalme wa Ai (karibu na Betheli) mmoja 10 12:10mfalme wa Yerusalemu mmoja mfalme wa Hebroni mmoja 11 12:11mfalme wa Yarmuthi mmoja mfalme wa Lakishi mmoja 12 12:12mfalme wa Egloni mmoja mfalme wa Gezeri mmoja 13 12:13mfalme wa Debiri mmoja mfalme wa Gederi mmoja 14 12:14mfalme wa Horma mmoja mfalme wa Aradi mmoja 15 12:15mfalme wa Libna mmoja mfalme wa Adulamu mmoja 16 12:16mfalme wa Makeda mmoja mfalme wa Betheli mmoja 17 12:17mfalme wa Tapua mmoja mfalme wa Heferi mmoja 18 12:18mfalme wa Afeki mmoja mfalme wa Lasharoni mmoja 19 12:19mfalme wa Madoni mmoja mfalme wa Hazori mmoja 20 12:20mfalme wa Shimron-Meroni mmoja mfalme wa Akishafu mmoja 21 12:21mfalme wa Taanaki mmoja mfalme wa Megido mmoja 22 12:22mfalme wa Kedeshi mmoja mfalme wa Yokneamu katika Karmeli mmoja 23 12:23mfalme wa Dori (katika Nafoth-Dori) 12:23 Au: katika miinuko ya Nafoth-Dori.mmoja mfalme wa Goimu katika Gilgali mmoja 24 12:24mfalme wa Tirsa mmoja
wafalme jumla yao ilikuwa thelathini na mmoja. 13Sehemu Za Kanaani Ambazo Hazijatwaliwa

1 13:1Yoshua alipokuwa mzee na umri wake ukiwa umesogea sana, Bwana akamwambia, “Wewe ni mzee sana, na bado kumesalia sehemu kubwa sana za nchi ambazo ni za kutwaliwa.

2 13:2“Nchi iliyosalia ni hii: maeneo yote ya Wafilisti na Wageshuri: 3 13:3kutoka Mto Shihori ulioko mashariki mwa Misri, kuelekea kaskazini kwenye eneo la Ekroni, ambayo yote ilihesabika kama ya Wakanaani (maeneo yale matano ya watawala wa Kifilisti, ambayo ni Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni: ndiyo nchi ya Waavi); 4 13:4kuanzia kusini, nchi yote ya Wakanaani, kuanzia Ara ambayo ni ya Wasidoni, ikienea hadi Afeki, na eneo la Waamori, 5 13:5eneo la Wagebali; 13:5 Yaani eneo la Bubilo, mji wa zamani sana wa Ufoinike (kama kilomita 80 kaskazini mwa Beiruti). Lebanoni yote kuelekea mashariki, kuanzia Baal-Gadi chini ya Mlima Hermoni hadi Lebo-Hamathi.

6 13:6“Na kuhusu wakaaji wote katika maeneo ya milima, kuanzia Lebanoni hadi Misrefoth-Maimu, pamoja na eneo lote la Wasidoni, mimi mwenyewe nitawafukuza watoke mbele ya Waisraeli. Hakikisha umegawa nchi hii kwa Israeli kuwa urithi, kama nilivyokuagiza, 7 13:7sasa basi, ligawanye eneo hili kwa yale makabila tisa na ile nusu ya kabila la Manase kuwa urithi.”

Mgawanyo Wa Nchi Mashariki Mwa Yordani 8 13:8Ile nusu nyingine ya Manase, Wareubeni na Wagadi, walishapokea urithi Mose aliokuwa amewapa mashariki mwa Yordani, sawasawa na mtumishi wa Bwana alivyowagawia. 9 13:9Eneo lao lilienea toka Aroeri, iliyoko ukingoni mwa Bonde la Arnoni kuanzia mji ulio katikati ya bonde, likijumlisha nchi ya uwanda wa juu wote wa Medeba mpaka Diboni, 10 13:10nayo miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, hadi mpakani mwa Waamoni. 11 13:11Vilevile ilijumlisha Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaaka, mlima wote wa Hermoni na Bashani yote ikienea hadi Saleka: 12 13:12yaani ufalme wote wa Ogu katika Bashani, aliyekuwa ametawala katika Ashtarothi na Edrei, na ndiye pekee alisalia kwa Warefai. Mose alikuwa amewashinda na kuteka nchi yao. 13 13:13Lakini Waisraeli hawakuwafukuza watu wa Geshuri na wa Maaka, kwa hiyo wanaendelea kuishi miongoni mwa Waisraeli mpaka leo hii.

14 13:14Lakini kwa kabila la Lawi, Mose hakupeana urithi, kwa kuwa sadaka za kuteketezwa kwa moto zilizotolewa kwa Bwana, Mungu wa Israeli, ndizo zilizokuwa urithi wao, kama alivyowaahidi.

15 13:15Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa kabila la Reubeni ukoo kwa ukoo: 16 13:16Eneo la Aroeri lililo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, na kuanzia mji ulio katikati ya bonde, pia uwanda wote wa juu kupita Medeba 17 13:17hadi Heshboni na miji yake yote kwenye uwanda wa juu, ikijumlishwa miji ya Diboni, Bamoth-Baali, Beth-Baal-Meoni, 18 13:18Yahasa, Kedemothi, Mefaathi, 19 13:19Kiriathaimu, Sibma, Sereth-Shahari juu ya kilima kilicho katika bonde, 20 13:20Beth-Peori, materemko ya Pisga na Beth-Yeshimothi: 21 13:21miji yote ya uwanda wa juu na eneo lote la utawala wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni. Mose alikuwa amemshinda Sihoni, pia watawala wakuu wa Wamidiani, ambao ni Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, waliokuwa wameungana na Sihoni, ambao waliishi katika nchi ile. 22 13:22Pamoja na wale waliouawa katika vita, Waisraeli walikuwa wamemuua kwa upanga Balaamu mwana wa Beori aliyekuwa mchawi. 23 13:23Mpaka wa Wareubeni ulikuwa ni ukingo wa Mto Yordani. Miji hii na vijiji vyake ndiyo iliyokuwa urithi wa Wareubeni ukoo kwa ukoo. 24 13:24Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa kabila la Gadi, ukoo kwa ukoo: 25 13:25Nchi ya Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Amoni iliyoenea hadi Aroeri, karibu na Raba; 26 13:26na kuanzia Heshboni mpaka Ramath-Mispa na Betonimu, na kutoka Mahanaimu hadi eneo la Debiri; 27 13:27na katika bonde, Beth-Haramu, Beth-Nimra, Sukothi na Safoni na sehemu iliyobaki ya eneo la utawala wa Sihoni mfalme wa Heshboni (upande wa mashariki mwa Mto Yordani, eneo inayoishia kwenye Bahari ya Kinerethi 13:27 Yaani Bahari ya Galilaya.). 28 13:28Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Gadi ukoo kwa ukoo. 29 13:29Haya ndiyo maeneo ambayo Mose alikuwa amewapa hiyo nusu ya kabila la Manase, yaani kwa nusu ya jamaa ya uzao wa Manase, ukoo kwa ukoo: 30 13:30Eneo lililoenea kuanzia Mahanaimu, na kujumlisha Bashani yote, ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, makazi yote ya Yairi huko Bashani, miji sitini, 31 13:31nusu ya Gileadi, na Ashtarothi na Edrei (miji ya kifalme ya Ogu katika Bashani). Hii ilikuwa kwa ajili ya wazao wa Makiri mwana wa Manase, kwa ajili ya nusu ya wana wa Makiri, ukoo kwa ukoo.

32 13:32Huu ndio urithi alioupeana Mose wakati alipokuwa katika tambarare za Moabu, ngʼambo ya Yordani mashariki mwa Yeriko. 33 13:33Lakini kwa kabila la Walawi, Mose hakuwapa urithi; Bwana Mungu, Mungu wa Israeli ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.

