Zaburi 2
Mfalme Aliyechaguliwa Na Mungu
Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya,
na kabila za watu kula njama bure?
Wafalme wa dunia wanajipanga
na watawala wanajikusanya pamoja
dhidi ya Bwana
na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.
Wanasema, “Tuvunje minyororo yao
na kuvitupilia mbali vifungo vyao.”
 
Yeye atawalaye mbinguni hucheka,
Bwana huwadharau.
Kisha huwakemea katika hasira yake
na kuwaogopesha katika ghadhabu yake, akisema,
“Nimemtawaza Mfalme wangu
juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.”
Ushindi Wa Mfalme
Nitatangaza amri ya Bwana:
Yeye aliniambia, “Wewe ni Mwanangu,
leo mimi nimekuzaa.
Niombe, nami nitayafanya mataifa
kuwa urithi wako,
miisho ya dunia kuwa milki yako.
Utawatawala kwa fimbo ya chuma
na kuwavunjavunja kama chombo cha mfinyanzi.”
 
10 Kwa hiyo, ninyi wafalme, kuweni na hekima;
mwonyeke, enyi watawala wa dunia.
11 Mtumikieni Bwana kwa hofu
na mshangilie kwa kutetemeka.
12 Mbusu Mwana, asije akakasirika
nawe ukaangamizwa katika njia yako,
kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula.
Heri wote wanaomkimbilia.