Mathayo 1MathayoKumbukumbu Za Ukoo Wa Yesu Kristo (Luka 3:23-38)

1 1:1Habari za ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu:

  • 2 1:2Abrahamu akamzaa Isaki,
  • Isaki akamzaa Yakobo, Yakobo akawazaa Yuda na ndugu zake, 3 1:3Yuda akawazaa Peresi na Zera, ambao mama yao alikuwa Tamari, Peresi akamzaa Hesroni, Hesroni akamzaa Aramu, 4 1:4Aramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni, 5 1:5Salmoni akamzaa Boazi, na mama yake Boazi alikuwa Rahabu, Boazi akamzaa Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruthu, Obedi akamzaa Yese, 6 1:6Yese akamzaa Daudi ambaye alikuwa mfalme.
  • Daudi akamzaa Solomoni, ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria.
  • 7 1:7Solomoni akamzaa Rehoboamu, Rehoboamu akamzaa Abiya, Abiya akamzaa Asa, 8 1:8Asa akamzaa Yehoshafati, Yehoshafati akamzaa Yoramu, 1:8 Yoramu ndiye Yehoramu, maana yake ni Yehova yu juu. Yoramu akamzaa Uzia, 9 1:9Uzia akamzaa Yothamu, Yothamu akamzaa Ahazi, Ahazi akamzaa Hezekia, 10 1:10Hezekia akamzaa Manase, Manase akamzaa Amoni, Amoni akamzaa Yosia, 11 1:11wakati wa uhamisho wa Babeli, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake.
  • 12 1:12Baada ya uhamisho wa Babeli:
  • Yekonia alimzaa Shealtieli, Shealtieli akamzaa Zerubabeli, 13 1:13Zerubabeli akamzaa Abiudi, Abiudi akamzaa Eliakimu, Eliakimu akamzaa Azori, 14 1:14Azori akamzaa Sadoki, Sadoki akamzaa Akimu, Akimu akamzaa Eliudi, 15 1:15Eliudi akamzaa Eleazari, Eleazari akamzaa Matani, Matani akamzaa Yakobo, 16 1:16naye Yakobo akamzaa Yosefu ambaye alikuwa mumewe Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo. 1:16 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.

    17 1:17Hivyo, kulikuwepo na jumla ya vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi hadi wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli, na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli hadi Kristo.

    Kuzaliwa Kwa Yesu Kristo (Luka 2:1-7)

    18 1:18Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19 1:19Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.

    20 1:20Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21 1:21Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, 1:21 Yesu ni Iesous kwa Kiyunani, na kwa Kiebrania ni Yoshua au Yeshua. Maana yake ni Yehova ni wokovu. kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”

    22 1:22Haya yote yalitukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: 23 1:23“Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli”: maana yake, “Mungu pamoja nasi.”

    24 1:24Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake. 25 1:25Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.

    2Wataalamu Wa Nyota Wafika Kumwona Mtoto Yesu

    1 2:1Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Uyahudi, wakati wa utawala wa Mfalme Herode, wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu 2 2:2wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.”

    3 2:3Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. 4 2:4Herode akawaita pamoja viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, akawauliza ni mahali gani ambapo Kristo 2:4 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. angezaliwa. 5 2:5Nao wakamwambia, “Katika Bethlehemu ya Uyahudi, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:

    6 2:6“ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, wewe si mdogo miongoni mwa watawala wa Yuda; kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala atakayekuwa mchungaji wa watu wangu Israeli.’ ”

    7 2:7Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilionekana. 8 2:8Kisha akawatuma waende Bethlehemu akiwaambia, “Nendeni mkamtafute kwa bidii huyo mtoto. Nanyi mara mtakapomwona, mniletee habari ili na mimi niweze kwenda kumwabudu.”

    9 2:9Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata mpaka iliposimama mahali pale alipokuwa mtoto. 10 2:10Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. 11 2:11Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. 12 2:12Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine.

    Yosefu, Maria Na Mtoto Yesu Wakimbilia Misri

    13 2:13Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”

    14 2:14Kisha Yosefu akaondoka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri 15 2:15ambako walikaa mpaka Herode alipofariki. Hili lilifanyika ili litimie lile lililonenwa na Bwana kwa kinywa cha nabii kusema: “Nilimwita mwanangu kutoka Misri.”

    16 2:16Herode alipongʼamua kwamba wale wataalamu wa nyota wamemshinda kwa akili, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kufuatana na ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota. 17 2:17Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia.

    18 2:18“Sauti ilisikika huko Rama, maombolezo na kilio kikubwa, Raheli akilia kwa ajili ya wanawe, akikataa kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.” Kurudi Kutoka Misri

    19 2:19Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri 20 2:20na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa.”

    21 2:21Basi Yosefu, akaondoka akamchukua mtoto na mama yake wakaenda mpaka nchi ya Israeli. 22 2:22Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Uyahudi mahali pa Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. Naye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya, 23 2:23akaenda akaishi katika mji ulioitwa Nazareti. Hivyo likawa limetimia neno lililonenwa na manabii, “Ataitwa Mnazarayo.”

    3Yohana Mbatizaji Atayarisha Njia (Marko 1:1-8; Luka 3:1-18; Yohana 1:19-28)

    1 3:1Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Uyahudi, akisema, 2 3:2“Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.” 3 3:3Huyu ndiye yule aliyenenwa habari zake na nabii Isaya aliposema:

    “Sauti ya mtu aliaye huko nyikani, ‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.’ ”

    4 3:4Basi Yohana alivaa mavazi yaliyotengenezwa kwa singa za ngamia, akiwa na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu. 5 3:5Watu walikuwa wakimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kandokando ya Mto Yordani. 6 3:6Nao wakaziungama dhambi zao, akawabatiza katika Mto Yordani.

    7 3:7Lakini alipowaona Mafarisayo na Masadukayo wengi wakija ili kubatizwa, aliwaambia: “Ninyi watoto wa nyoka! Ni nani aliyewaonya kuikimbia ghadhabu inayokuja? 8 3:8Basi zaeni matunda yastahiliyo toba. 9 3:9Wala msidhani mnaweza kusema mioyoni mwenu kuwa, ‘Sisi tunaye Abrahamu, baba yetu.’ Nawaambia kuwa Mungu anaweza kumwinulia Abrahamu watoto kutoka kwa mawe haya. 10 3:10Hata sasa shoka limeshawekwa tayari kwenye shina la kila mti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri, hukatwa na kutupwa motoni.

    11 3:11“Mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini nyuma yangu anakuja yeye aliye na uwezo kuliko mimi, ambaye sistahili hata kuvichukua viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu 3:11 …kwa Roho Mtakatifu hapa ina maana ya katika Roho Mtakatifu. na kwa moto. 12 3:12Pepeto lake liko mkononi mwake, naye atasafisha sakafu yake ya kupuria, na kuikusanya ngano ghalani na kuyateketeza makapi kwa moto usiozimika.”

    Yesu Abatizwa (Marko 1:9-11; Luka 3:21-22)

    13 3:13Kisha Yesu akaja kutoka Galilaya mpaka Mto Yordani ili Yohana ambatize. 14 3:14Lakini Yohana akajitahidi kumzuia, akimwambia, “Mimi ninahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu nikubatize?”

    15 3:15Lakini Yesu akamjibu, “Kubali hivi sasa, kwa maana ndivyo itupasavyo kwa njia hii kuitimiza haki yote.” Hivyo Yohana akakubali.

    16 3:16Naye Yesu alipokwisha kubatizwa, mara alipotoka ndani ya maji, ghafula mbingu zikafunguka, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua na kutulia juu yake. 17 3:17Nayo sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa, ambaye ninapendezwa sana naye.”

    4Kujaribiwa Kwa Yesu (Marko 1:12-13; Luka 4:1-13)

    1 4:1Kisha Yesu akaongozwa na Roho Mtakatifu kwenda nyikani ili akajaribiwe na ibilisi. 2 4:2Baada ya kufunga siku arobaini usiku na mchana, hatimaye akaona njaa. 3 4:3Mjaribu akamjia na kumwambia, “Ikiwa wewe ndiye Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.”

    4 4:4Lakini Yesu akajibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.’ ”

    5 4:5Ndipo ibilisi akamchukua Yesu mpaka mji mtakatifu na kumweka juu ya mnara mrefu wa Hekalu, 6 4:6akamwambia, “Kama wewe ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini. Kwa kuwa imeandikwa:

    “ ‘Atakuagizia malaika zake, nao watakuchukua mikononi mwao ili usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.’ ”

    7 4:7Yesu akamjibu, “Pia imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’ ”

    8 4:8Kwa mara nyingine, ibilisi akamchukua Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu na kumwonyesha falme zote za dunia na fahari zake, 9 4:9kisha akamwambia, “Nitakupa hivi vyote kama ukinisujudia na kuniabudu.”

    10 4:10Yesu akamwambia, “Ondoka mbele yangu, Shetani! Kwa maana imeandikwa, ‘Mwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’ ”

    11 4:11Ndipo ibilisi akamwacha, nao malaika wakaja na kumhudumia.

    Yesu Aanza Kuhubiri (Marko 1:14-15; Luka 4:14-15)

    12 4:12Yesu aliposikia kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa ametiwa gerezani, alirudi Galilaya. 13 4:13Akaondoka Nazareti akaenda kuishi Kapernaumu, mji ulioko karibu na bahari, katika mipaka ya nchi ya Zabuloni na Naftali, 14 4:14ili kutimiza unabii wa nabii Isaya, kama alivyosema:

    15 4:15“Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, kwenye njia ya kuelekea baharini, ngʼambo ya Yordani, Galilaya ya watu wa Mataifa: 16 4:16watu wale waliokaa gizani wameona nuru kuu; nao wale walioishi katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewazukia.”

    17 4:17Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.”

    Yesu Awaita Wanafunzi Wake Wa Kwanza (Marko 1:16-20; Luka 5:1-11)

    18 4:18Yesu alipokuwa anatembea kando ya Bahari ya Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake. Walikuwa wakizitupa nyavu zao baharini kwa kuwa wao walikuwa wavuvi. 19 4:19Yesu akawaambia, “Njooni, nifuateni nami nitawafanya mwe wavuvi wa watu.” 20 4:20Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

    21 4:21Alipoendelea mbele kutoka pale, akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, wakiwa wamekaa kwenye mashua pamoja na baba yao Zebedayo, wakizitengeneza nyavu zao. Yesu akawaita. 22 4:22Nao mara wakaiacha mashua yao, pamoja na baba yao, wakamfuata.

    Yesu Ahubiri Na Kuponya Wagonjwa (Luka 6:17-19)

    23 4:23Yesu akapita katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi miongoni mwa watu. 24 4:24Kwa hiyo sifa zake zikaenea sehemu zote za Shamu, nao watu wakamletea wote waliokuwa na magonjwa mbalimbali na maumivu, waliopagawa na pepo wachafu, wenye kifafa na waliopooza, naye akawaponya. 25 4:25Makutano makubwa ya watu yakawa yanamjia kutoka Galilaya, Dekapoli, 4:25 Yaani Miji Kumi. Yerusalemu, Uyahudi na kutoka ngʼambo ya Mto Yordani.

    Mahubiri Ya Yesu Kwenye Mlima (Mathayo 5–7) 5Sifa Za Aliyebarikiwa (Luka 6:20-23)

    1 5:1Basi Yesu alipoona makutano, alipanda mlimani akaketi chini, nao wanafunzi wake wakamjia. 2 5:2Ndipo akaanza kuwafundisha, akisema:

    3 5:3 “Heri walio maskini wa roho, maana Ufalme wa Mbinguni ni wao. 4 5:4 Heri wale wanaohuzunika, maana hao watafarijiwa. 5 5:5 Heri walio wapole, maana hao watairithi nchi. 6 5:6 Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watatoshelezwa. 7 5:7 Heri wenye huruma, maana hao watapata rehema. 8 5:8 Heri walio na moyo safi, maana hao watamwona Mungu. 9 5:9 Heri walio wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu. 10 5:10 Heri wanaoteswa kwa sababu ya haki, maana Ufalme wa Mbinguni ni wao.

    11 5:11 “Heri ninyi watu watakapowashutumu, na kuwatesa na kunena dhidi yenu mabaya ya aina zote kwa uongo kwa ajili yangu. 12 5:12 Furahini na kushangilia kwa maana thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo walivyowatesa manabii waliokuwa kabla yenu.

