Mika
1Mika1 1:1Neno la
Bwana lilimjia Mika, Mmoreshethi, wakati wa utawala wa Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda; ufunuo aliouona kuhusu Samaria na Yerusalemu.
2 1:2Sikieni, enyi mataifa, enyi nyote,
sikilizeni, ee dunia na wote mliomo ndani yake,
ili
Bwana Mwenyezi ashuhudie dhidi yenu,
Bwana kutoka Hekalu lake takatifu.
Hukumu Dhidi Ya Samaria Na Yerusalemu
3 1:3Tazama!
Bwana anakuja kutoka mahali pake;
anashuka na kukanyaga
mahali palipoinuka juu pa dunia.
4 1:4Milima inayeyuka chini yake
na mabonde yanagawanyika
kama nta mbele ya moto,
kama maji yatiririkayo kasi
kwenye mteremko.
5 1:5Yote haya ni kwa sababu ya kosa la Yakobo,
ni kwa sababu ya dhambi za nyumba ya Israeli.
Kosa la Yakobo ni lipi?
Je, sio Samaria?
Je, mahali pa juu pa Yuda pa kuabudia miungu ni nini?
Je, sio Yerusalemu?
6 1:6“Kwa hiyo nitaufanya Samaria kuwa lundo la kokoto,
mahali pa kuotesha mizabibu.
Nitayamwaga mawe yake katika bonde
na kuacha wazi misingi yake.
7 1:7Sanamu zake zote
zitavunjwa vipande vipande;
zawadi zake zote za Hekalu
zitachomwa kwa moto;
nitaharibu vinyago vyake vyote.
Kwa kuwa alikusanya zawadi zake
kutokana na ujira wa kahaba,
nazo zitatumika tena
kulipa mishahara ya kahaba.”
Kulia Na Kuomboleza
8 1:8Kwa ajili ya hili nitalia na kuomboleza;
nitatembea bila viatu na tena uchi.
Nitabweka kama mbweha
na kuomboleza kama bundi.
9 1:9Kwa sababu jeraha lake halitibiki;
limekuja Yuda.
Limefika hasa kwenye lango la watu wangu,
hata Yerusalemu kwenyewe.
10 1:10Usiliseme hili huko Gathi;
usilie hata kidogo.
Huko Beth-le-Afra
gaagaa mavumbini.
11 1:11Piteni mkiwa uchi na wenye aibu,
ninyi mkaao Shafiri.
Wale waishio Saanani
hawatatoka nje.
Beth-Eseli iko katika maombolezo;
kinga yake imeondolewa kwako.
12 1:12Wale waishio Marothi wanagaagaa kwa maumivu
wakingoja msaada,
kwa sababu maangamizi yamekuja
kutoka kwa
Bwana,
hata katika lango la Yerusalemu.
13 1:13Enyi mkaao Lakishi,
fungeni farasi kwenye magari ya vita.
Mlikuwa chanzo cha dhambi
kwa Binti Sayuni,
kwa kuwa makosa ya Israeli
yalikutwa kwako.
14 1:14Kwa hiyo utaipa Moresheth-Gathi
zawadi za kuagana.
Mji wa Akzibu utaonyesha wazi udanganyifu
kwa wafalme wa Israeli.
15 1:15Nitawaleteeni atakayewashinda
ninyi mnaoishi Maresha.
Yeye aliye utukufu wa Israeli
atakuja Adulamu.
16 1:16Nyoeni nywele zenu katika kuomboleza
kwa ajili ya watoto wenu mnaowafurahia;
jifanyieni upara kama tai,
kwa kuwa watawaacha
na kwenda uhamishoni.
2Mipango Ya Mwanadamu Na Ya Mungu
1 2:1Ole kwa wale wapangao uovu,
kwa wale wafanyao shauri la hila vitandani mwao!
Kunapopambazuka wanalitimiza
kwa sababu uko katika uwezo wao kutekeleza.
2 2:2Wanatamani mashamba na kuyakamata,
pia nyumba na kuzichukua.
Wanamlaghai mwanaume nyumba yake,
mwanadamu mwenzake urithi wake.
3 2:3Kwa hiyo,
Bwana asema:
“Ninapanga maangamizi dhidi ya watu hawa,
ambayo hamwezi kujiokoa wenyewe.
