Maombolezo
1
Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
1Maombolezo1 1:1Tazama jinsi mji ulivyoachwa ukiwa,
mji ambao zamani ulikuwa umejaa watu!
Jinsi ambavyo umekuwa kama mama mjane,
ambaye wakati fulani alikuwa maarufu miongoni mwa mataifa!
Yule ambaye alikuwa malkia miongoni mwa majimbo
sasa amekuwa mtumwa.
2 1:2Kwa uchungu, hulia sana usiku,
machozi yapo kwenye mashavu yake.
Miongoni mwa wapenzi wake wote
hakuna yeyote wa kumfariji.
Rafiki zake wote wamemsaliti,
wamekuwa adui zake.
3 1:3Baada ya mateso na kufanyishwa kazi kikatili,
Yuda amekwenda uhamishoni.
Anakaa miongoni mwa mataifa,
hapati mahali pa kupumzika.
Wote ambao wanamsaka wamemkamata
katikati ya dhiki yake.
4 1:4Barabara zielekeazo Sayuni zaomboleza,
kwa kuwa hakuna yeyote anayekuja
kwenye sikukuu zake zilizoamriwa.
Malango yake yote yamekuwa ukiwa,
makuhani wake wanalia kwa uchungu,
wanawali wake wanahuzunika,
naye yuko katika uchungu wa maumivu makuu.
5 1:5Adui zake wamekuwa mabwana zake,
watesi wake wana raha.
Bwana amemletea huzuni
kwa sababu ya dhambi zake nyingi.
Watoto wake wamekwenda uhamishoni,
mateka mbele ya adui.
6 1:6Fahari yote imeondoka
kutoka kwa Binti Sayuni.
Wakuu wake wako kama ayala
ambaye hapati malisho,
katika udhaifu wamekimbia
mbele ya anayewasaka.
7 1:7Katika siku za mateso yake na kutangatanga,
Yerusalemu hukumbuka hazina zote
ambazo zilikuwa zake siku za kale.
Wakati watu wake walipoanguka katika mikono ya adui,
hapakuwepo na yeyote wa kumsaidia.
Watesi wake walimtazama
na kumcheka katika maangamizi yake.
8 1:8Yerusalemu ametenda dhambi sana
kwa hiyo amekuwa najisi.
Wote waliomheshimu wanamdharau,
kwa maana wameuona uchi wake.
Yeye mwenyewe anapiga kite
na kugeukia mbali.
9 1:9Uchafu wake umegandamana na nguo zake;
hakuwaza juu ya maisha yake ya baadaye.
Anguko lake lilikuwa la kushangaza,
hapakuwepo na yeyote wa kumfariji.
“Tazama, Ee
Bwana, teso langu,
kwa maana adui ameshinda.”
10 1:10Adui ametia mikono
juu ya hazina zake zote,
aliona mataifa ya kipagani
wakiingia mahali patakatifu pake,
wale uliowakataza kuingia
kwenye kusanyiko lako.
11 1:11Watu wake wote wanalia kwa uchungu
watafutapo chakula;
wanabadilisha hazina zao kwa chakula
ili waweze kuendelea kuishi.
“Tazama, Ee
Bwana, ufikiri,
kwa maana nimedharauliwa.”
12 1:12“Je, si kitu kwenu, ninyi nyote mpitao kando?
Angalieni kote mwone.
Je, kuna maumivu kama maumivu yangu
yale yaliyotiwa juu yangu,
yale
Bwana aliyoyaleta juu yangu
katika siku ya hasira yake kali?
13 1:13“Kutoka juu alipeleka moto,
akaushusha katika mifupa yangu.
Aliitandia wavu miguu yangu
na akanirudisha nyuma.
Akanifanya mkiwa,
na mdhaifu mchana kutwa.
14 1:14“Dhambi zangu zimefungwa kwenye nira,
kwa mikono yake zilifumwa pamoja.
Zimefika shingoni mwangu
na Bwana ameziondoa nguvu zangu.
Amenitia mikononi mwa wale
ambao siwezi kushindana nao.
