\id 2TI - Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version \rem Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc. \h 2 Timotheo \toc1 2 Timotheo \toc2 2 Timotheo \toc3 2Tim \mt1 2 Timotheo \c 1 \p \v 1 Paulo mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, kulingana na ile ahadi ya uzima uliomo ndani ya Kristo Yesu. \p \v 2 Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa: \p Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba, na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. \s1 Shukrani Na Kutiwa Moyo \p \v 3 Ninamshukuru Mungu, ninayemtumikia kwa dhamiri safi, kama walivyofanya baba zangu, ninapokukumbuka usiku na mchana katika maombi yangu. \v 4 Nikiyakumbuka machozi yako, ninatamani sana kukuona ili nipate kujawa na furaha. \v 5 Nimekuwa nikiikumbuka imani yako ya kweli, waliokuwa nayo bibi yako Loisi na mama yako Eunike na ambayo mimi ninasadiki sasa wewe pia unayo. \v 6 Kwa sababu hii nakukumbusha uchochee ile karama ya Mungu, iliyowekwa ndani yako nilipokuwekea mikono yangu. \v 7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali roho ya nguvu, ya upendo na ya moyo wa kiasi. \p \v 8 Kwa hiyo usione haya kushuhudia kuhusu Bwana wetu, wala usinionee haya mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Bali uishiriki pamoja nami taabu ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu, \v 9 ambaye alituokoa na kutuita katika mwito mtakatifu: si kwa kadiri ya matendo yetu mema bali kwa sababu ya kusudi lake mwenyewe na neema yake. Neema hii tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele. \v 10 Lakini sasa imefunuliwa kwa kudhihirishwa kwake Mwokozi wetu, Kristo Yesu, ambaye amebatilisha mauti na kuleta uzima na kutokufa kwa njia ya Injili. \v 11 Nami nimewekwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu wa Injili hii. \v 12 Hii ndiyo sababu ninateseka namna hii, lakini sioni haya kwa maana ninamjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kuwa anaweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hadi siku ile. \p \v 13 Shika kwa uthabiti kielelezo cha mafundisho yenye uzima yale uliyoyasikia kwangu, pamoja na imani na upendo katika Kristo Yesu. \v 14 Ilinde ile amana uliyokabidhiwa kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu. \p \v 15 Unajua ya kuwa watu wote katika Asia wameniacha, miongoni mwao wamo Filego na Hermogene. \p \v 16 Bwana akawahurumie watu wa nyumbani mwa Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha mara kwa mara wala hakuionea aibu minyororo yangu. \v 17 Badala yake, alipokuwa Rumi, alinitafuta kwa bidii mpaka akanipata. \v 18 Bwana na amjalie kupata rehema zake siku ile! Nawe unajua vyema jinsi alivyonisaidia huko Efeso. \c 2 \s1 Askari Mwema Wa Kristo Yesu \p \v 1 Basi, wewe mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Kristo Yesu. \v 2 Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vilevile. \v 3 Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu. \v 4 Hakuna askari yeyote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari. \v 5 Vivyo hivyo, yeye ashindanaye katika michezo hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano. \v 6 Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno. \v 7 Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Bwana atakupa ufahamu katika mambo hayo yote. \p \v 8 Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, \v 9 ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. \v 10 Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. \p \v 11 Hili ni neno la kuaminiwa: \q1 Kwa maana kama tumekufa pamoja naye, \q2 tutaishi pia pamoja naye. \q1 \v 12 Kama tukistahimili, \q2 pia tutatawala pamoja naye. \q1 Kama tukimkana yeye, \q2 naye atatukana sisi. \q1 \v 13 Kama tusipoamini, \q2 yeye hudumu kuwa mwaminifu, \q2 kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. \s1 Mfanyakazi Aliyekubaliwa Na Mungu \p \v 14 Endelea kuwakumbusha mambo haya ukiwaonya mbele za Bwana waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yoyote bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia. \v 15 Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtendakazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. \v 16 Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu. \v 17 Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto \v 18 ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako, nao huharibu imani ya baadhi ya watu. \v 19 Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake”; tena, “Kila alitajaye jina la Bwana, na auache uovu.” \p \v 20 Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo; vingine kwa matumizi