Hamtatembea tena kwa majivuno,
kwa kuwa utakuwa ni wakati wa maafa.
4 2:4Siku hiyo watu watawadhihaki,
watawafanyia mzaha
kwa wimbo huu wa maombolezo:
‘Tumeangamizwa kabisa;
mali ya watu wangu imegawanywa.
Ameninyangʼanya!
Ametoa mashamba yetu kwa wasaliti.’ ”
5 2:5Kwa hiyo hutakuwa na yeyote katika kusanyiko la
Bwana
wa kugawanya mashamba kwa kura.
Manabii Wa Uongo
6 2:6Manabii wao husema, “Usitabiri.
Usitabiri kuhusu vitu hivi;
aibu haitatupata.”
7 2:7Je, ingesemwa, ee nyumba ya Yakobo:
“Je, Roho wa
Bwana amekasirika?
Je, yeye hufanya vitu kama hivyo?”
“Je, maneno yangu hayamfanyii mema
yeye ambaye njia zake ni nyofu?
8 2:8Siku hizi watu wangu wameinuka
kama adui.
Unawavua joho la kitajiri wale wanaopita
pasipo kujali,
kama watu warudio kutoka vitani.
9 2:9Unawahamisha wanawake wa watu wangu
kutoka kwenye nyumba zao za kupendeza.
Unaondoa baraka yangu
kwa watoto wao milele.
10 2:10Inuka, nenda zako!
Kwa maana hapa sio mahali pako pa kupumzikia,
kwa sababu pametiwa unajisi,
pameharibiwa, wala hapatengenezeki tena.
11 2:11Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema,
‘Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi,’
angekuwa ndiye nabii
anayekubalika na watu hawa!
Ahadi Ya Ukombozi
12 2:12“Hakika nitawakusanya ninyi nyote, ee Yakobo,
Hakika nitawaleta pamoja mabaki ya Israeli.
Nitawaleta pamoja kama kondoo ndani ya zizi,
kama kundi kwenye malisho yake,
mahali hapa patakuwa na msongamano wa watu.
13 2:13Yeye afunguaye njia atawatangulia;
watapita kwenye lango na kutoka nje.
Mfalme wao atawatangulia,
Bwana atakuwa kiongozi.”
3Viongozi Na Manabii Wakemewa
1 3:1Kisha nikasema,
“Sikilizeni enyi viongozi wa Yakobo,
enyi watawala wa nyumba ya Israeli.
Je, hampaswi kujua hukumu,
2 3:2ninyi mnaochukia mema
na kupenda maovu;
ninyi mnaowachuna watu wangu ngozi
na kuondoa nyama kwenye mifupa yao;
3 3:3ninyi mnaokula nyama ya watu wangu,
mnaowachuna ngozi
na kuvunja mifupa yao vipande vipande;
mnaowakatakata kama nyama
ya kuwekwa kwenye sufuria
na kama nyama
ya kuwekwa kwenye chungu?”
4 3:4Kisha watamlilia
Bwana,
lakini hatawajibu.
Wakati huo atawaficha uso wake
kwa sababu ya uovu waliotenda.
5 3:5Hili ndilo asemalo
Bwana:
“Kuhusu manabii wanaowapotosha watu wangu,
mtu akiwalisha,
wanatangaza ‘amani’;
kama hakufanya hivyo,
wanaandaa kupigana vita dhidi yake.
6 3:6Kwa hiyo usiku utawajieni, msiweze kuwa na maono,
na giza, msiweze kubashiri.
Jua litawachwea manabii hao,
nao mchana utakuwa giza kwao.
7 3:7Waonaji wataaibika
na waaguzi watafedheheka.
Wote watafunika nyuso zao
kwa sababu hakuna jibu litokalo kwa Mungu.”
8 3:8Lakini kuhusu mimi, nimejazwa nguvu,
nimejazwa Roho wa
Bwana,
haki na uweza,
kumtangazia Yakobo kosa lake,
na Israeli dhambi yake.
9 3:9Sikieni hili, enyi viongozi wa nyumba ya Yakobo,
enyi watawala wa nyumba ya Israeli,
mnaodharau haki
na kupotosha kila lililo sawa;
10 3:10mnaojenga Sayuni kwa kumwaga damu
na Yerusalemu kwa uovu.