    Chumvi Na Nuru (Marko 9:50; Luka 14:34-35)

    13 5:13 “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu. Lakini chumvi ikipoteza ladha yake, yawezaje kurudishiwa ladha yake tena? Haifai tena kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

    14 5:14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji uliojengwa kilimani hauwezi kufichika. 15 5:15 Wala watu hawawashi taa na kuifunika kwa bakuli. Badala yake, huiweka kwenye kinara chake, nayo hutoa mwanga kwa kila mtu aliyemo ndani ya ile nyumba. 16 5:16 Vivyo hivyo, nuru yenu iangaze mbele ya watu, ili wapate kuona matendo yenu mema wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

    Kutimiza Sheria

    17 5:17 “Msidhani kwamba nimekuja kufuta Sheria au Manabii; sikuja kuondoa bali kutimiza. 18 5:18 Kwa maana, amin nawaambia, mpaka mbingu na dunia zitakapopita, hakuna hata herufi moja ndogo wala nukta itakayopotea kwa namna yoyote kutoka kwenye Sheria, mpaka kila kitu kiwe kimetimia. 19 5:19 Kwa hiyo, yeyote atakayevunja mojawapo ya amri ndogo kuliko zote ya amri hizi, naye akawafundisha wengine kufanya hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni, lakini yeyote azitendaye na kuzifundisha hizi amri ataitwa mkuu katika Ufalme wa Mbinguni. 20 5:20 Kwa maana nawaambia, haki yenu isipozidi haki ya Mafarisayo na walimu wa sheria, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

    Kuhusu Hasira (Luka 12:57-59)

    21 5:21 “Mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiue. Yeyote atakayeua atapaswa hukumu.’ 22 5:22 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote atakayemkasirikia ndugu yake, atapaswa hukumu. Tena, yeyote atakayemwambia ndugu yake, ‘Raka,’ 5:22 Raka ni neno la Kiaramu ambalo maana yake ni dharau au dhihaka ya hali ya juu. atapaswa kujibu kwa Baraza la Wayahudi. 5:22 Baraza la Wayahudi lilikuwa kundi kuu kabisa la utawala wa Wayahudi lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. Lakini yeyote atakayesema ‘Wewe mpumbavu!’ atapaswa hukumu ya moto wa jehanamu.

    23 5:23 “Kwa hiyo, kama unatoa sadaka yako madhabahuni, ukakumbuka kuwa ndugu yako ana kitu dhidi yako, 24 5:24 iache sadaka yako hapo mbele ya madhabahu. Enda kwanza ukapatane na ndugu yako; kisha urudi na ukatoe sadaka yako.

    25 5:25 “Patana na mshtaki wako upesi wakati uwapo njiani pamoja naye kwenda mahakamani, ili mshtaki wako asije akakutia mikononi mwa hakimu, naye hakimu akakutia mikononi mwa askari, nawe ukatupwa gerezani. 26 5:26 Amin, nakuambia, hautatoka humo hadi uwe umelipa senti ya mwisho.

    Kuhusu Uzinzi

    27 5:27 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Usizini.’ 28 5:28 Lakini mimi nawaambia kwamba, yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. 29 5:29 Jicho lako la kuume likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima ukatupwa jehanamu. 30 5:30 Kama mkono wako wa kuume ukikusababisha kutenda dhambi, ukate, uutupe mbali. Ni afadhali kwako kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako kuliko mwili wako mzima utupwe jehanamu.

    Kuhusu Talaka (Mathayo 19:9; Marko 10:11-12; Luka 16:18)

    31 5:31 “Pia ilinenwa kwamba, ‘Mtu yeyote amwachaye mkewe sharti ampe hati ya talaka.’ 32 5:32 Lakini mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa kosa la uasherati, amfanya mkewe kuwa mzinzi. Na yeyote amwoaye yule mwanamke aliyeachwa, anazini.

    Kuhusu Kuapa

    33 5:33 “Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’ 34 5:34 Lakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu; 35 5:35 au kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. 36 5:36 Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. 37 5:37 ‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu.

    Kuhusu Kulipiza Kisasi (Luka 6:29-30)

    38 5:38 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ 39 5:39 Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. 40 5:40 Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. 41 5:41 Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. 42 5:42 Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa.

    Upendo Kwa Adui (Luka 6:27-28, 32-36)

    43 5:43 “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ 44 5:44 Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, 45 5:45 ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. 46 5:46 Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? 47 5:47 Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? 48 5:48 Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

    6Kuwapa Wahitaji

    1 6:1 “Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

    2 6:2 “Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3 6:3 Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4 6:4 ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

    Kuhusu Maombi (Luka 11:2-4)

    5 6:5 “Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupata thawabu yao. 6 6:6 Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. 7 6:7 Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. 8 6:8 Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.

    9 6:9 “Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba:

    “ ‘Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe. 10 6:10 Ufalme wako uje. Mapenzi yako yafanyike hapa duniani kama huko mbinguni. 11 6:11 Utupatie riziki yetu ya kila siku. 12 6:12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tulivyokwisha kuwasamehe wadeni wetu. 13 6:13 Usitutie majaribuni, bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu [kwa kuwa Ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amen].’ 14 6:14 Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi pia. 15 6:15 Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, naye Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. Kuhusu Kufunga

    16 6:16 “Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu. 17 6:17 Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani na kunawa nyuso zenu 18 6:18 ili kufunga kwenu kusionekane na watu wengine ila Baba yenu aketiye mahali pa siri; naye Baba yenu aonaye sirini atawapa thawabu yenu kwa wazi.

    Akiba Ya Mbinguni (Luka 12:33-34)

    19 6:19 “Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20 6:20 Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21 6:21 Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

    Jicho Ni Taa Ya Mwili (Luka 11:34-36)

    22 6:22 “Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utajaa nuru. 23 6:23 Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ni giza, hilo ni giza kuu namna gani!

    Mungu Na Mali (Luka 16:13; 12:22-31)

    24 6:24 “Hakuna mtu awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali. 6:24 Mali (au Utajiri) hapa inatoka neno Mamoni kwa Kiaramu au Mamona kwa Kiyunani.

    Msiwe Na Wasiwasi

    25 6:25 “Kwa hiyo nawaambia, msisumbukie maisha yenu kwamba mtakula nini au mtakunywa nini; au msumbukie miili yenu kwamba mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? 26 6:26 Waangalieni ndege wa angani; wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27 6:27 Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake anaweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake?

    28 6:28 “Nanyi kwa nini mnajitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29 6:29 Lakini nawaambia, hata Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo ya hayo maua. 30 6:30 Basi ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31 6:31 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ au ‘Tutakunywa nini?’ au ‘Tutavaa nini?’ 32 6:32 Watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kuwa mnahitaji haya yote. 33 6:33 Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake, na haya yote atawapa pia. 34 6:34 Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

    7Kuwahukumu Wengine (Luka 6:37-38, 41-42)

    1 7:1 “Usihukumu ili usije ukahukumiwa. 2 7:2 Kwa maana jinsi unavyowahukumu wengine, ndivyo utakavyohukumiwa, na kwa kipimo kile upimiacho, ndicho utakachopimiwa.

    3 7:3 “Mbona unatazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na wala huoni boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? 4 7:4 Au unawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Acha nitoe kibanzi kwenye jicho lako,’ wakati kuna boriti kwenye jicho lako mwenyewe? 5 7:5 Ewe mnafiki, ondoa boriti ndani ya jicho lako kwanza, ndipo utaweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako.

    6 7:6 “Msiwape mbwa vitu vilivyo vitakatifu; wala msitupie nguruwe lulu zenu. Kama mkifanya hivyo, watazikanyagakanyaga na kisha watawageukia na kuwararua vipande vipande.

    Omba, Tafuta, Bisha (Luka 11:9-13)

    7 7:7 “Ombeni nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtapata; bisheni nanyi mtafunguliwa mlango. 8 7:8 Kwa kuwa kila aombaye hupewa; naye kila atafutaye hupata; na kila abishaye hufunguliwa mlango.

    9 7:9 “Au ni nani miongoni mwenu ambaye mwanawe akimwomba mkate atampa jiwe? 10 7:10 Au mwanawe akimwomba samaki atampa nyoka? 11 7:11 Ikiwa ninyi basi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa vitu vizuri wale wamwombao? 12 7:12 Kwa hiyo chochote mnachotaka mtendewe na watu, ninyi nanyi watendeeni vivyo hivyo. Kwa kuwa hii ndiyo Sheria na Manabii.

    Njia Nyembamba Na Njia Pana

    13 7:13 “Ingieni kupitia mlango mwembamba, kwa maana lango ni pana na njia ni pana ielekeayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa kupitia lango hilo. 14 7:14 Lakini mlango ni mwembamba na njia ni finyu ielekeayo kwenye uzima, nao ni wachache tu waionao.

    Mti Na Tunda Lake (Luka 6:43-44)

    15 7:15 “Jihadharini na manabii wa uongo, wanaowajia wakiwa wamevaa mavazi ya kondoo, lakini ndani ni mbwa mwitu wakali. 16 7:16 Mtawatambua kwa matunda yao. Je, watu huchuma zabibu kwenye miiba, au tini kwenye michongoma? 17 7:17 Vivyo hivyo, mti mwema huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18 7:18 Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19 7:19 Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni. 20 7:20 Hivyo, mtawatambua kwa matunda yao.

    Mwanafunzi Wa Kweli (Luka 13:25-27)

    21 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika Ufalme wa Mbinguni, bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. 22 7:22 Wengi wataniambia siku ile, ‘Bwana, Bwana, hatukutoa unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo wachafu na kufanya miujiza mingi?’ 23 7:23 Ndipo nitakapowaambia wazi, ‘Sikuwajua kamwe. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’

    Msikiaji Na Mtendaji (Luka 6:47-49)

    24 7:24 “Kwa hiyo kila mtu ayasikiaye haya maneno yangu na kuyatenda, ni kama mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25 7:25 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, na upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba. Lakini haikuanguka; kwa sababu msingi wake ulikuwa kwenye mwamba. 26 7:26 Naye kila anayesikia haya maneno yangu wala asiyatende, ni kama mtu mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27 7:27 Mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, nao upepo ukavuma ukaipiga hiyo nyumba, nayo ikaanguka kwa kishindo kikubwa.”

    28 7:28Yesu alipomaliza kusema maneno haya, makutano ya watu wakashangazwa sana na mafundisho yake, 29 7:29kwa sababu alifundisha kama yeye aliye na mamlaka, wala si kama walimu wao wa sheria.

    8Yesu Amtakasa Mwenye Ukoma (Marko 1:40-45; Luka 5:12-16)

    1 8:1Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makutano makubwa ya watu yakamfuata. 2 8:2Mtu mmoja mwenye ukoma akaja na kupiga magoti mbele yake, akasema, “Bwana, kama ukitaka, unaweza kunitakasa.”

    3 8:3Yesu akanyoosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka. Takasika!” Mara yule mtu akatakasika ukoma wake. 4 8:4Kisha Yesu akamwambia, “Hakikisha humwambii mtu yeyote. Lakini nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na utoe sadaka aliyoamuru Mose, ili kuwa ushuhuda kwao.”

    Yesu Amponya Mtumishi Wa Jemadari (Luka 7:1-10)

    5 8:5Yesu alipoingia Kapernaumu, jemadari mmoja alimjia, kumwomba msaada, 6 8:6akisema, “Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani na amepooza, tena ana maumivu makali ya kutisha.”

    7 8:7Yesu akamwambia, “Nitakuja na kumponya.”

    8 8:8Lakini yule jemadari akamwambia, “Bwana, mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona. 9 8:9Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na mwingine nikimwambia, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hivi,’ yeye hufanya.”

    10 8:10Yesu aliposikia maneno haya, alishangaa, akawaambia wale waliomfuata, “Amin, nawaambia, hata katika Israeli sijapata kuona yeyote mwenye imani kubwa namna hii. 11 8:11 Ninawaambia kwamba wengi watatoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaki na Yakobo katika Ufalme wa Mbinguni. 12 8:12 Lakini warithi wa Ufalme watatupwa katika giza la nje, ambako kutakuwako kilio na kusaga meno.”

    13 8:13Kisha Yesu akamwambia yule jemadari, “Nenda na iwe kwako sawasawa na imani yako.” Naye yule mtumishi akapona saa ile ile.

    Yesu Aponya Wengi (Marko 1:29-34; Luka 4:38-41)

    14 8:14Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, akiwa ana homa. 15 8:15Akamgusa mkono wake na homa ikamwacha, naye akainuka na kuanza kumhudumia.

    16 8:16Jioni ile, wakamletea watu wengi waliopagawa na pepo wachafu, naye akawatoa wale pepo wachafu kwa neno lake, na kuwaponya wagonjwa wote. 17 8:17Haya yalifanyika ili litimie lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kwamba:

    “Mwenyewe alitwaa udhaifu wetu na alichukua magonjwa yetu.” Gharama Ya Kumfuata Yesu (Luka 9:57-62)

    18 8:18Yesu alipoona makutano mengi wamemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake wavuke mpaka ngʼambo ya ziwa. 19 8:19Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kokote uendako.”