maalum, na vingine kwa matumizi ya kawaida. \v 21 Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema. \p \v 22 Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. \v 23 Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. \v 24 Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. \v 25 Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, \v 26 ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake. \c 3 \s1 Hatari Za Siku Za Mwisho \p \v 1 Lakini yakupasa ufahamu jambo hili, kwamba siku za mwisho kutakuwa na nyakati za hatari. \v 2 Kwa maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kumkufuru Mungu, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio watakatifu, \v 3 wasio na upendo, wasiopenda kupatanishwa, wasingiziaji, wasiozuia tamaa zao, wakatili, wasiopenda mema, \v 4 wasaliti, wakaidi, waliojaa majivuno, wapendao anasa zaidi kuliko kumpenda Mungu: \v 5 wakiwa na mfano wa utauwa kwa nje, lakini wakizikana nguvu za Mungu. Jiepushe na watu wa namna hiyo. \p \v 6 Miongoni mwao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu na kuwachukua mateka wanawake wajinga, waliolemewa na dhambi zao na kuyumbishwa na aina zote za tamaa mbaya. \v 7 Wakijifunza siku zote lakini kamwe wasiweze kufikia ujuzi wa kweli. \v 8 Kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Mose, vivyo hivyo watu hawa hupingana na ile kweli. Hawa ni watu wenye akili zilizopotoka, ambao wamekataliwa kwa mambo ya imani. \v 9 Lakini hawataendelea sana, kwa sababu upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama ulivyokuwa dhahiri upumbavu wa hao watu wawili. \s1 Paulo Amwagiza Timotheo \p \v 10 Lakini wewe umeyajua mafundisho yangu, mwenendo, makusudi, imani, uvumilivu, upendo, ustahimilivu, \v 11 mateso na taabu, yaani mambo yote yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Listra, mateso yote niliyostahimili, lakini Bwana aliniokoa katika hayo yote. \v 12 Naam, yeyote anayetaka kuishi maisha ya utauwa ndani ya Kristo Yesu atateswa. \v 13 Lakini watu waovu na wadanganyaji watazidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika. \v 14 Bali wewe, udumu katika yale uliyojifunza na kuyaamini kwa uthabiti, ukitambua ya kuwa ulijifunza hayo kutoka kwa nani, \v 15 na jinsi ambavyo tangu utoto umeyajua Maandiko matakatifu, ambayo yanaweza kukuhekimisha upate wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. \v 16 Kila Andiko limevuviwa na Mungu na lafaa kwa mafundisho, kwa kuwaonya watu makosa yao, kwa kuwaongoza na kwa kuwafundisha katika haki, \v 17 ili mtu wa Mungu awe amekamilishwa, apate kutenda kila kazi njema. \c 4 \s1 Maagizo Ya Mwisho \p \v 1 Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: \v 2 Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. \v 3 Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu wapate kuwaambia yale ambayo masikio yao yanayowasha yanatamani kuyasikia. \v 4 Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo. \v 5 Kwa habari yako wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako. \p \v 6 Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia. \v 7 Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda. \v 8 Sasa nimewekewa taji ya haki ambayo Bwana, mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake. \s1 Maelekezo Ya Binafsi \p \v 9 Jitahidi kuja kwangu upesi \v 10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na amekwenda Thesalonike. Kreske amekwenda Galatia na Tito amekwenda Dalmatia. \v 11 Ni Luka peke yake aliye hapa pamoja nami. Mtafute Marko uje naye kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu. \v 12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso. \v 13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi. \p \v 14 Aleksanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda. \v 15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu. \p \v 16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Namwomba Mungu wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. \v 17 Lakini Bwana alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba. \v 18 Bwana ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe yeye milele na milele. Amen. \s1 Salamu Za Mwisho \p \v 19 Wasalimu Prisila\f + \fr 4:19 \ft Prisila kwa Kiyunani ni Priska, hivyo tafsiri nyingine zimemuita Priska.\f* na Akila, na wote wa nyumbani kwa Onesiforo. \v 20 Erasto alibaki Korintho. Nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa. \v 21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi. Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote. \p \v 22 Bwana awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi. Amen.