14Mgawanyo Wa Nchi Magharibi Mwa Yordani

1 14:1Basi haya ndiyo maeneo Waisraeli waliyopokea kama urithi katika nchi ya Kanaani, ambayo kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni na viongozi wa koo za kabila za Israeli waliwagawia. 2 14:2Urithi wao uligawanywa kwa kura kwa yale makabila tisa na nusu, kama Bwana alivyoamuru Mose. 3 14:3Mose alikuwa amewapa yale makabila mawili na nusu urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, lakini Walawi hawakupewa urithi miongoni mwa hao wengine, 4 14:4kwa kuwa wana wa Yosefu walikuwa makabila mawili; Manase na Efraimu. Walawi hawakupata mgawo wa ardhi, bali walipewa miji tu kwa ajili ya kuishi, pamoja na maeneo ya malisho kwa ajili ya makundi yao ya kondoo, mbuzi na ngʼombe wao. 5 14:5Kwa hiyo Waisraeli wakagawana ile nchi, kama vile Bwana alivyomwagiza Mose.

Kalebu Anapewa Mji Wa Hebroni

6 14:6Kisha watu wa Yuda wakamwendea Yoshua huko Gilgali, naye Kalebu mwana wa Yefune yule Mkenizi, akamwambia, “Unajua jambo ambalo Bwana alimwambia Mose mtu wa Mungu huko Kadesh-Barnea kukuhusu wewe na mimi. 7 14:7Nilikuwa na umri wa miaka arobaini, wakati Mose mtumishi wa Bwana, aliponituma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza hiyo nchi. Nami nikamletea taarifa kama kulingana na nilivyosadiki moyoni. 8 14:8Lakini ndugu zangu tuliopanda nao waliifanya mioyo ya watu iyeyuke kwa hofu. Bali mimi, nilimfuata Bwana Mungu wangu kwa moyo wote. 9 14:9Hivyo katika siku ile, Mose akaniapia, ‘Nchi ambayo umeikanyaga kwa miguu yako itakuwa urithi wako na wa watoto wako milele, kwa sababu umemfuata Bwana Mungu wangu kwa moyo wote.’

10 14:10“Sasa basi, kama vile Bwana alivyoahidi, ameniweka hai kwa miaka arobaini na mitano tangu wakati alipomwambia Mose jambo hili, wakati Waisraeli wakiwa wanazunguka jangwani. Hivyo mimi hapa leo, nina umri wa miaka themanini na mitano! 11 14:11Bado ninazo nguvu kama siku ile Mose aliponituma. Bado ninazo nguvu za kwenda vitani sasa kama vile nilivyokuwa wakati ule. 12 14:12Basi nipe nchi hii ya vilima, ambayo Bwana aliniahidi siku ile. Wewe mwenyewe ulisikia wakati ule kwamba Waanaki walikuwako huko na miji yao ilikuwa mikubwa na yenye maboma, lakini, kwa msaada wa Bwana, nitawafukuza watoke huko kama vile alivyonena.”

13 14:13Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune, na akampa Hebroni kama urithi wake. 14 14:14Hivyo Hebroni imekuwa mali ya Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi tangu wakati ule, kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa moyo wote. 15 14:15(Hebroni uliitwa Kiriath-Arba hapo mwanzo, kutokana na huyo Arba ambaye alikuwa mtu mkuu kupita wote miongoni mwa Waanaki.)

Kisha nchi ikawa na amani bila vita.

15Mgawo Kwa Yuda

1 15:1Mgawo kwa kabila la Yuda, ulienea ukoo kwa ukoo, ukishuka kufikia eneo la Edomu, hadi Jangwa la Sini mwisho kabisa upande wa kusini.

2 15:2Mpaka wao wa kusini ulianzia kwenye ghuba iliyoko kwenye ncha ya kusini mwa Bahari ya Chumvi, 3 15:3ukakatiza kusini mwa Akrabimu, ukaendelea hadi Sini ukaenda hadi kusini mwa Kadesh-Barnea. Tena ukapitia Hesroni ukapanda hadi Adari na ukapinda hadi Karka. 4 15:4Kisha ukaendelea mpaka Azmoni na kuunganika na Kijito cha Misri, na kuishia baharini. Huu ndio mpaka wao wa upande wa kusini. 5 15:5Mpaka wa upande wa mashariki ni Bahari ya Chumvi ukienea mahali Mto Yordani unapoingilia. Mpaka wa upande wa kaskazini ulianzia penye ghuba ya bahari mahali Mto Yordani unapoingilia, 6 15:6ukapanda hadi Beth-Hogla, na kuendelea kaskazini mwa Beth-Araba hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. 7 15:7Kisha mpaka ulipanda hadi Debiri kutoka Bonde la Akori na kugeuka kaskazini hadi Gilgali inayotazamana na materemko ya Adumimu, kusini mwa bonde. Ukaendelea sambamba hadi maji ya En-Shemeshi na kutokeza huko En-Rogeli. 8 15:8Kisha ukapanda kwa kufuata Bonde la Ben-Hinomu sambamba na mteremko wa kusini wa mji mkubwa wa Wayebusi (yaani Yerusalemu). Kutoka hapo ukapanda juu ya kilima magharibi ya Bonde la Hinomu mwisho wa ncha ya kaskazini mwa Bonde la Warefai. 9 15:9Kutoka juu ya kilima mpaka ule ukaendelea hadi kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa, ukatokea kwenye miji ya Mlima Efroni na kuteremka kuelekea Baala (yaani Kiriath-Yearimu). 10 15:10Kisha ukapinda upande wa magharibi kutoka Baala hadi Mlima Seiri, ukafuatia sambamba mteremko wa kaskazini mwa Mlima Yearimu (yaani Kesaloni), ukaendelea chini hadi Beth-Shemeshi na kukatiza hadi Timna. 11 15:11Ukaelekea hadi kwenye mteremko wa kaskazini mwa Ekroni, ukageuka kuelekea Shikeroni, ukapita hadi Mlima Baala na kufika Yabineeli. Mpaka ule ukaishia baharini. 12 15:12Mpaka wa magharibi ni pwani ya Bahari Kuu.

Hii ndiyo mipaka ya watu wa Yuda kwa koo zao.

Nchi Aliyopewa Kalebu (Waamuzi 1:11-15)

13 15:13Kwa kufuata maagizo ya Bwana kwake, Yoshua alimpa Kalebu mwana wa Yefune sehemu katika Yuda: Kiriath-Arba, yaani Hebroni (Arba alikuwa baba wa zamani wa Anaki). 14 15:14Kutoka Hebroni Kalebu alifukuza hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, Ahimani na Talmai, wazao wa Anaki. 15 15:15Kutoka hapo akaondoka kupigana dhidi ya watu walioishi Debiri (jina la Debiri hapo kwanza uliitwa Kiriath-Seferi). 16 15:16Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.” 17 15:17Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu yake Kalebu, akauteka; hivyo Kalebu akamtoa Aksa binti yake aolewe naye.

18 15:18Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka juu ya punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?”

19 15:19Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Basi Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.

