Zaburi
KITABU CHA KWANZA
1
(Zaburi 1–41)
Furaha Ya Kweli
Heri mtu yule ambaye
haendi katika shauri la watu waovu,
wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,
au kuketi katika baraza la wenye mizaha.
Bali huifurahia sheria ya Bwana,
naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana.
Mtu huyo ni kama mti uliopandwa
kando ya vijito vya maji,
ambao huzaa matunda kwa majira yake
na majani yake hayanyauki.
Lolote afanyalo hufanikiwa.
Huzuni Ya Waovu
Sivyo walivyo waovu!
Wao ni kama makapi
yapeperushwayo na upepo.
Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu,
wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki.
 
Kwa maana Bwana huziangalia njia za mwenye haki,
bali njia ya waovu itaangamia.