    20 8:20Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

    21 8:21Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”

    22 8:22Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”

    Yesu Atuliza Dhoruba (Marko 4:35-41; Luka 8:22-25)

    23 8:23Naye alipoingia kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata. 24 8:24Ghafula, kukainuka dhoruba kali baharini hata mashua ikaanza kufunikwa na mawimbi, lakini Yesu alikuwa amelala usingizi. 25 8:25Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakisema, “Bwana, tuokoe! Tunazama!”

    26 8:26Naye Yesu akawaambia, “Kwa nini mnaogopa, enyi wa imani haba?” Kisha akaamka na kukemea dhoruba na mawimbi, nako kukawa shwari kabisa.

    27 8:27Wale watu wakashangaa, wakisema, “Ni mtu wa namna gani huyu? Hata upepo na mawimbi vinamtii!”

    Wawili Wenye Pepo Waponywa (Marko 5:1-20; Luka 8:26-39)

    28 8:28Walipofika ngʼambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili waliopagawa na pepo wachafu walitoka makaburini nao wakakutana naye. Watu hawa walikuwa wakali mno kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kupita njia ile. 29 8:29Wakapiga kelele, “Una nini nasi, Mwana wa Mungu? Umekuja hapa kututesa kabla ya wakati ulioamriwa?”

    30 8:30Mbali kidogo kutoka pale walipokuwa, kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe wakilisha. 31 8:31Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu, “Ukitutoa humu, turuhusu twende kwenye lile kundi la nguruwe.”

    32 8:32Akawaambia, “Nendeni!” Hivyo wakatoka na kuwaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likateremka gengeni kwa kasi, likaingia katika ziwa na kufa ndani ya maji. 33 8:33Wale watu waliokuwa wakiwachunga hao nguruwe wakakimbia wakaingia mjini, wakaeleza yote kuhusu yale yaliyowatokea wale waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu. 34 8:34Kisha watu wote wa mji huo wakatoka kwenda kukutana na Yesu. Nao walipomwona wakamsihi aondoke kwenye nchi yao.

    9Yesu Amponya Mtu Aliyepooza (Marko 2:1-12; Luka 5:17-26)

    1 9:1Yesu akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao. 2 9:2Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.”

    3 9:3Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”

    4 9:4Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? 5 9:5 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 6 9:6 Lakini, ili mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani kusamehe dhambi…” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani kwako.” 7 9:7Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani kwake. 8 9:8Makutano walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu ambaye alikuwa ametoa mamlaka kama haya kwa wanadamu.

    Kuitwa Kwa Mathayo (Marko 2:13-17; Luka 5:27-32)

    9 9:9Yesu alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akaondoka, akamfuata.

    10 9:10Yesu alipokuwa akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na “wenye dhambi” wakaja kula pamoja naye na wanafunzi wake. 11 9:11Mafarisayo walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na ‘wenye dhambi’?”

    12 9:12Lakini Yesu aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 9:13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”

    Yesu Aulizwa Kuhusu Kufunga (Marko 2:18-22; Luka 5:33-39)

    14 9:14Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakaja na kumuuliza Yesu, “Imekuwaje kwamba sisi na Mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”

    15 9:15Yesu akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wawezaje kuomboleza wakati angali pamoja nao? Wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.

    16 9:16 “Hakuna mtu anayeshonea kiraka kipya kwenye nguo iliyochakaa, kwa maana kile kiraka kitachanika kutoka kwenye hiyo nguo, nayo hiyo nguo itachanika zaidi. 17 9:17 Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Kama wakifanya hivyo, viriba vitapasuka nayo divai itamwagika, navyo viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya, na hivyo divai na viriba huwa salama.”

    Mwanamke Aponywa (Marko 5:21-43; Luka 8:40-56)

    18 9:18Yesu alipokuwa akiwaambia mambo haya, mara akaingia kiongozi wa sinagogi akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye atakuwa hai.” 19 9:19Yesu akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye.

    20 9:20Wakati huo huo, mwanamke mmoja, ambaye alikuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaja nyuma ya Yesu, akagusa upindo wa vazi lake, 21 9:21kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”

    22 9:22Yesu akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo mkuu, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa ile ile.

    Yesu Amfufua Binti Wa Kiongozi Wa Sinagogi

    23 9:23Yesu alipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, 24 9:24akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. 25 9:25Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. 26 9:26Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.

    Yesu Awaponya Vipofu

    27 9:27Yesu alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipiga kelele kwa nguvu na kusema, “Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

    28 9:28Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Yesu akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?”

    Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”

    29 9:29Ndipo Yesu akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” 30 9:30Macho yao yakafunguka. Yesu akawaonya vikali, akisema, “Angalieni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” 31 9:31Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.

    Yesu Amponya Mtu Bubu

    32 9:32Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Yesu. 33 9:33Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea. Ule umati wa watu ukastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”

    34 9:34Lakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.”

    Watendakazi Ni Wachache

    35 9:35Yesu akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri habari njema za Ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi. 36 9:36Alipoona makutano, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. 37 9:37Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. 38 9:38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.”

    10Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili (Marko 3:13-19; 6:7-13; Luka 6:12-16; 9:1-6)

    1 10:1Ndipo Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, naye akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu, ili waweze kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.

    2 10:2Haya ndiyo majina ya hao mitume kumi na wawili: wa kwanza, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye; 3 10:3Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; 4 10:4Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.

    5 10:5Hawa kumi na wawili, Yesu aliwatuma akawaagiza: “Msiende miongoni mwa watu wa Mataifa, wala msiingie mji wowote wa Wasamaria. 6 10:6 Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea. 7 10:7 Wakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’ 8 10:8 Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure. 9 10:9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu. 10 10:10 Msichukue mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala jozi ya pili ya viatu, wala fimbo, kwa maana mtendakazi anastahili posho yake.

    11 10:11 “Mji wowote au kijiji chochote mtakapoingia, tafuteni humo mtu anayestahili, nanyi kaeni kwake mpaka mtakapoondoka. 12 10:12 Mkiingia kwenye nyumba, itakieni amani. 13 10:13 Kama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake. La sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi. 14 10:14 Kama mtu yeyote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kungʼuteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo. 15 10:15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa miji ya Sodoma na Gomora kustahimili katika hukumu kuliko mji huo.

    Mateso Yanayokuja (Marko 13:9-13; Luka 21:12-17)

    16 10:16 “Tazama, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua.

    17 10:17 “Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao. 18 10:18 Nanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na kwa watu wa Mataifa. 19 10:19 Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikiria mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo. 20 10:20 Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.

    21 10:21 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe, naye baba atamsaliti mtoto wake. Watoto nao wataasi dhidi ya wazazi wao na kusababisha wauawe. 22 10:22 Watu wote watawachukia kwa ajili ya Jina langu. Lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 23 10:23 Wakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.

    24 10:24 “Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, wala mtumishi hamzidi bwana wake. 25 10:25 Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli, 10:25 Beelzebuli kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu. je, si watawaita zaidi wale wa nyumbani mwake!

    Anayestahili Kuogopwa (Luka 12:2-9)

    26 10:26 “Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. 27 10:27 Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe. Na lile mnalosikia likinongʼonwa masikioni mwenu, lihubirini juu ya nyumba. 28 10:28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu. 10:28 Jehanamu kwa Kiyunani ni Gehena, maana yake ni Kuzimu, yaani motoni. 29 10:29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti moja tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka chini pasipo Baba yenu kujua. 30 10:30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 10:31 Hivyo msiogope; kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa kuliko shomoro wengi.

    32 10:32 “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 10:33 Lakini yeyote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

    Sikuleta Amani, Bali Upanga (Luka 12:51-53; 14:26-27)

    34 10:34 “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35 10:35 Kwa maana nimekuja kumfitini

    “ ‘mtu na babaye, binti na mamaye, mkwe na mama mkwe wake; 36 10:36 nao adui za mtu watakuwa ni wale watu wa nyumbani kwake.’

    37 10:37 “Yeyote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Yeyote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. 38 10:38 Tena yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu. 39 10:39 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata.

    Watakaopokea Thawabu (Marko 9:41)

    40 10:40 “Mtu yeyote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi, na yeyote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma. 41 10:41 Mtu yeyote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii atapokea thawabu ya nabii, naye mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki atapokea thawabu ya mwenye haki. 42 10:42 Kama yeyote akimpa hata kikombe cha maji baridi mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, nawaambia, hataikosa thawabu yake.”

    11Yesu Na Yohana Mbatizaji (Luka 7:18-35)

    1 11:1Baada ya Yesu kumaliza kutoa maagizo kwa wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

    2 11:2Yohana aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Kristo 11:2 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake 3 11:3ili wakamuulize, “Wewe ndiye yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”

    4 11:4Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mnayosikia na kuyaona: 5 11:5 Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. 6 11:6 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”

    7 11:7Wale wanafunzi wa Yohana walipokuwa wanaondoka, Yesu akaanza kusema na makutano kuhusu Yohana Mbatizaji. Akawauliza, “Mlipokwenda kule nyikani, mlikwenda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo? 8 11:8 Kama sivyo, mlikwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha, watu wanaovaa mavazi ya kifahari wako katika majumba ya wafalme. 9 11:9 Basi mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii. 10 11:10 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:

    “ ‘Tazama nitamtuma mjumbe wangu mbele yako, atakayetengeneza njia mbele yako.’ 11 11:11 Amin, nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji. Lakini aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mbinguni ni mkuu kuliko Yohana. 12 11:12 Tangu siku za Yohana Mbatizaji hadi sasa, Ufalme wa Mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wanauteka. 13 11:13 Kwa maana manabii wote na Sheria walitabiri mpaka wakati wa Yohana. 14 11:14 Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye ndiye yule Eliya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja. 15 11:15 Yeye aliye na masikio, na asikie.

    16 11:16 “Lakini kizazi hiki nikifananishe na nini? Kinafanana na watoto waliokaa sokoni wakiwaita wenzao na kuwaambia,

    17 11:17 “ ‘Tuliwapigia filimbi, lakini hamkucheza; tuliwaimbia nyimbo za maombolezo, lakini hamkuomboleza.’ 18 11:18 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuja, alikuwa hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’ 19 11:19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli kwa matendo yake.” Onyo Kwa Miji Isiyotubu (Luka 10:13-15)

    20 11:20Ndipo Yesu akaanza kushutumu miji ambamo alifanya miujiza yake mingi kuliko kwingine, kwa maana watu wake hawakutubu. 21 11:21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 22 11:22 Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 23 11:23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu. 11:23 Kuzimu ni Mahali pa wafu. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungalikuwepo hadi leo. 24 11:24 Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”

    Hakuna Amjuaye Baba Ila Mwana (Luka 10:21-22)

    25 11:25Wakati huo Yesu alisema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 11:26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

    27 11:27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.

    Yesu Awaita Waliolemewa Na Mizigo

    28 11:28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 11:29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. 30 11:30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

    12Bwana Wa Sabato (Marko 2:23-28; Luka 6:1-5)

    1 12:1Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. 2 12:2Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”

    3 12:3Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? 4 12:4 Aliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao. 5 12:5 Au hamjasoma katika Sheria kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? 6 12:6 Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. 7 12:7 Kama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia, 8 12:8 kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

    Yesu Anamponya Mtu Aliyepooza Mkono (Marko 3:1-6; Luka 6:6-11)

    9 12:9Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao, 10 12:10na huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”

    11 12:11Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? 12 12:12 Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”

    13 12:13Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. 14 12:14Lakini Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumuua.

    Mtumishi Aliyechaguliwa Na Mungu

    15 12:15Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wagonjwa wao wote, 16 12:16akiwakataza wasiseme yeye ni nani. 17 12:17Hii ilikuwa ili litimie lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kusema:

    18 12:18“Tazama mtumishi wangu niliyemchagua, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Nitaweka Roho wangu juu yake, naye atatangaza haki kwa mataifa. 19 12:19Hatagombana wala hatapiga kelele, wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani. 20 12:20Mwanzi uliopondeka hatauvunja, na utambi unaofuka moshi hatauzima, mpaka atakapoifanya haki ishinde. 21 12:21Katika Jina lake mataifa wataweka tumaini lao.” Yesu Na Beelzebuli (Marko 3:20-30; Luka 11:14-23)

    22 12:22Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, na alikuwa kipofu na bubu. Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona. 23 12:23Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”

    24 12:24Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli, 12:24 Beelzebuli au Beelzebubu; pia 12:27. mkuu wa pepo wachafu.”

    25 12:25Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, hivyo akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja waliogawanyika dhidi yao wenyewe hawawezi kusimama. 26 12:26 Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? 27 12:27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. 28 12:28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.

    29 12:29 “Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.

    30 12:30 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami, na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. 31 12:31 Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. 32 12:32 Mtu yeyote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini yeyote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.