Miji Ya Yuda

20 15:20Huu ndio urithi wa kabila la Yuda, ukoo kwa ukoo:

21 15:21Miji ya kusini kabisa ya kabila la Yuda katika Negebu kuelekea mpaka wa Edomu ilikuwa: Kabseeli, Ederi, Yaguri, 22 15:22Kina, Dimona, Adada, 23 15:23Kedeshi, Hazori, Ithnani, 24 15:24Zifu, Telemu, Bealothi, 25 15:25Hazor-Hadata, Kerioth-Hezroni (yaani Hazori), 26 15:26Amamu, Shema, Molada, 27 15:27Hasar-Gada, Heshmoni, Beth-Peleti, 28 15:28Hasar-Shuali, Beer-Sheba, Biziothia, 29 15:29Baala, Iyimu, Esemu, 30 15:30Eltoladi, Kesili, Horma, 31 15:31Siklagi, Madmana, Sansana, 32 15:32Lebaothi, Shilhimu, Aini na Rimoni; hiyo yote ni miji ishirini na tisa, pamoja na vijiji vyake. 33 15:33Kwenye shefela ya magharibi: Eshtaoli, Sora, Ashna, 34 15:34Zanoa, En-Ganimu, Tapua, Enamu, 35 15:35Yarmuthi, Adulamu, Soko, Azeka, 36 15:36Shaaraimu, Adithaimu na Gedera (au Gederothaimu); yote ni miji kumi na minne, pamoja na vijiji vyake. 37 15:37Senani, Hadasha, Migdal-Gadi, 38 15:38Dileani, Mispa, Yoktheeli, 39 15:39Lakishi, Boskathi, Egloni, 40 15:40Kaboni, Lamasi, Kitlishi, 41 15:41Gederothi, Beth-Dagoni, Naama na Makeda; yote ni miji kumi na sita pamoja na vijiji vyake. 42 15:42Libna, Etheri, Ashani, 43 15:43Yifta, Ashna, Nesibu, 44 15:44Keila, Akzibu na Maresha; yote ni miji tisa pamoja na vijiji vyake. 45 15:45Ekroni, pamoja na viunga vyake na vijiji vyake; 46 15:46magharibi ya Ekroni, maeneo yote yaliyokuwa karibu na Ashdodi, pamoja na vijiji vyake; 47 15:47Ashdodi, miji yake na vijiji vyake na Gaza viunga vyake na vijiji vyake, hadi kufikia Kijito cha Misri na Pwani ya Bahari Kuu. 48 15:48Katika nchi ya vilima: Shamiri, Yatiri, Soko, 49 15:49Dana, Kiriath-Sana (yaani Debiri), 50 15:50Anabu, Eshtemoa, Animu, 51 15:51Gosheni, Holoni na Gilo; miji kumi na mmoja pamoja na vijiji vyake. 52 15:52Arabu, Duma, Ashani, 53 15:53Yanimu, Beth-Tapua, Afeka, 54 15:54Humta, Kiriath-Arba (yaani Hebroni), na Siori; miji tisa pamoja na vijiji vyake. 55 15:55Maoni, Karmeli, Zifu, Yuta, 56 15:56Yezreeli, Yokdeamu, Zanoa, 57 15:57Kaini, Gibea na Timna; miji kumi pamoja na vijiji vyake. 58 15:58Halhuli, Beth-Suri, Gedori, 59 15:59Maarathi, Beth-Anothi na Eltekoni; miji sita pamoja na vijiji vyake. 60 15:60Kiriath-Baali (yaani Kiriath-Yearimu) na Raba; miji miwili pamoja na vijiji vyake. 61 15:61Huko jangwani: Beth-Araba, Midini, Sekaka, 62 15:62Nibshani, Mji wa Chumvi, na En-Gedi; miji sita pamoja na vijiji vyake.

63 15:63Yuda hakuweza kuwafukuza Wayebusi, waliokuwa wakiishi Yerusalemu; hadi leo Wayebusi huishi huko pamoja na watu wa Yuda.

16Mgawo Kwa Efraimu Na Manase 1 16:1Mgawanyo wa Yosefu ulianzia Yordani ya Yeriko, mashariki mwa miji ya Yeriko na kutoka hapo ulipanda kupitia jangwani na kuingia katika nchi ya vilima ya Betheli. 2 16:2Ukaendelea kutoka Betheli (ndiyo Luzu), ukavuka kuingia eneo la Waariki huko Atarothi, 3 16:3ukateremkia kuelekea magharibi hadi eneo la Wayafleti ukienea hadi eneo la Beth-Horoni ya Chini hadi Gezeri, ukiishia baharini. 4 16:4Kwa hiyo Manase na Efraimu, wazao wa Yosefu, walipokea urithi wao. 5 16:5Hili ndilo lilikuwa eneo la Efraimu, ukoo kwa ukoo: Mpaka wa urithi wao ulianzia Ataroth-Adari upande wa mashariki hadi Beth-Horoni ya Juu, 6 16:6na kuendelea mpaka baharini. Kutoka Mikmeta upande wa kaskazini ulipinda kuelekea mashariki hadi Taanath-Shilo, ukiupita hadi Yanoa upande wa mashariki. 7 16:7Kisha uliteremka kutoka Yanoa hadi Atarothi na Naara, ukagusa Yeriko na kutokea katika Mto Yordani. 8 16:8Kutoka Tapua mpaka ulikwenda magharibi hadi Bonde la Kana na kuishia baharini. Huu ulikuwa ndio urithi wa kabila la Waefraimu, ukoo kwa ukoo. 9 16:9Pia ulijumuisha miji yote na vijiji vyake ambavyo vilitengwa kwa ajili ya Waefraimu ndani ya urithi wa kabila la Manase. 10 16:10Hawakuwatoa Wakanaani waishio Gezeri; mpaka leo Wakanaani wanaishi miongoni mwa watu wa Efraimu lakini wanatakiwa kufanya kazi ngumu za kulazimishwa. 17Mgawo Wa Nusu Nyingine Ya Manase Upande Wa Magharibi

1 17:1Huu ndio mgawo wa kabila la Manase kama mzaliwa wa kwanza wa Yosefu, yaani kwa ajili ya Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase. Makiri alikuwa baba wa Wagileadi, ambao walipokea Gileadi na Bashani kwa sababu Wamakiri walikuwa askari wakuu. 2 17:2Kwa hiyo mgawo huu ulikuwa kwa ajili ya watu wa Manase waliokuwa wamebaki, ambao ni koo za Abiezeri, Heleki, Asirieli, Shekemu, Heferi na Shemida. Hawa ndio wanaume wale wengine wa uzao wa Manase mwana wa Yosefu kwa koo zao.

3 17:3Basi Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase hakuwa na wana waume ila mabinti tu, ambao majina yao yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. 4 17:4Wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi, wakasema: “Bwana alimwagiza Mose atupatie urithi miongoni mwa ndugu zetu.” Kwa hiyo Yoshua akawapa urithi pamoja na ndugu wa baba yao, kufuatana na agizo la Bwana. 5 17:5Fungu la Manase lilikuwa na sehemu kumi za nchi, licha ya Gileadi na Bashani mashariki mwa Yordani, 6 17:6kwa sababu wale binti za kabila la Manase walipokea urithi miongoni mwa wana wa kiume. Nchi ya Gileadi ilikuwa mali ya wazao wa Manase waliobaki.

7 17:7Eneo la Manase lilienea kuanzia Asheri hadi Mikmeta mashariki mwa Shekemu. Mpaka ule ulielekea upande wa kusini kutoka pale kujumuisha watu walioishi En-Tapua. 8 17:8(Nchi ya Tapua ilikuwa mali ya Manase, lakini Tapua yenyewe iliyo mpakani mwa nchi ya Manase ilikuwa ya Waefraimu.) 9 17:9Kisha mpaka ule uliendelea kuelekea kusini hadi Bonde la Kana. Kulikuwepo miji ya Efraimu iliyokuwa miongoni mwa miji ya Manase, lakini mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa lile bonde na kuishia kwenye bahari. 10 17:10Nchi ya kusini ilikuwa ya Efraimu, na ile iliyokuwa upande wa kaskazini ilikuwa ya Manase. Eneo la Manase lilifika bahari na ikapakana na Asheri upande wa kaskazini, na Isakari upande wa mashariki. 11 17:11Katika Isakari na Asheri Manase alikuwa na miji pia: Beth-Shani, Ibleamu na watu wa Dori, 17:11 Ndiyo Nafoth-Dori. Endori, Taanaki na Megido, pamoja na vijiji vyote vinavyohusika na miji hiyo (ya tatu katika orodha ni Nafothi). 12 17:12Lakini Wamanase hawakuweza kuimiliki miji hii, kwa kuwa Wakanaani walikazana kuishi katika maeneo hayo. 13 17:13Hata hivyo, Waisraeli walivyoendelea kupata nguvu waliwatumikisha Wakanaani na kuwatia katika kazi za kulazimishwa, lakini hawakuwafukuza kabisa. Kabila La Yosefu Lakataa

14 17:14Watu wa Yosefu wakamwambia Yoshua, “Kwa nini umetupa sisi mgawo mmoja tu na sehemu moja tu kuwa urithi? Sisi tu watu wengi sana, na Bwana ametubariki kwa wingi.”