15 1:15“Bwana amewakataa wapiganaji wa vita
wote walio kati yangu,
ameagiza jeshi dhidi yangu
kuwaponda vijana wangu wa kiume.
Katika shinikizo lake la divai Bwana amemkanyaga
Bikira Binti Yuda.
16 1:16“Hii ndiyo sababu ninalia
na macho yangu yanafurika machozi.
Hakuna yeyote aliye karibu kunifariji,
hakuna yeyote wa kuhuisha roho yangu.
Watoto wangu ni wakiwa
kwa sababu adui ameshinda.”
17 1:17Sayuni ananyoosha mikono yake,
lakini hakuna yeyote wa kumfariji.
Bwana ametoa amri kwa ajili ya Yakobo
kwamba majirani zake wawe adui zake;
Yerusalemu umekuwa
kitu najisi miongoni mwao.
18 1:18“Bwana ni mwenye haki,
hata hivyo niliasi dhidi ya amri yake.
Sikilizeni, enyi mataifa yote,
tazameni maumivu yangu.
Wavulana wangu na wasichana wangu
wamekwenda uhamishoni.
19 1:19“Niliita washirika wangu
lakini walinisaliti.
Makuhani wangu na wazee wangu
waliangamia mjini
walipokuwa wakitafuta chakula
ili waweze kuishi.
20 1:20“Angalia, Ee
Bwana, jinsi nilivyo katika dhiki!
Nina maumivu makali ndani yangu,
nami ninahangaika moyoni mwangu,
kwa kuwa nimekuwa mwasi sana.
Huko nje, upanga unaua watu,
ndani, kipo kifo tu.
21 1:21“Watu wamesikia ninavyolia kwa uchungu,
lakini hakuna yeyote wa kunifariji.
Adui zangu wote wamesikia juu ya dhiki yangu,
wanafurahia lile ulilolitenda.
Naomba uilete siku uliyoitangaza
ili wawe kama mimi.
22 1:22“Uovu wao wote na uje mbele zako;
uwashughulikie wao
kama vile ulivyonishughulikia mimi
kwa sababu ya dhambi zangu zote.
Kulia kwangu kwa uchungu ni kwingi
na moyo wangu umedhoofika.”
2
Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
21 2:1Tazama jinsi Bwana alivyomfunika Binti Sayuni
kwa wingu la hasira yake!
Ameitupa chini fahari ya Israeli
kutoka mbinguni mpaka duniani,
hakukumbuka kiti chake cha kuwekea miguu
katika siku ya hasira yake.
2 2:2Bila huruma Bwana ameyameza
makao yote ya Yakobo;
katika ghadhabu yake amebomoa
ngome za Binti Yuda.
Ameuangusha ufalme wake na wakuu wake
chini kwa aibu.
3 2:3Katika hasira kali amevunja
kila pembe
2:3
Pembe inawakilisha nguvu; pia 2:17. ya Israeli.
Ameuondoa mkono wake wa kuume
alipokaribia adui.
Amemteketeza Yakobo kama moto uwakao
ule uteketezao kila kitu kinachouzunguka.
4 2:4Ameupinda upinde wake kama adui,
mkono wake wa kuume uko tayari.
Kama vile adui amewachinja
wote waliokuwa wanapendeza jicho,
amemwaga ghadhabu yake kama moto
juu ya hema la Binti Sayuni.
5 2:5Bwana ni kama adui;
amemmeza Israeli.
Amemeza majumba yake yote ya kifalme
na kuangamiza ngome zake.
Ameongeza huzuni na maombolezo
kwa ajili ya Binti Yuda.
6 2:6Ameharibu maskani yake kama bustani,
ameharibu mahali pake pa mkutano.
Bwana amemfanya Sayuni kusahau
sikukuu zake zilizoamriwa na Sabato zake;
katika hasira yake kali amewadharau
mfalme na kuhani.
7 2:7Bwana amekataa madhabahu yake
na kuacha mahali patakatifu pake.
Amemkabidhi adui kuta
za majumba yake ya kifalme;
wamepiga kelele katika nyumba ya
Bwana
kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa.
8 2:8
Bwana alikusudia kuangusha
ukuta uliomzunguka Binti Sayuni.