    Mti Na Matunda Yake (Luka 6:43-45)

    33 12:33 “Ufanye mti kuwa mzuri, nayo matunda yake yatakuwa mazuri. Au ufanye mti kuwa mbaya, na matunda yake yatakuwa mabaya. Kwa maana mti hutambulika kwa matunda yake. 34 12:34 Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake. 35 12:35 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake. 36 12:36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena. 37 12:37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.”

    Ishara Ya Yona (Marko 8:11-12; Luka 11:29-32)

    38 12:38Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”

    39 12:39Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. 40 12:40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumi 12:40 Nyangumi ni samaki mkubwa sana. kwa siku tatu, usiku na mchana, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana. 41 12:41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu; kwa maana wao walitubu waliposikia mahubiri ya Yona. Na tazama, hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona. 42 12:42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki. Kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni. Na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.”

    Mafundisho Kuhusu Pepo Mchafu (Luka 11:24-26)

    43 12:43 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. 44 12:44 Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba yangu nilikotoka.’ Naye arudipo huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri. 45 12:45 Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba wabaya kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo. Nayo hali ya mwisho ya yule mtu huwa ni mbaya kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kiovu.”

    Mama Na Ndugu Zake Yesu (Marko 3:31-35; Luka 8:19-21)

    46 12:46Wakati alikuwa angali anazungumza na makutano, mama yake na ndugu zake wakasimama nje wakitaka kuongea naye. 47 12:47Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”

    48 12:48Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?” 49 12:49Akawanyooshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu zangu! 50 12:50 Kwa maana yeyote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”

    13Mfano Wa Mpanzi (Marko 4:1-9; Luka 8:4-8)

    1 13:1Siku iyo hiyo Yesu akatoka nje ya nyumba, akaketi kando ya bahari. 2 13:2Umati mkubwa mno wa watu ukakusanyika kumzunguka, hata ikabidi aingie katika chombo na kuketi humo, nao watu wote wakawa wamesimama ukingoni mwa bahari. 3 13:3Ndipo akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema: “Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake. 4 13:4 Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, nao ndege wakaja na kuzila. 5 13:5 Nyingine zilianguka kwenye ardhi yenye mwamba isiyo na udongo wa kutosha. Zikaota haraka, kwa kuwa udongo ulikuwa haba. 6 13:6 Lakini jua lilipozidi, mimea ikanyauka na kukauka kwa kuwa mizizi yake haikuwa na kina. 7 13:7 Mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, nayo miiba hiyo ikakua, ikaisonga hiyo mimea. 8 13:8 Mbegu nyingine zilianguka kwenye udongo mzuri ambapo zilitoa mazao, nyingine mara mia moja, nyingine mara sitini, na nyingine mara thelathini. 9 13:9 Mwenye masikio ya kusikia, na asikie.”

    Sababu Ya Kufundisha Kwa Mifano (Marko 4:10-12; Luka 8:9-10)

    10 13:10Wanafunzi wake wakamwendea, wakamuuliza, “Kwa nini unasema na watu kwa mifano?”

    11 13:11Akawajibu, “Ninyi mmepewa kuzifahamu siri za Ufalme wa Mbinguni, lakini wao hawajapewa. 12 13:12 Kwa maana yule aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa. 13 13:13 Hii ndiyo sababu nasema nao kwa mifano:

    “Ingawa wanatazama, hawaoni; wanasikiliza, lakini hawasikii, wala hawaelewi. 14 13:14 Kwao unatimia ule unabii wa Isaya aliposema: “ ‘Hakika mtasikiliza lakini hamtaelewa; na pia mtatazama lakini hamtaona. 15 13:15 Kwa kuwa mioyo ya watu hawa imekuwa migumu; hawasikii kwa masikio yao, na wamefumba macho yao. Wasije wakaona kwa macho yao, na wakasikiliza kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, na kugeuka nami nikawaponya.’ 16 13:16 Lakini heri macho yenu kwa sababu yanaona, na heri masikio yenu kwa sababu yanasikia. 17 13:17 Amin, nawaambia, manabii wengi na wenye haki walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia. Maelezo Ya Mfano Wa Mbegu (Marko 4:13-20; Luka 8:11-15)

    18 13:18 “Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi: 19 13:19 Mtu yeyote anaposikia neno la Ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia. 20 13:20 Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na mara hulipokea kwa furaha. 21 13:21 Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, yeye mara huchukizwa. 22 13:22 Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu alisikiaye neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. 23 13:23 Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.”

    Mfano Wa Magugu

    24 13:24Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25 13:25 Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. 26 13:26 Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea.

    27 13:27 “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’

    28 13:28 “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’

    “Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayangʼoe?’

    29 13:29 “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyangʼoe, kwa maana wakati mkingʼoa magugu mnaweza mkangʼoa na ngano pamoja nayo. 30 13:30 Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”

    Mfano Wa Mbegu Ya Haradali (Marko 4:30-32; Luka 13:18-19)

    31 13:31Akawaambia mfano mwingine, akasema, “Ufalme wa Mbinguni ni kama punje ya haradali, ambayo mtu aliichukua, akaipanda shambani mwake. 32 13:32 Ingawa mbegu hiyo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini inapokua ni mmea mkubwa kuliko yote ya bustanini, nao huwa mti mkubwa, hadi ndege wa angani wanakuja na kutengeneza viota katika matawi yake.”

    Mfano Wa Chachu (Luka 13:20-21)

    33 13:33Akawaambia mfano mwingine, “Ufalme wa Mbinguni unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga mpaka wote ukaumuka.”

    Sababu Ya Yesu Kutumia Mifano (Marko 4:33-34)

    34 13:34Yesu alinena mambo haya yote kwa makutano kwa mifano. Wala hakuwaambia lolote pasipo mfano. 35 13:35Hii ilikuwa ili kutimiza lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii aliposema:

    “Nitafungua kinywa changu niseme nao kwa mifano; nitahubiri mambo yaliyofichika tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.” Ufafanuzi Wa Mfano Wa Magugu

    36 13:36Kisha Yesu akaagana na makutano, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamjia wakamwambia, “Tueleze maana ya ule mfano wa magugu shambani.”

    37 13:37Akawaambia, “Aliyepanda mbegu nzuri ni Mwana wa Adamu. 38 13:38 Shamba ni ulimwengu na mbegu nzuri ni wana wa Ufalme. Magugu ni wana wa yule mwovu. 39 13:39 Yule adui aliyepanda magugu ni ibilisi. Mavuno ni mwisho wa dunia, nao wavunaji ni malaika.

    40 13:40 “Kama vile magugu yangʼolewavyo na kuchomwa motoni, ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. 41 13:41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka Ufalme wake kila kitu kinachosababisha dhambi na watenda maovu wote. 42 13:42 Nao watawatupa katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno. 43 13:43 Ndipo wenye haki watangʼaa kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Yeye aliye na masikio, na asikie.

    Mfano Wa Hazina Iliyofichwa Na Lulu

    44 13:44 “Ufalme wa Mbinguni unafanana na hazina iliyofichwa shambani, ambayo mtu mmoja alipoiona akaificha tena. Kisha katika furaha yake, akaenda akauza vyote alivyokuwa navyo, akalinunua lile shamba.”

    45 13:45 “Tena, Ufalme wa Mbinguni unafanana na mfanyabiashara aliyekuwa akitafuta lulu safi. 46 13:46 Alipoipata lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza vyote alivyokuwa navyo akainunua.”

    Mfano Wa Wavu

    47 13:47 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama wavu wa kuvua samaki uliotupwa baharini ukavua samaki wa kila aina. 48 13:48 Ulipojaa, wavuvi wakavuta pwani, wakaketi na kukusanya samaki wazuri kuwaweka kwenye vyombo safi, lakini wale samaki wabaya wakawatupa. 49 13:49 Hivi ndivyo itakavyokuwa wakati wa mwisho wa dunia. Malaika watakuja na kuwatenganisha watu waovu na watu wenye haki. 50 13:50 Nao watawatupa hao waovu katika tanuru la moto ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.”

    51 13:51Yesu akauliza, “Je, mmeyaelewa haya yote?”

    Wakamjibu, “Ndiyo.”

    52 13:52Akawaambia, “Basi kila mwalimu wa sheria aliyefundishwa elimu ya Ufalme wa Mbinguni ni kama mwenye nyumba anayetoa kutoka ghala yake mali mpya na mali ya zamani.”

    Yesu Akataliwa Nazareti (Marko 6:1-6; Luka 4:16-30)

    53 13:53Yesu alipomaliza kutoa mifano hii, akaondoka. 54 13:54Alipofika mji wa kwao, akawafundisha watu katika sinagogi lao. Nao wakastaajabu, wakauliza, “Mtu huyu amepata wapi hekima hii na uwezo huu wa kufanya miujiza?” 55 13:55“Huyu si yule mwana wa seremala? Mama yake si yeye aitwaye Maria, nao ndugu zake si Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda? 56 13:56Nao dada zake wote, hawako hapa pamoja nasi? Mtu huyu amepata wapi basi mambo haya yote?” 57 13:57Wakachukizwa naye.

    Lakini Yesu akawaambia, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani kwake.”

    58 13:58Naye hakufanya miujiza mingi huko kwa sababu ya kutokuamini kwao.

    14Yohana Mbatizaji Akatwa Kichwa (Marko 6:14-29; Luka 9:7-9)

    1 14:1Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Yesu, 2 14:2akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yohana Mbatizaji; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”

    3 14:3Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, 4 14:4kwa kuwa Yohana alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.” 5 14:5Herode alitaka sana kumuua Yohana, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii.

    6 14:6Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti wa Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria, akamfurahisha sana Herode, 7 14:7kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. 8 14:8Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” 9 14:9Mfalme akasikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake. 10 14:10Hivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani. 11 14:11Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake. 12 14:12Wanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu.

    Yesu Alisha Wanaume 5,000 (Marko 6:30-44; Luka 9:10-17; Yohana 6:1-14)

    13 14:13Yesu aliposikia yaliyokuwa yametukia, aliondoka kwa chombo akaenda mahali pasipo na watu ili awe peke yake. Lakini watu walipopata habari, wakamfuata kwa miguu kupitia nchi kavu kutoka miji. 14 14:14Yesu alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia na akawaponya wagonjwa wao.

    15 14:15Ilipofika jioni, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na muda sasa umekwisha. Waage makutano ili waende zao vijijini wakajinunulie chakula.”

    16 14:16Yesu akawaambia, “Hakuna sababu ya wao kuondoka. Ninyi wapeni chakula.”

    17 14:17Wakamjibu, “Tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”

    18 14:18Akawaambia, “Nileteeni hivyo vitu hapa.” 19 14:19Yesu akaagiza makutano wakae chini kwenye nyasi. Akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi, nao wanafunzi wakawagawia makutano. 20 14:20Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu kumi na viwili. 21 14:21Idadi ya watu waliokula walikuwa wanaume wapatao 5,000, bila kuhesabu wanawake na watoto.

    Yesu Atembea Juu Ya Maji (Marko 6:45-52; Yohana 6:15-21)

    22 14:22Mara Yesu akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda ngʼambo ya bahari, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano. 23 14:23Baada ya kuwaaga, akaenda zake mlimani peke yake kuomba. Jioni ilipofika, Yesu alikuwa huko peke yake. 24 14:24Wakati huo ile mashua ilikuwa mbali kutoka nchi kavu ikisukwasukwa na mawimbi, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho.

    25 14:25Wakati wa zamu ya nne ya usiku, 14:25 Zamu ya nne ya usiku ni kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi. Yesu akawaendea wanafunzi wake akiwa anatembea juu ya maji. 26 14:26Wanafunzi wake walipomwona akitembea juu ya maji, waliingiwa na hofu kuu, wakasema, “Ni mzimu.” Wakapiga yowe kwa kuogopa.

    27 14:27Lakini mara Yesu akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope.”

    28 14:28Petro akamjibu, “Bwana, ikiwa ni wewe, niambie nije kwako nikitembea juu ya maji.”

    29 14:29Yesu akamwambia, “Njoo.”

    Basi Petro akatoka kwenye chombo, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. 30 14:30Lakini alipoona upepo mkali aliingiwa na hofu, naye akaanza kuzama, huku akipiga kelele, “Bwana, niokoe!”

    31 14:31Mara Yesu akaunyoosha mkono wake na kumshika, akamwambia, “Wewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka?”

    32 14:32Nao walipoingia ndani ya mashua, upepo ukakoma. 33 14:33Ndipo wote waliokuwa ndani ya ile mashua wakamwabudu Yesu, wakisema, “Hakika, wewe ndiwe Mwana wa Mungu.”

    Yesu Awaponya Wagonjwa Genesareti (Marko 6:53-56)

    34 14:34Walipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti. 35 14:35Watu wa eneo lile walipomtambua Yesu, walipeleka habari sehemu zote za jirani. Watu wakamletea wagonjwa wao wote, 36 14:36wakamsihi awaruhusu wagonjwa waguse tu pindo la vazi lake, nao wote waliomgusa, wakaponywa.