15 17:15Yoshua akajibu, “Kama ninyi ni wengi sana, na kama nchi ya vilima ya Efraimu ni ndogo sana kwenu, pandeni msituni mkafyeke eneo kwa ajili yenu wenyewe huko kwenye nchi ya Waperizi na Warefai.”

16 17:16Watu wa Yosefu wakajibu, “Hiyo nchi ya vilima haitutoshi, nao Wakanaani wote wanaoishi katika tambarare wanayo magari ya vita ya chuma, wote wa Beth-Shani na miji yake, na wale walio katika Bonde la Yezreeli.”

17 17:17Lakini Yoshua akanena na nyumba ya Yosefu, yaani Efraimu na Manase: “Ninyi ni wengi sana na wenye nguvu sana. Hamtakuwa na mgawo mmoja tu, 18 17:18bali pia nchi hii ya kilima yenye msitu. Ifyekeni, nayo mipaka yake itakuwa yenu umbali mtakaoweza kufika. Ingawa Wakanaani wana magari ya chuma, nao wana nguvu, mwaweza kuwafukuza humo.”

18Mgawanyo Wa Nchi Iliyobaki

1 18:1Kusanyiko lote la Waisraeli likakusanyika huko Shilo na kusimamisha Hema la Kukutania. Nchi ikawa chini ya utawala wao, 2 18:2lakini palikuwa bado makabila saba ya Israeli ambayo yalikuwa hayajapokea urithi wao.

3 18:3Hivyo Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtasubiri hata lini ili kuingia kumiliki nchi ambayo Bwana, Mungu wa baba zenu, amewapa? 4 18:4Chagueni watu watatu kutoka kwenye kila kabila. Nitawatuma hao watu kukagua hiyo nchi na kuniandikia mapendekezo ya mgawanyo wa urithi wa kila kabila. Nao watanirudia. 5 18:5Mtaigawanya hiyo nchi katika sehemu saba. Yuda atabaki katika eneo lake upande wa kusini na nyumba ya Yosefu katika nchi yake upande wa kaskazini. 6 18:6Baada ya kuandika maelezo ya hizo sehemu saba za nchi, yaleteni kwangu, nami nitawapigia kura kwa kura mbele za Bwana Mungu wetu. 7 18:7Hata hivyo, Walawi hawatakuwa na sehemu miongoni mwenu, kwa maana huduma ya ukuhani kwa Bwana ndio urithi wao. Nao Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase wameshapata urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, ambako Mose mtumishi wa Bwana aliwapa.”

8 18:8Watu hao walipokuwa wanaondoka kwenda kuandika vizuri kuhusu hiyo nchi, Yoshua akawaagiza, “Nendeni mkakague hiyo nchi na mwandike maelezo kuihusu. Kisha mrudi kwangu, nami nitawapigia kura hapa Shilo mbele za Bwana.” 9 18:9Ndipo hao watu walipoondoka na kupita katika ile nchi. Wakaandika maelezo yake kwenye kitabu, mji kwa mji, katika sehemu saba na kurudisha taarifa kwa Yoshua huko kambini Shilo. 10 18:10Basi Yoshua akawapigia kura huko Shilo mbele za Bwana, na hapo akagawanya ile nchi kwa Waisraeli kufuatana na mgawanyo wa kabila zao.

Mgawo Kwa Benyamini 11 18:11Kura iliangukia kabila la Benyamini, ukoo kwa ukoo. Eneo lao walilogawiwa lilikuwa kati ya kabila la Yuda na la Yosefu. 12 18:12Upande wa kaskazini mpaka wao ulianzia pale Yordani, kupitia kaskazini ya mteremko wa Yeriko na kuendelea magharibi kuingia katika nchi ya vilima, ukitokea kwenye jangwa la Beth-Aveni. 13 18:13Kutoka hapo ulikatiza kwenye mteremko wa kusini mwa Luzu (yaani Betheli) na kushuka hadi Ataroth-Adari katika kilima kusini mwa Beth-Horoni ya Chini. 14 18:14Kutoka kilima kinachotazamana na Beth-Horoni upande wa kusini mpaka ule ukazunguka kusini kufuatia upande wa magharibi, na ukatokezea Kiriath-Baali (yaani Kiriath-Yearimu), mji wa watu wa Yuda. Huu ndio uliokuwa upande wa magharibi. 15 18:15Upande wa kusini mpaka ulianzia kwenye viunga vya Kiriath-Yearimu kwa upande wa magharibi, nao ukatokeza kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa. 16 18:16Mpaka ukateremka hadi shefela inayotazamana na Bonde la Ben-Hinomu, kaskazini mwa Bonde la Refaimu. Ukaendelea chini kwenye Bonde la Hinomu sambamba na mteremko wa kusini mwa mji mkubwa wa Wayebusi na kisha hadi En-Rogeli. 17 18:17Kisha ukapinda kuelekea kaskazini, ukaenda hadi En-Shemeshi na kuendelea mpaka Gelilothi, inayotazamana na Njia ya Adumimu, ukateremka hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. 18 18:18Ukaendelea upande wa mteremko wa kaskazini wa Beth-Araba ukateremka hadi Araba. 19 18:19Kisha ukaenda mpaka kwenye mteremko wa kaskazini wa Beth-Hogla na kujitokeza kwenye ghuba ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi, kwenye maingilio ya Yordani upande wa kusini. Huo ulikuwa mpaka wa kusini. 20 18:20Nayo Yordani ikawa ndio mpaka wa upande wa mashariki. Hii ilikuwa ndiyo mipaka iliyoonyesha urithi wa koo za Benyamini pande zote. 21 18:21Kabila ya Benyamini, ukoo kwa ukoo, ilikuwa na miji mikubwa ifuatayo: Yeriko, Beth-Hogla, Emeki-Kesisi, 22 18:22Beth-Araba, Semaraimu, Betheli, 23 18:23Avimu, Para na Ofra, 24 18:24Kefar-Amoni, Ofni, na Geba; miji kumi na miwili pamoja na vijiji vyake. 25 18:25Gibeoni, Rama na Beerothi, 26 18:26Mispa, Kefira, Moza, 27 18:27Rekemu, Irpeeli, Tarala, 28 18:28Zela, Elefu, mji wa Wayebusi (yaani Yerusalemu), Gibea na Kiriathi; miji kumi na minne pamoja na vijiji vyake. Huu ndio uliokuwa urithi wa Benyamini kwa ajili ya koo zake. 19Mgawo Kwa Simeoni

1 19:1Kura ya pili ikaangukia kabila la Simeoni, ukoo kwa ukoo. Urithi wao ulikuwa ndani ya eneo la Yuda. 2 19:2Ulijumuisha:

Beer-Sheba (au Sheba), Molada, 3 19:3Hasar-Shuali, Bala, Esemu, 4 19:4Eltoladi, Bethuli, Horma, 5 19:5Siklagi, Beth-Markabothi, Hasar-Susa, 6 19:6Beth-Lebaothi na Sharuheni; hii ilikuwa miji kumi na mitatu pamoja na vijiji vyake. 7 19:7Pia Aini, Rimoni, Etheri, na Ashani; hii ilikuwa miji minne na vijiji vyake, 8 19:8pamoja na vijiji vyote vinavyoizunguka miji hii mpaka Baalath-Beeri (ambayo ndiyo Rama iliyo katika Negebu). Huu ulikuwa ni urithi wa kabila la Simeoni ukoo kwa ukoo. 9 19:9Urithi wa Wasimeoni ulitolewa kutoka fungu la Yuda, kwa kuwa fungu la Yuda lilikuwa kubwa kuliko walivyohitaji. Hivyo kabila la Simeoni lilipewa urithi wao ndani ya eneo la Yuda. Mgawo Kwa Zabuloni 10 19:10Kura ya tatu ikaangukia kabila la Zabuloni, ukoo kwa ukoo: Mpaka wa urithi wao uliendelea hadi Saridi. 11 19:11Kuelekea upande wa magharibi ukafika Marala, ukagusa Dabeshethi, na kuendelea mpaka kwenye bonde karibu na Yokneamu. 12 19:12Ukageuka mashariki, kuanzia Saridi kuelekea mawio ya jua hadi kwenye nchi ya Kisiloth-Tabori, na kwenda hadi Daberathi, kupanda Yafia. 13 19:13Kisha ukaendelea mashariki hadi Gath-Heferi na kufika Eth-Kasini, ukatokea Rimoni na kugeuka kuelekea Nea. 14 19:14Huko mpaka ukazungukia upande wa kaskazini hadi Hanathoni na kuishia katika Bonde la Ifta-Eli. 15 19:15Miji mingine iliyojumuishwa ni Katathi, Nahalali, Shimroni, Idala na Bethlehemu. Kulikuwa na miji kumi na miwili pamoja na vijiji vyake. 16 19:16Miji hii na vijiji vyake ilikuwa ndio urithi wa Zabuloni, ukoo kwa ukoo. Mgawo Kwa Isakari 17 19:17Kura ya nne ikamwangukia Isakari, ukoo kwa ukoo. 18 19:18Eneo lao lilijumuisha: Yezreeli, Kesulothi, Shunemu, 19 19:19Hafaraimu, Shioni, Anaharathi, 20 19:20Rabithi, Kishioni, Ebesi, 21 19:21Remethi, En-Ganimu, En-Hada na Beth-Pasesi. 22 19:22Mpaka ule ukagusa Tabori, Shahasuma na Beth-Shemeshi, na ukaishia kwenye Yordani. Ilikuwa miji kumi na sita, pamoja na vijiji vyake. 23 19:23Miji hii pamoja na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Isakari, ukoo kwa ukoo. Mgawo Kwa Asheri 24 19:24Kura ya tano ikaangukia kabila la Asheri, ukoo kwa ukoo. 25 19:25Eneo lao lilijumuisha: Helkathi, Hali, Beteni, Akishafu, 26 19:26Alameleki, Amadi na Mishali. Upande wa magharibi mpaka uligusa Karmeli na Shihor-Libnathi. 27 19:27Tena ukageuka mashariki kuelekea Beth-Dagoni, ukagusa Zabuloni na Bonde la Ifta-Eli, ukaenda upande wa kaskazini hadi Beth-Emeki na Neyeli, ukipitia Kabul upande wa kushoto. 28 19:28Ukaendelea hadi Abdoni, Rehobu, Hamoni na Kana, na kufika Sidoni Kuu. 29 19:29Mpaka huo ukageukia nyuma kuelekea Rama na kwenda hadi kwenye mji wenye ngome wa Tiro, ukageuka kuelekea Hosa na kutokeza baharini katika eneo la Akzibu, 30 19:30Uma, Afeki na Rehobu. Ilikuwepo miji ishirini na miwili, pamoja na vijiji vyake. 31 19:31Miji hii pamoja na vijiji vyake ilikuwa ndio urithi wa kabila la Asheri, ukoo kwa ukoo. Mgawo Kwa Naftali 32 19:32Kura ya sita ikaangukia kabila la Naftali, ukoo kwa ukoo: 33 19:33Mpaka wao uliendelea kutoka Helefi na kwenye mti mkubwa ulio katika Saananimu, ukipitia Adami-Nekebu na Yabineeli hadi Lakumu, na kuishia katika Mto Yordani. 34 19:34Mpaka ukaendelea magharibi kupitia Aznoth-Tabori na kutokea Hukoki. Ukagusa Zabuloni upande wa kusini, Asheri upande wa magharibi, na Yordani upande wa mashariki. 35 19:35Miji yenye ngome ilikuwa Sidimu, Seri, Hamathi, Rakathi, Kinerethi, 36 19:36Adama, Rama, Hazori, 37 19:37Kedeshi, Edrei, na En-Hasori, 38 19:38Ironi, Migdal-Eli, Horemu, Beth-Anathi na Beth-Shemeshi. Kulikuwa na miji kumi na tisa na vijiji vyake. 39 19:39Miji hiyo pamoja na vijiji vyake ndio iliyokuwa urithi wa kabila la Naftali, ukoo kwa ukoo. Mgawo Kwa Dani 40 19:40Kura ya saba ikaangukia kabila la Dani, ukoo kwa ukoo. 41 19:41Eneo la urithi wao lilijumuisha: Sora, Eshtaoli, Iri-Shemeshi, 42 19:42Shaalabini, Aiyaloni, Ithla, 43 19:43Eloni, Timna, Ekroni, 44 19:44Elteke, Gibethoni, Baalathi, 45 19:45Yehudi, Bene-Beraki, Gath-Rimoni, 46 19:46Me-Yarkoni na Rakoni, pamoja na eneo linalotazamana na Yafa.

47 19:47(Lakini Wadani walipata shida kulimiliki eneo lao; kwa hiyo walipanda kuishambulia Leshemu, wakaitwaa, wakawaua watu wake kwa upanga na kuukalia. Walikaa Leshemu na kuuita Dani kufuatana na jina la baba yao.)

48 19:48Miji hii na vijiji vyake ndio iliyokuwa urithi wa kabila la Dani, ukoo kwa ukoo. Mgawo Kwa Yoshua

49 19:49Walipomaliza kugawanya nchi katika migawo kulingana na sehemu zao zilizowaangukia, Waisraeli wakampa Yoshua mwana wa Nuni urithi katikati yao, 50 19:50kama vile Bwana alivyokuwa ameamuru. Walimpa mji alioutaka, ambao ni Timnath-Sera 19:50 Unajulikana pia kama Timnath-Heresi, ona Yos 24:30; Amu 2:9. ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu. Naye akajenga mji, akakaa huko.

51 19:51Haya ndiyo maeneo ambayo kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa koo za kabila za Israeli waliyoyagawanya kwa kura huko Shilo mbele za Bwana penye ingilio la Hema la Kukutania. Hivyo wakamaliza kuigawanya nchi.

20Miji Ya Makimbilio (Hesabu 35:9-34)

1 20:1Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, 2 20:2“Waambie Waisraeli, watenge miji mikubwa ya kukimbilia, kama nilivyokuagiza kupitia Mose, 3 20:3ili mtu yeyote atakayemuua mtu kwa bahati mbaya na pasipo kukusudia aweze kukimbilia huko na kujiepusha na mlipiza kisasi wa damu.