Ameinyoosha kamba ya kupimia
na hakuuzuia mkono wake usiangamize.
Alifanya maboma na kuta ziomboleze,
vyote vikaharibika pamoja.
9 2:9Malango yake yamezama ardhini,
makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu.
Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni
miongoni mwa mataifa,
sheria haipo tena,
na manabii wake hawapati tena
maono kutoka kwa
Bwana.
10 2:10Wazee wa Binti Sayuni
wanaketi chini kimya,
wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao
na kuvaa nguo za gunia.
Wanawali wa Yerusalemu
wamesujudu hadi ardhini.
11 2:11Macho yangu yamedhoofika kwa kulia,
nina maumivu makali ndani,
moyo wangu umemiminwa ardhini
kwa sababu watu wangu wameangamizwa,
kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia
kwenye barabara za mji.
12 2:12Wanawaambia mama zao,
“Wapi mkate na divai?”
wazimiapo kama watu waliojeruhiwa
katika barabara za mji,
maisha yao yadhoofikavyo
mikononi mwa mama zao.
13 2:13Ninaweza kusema nini kwa ajili yako?
Nikulinganishe na nini,
ee Binti Yerusalemu?
Nitakufananisha na nini,
ili nipate kukufariji,
ee Bikira Binti Sayuni?
Jeraha lako lina kina kama bahari.
Ni nani awezaye kukuponya?
14 2:14Maono ya manabii wako
yalikuwa ya uongo na yasiyofaa kitu,
hawakuifunua dhambi yako
ili kukuzuilia kwenda utumwani.
Maneno waliyokupa
yalikuwa ya uongo na ya kupotosha.
15 2:15Wote wapitiao njia yako
wanakupigia makofi,
wanakudhihaki na kutikisa vichwa vyao
kwa Binti Yerusalemu:
“Huu ndio ule mji ulioitwa
mkamilifu wa uzuri,
furaha ya dunia yote?”
16 2:16Adui zako wote wanapanua
vinywa vyao dhidi yako,
wanadhihaki na kusaga meno yao
na kusema, “Tumemmeza.
Hii ndiyo siku tuliyoingojea,
tumeishi na kuiona.”
17 2:17
Bwana amefanya lile alilolipanga;
ametimiza neno lake
aliloliamuru siku za kale.
Amekuangusha bila huruma,
amewaacha adui wakusimange,
ametukuza pembe ya adui yako.
18 2:18Mioyo ya watu
inamlilia Bwana.
Ee ukuta wa Binti Sayuni,
machozi yako na yatiririke kama mto
usiku na mchana;
usijipe nafuu,
macho yako yasipumzike.
19 2:19Inuka, lia usiku,
zamu za usiku zianzapo;
mimina moyo wako kama maji
mbele za Bwana.
Mwinulie yeye mikono yako
kwa ajili ya maisha ya watoto wako,
ambao wanazimia kwa njaa
kwenye kila mwanzo wa barabara.
20 2:20“Tazama, Ee
Bwana, ufikirie:
Ni nani ambaye umepata
kumtendea namna hii?
Je, wanawake wakule wazao wao,
watoto waliowalea?
Je, kuhani na nabii auawe
mahali patakatifu pa Bwana?
21 2:21“Vijana na wazee hujilaza pamoja
katika mavumbi ya barabarani,
wavulana wangu na wasichana
wameanguka kwa upanga.
Umewaua katika siku ya hasira yako,
umewachinja bila huruma.
22 2:22“Kama ulivyoita siku ya karamu,
ndivyo ulivyoagiza hofu kuu
dhidi yangu kila upande.
Katika siku ya hasira ya
Bwana
hakuna yeyote aliyekwepa au kupona;
wale niliowatunza na kuwalea,
adui yangu amewaangamiza.”
3
Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
31 3:1Mimi ndiye mtu aliyeona mateso
kwa fimbo ya ghadhabu yake.
2 3:2Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee
gizani wala si katika nuru;
3 3:3hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu
tena na tena, mchana kutwa.
4 3:4Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa
na ameivunja mifupa yangu.