    15Mapokeo Ya Wazee (Marko 7:1-13)

    1 15:1Ndipo baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamjia Yesu kutoka Yerusalemu na kumuuliza, 2 15:2“Mbona wanafunzi wako wanakiuka mapokeo ya wazee? Kwa maana wao hawanawi mikono yao kabla ya kula!”

    3 15:3Yesu akawajibu, “Mbona ninyi mnavunja amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? 4 15:4 Kwa maana Mungu alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’ 5 15:5 Lakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia kimewekwa wakfu kwa Mungu,’ 6 15:6 basi hana tena sababu ya kumheshimu baba yake nacho. Basi kwa ajili ya mafundisho yenu mnavunja amri ya Mungu. 7 15:7 Ninyi wanafiki! Isaya alikuwa sawa alipotabiri juu yenu kwamba:

    8 15:8 “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami. 9 15:9 Huniabudu bure; nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’ ” Vitu Vitiavyo Unajisi (Marko 7:14-23)

    10 15:10Yesu akaita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni na mwelewe: 11 15:11 kinachomfanya mtu kuwa najisi mbele za Mungu si kile kiingiacho kinywani mwake, bali ni kile kitokacho kinywani mwake.”

    12 15:12Kisha wanafunzi wake wakamjia na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa sana waliposikia yale uliyosema?”

    13 15:13Akawajibu, “Kila pando ambalo Baba yangu wa mbinguni hakulipanda, litangʼolewa. 14 15:14 Waacheni; wao ni viongozi vipofu, wanaoongoza vipofu. Kama kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, wote wawili watatumbukia shimoni.”

    15 15:15Petro akasema, “Tueleze maana ya huu mfano.”

    16 15:16Yesu akawauliza, “Je, bado ninyi hamfahamu? 17 15:17 Je, hamwelewi kwamba chochote kiingiacho kinywani huenda tumboni, na hatimaye hutolewa nje kikiwa uchafu? 18 15:18 Lakini kitokacho kinywani hutoka moyoni, na hiki ndicho kimtiacho mtu unajisi. 19 15:19 Kwa maana ndani ya moyo hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati, wizi, ushahidi wa uongo na masingizio. 20 15:20 Haya ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula bila kunawa mikono hakumtii mtu unajisi.”

    Imani Ya Mwanamke Mkanaani (Marko 7:24-30)

    21 15:21Yesu aliondoka mahali pale, akaenda sehemu za Tiro na Sidoni. 22 15:22Mwanamke mmoja Mkanaani aliyeishi sehemu jirani na hizo akaja kwake akilia, akasema, “Nihurumie, Ee Bwana, Mwana wa Daudi! Binti yangu amepagawa na pepo mchafu, na anateseka sana.”

    23 15:23Lakini Yesu hakumjibu neno. Hivyo wanafunzi wake wakamwendea na kumsihi sana, wakisema, “Mwambie aende zake, kwa maana anaendelea kutupigia kelele.”

    24 15:24Yesu akajibu, “Nimetumwa tu kwa ajili ya kondoo wa Israeli waliopotea.”

    25 15:25Lakini yule mwanamke akaja, akapiga magoti mbele ya Yesu, akasema, “Bwana, nisaidie!”

    26 15:26Yesu akajibu, “Si haki kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

    27 15:27Yule mwanamke akajibu, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza za bwana zao.”

    28 15:28Ndipo Yesu akamwambia, “Mwanamke, imani yako ni kubwa! Iwe kwako kama unavyotaka.” Naye binti yake akapona tangu saa ile.

    Yesu Aponya Watu Wengi

    29 15:29Yesu akaondoka na kwenda kando ya Bahari ya Galilaya. Kisha akapanda mlimani, akaketi huko. 30 15:30Umati mkubwa wa watu ukamjia, wakiwaleta vilema, vipofu, viwete, bubu na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; naye akawaponya. 31 15:31Hao watu wakashangaa walipoona bubu wakisema, vilema wakipona, viwete wakitembea na vipofu wakiona, wakamtukuza Mungu wa Israeli.

    Yesu Alisha Watu Elfu Nne (Marko 8:1-10)

    32 15:32Kisha Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia, “Ninauhurumia huu umati wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa pamoja nami kwa muda wa siku tatu, na hawana chakula chochote. Nami sipendi kuwaaga wakiwa na njaa, wasije wakazimia njiani.”

    33 15:33Wanafunzi wake wakasema, “Tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha umati huu wa watu mkubwa namna hii, nasi tuko nyikani?”

    34 15:34Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi?”

    Wakamjibu, “Tunayo mikate saba na visamaki vichache.”

    35 15:35Yesu akawaambia ule umati wa watu waketi chini. 36 15:36Kisha akachukua ile mikate saba na wale samaki, naye akiisha kumshukuru Mungu, akavimega na kuwapa wanafunzi wake, nao wakawapa ule umati wa watu. 37 15:37Wote wakala na kushiba. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba. 38 15:38Idadi ya watu walikuwa wanaume 4,000, bila kuhesabu wanawake na watoto. 39 15:39Baada ya kuaga ule umati wa watu, Yesu aliingia katika mashua, akaenda sehemu za Magadani. 15:39 Magadani ni Magdala, mji wa Galilaya, kama kilomita 16 kusini mwa Kapernaumu.

    16Mafarisayo Wadai Ishara (Marko 8:11-13; Luka 12:54-56)

    1 16:1Mafarisayo na Masadukayo wakamjia Yesu na kumjaribu kwa kumwomba awaonyeshe ishara kutoka mbinguni.

    2 16:2Yesu akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’ 3 16:3 Nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua dalili za nyakati. 4 16:4 Kizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Yesu akawaacha, akaenda zake.

    Chachu Ya Mafarisayo Na Masadukayo (Marko 8:14-21)

    5 16:5Wanafunzi wake walipofika ngʼambo ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate. 6 16:6Yesu akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”

    7 16:7Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”

    8 16:8Yesu, akifahamu majadiliano yao, akauliza, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate? 9 16:9 Je, bado hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano iliyolisha watu 5,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya? 10 16:10 Au ile mikate saba iliyolisha watu 4,000 na idadi ya vikapu vingapi vya mabaki mlivyokusanya? 11 16:11 Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” 12 16:12Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi juu ya chachu ya kutengeneza mikate, bali juu ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

    Petro Amkiri Yesu Kuwa Ni Mwana Wa Mungu (Marko 8:27-30; Luka 9:18-21)

    13 16:13Basi Yesu alipofika katika eneo la Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”

    14 16:14Wakamjibu, “Baadhi husema ni Yohana Mbatizaji; wengine husema ni Eliya; na bado wengine husema ni Yeremia au mmojawapo wa manabii.”

    15 16:15Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”

    16 16:16Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo, 16:16 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. Mwana wa Mungu aliye hai.”

    17 16:17Naye Yesu akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona, 16:17 Bar-Yona ni neno la Kiaramu, maana yake ni Mwana wa Yona. kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni. 18 16:18 Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, hata malango ya Kuzimu hayataweza kulishinda. 19 16:19 Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.” 20 16:20 Kisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.

    Yesu Anatabiri Juu Ya Kifo Chake (Marko 8:31–9:1; Luka 9:22-27)

    21 16:21Tangu wakati huo, Yesu alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini siku ya tatu kufufuliwa.

    22 16:22Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”

    23 16:23Lakini Yesu akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

    24 16:24Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25 16:25 Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. 26 16:26 Kwa maana, je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 27 16:27 Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 28 16:28 Nawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika Ufalme wake.”

    17Yesu Abadilika Sura Mlimani (Marko 9:2-13; Luka 9:28-36)

    1 17:1Siku sita baada ya jambo hili, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao. 2 17:2Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukangʼaa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho. 3 17:3Ghafula wakawatokea mbele yao Mose na Eliya, wakizungumza na Yesu.

    4 17:4Ndipo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”

    5 17:5Petro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililongʼaa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye.”

    6 17:6Wanafunzi waliposikia haya, wakaanguka chini kifudifudi, wakajawa na hofu. 7 17:7Lakini Yesu akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.” 8 17:8Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine yeyote isipokuwa Yesu.

    9 17:9Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaagiza, “Msimwambie mtu yeyote mambo mliyoyaona hapa, mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”

    10 17:10Wale wanafunzi wakamuuliza, “Kwa nini basi walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?”

    11 17:11Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya lazima aje kwanza, naye atatengeneza mambo yote. 12 17:12 Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.” 13 17:13Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yohana Mbatizaji.

    Yesu Amponya Kijana Mwenye Pepo (Marko 9:14-29; Luka 9:37-43)

    14 17:14Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema, 15 17:15“Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. 16 17:16Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”

    17 17:17Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.” 18 17:18Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

    19 17:19Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”

    20 17:20Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [ 21 17:21 Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]”

    22 17:22Siku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. 23 17:23 Nao watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika sana.

    Yesu Na Petro Watoa Kodi Ya Hekalu

    24 17:24Baada ya Yesu na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu 17:24 Kodi ya Hekalu ilikuwa didrachmas, yaani drakma mbili, ambazo ni sawa na nusu shekeli. wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”

    25 17:25Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Yesu akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”

    26 17:26Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Yesu akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27 17:27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”

    18Aliye Mkuu Katika Ufalme Wa Mbinguni (Marko 9:33-37; Luka 9:46-48)

    1 18:1Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni?”

    2 18:2Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao. 3 18:3Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipookoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni. 4 18:4 Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni.

    5 18:5 “Yeyote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi. 6 18:6 Lakini kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa katika kilindi cha bahari.

    Kujaribiwa Ili Kutenda Dhambi (Marko 9:42-48; Luka 17:1-2)

    7 18:7 “Ole kwa ulimwengu kwa sababu ya yale mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi! Mambo hayo lazima yawepo, lakini ole wake mtu yule ambaye huyasababisha. 8 18:8 Ikiwa mkono wako au mguu wako unakusababisha utende dhambi, ukate na uutupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa huna mkono mmoja au mguu mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. 9 18:9 Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe, ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa katika moto wa jehanamu.

    Mfano Wa Kondoo Aliyepotea (Luka 15:3-7)

    10 18:10 “Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [ 11 18:11 Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea.]

    12 18:12 “Mwaonaje? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea? 13 18:13 Naye akishampata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea. 14 18:14 Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmojawapo wa hawa wadogo apotee.

    Ndugu Yako Akikukosea

    15 18:15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. 16 18:16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. 17 18:17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.

    18 18:18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.

    19 18:19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. 20 18:20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”

    Kusamehe

    21 18:21Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”

    22 18:22Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

    Mfano Wa Mtumishi Asiyesamehe

    23 18:23 “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. 24 18:24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta 18:24 Talanta moja ni sawa na mshahara wa kibarua wa miaka 15. 10,000, aliletwa kwake. 25 18:25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.

    26 18:26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ 27 18:27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.

    28 18:28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari 18:28 Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja. mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’

    29 18:29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’

    30 18:30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. 31 18:31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.

    32 18:32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. 33 18:33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ 34 18:34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.

    35 18:35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”

    19Yesu Afundisha Kuhusu Talaka (Marko 10:1-12)

    1 19:1Yesu alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Uyahudi, ngʼambo ya Mto Yordani. 2 19:2Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akawaponya huko.

    3 19:3Baadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu, wakamuuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?”

    4 19:4Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mwanaume na mwanamke, 5 19:5 naye akasema, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’? 6 19:6 Hivyo si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

    7 19:7Wakamuuliza, “Kwa nini basi Mose aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”

    8 19:8Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. 9 19:9 Mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”

    10 19:10Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”

    11 19:11Yesu akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu. 12 19:12 Kwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo; wengine wamefanywa matowashi na wanadamu; na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.”

    Yesu Awabariki Watoto Wadogo (Marko 10:13-16; Luka 18:15-17)

    13 19:13Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.

    14 19:14Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.” 15 19:15Naye akaweka mikono yake juu yao, na akaondoka huko.

    Kijana Tajiri (Marko 10:17-31; Luka 18:18-30)

    16 19:16Mtu mmoja akamjia Yesu na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”

    17 19:17Yesu akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”

    18 19:18Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?”

    Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19 19:19 waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.”

    20 19:20Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”

    21 19:21Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

    22 19:22Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

    Hatari Za Utajiri

    23 19:23Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. 24 19:24 Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

    25 19:25Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

    26 19:26Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”

    27 19:27Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata! Tutapata nini basi?”

    28 19:28Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake kitukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29 19:29 Kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu zake wa kiume au wa kike, baba au mama, watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na ataurithi uzima wa milele. 30 19:30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

    20Mfano Wa Wafanyakazi Katika Shamba La Mizabibu

    1 20:1 “Kwa maana Ufalme wa Mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba aliyetoka alfajiri ili kwenda kuajiri vibarua kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu. 2 20:2 Baada ya kukubaliana na hao vibarua kuwalipa ujira wa dinari 20:2 Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja. moja kwa siku, akawapeleka kwenye shamba lake la mizabibu.