4 20:4“Anapokimbilia mojawapo ya hii miji mikubwa atasimama kwenye maingilio ya lango la mji mkuu na kueleza wazee wa mji kuhusu shauri lake. Kisha watampokea katika mji wao na kumpa mahali pa kuishi nao. 5 20:5Kama mlipiza kisasi wa damu akimfuatilia, wasimkabidhi yule mshtakiwa, kwa sababu alimuua jirani yake bila kukusudia, na bila kuwa na nia ya kudhuru. 6 20:6Huyu aliyeua atakaa kwenye mji mkubwa huo mpaka awe amesimama kukabili mashtaka yake mbele ya kusanyiko na mpaka kuhani mkuu anayehudumu kwa wakati huo atakapokufa. Ndipo atakapoweza kurudi nyumbani kwake katika mji ambao aliukimbia.”

7 20:7Basi wakatenga Kedeshi katika Galilaya kwenye nchi ya vilima ya Naftali, Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-Arba (yaani Hebroni) kwenye nchi ya vilima ya Yuda. 8 20:8Katika upande wa mashariki mwa Yordani ya Yeriko wakatenga Bezeri katika jangwa katika uwanda wa juu katika kabila la Reubeni, Ramothi katika Gileadi katika kabila la Gadi, na Golani huko Bashani katika kabila la Manase. 9 20:9Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote aishiye miongoni mwao aliyemuua mtu kwa bahati mbaya, angeweza kukimbilia katika miji mikubwa hiyo iliyotengwa na asiuawe na mlipiza kisasi wa damu kabla hajasimama kukabili mashtaka mbele ya kusanyiko.

21Miji Kwa Walawi

1 21:1Basi viongozi wa jamaa ya Walawi, wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa nyingine za makabila ya Israeli 2 21:2huko Shilo katika Kanaani na kuwaambia, “Bwana aliamuru kupitia Mose kuwa mtupe miji ya kuishi yenye sehemu za malisho kwa mifugo yetu.” 3 21:3Hivyo kama vile Bwana alivyoamuru, Waisraeli wakawapa Walawi miji ifuatayo pamoja na sehemu zake za malisho kutoka urithi wao wenyewe.

4 21:4Kura ya kwanza ikaangukia Wakohathi, ukoo kwa ukoo. Walawi waliokuwa wazao wa kuhani Aroni walipewa miji kumi na mitatu kutoka makabila ya Yuda, Simeoni na Benyamini. 5 21:5Wazao wengine waliobaki wa Wakohathi walipewa miji kumi kutoka koo za makabila ya Efraimu, Dani na nusu ya Manase.

6 21:6Wazao wa Gershoni walipewa miji kumi na mitatu kutoka koo za makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na nusu ya Manase huko Bashani.

7 21:7Wazao wa Merari, ukoo kwa ukoo, walipewa miji kumi na miwili kutoka makabila ya Reubeni, Gadi na Zabuloni.

8 21:8Kwa hiyo Waisraeli wakawapa Walawi miji hii pamoja na sehemu zake za malisho, kama vile Bwana alivyokuwa ameamuru kupitia kwa Mose.

9 21:9Kutoka makabila ya Yuda na Simeoni waligawa miji ifuatayo kwa majina 10 21:10(miji hii walipewa wazao wa Aroni ambao walitokana na koo za Wakohathi wa Walawi, kwa sababu kura ya kwanza iliwaangukia): 11 21:11Waliwapa Kiriath-Arba (yaani Hebroni), pamoja na sehemu zake za malisho zilizoizunguka, katika nchi ya vilima ya Yuda. (Arba alikuwa baba wa Anaki.) 12 21:12Lakini mashamba na vijiji vilivyozunguka mji mkubwa walikuwa wamempa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake. 13 21:13Kwa hiyo wazao wa kuhani Aroni wakapewa Hebroni (mji mkuu wa makimbilio kwa ajili ya yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji), Libna, 14 21:14Yatiri, Eshtemoa, 15 21:15Holoni, Debiri, 16 21:16Aini, Yuta na Beth-Shemeshi, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji tisa kutoka kwa makabila haya mawili. 17 21:17Kutoka kabila la Benyamini wakawapa Gibeoni, Geba, 18 21:18Anathothi na Almoni, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne. 19 21:19Miji yote waliyopewa makuhani, wazao wa Aroni, ilikuwa kumi na mitatu, pamoja na sehemu zake za malisho. 20 21:20Koo nyingine za Wakohathi, ambao pia ni Walawi, walipewa miji kutoka kabila la Efraimu: 21 21:21Katika nchi ya vilima ya Efraimu walipewa Shekemu (mji mkubwa wa makimbilio kwa yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji) na Gezeri, 22 21:22Kibsaimu na Beth-Horoni, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne. 23 21:23Pia kutoka kabila la Dani wakapokea Elteke, Gibethoni, 24 21:24Aiyaloni na Gath-Rimoni pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne 25 21:25Kutoka nusu ya kabila la Manase, wakapokea Taanaki na Gath-Rimoni pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji miwili. 26 21:26Miji yote hii kumi pamoja na sehemu zake za malisho ilipewa koo za Wakohathi zilizobaki. 27 21:27Koo za Walawi za Wagershoni walipewa: kutoka nusu ya kabila la Manase, Golani katika Bashani (mji mkuu wa makimbilio kwa yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji) na Beeshtera, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji miwili; 28 21:28kutoka kabila la Isakari walipewa, Kishioni, Daberathi, 29 21:29Yarmuthi na En-Ganimu, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne 30 21:30kutoka kabila la Asheri walipewa, Mishali, Abdoni, 31 21:31Helkathi na Rehobu, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne. 32 21:32Kutoka kabila la Naftali walipewa, Kedeshi katika Galilaya (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji), Hamoth-Dori na Kartani, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji mitano. 33 21:33Miji yote ya koo za Wagershoni ilikuwa kumi na mitatu, pamoja na sehemu zake za malisho. 34 21:34Koo za Wamerari (Walawi waliobaki) walipewa: kutoka kabila la Zabuloni, Yokneamu, Karta, 35 21:35Dimna na Nahalali, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne; 36 21:36kutoka kabila la Reubeni walipewa Bezeri, Yahasa, 37 21:37Kedemothi na Mefaathi, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne; 38 21:38kutoka kabila la Gadi walipewa, Ramothi katika Gileadi (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa ajili ya mauaji), Mahanaimu, 39 21:39Heshboni na Yazeri, pamoja na sehemu zake za malisho, ilikuwa miji minne. 40 21:40Miji yote waliyopewa koo za Wamerari, waliokuwa mabaki ya Walawi, ilikuwa ni kumi na miwili.

41 21:41Miji yote ya Walawi katika eneo lililoshikwa na Waisraeli lilikuwa arobaini na minane, pamoja na sehemu zake za malisho. 42 21:42Kila mmoja wa miji hii ulikuwa na sehemu ya malisho kuuzunguka; ndivyo ilivyokuwa kwa miji hii yote.

43 21:43Kwa hiyo Bwana akawapa Israeli nchi yote aliyokuwa ameapa kuwapa baba zao, nao wakaimiliki na kukaa humo. 44 21:44 Bwana akawapa pumziko kila upande, kama vile alivyokuwa amewaapia baba zao, hakuna hata mmoja wa adui zao aliyeweza kusimama mbele yao, Bwana akawatia adui zao wote mikononi mwao. 45 21:45Hakuna hata mojawapo ya ahadi nzuri ya Bwana kwa nyumba ya Israeli ambayo haikutimia; kila moja ilitimia.