5 3:5Amenizingira na kunizunguka
kwa uchungu na taabu.
6 3:6Amenifanya niishi gizani
kama wale waliokufa.
7 3:7Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka,
amenifunga kwa minyororo mizito.
8 3:8Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada,
anakataa kupokea maombi yangu.
9 3:9Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe,
amepotosha njia zangu.
10 3:10Kama dubu aviziaye,
kama simba mafichoni,
11 3:11ameniburuta kutoka njia,
akanirarua na kuniacha bila msaada.
12 3:12Amevuta upinde wake
na kunifanya mimi niwe lengo
kwa ajili ya mishale yake.
13 3:13Alinichoma moyo wangu kwa mishale
iliyotoka kwenye podo lake.
14 3:14Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote,
wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa.
15 3:15Amenijaza kwa majani machungu
na kunishibisha kwa nyongo.
16 3:16Amevunja meno yangu kwa changarawe,
amenikanyagia mavumbini.
17 3:17Amani yangu imeondolewa,
nimesahau kufanikiwa ni nini.
18 3:18Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka
na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa
Bwana.”
19 3:19Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu,
uchungu na nyongo.
20 3:20Ninayakumbuka vyema,
nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.
21 3:21Hata hivyo najikumbusha neno hili
na kwa hiyo ninalo tumaini.
22 3:22Kwa sababu ya upendo mkuu wa
Bwana, hatuangamii,
kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.
23 3:23Ni mpya kila asubuhi,
uaminifu wako ni mkuu.
24 3:24Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu,
kwa hiyo nitamngojea.”
25 3:25
Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake,
kwa yule ambaye humtafuta;
26 3:26ni vyema kungojea kwa utulivu
kwa ajili ya wokovu wa
Bwana.
27 3:27Ni vyema mtu kuchukua nira
bado angali kijana.
28 3:28Na akae peke yake awe kimya,
kwa maana
Bwana ameiweka juu yake.
29 3:29Na azike uso wake mavumbini
bado panawezekana kuwa na matumaini.
30 3:30Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye,
na ajazwe na aibu.
31 3:31Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali
na Bwana milele.
32 3:32Ingawa huleta huzuni, ataonyesha huruma,
kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu.
33 3:33Kwa maana hapendi kuwaletea mateso
au huzuni watoto wa wanadamu.
34 3:34Kuwaponda chini ya nyayo
wafungwa wote katika nchi,
35 3:35Kumnyima mtu haki zake
mbele za Aliye Juu Sana,
36 3:36kumnyima mtu haki:
Je, Bwana asione mambo kama haya?
37 3:37Nani awezaye kusema nalo likatendeka
kama Bwana hajaamuru?
38 3:38Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana
ndiko yatokako maafa na mambo mema?
39 3:39Mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika
wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake?
40 3:40Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu,
na tumrudie
Bwana Mungu.
41 3:41Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu
kwa Mungu mbinguni, na tuseme:
42 3:42“Tumetenda dhambi na kuasi
nawe hujasamehe.
43 3:43“Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia;
umetuchinja bila huruma.
44 3:44Unajifunika mwenyewe kwa wingu,
ili pasiwe na ombi
litakaloweza kupenya.
45 3:45Umetufanya takataka na uchafu
miongoni mwa mataifa.
46 3:46“Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao
wazi dhidi yetu.
47 3:47Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula,
uharibifu na maangamizi.”
48 3:48Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu,
kwa sababu watu wangu wameangamizwa.
49 3:49Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma,
bila kupata nafuu,
50 3:50hadi
Bwana atazame chini
kutoka mbinguni na kuona.
51 3:51Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini
kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu.
52 3:52Wale waliokuwa adui zangu bila sababu
wameniwinda kama ndege.
53 3:53Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo
na kunitupia mawe;
54 3:54maji yalifunika juu ya kichwa changu,
nami nikafikiri nilikuwa karibu
kukatiliwa mbali.
55 3:55Nililiitia jina lako, Ee
Bwana,
kutoka vina vya shimo.
56 3:56Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako
kilio changu nikuombapo msaada.”
57 3:57Ulikuja karibu nilipokuita,
nawe ukasema, “Usiogope.”