11 3:11Viongozi wake wanahukumu kwa rushwa,
na makuhani wake wanafundisha kwa malipo,
nao manabii wake wanatabiri kwa fedha.
Hata hivyo wanamwegemea
Bwana na kusema,
“Je,
Bwana si yumo miongoni mwetu?
Hakuna maafa yatakayotupata.”
12 3:12Kwa hiyo kwa sababu yenu,
Sayuni italimwa kama shamba,
Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto,
na kilima cha Hekalu
kitakuwa kichuguu
kilichofunikwa na vichaka.
4Mlima Wa
Bwana
(Isaya 2:2-4)
1 4:1Katika siku za mwisho
mlima wa Hekalu la
Bwana utaimarishwa
kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote;
utainuliwa juu ya vilima,
na watu wa mataifa watamiminika humo.
2 4:2Mataifa mengi yatakuja na kusema,
“Njooni, twendeni mlimani mwa
Bwana,
kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.
Atatufundisha njia zake,
ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”
Sheria itatoka Sayuni,
neno la
Bwana litatoka Yerusalemu.
3 4:3Atahukumu kati ya mataifa mengi,
na ataamua migogoro ya mataifa
yenye nguvu na yaliyo mbali.
Watafua panga zao ziwe majembe,
na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.
Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,
wala hawatajifunza vita tena.
4 4:4Kila mtu ataketi chini ya mzabibu wake
na chini ya mtini wake,
wala hakuna mtu atakayewaogopesha,
kwa kuwa
Bwana Mwenye Nguvu Zote amesema.
5 4:5Mataifa yote yanaweza kutembea
katika jina la miungu yao;
sisi tutatembea katika jina la
Bwana
Mungu wetu milele na milele.
Mpango Wa
Bwana
6 4:6“Katika siku hiyo,” asema
Bwana,
“nitawakusanya walemavu;
nitawakusanya walio uhamishoni
na wale niliowahuzunisha.
7 4:7Nitawafanya walemavu kuwa mabaki,
wale waliofukuzwa kuwa taifa lenye nguvu.
Bwana atatawala juu yao katika Mlima Sayuni
kuanzia siku hiyo na hata milele.
8 4:8Lakini kuhusu wewe, ee mnara wa ulinzi wa kundi,
ee ngome ya Binti Sayuni,
milki ya awali itarudishwa kwako,
ufalme utakuja kwa Binti Yerusalemu.”
9 4:9Kwa nini sasa unalia kwa nguvu:
kwani huna mfalme?
Je, mshauri wako amekufa, hata maumivu yakukamate
kama ya mwanamke
aliye na utungu wa kuzaa?
10 4:10Gaagaa kwa utungu, ee Binti Sayuni,
kama mwanamke mwenye utungu wa kuzaa,
kwa kuwa sasa ni lazima uuache mji
ukapige kambi uwanjani.
Utakwenda Babeli;
huko utaokolewa.
Huko
Bwana atakukomboa
kutoka mikononi mwa adui zako.
11 4:11Lakini sasa mataifa mengi
yamekusanyika dhidi yako.
Wanasema, “Mwache anajisiwe,
macho yetu na yatazame Sayuni kwa furaha!”
12 4:12Lakini hawayajui
mawazo ya
Bwana;
hawauelewi mpango wake,
yeye awakusanyaye kama miganda
kwenye sakafu ya kupuria.
13 4:13“Inuka upure, ee Binti Sayuni,
kwa kuwa nitakupa pembe za chuma;
nitakupa kwato za shaba
na utavunja vipande vipande mataifa mengi.”
Utatoa mapato yao waliopata kwa udanganyifu kwa
Bwana,
utajiri wao kwa Bwana wa dunia yote.
5Mtawala Aliyeahidiwa Kutoka Bethlehemu
1 5:1Panga majeshi yako, ee mji wa majeshi,
kwa kuwa kuzingirwa kumepangwa dhidi yetu.
Watampiga mtawala wa Israeli
shavuni kwa fimbo.
2 5:2“Lakini wewe, Bethlehemu Efrathi,
ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda,
kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu
yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli,
ambaye asili yake ni kutoka zamani,
kutoka milele.”
3 5:3Kwa hiyo Israeli utaachwa mpaka wakati
mwanamke aliye na utungu atakapozaa
na ndugu zake wengine warudi
kujiunga na Waisraeli.