    3 20:3 “Mnamo saa tatu akatoka tena, akawakuta wengine wamesimama sokoni bila kazi. 4 20:4 Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu, nami nitawalipa chochote kilicho haki yenu.’ 5 20:5 Kwa hiyo wakaenda.

    “Akatoka tena mnamo saa sita na pia saa tisa akafanya vivyo hivyo. 6 20:6 Mnamo saa kumi na moja akatoka tena akawakuta wengine bado wamesimama bila kazi. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa kutwa nzima pasipo kufanya kazi?’

    7 20:7 “Wakamjibu, ‘Ni kwa sababu hakuna yeyote aliyetuajiri.’

    “Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu.’

    8 20:8 “Ilipofika jioni, yule mwenye shamba la mizabibu akamwambia msimamizi, ‘Waite hao vibarua na uwalipe ujira wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho na kuishia na wale walioajiriwa kwanza.’

    9 20:9 “Wale vibarua walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakaja na kila mmoja wao akapokea dinari moja. 10 20:10 Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja. 11 20:11 Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba, 12 20:12 wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’

    13 20:13 “Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja? 14 20:14 Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe. 15 20:15 Je, sina haki yangu kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’

    16 20:16 “Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”

    Yesu Atabiri Tena Kuhusu Kifo Chake (Marko 10:32-34; Luka 18:31-34)

    17 20:17Basi Yesu alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua kando wale wanafunzi wake kumi na wawili na kuwaambia, 18 20:18 “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa sheria. Nao watamhukumu kifo 19 20:19 na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulubisha msalabani. Naye atafufuliwa siku ya tatu!”

    Ombi La Mama Yake Yakobo Na Yohana (Marko 10:35-45)

    20 20:20Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Yesu pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Yesu amfanyie jambo fulani.

    21 20:21Yesu akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika Ufalme wako.”

    22 20:22Yesu akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?”

    Wakajibu, “Tunaweza.”

    23 20:23Yesu akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba yangu.”

    24 20:24Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili. 25 20:25Lakini Yesu akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonyesha mamlaka yao. 26 20:26 Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27 20:27 naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28 20:28 kama vile ambavyo Mwana wa Adamu hakuja ili kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”

    Yesu Awaponya Vipofu Wawili (Marko 10:46-52; Luka 18:35-43)

    29 20:29Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu ulimfuata. 30 20:30Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapita, wakapiga kelele wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie!”

    31 20:31Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, “Bwana, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”

    32 20:32Yesu akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

    33 20:33Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”

    34 20:34Yesu akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.

    21Yesu Anaingia Yerusalemu Kwa Shangwe (Marko 11:1-11; Luka 19:28-40; Yohana 12:12-19)

    1 21:1Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili, 2 21:2akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu, nanyi mtamkuta punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. 3 21:3 Kama mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara.”

    4 21:4Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema:

    5 21:5“Mwambieni Binti Sayuni, ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mnyenyekevu, naye amepanda punda, juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”

    6 21:6Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza. 7 21:7Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake. 8 21:8Umati mkubwa wa watu ukatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kutoka kwenye miti, wakayatandaza barabarani. 9 21:9Ule umati wa watu uliomtangulia na ule uliomfuata ukapiga kelele ukisema,

    “Hosana, 21:9 Kiebrania kusema Okoa, basi likawa neno la shangwe. Mwana wa Daudi!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Hosana juu mbinguni!”

    10 21:10Yesu alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?”

    11 21:11Ule umati wa watu ukajibu, “Huyu ni Yesu, yule nabii kutoka Nazareti katika Galilaya.”

    Yesu Atakasa Hekalu (Marko 11:15-19; Luka 19:45-48; Yohana 2:13-22)

    12 21:12Yesu akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 13 21:13Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyangʼanyi.”

    14 21:14Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. 15 21:15Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walipoona mambo ya ajabu aliyofanya na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika.

    16 21:16Wakamuuliza Yesu, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?”

    Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma,

    “ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanyonyao umeamuru sifa’?”

    17 21:17Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.

    Mtini Wanyauka (Marko 11:12-14, 20-24)

    18 21:18Asubuhi na mapema, Yesu alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. 19 21:19Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka.

    20 21:20Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”

    21 21:21Yesu akawajibu, “Amin, nawaambia, kama mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ngʼoka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. 22 21:22 Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”

    Wahoji Kuhusu Mamlaka Ya Yesu (Marko 11:27-33; Luka 20:1-8)

    23 21:23Yesu alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha na kusema, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka hayo?”

    24 21:24Yesu akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Kama mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 25 21:25 Ubatizo wa Yohana, ulitoka wapi? Je, ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

    Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema ulitoka mbinguni atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’ 26 21:26Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yohana kuwa ni nabii.”

    27 21:27Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Sisi hatujui.”

    Naye akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

    Mfano Wa Wana Wawili

    28 21:28 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’

    29 21:29 “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitakwenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda.

    30 21:30 “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitakwenda, bwana,’ lakini hakwenda.

    31 21:31 “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?”

    Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.”

    Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika Ufalme wa Mungu. 32 21:32 Kwa maana Yohana alikuja kwenu kuwaonyesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.

    Mfano Wa Wapangaji Waovu (Marko 12:1-12; Luka 20:9-19)

    33 21:33 “Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo ndani yake na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri kwenda nchi nyingine. 34 21:34 Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake.

    35 21:35 “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe. 36 21:36 Kisha akawatuma kwao watumishi wengine, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile. 37 21:37 Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’

    38 21:38 “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’ 39 21:39 Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.

    40 21:40 “Kwa hiyo, huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?”

    41 21:41Wakamjibu, “Kwa huzuni kuu atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”

    42 21:42Yesu akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba:

    “ ‘Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la pembeni. Bwana ndiye alitenda jambo hili, nalo ni la ajabu machoni petu’?

    43 21:43 “Kwa hiyo ninawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake. 44 21:44 Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”

    45 21:45Viongozi wa Makuhani na Mafarisayo waliposikia mifano ya Yesu, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao. 46 21:46Wakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Yesu kuwa ni nabii.

    22Mfano Wa Karamu Ya Arusi (Luka 14:15-24)

    1 22:1Yesu akasema nao tena kwa mifano, akawaambia, 2 22:2 “Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme mmoja aliyemwandalia mwanawe karamu ya arusi. 3 22:3 Akawatuma watumishi wake kuwaita wale waliokuwa wamealikwa karamuni, lakini wakakataa kuja.

    4 22:4 “Kisha akawatuma watumishi wengine akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa kwamba nimeandaa chakula. Nimekwisha kuchinja mafahali wangu na vinono, karamu iko tayari. Karibuni kwa karamu ya arusi.’

    5 22:5 “Lakini hawakuzingatia, wakaenda zao: huyu shambani mwake na mwingine kwenye biashara zake. 6 22:6 Wengine wao wakawakamata wale watumishi wake, wakawatesa na kuwaua. 7 22:7 Yule mfalme akakasirika sana, akapeleka jeshi lake likawaangamiza wale wauaji na kuuteketeza mji wao kwa moto.

    8 22:8 “Kisha akawaambia watumishi wake, ‘Karamu ya arusi imeshakuwa tayari, lakini wale niliowaalika hawakustahili kuja. 9 22:9 Kwa hiyo nendeni katika njia panda mkamwalike karamuni yeyote mtakayemwona.’ 10 22:10 Wale watumishi wakaenda barabarani, wakawakusanya watu wote waliowaona, wema na wabaya. Ukumbi wa arusi ukajaa wageni.

    11 22:11 “Lakini mfalme alipoingia ndani ili kuwaona wageni, akamwona mle mtu mmoja ambaye hakuwa amevaa vazi la arusi. 12 22:12 Mfalme akamuuliza, ‘Rafiki, uliingiaje humu bila vazi la arusi?’ Yule mtu hakuwa na la kusema.

    13 22:13 “Ndipo mfalme akawaambia watumishi wake, ‘Mfungeni mikono na miguu mkamtupe nje, kwenye giza. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.’

    14 22:14 “Kwa maana walioitwa ni wengi, lakini walioteuliwa ni wachache.”

    Kulipa Kodi Kwa Kaisari (Marko 12:13-17; Luka 20:20-26)

    15 22:15Ndipo Mafarisayo wakatoka nje wakaandaa mpango wa kumtega Yesu katika maneno yake. 16 22:16Wakatuma wanafunzi wao kwake pamoja na Maherode. Nao wakasema, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwadilifu na unafundisha njia ya Mungu katika kweli bila kuyumbishwa na mtu wala kuonyesha upendeleo. 17 22:17Tuambie basi, wewe unaonaje? Je, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari, au la?”

    18 22:18Lakini Yesu, akijua makusudi yao mabaya, akawaambia, “Enyi wanafiki, kwa nini mnajaribu kunitega? 19 22:19 Nionyesheni hiyo sarafu inayotumika kwa kulipia kodi.” Wakamletea dinari. 20 22:20Naye akawauliza, “Sura hii ni ya nani? Na maandishi haya ni ya nani?”

    21 22:21Wakamjibu, “Ni vya Kaisari.”

    Basi Yesu akawaambia, “Mpeni Kaisari kilicho cha Kaisari, naye Mungu mpeni kilicho cha Mungu.”

    22 22:22Waliposikia hili, wakashangaa. Hivyo wakamwacha, wakaenda zao.

    Ndoa Na Ufufuo (Marko 12:18-27; Luka 20:27-40)

    23 22:23Siku hiyo hiyo Masadukayo, wale wasemao kwamba hakuna ufufuo wa wafu, wakamjia Yesu na kumuuliza swali, wakisema, 24 22:24“Mwalimu, Mose alisema, ‘Kama mtu akifa bila kuwa na watoto, ndugu yake inampasa amwoe huyo mjane ili ampatie watoto huyo nduguye aliyekufa.’ 25 22:25Basi palikuwa na ndugu saba miongoni mwetu. Yule wa kwanza akaoa mke, naye akafa, na kwa kuwa hakuwa na watoto, akamwachia nduguye yule mjane. 26 22:26Ikatokea vivyo hivyo kwa yule ndugu wa pili, na wa tatu, hadi wote saba. 27 22:27Hatimaye, yule mwanamke naye akafa. 28 22:28Sasa basi, siku ya ufufuo, yeye atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba, kwa kuwa wote walikuwa wamemwoa huyo mwanamke?”

    29 22:29Yesu akawajibu, “Mwapotoka kwa sababu hamjui Maandiko wala uweza wa Mungu. 30 22:30 Wakati wa ufufuo, watu hawataoa wala kuolewa, bali watakuwa kama malaika wa mbinguni. 31 22:31 Lakini kuhusu ufufuo wa wafu, hamjasoma kile Mungu alichowaambia, kwamba, 32 22:32 ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo’? Yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.”

    33 22:33Ule umati wa watu uliposikia hayo, ulishangaa sana kwa mafundisho yake.

    Amri Kuu Kuliko Zote (Marko 12:28-34; Luka 10:25-28)

    34 22:34Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, Mafarisayo wakakusanyika pamoja. 35 22:35Mmoja wao, mtaalamu wa sheria, akamuuliza swali ili kumjaribu, akisema, 36 22:36“Mwalimu, ni amri ipi katika Sheria iliyo kuu kuliko zote?”

    37 22:37Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote.’ 38 22:38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 22:39 Nayo ya pili ni kama hiyo, nayo ni hii: ‘Mpende jirani yako kama nafsi yako.’ 40 22:40 Amri hizi mbili ndizo msingi wa Sheria na Manabii.”

    Swali Kuhusu Mwana Wa Daudi (Marko 12:35-37; Luka 20:41-44)

    41 22:41Wakati Mafarisayo walikuwa wamekusanyika pamoja, Yesu akawauliza, 42 22:42 “Mnaonaje kuhusu Kristo? 22:42 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. Yeye ni mwana wa nani?”

    Wakamjibu, “Yeye ni mwana wa Daudi.”

    43 22:43Akawaambia, “Inakuwaje basi kwamba Daudi, akinena kwa kuongozwa na Roho, anamwita Kristo ‘Bwana’? Kwa maana asema,

    44 22:44 “ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: “Keti mkono wangu wa kuume, hadi nitakapowaweka adui zako chini ya miguu yako.” ’ 45 22:45 Kama basi Daudi anamwita yeye ‘Bwana,’ awezaje kuwa mwanawe?” 46 22:46Hakuna mtu aliyeweza kumjibu Yesu neno. Tena tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu kumuuliza tena maswali. 23Yesu Awashutumu Walimu Wa Sheria Na Mafarisayo (Marko 12:38-40; Luka 11:39-52; 20:45-47)

    1 23:1Kisha Yesu akauambia umati wa watu pamoja na wanafunzi wake: 2 23:2 “Walimu wa sheria na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Mose, 3 23:3 hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri. 4 23:4 Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza.