58 3:58Ee Bwana, ulichukua shauri langu,
ukaukomboa uhai wangu.
59 3:59Umeona, Ee
Bwana, ubaya niliotendewa.
Tetea shauri langu!
60 3:60Umeona kina cha kisasi chao,
mashauri yao yote mabaya dhidi yangu.
61 3:61Ee
Bwana, umesikia matukano yao,
mashauri yao yote mabaya dhidi yangu:
62 3:62kile adui zangu wanachonongʼona na kunungʼunikia
dhidi yangu mchana kutwa.
63 3:63Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama,
wananidhihaki katika nyimbo zao.
64 3:64Uwalipe kile wanachostahili, Ee
Bwana,
kwa yale ambayo mikono yao imetenda.
65 3:65Weka pazia juu ya mioyo yao,
laana yako na iwe juu yao!
66 3:66Wafuatilie katika hasira na uwaangamize
kutoka chini ya mbingu za
Bwana.
4
Sura hii imetungwa kila beti likianzia, na pia kila mstari katika lile beti, na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.
41 4:1Jinsi dhahabu ilivyopoteza mngʼao wake,
dhahabu iliyo safi haingʼai!
Vito vya thamani vimetawanywa
kwenye mwanzo wa kila barabara.
2 4:2Wana wa Sayuni wenye thamani,
ambao mwanzo uzito wa thamani yao
ulikuwa wa dhahabu,
sasa wanaangaliwa kama vyungu vya udongo,
kazi ya mikono ya mfinyanzi!
3 4:3Hata mbweha hutoa matiti yao
kunyonyesha watoto wao,
lakini watu wangu wamekuwa wasio na huruma
kama mbuni jangwani.
4 4:4Kwa sababu ya kiu ulimi wa mtoto mchanga
umegandamana na kaakaa la kinywa chake,
watoto huomba mkate,
lakini hakuna yeyote awapaye.
5 4:5Wale waliokula vyakula vya kifahari
ni maskini barabarani.
Wale waliokuzwa wakivaa nguo za zambarau
sasa wanalalia majivu.
6 4:6Adhabu ya watu wangu
ni kubwa kuliko ile ya Sodoma,
ambayo ilipinduliwa ghafula
bila kuwepo mkono wa msaada.
7 4:7Wakuu wao walikuwa wamengʼaa kuliko theluji
na weupe kuliko maziwa,
miili yao ilikuwa myekundu kuliko marijani,
kuonekana kwao kama yakuti samawi.
8 4:8Lakini sasa ni weusi kuliko masizi;
hawatambulikani barabarani.
Ngozi yao imeshikamana juu ya mifupa yao,
imekuwa mikavu kama fimbo.
9 4:9Wale waliouawa kwa upanga ni bora
kuliko wale wanaokufa njaa;
wanateseka kwa njaa, wanatokomea
kwa kukosa chakula kutoka shambani.
10 4:10Kwa mikono yao wenyewe wanawake wenye huruma
wanapika watoto wao wenyewe,
waliokuwa chakula chao
watu wangu walipoangamizwa.
11 4:11
Bwana ametoa nafasi kamilifu ya ghadhabu yake;
ameimwaga hasira yake kali.
Amewasha moto katika Sayuni
ambao umeteketeza misingi yake.
12 4:12Wafalme wa dunia hawakuamini,
wala mtu yeyote wa duniani,
kwamba adui na watesi wangeweza kuingia
kwenye malango ya Yerusalemu.
13 4:13Lakini hili lilitokea kwa sababu ya dhambi za manabii wake,
na maovu ya makuhani wake,
waliomwaga ndani yake
damu ya wenye haki.
14 4:14Sasa wanapapasa papasa barabarani
kama watu ambao ni vipofu.
Wamenajisiwa kabisa kwa damu,
hata hakuna anayethubutu kugusa mavazi yao.
15 4:15Watu wanawapigia kelele, “Ondokeni! Ninyi ni najisi!
Ondokeni! Ondokeni! Msituguse!”
Wanapokimbia na kutangatanga huku na huko,
watu miongoni mwa mataifa wanasema,
“Hawawezi kukaa hapa zaidi.”