4 5:4Atasimama na kulichunga kundi lake
katika nguvu ya
Bwana,
katika utukufu wa jina la
Bwana Mungu wake.
Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo
ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia.
5 5:5Naye atakuwa amani yao.
Ukombozi Na Uharibifu
Wakati Mwashuru atakapovamia nchi yetu
na kupita katika ngome zetu,
tutawainua wachungaji saba dhidi yake,
hata viongozi wanane wa watu.
6 5:6Wataitawala nchi ya Ashuru kwa upanga,
nchi ya Nimrodi kwa upanga.
Atatuokoa kutoka kwa Mwashuru
atakapoivamia nchi yetu
na kuingia katika mipaka yetu.
7 5:7Mabaki ya Yakobo yatakuwa
katikati ya mataifa mengi
kama umande kutoka kwa
Bwana,
kama manyunyu juu ya majani,
ambayo hayamngoji mtu
wala kukawia kwa mwanadamu.
8 5:8Mabaki ya Yakobo yatakuwa miongoni mwa mataifa,
katikati ya mataifa mengi,
kama simba miongoni mwa wanyama wa msituni,
kama mwana simba miongoni
mwa makundi ya kondoo,
ambaye anaumiza vibaya na kuwararua
kila anapopita katikati yao,
wala hakuna awezaye kuokoa.
9 5:9Mkono wako utainuliwa juu kwa ushindi juu ya watesi wako,
nao adui zako wote wataangamizwa.
10 5:10“Katika siku ile,” asema
Bwana,
“nitaangamiza farasi zenu katikati yenu
na kubomoa magari yenu ya vita.
11 5:11Nitaiangamiza miji ya nchi yenu
na kuziangusha chini ngome zenu zote.
12 5:12Nitaangamiza uchawi wenu
na hamtapiga tena ramli.
13 5:13Nitaangamiza vinyago vyenu vya kuchonga
na mawe yenu ya ibada yatoke katikati yenu;
hamtasujudia tena
kazi ya mikono yenu.
14 5:14Nitangʼoa nguzo za Ashera katikati yenu
na kubomoa miji yenu.
15 5:15Nitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu
juu ya mataifa ambayo hayajanitii.”
6Shauri La
Bwana Dhidi Ya Israeli
1 6:1Sikiliza asemalo
Bwana:
“Simama, tetea shauri lako mbele ya milima;
vilima na visikie lile unalotaka kusema.
2 6:2Sikilizeni, ee milima, mashtaka ya
Bwana,
sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia.
Kwa kuwa
Bwana ana shauri dhidi ya watu wake;
anatoa mashtaka dhidi ya Israeli.
3 6:3“Watu wangu, nimewatendea nini?
Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu.
4 6:4Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa
kutoka nchi ya utumwa.
Nilimtuma Mose awaongoze,
pia Aroni na Miriamu.
5 6:5Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu
alivyofanya shauri
na kile Balaamu mwana wa Beori alichojibu.
Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu mpaka Gilgali,
ili mfahamu matendo ya haki ya
Bwana.”
6 6:6Nimjie
Bwana na kitu gani na kusujudu
mbele za Mungu aliyetukuka?
Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa,
nije na ndama za mwaka mmoja?
7 6:7Je,
Bwana atafurahishwa na kondoo dume elfu,
au mito elfu kumi ya mafuta?
Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu,
mtoto wangu mwenyewe
kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu?
8 6:8Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.
Bwana anataka nini kwako?
Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,
na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.
Hatia Na Adhabu Ya Israeli
9 6:9Sikiliza!
Bwana anauita mji:
kulicha jina lako ni hekima:
“Tii hiyo fimbo na yeye aliyeiamuru.
10 6:10Je, bado nisahau, ee nyumba ya uovu,
hazina yako uliyopata kwa udanganyifu
na vipimo vilivyopunguka,
ambavyo vimelaaniwa?
11 6:11Je, naweza kuhukumu kuwa
mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia,
aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo?
12 6:12Matajiri wake ni wajeuri;
watu wake ni waongo
na ndimi zao zinazungumza
kwa udanganyifu.
13 6:13Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu,
kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.
14 6:14Mtakula lakini hamtashiba;
matumbo yenu bado yatakuwa matupu.
Mtaweka akiba lakini hamtaokoa chochote,
kwa sababu mtakachoweka akiba
nitatoa kwa upanga.