    5 23:5 “Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hupanua vikasha vyao vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao. 6 23:6 Wanapenda kukalia viti vya heshima katika karamu, na vile viti maalum sana katika masinagogi. 7 23:7 Hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Rabi.’ 23:7 Rabi maana yake Bwana, Mwalimu.

    8 23:8 “Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi,’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu. 9 23:9 Nanyi msimwite mtu yeyote ‘Baba,’ hapa duniani, kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni. 10 23:10 Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo. 23:10 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. 11 23:11 Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. 12 23:12 Kwa kuwa yeyote anayejikweza atashushwa, na yeyote anayejinyenyekeza atakwezwa.

    13 23:13 “Lakini ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya Ufalme wa Mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [ 14 23:14 Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo hukumu yenu itakuwa kuu zaidi.]

    15 23:15 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja mwongofu, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa jehanamu mara mbili kuliko ninyi!

    16 23:16 “Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu; lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’ 17 23:17 Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi: ni ile dhahabu, au ni lile Hekalu linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? 18 23:18 Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu; lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’ 19 23:19 Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi: ni sadaka, au ni madhabahu yanayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu? 20 23:20 Kwa hiyo, mtu aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hayo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake. 21 23:21 Naye mtu aapaye kwa Hekalu, huapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake. 22 23:22 Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye aketiye juu ya kiti hicho.

    23 23:23 “Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani haki, huruma na uaminifu. Iliwapasa kufanya haya makuu ya sheria bila kupuuza hayo matoleo. 24 23:24 Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia!

    25 23:25 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani mmejaa unyangʼanyi na kutokuwa na kiasi. 26 23:26 Ewe Farisayo kipofu! Safisha ndani ya kikombe na sahani kwanza, ndipo nje itakuwa safi pia.

    27 23:27 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje, lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28 23:28 Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

    29 23:29 “Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki. 30 23:30 Nanyi mwasema, ‘Kama tungaliishi wakati wa baba zetu, tusingalikuwa tumeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’ 31 23:31 Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii. 32 23:32 Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu!

    33 23:33 “Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya jehanamu? 34 23:34 Kwa sababu hii, tazameni, natuma kwenu manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulubisha, na wengine wao mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na kuwafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine. 35 23:35 Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Abeli, ambaye alikuwa hana hatia, hadi damu ya Zekaria mwana wa Barakia, mliyemuua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu. 36 23:36 Amin, nawaambia, haya yote yatakuja juu ya kizazi hiki.

    Yesu Aililia Yerusalemu (Luka 13:34-35)

    37 23:37 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka! 38 23:38 Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. 39 23:39 Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena tangu sasa mpaka mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana.’ ”

    24Kubomolewa Kwa Hekalu Kwatabiriwa (Marko 13:1-2; Luka 21:5-6)

    1 24:1Yesu akatoka Hekaluni na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya Hekalu. 2 24:2Ndipo Yesu akawauliza, “Je, mnayaona haya yote? Amin, nawaambia, hakuna hata jiwe moja hapa litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”

    Ishara Za Nyakati Za Mwisho (Marko 13:3-23; Luka 21:7-24)

    3 24:3Yesu alipokuwa ameketi kwenye Mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamjia faraghani, wakamuuliza, “Tuambie, mambo haya yatatukia lini, nayo dalili ya kuja kwako na ya mwisho wa dunia ni gani?”

    4 24:4Yesu akawajibu, “Jihadharini, mtu yeyote asiwadanganye. 5 24:5 Kwa maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye Kristo,’ 24:5 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. nao watawadanganya wengi. 6 24:6 Mtasikia habari za vita na matetesi ya vita. Angalieni msitishike, kwa maana haya hayana budi kutukia. Lakini ule mwisho bado. 7 24:7 Taifa litainuka dhidi ya taifa, na ufalme dhidi ya ufalme. Kutakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi sehemu mbalimbali. 8 24:8 Haya yote yatakuwa ndio mwanzo wa utungu.

    9 24:9 “Ndipo mtasalitiwa, ili mteswe na kuuawa, nanyi mtachukiwa na mataifa yote kwa ajili yangu. 10 24:10 Wakati huo, wengi wataacha imani yao, nao watasalitiana kila mmoja na mwenzake na kuchukiana. 11 24:11 Watatokea manabii wengi wa uongo, nao watawadanganya watu wengi. 12 24:12 Kwa sababu ya kuongezeka kwa uovu upendo wa watu wengi utapoa, 13 24:13 lakini yule atakayevumilia hadi mwisho ataokolewa. 14 24:14 Injili ya Ufalme itahubiriwa ulimwenguni kote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Ndipo mwisho utakapokuja.

    15 24:15 “Hivyo mtakapoona lile ‘chukizo la uharibifu’ lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu (asomaye na afahamu), 16 24:16 basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani. 17 24:17 Yeyote aliye juu ya dari ya nyumba asishuke ili kuchukua chochote kutoka ndani ya nyumba. 18 24:18 Aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua vazi lake. 19 24:19 Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! 20 24:20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato. 21 24:21 Kwa maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa dunia mpaka sasa: wala haitakuwako tena kamwe. 22 24:22 Kama siku hizo zisingefupishwa, hakuna hata mtu mmoja ambaye angeokoka. Lakini kwa ajili ya wateule, siku hizo zitafupizwa. 23 24:23 Wakati huo kama mtu yeyote akiwaambia, ‘Tazama, Kristo huyu hapa!’ Au, ‘Kristo yuko kule,’ msisadiki. 24 24:24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo na manabii wa uongo, nao watafanya ishara kubwa na maajabu mengi ili kuwapotosha, ikiwezekana, hata wale wateule hasa. 25 24:25 Angalieni, nimekwisha kuwaambia mapema.

    26 24:26 “Kwa hiyo mtu yeyote akiwaambia, ‘Yule kule nyikani,’ msiende huko. Au akisema, ‘Yuko kwenye chumba,’ msisadiki. 27 24:27 Kwa maana kama vile umeme utokeavyo mashariki na kuonekana hata magharibi, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28 24:28 Kwa maana popote ulipo mzoga, huko ndiko wakusanyikapo tai.

    Kuja Kwa Mwana Wa Adamu (Marko 13:24-31; Luka 21:25-33)

    29 24:29 “Mara baada ya dhiki ya siku zile,

    “ ‘jua litatiwa giza, nao mwezi hautatoa nuru yake; nazo nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za anga zitatikisika.’

    30 24:30 “Ndipo itakapotokea ishara ya Mwana wa Adamu angani, na makabila yote ya dunia yataomboleza. Nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya angani, katika uwezo na utukufu mkuu. 31 24:31 Naye atawatuma malaika zake kwa sauti kuu ya tarumbeta, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine.

    32 24:32 “Basi jifunzeni somo hili kutokana na mtini: Matawi yake yanapoanza kuchipua na kutoa majani, mnatambua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia. 33 24:33 Vivyo hivyo, myaonapo mambo haya yote, mnatambua kwamba wakati u karibu, hata malangoni. 34 24:34 Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 35 24:35 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

    Hakuna Ajuaye Siku Wala Saa (Marko 13:32-37; Luka 17:26-30, 34-36)

    36 24:36 “Kwa habari ya siku ile na saa, hakuna ajuaye, hata malaika walio mbinguni wala Mwana, ila Baba peke yake. 37 24:37 Kama ilivyokuwa wakati wa Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38 24:38 Kwa maana siku zile kabla ya gharika, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka siku ile Noa alipoingia katika safina. 39 24:39 Nao hawakujua lolote mpaka gharika ilipokuja ikawakumba wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa atakapokuja Mwana wa Adamu. 40 24:40 Watu wawili watakuwa shambani, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. 41 24:41 Wanawake wawili watakuwa wanasaga pamoja, naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa.

    42 24:42 “Basi kesheni, kwa sababu hamjui ni siku gani atakapokuja Bwana wenu. 43 24:43 Lakini fahamuni jambo hili: Kama mwenye nyumba angejua ni wakati gani wa usiku ambao mwizi atakuja, angekesha na hangekubali nyumba yake kuvunjwa. 44 24:44 Kwa hiyo ninyi pia hamna budi kuwa tayari, kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja saa msiyotazamia.

    Mfano Wa Mtumishi Mwaminifu (Luka 12:41-48)

    45 24:45 “Ni nani basi aliye mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake amemweka kusimamia watumishi wengine katika nyumba yake, ili awape chakula chao kwa wakati unaofaa? 46 24:46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo. 47 24:47 Amin, nawaambia, atamweka mtumishi huyo kuwa msimamizi wa mali yake yote. 48 24:48 Lakini kama huyo mtumishi ni mwovu, naye akasema moyoni mwake, ‘Bwana wangu atakawia muda mrefu,’ 49 24:49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, na kula na kunywa pamoja na walevi. 50 24:50 Basi bwana wa mtumishi huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua. 51 24:51 Atamkata vipande vipande na kumweka katika sehemu moja pamoja na wanafiki, mahali ambako kutakuwa ni kulia na kusaga meno.

    25Mfano Wa Wanawali Kumi

    1 25:1 “Wakati huo, Ufalme wa Mbinguni utakuwa kama wanawali kumi waliochukua taa zao na kwenda kumlaki bwana arusi. 2 25:2 Watano wao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara. 3 25:3 Wale wapumbavu walichukua taa zao lakini hawakuchukua mafuta ya akiba, 4 25:4 lakini wale wenye busara walichukua taa zao na mafuta ya akiba kwenye vyombo. 5 25:5 Bwana arusi alipokawia kuja wale wanawali wote wakasinzia na kulala.

    6 25:6 “Usiku wa manane pakawa na kelele: ‘Tazameni, huyu hapa bwana arusi! Tokeni nje mkamlaki!’

    7 25:7 “Ndipo wale wanawali wote wakaamka na kuzitengeneza taa zao. 8 25:8 Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara, ‘Tupatieni mafuta yenu kidogo; taa zetu zinazimika.’

    9 25:9 “Lakini wale wenye busara wakawajibu, ‘Sivyo, hayatutoshi sisi na ninyi pia. Afadhali mwende kwa wauzao mkajinunulie mafuta yenu.’

    10 25:10 “Nao walipokuwa wakienda kununua mafuta, bwana arusi akafika. Wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia ndani pamoja naye kwenye karamu ya arusi na mlango ukafungwa.

    11 25:11 “Baadaye wale wanawali wengine nao wakaja, wakaita, ‘Bwana! Bwana! Tufungulie mlango!’

    12 25:12 “Lakini yeye bwana arusi akawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, siwajui ninyi!’

    13 25:13 “Kwa hiyo kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa.

    Mfano Wa Watumishi Watatu Na Talanta (Luka 19:11-27)

    14 25:14 “Tena, Ufalme wa Mbinguni ni kama mtu aliyetaka kusafiri, naye akawaita watumishi wake na kuweka mali yake kwenye uangalizi wao. 15 25:15 Mmoja akampa talanta 25:15 Talanta moja ilikuwa sawa na mshahara wa kibarua wa miaka 15. tano, mwingine talanta mbili, na mwingine talanta moja. Kila mmoja alipewa kwa kadiri ya uwezo wake. Kisha yeye akasafiri. 16 25:16 Yule aliyepewa talanta tano akaenda mara moja akafanya nazo biashara akapata talanta nyingine tano zaidi. 17 25:17 Yule aliyepewa talanta mbili akafanya vivyo hivyo, akapata nyingine mbili zaidi. 18 25:18 Lakini yule mtumishi aliyekuwa amepokea talanta moja, alikwenda akachimba shimo ardhini na kuificha ile fedha ya bwana wake.

    19 25:19 “Baada ya muda mrefu, yule bwana wa wale watumishi akarudi na kufanya hesabu nao. 20 25:20 Yule mtumishi aliyepokea talanta tano akaja, akaleta nyingine tano zaidi. Akasema, ‘Bwana uliweka kwenye uangalizi wangu talanta tano. Tazama, nimepata faida ya talanta tano zaidi.’

    21 25:21 “Bwana wake akamwambia, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu! Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

    22 25:22 “Yule mwenye talanta mbili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, uliweka kwenye uangalizi wangu talanta mbili. Tazama nimepata hapa talanta mbili zaidi.’

    23 25:23 “Bwana wake akajibu, ‘Umefanya vizuri sana, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu kwa vitu vichache; nami nitakuweka kuwa msimamizi wa vitu vingi. Njoo ushiriki katika furaha ya bwana wako!’