22Makabila Ya Mashariki Yarudi Nyumbani

1 22:1Ndipo Yoshua akawaita Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, 2 22:2naye akawaambia, “Mmeshafanya yale yote Mose mtumishi wa Bwana aliyowaamuru, nanyi mmenitii kwa kila jambo nililowaamuru. 3 22:3Kwa muda mrefu sasa, hadi siku hii ya leo, hamkuwaacha ndugu zenu, bali ninyi mmetimiza ile kazi Bwana Mungu wenu aliyowapa. 4 22:4Sasa kwa kuwa Bwana Mungu wenu amewapa ndugu zenu pumziko kama alivyoahidi, rudini nyumbani mwenu katika nchi ile ambayo Mose mtumishi wa Bwana aliwapa ngʼambo ya Yordani. 5 22:5Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria zile Mose mtumishi wa Bwana alizowapa: yaani kumpenda Bwana Mungu wenu na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wenu wote na roho yenu yote.”

6 22:6Ndipo Yoshua akawabariki na kuwaaga waende zao, nao wakaenda nyumbani mwao. 7 22:7(Kwa nusu ya kabila la Manase Mose alikuwa amewapa eneo katika Bashani na ile nusu nyingine ya hilo kabila Yoshua aliwapa eneo upande wa magharibi ya Yordani pamoja na ndugu zao). Yoshua alipowaaga waende zao nyumbani, aliwabariki, 8 22:8akisema, “Rudini nyumbani mwenu na utajiri wenu mwingi, yaani makundi makubwa ya mifugo, mkiwa na fedha, dhahabu, shaba na chuma, pia wingi wa nguo, nanyi mkagawane na ndugu zenu hizo nyara zilizotoka kwa adui zenu.”

9 22:9Kwa hiyo Wareubeni, Wagadi na hiyo nusu ya kabila la Manase wakawaacha Waisraeli huko Shilo katika nchi ya Kanaani ili kurudi Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoipata sawasawa na agizo la Bwana kupitia Mose.

10 22:10Walipofika Gelilothi karibu na Yordani, katika nchi ya Kanaani, Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakajenga madhabahu ya fahari kubwa huko kando ya Yordani. 11 22:11Waisraeli wengine waliposikia kwamba Wareubeni, Wagadi na ile nusu ya kabila la Manase walikuwa wamejenga madhabahu kwenye mpaka wa Kanaani huko Gelilothi karibu na Yordani kwenye upande wa Israeli, 12 22:12kusanyiko lote la Israeli wakakusanyika huko Shilo ili wakapigane vita dhidi yao.

13 22:13Kwa hiyo Waisraeli wengine wakamtuma Finehasi mwana wa kuhani Eleazari katika nchi ya Gileadi, kwa Wareubeni, Wagadi na hiyo nusu ya kabila la Manase. 14 22:14Wakatuma pamoja naye watu kumi ambao ni viongozi, mmoja kwa kila kabila la Israeli, kila mmoja aliyekuwa kiongozi katika mgawanyiko wa jamaa miongoni mwa koo za Israeli.

15 22:15Walipofika Gileadi, kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, wakawaambia: 16 22:16“Kusanyiko lote la Bwana lasema: ‘Je, mmewezaje kuacha kumwamini Mungu wa Israeli jinsi hii? Mmewezaje kumwacha Bwana na kujijengea madhabahu dhidi yake na kumwasi? 17 22:17Je, dhambi ya Peori haikutosha? Hata ingawa kulikuja tauni juu ya kusanyiko la Bwana, mpaka leo hii hatujatakasika kutokana na dhambi hiyo! 18 22:18Je, sasa ndiyo mnamwacha Bwana?

“ ‘Kama mkimwasi Bwana leo, kesho atalikasirikia kusanyiko lote la Israeli. 19 22:19Kama nchi mnayomiliki imenajisika, vukeni mje katika nchi ya Bwana, mahali Maskani ya Bwana ilipo, nanyi mkajitwalie sehemu miongoni mwetu, lakini msije mkaasi dhidi ya Bwana wala dhidi yetu sisi kwa kujijengea madhabahu, zaidi ya madhabahu ya Bwana Mungu wetu. 20 22:20Wakati Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu kwa vitu vilivyowekwa wakfu, je, ghadhabu haikulipata kusanyiko lote la Israeli? Hakuwa yeye peke yake aliyekufa kwa ajili ya dhambi yake.’ ”

21 22:21Ndipo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walipowajibu viongozi wa koo za Israeli, wakisema: 22 22:22“Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana! Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana! Yeye anajua! Israeli na wajue! Kama huu umekuwa ni uasi au kukosa utii kwa Bwana, msituache hai siku hii ya leo. 23 22:23Kama tumejijengea madhabahu yetu wenyewe ili kumwacha Bwana na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, au kutoa sadaka za amani juu yake, Bwana mwenyewe na atupatilize leo.

24 22:24“Sivyo! Tulifanya hivyo kwa hofu kwamba siku zijazo wazao wenu wanaweza wakawaambia wazao wetu, ‘Mna uhusiano gani na Bwana, Mungu wa Israeli? 25 22:25 Bwana ameifanya Yordani kuwa mpaka kati yetu na ninyi, ninyi Wareubeni na Wagadi! Hamna fungu kwa Bwana.’ Kwa hiyo wazao wenu wanaweza wakawasababisha wazao wetu wakaacha kumcha Bwana.

26 22:26“Hii ndiyo sababu tulisema, ‘Tujiweke tayari na tujenge madhabahu, lakini si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa au dhabihu.’ 27 22:27Badala yake, itakuwa ni ushahidi kati yetu na ninyi na vizazi vijavyo, kwamba tutamwabudu Bwana katika mahali patakatifu pake pamoja na sadaka zetu za kuteketezwa, dhabihu na sadaka za amani. Ndipo katika siku zijazo, wazao wenu hawataweza kuwaambia wazao wetu, ‘Ninyi hamna fungu katika Bwana.’

28 22:28“Nasi tulisema, ‘Ikiwa wakati wowote watatuambia hilo, au kuwaambia uzao wetu, tutawajibu hivi: Angalieni nakala hii ya madhabahu ya Bwana, ambayo baba zetu waliijenga, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu, bali kama ushahidi kati yetu na ninyi.’

29 22:29“Hili jambo la kumwasi Bwana na kumwacha siku hii ya leo kwa kujenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na dhabihu, zaidi ya madhabahu ya Bwana Mungu wetu iliyo mbele ya maskani yake na liwe mbali nasi.”

30 22:30Wakati kuhani Finehasi na viongozi wa kusanyiko na wakuu wa koo za Israeli, waliposikia hayo waliyosema Wareubeni, Wagadi na Manase, wakaridhika. 31 22:31Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akawaambia Wareubeni, Wagadi na Manase, “Leo tunajua kwamba Bwana yuko pamoja nasi, kwa sababu hamkukosa uaminifu kwa Bwana katika jambo hili. Sasa mmewaokoa Waisraeli na mkono wa Bwana.”

32 22:32Ndipo Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari na viongozi wakarudi Kanaani kutoka kwenye kukutana kwao na Wareubeni na Wagadi huko Gileadi nao wakatoa taarifa kwa Waisraeli. 33 22:33Walifurahi kusikia taarifa hiyo, na wakamhimidi Mungu. Wala hawakuzungumza tena habari za kupigana vita dhidi yao ili kuharibu nchi ambayo Wareubeni na Wagadi waliishi.

34 22:34Nao Wareubeni na Wagadi wakayaita yale madhabahu Edi, yaani Shahidi: kwa kuwa itakuwa shahidi kati yetu na ninyi kwamba Bwana ndiye Mungu.

23Yoshua Anawaaga Viongozi

1 23:1Baada ya muda mrefu kupita, naye Bwana akawa amewapa Israeli pumziko mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo akiwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana, 2 23:2akawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa Yoshua akawaambia: “Mimi ni mzee na umri wangu umeendelea sana. 3 23:3Ninyi wenyewe mmeona kila kitu Bwana Mungu wenu, alichowatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Ilikuwa ni Bwana Mungu wenu aliyewapigania. 4 23:4Kumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari kuu upande wa magharibi. 5 23:5 Bwana Mungu wenu mwenyewe atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vile Bwana Mungu wenu alivyowaahidi.