15 6:15Mtapanda lakini hamtavuna;
mtakamua zeituni lakini
hamtatumia mafuta yake.
Mtakamua zabibu
lakini hamtakunywa hiyo divai.
16 6:16Mmezishika sheria za Omri
na matendo yote ya nyumba ya Ahabu,
tena umefuata desturi zao.
Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi
na watu wako kuwa dhihaka;
mtachukua dharau za mataifa.”
7Taabu Ya Israeli
1 7:1Taabu gani hii niliyo nayo!
Nimefanana na yule akusanyaye
matunda ya kiangazi,
aokotaye masazo baada ya kuvunwa
shamba la mizabibu;
hakuna kishada chenye matunda ya kula,
hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani.
2 7:2Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka nchi;
hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki.
Watu wote wanavizia kumwaga damu,
kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu.
3 7:3Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya,
mtawala anadai zawadi,
hakimu anapokea rushwa,
wenye nguvu wanaamuru wanachotaka:
wote wanafanya shauri baya pamoja.
4 7:4Aliye mwema kupita wote kati yao
ni kama mchongoma,
anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao
ni mbaya kuliko uzio wa miiba.
Siku ya walinzi wako imewadia,
siku atakayokutembelea Mungu.
Sasa ni wakati wao
wa kuchanganyikiwa.
5 7:5Usimtumaini jirani;
usiweke matumaini kwa rafiki.
Hata kwa yule alalaye kifuani mwako
uwe mwangalifu kwa maneno yako.
6 7:6Kwa kuwa mwana humdharau baba yake,
naye binti huinuka dhidi ya mama yake,
mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake:
adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa.
7 7:7Lakini mimi, namtazama
Bwana kwa matumaini,
namngoja Mungu Mwokozi wangu;
Mungu wangu atanisikia mimi.
Israeli Atainuka
8 7:8Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu!
Ingawa nimeanguka, nitainuka.
Japo ninaketi gizani,
Bwana atakuwa nuru yangu.
9 7:9Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake,
nitabeba ghadhabu ya
Bwana,
mpaka atakaponitetea shauri langu
na kuithibitisha haki yangu.
Atanileta nje kwenye mwanga,
nami nitaiona haki yake.
10 7:10Kisha adui yangu ataliona
naye atafunikwa na aibu,
yule aliyeniambia,
“Yu wapi
Bwana Mungu wako?”
Macho yangu yataona kuanguka kwake,
hata sasa atakanyagwa chini ya mguu
kama tope barabarani.
11 7:11Siku ya kujenga kuta zako itawadia,
siku ya kupanua mipaka yako.
12 7:12Siku hiyo watu watakuja kwako
kutoka Ashuru na miji ya Misri,
hata kutoka Misri hadi Frati
na kutoka bahari hadi bahari
na kutoka mlima hadi mlima.
13 7:13Dunia itakuwa ukiwa kwa sababu ya wakazi wake,
kwa sababu ya matunda ya matendo yao.
Sala Na Sifa
14 7:14Wachunge watu wako kwa fimbo yako,
kundi la urithi wako,
ambalo linaishi peke yake msituni,
katika nchi ya malisho yenye rutuba.
Waache walishe katika Bashani na Gileadi
kama ilivyokuwa siku za kale.
15 7:15“Kama siku zile mlipotoka Misri,
nitawaonyesha maajabu yangu.”
16 7:16Mataifa yataona na kuaibika,
waliondolewa nguvu zao zote.
Wataweka mikono yao kwenye vinywa vyao
na masikio yao yatakuwa na uziwi.
17 7:17Wataramba mavumbi kama nyoka,
kama viumbe vitambaavyo juu ya ardhi.
Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka;
watamgeukia
Bwana Mungu wetu kwa hofu
nao watakuogopa.
18 7:18Ni nani Mungu kama wewe,
ambaye anaachilia dhambi
na kusamehe makosa
ya mabaki ya urithi wake?
Wewe huwi na hasira milele,
bali unafurahia kuonyesha rehema.
19 7:19Utatuhurumia tena,
utazikanyaga dhambi zetu
chini ya nyayo zako,
na kutupa maovu yetu yote
katika vilindi vya bahari.
20 7:20Utakuwa wa kweli kwa Yakobo,
nawe utamwonyesha Abrahamu rehema,
kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu
siku za kale.