16 4:16
Bwana mwenyewe amewatawanya;
hawaangalii tena.
Makuhani hawaonyeshwi heshima,
wazee hawakubaliki.
17 4:17Zaidi ya hayo, macho yetu yalichoka,
kwa kutazamia bure msaada;
tuliangalia kutoka minara yetu
kwa taifa lisiloweza kutuokoa.
18 4:18Watu walituvizia katika kila hatua
hata hatukuweza kutembea katika barabara zetu.
Mwisho wetu ulikuwa karibu, siku zetu zilikuwa zimetimia,
kwa maana mwisho wetu ulikuwa umefika.
19 4:19Waliotufuatia walikuwa wepesi
kuliko tai angani;
walitusaka juu milimani
na kutuvizia jangwani.
20 4:20Mpakwa mafuta wa
Bwana, pumzi ya uhai wetu hasa,
alinaswa katika mitego yao.
Tulifikiri kwamba chini ya kivuli chake
tungeliweza kuishi miongoni mwa mataifa.
21 4:21Shangilia na ufurahi, ee Binti Edomu,
wewe unayeishi nchi ya Usi.
Lakini kwako pia kikombe kitapitishwa,
Utalewa na kuvuliwa nguo ubaki uchi.
22 4:22Ee Binti Sayuni, adhabu yako itaisha,
hatarefusha muda wako wa kukaa uhamishoni.
Lakini, ee Binti Edomu, ataadhibu dhambi yako,
na atafunua uovu wako.
51 5:1Kumbuka, Ee
Bwana, yaliyotupata,
tazama, nawe uione aibu yetu.
2 5:2Urithi wetu umegeuziwa kwa wageni,
na nyumba zetu kwa wageni.
3 5:3Tumekuwa yatima wasio na baba,
mama zetu wamekuwa kama wajane.
4 5:4Ni lazima tununue maji tunayokunywa,
kuni zetu zapatikana tu kwa kununua.
5 5:5Wanaotufuatilia wapo kwenye visigino vyetu,
tumechoka na hakuna pumziko.
6 5:6Tumejitolea kwa Misri na Ashuru
tupate chakula cha kutosha.
7 5:7Baba zetu walitenda dhambi na hawapo tena,
na sisi tunachukua adhabu yao.
8 5:8Watumwa wanatutawala
na hakuna wa kutuokoa mikononi yao.
9 5:9Tunapata chakula chetu kwa kuhatarisha maisha yetu
kwa sababu ya upanga jangwani.
10 5:10Ngozi yetu ina joto kama tanuru,
kwa sababu ya fadhaa itokanayo na njaa.
11 5:11Wanawake wametendwa jeuri katika Sayuni,
na mabikira katika miji ya Yuda.
12 5:12Wakuu wametungikwa juu kwa mikono yao,
wazee hawapewi heshima.
13 5:13Vijana wanataabika kwenye mawe ya kusagia,
wavulana wanayumbayumba chini ya mizigo ya kuni.
14 5:14Wazee wameondoka langoni la mji,
vijana wameacha kuimba nyimbo zao.
15 5:15Furaha imeondoka mioyoni mwetu,
kucheza kwetu kumegeuka maombolezo.
16 5:16Taji imeanguka kutoka kichwani petu.
Ole wetu, kwa maana tumetenda dhambi!
17 5:17Kwa sababu hiyo, mioyo yetu inazimia,
kwa sababu ya hayo, macho yetu yamefifia,
18 5:18kwa ajili ya Mlima Sayuni, ambao unakaa ukiwa,
nao mbweha wanatembea juu yake.
19 5:19Wewe, Ee
Bwana unatawala milele,
kiti chako cha enzi chadumu kizazi hadi kizazi.
20 5:20Kwa nini watusahau siku zote?
Kwa nini umetuacha kwa muda mrefu?
21 5:21Turudishe kwako mwenyewe, Ee
Bwana,
ili tupate kurudi.
Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale,
22 5:22isipokuwa uwe umetukataa kabisa
na umetukasirikia pasipo kipimo.