Filemoni

1Filemoni1 1:1Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu:

Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtendakazi mwenzetu, 2 1:2kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako:

3 1:3Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

Shukrani Na Maombi

4 1:4Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu, 5 1:5kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote. 6 1:6Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo. 7 1:7Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.

Maombi Ya Paulo Ya Kumtetea Onesimo

8 1:8Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda, 9 1:9lakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu, 10 1:10nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo, 1:10 Onesimo maana yake ni Wa manufaa. aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo. 11 1:11Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.

12 1:12Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa. 13 1:13Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili. 14 1:14Lakini sikutaka kufanya lolote bila idhini yako, ili wema wowote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari. 15 1:15Huenda sababu ya yeye kutengwa nawe kwa kitambo kidogo ni ili uwe naye daima. 16 1:16Si kama mtumwa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana.

17 1:17Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika wako, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe. 18 1:18Kama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi. 19 1:19Ni mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa. Sitaji kwamba nakudai hata nafsi yako. 20 1:20Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, uuburudishe moyo wangu katika Kristo. 21 1:21Nikiwa na hakika ya utii wako, nakuandikia, nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale ninayokuomba.

22 1:22Jambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.

Salamu Za Mwisho Na Dua Ya Kuwatakia Heri

23 1:23Epafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu, anakusalimu. 24 1:24Vivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watendakazi wenzangu wanakusalimu.

25 1:25Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.