6 23:6“Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria ya Mose, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto. 7 23:7Msishirikiane na mataifa yaliyobakia katikati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia. 8 23:8Bali mtashikamana kwa uthabiti na Bwana, Mungu wenu, kama vile ambavyo mmefanya mpaka sasa.

9 23:9Bwana amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, mpaka siku ya leo hakuna yeyote aliyeweza kusimama mbele yenu. 10 23:10Mtu mmoja miongoni mwenu anafukuza watu elfu, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anawapigania, kama alivyoahidi. 11 23:11Kwa hiyo kuweni waangalifu sana kumpenda Bwana Mungu wenu.

12 23:12“Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia katikati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao, 13 23:13basi mwe na hakika kuwa Bwana Mungu wenu hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu, na miiba machoni mwenu, mpaka mwangamie kutoka nchi hii nzuri, ambayo Bwana Mungu wenu amewapa.

14 23:14“Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zozote njema Bwana Mungu wenu alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia. 15 23:15Lakini kama vile kila ahadi njema ya Bwana Mungu wenu imekuwa kweli, vivyo hivyo Bwana ataleta maovu yote kama alivyo onya, mpaka awe amewaangamiza kutoka nchi hii nzuri aliyowapa. 16 23:16Kama mkilivunja agano la Bwana Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya Bwana itawaka dhidi yenu, nanyi mtaangamia kutoka nchi nzuri aliyowapa ninyi.”

24Agano Lafanywa Upya Huko Shekemu

1 24:1Ndipo Yoshua akaita pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maafisa wa Israeli, nao wakaja mbele za Mungu.

2 24:2Yoshua akawaambia watu wote, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Hapo zamani baba zenu, pamoja na Tera baba yake Abrahamu na Nahori, waliishi ngʼambo ya Mto nao waliiabudu miungu mingine. 3 24:3Lakini nilimwondoa baba yenu Abrahamu kutoka nchi hiyo ngʼambo ya Mto, nami nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani, nikampa wazao wengi. Nikampa Isaki, 4 24:4naye Isaki nikampa Yakobo na Esau. Esau nikampa nchi ya vilima ya Seiri, lakini Yakobo pamoja na wanawe wakashuka Misri.

5 24:5“ ‘Kisha nikawatuma Mose na Aroni, nami nikawapiga Wamisri kwa kile nilichokitenda huko, tena nikawatoa ninyi huko. 6 24:6Nilipowatoa baba zenu Misri, mlifika kwenye bahari, nao Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka kwenye Bahari ya Shamu. 7 24:7Lakini wakamlilia Bwana wakitaka msaada, naye akaweka giza kati yenu na Wamisri, akaileta bahari juu yao ikawafunika. Ninyi mliona kwa macho yenu wenyewe kile nilichowatendea Wamisri. Kisha mliishi jangwani kwa muda mrefu.

8 24:8“ ‘Nikawaleta katika nchi ya Waamori ambao waliishi mashariki mwa Yordani. Wakapigana nanyi, lakini nikawatia mikononi mwenu. Nikawaangamiza mbele yenu nanyi mkaimiliki nchi yao. 9 24:9Wakati Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipojiandaa kupigana dhidi ya Israeli, alimwita Balaamu mwana wa Beori apate kuwalaani. 10 24:10Lakini sikumkubali Balaamu, kwa hiyo aliwabariki tena na tena, nami niliwaokoa toka mkononi mwake.

11 24:11“ ‘Ndipo mlipovuka Yordani mkafika Yeriko. Raiya wa Yeriko wakapigana nanyi, kama walivyofanya Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi, lakini niliwatia mikononi mwenu. 12 24:12Nikatuma manyigu mbele yenu, ambao pia waliwafukuza mbele yenu, hao wafalme wawili wa Waamori. Siyo upanga au upinde wenu wenyewe vilivyowapatia ushindi. 13 24:13Hivyo nikawapa ninyi nchi ambayo hamkuitaabikia na miji ambayo hamkuijenga na mnaishi ndani yake na kula toka kwa mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.’

14 24:14“Sasa basi mcheni Bwana na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ngʼambo ya Mto Frati na huko Misri, nanyi mtumikieni Bwana. 15 24:15Lakini msipoona vyema kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ngʼambo Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Bwana.”

16 24:16Ndipo hao watu wakajibu, “Hili jambo liwe mbali nasi la kumsahau Bwana na kuitumikia miungu mingine! 17 24:17 Bwana Mungu wetu mwenyewe ndiye alitutoa sisi na baba zetu akatupandisha kutoka Misri, kutoka nchi ile ya utumwa, na kutenda zile ishara kubwa mbele ya macho yetu. Ndiye aliyetulinda katika safari yetu yote na kutokana na mataifa yote ambayo tulipita katikati yao. 18 24:18 Bwana akayafukuza mbele yetu mataifa yote pamoja na Waamori, walioishi katika nchi hii. Hivyo sisi nasi tutamtumikia Bwana kwa kuwa yeye ndiye Mungu wetu.”

19 24:19Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Bwana. Yeye ni Mungu Mtakatifu, ni Mungu mwenye wivu. Hatasamehe uasi wenu na dhambi zenu. 20 24:20Ikiwa mkimwacha Bwana na kuitumikia miungu migeni, atageuka na kuwaleteeni maafa na kuwaangamiza, baada ya kuwa mwema kwenu.”

21 24:21Lakini watu wakamwambia Yoshua, “Sivyo! Sisi tutamtumikia Bwana.”

22 24:22Ndipo Yoshua akawaambia, “Ninyi mmekuwa mashahidi juu yenu wenyewe kuwa mmechagua kumtumikia Bwana.”

Nao wakajibu, “Ndiyo, tu mashahidi.”

23 24:23Yoshua akawaambia, “Sasa basi, itupeni mbali hiyo miungu migeni iliyo katikati yenu, nanyi mtoleeni Bwana, Mungu wa Israeli, mioyo yenu.”

24 24:24Nao watu wakamwambia Yoshua, “Tutamtumikia Bwana Mungu wetu na kumtii yeye.”

25 24:25Siku ile Yoshua akafanya agano kwa ajili ya watu na hapo Shekemu ndipo alipowaandikia amri na sheria. 26 24:26Naye Yoshua akayaandika mambo haya katika Kitabu cha Sheria ya Mungu. Ndipo akalitwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko chini ya mwaloni, karibu na mahali patakatifu pa Bwana.

27 24:27Yoshua akawaambia watu wote, “Angalieni! Jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu. Limesikia maneno yote Bwana aliyotuambia. Litakuwa shahidi juu yenu kama mtakuwa waongo kwa Mungu wenu.”

Kuzikwa Katika Nchi Ya Ahadi

28 24:28Basi Yoshua akawatuma watu kila mmoja aende katika urithi wake mwenyewe.

29 24:29Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. 30 24:30Nao wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Sera 24:30 Unajulikana pia kama Timnath-Heresi, ona Yos 19:50; Amu 2:9. katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini ya Mlima wa Gaashi.

31 24:31Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, ambao waliona kila kitu Bwana alichowatendea Israeli.

32 24:32Nayo ile mifupa ya Yosefu, ambayo Waisraeli waliipandisha kutoka huko Misri, wakaizika huko Shekemu kwenye eneo, ambalo Yakobo alilinunua kwa wana wa Hamori baba yake Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Eneo hili likawa ni urithi wa uzao wa Yosefu.

33 24:33Naye Eleazari mwana wa Aroni akafariki akazikwa huko Gibea, mlima aliokuwa amepewa mtoto wake Finehasi, kwenye nchi ya vilima ya Efraimu.