    24 25:24 “Kisha yule mtumishi aliyepokea talanta moja akaja, akasema, ‘Bwana, nilijua kwamba wewe ni mtu mgumu, unayevuna mahali usipopanda na kukusanya mahali usipotawanya mbegu. 25 25:25 Kwa hiyo niliogopa, nikaenda, nikaificha talanta yako ardhini. Tazama, hii hapa ile iliyo mali yako.’

    26 25:26 “Bwana wake akajibu, ‘Wewe mtumishi mwovu na mvivu! Ulijua kwamba ninavuna mahali nisipopanda na kukusanya mahali nisipotawanya mbegu. 27 25:27 Vyema basi, ingekupasa kuweka fedha yangu kwa watoa riba, ili nirudipo, nichukue ile iliyo yangu na faida yake.

    28 25:28 “ ‘Basi mnyangʼanyeni hiyo talanta, mkampe yule mwenye talanta kumi. 29 25:29 Kwa maana kila mtu aliye na kitu atapewa zaidi, naye atakuwa navyo tele. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyangʼanywa. 30 25:30 Nanyi mtupeni huyo mtumishi asiyefaa nje, kwenye giza, mahali ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno.’

    Kondoo Na Mbuzi

    31 25:31 “Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. 32 25:32 Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. 33 25:33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume, na mbuzi upande wake wa kushoto.

    34 25:34 “Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njooni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu; urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35 25:35 Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36 25:36 nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’

    37 25:37 “Ndipo wale wenye haki watakapomjibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakulisha, au ukiwa na kiu tukakunywesha? 38 25:38 Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha, au ukiwa uchi tukakuvika? 39 25:39 Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza, au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’

    40 25:40 “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi mlivyomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.’

    41 25:41 “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele ulioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. 42 25:42 Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43 25:43 nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza, na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’

    44 25:44 “Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi, au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’

    45 25:45 “Naye atawajibu, ‘Amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’

    46 25:46 “Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele.”

    26Shauri Baya La Kumuua Yesu (Marko 14:1-2; Luka 22:1-2; Yohana 11:45-53)

    1 26:1Yesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake, 2 26:2 “Kama mnavyojua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulubiwe.”

    3 26:3Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la kuhani mkuu, jina lake Kayafa. 4 26:4Wakafanya shauri ili kumkamata Yesu kwa siri na kumuua. 5 26:5Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa Sikukuu, kusitokee ghasia miongoni mwa watu.”

    Yesu Anapakwa Mafuta Huko Bethania (Marko 14:3-9; Yohana 12:1-8)

    6 26:6Yesu alikuwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma, 7 26:7naye mwanamke mmoja akamjia akiwa na chupa ya marhamu yenye manukato ya thamani kubwa; akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula.

    8 26:8Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Upotevu huu wote ni wa nini? 9 26:9Manukato haya yangeuzwa kwa bei kubwa, na fedha hizo wakapewa maskini.”

    10 26:10Yesu, akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana. 11 26:11 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. 12 26:12 Alipomiminia haya manukato kwenye mwili wangu, amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu. 13 26:13 Amin, nawaambia, mahali popote ulimwenguni ambapo hii Injili itahubiriwa, jambo hili alilolitenda huyu mwanamke litatajwa pia kwa ukumbusho wake.”

    Yuda Akubali Kumsaliti Yesu (Marko 14:10-11; Luka 22:3-6)

    14 26:14Kisha mmojawapo wa wale kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa viongozi wa makuhani 15 26:15na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. 16 26:16Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu.

    Yesu Ala Pasaka Pamoja Na Wanafunzi (Marko 14:12-21; Luka 22:7-23; Yohana 13:21-30)

    17 26:17Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimjia Yesu wakamuuliza, “Unataka twende wapi ili tukuandalie mahali pa kula Pasaka?”

    18 26:18Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini, mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia. Nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” 19 26:19Hivyo wanafunzi wakafanya kama vile Yesu alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.

    20 26:20Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale wanafunzi wake kumi na wawili. 21 26:21Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

    22 26:22Wakahuzunika sana, wakaanza kumuuliza mmoja baada ya mwingine, “Je, ni mimi Bwana?”

    23 26:23Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami ndiye atakayenisaliti. 24 26:24 Mwana wa Adamu anaenda zake kama vile alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingekuwa heri kwake mtu huyo kama hangezaliwa!”

    25 26:25Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, akasema, “Je, ni mimi Rabi?”

    Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”

    Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana (Marko 14:22-26; Luka 22:14-20; 1 Wakorintho 11:23-25)

    26 26:26Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa wanafunzi wake, akisema, “Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu.”

    27 26:27Kisha akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28 26:28 Hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29 26:29 Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena katika uzao huu wa mzabibu, hadi siku ile nitakapounywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”

    30 26:30Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka wakaenda Mlima wa Mizeituni.

    Yesu Atabiri Petro Kumkana (Marko 14:27-31; Luka 22:31-34; Yohana 13:36-38)

    31 26:31Kisha Yesu akawaambia, “Usiku huu, ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa:

    “ ‘Nitampiga mchungaji, nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’ 32 26:32 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”

    33 26:33Petro akajibu, “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”

    34 26:34Yesu akamjibu, “Amin, nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

    35 26:35Lakini Petro akasisitiza, “Hata kama itabidi kufa pamoja nawe, sitakukana kamwe.” Nao wanafunzi wale wengine wote wakasema vivyo hivyo.

    Yesu Anaomba Gethsemane (Marko 14:32-42; Luka 22:39-46)

    36 26:36Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa, nami niende kule nikaombe.” 37 26:37Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kufadhaika. 38 26:38Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

    39 26:39Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniondokee. Lakini si kama nipendavyo mimi, bali kama upendavyo wewe.”

    40 26:40Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawakuta wamelala. Akamuuliza Petro, “Je, ninyi hamkuweza kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41 26:41 Kesheni na mwombe, msije mkaingia majaribuni. Roho iko radhi, lakini mwili ni mdhaifu.”

    42 26:42Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”

    43 26:43Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. 44 26:44Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.

    45 26:45Kisha akarudi kwa wanafunzi wake, akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu anasalitiwa na kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. 46 26:46 Inukeni, twende zetu! Tazameni, msaliti wangu yuaja!”

    Yesu Akamatwa (Marko 14:43-50; Luka 22:47-53; Yohana 18:3-12)

    47 26:47Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48 26:48Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.” 49 26:49Mara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu.

    50 26:50Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”

    Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu. 51 26:51Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.

    52 26:52Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. 53 26:53 Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54 26:54 Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”

    55 26:55Wakati huo, Yesu akawaambia ule umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? 56 26:56 Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.

    Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu (Marko 14:53-65; Luka 22:54-71; Yohana 18:13-24)

    57 26:57Wale waliokuwa wamemkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika. 58 26:58Lakini Petro akamfuata kwa mbali hadi uani kwa kuhani mkuu. Akaingia ndani, akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.

    59 26:59Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. 60 26:60Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.

    Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo 61 26:61na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”

    62 26:62Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?” 63 26:63Lakini Yesu akakaa kimya.

    Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo, 26:63 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. Mwana wa Mungu.”

    64 26:64Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

    65 26:65Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru. 66 26:66Uamuzi wenu ni gani?”

    Wakajibu, “Anastahili kufa.”

    67 26:67Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi 68 26:68na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”

    Petro Amkana Bwana Yesu (Marko 14:66-72; Luka 22:56-62; Yohana 18:15-18, 25-27)

    69 26:69Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mtumishi mmoja wa kike akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”

    70 26:70Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”

    71 26:71Alipotoka nje kufika kwenye lango, mtumishi mwingine wa kike alimwona, akawaambia watu waliokuwepo, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

    72 26:72Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”

    73 26:73Baada ya muda mfupi, wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro, wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana usemi wako ni kama wao.”

    74 26:74Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!”

    Papo hapo jogoo akawika. 75 26:75Ndipo Petro akakumbuka lile neno Yesu alilokuwa amesema: “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.

    27Yesu Aletwa Mbele Ya Pilato (Marko 15:1; Luka 23:1-2; Yohana 18:28-32)

    1 27:1Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumuua. 2 27:2Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala wa Kirumi.

    Yuda Ajinyonga (Matendo 1:18-19)

    3 27:3Yuda, ambaye alikuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 4 27:4Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”

    Wakamjibu, “Hilo latuhusu nini sisi? Ni shauri yako.”

    5 27:5Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.

    6 27:6Wale viongozi wa makuhani wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” 7 27:7Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. 8 27:8Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. 9 27:9Ndipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia, kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli, 10 27:10wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”

    Yesu Mbele Ya Pilato (Marko 15:2-15; Luka 23:3-25; Yohana 18:33–19:16)

    11 27:11Wakati huo Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

    Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.”

    12 27:12Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. 13 27:13Ndipo Pilato akamuuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” 14 27:14Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.

    15 27:15Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja aliyechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. 16 27:16Wakati huo alikuwepo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. 17 27:17Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?” 18 27:18Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.

    19 27:19Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lolote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”

    20 27:20Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe, naye Yesu auawe.

    21 27:21Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”

    Wakajibu, “Baraba.”

    22 27:22Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?”

    Wakajibu wote, “Msulubishe!”

    23 27:23Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”

    Lakini wao wakazidi kupiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”

    24 27:24Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lolote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”

    25 27:25Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”

    26 27:26Basi akawafungulia Baraba. Lakini baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.

    Askari Wamdhihaki Yesu (Marko 15:16-20; Yohana 19:2-3)

    27 27:27Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitorio 27:27 Praitorio maana yake ni makao makuu ya mtawala, jumba la kifalme lililokuwa linakaliwa na Pontio Pilato huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu. na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka. 28 27:28Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha 29 27:29wakasokota taji ya miiba, wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, na wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 30 27:30Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. 31 27:31Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili wakamsulubishe.

    Yesu Asulubishwa (Marko 15:21-32; Luka 23:26-43; Yohana 19:17-27)

    32 27:32Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. 33 27:33Wakafika mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). 34 27:34Hapo wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe; lakini alipoionja, akakataa kuinywa. 35 27:35Walipokwisha kumsulubisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. [Hili lilifanyika ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] 36 27:36Kisha wakaketi, wakamchunga. 37 27:37Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake hivi: Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi. 38 27:38Wanyangʼanyi wawili walisulubiwa pamoja naye, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. 39 27:39Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao 40 27:40na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.”

    41 27:41Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wakamdhihaki wakisema, 42 27:42“Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, nasi tutamwamini. 43 27:43Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” 44 27:44Hata wale wanyangʼanyi waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.

    Kifo Cha Yesu (Marko 15:33-41; Luka 23:44-49; Yohana 19:28-30)

    45 27:45Tangu saa sita hadi saa tisa giza liliifunika nchi yote. 46 27:46Ilipofika saa tisa, Yesu akapaza sauti akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)

    47 27:47Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia hayo, wakasema, “Anamwita Eliya.”

    48 27:48Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo, akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe. 49 27:49Wengine wakasema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.”

    50 27:50Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.

    51 27:51Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. 52 27:52Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuliwa. 53 27:53Wakatoka makaburini, na baada ya Yesu kufufuka, waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.

    54 27:54Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, waliogopa, wakasema, “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”

    55 27:55Walikuwako wanawake huko wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulikia mahitaji yake. 56 27:56Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo na Yosefu, na mama yao wana wa Zebedayo.

    Maziko Ya Yesu (Marko 15:42-47; Luka 23:50-56; Yohana 19:38-42)

    57 27:57Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathaya aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58 27:58Akamwendea Pilato ili kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe. 59 27:59Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akaufunga katika kitambaa cha kitani safi, 60 27:60na kuuweka katika kaburi lake mwenyewe jipya, alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa katika ingilio la kaburi, akaenda zake. 61 27:61Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwepo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.

    Walinzi Pale Kaburini

    62 27:62Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato 63 27:63na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu wakati alikuwa bado hai alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ 64 27:64Kwa hiyo uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti mpaka baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuliwa kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”

    65 27:65Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadri mwezavyo.” 66 27:66Kwa hiyo wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.

    28Yesu Afufuka (Marko 16:1-10; Luka 24:1-12; Yohana 20:1-10)

    1 28:1Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.

    2 28:2Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaenda penye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. 3 28:3Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4 28:4Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.

    5 28:5Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. 6 28:6Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. 7 28:7Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ”

    8 28:8Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, bali wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. 9 28:9Ghafula, Yesu akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. 10 28:10Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”

    Taarifa Ya Walinzi

    11 28:11Wakati wale wanawake walikuwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. 12 28:12Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kutunga hila, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha 13 28:13wakiwaambia, “Inawapasa mseme, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ 14 28:14Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lolote.” 15 28:15Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi mpaka leo.

    Yesu Awatuma Wanafunzi Wake (Marko 16:14-18; Luka 24:36-49; Yohana 20:19-23; Matendo 1:6-8)

    16 28:16Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza. 17 28:17Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. 18 28:18Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 28:19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 28:20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”